UKURASA WA KWANZA
*****************
MIMI NI MWANDISHI TU
Radi ilipiga kwa nguvu na kuzalisha mwanga mkali ambao ulimshtua mwanaume mmoja ambaye alikuwa ameketi kwenye kiti nyakati za usiku. Bwana yule alipatwa na mshtuko kwakuwa alikuwa kwenye utulivu mkubwa na akili yake ilikuwa inafanya kazi kwa amani hivyo ule mshtuko uliharibu kwa kiasi fulani ule utulivu wake.
Alisimama na kwenda kuchungulia dirishani ili atambue kama huenda kulikuwa na mvua kali inashuka kwa sababu nyumba ambayo alikuwepo haikuwa ikiingiza sauti kubwa ndani yake. Eneo hilo lilikuwa kimya, nje ni manyunyu tu ambayo yalikuwa yakishuka taratibu bila taabu, ulikuwa ni usiku bora kwa wale watu ambao wanaupenda utulivu mkubwa na kuutafuta usingizi mtamu wa pono.
Kwenye nyumba ambayo yeye alikuwepo palikuwa kimya tena na kiza kinene, ni yeye alikuwa amezima taa zote kwa sababu alihitaji utulivu hivyo akawa anatumia taa ndogo ya sola ambayo ilikuwa inamulika mezani tu ambapo alikuwepo yeye. Madirisha na milango yalifunikwa kwa mapazia mazito hivyo hata mtu wa nje asingeweza kuuona ule mwanga wa ndani, alionekana kuwa na jambo la mhimu ambalo alikuwa analifanya kwa wakati ule.
Wakati ananyanyuka mezani taa aliizima hivyo alikaa dirishani kwa muda wa dakika mbili akiwa anahema taratibu na kuyasikilizia mapigo yake ya moyo mpaka pale ambapo aligundua kwamba kila kitu kilikuwa sawa. Alipafunika kama mwanzo na kurejea kwenye meza yake huku akionekana kutofurahishwa na mshtuko ule wa radi japo alijua hakuwa na jambo la kufanya kuhusu radi ile.
Aliketi tena kwenye kiti na kuiwasha taa yake vizuri mezani. Kwenye ile meza kulikuwa na vitabu vingi, alionekana kabisa kwamba alikuwa ni mtu ambaye alipenda kusoma vitabu kama haikuwa kazi yake kabisa kuweza kuandika baadhi ya hivyo vitabu. Kuna kitabu kimoja kilikuwa mbele yake na bila shaka wakati ile radi inapiga ndicho ambacho alikuwa anakipitia.
TONE LA DAMU ndilo lilikuwa jina la kitabu, ni kitabu kilicho onekana kuweza kumgusa vilivyo ndiyo maana alikuwa anakisoma kwa umakini usiku mzito tena akiwa amejifungia mwenyewe. Ni kitabu ambacho ndani yake kilionekana kuwa na mambo makubwa na mazito kwa sababu mwandishi wa kitabu hicho mpaka wakati huo hakuwa akitambulika kama amekufa au yupo hai kwa sababu ni hicho kitabu ambacho kilimuingiza matatizoni hivyo bwana huyo alikuwa anahitaji kuweza kujua ni mambo gani ambayo mtu huyo aliyaandika kitabuni mpaka yakamuingiza kwenye hatari kubwa ya maisha.
Alikuwa amekata kurasa za kutosha hivyo kwa namna fulani alikuwa ameshaanza kuelewa kwamba ni jambo gani lilikuwa linaendelea. Aliufunua ukurasa mwingine kwa ajili ya kuanza tena kuusoma lakini alishtuka kwa mara nyingine na kukosa utulivu. Awamu ya pili haikuwa sauti ya radi tena bali mlio wa simu yake ndio ambao ulimshtua, ilikuwa ni simu janja ambayo kwa kumbukumbu zake ilikuwa na zaidi ya masaa manne bila kuigusa jambo ambalo lilimfanya aweze kuisahau kabisa kama ipo mezani hapo ambapo alikuwa anasomea.
Aliangalia saa yake mkononi na kugundua kwamba ilikuwa ni saa nane usiku, alishangaa kupigiwa simu majira kama hayo kwa sababu haikuwahi kutokea kwa nyakati kama hizo. Aliinyanyua na kuiangalia ile namba lakini aligundua kwamba ni namba ambayo hakuwahi kuwa nayo na namba ile ilionekana kabisa kwamba inatoka ndani ya taifa la Wazulu huko kwa Mandela yaani Afrika ya Kusini. Alijishauri mara mbili kuweza kutambua kama aliwahi kuwa na marafiki huko lakini jibu lilikuwa hapana, akawaza kama yeye alikuwa ni mtu mhimu kwa watu kiasi kwamba wamtafute usiku kama huo jibu likawa hapana. Sasa alianza kuwaza kwamba ni nani alikuwa anampigia wakati kama huo?
