Reader Settings

DYLAN

Story by Elton Tonny

Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

(R-rated 18+)

Enjoy!


★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA PILI

★★★★★★★★★★★


Dylan akaanza kutembea kutokea mlangoni pale kama mwanamitindo. Alipendeza sana kwa kuvalia suti nyeusi iliyoubana mwili wake kiasi, ikiwa imefungwa kifungo kimoja tu kwenye koti. Kiatu chake cheusi kiling'aa, na kwa ndani alivalia shati jeusi pia aliloachia vifungo viwili kwa juu. Mkononi alivaa saa nzito ya rangi ya dhahabu iliyokuwa ya gharama, na nywele zake kichwani zilitengenezwa kwa utundu kiasi; pembe za kichwa zilikuwa zimenyolewa na kuacha nywele kidogo, huku kwa juu akiwa na rasi alizobana kwa nyuma na chache zikidondokea mbele ya uso wake pembeni ya jicho. Sikio moja alivaa hereni ndogo iliyolibana vyema, na mdomoni alitafuna jojo. 

Viongozi wengi pale walimshangaa kwa kuwa hawakumjua, naye akatembea kufikia kiti cha mbele cha baba yake na kusimama hapo. Gilbert akasimama na kutazamana naye machoni, naye Dylan akatikisa kichwa mara moja kumwonyesha kuwa walikuwa kitu kimoja sasa. Gilbert akafurahi sana moyoni baada ya kutambua mwanaye aliyatilia maanani maneno yake.

"Wewe ni nani?" Mr. Bernard akamuuliza.

"Board members, I would like to introduce to you this very important person in the room, and my only son, Dylan Gilbert," Jaquelin akamtambulisha mwanaye kwa kujivunia.

Wengi walionekana kushangaa kwa kuwa hawakutegemea angekuja hapo. Wengi wao walifahamu kuwa Gilbert na Jaquelin walikuwa na mwana, lakini hawakuwahi kumwona kabla; zaidi walisikia tu habari zake zamani za jinsi alivyokuwa mwerevu sana.

"Ana cheo gani hapa?" Mr. Bernard akauliza.

"Kila kitu unachokiona kwenye hii kampuni ni chake," Gilbert akajibu kwa uthabiti.

Dylan akacheka kijeuri kama kawaida yake. 

Mama yake alimwangalia kwa matumaini mengi sana, akijua bila shaka mwanaye angeleta mambo mapya kwenye meza kuu.

"Kwa hiyo kijana wako ndiye atakaye..toa suluhisho la tatizo hili?" akauliza mshiriki fulani mzee kiasi.

"Ikiwa tu mtanisikiliza kwa makini," Dylan akasema.

Wote wakaweka utulivu kusikiliza alichotaka kuwapa kijana wa Gilbert. Gilbert mwenyewe akaketi kwenye kiti na kumwangalia mwanaye kwa umakini, akimruhusu aendelee kutoa mawazo yake.

"Kama ilivyo kawaida, matatizo yakianza kwenye kampuni, wengi hukimbilia lawama na kuanza kuingiza siasa," Dylan akasema.

"Siyo lawama kijana. Tunatafuta sul...."

"Naitwa Dylan. Usirudie tena kuniita kijana," akamkatisha mzee huyo kwa uthabiti sana.

Wote wakashangaa. 

Jaquelin akatabasamu kikejeli akiangalia chini.

"Tatizo siyo suluhisho tu. Ni kile ambacho nyie MMEKAZIA fikra. Mnaangalia zaidi tatizo badala ya njia za kulitatua," akasema Dylan.

"Unazungumzia tatizo gani Dylan?" akauliza Gilbert.

"Mawili. Kwanza, generation ya wafanyakazi wenye ustadi zaidi inazidi kukua kiumri. Mkiangalia, karibia wote walio na experience nyingi kwenye masuala haya ni wakubwa sana kiumri... soon wata-retire. Hiyo inamaanisha ni muhimu kutafuta mapema vijana wenye uzoefu wa kazi kwa kuwa project nyingi za masuala ya construction zinazidi kuwa ngumu... na demand ni kubwa," akaeleza.

"Kwa hiyo point yako inaelekea wapi Mr. Dylan?" akauliza Mr. Bernard.

"Wazo la president kuhusiana na ku-implement teknolojia kubwa hapa, ni sahihi kabisa," akajibu Dylan.

