STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: [email protected]
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA KWANZA
ANZA NAYO................
NDOTO YANGU NDANI YA MSITU WA KUTISHA
MSITU WA MAU, KENYA.
Ndani ya msitu mmoja uliokuwa na miti mirefu iliyoshonana, katikati kabisa ya msitu huo palikuwa na nyumba ndogo ambayo ilijengwa kwa mbao iliyo onekana kabisa kwamba ilikuwa imetelekezwa kwa muda mrefu kama sio mhusika kuijenga kwa ajili ya kazi yake maalumu. Msitu ulikuwa kimya, ni sauti za ndege tu ambazo zilikuwa zikipenya ndani ya eneo hilo tulivu, hakukuwa na upepo uliokuwa unasikika kwa sababu ya maeneo mengi kushonana kiasi kwamba ilikuwa ni ngumu upepo kupenya mpaka chini.
Kwenye nyumba ambayo ilitelekezwa hilo eneo kulikuwa na watu kadhaa ambao walikuwa wamevaa nguo za jeshi. Ndani kabisa ya hiyo nyumba kulikuwa na mateka mmoja ambaye alikuwa amefungwa vyema kwa minyororo kwenye mwili wake. Mwili wake ulikuwa umechoka, alikuwa anavuja damu kwenye maeneo mengi ya mwili huku watu kadhaa ambao walikuwa kwenye yale mavazi ya jeshi wakiwa wamelazwa kwenye vitanda nje kidogo ya chumba hicho wakiendelea kuvuja damu.
Ni wachache ambao walikuwa ni wazima wa afya kabisa na wengine ndio ambao walikuwa naye ndani ya hicho chumba bwana huyo aliyekuwa amechakaa kwa kipigo ambacho alikipata. Pembezoni mwa hicho chumba alikuwepo mwanamke mmoja ambaye alikuwa mrembo kwa mwonekano wake japo haukuwa ukiridhisha kutokana na mazingira ambayo alikuwepo na kukosa mahitaji ya mhimu kuuweka mwili wake kwenye hali ya usafi zaidi. Mwanamke yule hakuonekana kupendezeshwa na kilichokuwa kinaendelea ndani ya lile eneo ila hakuwa na namna angeweza kufanya hivyo alitoka kwa hasira na ghadhabu kwenye nje kupunga upepo huku akiwaacha watu wale wafanye kile ambacho walikuwa wamedhamiria kukifanya humo ndani.
Ndani ya hicho chumba walibakia wanaume watatu, wawili walikuwa wamesimama pembezoni wakiwa wameegamia ukuta na mmoja ndiye ambaye alikuwa amesimama mbele ya bwana huyo aliyekuwa amefungwa kwenye kiti. Mwanaume ambaye alikuwa amesimama mbele yake, alivaa mavazi ya jeshi kasoro upande wa juu, kifuani kwake alikuwa amevaa vesti ya rangi nyeusi na kwenye mkono wake alikuwa ameishika sigara ambayo alikuwa anaivuta kwa mbwembwe iliyo changanyikana na gadhabu huku moshi akiwa anampulizia huyo mtu wake usoni.
Alitoa ishara kwa mwanajeshi mmoja, hakusita zaidi ya kulibeba dumu kubwa ambalo lilikuwa pembeni yake, dumu lilijaa mafuta ya petroli ambayo aliyamiminia kwenye mwili wa mwanaume ambaye alikuwa amefungwa kwenye kile kiti kwa umakini bila kumwaga mwaga hovyo chini. Alipo ona inatosha alisogea pembeni na kulipeleka lile dumu mbali ili isije kuwa hatari hata kwa upande wao pia, mwanaume yule ambaye alikuwa anaendelea kuivuta sigara yake aliinama kidogo mpaka alipokuwa ameketi bwana yule kwenye kiti.
"Wakati napewa kazi ya kukutafuta kwa namna na gharama yoyote, binafsi nilijua kwamba ingenichukua zaidi ya mwaka mzima au zaidi kukupata ukizingatia umetafutwa kwa miaka zaidi ya mitano na hukuwahi kujulikana kwamba ni wapi uliwahi kuwepo. Maajabu nimekupata ndani ya muda mfupi tu kiasi kwamba kazi imekuwa rahisi lakini kwa upande wako mambo hayawezi kuwa rahisi kwa sababu unatakiwa kufa leo kwa maumivu" mwanajeshi yule alivuta tena sigara na kuutoa moshi kwa mara nyingine kwa kejeli na majivuno.
"Hii usiichukulie personal ndugu yangu, hii ni kazi na walio nituma ndio wanahitaji iwe hivi kwahiyo kama nisipo kuua mimi ndiye nitakufa. It's over" aliongeza sentensi fupi kisha akasimama, alivuta sigara yake kwa mara nyingine na kuiachia kwenda kwenye mwili wa yule mwanaume ambaye alianza kupiga kelele baada ya moto kuwaka na kuanza kuuunguza mwili wake. Mwanajeshi yule aliitoa simu yake akapiga picha za kutosha na kuchukua video fupi kabla uso wa mwanaume yule haujaharibika kisha aliichomoa bastola kwenye kiuno chake, aliikoki kwa kuigongesha kwenye buti lake na kumimina risasi zote kwenye kichwa cha mwanaume ambaye alikuwa anawaka moto baada ya kuzidisha makelele.
