Reader Settings

DYLAN

Story by Elton Tonny

Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

(R-rated 18+)

Enjoy!


★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA NANE

★★★★★★★★★★★


"Dylan..." Harleen akaita, lakini akashindwa kuongea.

Dylan akawa anamtazama tu kama mtu aliyezubaa, na hapo akatoka mwanaume fulani mweupe, aliyekuwa na mwili uliokaribiana na wa Dylan kwa upana. Alikuwa na nywele fupi zilizonyolewa vizuri, na ndevu nyingi kiasi zilizochongwa vyema kutokea kwenye timba. Alikuwa amevalia vest nyeupe na suruali nyepesi, naye akamwangalia Dylan kwa umakini.

"Habari yako?" mwanaume huyo akamsalimu Dylan.

"Ni nzuri. Vipi wewe?" Dylan akauliza kirafiki.

"Fresh. Mgeni wako?" mwanaume huyo akamuuliza Harleen.

Harleen alikuwa amepandwa na presha, lakini akajitahidi kujidhibiti. "Ndiyo... aam... Alex, Dylan. Dylan... Alex," akajibu na kuwatambulisha.

"Ooh... huyu ndiyo Dylan kumbe?" Alex akauliza.

"Ndiyo," Harleen akajibu.

"Okay. Nimefurahi kukutana nawe bro," Akex akamwambia Dylan.

Alimsogelea na kumpa mkono, naye Dylan akatoa wake na kumpa ili waitingishe pamoja kwa utambulisho.

"Harleen aliniambia kukuhusu. Wewe ni rafiki yake wa utotoni," Alex akasema.

"Ndiyo, ni mimi. Nimefurahi pia kukujua Alex," Dylan akajibu kistaarabu.

"Please... niite tu Ray. Harleen anapenda kuniita kwa jina langu la mwanzo ila nimeshazoea la mzee," Alex akasema kiutani.

"Aaaa... sawa sawa, Ray," Dylan akasema.

Hapa Dylan akawa ametambua kuwa bila shaka huyu ndiyo Ray aliyempigia simu Harleen jana. Aliingiwa na hisia za kujiona mpumbavu sana kutohisi lolote baya kumwelekea Harleen, na sasa akajikuta kwenye mzunguko wa mapenzi (love triangle).

"Aa... Harleen... utamwambia basi aunty Beatrice kuhusu ile ishu sawa?" Dylan akatokeza hadithi ya uwongo ili Alex asihisi chochote.

Harleen, kwa wasiwasi, akasema, "S..sawa. Nitamwambia."

"Okay. Samahani kwa... ahah... kuja bila taarifa. Nilikuwa nampitishia huyu ujumbe," Dylan akasema kwa kujikaza.

"Oh, usijali kabisa," Alex akajibu.

"Kwa hiyo... we' ndo' shem au siyo?" Dylan akauliza kwa njia ya masihara, lakini alikuwa anachimba ukweli.

"Ahahah... yeah. Nimekuja leo tokea South Africa kumtembelea huyu sweetheart," Alex akasema huku akikibana kiuno cha Harleen kwake kwa upendo.

Harleen akatoa tabasamu la bandia akijifanya mambo yako sawa, lakini mapigo yake ya moyo yalidunda kwa nguvu sana.

"Okay sawa. Basi, wacha me niende. Tutaonana... wakati mwingine," Dylan akasema.

"Sawa sawa. Harleen mbona uko kimya? Anaaga," Alex akamwambia.

"A..aa... sawa. Nita... nitakujulisha... nitamjulisha mama... kuhusu ujumbe," Harleen akasema kwa kubabaika.

"Haya, usiku mwema kwenu," Dylan akawaaga na kuondoka hapo upesi.

Alirudi kwenye gari lake akiwa amevunjika moyo kwa kiasi fulani. Lilikuwa ni jambo ambalo hakutegemea kutoka kwa Harleen, hasa kwa sababu alikuwa ni rafiki yake wa muda mrefu pia. Aliondoka eneo hilo na kuendelea kuendesha gari bila kuwa na sehemu maalumu ya kwenda. Alihisi hasira pia, naye alitaka kufanya jambo fulani ili azipunguze kwa kuwa alihisi huenda hata angefanya jambo baya.