Wengi wakaanza kuangaliana kwa mashaka. Hata Jaquelin alishangaa kiasi kwamba Dylan aliunga mkono jambo hilo. Gilbert akaendelea kumkazia fikira mwanaye.

"Now, now... najua wengi mnaona kwamba sekta ya ujenzi haihitaji teknolojia kwa sababu kazi zinafanywa in physical environments, lakini kuingiza technology kuna faida nyingi za pembeni kwenye sekta hii. Faida hizo ni kama... kufanya kazi kwenye mazingira salama zaidi, more efficient use of materials, improved health and safety, na recruitment process zenye ubora zaidi," Dylan akaeleza.

"Shida nyingine ni nini?" akauliza yule mzee.

"Mnahitaji kuacha ubaguzi. Mfanye kuajiri wanawake pia kwenye sekta hii, msijidanganye kwamba inawahusu 'macho-men' peke yao," Dylan akasema.

"Asa' wanawake watafanya nini? Sanasana labda kujiremba wakati wa kazi," akasema Mr. Bernard kwa dharau.

"Kumbuka kelele za chura hazimzuii tembo kunywa maji, Mr. Bernard," akasema Dylan kikejeli.

Gilbert, Jaquelin, pamoja na wengine baadhi wakacheka kidogo.

Dylan akasema, "Maoni ya namna hiyo yamepitwa na wakati. Kuna opportunity nyingi sana kwenye viwanda vya ujenzi mbali na kubeba matofali na zege tu, kuanzia kwenye mambo ya construction software mpaka design; na hata architecture. Siyo lazima walioajiriwa kufanya kazi wafanye kwenye maeneo ya ujenzi tu ili kuhusika. Hivi mnafikiri wenzetu kule wanazifanya vipi nchi zao mpaka zinakua kimaendeleo namna ile?"

Wote wakabaki kimya.

"Hii kama kampuni yenye usawa, inahitaji kuondoa wazo la kwamba 'ujenzi na ukandarasi ni kwa ajili ya wanaume tu.' Tafuta sehemu zote, utakuta wengi waliosomea masuala haya ni wanawake, na wana ujuzi mwingi sana kuweza kusaidia kuleta maendeleo. Lakini wanapuuzwa na kuishia kufanya kazi ndogo ndogo kujikimu kimaisha wakati wangekuwa sehemu kama hii. Msilazimishe watu wale wale tu, mtasababisha kampuni iwe ya ubabaishaji," akaeleza.

"Ndiyo. Ni kweli kabisa," Gilbert akapigia mstari.

"Yeah. Technology has opened a new world of possibilities for everyone. But HOW we unleash this potential is what will set us apart and help us deliver what's required in order to get what we expect to gain. Trust me, implementation hii ikifanywa haraka, ndani ya wiki tatu tu mtaona matokeo mazuri," akamalizia Dylan.

Wengi wakaonyesha kuafikiana na mawazo yake. Hivi ni vitu ambavyo kama wangeanza kufanya zamani, basi wangekuwa hawakabiliani na matatizo waliyopitia sasa. Lakini kwa sababu ya ubinafsi wa watu kadhaa, mambo sikuzote huwa yanaanguka vibaya, na Dylan alilijua hilo. Kwa hiyo akawa ameamua kuwasaidia waache ushamba na kuwekeza kwenye teknolojia kuweza kuokoa mipango ya kampuni.

Baada ya mkutano huo kuisha, wengi walizungumza na Dylan wakitaka kujua mawazo yake. Ijapokuwa wengi walivutiwa na werevu wake, baadhi walikasirishwa naye kwa kuwa aliongea vitu vya kweli. Mwishowe, Dylan akaongozwa na mama yake mpaka kwenye ofisi ambayo yeye angetumia hapo kwenye kampuni, ambayo alikuwa amemtunzia kwa muda mrefu sana.

Jaquelin alimpongeza sana kwa alichokifanya, na akasema alifurahishwa hata zaidi na jinsi alivyowapausha wenye viherehere mule ndani. Alipomuuliza jana alikwenda wapi, Dylan akasema tu alikuwa na mizunguko yake, kisingizio ambacho kilikuwa cha kawaida sana kwake kutumia. Akamwambia mama yake angependa kuifanyia ofisi yake marekebisho ya vitu kadhaa, naye akamruhusu.

