Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

STORY: JUMBA JEUSI 

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA 

Kwenye mfuko wake wa koti alitoa picha ambayo ilikuwa na sura ya mtoto, aliitazama kwa muda wa dakika kadhaa kisha akasikitika, alionekana kabisa kuwa kwenye jela ambayo ilimfanya yeye kuishi mtaani maisha ambayo bila shaka hakuwa anayafurahia ila hakuonekana kuwa na namna zaidi ya kuishi kama vile misingi ya asili inavyo mtaka aishi kama sio kwa maamuzi ambayo huenda aliyafanya bila kujua madhara yake ambayo yangekuja baadae.

“Nitaua hawa watu mpaka lini? ona sasa nimeliuza taifa langu kwa watu ambao huenda watalifanya taifa hili kuingia kwenye hali mbaya kwa zaidi ya miaka hamsini ijayo. Lakini nilipaswa kufanya nini? Kuna nyakati inabidi ukubali kwamba akili yako haiwezi kufanya maamuzi ya mwisho bali mazingira yanakufanya uje na maamuzi ambayo hata nafsi yako inabaki inakushangaa hivyo najua ni ngumu kuishi na hili lakini ndiyo namna pekee ya kuishi” alitamka mithili ya mtu ambaye alikuwa analijutia jambo ambalo lilikuwa linaendelea ila hakuwa na namna nyingine ya kuweza kufanya. Aligonga mlango wa gari, walinzi waliingia ndani na gari hiyo ikaondoshwa hilo eneo.

 

 

Saa nane na nusu usiku maeneo ya Sogea, ilionekana gari moja aina ya Land Rover rangi nyeusi ambayo bila shaka ilikuwa imetokea njia ya Mpemba kuelekea Tunduma. Gari hiyo ilikuwa kwenye mwendo mkali ambao ulionyesha dhahiri kwamba dereva alikuwa ana mahali ambapo alitakiwa kumfikisha mtu ambaye alikuwa amembeba kwa uharaka zaidi. Gari hiyo ilipofika Kilimanjaro, ilikunja kulia barabara ndogo ambayo iliwazungusha mpaka HIGH CLASS, moja kati ya kumbi kubwa na kongwe ndani ya mji mdogo wa Tunduma. baada ya kufika mitaa hiyo, gari ilikunja kushoto na kuanza kuitafuta barabara kubwa ambayo ulitumika muda mfupi tu kuweza kuifikia nyakati hizo. 

 

Baada ya kuifikia, ilikunja kulia na kuanza kupandisha Mwaka ambako bila shaka ndiko mhusika alikuwa anaelekea nyakati hizo. Wakati huo ambao magari hayakuwa mengi barabarani, gari hiyo haikuwa kwenye kasi kama mwanzo bali ilikuwa kwenye mwendo wa kawaida tu ambao ulikuwa rafiki kwa kila mtu ambaye alikuwa ananufaika na hiyo barabara. Safari hiyo ilienda kuishia kwenye uwanja wa Mwaka, eneo hilo lilikuwa kimya mno majira hayo, hakuonekana mtu yeyote kuwepo eneo hilo zaidi ya taa za umeme ambazo zilikuwa kwenye majengo ambayo yalikuwa hatua kadhaa kutoka hapo.

 

Gari ilisimamishwa eneo hilo kwa muda kidogo, zilipita dakika kumi ambazo zilitawaliwa na ukimya mkubwa, hakukuwa na dalili za mtu kutoka kwenye gari hiyo na baada ya dakika hizo kupita ndipo mlango wa dereva ulipo funguliwa. Alishuka mwanaume mmoja ambaye alikuwa amevaa mavazi ya kawaida ya kiraia, alisubiri mpaka mwenzake wa mlango wa nyuma alipotoka! Walitazama kila pembe ya eneo hilo wakiwa makini mno na baada ya kuwa na uhakika na usalama wake ndipo walipoufungua ule mlango mwingine ambao bila shaka ndio ambao ulikuwa na mlengwa ambaye alikuwa amefika eneo hilo. Alishuka bwana mmoja ambaye kwa mwonekano wake tu alionekana kuwa mtu mwenye asili ya taifa la Zambia, alikuwa ndani ya suti nyeusi huku akiwa amebeba begi dogo kwenye mkono wake wa kulia.