Kisha wazo moja likaja. Alikumbuka kwamba Bosco alimwambia kuhusu 'challenge' ya mpiganaji fulani dhidi yake leo usiku, na nafasi bado ilikuwepo ya kukubali au kukataa moja kwa moja mpaka kufikia saa nne. Ilikuwa saa mbili kasoro sasa, hivyo akasimamisha gari na kumpigia simu Bosco kumjulisha kuwa alikubali challenge hiyo. Bosco akafurahi na kusema angesaini karatasi mapema ili yeye akifika kule show ipigwe kiaina.

Wazo la Dylan lilikuwa ni kwenda kuzipunguza hasira zake kule, siyo kupata pesa. Akaelekea kule upesi na kujiandaa kwa ajili ya pambano hilo ambalo lilisubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa mchezo huo haramu kwenye mtandao. Dylan, akijulikana kama Killmonger hapo, alivaa mask yake na kuingia kuziruka pamoja na jamaa yule aliyejiita The Crusher. Huyu jamaa alikuwa ametoa challenge hiyo kwa kuwa siku ile Dylan alimfumua vibaya pamoja na kwamba alikuwa amechoka, hivyo ni kama alikuwa anataka kumlipa, kwa kuwa alijisifu kuwa usiku huu angehakikisha anamwonyesha Killmonger nini maana ya jina lake The Crusher, yaani mvunjaji.

Wala hata jina lake halikumtisha Dylan, kwa kuwa pambano lilianza kwa The Crusher kupigwa vibaya na Killmonger mpaka akaishiwa nguvu. Yaani usiku huu Dylan alihakikisha haguswi sehemu hata moja, na ijapokuwa alizoeleka kupigana kwa mtindo wa masihara, sasa alihakikisha anatia maumivu mengi kwenye mwili wa mwanaume huyo. Alimpiga sana, hata iliposemwa tayari ameshinda, bado akaendelea kumpiga tu na kusababisha azimie; hii ikiwa ni mara ya pili anamzimisha huyo mwanaume!

Ilibidi mabaunsa kadhaa waingie kumzuia asiendelee kwa kuwa kama angeendelea basi angemuua. Dylan akatoka hapo akiwa anapumua kwa hasira sana, na hakusemeshana na yeyote yule hadi akatokomea. Queen, na hata Bosco mwenyewe alishindwa kuelewa nini kilikuwa kimetokea, na baada ya hapo shindano hilo likasitishwa mpaka wakati mwingine.


★★★


Dylan akawa ofisini kwake siku iliyofuata akiendelea na kazi. Harleen alikuwa amepiga simu mara 28 tokea asubuhi, lakini Dylan hakupokea. Alimtumia jumbe nyingi sana pia, lakini Dylan hakusoma hata moja. Ilikuwa ni kama haoni na hasikii, naye alikuwa mbali mno kwenye kujali tena kwamba Harleen angehisije. Dylan alikuwa ni mtu makini sana ilipokuja kwenye suala la mapenzi, na ndiyo maana hakuwa kwenye uhusiano na yeyote tokea aliporudi nchini. Hata kule Brazil, alikuwa makini pia kutojiingiza kwenye masuala ya mapenzi kwa kuwa aliwahi kupitia hali zenye kuvunja moyo.

Lakini kwa Harleen alihisi labda kungekuwa na afadhali kwa sababu ni mtu aliyemjua tokea utotoni, na hata ingawa hawakuwa pamoja kwa muda mrefu, alimwamini kama rafiki wa karibu, hivyo hakufikiria angemfanyia vile. Wakati huu hakutaka kusikia maelezo yoyote kutoka kwa mwanamke huyo, kwa kuwa aliona yasingesaidia lolote lile zaidi tu ya kurudisha kumbukumbu zenye kukwaza.

Kwenye suala la marafiki pia, Dylan alikuwa aina ya mtu asiyejichanganya na watu hata kidogo, ijapokuwa alikuwa mtu mchangamfu na mwenye kufunguka sana. Mpaka anakuwa rafiki ya mtu ilihitajika awe amesitawisha upendezi wa hali ya juu kumwelekea mtu huyo; kama ilivyokuwa kwa Bosco na Fetty.

