“Zamani wakati sisi tunakua maisha yalikuwa tofauti na sasa, zamani nilikuwa naweza kwenda kwa jirani yangu shambani kwake nikala mpaka nikashiba kisha nikaondoka kwenda nyumbani kwangu ilimradi niwe mstaarabu tu lakini kwa miaka hii hili jambo haliwezekani. Kwa sasa hata ukiiba maji ya kunywa tu nyumba ya jirani hapo lazima watakuua, maji tu unauawa, angalia dunia inako elekea mwanangu. Maisha ya sasa yanamfundisha mwanadamu namna ya kuwa mtu katili kwenye jamii, dunia haitupatii ile haki ya kujua namna ya kuishi kwa usahihi na wadamu bali inakutaka wewe uwe mkatili zaidi kwa wanadamu wenzako ili uweze kuwa juu yao kwa kila kitu.
Hapo baadae kikaingizwa kitu kinaitwa dini, kwa hili huwa nashindwa kuwalaumu hawa mabepari na wageni ambao waliwahi kuingia kwenye ardhi ya Afrika kwa sababu mpaka sasa sijajua dhumuni halisi la ujio wa hizi dini. Kwa akili yangu nilitamani kama dini ingekuwa sehemu ya kutoa tumaini kwa watu, ingekuwa sehemu ya kukumbushana kwamba sisi ni wanadamu tu na maisha yetu yana mwisho hivyo tunapaswa kuishi kwa amani na upendo kwa sababu siku moja hatutakuwa sehemu ya huu ulimwengu. Ajabu siku hizi ni kwamba dini imekuwa sehemu ya kutishia watu, sehemu ya biashara ya ulaghai ambapo watu wameanza kukata tamaa kuhusu uhalali wa Mungu. Kuna watu hawana imani tena kuhusu uwepo wake kwa sababu ya tamaa za watu kadhaa tu ambao wanautumia mlengo wa dini kukamilisha mambo yao na……” mzee huyo alitaka kuendelea lakini alikatishwa, kijana yule alikuwa na swali ambalo lilimkaba kwenye shingo yake na alitamani kuweza kupata majibu yake kwa wakati huo.
“Mzee kwamba dini ni utapeli na sio jambo la kweli kama linavyo hubiriwa?” mzee alitabasamu kidogo lakini halikuwa tabasamu lile la kuonyesha furaha kubwa kwa sababu ndani yake alikuwa na majuto mengi na mambo ya kutisha ambayo yaliwahi kumkuta siku za huko nyuma.
“Haahaha nafurahi kwamba upo makini pia kwenye kumjua Mungu. Ukweli ni kwamba dini sio utapeli na wala haijawahi kuwa utapeli kijana wangu ila matapeli ndio ambao wamevamia dini siku hizi na kuanza kuifanya dini ionekane kama ni utapeli na uhuni jambo ambalo sio kweli. Kuna namna unaweza ukawa na uwalakini kuhusu baadhi ya vitu ambavyo walituletea hawa wenzetu wakati wanakuja kwenye bara letu hili lililo barikiwa lakini sio kuwa na shaka kwamba dini ni utapeli.
Dini ni misingi ya maisha ya watu, dini ni misingi ya imani, dini imekuwepo hata kabla ya hawa watawala kuweza kufika. Dini ilikuwa ni imani ya kuweza kuifikia nguvu kubwa ambayo ni msaada mkubwa kwa maisha ya mwanadamu na mwenye hiyo nguvu ndiye tunamuita Mungu ila walipokuja wageni kidogo namna ya hizo imani ilianza kubadilika. Kwenye imani ambazo wao walizileta ndizo ambazo zimefanya mpaka baadhi ya watu kuwa na wasiwasi na kuhisi kwamba dini ni jambo la kitapeli na ulaghai. Unajua wanadamu tupo tofauti kwenye kuzaliwa, uumbaji na namna watu wanavyo yaishi maisha yao.
