Sehemu ya 02
Maisha Dar es Salaam hayakuwa rahisi wala mepesi kama nilivyodhani. Nilipoondoka kijijini, nilijua kwamba mjini ni sehemu ya neema, sehemu ambayo kila mtu akifika anapata ajira, fedha, na maisha mazuri. Lakini ukweli ulionekana haraka sana. Hata kupata mlo mmoja tu ilikuwa ni changamoto kubwa.
Siku za mwanzo, nilijikuta nikihangaika kuzunguka mitaa ya Mbezi Mwisho, nikitafuta kazi za vibarua. Nilijiunga na kundi la vijana waliokuwa wakisimama kwenye barabara kubwa kila alfajiri, tukisubiri magari makubwa au wakandarasi wa ujenzi waje kutuchukua. Wakati mwingine tulipata kazi ya kubeba tofali, saruji, au mchanga, na tukilipwa elfu tano au saba kwa siku. Lakini pia kulikuwa na siku nyingi ambazo tulikaa kuanzia asubuhi hadi jioni bila mtu yeyote kutuita.
Nilipochoka kusubiri, nilianza kuzunguka kwenye maduka na migahawa, nikiuliza kama kulikuwa na nafasi za kufagia au kuosha vyombo. Lakini mara nyingi nilipokutana na macho ya wamiliki, walinikazia macho na kusema:
"Hatuna kazi, kijana. Rudi wiki ijayo."
Wiki zikapita, lakini majibu yakawa yale yale.
Kwa siku ambazo nilibahatika kupata kazi ya kubeba mizigo sokoni, nilikuwa napata hela ya kula mlo mmoja tu – mara nyingi wali na maharage au ugali na mboga za majani. Lakini kulikuwa na siku ambazo nilirudi chumbani nikiwa sina kitu tumboni. Nililala nikiwa nimejikunyata, nikisikia sauti za tumbo langu likilia, nikijifariji kwamba kesho pengine itanibeba.
Chumba nilichokodishiwa na Shafii kilikuwa cha kuta za matope zilizojaa nyufa, na dari lake lilivuja mvua iliponyesha. Hakukuwa na umeme, na nilipokuwa napenda kusoma au kuandika mawazo yangu, nililazimika kutumia mshumaa mdogo uliokuwa ukimalizika haraka. Nilipozima mshumaa huo usiku, giza lilikuwa nzito kiasi kwamba nilihisi kama dunia imezima kabisa.
Nilianza kugundua kuwa mjini hapendwi mtu. Kila mmoja alishughulika na maisha yake, na kama hukujua namna ya kusimama imara, ungeishia kusahaulika kwenye kelele za magari na harufu ya vumbi. Niliona vijana wengi waliokuja kutoka mikoani wakikata tamaa, wengine wakijiingiza kwenye makundi ya kihalifu, na wengine wakibadilika kuwa walevi ili kusahau shida zao.
Lakini mimi nilijipa moyo. Nilijua nilikuja mjini kwa ndoto kubwa. Nilijikumbusha kila siku maneno ya baba: "Usidanganyike na starehe, kumbuka kazi ndiyo inamjenga mtu." Ndipo nikaanza kuwa na nidhamu. Nilijiwekea utaratibu wa kuamka mapema, kufanya mazoezi kama nilivyozoea kijijini, kisha kuanza kutafuta kazi kwa miguu yangu.
Haikuwa rahisi. Nilihisi upweke. Nilimkumbuka sana mama yangu na uso wake wa upendo. Nilimkumbuka babu yangu na hekima zake. Mara nyingi nilipoona hali inakuwa ngumu, nilikaa chini na kuandika kwenye daftari langu dogo. Nilijifariji kuwa siku moja nitakuja kusoma maandishi yangu na kuona safari yangu imekuwa na maana.
Lakini siku moja, bahati ilianza kunisogelea taratibu. Nilipokuwa naelekea sokoni, nilikutana na mtu ambaye aligeuza kabisa mwelekeo wa maisha yangu jijin
Comments