Kusita kwake kulimfanya aamue kutoipokea simu hiyo kwa sababu aliwahi kusikia kuhusu matapeli wa mitandaoni aliona kabisa kwamba wangempotezea muda wake tu na kusingekuwa na la maana lolote hivyo akaipotezea kwa kuikata. Kuikata kwake ikawa safari nyingine ya kuweza kuiruhusu simu hiyo kuanza kuita kwa mara ya pili kwa fujo ile ile, kishingo upande aliamua kuipokea simu hiyo kisha akawa kimya kuweza kumsikiliza mtu wa upande wa pili.
“Nenda Temeke Mwisho nyuma ya stendi ya Mtwara kuna gereji moja pale, ukifika simama kuna mtu anakuja kukupatia ushahidi wa mauaji wa mwandishi wa habari Amani Kilonzo” ilisikika sauti nzito kutoka upande wa pili ambayo ilimshtua kiasi kwamba alitoa simu sikioni kuhakiki tena ile namba maana mhusika alionekana kwamba anamfahamu yeye vizuri.
“Wewe ni nani?”
“Mpaka nakupigia simu ni kwa sababu nakuamini sana hivyo nina uhakika kwamba wewe ni mtu pekee ambaye unaweza kulifanya suala hili likawa wazi. Ni nafasi moja tu kwenye maisha yako kuweza kufanya jambo ambalo ni sahihi kwa sababu kama ukiukosa huu ushahidi hii leo basi hautakuja kuupata tena na huenda mwenye nao anaenda kufa baada ya leo”
“Ushahidi wa nini?”
“Wa kila kitu kilicho tokea. Nakupa nusu saa tu uwe pale vinginevyo nikutakie maisha mema” haikuwa sauti ya kubembeleza kabisa kwa sababu mhusika alionekana kulazimisha jambo hilo kuweza kufanyika. Alibaki akiwa anausikilizia upande wa pili mpaka pale alipo tambua kwamba simu ilikuwa imekatwa akiwa amebaki kwenye mataa.
Alikuwa anawaza kwamba ni nani ambaye alikuwa amempigia yeye kumpatia taarifa hizo, alikuwa na lengo lipi hasa la kuweza kumlenga yeye na kwanini amuamini kiasi hicho? Njia ya kuweza kuujua ukweli ilikuwa ni moja tu pekee, kuweza kukutana na mtu ambaye alidaiwa kuwepo huko Temeke Mwisho majira hayo ya usiku wa manane. Aliwaza kwa muda kidogo akaamua kutokwenda kwa sababu aliamini kwamba huo unaweza kuwa mtego mbaya kwake na ikala kwake, lakini aliwaza mbona hana maadui kiasi kwamba awekewe mtego kama huo? kama mtu huyo angehitaji kumdhuru si angemtafuta kwa namna nyingine? Alihisi kwamba huenda kulikuwa na umuhimu wa yeye kuweza kwenda hilo eneo ajionee yeye mwenyewe.
Alikuwa amefanya maamuzi ya kwenda huko kuweza kuona yale ambayo yalikuwa yanaendelea na hatima ya hayo mambo ingekuwa vipi. Alinyanyuka na kufunika kila kitu akasogea kwenye dirisha moja, pembezoni mwa lile dirisha palikuwa na switch ya taa ya umeme, aliibonyeza kwa muda mrefu mpaka ikatoa mlio kama wa kitu kufunguka, ukuta ulijigawa kiasi akaivuta droo moja nzito kisha akaweka nywila kadhaa na kuvuta bastola ndani ya hilo eneo. Pembezoni palikuwa na kisu kirefu kiasi na kipana, alikiangalia kwa muda kisha akakipakia kiunoni.
Mwanaume huyo alivuta funguo na kutoka nje eneo hilo likiwa kimya bado, aliingia kwenye gereji yake na kufungua ambapo alienda moja kwa moja na kuingia kwenye gari ambayo aliitoa taratibu mpaka nje ya geti. Alihakikisha amefunga geti kwa rimoti na kutoka hilo eneo kwa kasi kubwa kuweza kuwahi Temeke mwisho kwa sababu kuwaza waza kwake kulimlia muda hivyo alitakiwa kuufidia ili asije akampoteza mtu wake ambaye alimpatia nusu saa tu ya kuweza kumuwahi mhusika wake.