 

Alisimama kwa muda akiwa anayatazama hayo mazingira kwa usahihi, hayakuonekana kuwa mageni kwake lakini hata hivyo sura yake haikuwa kirafiki kabisa kuweza kusadiki ukweli wa mawazo yake. Alihema na kuangalia saa yake na kujisogeza mbele hatua kadhaa, aliangalia tena saa yake lakini ni kama kuna jambo alihisi halipo sawa.

“Mbona hafiki mpaka sasa?” aliuliza akiwa anamgeukia yule dereva”

“Alitakiwa awe hapa kwa muda wa dakika tano zilizo pita, maana yake ni kwamba kuna tatizo” yule dereva aliongea jambo ambalo liliongeza mashaka kwa yule bwana, bila shaka kuna mtu ambaye alitakiwa kuja kumpokea pale nyakati zile ndiye alikuwa anaongelewa kwa kuchelewa.

“Una maana kwamba?”

 

“Toby hajawahi kuchelewa hata dakika moja kwenye jambo lolote, kama mpaka sasa hajafika lazima ameuawa” ile kauli ya dereva ilimfanya bwana yule kugeuka kwa mara nyingine kuweza kuangalia ule upande ambao alikuwepo muongeaji.

“Auawe na nani?”

“Huenda wanajua kwamba wewe upo hapa hivyo tunatakiwa kuondoka haraka”

“Ni sisi watatu tu ambao tunajua kwamba nipo hapa muda huu pamoja na Toby, kwa namna yoyote ile Toby asingeweza kuniuza maana yake ni kwamba….” alipata kigugumizi kuweza kuendelea, ni kwa sababu aligundua kwamba miongoni mwao alikuwepo msaliti ambaye bila shaka alikuwa amewauza. Aligeuka kumwangalia mwanaume yule mwingine ambaye alikuwa upande wa pili wa gari, bwana yule alikuwa na bastola kwenye mkono wake tayari.

“Ni wewe?”

 

“Utanisamehe kwa hili, sikuwa na namna nyingine naweza kufanya. Hawa watu wanataka kila ambaye alikuwa karibu na raisi auawe”

“Wewe leo unaniuza mimi mpuuzi mkubwa wewe nimekutoa kijijini hauna hata maisha?” aliongea kwa jazba na kufoka huku hali yake ikiwa yenye hasira zaidi, hili lilijidhihirisha wazi kwa namna alivyokuwa na hasira kali.

“Maisha yanabadilika ndugu yangu, kunisaidia haina maana mimi niwe tayari kufa kwa ajili yako” bwana yule alimaliza kuongea na kurusha risasi yake kwenda kwa dereva ambayo ilipasua ubongo na kumtupa mbali. Wakati anaigeuzia kwa yule mwingine ambaye alitakiwa kusafiri kwenda Zambia kwa nyakati hizo, yule bwana alirusha begi lake kwa nguvu ambalo lilimyumbisha yule mpigaji ambaye alijikuta anapiga hewa na kurudi nyuma kwani begi lilimyumbisha hesabu zake zote.