Gilbert alifika pia na kumpongeza mwanaye kwa msaada wake. Ijapokuwa alikuwa na ofisi hapa kwenye kampuni sasa, Dylan aliweka wazi kuwa wasitarajie atakuwa mtu wa kukaa tu ofisini akifanya makazi mengi kuanzia asubuhi mpaka jioni, maana alikuwa na mambo yake mengine. Gilbert hakuwa na neno kwa kuwa sasa alijua Dylan yuko pamoja naye, lakini Jaquelin akawa anamsisitizia kuwa ni lazima awe anakaa ofisini ili kushughulikia mambo hapo; kitu ambacho kwa Dylan hakikuwa muhimu sana.

Wazazi wake wakatoka na kumwacha akiwa mwenyewe ofisini anapitia mambo kadha wa kadha.


★★★


Ilipita wiki moja baada ya matukio hayo kwenye kampuni ya Gilbert. Mambo sasa yalikuwa yameanza kwenda vizuri zaidi kwa kuwa walifuata ushauri wa Dylan, na ni wiki moja tu tayari matokeo yakaanza kujionyesha kuwa mazuri.

Ikawa ni Jumamosi jioni ya saa 11 sasa. Gilbert, Jaquelin, pamoja na Dylan wote walikuwa nyumbani. Siku hii, kulikuwa na rafiki yake Jaquelin ambaye aliahidi kuwatembelea. Hawakuonana kwa kitambo kirefu sasa, kwa kuwa rafiki huyo alikuwa akiishi sehemu nyingine ya mbali kwenye jiji hilo.

Gilbert alikuwa sebuleni akipitia masuala fulani ya kazi kwenye iPad, huku Jaquelin akisaidiana na wasaidizi wa kazi kutengeneza chakula kitamu kwa ajili ya wageni. Dylan alikuwa upande wa nyuma wa nyumba ambao ulikuwa mpana sana na uliojengewa vitu vingi kwa ajili ya kuupendezesha. Alikuwa akifanya mazoezi ya mwili, akichanganya mikao tofauti na mitindo ya mazoezi hayo. Alipenda sana kufanya hivi nyakati za jioni, na ilimburudisha na kumfanya ahisi uchangamfu pia.

Baada ya dakika kadhaa, sauti ya 'horn' ya gari ilisikika kutoka nje ya geti la uzio kubwa la nyumba, naye mlinzi wa pale akafungua geti kuruhusu gari ipite ndani. Tayari Jaquelin alikuwa amesimama katikati hapo huku anatabasamu kwa furaha sana. Gari lilipoegeshwa, wakashuka wanawake wawili, kisha aliyekuwa akiendesha akamkimbilia Jaquelin kwa furaha na kukumbatiana naye.

"Wow jamani! Heh... shoga! Za siku?" akauliza rafiki yake.

"Nzuri jamani mpenzi. Nimeku-miss sana Beatrice," akasema Jaquelin.

"Heh... jamani yaani unazidi kupendeza tu. Gilbert kweli anakutunza. Sijui ulimpiga limbwata gani vile!"

"Hahaaa... hapa ndo' Kigoma mwisho wa reli, habanduki," akasema Jaquelin huku anapiga kalio lake, na wote wakacheka.

"Shikamoo aunt Jacky?" akasema mwanamke yule mwingine nyuma yao.

Jaquelin akasema, "Marahaba. Em' ngoja kwanza... huyu ni..." 

Beatrice akatikisa kichwa kukubali.

"Haa! Jamani... Harleen umekua!" akasema Jaquelin huku anapanua mikono yake.

Mwanamke huyu, Harleen, akamfata akiwa anatabasamu na kumkumbatia. Alikuwa ni mtoto wa kwanza wa Beatrice. Mara ya mwisho Jaquelin amemwona alikuwa na miaka 14 tu, na sasa akawa anashangaa jinsi alivyobadilika na kuwa mwanamke mkubwa mwenye kuvutia sana.

Harleen alivalia gauni ndefu ya njano kufikia miguuni, iliyoubana mwili wake vyema na kufanya hips zake nene kiasi pembeni na kalio lake litokeze vizuri kwa nyuma. Kichwani, alitengeneza nywele zake kwa kuzisuka kwa rasta ndefu juu ya kichwa, pembe za kichwa chake zilikuwa na nywele fupi na laini, hivyo ilionekana ni kama kiduku fulani hivi. Alikuwa mrembo pia, mwenye mashavu makubwa kidogo na macho mazuri sana.

Beatrice alikuwa amesuka nywele laini za kulala na alivalia kigauni kifupi kufikia magotini; alipenda sana kujiachia kwa kuwa wote walipenda maisha ya kizungu kutokana na kuwa na pesa nyingi.

