Reader Settings

Mara baada ya kuona mzee huyo anamvimbishia Prisila kifua, Hamza aliingilia na kuuliza:

“Hili eneo limetolewa na Wizara kwa ajili ya makazi ya watoto. Kwanini mnalazimisha kubomoa usiku wote huu? Vibali vyenu vipo wapi?”

Kiongozi huyo aliishia kumwangalia Hamza kwa kumpandisha na kumshusha, kisha akasema:

“Wewe ni nani? Hili eneo sio la Wizara, ni eneo la ujenzi uliopaswa kuanza muda wowote. Sio mahali pa kulala hapa, tunataka wote muondoke.”

“Nauliza kama mna nyaraka zozote za kuthibitisha hili eneo ni la ujenzi. Haiwezekani mnakurupuka tu na kutaka kuanza kubomoa.”

“Unaongea ujinga, dogo! Wewe ni nani kwanza mpaka nikuonyeshe vibali? Wewe ndio Meya wa hapa?”

Aliongea bwana yule huku akicheka, na wale wafanyakazi aliokuwa nao walicheka pia, wakionekana kutomchukulia Hamza siriasi kabisa.

Hamza aliishia kuangalia sare zao za kazi na kusoma jina la kampuni ya ujenzi wanayotokea. Aliweza kuona neno Taita Real Estate.

Mara baada ya kusoma maandishi hayo, alijikuta akigeuza uso wake na kuangalia majengo ya makazi ya Tatilia Village. Palepale alijua majengo hayo ya Tatilia yanamilikiwa na watu hao hao wa kampuni ya Taita. Haraka alipambanua na kuamini kwamba lazima mradi huo ulikuwa umeweka macho yao kwenye eneo hilo ambalo mwanzoni lilikuwa la kanisa kwa muda mrefu.

Ilikuwa wazi kwamba, kama eneo hilo lingekuwa makazi ya watoto yatima, moja kwa moja thamani ya mradi wao wa majengo ya apartment ingepungua.

Hamza alipogundua hivyo, alipuuza wafanyakazi wale na akapiga hatua kusogelea greda ambalo lilikuwa lishaanza kutifua ukuta.

“Wewe, unafanya nini? Sogea hapo haraka!”

Hamza hakujali makelele yake. Haraka aliruka na kutua juu ya kijiko cha greda lile. Akapiga teke kwenye chuma cha shingo ya kijiko.

“Clanng!”

Kilikuwa kishindo kizito cha vyuma kugongana. Shingo ya greda ilipinda huku greda lote likipinduka, na kufanya isiwezekane kabisa kuendelea na kazi.

Wafanyakazi wote walioshuhudia tukio hilo walipigwa na butwaa. Walidhani walikuwa ndotoni. Yaani, nguzo nzito ya chuma yenye uzito wa tani imeweza kupindishwa kwa mguu tu?!

Hamza hakujali mshangao wao. Aliruka kutoka kwenye eksaveta na kwenda kusimama mbele ya yule bwana kiongozi.

“Kama una nyaraka za uthibitisho, nionyeshe.”

Awamu hiyo, msimamizi alianza kupaniki. Akawaza, kama mtu huyu ameweza kupindisha mikono ya greda kwa mguu, je, akinikanyaga si nitakuwa nyama tu?

“Nyaraka hatuna. Ila boss kasema atakuja nazo, ila sisi tuendelee na kazi,” aliongea bwana yule akiwa na tabasamu la uchungu.

“Kwahiyo ulikuwa ukidanganya? Mnaanza kubomoa eneo hili bila ruhusa kutoka serikalini? Mnachofanya ni kukiuka sheria!” aliongea Prisila kwa hasira.

“Hapana. Bosi wetu kasema tusiwazie kuhusu masuala ya vibali, tuendelee na kazi, na muda wowote vibali vyote kutoka serikalini vitafika.”

“Sijali huyo bosi wako ni nani. Chukua kila kitu chenu na muondoke hapa,” aliongea Hamza akiwa na ukali.

Msimamizi alionekana kuwa na wasiwasi mno na akaongea:

“Bro, acha kufanya mambo kuwa magumu kwetu. Tupo hapa kwa sababu tumeagizwa na bosi. Kama tusipobomoa eneo hili usiku wa leo, tunaweza kukatwa mishahara yetu au kufukuzwa kazi kabisa. Ila wewe unaweza kupoteza hata maisha.”

“Oh, kwahiyo unasema bosi wako ataniua?”