Utulivu ulichukua nafasi, mwanajeshi mmoja alisogea na kuanza kuuzima ule moto ili usije ukaleta madhara kwenye hiyo nyumba kwa ujumla lakini kipindi anaendelea na zoezi hilo, walisikia mlio wa risasi eneo la mbali na hiyo nyumba. Hiyo hali haikuwa ya kawaida kwenye eneo kama lile, ni eneo ambalo hakuna mtu mwingine angeweza kufika kwa wakati huo, ni eneo ambalo hakuna binadamu alikuwa na ujasiri wa kwenda kufanya hata utalii kwa sababu lilikuwa linatisha na liliaminika kwamba lilikuwa na viumbe hatari ndani yake, sasa wakati huo hiyo risasi ilipigwa na nani? Kiongozi wao ambaye ndiye alitoka kumuua yule mateka wao alitoka humo ndani kwenda nje kujua ni kipi kilikuwa kinaendelea.
Kutokana na baridi kali ambalo lilikuwa huko, watu wengine ambao walikuwa pale nje ambao nao walikuwa kwenye mavazi ya jeshi walikuwa wakiota moto huku yule mwanamke ambaye alionekana wazi kwamba hakupendezwa na kile ambacho kilikuwa kinafanyika pale akiwa amejitenga mwenyewe na kuegamia kwenye mti mmoja ambao ulikuwa karibu na pale ambapo wenzake walikuwa wakiota moto na kuchoma nyama. Wote ambao walikuwa nje waliusikia ule mlio wa risasi hivyo kila mtu alitahayari kutaka kujua kwamba ni kipi kilikuwa kinaendelea.
Hawakukaa tena bali kila mtu alisimama wakiwa wanaangaza huku na huko lakini hawakuona kitu ndipo mmoja wao alishtuka baada ya kuona kuna mwenzao amekosekana hilo eneo.
"Jordan yuko wapi?" yule aliyeshtuka aliuliza kwa wasiwasi akiwa anamwangalia kila mmoja wao usoni ili kuhakiki kuhusu huyo ambaye alikuwa anamuulizia.
"Alisema anataka kupunga upepo nje kidogo ya hapa hivyo aliingia huko msituni" sauti ya mmoja wao ndiyo ambayo iliamsha hisia ambazo hazikuwa sawa, kiongozi wao huyo aliinyanyua simu yake kupiga kwa kutumia radio call ambayo kila mmoja wao alikuwa anatembea nayo. Simu hiyo iliita mara tatu mfululizo bila kupokelewa, jambo hilo lilitoa ishara mbaya, hapakuwa pema hivyo alimtaka mwanamke yule ambaye hakuwa kwenye mood nzuri kuangalia kwa kutumia kumpyuta yake kujua huyo mwenzao yuko wapi kwa wakati huo.
Alikimbilia ndani na kuhaki mfumo wa mawasiliano kupitia kifaa cha mwenzao, alionekana kuwa mita miambili kutoka walipokuwa wao na kifaa hicho kilionekana kusimama sehemu moja bila kujongea, hawakuwa na muda wa kusubiri, kiongozi wao aliwataka wajiandae kwenye kuangalia hali ya mwenzao kwa sababu ukimya kama huo haukuwa utaratibu kwenye kazi yao, maana yake hakukuwa na usalama kwa mwenzao na walitakiwa kumsaidia kwa haraka kama kuna shida yoyote ingekuwa imempata.
Walitembea kwa umakini kwa dakika mbili ndipo walifika ile sehemu ambayo ilionyesha kwamba kulikuwa na kifaa cha mawasiliano cha mwenzao, kifaa kilikutwa kikiwa kwenye nyasi pembeni yake kukiwa na damu ambayo ilionyesha kuendelea kuelekea mbele ikabidi waifuate. Hatua kumi kutoka hapo ndiyo sehemu ambayo waliukuta mwili wa Jordan shingo yake ikiwa na alama za kutoboka na kichwa kikiwa kimepasuka kwa nyuma. Jordan alikuwa amekufa na kichwa chake kilionekana kujibamiza kwenye mti sehemu ambayo ilikuwa na damu na nywele kiasi. Bastola yake ilikuwa pembeni ya mwili wake, aliyekufa alikuwa ni miongoni mwa watu wa kuaminika vilivyo, kifo chake tena cha ghafla namna hiyo ni ishara kwamba walikuwa wameupokea ugeni ambao hawakuutarajia kwa sababu mtu ambaye aliwaleta ndani ya hilo eneo walitoka kumuua muda sio mrefu. Sasa huyo mtu mwingine ambaye aliingilia hiyo shughuli alikuwa ni nani? Ilizaliwa hofu na maswali ambayo hata wao hawakuelewa namna ya kuweza kuyapatia majibu yake.