Jaquelin akawakaribisha wote ndani na kuingia nao mpaka sebuleni. Baada ya Gilbert kuwaona, akatabasamu na kufunga iPad yake, kisha akawafata waliposimama. Akatazamana na Beatrice kwa sekunde kadhaa, kisha wakakumbatiana kwa kuwa ilikuwa ni miaka kadhaa imepita bila kuonana na rafiki yao huyo. Akatambulishwa kwa Harleen, ambaye pia alimshangaa kwa jinsi alivyokua mkubwa. Wakaketi pamoja kwenye masofa ya kisasa hapo ndani na kuanza kuongea.

"... hahahah... yaani ulivyokunyugwa hiyo siku sitasahau!" Beatrice akawa anakumbushia maisha ya shule, akiwa anamwambia Gilbert.

"Aah... kitambo sana. Enzi hizo tulikuwa tunavaa maboksi nyuma ya kaptura mwalimu akianza kutembeza mboko zitupunguzie maumivu," akasema Gilbert, na wote wakacheka.

"Siku hizi wanafunzi wanaweka nini?" akauliza Jaquelin.

"Bado wanatumia maboksi, ila walimu ni wajanja sana. Wakiona nyuma panadunda wanahamishia kwenye supu," akasema Beatrice.

"Kwa shule ambazo fimbo haziruhusiwi ndiyo unakuta mwanafunzi akileta fujo, mwalimu hana jinsi ila kubaki anang'ata kucha tu," akasema Gilbert kiutani.

"Hahahah... kwa hiyo madam principal hauachani na chuo?" Jaquelin akamuuliza Beatrice.

"Hapana, bado sana. Napenda kufundisha. Ndiyo maisha yangu yaani," akajibu.

"Toka ulivyowekwa kuwa principal naona ni ming'aro tu," Jaquelin akasema kiutani.

"Ahahaaa... ming'aro mbona tokea kitambo? Tena kwa kuwa me ndiyo mkuu, ni kunyoosha miguu tu," akasema Beatrice.

"Wacha we!" akasema Jaquelin, na wote wakacheka.

"Umemaliza kusoma?" Gilbert akamuuliza Harleen.

"Ndiyo. Ninafanya kazi sasa," mrembo akajibu.

"Wapi?" akauliza Jaquelin.

"Hospitali kuu. Yeye ni daktari sasa hivi," akajibu Beatrice.

"Wewe! Acha basi!" Jaquelin akashangaa.

Harleen akatabasamu kwa furaha.

"Hongera sana. Umesheheni kwenye mambo yapi?" akauliza Gilbert.

"Mambo mengi. Nafanya upasuaji, ninadili na watu wenye matatizo mbalimbali yanayohusiana na organ muhimu mwilini; hata moyo pia," akaeleza.

"Haaa... Beatrice umekuza," Jaquelin akasifu.

"Ndiyo maana yake," akajibu Beatrice kwa kujivuna.

"Hongera sana. Wakati uko mdogo nakumbuka ulikuwa unalia-lia kweli," Gilbert akakumbusha.

Wote wakacheka.

"Lakini umekua binti mkubwa na mzuri sana. Me nikafikiria labda unafanya modelling," Gilbert akamwambia.

"Yaani kama angeenda huko, hakuna mtu angemfikia," Beatrice akamsifu binti yake.

Harleen akacheka kidogo, kisha akamwambia Gilbert, "Asante."

Jaquelin, alimwangalia sana Gilbert kwa jinsi alivyomtazama Harleen kwa upendezi. Kichwani kwake akawa anafikiri mume wake tayari amevutiwa na dada huyo mrembo sana na mwenye umbo lenye kuvutia, hivyo akaanza kuingiwa na hisi za wivu kumwelekea Harleen bila sababu yoyote.

"Nani yule?" akauliza Beatrice.

Alikuwa amemwona Dylan kupitia mlango wa kioo mbele zaidi ya sehemu waliyoketi, akiwa anakimbia-kimbia na hivyo kuvuta uangalifu wake.

"Ni Dylan," akajibu Jaquelin huku anatabasamu.

"Ni Dylan?! Wewee... amerudi lini?" akauliza Beatrice.

"Ana muda sasa. Kwani sikukwambia?" Jaquelin akauliza.

"Hamna hukuniambia."

"Mmmm... nilikwambia bwana."

"Hujaniambia nawe. Nisingeshangaa kama ningekuwa najua."

"Mh... basi. Amerudi. Ana... kama miezi minne mitano hivi."