Baadaye, aliondoka ofisini pale na kuelekea nyumbani. Karibia kila mtu kwenye kampuni ambaye alimwona Dylan angeweza kutambua kwamba mwanaume hakuwa sawa siku hiyo kutokana na kuwa makini muda wote kuliko kawaida  Walikuwa wamemzoea kuwa mwanaume mchangamfu lakini thabiti, ila kwa wakati huu alikuwa amekaza mno.

Dylan aliporudi nyumbani alifanya zoezi kiasi tu, siyo kwa jinsi alivyozoea, kisha akaondoka kwenda tu kutembea. Bosco alikuwa amemtafuta baada ya kushangazwa na jinsi alivyotenda jana usiku, naye Dylan akasema tu alikuwa na misongo ndiyo maana. Bosco alimwambia pamoja na yote lakini bado pesa alipewa, hivyo ikiwa angeihitaji sehemu yake angemletea, lakini Dylan akamwambia abaki nayo tu.

Alikwenda sehemu ile ambayo mara ya kwanza ametoka na Harleen waliitumia kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi. Uwanja huo ulikuwa bila watu wengi wakati huu, na walioonekana hapo walikuwa mmoja mmoja au wawili wawili waliokaa sehemu za mbali mbali, hivyo palikuwa pametulia sana. Akaketi kwenye jiwe dogo la msingi, akiwaangalia watu fulani wawili kwa mbele walioonekana kuwa wapenzi. 

Walionekana wakipiga story zenye kufurahisha bila shaka kwa namna walivyocheka pamoja na kulalianalaliana. Aliwaangalia wao tu, lakini kichwani kwake Dylan alikuwa anawaza vitu vingine tofauti nao kabisa. Vingi vilivyotokea, vinavyotokea, na huenda hata ambavyo vingetokea baadaye. Kwenye suala la mapenzi alikuwa amefeli wapi? Mwili na sura nzuri anavyo, pesa anayo, akili ndiyo usiseme, kwa nini bado moyo wake ulitangishwa ilipokuja kwenye suala la mahusiano?

Giza lilikuwa linaanza kuingia, na sasa Dylan alipata wazo kwamba labda aondoke tu hapo na kwenda sehemu fulani apate kinywaji. Lakini kutoka kwenye mfuko wa suruali yake, alihisi simu yake ikitetemesha paja lake, kuashiria ujumbe mpya umeingia. Alijua bila shaka ingekuwa ni Harleen tena, na kufikia wakati huu alielewa mwanamke huyo angekuwa na mambo mengi aliyotaka wazungumze pamoja; sanasana labda kujitetea. Hakuona haja ya kuendelea kukausha, hivyo akaona aweke usawaziko kidogo na kuitoa simu yake. Lakini aliyetuma ujumbe wakati huu hakuwa Harleen, bali Fetty. Akaachia tabasamu la mbali.

'uko wp?' ujumbe ulisomeka hivyo.

'niko kwenye kiwanja fulani huku town,' Dylan akamjibu kwa text.

'unafany nn?'

'nimekaa tu.'

'nije na mimi tukae wote?'

Dylan akatabasamu.

'sitakuwa mwenye kuburudisha sana leo,' Dylan akamwandikia.

"Acha uwongo," Fetty akasema.

Dylan aligeuka nyuma na kukuta Fetty amesimama hapo huku anamwangalia. Aliachia tabasamu na kusimama akishangaa kiasi kwamba hakuweza kuhisi uwepo wa mwanamke huyu nyuma yake.

"Hey... kumbe ulikuwa hapo muda wote!" Dylan akasema.

Fetty akatabasamu na kusema, "Siyo muda wote. Nilikuwa napita kule nikakuona... ndiyo nikasogea."

"Aaa... unatokea kazini?" Dylan akauliza.

"Ndiyo."

"Sawa."

"Na wewe? Kwa nini uko hapa?"

"Napenda kuja hapa mara nyingi. Huwa nafanyiaga na mazoezi ya asubuhi huku," Dylan akajibu.