Kuna watu ambao wanaishi wakiwa wanazitafuta fursa kila sehemu, kwao kila kitu kinakuja na fursa mpya za maisha hivyo hata kwenye dini watu waliona mlango wa upigaji na ndipo hapo masela wakaanza kuingia kila sehemu kuhakikisha tu kwamba wananufaika na zile hofu za watu kupitia dini. Watu wengi leo hii ukiwajaza hofu kupitia Mungu basi wapo radhi kufanya lolote lile ili kuweza kuiondoa hofu yao na ndipo ulimwengu ulipokea uwepo wa manabii wasio isha kila kukicha mwanangu, utapeli na uwizi kwenye dini ulizaliwa hapo”
“Kwahiyo manabii wote wa siku hizi ni matapeli na wafanya biashara?”
“Nikisema ni wote basi nitakuwa nawakosea wale wote ambao wamekuja kwa nia nzuri na ni kweli ni mitume wa Mungu ila naweza kukuhakikishia kwamba asilimia zaidi ya sabini ni wafanya biashara na wengine ni matapeli. Siku hizi dini inauzwa kijana wangu, ogopa sana mtu anakuuzia neno la Mungu au kukuahidi kukusaidia baada ya wewe kumlipa, neno la Mungu ni la bure, sasa kwanini ulipie? Jitahidi kwenye maisha yako kichwa kisiwe mzigo kwa shingo yako”
“Sawa mzee” alijibu kinyonge huku akianza kuzivuta hatua zake kutaka kuondoka mahali hapo lakini mzee huyo aliyavuta mahindi kadhaa kwenye mfuko na kumpatia.
“Mdogo wako anaendeleaje kwa sasa?”
“Bado hali yake sio nzuri sana mzee”
“Mungu amekupatia mtihani mzito kwenye maisha yako ila hakikisha kwamba unapambana nao na unauvuka. Kwa umri wako huo kupata majukumu mapema namna hiyo ni jambo ambalo litakukomaza haraka lakini utapitia mateso mengi. Fanya kila namna kuhakikisha dada yako anakuwa salama na usiruhusu yeye ndiye aje kusimama kwenye nafasi yako kwa sababu huu ulimwengu hauna huruma kabisa kwa mtoto wa kike ambaye ana maisha magumu.
Usiruhusu mdogo wako kuwa daraja la wanaume ambao wamezoea kuharibu ulimwengu kulipitia, pigana, soma sana na upambanie maisha yako kuhakikisha siku moja mdogo wako anaishi maisha mazuri. Wewe ni mtoto wa kimaskini, familia ambayo umetokea haitakiwi kwa namna yoyote uweze kupoteza lolote na hauna msaada wa mtu hata mmoja hivyo msaada wako mkubwa ni kalamu na daftari lako. Inaweza isikuhakikishie maisha mazuri kwa baadae lakini usiitupe elimu, ifanye elimu kuwa sehemu ya maisha yako, ipambanie elimu tena na tena. Jiamini wewe mwenyewe, amini kwenye kila jambo ambalo unalifanya, usiwaogope wanadamu kwa sababu wengi hawana muda na wewe ila watajaribu tu kukutoa kwenye reli na kwenye msingi wa maisha yeko. Siku moja natamani uje unibebe na gari yako hapa hata kama nitakuwa na miaka tisini mwanangu. Nikutakie usiku mwema, wahi ukamuuguze mdogo wako” yalikuwa maneno ya uchungu na nasaha kubwa za maisha kutoka kwa mzee ambaye alikuwa anauza mahindi barabarani kwenye mitaa hiyo ya Mwenge.