"Hee! Twende tukamwone, sijui atatukumbuka?" akasema Beatrice, akimwambia Harleen hivyo.

Wanawake wote watatu wakanyanyuka na kuelekea kwenye mlango wa kioo ambao ulikuwa njia ya kupita kufikia uwanja ule mpana nyuma ya nyumba. Wakafika na kusimama nje hapo, wakimtazama Dylan ambaye alikuwa bize akifanya zoezi fulani wakati huu. Wote walipendezwa sana na jinsi alivyoonyesha wepesi katika kile alichokifanya.

Sasa mwanaume huyu kijana alikuwa ameweka mikono chini, kisha ananyanyua miguu yake juu taratibu, akijibeba namna hiyo mpaka inaponyooka kuelekea juu hewani, kisha anaisambaza hewani hapo akisimama kwa mikono. Alifanya hivyo kwa utulivu mkubwa sana na kuendelea kukaa namna hiyo hiyo kwa dakika kadhaa.

"Ndo' anafanya nini?" akauliza Beatrice.

"Mwenzangu hata najua! Mhm... toka aliporudi ana hiyo kawaida ya kufanya mazoezi... mengine ambayo hata sijawahi kuona," akajibu Jaquelin.

"Amekuwa mkubwa jamani!" akasema Beatrice.

Ni hapa ndipo Dylan aliirudisha miguu yake chini na kusimama wima.

"Dylan..." Jaquelin akamwita.

Jamaa akageuka nyuma na kupata kuwaona wanawake hao wamesimama pale wakimwangalia. Akaonyesha uso wenye udadisi na kuanza kuwaelekea waliposimama, huku akiwa kifua wazi na chini akivaa suruali na viatu vya mazoezi.

"Cheki kifua hicho Harleen!" Beatrice akamtania binti yake.

"Ahahahah... yaani wewe!" Jaquelin akasema.

Harleen akatabasamu na kukaa kimya tu, akimtazama jamaa alivyoendelea kuwakaribia huku anadunda.

"Unasema me nimekuza, ila nawe umekuza kwa kweli. Hadi natamani kuwa mdogo tena. Nisingemwacha mwanao salama," Beatrice akasema kiutani.

"Kwenda huko! Dylan wangu katulia, hapaparikagi na hivyo vitu," akajivuna Jaquelin.

Dylan akawa amewafikia akiwa anatabasamu. "Aunty Beatrice!" akasema kwa shauku.

"Jamani... Dylan wangu mie!" akasema Beatrice kwa furaha.

"Dah! Ningekukumbatia sema nanuka mijasho!" akasema Dylan.

Wote wakacheka.

"Yaani unazidi kupendeza tu!" Dylan akamsifia Beatrice.

"Ndiyo kawaida yangu hiyo mwanangu. Na wewe umekuwa mbaba sasa. Eeeh... naona una rasi kichwani kama mbrazili kweli," Beatrice akamsifia pia.

Dylan akajipiga-piga kidevu chake kwa kiganja kuonyesha anajivuna, na wote wakacheka.

Harleen alikuwa anamtazama Dylan kwa uvutio mwingi sana. Alipendezwa na uso wake mzuri ambao kwa asilimia kubwa ulichangiwa na uzuri wa mama yake, Jaquelin. Alimtazama kifuani na kuona jinsi kilivyojikata vizuri na kutunisha matiti yake kiume zaidi, moja la upande wa kushoto likiwa na tattoo ya kichwa cha simba anayeunguruma, huku tumboni pakikazika haswa na kuonyesha 'six pack' zake vizuri. Mikono ya Dylan ilikuwa imejaa vizuri kuonyesha alikuwa mtu wa mazoezi sana.

Ni wakati huu ndipo Dylan akawa amemwangalia Harleen baada ya kumwona akiwa amesimama pembeni hapo. Akaanza kumfata huku amenyoosha kidole chake kumwelekea, na usoni akionyesha kudadisi Harleen alikuwa nani. Harleen akawa anatabasamu tu.

"Wewe... binti-mashavu! Ni wewe kweli?" akasema Dylan kwa kushangaa.

Wanawake wote wakacheka.

"Haujasahau kumtania hivyo?" Jaquelin akamuuliza.

"Nisahau vipi? Huyu ni binti-mashavu kweli?" akauliza tena Dylan.

"Ahahahah... ndiyo ni mimi, bichwa wewe!" Harleen akatania pia.

"Ahahahah... eeh! Haki ya Mungu! Umekua... ume... umenona!" Dylan akamsifia.