“Ndiyo! Najua una nguvu nyingi, lakini ni bure kama uko peke yako. Labda nikupe fununu kidogo… umesikia habari za kubomolewa nyumba zote za eneo la Chumbe miezi miwili iliyopita? Familia mbili zilizokataa kuhama ili kupisha ujenzi na kusumbua kwa kudai fidia zaidi! Kwa taarifa yako, tukio la nyumba zao kushika moto na wote kupoteza maisha halikuwa ajali ya bahati mbaya.”

“Kweli… inaonekana bosi wako ni mtu mzito sana. Yaani hadi kuunguza familia bila wasiwasi?” aliuliza Hamza akiwa na tabasamu.

“Bosi hajawaunguza! Walisababisha moto wao wenyewe kwa kuweka mitungi ya gesi ndani,” aliongea msimamizi yule akibadilisha kauli.

“Bro, nakushauri sana. Tuacheni tufanye kazi yetu na ondoeni hawa watoto. Sidhani kama kuna faida ukipoteza uhai wako, ilhali kuna maeneo mengi wanaweza kuishi.”

“Kwahiyo unasema kwamba, ingawa unajua moto uliua familia hizo mbili, bosi wako ndiye muhusika, lakini bado unaendelea kumtii na kutaka kubomoa hapa?”

“Kijana, sijasema bosi anahusika. Mimi nakupa ushauri tu kwa nia nzuri.”

“Si umesema mwenyewe kuwa bosi wako ndiye aliyehusika?” aliuliza Hamza.

“Sijasema bosi kahusika. Nimesema ni fununu tu. Hivyo pengine na wewe unaweza kupata ajali.”

“Basi na mimi nakwambia hivi,” alisema Hamza. “Nitahesabu mpaka tatu. Kama mtaendelea kubaki hapa na hamtaki kuondoka, nitahakikisha wote hamuondoki mkiwa na miguu.”

Msimamizi alishangaa. Hakutarajia Hamza awe hana woga licha ya kumpa fununu juu ya uzito wa bosi wake.

“Moja… mbili…”

Sekunde ambayo Hamza alihesabu mpaka tatu, msimamizi ndiye aliyekuwa wa kwanza kukimbia kutoka eneo hilo, na wengine wakamfuata.

Hawakuwa wajinga. Hawakuona haja ya kuvunjwa miguu kwa ajili ya kazi inayowapa ujira mdogo. Vinginevyo baada ya kuwa vilema wangeendeleaje kupata hela?

Muda mfupi tu, eneo hilo lilibakia tulivu baada ya wafanyakazi wote kukimbia. Hawakujali tena kuhusu vifaa vyao.

“Hamza, hawa watu wa kampuni ya Taita wana nini? Kwanini wanataka kuanza ubomoaji bila hata kibali?” aliuliza Prisila huku akikunja sura.

Hamza alifikiria kidogo, kisha akamwambia Prisila asubiri afuatilie. Palepale akatoa simu na kumpigia Dina.

Dina mara baada ya kupokea simu, aliweza kusikia kulikuwa na mazungumzo upande wa pili.

“Hubby, nini tatizo?”

“Dina, uko bize?”

“Nipo kwenye kikao na vijana wa mtandao wetu, wameshatulia,” aliongea.

Hamza palepale alimwelezea Dina kuhusu kinachoendelea na kutaka kujua zaidi kuhusu kampuni ya Tati.

“Oh, boss wa hiyo kampuni ni Mhindi mmoja anaitwa Ratai Hinjuta. Kuna fununu zinasema ni mtoto wa kiongozi mkuu wa Black Trinity, ila hazijathibitishwa. Ila Ratai ana urafiki wa karibu sana na Mkuu wa mkoa na Meya wa Ubungo. Hajawahi kuomba kibali serikalini akakataliwa, labda ni kwa sababu ya hizo fununu.”

“Kwahiyo haya yote ni kwa sababu ya huu umoja wa siri wa Black Trinity?”

Hamza alishawahi kusikia habari nyingi kuhusu umoja huo wa utatu. Ulikuwa umoja wa siri wenye tofauti kubwa sana na mashirika ya siri mengine.

Kwa taarifa alizokuwa nazo, umoja huu ulikuwa ukijiendesha karibu dunia nzima na ndio waliokuwa wakifadhili kwa kiasi kikubwa vikao vya kimataifa vya siri maarufu kama Trilateral Commission Meeting.

Ulikuwa umoja ulijiopenyeza kila kona ya dunia, na kulikuwepo na habari nyingi ambazo hazijawahi kuthibitishwa kwamba umoja huu ni tawi la Freemason.