"Ahaa... lakini sasa hivi kwani unafanya mazoezi?"

"Aam... hapana. Nilitaka tu kuja kuituliza akili."

"Mh... ahahahah... Leo unaigiza mpole kweli utafikiri umepatwa na shida kuuubwa," Fetty akasema kiutani.

"Kwani me ni nani nisipatwe na shida?"

"Aah.. nyie watu huwa mna shida gani sasa pesa ikiwepo? Shida gani itakayokupata wewe labda? Au umetendwa nini? Ahahahah..." Fetty akamtania.

Dylan akaangalia chini kwa njia iliyoonyesha ana huzuni, nalo tabasamu la Fetty likafifia baada ya kuwa ametambua kuna kitu kinamsumbua jamaa.

"Ume... umetendwa?" Fetty akauliza.

"Siwezi kusema kwa njia hiyo, lakini... ndiyo. Nimepatwa na shida fulani kimahusiano," Dylan akasema.

"Heh... pole mwaya. Yaani mabinti wa kibongo bwana," Fetty akasema.

"Kwani wewe ni binti wa wapi?"

"Wa bongo ndiyo, lakini..."

"Sasa si ni wale wale tu!"

"Akha! Mimi hayo masuala huwa sina kabisa. Wengi waongo siku hizi... wanakuwa kwenye mapenzi ili kujichumia hela au kuondoa tu upweke."

"Ndiyo ni kweli. Na me najiona mjinga kwa sababu nahisi mimi pia ni mmoja wa hao wanaotaka kuondoa upweke namna hiyo," Dylan akasema kwa hisia.

"Wewe si una hela? Upweke unatoka wapi?"

"Kuwa na pesa nyingi siyo chanzo kikuu cha furaha na kuridhika. Ni mahusiano ambayo hayana ubinafsi ndiyo humpa mtu furaha... lakini kama ulivyosema... watu wengi ni wabinafsi mno siku hizi," Dylan akamwambia.

Fetty akatathmini maneno hayo kwa ufupi, kisha akauliza, "Ni... yule yule dada uliyekuja naye siku ile?" 

"Ndiyo. Nimegundua ghafla sana kwamba ana mwanaume mwingine."

"Hmmm... na uzuri wote ule! Mapenzi tuwaachie mnaoyaweza," Fetty akasema kiutani.

Dylan akatabasamu na kuuliza, "Ulikuwa unaenda nyumbani?"

"Ndiyo. Tena ni afadhali nimekuona ili unipe na lifti kabisa."

"Ahahah... leo bajaji hamna?"

"Bajaji ya nini wakati una gari linanukia vizuri zaidi ya mwanamke?" Fetty akatania tena.

Dylan alifurahishwa kwa kadiri kubwa na Fetty. Hakuwa ametegemea kufurahia chochote kwa leo, na sasa mwanamke huyu akawa ameweza kubadili matarajio yake. 

Walielekea kwenye gari na kuondoka eneo hilo, lakini Dylan hakumpeleka Fetty moja kwa moja kwake. Alimpeleka kwenye hoteli kubwa ya kifahari ili wapate mlo mzuri hapo. Fetty mwanzoni alikuwa anasita kwenda kwa sababu alijiona mchafu; ndiyo alikuwa tu ametoka kazini, lakini Dylan akamsisitizia kwenda bila kujali jinsi alivyojiona kwa kuwa yeye aliona yuko kawaida tu.

Fetty alifurahia sana kwa kuwa vyakula alivyoagiziwa vilikuwa vya gharama na vitamu mno. Walikula pamoja huku wanapiga story, hii ikimsahaulisha Dylan mawazo yake yenye kulemea aliyokuwa nayo. Walishiba na kuondoka hapo, Fetty akiwa ametunza nyama nyingi za kuku kwenye tishu na kuweka kwenye mfuko mdogo ili zikatumike nyumbani kwa kuwa Dylan aliagiza chakula kingi kupita maelezo.

