Reader Settings

“Ni watu wa namna gani walitumwa kuifanya kazi hiyo”

“Wote wanadaiwa kuwa ni watu wenye uwezo mkubwa kwenye mapigano”

“Na wamekutwa wakiwa wamekufa?”

“Ndiyo”

“Kwa maana hiyo mhusika pia ni mtu ambaye hana uwezo wa kawaida?”

“Hilo sio swali Kato”

“Yule mwandishi wa habari alikuwa na umuhimu gani kwa watu mpaka wakati kama huu aweze kuwa gumzo na watu waonekane kutaka kuzifukua zile habari ambazo zilizikwa kwa gharama kubwa?”

“Kwenye kundi la watu wengi, watu hatari zaidi ni wale ambao huwa wanainamisha vichwa vyao. Mara nyingi watu wa nanma hiyo huwa wanajifanya kama vile hawaoni yanayo totea, jambo ambalo huwa linamfanya adui aweze kujisahau na hapo ndipo huwa wanaibuka kutokea maeneo tofauti na kuweza kushambulia. Wale ambao huwa unawaona ni wapiga kelele kwenye mitanao huwa hawana la maana lolote wala sio hatari ndiyo sababu hata serikali yenyewe ya Tanzania iliwapuuza ila kuna watu wanaonekana kwamba walikuwa wanalifuatilia jambo hili kimya kimya na mpaka wameamua kujitokeza maana yake ni kwamba lazima watakuwa na ushahidi wa jambo hili”

“Kama watakuwa na ushahidi hata sisi tutajulikana kuhusu uhusika wetu kwenye hili. Hii haitaleta sura nzuri kwetu kwani kila kitu kinaweza kuwa wazi”

“Ndiyo maana nataka kutuma watu wangu kule kwa siri, hii ni kama tahadhari kwa sababu mhusika ambaye alikuwa anafuatiliwa ni kwamba kuna mtu alikuwa ameenda kukutana naye na kama hilo ni kweli maana yake huenda kuna vitu alitaka kumkabidhi na kama amesha mkabidhi hatupo salama mpaka sasa”

“Mhhhhh sikutegemea kama nitapokea habari mbaya kwenye nyakati kama hizi ambazo niliona kama ni muda wa kula matunda ya muda mrefu. Wamefanikiwa kumjua mtu ambaye bwana huyo alienda kukutana naye?”

“Hapana, hakuna ambalo wanalijua mpaka sasa”

“Huyu mtu ni nani na kwanini aje kwa wakati kama huu?”

“Hilo ndilo jambo ambalo tunatakiwa kulifanya kwa sasa, tusimtegemee mtu mmoja kuifanya kazi hii. Wakati wao wanaendelea kumtafuta mhusika, na sisi tunapaswa kuwa makini na kulifuatilia kwa njia zetu na kama ikishindikana basi tukate mzizi ambao unaweza kuonyesha uhusika wetu kwenye hili jambo wabaki wao kwa wao”

“Unahisi hilo linawezekana?”

“Kama ndiyo itakuwa njia pekee ya kuweza kuwa salama itatakiwa itafutwe njia ya kufanya hilo lakini kwanza kabisa nataka kuwajua hawa watu ni akina nani, wanafanya kazi na nani na wanafanya haya kwa maslahi yapi ili kama ni watu ambao wanaweza kununulika tumalize hii biashara haraka”

“Unataka nifanye jambo gani mheshimiwa?”

“Kwa sasa nahitaji ulifuatilie jambo hili kwa nguvu zako zote, nitakupatia vijana ambao wewe ndiye utawasimamia kwa sababu unaelewa kabisa kwamba sitakiwi kujulikana kwamba naingia kwenye skendo mbayambaya kama hizi hususani kwa nafasi yangu’’

“Wanatakiwa kwenda lini Tanzania kwa ajili ya hii kazi?”

“Leo usiku”

“Vijana wangapi?”

“Kumi”

“Vijana kumi kwa ajili ya kuhangaikia kesi ya mwandishi wa habari tu?”

“Nikiwa na miaka ishirini na tisa nilipo fanikiwa kupanda cheo, mimi na wenzangu tulienda kukamata majambazi maeneo ya Kampala mimi nikiwa ndiye kiongozi wa kikosi. Kwenye eneo lile tulimkuta mtu mmoja tu ambaye alikuwa jambazi hivyo tulijaa kiburi na sifa tukamdharau kwa sababu tuliona kama sisi ni watu ambao tulikuwa na mafunzo hivyo tungeweza kufanya lolote lile ila mpaka wakati huu naongea na wewe hapo kati yetu sisi saba ambaye alifanikiwa kutoka salama lile eneo ni mimi pekee. Wenzangu wote waliuawa usiku ule na mimi nilipona kwa sababu nilikuwa na mbio kali vinginevyo ningekufa siku ile ile. Kama umenielewa basi utajifunza kuheshimu mipango ya watu ambao hauwajui na hujui kwanini wanafanya yale ambayo wanayafanya’’ Generali Kagimu alimaliza mazungumzo yake ambayo kiuhalisia ni kwamba yalikuwa tata, aliondoka na kumuacha generali Kato akiwa kwenye mawazo kwa sababu alidai kwamba hata wao walikuwa wamehusika kwenye jambo ambalo lilionekana kuanza kushika hatamu kwa siri.