Kutokana na ushawishi wake kwa mataifa makubwa ya Ulaya, Asia, Amerika na kwingineko, nchi nyingi za Kiafrika zilikuwa na ushirika na umoja huu. Isitoshe, mataifa mengi ya Afrika ndiyo wakopaji wakubwa wa pesa kutoka kwenye mashirika yanayotambulika kwa ajili ya maendeleo. Lakini nyuma ya hayo mashirika, walikuwepo wafadhili kama hao Black Trinity.

Kwa hiyo, nchi nyingi za kiafrika ili kuwa na diplomasia nzuri na mataifa ya nje ili kupata idhini ya mikopo kwenye mashirika ya fedha, hatua ya kwanza ilikuwa  ni kuweka mahusiano mazuri na huu umoja..

Kwa lugha nyepesi, nchi nyingi ni sehemu ya mashirika makubwa ya kitaifa duniani, na mashirika hayo yapo chini ya wafadhili — watu wenye pesa kubwa, mfano familia kama za Rockefeller, Rothchild  na kuendelea.

Kwahiyo nguvu yao ndani ya nchi yoyote ambayo ipo chini ya maendeleo ya mikopo yao ni rahisi kwao kupata vibali vya kufanya biashara bila kuzuiliwa.

Mfano mwepesi zaidi ni pale kampuni ya kimataifa inapokuja nchini kwa ajili ya uwekezaji. Inachagua eneo inalotaka kuwekeza, na kwa nje inaonekana kama ni kampuni moja labda kutoka India. Lakini ukifuatilia msururu wa wamiliki, unakuta ni wanachama wa Black Trinity. Hivyo, hata mradi wowote unapopitishwa na shirika hilo, kampuni huwekwa mbele tu kama kisingizio.

Ushawishi wa Hamza kwenye umoja huo ulikuwa mdogo sana. Isitoshe kwake, ulikuwa kama umoja wa siri wa aina ya Bilderberg Group, ambao aliwahi kupambana nao vikali.

“Ndio maana wana majivuno yote haya… kumbe wanatokea kwenye shirika hili la siri?” aliongea Hamza huku akishika shingo yake, kisha akasema:
“Basi fanya mpango uwasiliane na huyo Ratai. Vyovyote vile, eneo hili limetolewa na serikali kwa ajili ya watoto kukaa. Hatutaondoka hivi hivi tu.”

“Nilidhani unataka nitume watu kwenda kumuua Ratai. Usiniambie siku hizi umezeeka na hasira zako zimepungua,” aliongea Dina.

“Hili sio suala la mimi kupunguza hasira. Ni kwamba sitaki kupoteza nguvu nyingi kudili nao. Sioni kama wana thamani hiyo. Halafu pia Madam Wadeni hakutaka jina la kituo chake kuhusishwa na mambo mengi,” aliongea Hamza.

Mara baada ya kuonana na wataalamu wale wa levo za uhodari na kupata uzoefu juu ya ukubwa wa dunia, Hamza alizidi kupoteza hamu ya kujihusisha na mambo mengi ya kibinadamu. Alichohitaji ni kuona watoto walioachwa na Wadeni wanakua na kufikia mafanikio yao wakiwa na furaha.

Kuhusu huyo bwana anayefahamika kwa jina la Ratai wa kampuni ya Taita, hakuona haja ya kushindana naye. Kadri upana wa mawazo ya mtu ulivyo, ndivyo upana wa uwezo wake wa kuliangalia anga—na ndivyo namna ya kuona yale yasiyoonekana.

“Nimekupata. Nitatumia nguvu ya mtandao wangu wa Chatu ili kutafuta namna ya kuongea naye ana kwa ana. Nitakupa taarifa ya kitakachoendelea,” aliongea Dina.

Kwa ukubwa wa Black Trinity, mtandao wa Chatu ulikuwa mdogo sana. Hata hivyo, hadhi ya Dina katika ulimwengu wa giza ilitosha kabisa kuzingatiwa kama angependa kukutana na bwana huyo. Isitoshe, ushawishi wa mtandao wa Chatu ulikuwa mpana mpaka nje ya mipaka ya Tanzania.

Hamza mara baada ya kukata simu alimwangalia Prisila na kumwambia:
“Dina analishughulikia hili suala. Muda umeenda sana, fanyeni mpango kwanza watoto wapumzike.”

Prisila alitingisha kichwa kuelewa na kisha akawapa maelekezo wamama waliokuwa wakisaidia watoto na kuwaingiza kwenye mabweni kwa ajili ya kupumzika.

Ingawa eneo hilo mwanzoni lilikuwa na mabweni kwa ajili ya watu wazima, mazingira yake yalikuwa rafiki pia kwa watoto.