Waliagana muda fulani baadaye Dylan alipompeleka binti kule alipopanga, huku Fetty akimwambia kama vipi amtoe tena kesho, na wakati huu angehakikisha amependeza. Dylan alifurahi na kumkubalia, kisha akamwacha na kurudi zake nyumbani. Hakuhitaji kula alipofika kutokana na kushiba baada ya kula na Fetty, hivyo alienda zake chumbani na kuamua kuchukua hatua ya kwanza kumtafuta Harleen.

Wakati huu akili yake ilikuwa imetulia zaidi, hivyo akampigia, kisha akamwambia wakutane kesho mahali fulani ili wazungumze; kama ataweza. Harleen alionekana kutaka kuongea naye zaidi, lakini Dylan akakatisha mazungumzo hayo na kuweka simu pembeni. Hakutaka kutenda kwa hasira kumwelekea Harleen ijapokuwa alikuwa amemuumiza hisia, hivyo akaona aingie tu kupumzika kwa ajili ya kesho.


★★★


Ilifika mida ya saa tisa alasiri siku iliyofuata, naye Dylan akawa amefika kwenye sehemu ile aliyokubaliana kukutana na Harleen. Alimkuta mwanamke huyu ameshafika; akiwa amevalia blauzi nyeusi iliyobana yenye mikono mirefu na suruali ya skinny nyeupe iliyombana vyema na kuchoresha umbo lake vizuri. Alikuwa amependeza sana usoni pia, naye Dylan akafika aliposimama na kumwangalia machoni kwa njia ya kawaida. Harleen akamkumbatia hapo hapo na kuanza kulia, huku Dylan akiwa ametulia tu bila kurudisha kumbatio la mrembo huyu. Kisha akamtoa kwake taratibu na kumfuta machozi, naye mrembo akawa analia kwa aibu tu.

"Harleen... nataka kujua ukweli. Alex... ni nani kwako?" Dylan akauliza kwa upole.

"Ni... ni mchumba... wangu," Harleen akajibu huku akilia.

Dylan akafumba macho kwa kusikitika sana. 

Harleen akaendelea kulia kwa huzuni.

"Basi inatosha Harleen... usilie," Dylan akamwambia kiupole.

"Dylan... hh... Dylan nisamehhh... please my love... nisamehehh..." Harleen akaanza kumwomba kwa huzuni.

"Harleen..."

"... please, no, haikuwa nia yangu kukufanyia vile...hh... ni kwamba tu... Alex..." akashindwa kuendelea.

Dylan alikuwa anamtazama tu kwa makini.

"Dylan... mimi niko tayari kuachana na Alex kwa ajili yako... hh... ninakupenda, na ninaku..."

"Harleen... please. Inatosha, okay?" Dylan akamkatisha.

"Dylan..." Harleen akaendelea kulia.

"Mimi... sijui nisemeje yaani... kama ni kitu nachochukia kwenye mahusiano Harleen... ni betrayal. I've had a rough past when it came to relationships... nilifikiri kwako labda ningeweza kupata ahueni, ila..."

"Dylan mimi ni wako... usikasirike mpenzi wangu kwa sababu... hh... ona, niko kwenye harakati za kuachana na Alex... hatujawa katika mwendo mzuri, na mimi tayari nime..."

Dylan alitazama pembeni tu akiendelea kusikiliza jinsi Harleen alivyojitetea. Alitambua kwamba kwa kiasi fulani mwanamke huyu alikuwa mbinafsi, kwa kuwa kwa mambo mengi alichosema tu ilikuwa ni mimi, mimi, mimi. Ijapokuwa Harleen alikuwa mwenye kuvutia sana, mrembo, mwenye elimu ya juu, na mwenye sifa nyingi nzuri, jambo alilomfanyia Dylan lilikuwa limemaliza hamu yote mwanaume huyu aliyokuwa nayo kumwelekea. Ikabidi amshike na kumkumbatia ili atulie, kisha akaanza kuzungumza akiwa bado amemshikilia hivyo hivyo.

"Harleen... nimefurahi kwamba angalau nime-share jambo fulani zuri pamoja nawe, lakini nafikiri tutapaswa kuishia hapa. Alex... anaonekana kuwa mwanaume anayekupenda sana... hastahili hata kidogo kutendewa namna unavyomtendea. Unafikiri angejua kuhusu sisi hiyo ingekuweka wewe wapi? Nakuomba usiwe mbinafsi Harleen..." Dylan akasema kwa hisia.

