“Sipo hapa ili kuweza kujibu maswali yako”
“Ila?”
“Sina muda mrefu wa kikaa hapa ila kuna mzigo ambao inabidi ubaki nao na hakikisha hakuna mtu hata mmoja anakuja kujua kwamba unao”
“Ndo wewe ambaye tulikuwa tunaongea kwenye simu?”
“Hiyo haijalishi tena”
“Kwanini mimi?”
“Haya tutayaongea muda mwingine ila kwa sasa unatakiwa kuondoka hili eneo haraka sana”
“Ulikuwa unafuatiliwa?”
“Sina uhakika na hilo” mwanaume huyo alimsogelea mwandishi huyo na kumkabidhi frash moja ndogo na bastola yake.
“Tunaweza tusionane baada ya hii leo hivyo hakikisha unayafanyia kazi ambayo yapo ndani ya hiyo frash. Ni watu wengi wameyaweka maisha yao rehani ili tu wewe uweze kuipata hiyo frash kwakuwa wana imani kubwa na wewe, natumai hautawaangusha watu hawa ambao damu zao zimepotea kwa sababu hiyo”
“Kwanini unaniamini na hatufahamiani?” mwanaume huyo alitabasamu na kuanza kuondoka ambapo alidunda kwenye gari moja na kutua juu ya paa la nyumba kisha akaishia upande wa pili. Mwandishi alibaki ameganda pale pale akiwa kama haamini bado, alikuwa anahisi anaangalia ni sinema na maisha yale yangeweza kufika mwisho mpaka alipo tambua kwamba haikuwa sinema ile bali yalikuwa ni maisha ya kweli kabisa ambayo yeye alitakiwa kuweza kuyapitia.
Kuwaza waza kwa muda kulimfanya apoteze sekunde arobaini akiwa haelewi anatakiwa kufanya nini kwa wakati ule, maamuzi yake yalikuwa ni kumfuatilia yule bwana aweze kujua kwamba alikuwa anaenda wapi kwa wakati ule na alikuwa ni nani haswa mpaka kumuamini kumpatia siri ambazo alidai zilikuwa na majibu yote kuhusu vifo vya watu wawili ambao walipotea kwenye mazingira ya kutatanisha. Alitembea kwa kasi na kudunda kwenye tairi ya gari akatua juu ambapo hakusimama akaudaka ukuta na kurukia upande wa pili.
Mwandishi alianza kushangaza kwa uwezo ambao alikuwa nao mwilini mwake, alikuwa ni mtu wa kuishika kalamu na kompyuta mpakato tu muda wote kwa ajili ya kuandika. Alipotua upande wa pili aliona alama za miguu ya mabuti ambayo aliyavaa mwanaume yule zikiwa zinaelekea kwenye uchochoro mmoja ambapo alilazimika kuweza kuzifuata kwa sababu aliamini kwamba ndiko ambako bwana huyo alielekea kwa wakati huo.
Alianza kuufuata akiwa anatembea kwa umakini kwa sababu mitaa haikuwa salama kwa nyakati kama hizo, alisimama baada ya kusikia vishindo vya watu vikiwa vinasogea kila alipokuwa anapiga hatua. Alisimama na kusikiliza vizuri ndipo akagundua kwamba hazikuwa hatua za kutembea bali ni watu walikuwa wanapigana akatambua kwamba huenda yule mtu ambaye alikuwa amekuta naye alikuwa amevamiwa na ndiyo sababu ambayo ilimfanya yeye kumtaka mwandishi huyo kuweza kuondoka haraka hilo eneo kwa sababu alitambua hata yeye anaweza kuuawa na ile kazi kubwa ambayo alidai kwamba watu wengi waliitolea jasho ingeishia njiani.
Alikimbilia lile eneo na wakati anafika pale alimuona yule mtu ambaye alimpatia frash akiwa anazamishiwa kisu kwenye kifua. Mwanaume yule alijibetua na kukita buti zito kwenye shingo ya yule mwanaume ambaye alimzamishia kisu mpaka akayumbia pembeni. Alikivuta kile kisu na kukirushia pembeni ila kilionekana kumuathiri kwa sehemu kubwa kwa sababu damu nyingi ilikuwa inamvuja. Yule mwanaume ambaye aliyumbia pembeni, alijikusanya na kutembea kama umeme kwenye maji akiwa anayapiga kwa nguvu ambapo ni wazi kabisa yalimchanganya mvamiwaji hivyo akawa hamuoni mwanaume yule wakati anakuja.