“Hamza, unarudi nyumbani?” aliuliza Prisila baada ya kusita. Hata hivyo, sauti yake ilikuwa dhaifu.

Hamza alifikiria kwa dakika kadhaa kisha akasema kwa tabasamu la upole:
“Hapana, nitalala leo hapa hapa. Siwezi kuondoka mpaka hili suala lipate muafaka.”

Prisila baada ya kusikia kauli hiyo alijikuta akiwa na furaha. Akamkumbatia Hamza huku akimbusu shavuni.

Hamza alihisi haya usoni. Ingawa Prisila alikuwa msomi na mwenye uzoefu mkubwa, bado jukumu la kusimamia watoto kama hao—hasa baada ya eneo la makazi kuharibika—halikuwa dogo.

Kama ambavyo shule za awali na chekechea hutumia juhudi kubwa kupokea watoto asubuhi mpaka muda wa kuondoka, Prisila alikuwa akiweka juhudi masaa ishirini na nne, wiki nzima, kuhakikisha watoto wako salama na wenye furaha.

“Twende tukaangalie kama watoto wote wamepata pa kulala,” aliongea Hamza akimshika Prisila mkono.

Mara baada ya kukagua mazingira na kuona watoto wote wamepata vitanda na usafi umetunzwa, Hamza hatimaye alitoa simu yake na kumtumia Regina ujumbe kupitia WhatsApp akimueleza kwamba hatorudi nyumbani.

“Prisila, vipi kuhusu baba? Namaanisha Profesa Singano” aliuliza Hamza mara baada ya kutoka kwenye mabweni ya watoto. Ukweli ni kwamba alitarajia kumuona Profesa Singano akihudhuria msiba wa Mzee Hizza, maana walikuwa ndugu.

“Baba kwa sasa yupo nchini Peru. Nimewasiliana naye kuhusu msiba na amesikitika sana kwa kile kilichotokea. Hata hivyo, kutokana na majukumu imekuwa ngumu kwake kusafiri kurudi. Nimeongea naye na amekutaja pia na anakukumbuka. Lakini kubwa zaidi, amesema kuna mzigo baba mdogo atakupatia.”

“Baba mdogo?”

“Ndiyo. Mdogo wake anayemfuatia anaitwa Peter. Kwa sasa ni raia wa Canada,” aliongea Prisila, na kumfanya Hamza kushangaa kidogo na kujiuliza ni mzigo gani huo.

Ukweli ni kwamba, licha ya kumjua Profesa Singano, Hamza alikuwa akimfahamu kwa uchache sana. Alitamani kumjua zaidi, kwani kwa uzoefu wake alimwona Profesa kama mtu mwenye hekima na uzoefu mkubwa.

Hata hivyo, muda huo huo simu yake ilianza kuita. Mara baada ya kuona ni Dina, alipokea mara moja.

“Dina, vipi? Kimekuwaje?”

Upande wa pili, sauti ya Dina ilionekana kutokuwa na utulivu.

“Hubby… huyu Ratai amekataa kabisa kunipa uzito wowote…”

“Oh!” Hamza alionekana kushangaa kidogo. Hata hivyo, mwonekano wake uliendelea kubaki wa kawaida na akauliza:

 “Amesameje baada ya kuonana nae”

“Ratai kasema tuwe mtandao wa Chatu au wa Panya. Sisi ni kajikundi kadogo tu ambako hatuna hadhi ya kufanya maongezi nae. Kasema kwamba eneo hilo la kanisa lazima libomolewe usiku huu na kisha kujengwa shule ya watoto wa matajiri… na mtu yoyote atakaemzuia ata…”

“Atafanya nini…?” aliuliza Hamza akiwa na tabasamu.

“Anamaanisha kwamba ataua yoyote ambaye atamwingilia katika mpango wake,” aliongea Dina.

Hamza alionekana kuinamisha kichwa chake huku akiangalia pakiti ya sigara aliyoshikilia. Palepale alijikuta akibana simu kwa bega na kuchomoa moja, kisha kuiwasha na kuvuta moshi.

“Dina, huyo jamaa anaonekana kuwa na kiburi mno na maringo. kwanini usingeenda na watu ukamshikisha adabu?”

“Nilitaka kufanya hivyo, ila kwa sababu mpango wangu wa mwanzo ulikuwa kuongea nae kiuungwana na kufikia makubaliano, ndio maana nikaona nionane nae mwenyewe. Ila hata hivyo, kwa sababu ana ujeuri wa kuongea maneno haya mbele yangu licha ya kujua nguvu yetu sio ndogo, lazima kuna nguvu nyuma yake inayomfanya aamini hatuwezi kufanya chochote,” aliongea Dina.