"Lakini mimi nakupenda Dylan... siwezi tena kuwa bila wewe!" Harleen akasisitiza.

Dylan akamwachia na kumwangalia usoni. "Ungehisije kama ungejua mimi pia nina mwanamke mwingine huku bado natoka nawe?" akamuuliza.

"Mimi sijali! Bado ningeendelea kuwa pamoja na wewe hata kama ungekuwa nao mia moja," Harleen akasema kwa uhakika.

Dylan akacheka huku amefumba mdomo, kisha akasema, "Basi wewe na mimi ni tofauti sana."

"Dylan... tafadhali nisamehe... nitaachana na..."

"No. Usiniambie hivyo Harleen. Kwa ufupi ni kwamba siwezi TENA kuwa nawe," Dylan akasema kwa uhakika.

"Dylanhh..." Harleen akaanza kulia.

"Ikiwa utafanya hivyo mimi haitaniathiri kwa vyovyote vile, lakini wewe utakuwa umepoteza vyote. Kwa hiyo... nilichokuwa nataka nikwambie ni kwamba... nitaendelea kukuona kama rafiki, na siyo vinginevyo," Dylan akaeleza.

Harleen, akiwa analia, akamshika mikono Dylan na kuing'ang'ania ili amsisitizie kubaki naye. Lakini Dylan akaitoa na kugeuka ili aanze kuondoka. Harleen akabaki kumwita kwa huzuni, kisha akachuchumaa huku analia sana, akimwangalia mwanaume anatokomea.

Dylan akarejea kwenye gari lake na kutulia kidogo. Akafumba macho akivuta taswira ya jinsi Harleen alivyokuwa akilia pale alipomwacha. Kihalisi kuondoka kwake pale upesi namna ile ilikuwa ni kukwepa zile hisia za huruma ambazo zingejengeka kumwelekea Harleen ikiwa angeendelea kumtazama anavyolia. Hakupenda usaliti kabisa. Na Harleen alikuwa mwenye pendeleo kwamba angalau Dylan alimwambia angeendelea kumwona kama rafiki, vinginevyo angemtolea nje mazima kabisa kwa kuwa sikuzote kama angechukia mtu, basi ilikuwa ni milele.

Akajiondokea hapo haraka na kwenda ofisini tena kujaribu kupiga kazi yoyote ili aondoe misongo kichwani. Kulipokuwa hakuna kazi alianza kucheza game la PS, akipoteza muda ili baadaye amfate Fetty na kumtoa out kama alivyomwahidi jana. Simu yake iliita mara nyingi sana, na mpigaji alikuwa ni Harleen. Dylan hakupokea hata mara moja, na baada ya muda Harleen akaacha kupiga. 

Huu ndio uliokuwa wakati mgumu kihisia kwake kwa mara ya kwanza tokea aliporudi nchini. Hakutaka kuendelea kuhisi kama ameshuka moyo, hivyo akaondoka hapo na kumfata Fetty kule mgahawani.


★★


Alifika mgahawani kwenye mida ya saa kumi na mbili jioni kukuta Fetty hayupo. Alipomuulizia, aliambiwa binti alikuwa ameondoka mapema leo baada ya kazi kuisha. Alitegemea angemkuta hapo kwa kuwa aliona mara nyingi Fetty hurudi nyumbani giza likiwa limeingia, lakini ndiyo akaambiwa huwa anakaa tu na wenzake hapo wakipiga story baada ya kazi kuisha kisha ndiyo anakwenda nyumbani. Lakini wakamwambia leo alipomaliza tu kazi aliwahi kuondoka, hivyo Dylan akarudi kwenye gari lake na kumpigia simu.

"Vipi?" Fetty akasema baada ya kupokea.

"Uko wapi wewe?" Dylan akauliza.

"Ghetto... wewe uko wapi?"

"Aah... si tulikubaliana nitakupitia, ama?"

"Nami si nilikwambia nitajiandaa vizuri? Ndiyo nimekuja kujiandaa, kwani uko wapi?"