Alitumia dakika ishirini kutembea na kasi ya mwewe, ulikuwa usiku na mvua ilikuwa inazidi kushuka hivyo njia hazikuwa na watu kabisa. Eneo lilikuwa tulivu na kimya, ni maeneo kadhaa tu ambayo yalikuwa yanakesha kwa biashara ndiyo alikuwa anaona watu wa kuhesabu, wale ambao starehe kwao walizipa umuhimu kuliko hata maisha ya kuweza kujitafutia ridhiki mtaani. Maisha ya jiji hayakuwa yakimshangaza kuona vitu kama hivyo kwa sababu alikuwa ameyazoea kwa miaka na miaka, dakika ya ishirini ilimkutia akiwa SUDAN.
Alisogea pembezoni mwa barabara njia ya kuelekea Tandika Sokoni akapaki gari pembezoni na kushuka. Mvua bado ilikuwa inateremka kwa wingi ila hakujali, alivaa hood safi kabisa kisha akaanza kutembea kwenye mvua kuelekea stendi. Aliangalia saa yake na kugundua kwamba alikuwa amebakiwa na dakika tano hivyo alikuwa anaenda sawa na muda, eneo hilo ambalo mchana huwa linatawaliwa na wafanya biashara wengi huku maduka ya vifaa vya magari na pikipiki yakiwa yamesheheni na mafundi wa kutosha lakini kwa usiku ilikuwa tofauti kabisa.
Eneo lilipoa, alikuwa anaielewa vizuri mitaa hiyo kwa sababu ilikuwa ikitawaliwa na vibaka wengi ila hawakumpatia homa kwa sababu hakuwa anawahofia. Ni majira hayo ya mvua alitambua kwamba hata wao walikuwa wamejificha ili wasipatwe na hiyo kadhia ya kuanza kuloa bila sababu za msingi kwa sababu tu ya kutaka kukaba watu ambao nao kwa hali kama hiyo usingeweza kuwapata. Alifika mpaka stendi na kuona gari kadhaa tu zikiwa zimepaki, hakuonekana mtu hata mmoja na hata zile ofisi za kukatishia tiketi za magari zilikuwa zimefunga hapo ndipo akakumbuka kuiangalia saa yake tena na kugundua kwamba ilikuwa saa tisa.
Alikunja kulia na kunyoosha mpaka ndani ya gereji moja ambayo haikuwa mbali na hapo na ndiyo gereji ambayo ilikuwa ikitumika kutengenezea magari mengi ambayo yalikuwa yakienda mikoa ya nyanda za juu kusini. Alipofika sehemu ya kuingilia alisimama kwanza, alisimama kwa sababu usalama ulionekana kuwa sifuri kabisa baada ya kuona walinzi wakiwa wamelala. Haukuwa usingizi wa kawaida walionekana kuzimishwa watu hao, aliivuta bastola yake taratibu akiwa anahema kwa utulivu mkubwa ambao haukuwa unaendeshwa na hofu ndani yake.
Alihisi kuna mtu nyuma yake ila wakati anahitaji kufanya maamuzi ya kugeuka alikuwa amechelewa hususani baada ya kuguswa na kitu cha ubaridi kisogoni. Alikuwa kwenye mikono ya mtu mwingine hali ambayo ilimhitaji yeye kuwa mpole kwanza kwani hatima ya maisha yake ilikuwa kwenye mikono ya huyo mtu na alilielewa hilo vizuri kabisa.
“Nipatie bastola yako” ni sauti nzito upande wa pili ilisikika hivyo hakuwa na namna zaidi ya kumpatia kwa nyuma bwana huyo bastola.
“Tembea” alianza kujongea taratibu mpaka wakafika karibu na gari moja bovu ambalo lilionekana kuendelea na matengenezo’’
‘Simama na ugeuke” alipo geuka tu yule mwanaume aliishusha ile bastola, ni mwanaume mmoja ambaye alionekana kuwa na hofu ndani yake, hakuwa na utulivu.
“Tunajuana kabla mimi na wewe?’’
Ndo kwanza tunaufungua ukurasa wa kwanza kabisa wa simulizi hii. Ungani nami mwanzo mpaka mwisho ili uweze kujua hatima ya hawa waandishi na hawa wanadamu ambao wamekutana hili eneo la Temeke.
Febiani Babuya.
Comments