"Heee! Wewe! Usianze mambo yako!" Beatrice akasema kiutani.

"Ahahahah... lazima mtoto asifiwe bwana. Utam-lock mpaka lini?" Dylan akamwambia Beatrice.

"Hakuna. Yaani badala unisifie mimi..."

"Hahaaa... hauna lolote. Kama kikongwe kikongwe tu," Jaquelin akamtania Beatrice.

"Ahahahah... za huko lakini kijana wangu?" Beatrice akamuuliza Dylan.

"Ah... nzuri tu. Mama, mbona hukuniambia kama ni aunty Beatrice na binti-mashavu ndiyo wanakuja?"

"Iih jamani, yaani hukumwambia?" Beatrice akamuuliza Jaquelin.

"Lakini Dylan..." Jaquelin akasema.

"Hakuniambia, aunty. Ningekuwa najua msingenikuta hivi. Yaani mama hujafanya fresh kabisa," Dylan akasema akijifanya kuudhika.

"Lione kwanza! Em' toka hapa nenda kaoge," Jaquelin akasema.

Dylan akawa anacheka kimasihara, nao wote wakatambua alikuwa anatania tu. Kisha akawaacha ili aende kujisafisha haraka na kurudi waweze kutumia muda pamoja kwa urafiki.

Wakati wakiwa wadogo, Dylan na Harleen walicheza pamoja, walisoma shule moja, na kuwa pamoja pindi nyingi ambazo wazazi wao walitembeleana. Jaquelin, Gilbert na Beatrice walikuwa marafiki kabla hata watoto hawajazaliwa, na walisaidiana kwa mambo mengi mno katika safari ya maisha yao. Ilikuwa ni kama Jaquelin na Beatrice ni dada wa damu maana walijuana vizuri na kusaidiana sana kwa mambo mengi kihisia. Baba yake Harleen alikufa wakati binti huyo alipokuwa na miaka 19, kwa kupigwa risasi vibaya na mtu fulani ambaye utambulisho wake haukujulikana mpaka leo. Hiyo ikamwacha Beatrice akiwa mjane mwenye watoto wawili; Harleen na mdogo wake wa kiume aliyeitwa David.

Kufikia wakati ambao Dylan alikuwa amemaliza kuoga na kuvaa, huko chini wadada wa kazi na Jaquelin walikuwa wanaandaa meza ya chakula huku Beatrice na Harleen wakiwa wameketi na Gilbert wakipata maongezi. Walikuwa sanasana wanaongelea kuhusu ujio wa Dylan kwenye kampuni ya Gilbert, nao walipendezwa kutambua kwamba kijana huyu alikuwa na werevu ule ule aliokuwa nao tokea udogoni.

Jaquelin akawaita na kuwaambia wakanawe kwenye sinki safi ili waende mezani kwa ajili ya kupata msosi. Kwa kuwa Beatrice alizoeana nao sana, ilikuwa rahisi kwake kujiachia mno hapo, lakini Harleen alikuwa mwenye utulivu zaidi. Hakuwa na mzuka sana kama mama yake ambaye alipenda kufanya mambo kwa uzungu mwingi wa uswahilini.

Baada ya wote kuwa wameketi, Jaquelin akawaambia wajisikie huru kuchukua chakula chochote hapo kwa upendo wao, hakukuwa na masuala ya kupakuliana. Meza hii ilikuwa ya duara yenye kioo kizito, ambayo ilikuwa pana yenye kuzungukwa na viti vitano vikubwa vyenye kwisheni (cushion) nene za manyoya kwa ajili ya kutuliza mwili. Katikati ya meza, kulikuwa na kioo cha duara kwa juu kilichotoshea kuwekea vyakula vingi, nacho kilizunguka ili mlaji aweze kuchukua chakula alichohitaji kwa wakati wake.

Wakati wanajiandaa kuanza kuzungusha kuchagua chakula, Dylan akasikika akishuka kutoka ngazini na wote wakatazama upande wake. Akafikia meza na kuketi kwenye kiti kilichokuwa wazi, kisha akachukua paja la kuku katikati pale na mboga za majani na kuweka kwenye sahani; kwa haraka sana. Wote wakawa wanamwangalia kwa jinsi alivyoonyesha utundu mwingi.

"Chicken looks great mom! (kuku inaonekana kuwa nzuri sana mama)," akasifia nyama ya kuku kwa mama yake.