Alijua habari yake imeisha na alikuwa tayari kwa ajili ya hilo hivyo aliyafumba macho yake mpaka alipo sikia kishindo kikali kwenye ukuta wa pembeni. Alipofumbua alishangaa kumuona yule mwanaume ambaye alikuwa anamjia akiwa ananyanyuka huku anavuja damu na mguu wake umeteguka ndipo akageukia pembeni yake na kushangaa kumuona yule mwandishi akiwa amesimama. Akiwa anaendelea kujiuliza maswali ambayo hakuwa anapata majibu yake kwa wakati ule alisikia sauti ya mwandishi yule;
‘Run’’ alitakiwa kuondoka eneo lile. Alibaki njiapanda kwa sababu yeye alitakiwa kujitoa sadaka ili mwandishi yule awe hai kwa namna yoyote ile lakini kwa wakati ule yeye ndiye alikuwa anaambiwa akimbie tena? Kwake hakuona kama ni jambo ambalo lilikuwa linawezekana, ile frash ilikuwa na mambo mengi mno mhimu na kwa akili yake alijua lazima wale watu wamuue yule mwandishi lakini wakati akiwa amefanya maamuzi ya kutoondoka eneo hilo alisikia sauti kali tena.
‘Ruuuuuuuuun’’ mpaka akawa anaogopa na kuanza kuondoka kwa kukimbia akiwa anachechemea huku ameshikilia mkono mmoja kifuani kwake. Akiwa anaendelea kukimbia, mwanaume mmoja alikuwa anaelekea ule upande wake kwa spidi kubwa kwa sababu hakutaka kumruhusu yeye kuweza kupotea kirahisi namna ile. Bwana yule alisimama ghafla baada ya kisu kukita kwenye kuta ya nyumba akabaki anahema kwa sauti ya juu, kile kisu kama angetembea kidogo mbele kingetoboa uso wake hivyo kilipita kwa sekunde zaidi kikaikosa pua yake. Aligeuka kuangalia ni nani alikuwa amekirusha, alikuwa ni yule mwandishi basi hakuwa na haja ya kumfukuza yule ambaye alikimbia, walitakiwa kumalizana na yule mwandishi ambao wao hawakuwa wanamjua ni nani kwa sababu ya hood ambayo alikuwa ameivaa.
Walikuwa jumla yao wanne, mmoja alikuwa ameteguliwa mguu wake akiwa anavuja damu lakini hakuwa mnyonge. Walionekana kuwa wanaume mithili ya mashine, miili ilishiba vizuri na bila shaka walikuwa ni watu wa kazi kwelikweli. Mwandishi yule mpole na mstaarabu alikuwa amesimama akiwa anawatazama mabeberu wale lakini kuna jambo hakulishtukia, kuna mwanaume alimpiga picha wakati amekirusha kile kisu hivyo uso wake ulionekana.
Mwanaume ambaye alikuwa mbele alitembea kwa nguvu kubwa kwenye maji, alijipinda na kugeuka kwa miguu yote miwili. Aliirusha kwa nguvu na kudunda kisha akabinuka tena baada ya kumkosa mwandishi. Nguvu ambazo alikuwa anazitumia zilikuwa zinatisha mno, buti moja lilitua begani mwandishi akayumbia upande wa pili, alipokuja kukaa sawa aliona ngumi nzito inakuja upande wake ambapo alijizungusha na kuupishanisha mkono wa yule mwanaume.
Aliuvunja ule mkono na kuipasulia shingo yake ukutani tena ghafla. Nguvu ambayo aliitumia kuishika ile shingo na kuibamizia ukutani haikuwa inaendana na mtu ambaye alikuwa anashinda kwenye kalamu kuandika pamoja na kushika kompyuta muda wote. Watu wale walishangazwa na hali ile hivyo wakamuendea wote ambapo alirudi nyuma kidogo na kukivuta kile kisu ukutani.
Walipo mkaribia aligeuka nyuma na kudunda kwenye ukuta ambapo aliruka sarakasi tano za harakaharaka akiwa hewani. Alimdaka mmoja na kumvutia upande wake ambapo alimtoboa toboa shingoni kisha akageuka na kisu kwenye moyo wa mwingine na kukiharibu kifua vibaya. Yule mmoja ambaye alibakia pale ni yule ambaye alikuwa amemtegua mguu wake, alimpiga risasi zote ambazo zilikuwa kwenye bastola habari yake ikaishia pale pale. Wanaume wanne tena ambao walionekana kuwa hatari waliuliwa na mwandishi ndani ya dakika mbili, mwandishi huyo hakusimama hilo eneo alitoweka haraka bila kujua kama sura yake ilipatikana.
Muda ambao aliutumia kuyatekeleza yale mambo, yule mwanaume ambaye alikuwa amemletea frash, alikuwa amejibanza kwenye paa moja la nyumba akiwa kwenye maumivu kuweza kushuhudia jambo lile. Hata yeye mwenyewe alibaki anaogopa, mwandishi alikuwa zaidi ya yale ambayo wao walikuwa wanayajua, alibaki na maswali mengi kuhusu maisha ya mwandishi yule mpole na mstaarabu tena mtu ambaye hakuwa na umaarufu. Yale mambo aliyajulia wapi na mbona kama kuna mengi wao hawakuyajua kutoka kwake? Alibaki amechanganyikiwa lakini hata hivyo haikuwa sehemu salama ya yeye kuendelea kuwepo hivyo aliondoka haraka iwezekanavyo.
Ukurasa wa pili unafika mwisho.
Febiani.
Comments