 

Aligeuka ghafla lakini wakati anatekeleza hilo alikutana na goti la shingo ambalo lilimyumbisha, alitua kwa goti na kujigeuza ili aruke sarakasi na kusimama. Alipigwa na kibao usoni akarudi ardhini kwa kujibamiza, akiwa anahangaika kujiinua alikutana na mguu kwenye ubavu wake, alitoa ukelele wa mauamivu ila bwana huyo hakuwa hapo kwa ajili ya kumuonea huruma, ngumi yake moja ilipasua pua yake kisha akakitoa kisu kwenye suruali yake ya suti upande wa kiunoni. Alikizamisha kwenye sikio moja kwa kiasi akakitoa na kulikata sikio hilo

 

“Wamekulipa shingapi mpuuzi mkubwa wewe mpaka unanisaliti mimi?” aliuliza kwa jazba pamoja na sauti ya kukata matumaini kwani mpango mzima ulikuwa umeharibika hivyo alitakiwa kukaa upya na kuanza kupanga kwa namna nyingine na alielewa kabisa kwamba muda haukuwa rafiki kwake kwani kila sekunde moja ambayo ilikuwa inaenda, ilikuwa inayahatarisha maisha yake yote. Kabla hajafanya lolote wala bwana yule hajamjibu alishangaa kusikia mlio wa risasi ambao ulipasua kichwa cha kijana wake. Alisita kwanza kugeuka kwa sababu alitambua kabisa kama mhusika ambaye alikuwa aneo la tukio alihitaji kumuua basi mpaka ageuke angekuwa amekufa muda mrefu. Aliangalia pembeni na kugundua kwamba begi lilikuwa karibu yake hivyo akaanza kuhesabu namna ya kuondoka, alipo yasogeza macho mbele kidogo aliiona ile bastola ambayo ilitumika kumuulia dereva wake hivyo akajua kabisa ilimponyoka wakati ule begi linamtinga na wakati yeye anamshambulia, angeipataje? Aligundua kwamba ilikuwa mbali na pale hivyo asingeweza kabisa kuiwahi, wazo pekee ambalo lilisimama kwenye akili yake ni kuweza kukimbia, lakini angekimbiaje mbele ya mtu ambaye alionekana kuwa makini namna hiyo? Alijikuta anayakatia tamaa maisha yake mwenyewe kabla hata hajamuona mhusika ambaye alikuwa nyuma yake. Jambo hilo lilifanyika kwa muda wa sekunde kadhaa tu ambapo akili yake ilikuwa inafanya kazi kwa kasi kubwa zaidi ya mashine.

 

“Alikuwa amepewa zawadi ya uhai ila kwa sasa hana kazi tena. Najua wewe sio mtanzania kwa asili japo ulipewa uraia na watu ambao walikuona wewe unafaa kulitumikia taifa hili. Naweza kusema kwamba nakushukuru kwa kulitumikia taifa langu kwa moyo na uzalendo mkubwa kama vile la kwako lakini kwa sasa hauhitajiki tena kwa sababu kazi ambayo ilikufanya uwepo Tanzania imesha isha hivyo wamiliki mpya wa hili taifa hataki wewe uendelee kuwa hai kwani kuna siku unaweza kuwa tatizo kwao.

 

Hawa watu wanataka wewe ufe kabisa lakini mimi ni mstaarabu ndugu yangu, najua kuna maisha baada ya haya ya wanasiasa ambayo yanatufanya tuuane wenyewe hivyo nitakulipa fadhila ya kukupa nafasi ya kuweza kuishi kwa mara nyingine tena. Nakupa hii nafasi kwa sababu hautatakiwa kuonekana sehemu yoyote ile wala kutambulika kwamba kuna alama za uwepo wako. Nitafikisha taarifa kwamba tayari nimekuua na kwa sababu wananiamini hawawezi kuwa na wasiwasi lakini kufanikisha hili nahitaji uweze kunikabidhi begi ambalo umekuja nalo huku” hayo maelezo ya huyo mwanaume ndiyo ambayo yalimfanya bwana huyo atambue kwamba hakuwa ameliona begi hilo kwanza kutokana na sehemu ambayo alisimama kwani begi ilikuwa karibu na tairi moja ya gari ambayo alikuwa ameiziba na kwakuwa ulikuwa ni usiku, mwanga haukuwa unamulika vyema kwenye vile vivuli.

 

Episode ya Tano ya JUMBA JEUSI inafika mwisho.

 

FEBIANI BABUYA.

Previoua Next