"Dylan... manners (adabu)," Jaquelin akamwambia kwa sauti ya chini yenye mkazo.

Alikuwa amekaribia kuanza kula nyama yake, pale alipowatazama wote na kukuta wanamwangalia. Alipotazama sahani zao, akagundua hakuna hata mmoja wao aliyekuwa ameweka chakula.

"Ooh... sorry," akasema kiajabu-ajabu.

"D una miaka mingapi sa'hivi?" Beatrice akamuuliza.

"27," Dylan akajibu.

"Oooh kweli... Harleen anakuacha mwaka mmoja," akasema Beatrice.

"Eee... si kabibi kizee haka!" Dylan akamtania Harleen.

"Mhm... bado hajauacha utoto tu!" akasema Harleen, akimaanishia Dylan kufika na kuvamia nyama.

"Yaani!" Jaquelin akasema.

"Nyama ndiyo go yangu ya kwanza. Acha kujishaua binti-mashavu... kamata msosi hapo," akasema Dylan huku anachukua chakula kingine.

Wote wakaanza kuweka vyakula kwenye sahani zao taratibu, kisha wakaanza kula pamoja. Story walizopiga hasa zilihusiana na mambo ya zamani na maisha ya sasa. Pia walizungumzia kuhusu mdogo wake Harleen, yaani David, na Beatrice akawajulisha kwamba mwanaye huyo alikuwa shule ya sekondari boarding; wakati huu akiwa kidato cha pili. Dylan alikuwa mwepesi sana wa kuongea, hivyo alifanya mazungumzo yawe yenye kuchangamsha sana kila wakati ambao angeongea.

"Mmmm... kweli?" akauliza Dylan.

"Ndiyo," akajibu Harleen.

"Mh? Hapana," Dylan akakataa.

"Ish... kwa hiyo hautaki au?" Beatrice akauliza.

"Siyo sitaki, ila bado siamini-amini. Huyu binti-mashavu alikuwaga anataka sana kuwa Wema Sepetu, sasa nashangaa sa' hivi mnaniambia ni daktari. Mwangalie tu kwanza alivyo, udaktari wapi na wapi!" Dylan akasema kichokozi.

"Bichwa lako!" Harleen akamwambia, na wote wakacheka.

"Ni daktari ndiyo. Tena daktari mzuri sana," Gilbert akasema, na Jaquelin akamtazama kwa umakini.

"Okay... kwa hiyo unatibu nini? Au ndiyo wale wale wa vikombe vya Loliondo?" Dylan akamtania Harleen.

"Naweza kuuchana-chana mwili wako wote na kuurudishia jinsi ulivyokuwa," akasema Harleen.

"Mmm... labda mwili wa maboksi," akasema Dylan.

Wazazi wao wote walifurahishwa sana na jinsi watoto wao walivyoonyesha ukaribu, ijapokuwa bado Jaquelin alimwona Harleen kwa njia tofauti sana.

"Umeshafanya upasuaji mara nyingi eti?" Jaquelin akamuuliza binti.

"Ndiyo. Kila mara napofanya upasuaji lazima tutoke washindi," akajisifu ili kumkera Dylan.

"Huwa unajisumbua tu wewe. Mnakaa huko mnapasua mende, akifa mnasema mmeshinda kwa kuwa haijawa-cost kununua dawa ya kupulizia," akasema Dylan na kufanya wote wacheke sana, hasa Beatrice.

"Hmm... hiyo kazi ngumu aisee. Unahifaji kuwa katili sana," akasema Gilbert.

"Ahahah... siyo sana. Na... nina muda sijafanya upasuaji, nilitaka kupumzika kwanza," akasema Harleen.

"Umeshapasua mende wengi eeh?" Dylan akamuuliza kichokozi.

"Siyo mende Dylan, ni watu," akasema Gilbert.

"Najua. Namtania tu," akasema Dylan kwa uthabiti kiasi.

"Kwa hiyo haujawahi kufeli upasuaji hata mara moja?" Jaquelin akamuuliza.

"Hapana. Unajua... hata wakati wewe ulipohitaji liver transplant, mimi ndiye niliyekufanyia upasuaji... pamoja na wengine," Harleen akamwambia Jaquelin.

Uso wa Jaquelin ukabadilika na kuwa makini. Gilbert, Beatrice na Dylan, wote walionekana kutotarajia jambo ambalo Harleen alisema.