Hamza aliishia kukubaliana nae na kisha akaongea:
“Basi wewe rudi tu nyumbani kwanza. Ngoja nifanye utafiti wa kujua mtandao wote wa Black Trinity hapa nchini na kuona kama kuna kitu cha upekee.”

Aliongea Hamza, kisha alikata simu na kumpigia Regina.

Regina, upande wake, hakuwa amepumzika bado. Mara baada ya Hamza kumwambia alitaka kujua kwa undani kuhusu umoja wa siri wa Utatu Mweusi, haraka sana alituma ombi hilo moja kwa moja kwenye kitengo cha Binamu.

Utatu Mweusi sio umoja mdogo kabisa, hivyo Binamu walikuwa tayari na taarifa zao. Hata hivyo, kwa taarifa ambazo Regina alipata kutoka Binamu, umoja huo kwa upande wa Afrika haukuwa na nguvu kubwa sana. Ulitegemea zaidi kufundisha wanajeshi mafunzo ya nishati, kuingia ushirika na wanajeshi wa nchi, pamoja na kukodi masenari.

Kwa lugha nyepesi, nguvu yao ya kujilinda ilikuwa kwenye kutegemea walinzi na wanajeshi wa kawaida walioko vitengoni ili kupata intelijensia za mapema na kujilinda.

Hamza, mara baada ya kusikia taarifa hiyo, alijikuta akishangaa kidogo na kujiuliza: Inamaana huyo Ratai ni mjinga kiasi hicho?

Ni muda huo huo, Hamza aliweza kusikia sauti za vishindo vya viatu zikitokea upande wa geti la kuingilia eneo hilo. Aliishia kukunja sura na kisha kupiga hatua kuelekea huko.

Mara baada ya kufika eneo la uwanja karibu na mahema ya kusalia, aliweza kuona gari aina ya Bentley nyeusi ikiingia eneo hilo huku kushoto na kulia ikiwa imezingirwa na mabodigadi waliokuwa wamevalia nguo nyeusi.

Walinzi hao walikuwa wazungu pamoja na weusi, kwa ufupi walikuwa mchanganyiko na wote walikuwa wamejazia miili. Hamza, mara baada ya kukagua mabodigadi hao, palepale aliweza kuhisi msisimko wao ulikuwa sio wa kawaida na alielewa moja kwa moja lazima watakuwa wameajiriwa kutoka kwenye taasisi za kimasenari zenye nguvu, ambazo hutumia mbinu mbalimbali kuwafanya kuwa na uwezo usio wa kawaida.

Kubwa zaidi ni kwamba mabodigadi hao wote viunoni mwao walikuwa na bastola. Kutokana na sheria za nchi, ni mara chache sana kuona walinzi wakitembea na silaha waziwazi namna hiyo. Hata kama wewe ni tajiri, bado mabodigadi wengi hawakupewa silaha za moto bila ridhaa ya serikali.

Mara baada ya gari ile kusimama, bodigadi aliyeonekana kuwa kiongozi wa wenzake alisogea na kufungua mlango wa nyuma wa gari hilo.

Palepale alionekana mwanaume wa Kihindi alievalia shati refu kama koti la kufika magotini la rangi ya light blue, huku eneo la kiunoni akiwa amefunga mkanda wa Hermes. Chini alivalia suruali nyeusi na viatu vilivyong’arishwa vyema. Ni staili flani ya mavazi aina ya tabard, lakini yenye muundo wa kisasa zaidi.

Bwana huyo alikuwa na nywele flani zilizojikunja kichwani na alikuwa ameshikilia kitambaa cha hariri, akionekana kufuta kioo cha miwani. Kulikuwa na hali flani ya maringo, kama vile ni mfalme wa miliki kubwa.

“Nimesikia hapa kuna mtu kutoka mtandao wa Chatu anataka kutuzuia kubomoa hili eneo. Kwa ninavyoona hapa, nadhani utakuwa wewe bwana mdogo,” aliongea yule Mhindi huku akimwangalia Hamza.

Hamza aliishia kumwangalia bwana huyo aliyejaa maringo, kisha akauliza akiwa na tabasamu:
“Wewe ndio Ratai?”

Yule bwana, mara baada ya kuulizwa swali hilo, macho yake yalijaa ukali na kisha akasema:
“Unajiona nani mpaka kuniita kwa jina langu moja?”

ITAENDELEA

Previoua Next