"Kuna mtu mwingine ndani ya huu msitu na huenda mpaka muda huu anatuona kwa kila tunacho kifanya hapa" aliongea kiongozi wao huku akiwa anainama kuufanyia uchunguzi mwili wa mwenzake. Mwili ulikuwa bado wa moto, ni ishara kwamba ni muda mfupi; ulipita tangu mtu huyo aweze kuuawa, alitoa ishara ya vijana wake kuweza kutawanyika kwa ajili ya kumsaka mgeni ambaye alikuwa ameingia ndani ya msitu bila wao kuwa na taarifa na kuanza kuwapunguza.
Yalikuwa ni majira ya jioni jua likiwa linazama hivyo chini ya msitu kulikuwa na mwanga kwa mbali ambao kadri dakika zilivyokuwa zinasonga ulikuwa unafifia taratibu. Mwanajeshi mmoja akiwa anatembea, alishangaa kuna shilingi ya zamani ambayo ilikuwa inang'aa ikitua mbele ya macho yake. Hakuelewa ilirushwa na nani na ilitokea wapi hivyo alisogea ili kuweza kuyashuhudia hayo maajabu, akiwa ameikaribia na kuinama ili aipate mwili wake ulihisi uzito ambao haukuwa wake, akajua kabisa kwamba kulikuwa na ongezeko la mtu mwingine karibu yake. Aligeuka haraka akiwa ameinyoosha bastola yake ila hakuona kitu ikamlazimu kuyarudisha macho yake haraka kwenye ile shilingi ambayo ilikuwa nyuma yake.
Wakati anageuka alikutana na kitu cha ajabu, alifanikiwa kuyafungua macho yake mara moja tu pekee, kwa sababu ile shilingi hakuiona tena na alipo jaribu kuweza kuangalia alihisi kama kuna kivuli ndipo akayafumbua macho yake baada ya kuhisi kulikuwa na kivuli kutokea juu kwenye mti. Ni kweli kuna mwanaume alikuwa amenasa kwenye mti kwa kutumia miguu yake huku mikono ikiwa imeleelekezwa chini. Wakati anapata mshtuko, alihitaji kuielekezea bastola yake kuelekea kwa yule mtu, kwa bahati mbaya kidole kilizama kwenye koromeo lake na kulivunja, alirudi nyuma akiwa ameishika shingo yale ila hakumaliza hata sekunde tano, alikufa baada ya ile shilingi kuzamishwa kwenye paji yake la uso na kifua kilivunjwa kwa ngumi ambayo ilimgandamiza kwenye ule mti kiasi kwamba hata mifupa ya uti wake wa mgongo ikavunjika vibaya.
Ukimya wake uliokithiri ndio ambao ulimsogeza yule mwanamke ambaye alikuwa mtaalamu wa kompyuta karibu na eneo hilo, aliitoa sauti ya mshtuko huku moyo wake ukianza kwenda na kupiga kwa nguvu. Hakutarajia kukutana na kitu kama hicho kwa mara nyingine tena, ni muda mfupi walitoka kushuhudia mwili wa Jordan lakini haikuchukua muda mwingine tena mwenzao alikuwa ameuliwa kikatili kama mwanzo lakini huyo wa pili kwenye paji lake la uso iliachwa shilingi ambayo ilibaki imeshikilia hapo ikiwa inang'aa isivyokuwa kawaida.
Ile hofu yake ilimfanya aanze kurudi nyuma huku akiwa anaitoa simu yake mfukoni baada ya kugundua kwamba hata kile kifaa cha mawasiliano kwenye sikio lake hakikuwepo huenda ni kwa sababu alikisahau kule kwenye kumpyuta. Alisimama na kujibanza kwenye mti baada ya kuhisi kama kuna kitu kilikuwa kimempita kwa kasi nyuma ya alipokuwepo yeye, jambo hilo alihisi ni ndoto ila aliamini kwamba ni kweli baada ya kuiona ile simu yake ambayo alikuwa ameishika mkononi ikiwa imepasuka baada ya kubamizwa kwenye mti. Lilikuwa ni jambo la haraka kufanyika kiasi kwamba yeye mwenyewe alibaki anashangaa asijue tukio hilo lilitokeaje na kwanini aliyelifanya hakumdhuru yeye? Hakuwa na muda wa kusubiri zaidi ya kuanza kukimbia kuelekea upande ambao walikuwepo wenzao wakiwa wanaendelea kumsaka mtu ambaye bila shaka naye alikuwa anawasaka ndani ya msitu huo mzito.
Ndiyo kwanza tunaifungua sehemu ya kwanza kabisa ya simulizi hii, ungana nami mpaka mwisho ili tuweze kwenda sawa pamoja.
FEBIANI BABUYA.
Comments