"Unapofanyia kazi."

"Ai! Ahahahah... pole. Niko huku sasa," Fetty akasema.

"Haya, nakuja."

Akaondoka hapo mara moja na kuelekea kwa Fetty. 

Hii ilikuwa ni njia moja ya kumsaidia ili kutoikita akili yake kwenye mawazo kumwelekea Harleen. Alifika eneo la nje karibu na nyumba aliyopanga bibie, kisha akamwambia atoke. Fetty alitokea baada ya muda mfupi, na Dylan alipata kuona jinsi alivyokuwa amependeza kadiri alivyolikaribia gari. Alivaa gauni yenye kubana mwili, iliyokuwa na mtindo wa rangi ya pundamilia. Ilikuwa ni aina ya vazi la kawaida tu, na hakujiremba kupita kiasi kana kwamba anatoka na boyfriend wake, lakini Dylan alipendezwa sana na jinsi mwonekano wake ulivyomfanya avutie.

Fetty akaingia ndani ya gari na kumwangalia Dylan huku anatabasamu, naye Dylan akamsalimu, kisha akaondoa gari hapo na kuelekea mpaka kwenye hoteli nyingine tofauti na ile ya jana. Ilikuwa ya kifahari pia, naye Fetty akatania kwamba alihakikisha hajala siku hiyo, hivyo angekula hotelini hapo mpaka Dylan angeona aibu. Dylan akamwambia asiwaze kabisa, chochote kile alichotaka angefanya.

Walifika na kuanza kutembea kidogo kuzunguka hoteli ile, wakiangalia mambo kadhaa yaliyovutia sana hapo. Wengi waliokuwepo walikuwa watu wenye pesa sana, na wazungu pia. Hoteli hii ilikuwa mbali kidogo kutokea kule wawili hawa walipoishi, na mandhari na vitu vingi vya kisasa vilimfurahisha sana Fetty. Ijapokuwa urafiki wake na Dylan ulikuwa mpya, alihisi ni kama amemjua kwa muda mrefu, hivyo kwa kadiri fulani aliweza kujiachia akiwa naye.

Baada ya muda fulani, Dylan alimpeleka sehemu ambayo wangepata vyakula. Alimwagizia binti burger (yenye nyama, mboga majani kidogo, na viungo mbalimbali), chips, nyama ya kukaangwa, na kinywaji kizito cha cream na maziwa (milk shake). Vilikuwa mara mbili, yaani Dylan pia aliletewa vya aina hiyo hiyo, kisha wote wakaanza kula. Maongezi yao yalikuwa kuhusiana na mambo ya shule, na kumbukumbu nyingi za zamani zilifanya mazungumzo hayo yawe yenye kufurahisha sana.

"Kweli?" Fetty akauliza huku wakiendelea kula.

"Ndiyo. Haitachukua muda mrefu sana nitaufungua," Dylan akasema, akimaanisha mgahawa wake.

"Halafu unajua... nilisahau tu kuuliza... hivi unafanya kazi gani?" Fetty akamuuliza.

"Nina... sijui nielezeeje... ni kazi.... ya masuala ya ujenzi."

"Kwo' we' fundi mwashi?"

"Ahahahah... yeah unaweza ukasema hivyo."

"Mmm... usinidanganye bwana."

"Kwa nini unafikiri nakudanganya?"

"Jinsi tu ulivyo... unavyoongea, unavyovaa... gari lako... vitu vingi ni vya kifahari tu. Nisingetolewa out na fundi mwashi kwenye sehemu kama hii," Fetty akasema.

Dylan akacheka sana.

"Hivi unawaonaje mafundi? Wana hela hao!" Dylan akasema.

"Lakini ni mabahili mno."

"Kwa hiyo kumbe una experience nao eeh?" Dylan akatega.

"Hamna... marafiki zangu tu husimulia."

"Mmh... kwani ungekubali sasa hata kama ni kweli?"

"Wala, yaani me sinaga hizo kabisa. Tena nakwambiaje, yaani mimi nikijua tu mtu wa namna hiyo ananivizia-vizia nampiga chini faster... huwa sichelewi," Fetty akasema kwa uhakika.