Mzee huyo umri wake ulikuwa umeenda lakini kutokana na ugumu wa maisha ambao alikuwa nao, alilazimika kujitafutia ridhiki zake pembezoni mwa barabara ambapo alitegemea kuishi kwa kuuza mahindi ya shilingi miatano miatano. Kijana ambaye alikuwa anaongea naye alikuwa anaitwa Amani, alikuwa ni kijana mpole mwenye akili, hakuwa kijana yule wa mtaani kama walivyo vijana wengine kwa sababu kubwa mbili. Sababu ya kwanza ilikuwa ni kwamba alikuwa akiijua hasara ya kujichanganya na vijana wa mtaani lakini sababu ya pili ni kwamba alikuwa na jukumu zito mbele yake, jukumu la kumtunza mdogo wake ambaye alikuwa na miaka kumi kwa wakati huo.
Alionekana kuwa kijana ambaye alikuwa sehemu ya maisha yale ya umaskini wa kutupwa, alikuwa mwanafunzi wakati huo wa kidato cha nne ambaye alikuwa akijisomesha kwa shida kubwa. Mzee huyo alionekana kumjua vyema kijana huyo na huenda alikuwa anatamani kuweza kumsaidia lakini hali yake haikumpatia hiyo nafasi ambayo yeye alikuwa anaitamani kuwa nayo. Kijana yule yale maneno yalimfanya aondoke pale huku akiwa anatokwa na machozi, ni mengi ambayo yalionekana kujificha kwenye mtima wake ambayo alihitaji iwe siri yake mwenyewe kwani hakukuwa na umuhimu wa dunia kuweza kutambua na hata kama dunia ingetambua basi haikuwa na jambo lolote la kuweza kumsaidia.
Amani, jina lake lilikuwa tofauti kabisa na uhalisia wa maisha yake, kijana huyo ambaye alikuwa anajishughulisha na shughuli ngumu mtaani ili aweze kuishi na kumlisha mdogo wake ambaye pia alikuwa anasoma hakuwa na tafsiri sahihi ya lile jina lake ambalo alipewa akiwa anazaliwa. Maisha yake yalijaa misukosuko ya kutisha kiasi kwamba alikuwa anatamani kukata tamaa ila uwepo wa mdogo wake ndio ambao kila siku ulimfanya aendelee kuiona sababu ya yeye kuwa hai ila vinginevyo basi asingeona umuhimu wa kuishi kwake.
Alifika kwenye kijumba kimoja kidogo, kijumba ambacho kilionekana kuwa cha zamani na maskani ya watu ambao walikuwa na maisha magumu ila yeye ndipo ambapo alikuwa anapaita nyumbani. Alikuwa anamtazama mdogo wake kwa hasira na uchungu, hakuona kama malaika yule alikuwa anastahili kuweza kuishi maisha ya namna ile, aliona kabisa kwamba mdogo wake alistahili kuishi maisha mazuri na yenye furaha kama ilivyo kwa watoto wengine wa kike lakini kwa bahati mbaya alikuwa amepigwa buti na fuko la hela, ufukara ukawa rafiki kwake.
Kijana yule ambaye uso wake ulikuwa unafifia kwa sababu haukuwa na nuru, uso ambao uliongea mengi kwa hisia kali kiasi kwamba mpaka mdogo wake aliweza kumuona kaka yake na kumuonea huruma kwa hali ambayo alikuwa nayo.
“Kaka usijali mimi nitakuwa salama na nakuahidi siku za hivi karibuni nitanyanyuka tena na kuendelea na masomo yangu. Namshukuru Mungu kunipatia ndugu kama wewe, wewe ndiye kaka bora zaidi kuwahi kuwepo hapa duniani, kama kungekuwa na maisha ya mara ya pili huko ambako huwa inaaminika kwamba tunaenda baada ya kifo basi ningekuchagua uwe kaka yangu kwa mara nyingine tena” alimsogelea mdogo wake na kumkumbatia kwa furaha ile ya kulazimisha lakini ambayo ilikuwa na matumaini ndani yake kwa sababu alikuwa anaona ishara ya ushindi kuungwa mkono na mdogo wake.
Ukurasa wa 5 unafika mwisho.
Comments