VWAWA, SONGWE.

Mtaa wa Mwenge Vwawa Mbozi, moja kati ya sehemu ambazo zinaaminika kwa kuwa na watu wastaarabu ndani ya mkoa wa Songwe ni Vwawa. Ni eneo tulivu ambalo linajumuisha maisha ya watu wa hali ya juu na hali ya kawaida lakini wengi wa eneo hilo ni wale watu ambao wana maisha ya kati, yale maisha ya mtanzania ya kula milo mitatu na kuendelea na maisha mengine ya kawaida.

Eneo hilo linapatikana kwenye moja ya ukanda ambao unasifika kuwa na utajiri mkubwa wa ardhi, ardhi ambayo ni sehemu mhimu kwa ajili ya shughuli za kilimo. Ni eneo ambalo wanapatikana watu wa makabila tofauti tofauti hususani Wanyiha ambao ni wengi zaidi kwa sababu watu wengi ambao wanaishi eneo hilo wametokea vijijini ambako wengi wao wanaiongea hiyo lugha ya Kibantu.

Kwenye hilo eneo la Mwenge, watu walikuwa wanaendelea na shughuli za maisha kama ilivyokuwa kawaida kwa kila mtu kuendelea kuupambania mkate wake wa kila siku. Kuna baadhi ya watu ambao walikuwa wamejipata kwenye maisha yao ama wale watoto ambao walizaliwa kwenye familia zenye uwezo wa juu walikuwa wakiamini kwamba wengine kuishi kwenye maisha magumu ilikuwa ni kwa sababu ya uvivu ama kuwa wazembe jambo ambalo halikuwa la kweli kwa sababu kuna watu walikuwa wapambanaji wakubwa lakini bahati haikuwa upande wao hivyo wakijikuta bado wanaishia kwenye ufukara mkubwa.

“Kijana wangu haya maisha ni zaidi ya zile tamathali za semi, ni rahisi mno kuzisoma zikiwa ubaoni au kitabuni lakini ukija kwenye maisha ya ukweli zile ni ngumu sana kuzifuata na muda mwingine unaweza usizielewe. Zile zinapatikana ndani ya fasihi, wewe ni msomi nina imani unaelewa kwamba hapa nipo nazungumzia kitu gani. Fasihi ni maisha yako na zile tamathali za semi ni jumla ya mambo yote ambayo wewe unakutana nayo kwenye maisha yako ya utafutaji mpaka ile siku ambayo unakuja kufa na kupuzishwa kaburini.

Nimekufahamu kwa muda, wewe ni kijana mmoja mtiifu, mwenye nidhamu kubwa lakini hauna uoga, hali hii itakufanya wewe uweze kufika mbali tofauti kabisa na vijana wengine wa umri wako ambao mpaka sasa hawajui waweze kufanya nini. Unaweza ukajiuliza kwamba ni kwanini leo nimekaa hapa nikiwa nakwambia mambo yote haya ambayo pengine kutokana na umri wako unaweza usione kama ni ya mhimu kuweza kuambiwa lakini niamini mimi kijana wangu, haya yote yatakutokea wewe kwenye maisha yako na ni lazima tu uyapitie.

Mimi nikiwa na miaka ishirini na mitano nilifanikiwa kumpatia mwanamke mmoja mimba lakini kwa sababu ya tamaa za ujana wangu nilimkataa na kumlazimisha aweze kuitoa ile mimba lakini haikuwa hivyo. Mwanamke yule aligoma kabisa kutoa mimba ile na hatimae baadae akaja kufa yeye na mtoto wakati wa kujifungua, kuna watu kwenye huu ulimwengu huwa hawaamini kweye hatima na laana ila hivyo vitu vipo kwa sababu yamenikuta na vyote hivyo mimi navipitia mpaka leo hii. Ile ilikuwa kama ni laana kubwa na mbaya sana kwangu kwa sababu tangu pale mambo yangu yalianza kuyumba, sio kwa upande wa maendeleo tu bali kwenye kutengeneza familia pia kwa sababu baada ya kumkana yule mwanamke sikuwahi kuja kupata tena mtoto.

Nimejaribu kila njia ambayo umewahi kuisikia wewe hapa duniani lakini nimeshindwa, ilifikia hatua nikawa nimeamua kuyabeba tu maisha yangu lakini napo bado ilishindikana mara mbili ambayo nilijaribu kufanya hivyo. Mungu aliamua kuniadhibu nikiwa hai, alitaka mimi niwe shuhuda kwa watu wengine ndiyo maana nakusihi kuhusu maisha mwanangu ili usije kuyarudia makosa ambayo yanafanywa na wanadamu wengi na mwisho wa siku huwa yanaishia kuwa majuto makubwa na wengi hutamani kama wanaweza kurudisha muda nyuma waweza kuyafanya kwa usahihi zaidi lakini hilo halipo kwenye maisha haya.” Alimeza mate mzee huyo akiwa anaukata mhindi wa kuchoma na kumpatia kijana mdogo ambaye alikuwa pembeni akiwa anamsikiliza kwa umakini huku kwa mbali kukiwa na manyunyu ya mvua. Ni kijana wa miaka kumi na saba ndiye alionekana kuwa karibu yake. Alitulia baada ya kuona wote wapo sawa, aliendelea;

Ukurasa wa nne unafika mwisho.

Febiani Babuya

Previoua Next