Walikuwa wanajua kwamba Jaquelin alifanyiwa upasuaji wa ini miaka mitatu iliyopita, kwa hiyo haikuwa kile Harleen alichosema kilichowafanya waishiwe pozi, bali ni SABABU ya kile alichosema Harleen. Wanne hao walijua vizuri sababu iliyofanya Jaquelin ahitaji kubadilishiwa ini, lakini Harleen hakujua. Yeye alijua sababu ya kidaktari ilikuwa ni kwamba Jaquelin alipatwa na kansa ya ini, lakini siyo kilichopelekea mpaka akaipata.

Harleen akaendelea kula, bila kujua kwamba alikuwa amewarudishia kumbukumbu mbalimbali wanne hao. Alipomtazama Dylan, jamaa akavunja uso wenye kughafilika na kutoa tabasamu bandia.

"Kumbe?" Dylan akauliza ili kufanya Harleen ahisi mambo yako sawa.

Harleen akatikisa kichwa kukubali.

Gilbert pamoja na Beatrice wakazisawazisha sura zao pia na kuendelea kula. Ni Jaquelin pekee ndiye aliyeendelea kumtazama Harleen sana, mpaka dada wa watu akaanza kujishtukia.

"Aunt Jacky... uko sawa?" Harleen akamuuliza.

"Aa... yeah.. I'm fine. Sikujua kwamba... wewe pia uli.... asante,"Jaquelin akasema bila raha.

"Hey Dylan, chuo ulichosomea kiliitwaje? Beatrice akauliza ili kubadili mada upesi.

"Aam... USP. University of Saõ Paulo," akajibu.

"Aa-aaah... iseme kibrazili bwana," akasema Beatrice.

"Universidade de Saõ Paulo," Dylan akajibu.

"Wacha! Ahahaaa... umekuwa mtaalamu wa lugha yao. Hata Harleen anaweza Spanish pia," akasema Beatrice.

"Kweli?" akauliza Gilbert.

"Yeah," akajibu Harleen.

"Ahahah... naona nyie lenu moja. Yaani aunty hata kama utasema binti-mashavu anajua kuendesha ndege, tayari atajua," Dylan akatania.

"Hivi we' vipi? Kwa hiyo unafikiri tu ni wewe ndiyo unaweza Spanish?" akauliza Harleen.

"Sijasema hivyo. Lakini wewe... aagh... huwezi," Dylan akamkejeli.

"Culo!" Harleen akamwambia Dylan, akimaanisha 'tako!'

Dylan akakodoa macho, kisha akaanza kucheka.

"Vipi? Amekwambiaje?" akauliza Beatrice.

Harleen akamwangalia Dylan kiukali, kama kumwambia 'ole wako useme!'

"Ahahah... ameniambia eti me boya," jamaa akapindisha maana.

Gilbert alijua Spanish kiasi, hivyo alikuwa ameelewa kihalisi Harleen alichosema. Akatabasamu tu na kuendelea kula.

"Unajua Spanish kweli?" akauliza Dylan.

"Ndiyo," akajibu Harleen.

"Con fluidez? (vizuri kabisa?)" Dylan akauliza.

"Kabisa," Harleen akajibu.

"Huna lolote wewe. Hapo najua umeotea tu," Dylan akamwambia Harleen.

"Hebu msemeshe uone," akasema Beatrice.

"Cúal es tu nombre? (unaitwa nani?)" Dylan akamuuliza binti.

"Me llamo Harleen (naitwa Harleen)," akajibu.

"Ahahahah... umeotea," Dylan akakejeli tena.

"Ah-aah we' endelea kumsemesha," Beatrice akasisitiza.

"De donde eres? (unatokea wapi?)" akauliza Dylan.

"Tanzania," akajibu Harleen.

"Vosotros de donde sois? (unatokea wapi?)" akauliza tena Dylan.

"Tanzania," akajibu Harleen.

Hii ikamfanya Dylan atabasamu.

"Ahahah... eti anajaribu kunichanganya kwa kuniuliza swali lile lile kwa njia tofauti," Harleen akamwambia mama yake.

"Hahaa... umemweza," akasema Beatrice.

Muda wote walioendelea kula na kupiga story baada ya hapo, Jaquelin pamoja na Gilbert hawakuchangia sana maongezi. Ilikuwa ni kama walipatwa na jambo fulani baya sana kwenye akili zao, hasa Jaquelin, ambaye alionekana kukosa uchangamfu kabisa. Hapo kulikuwa na siri nzito iliyofichika, na Harleen alikuwa ameichokonoa ilikofichwa bila kutambua. Ilikuwa nini?


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next