"Kwa hiyo... tuseme siku moja unanikuta barabarani... niko kwenye mtaro napiga kazi huku nimepauka... halafu nikakusalimia, utaacha kuniitikia?" Dylan akauliza.

"Tena nakupita kama sikujui!" Fetty akajibu.

Dylan alicheka kwa furaha sana mpaka akasitisha kula. Fetty alikuwa akicheka pia huku anamwangalia jamaa kwa furaha.

"Dah aisee... itabidi nijipange," Dylan akasema baada ya kutulia.

"Kwa lipi?" Fetty akauliza.

"Kuhakikisha huji kunikuta hivyo siku moja."

"Kwani we' ni fundi mwashi kweli? Acha masihara bwana."

"Ahah... aam... ninafanya kazi kwenye kampuni ya baba yangu."

"Kampuni gani?"

"GJD Construction Company... iko huko tulikotoka sijui kama unaijua."

"Ile ambayo... jengo lake liko karibu na ile round about... ukiwa unaelekea Exim Bank?" Fetty akauliza.

"Eeh... upande wa kushoto kutokea huko..."

"Kushoto eeh..."

"Ndiyo, hapo hapo."

"Lile jengo ni kampuni ya baba yako?!" Fetty akauliza kimshangao.

"Ndiyo."

"Aisee... kumbe nimekaa na tajiri mkubwa hapa!"

"Ahahah... acha hizo bwana."

"Siyo poa. Ninatamani nije niione nyumba yenu siku moja, najua ina maghorofa kumi kama sikosei," Fetty akatania.

Dylan akacheka.

"Huwa unalala kwenye King size bed, au siyo?" Fetty akatania.

"Hamna wala. Huwa nalala chini," Dylan akasema.

"Chini?"

"Yeah."

"Hm? Hauna lolote wewe... yaani mna mihela halafu ulale chini?"

"Ahahah... najua ni ngumu kuamini, lakini ni kweli."

"Kwa hiyo unataka kuniambia huwa unalala chini kabisa?"

"Siyo chini kabisa. Sipendelei kulala kwenye kitanda. Huwa naweka godoro chini ndiyo nalala."

"Kwa nini sasa?"

"Huwa napenda tu. Tokea zamani sana... napenda mno kulala chini yaani najihisi comfortable."

"Mh... haya bwana tajiri. Kama mna pesa hivyo nataka kila siku uwe unaninunulia baga..."

"Ahah... halafu unanipa nini?" Dylan akauliza kimasihara.

Fetty alikuwa anatabasamu, lakini baada ya Dylan kusema hivyo tabasamu lake likafifia. Akamwangalia Dylan kwa sekunde kadhaa, huku jamaa akiendelea tu kula taratibu, na akimtazama Fetty kwa makini pia. Alijua bila shaka swali lake la kichokozi lilimkonga nyoyo mwanamke huyu.

Fetty akavunja utizami huo kisha akasema kwa sauti ya chini, "Nilikuwa natania tu."

"Hata me nilikuwa natania tu," Dylan akajibu pia.

"Ona... sitaki ufikiri kwamba labda niko hapa kwa sababu..." Fetty akashindwa kumalizia.

Dylan alipomwangalia vizuri, akatambua kuwa sura ya Fetty ilionyesha kama... amekwazika. Akagundua kuwa kwa njia fulani huenda maneno yake bila kutarajia yalimfanya binti ajihisi vibaya, ijapokuwa alikuwa anatania tu.

"Oh... no, no, no, Fetty... please usifikirie hivyo. Nina... nafurahia company yako sana. Jambo hilo halijaingia akilini mwangu kabisa, tafadhali niwie radhi kama nimekufanya ujihisi vibaya," Dylan akasema kwa upole.

"Sawa. Haina shida. Hata mimi... nafurahia company yako," Fetty akasema.

Dylan akatabasamu kisha akasema, "Sasa je! Mafundi mwashi hawaboi kama unavyofikiria."

Fetty akacheka kidogo na kusema, "Eti mafundi mwashi! Ni mafundi waashi."

"Wewe! Kiswahili cha wapi hicho?"

"Cha kitanzania... we' unachoongea sijui ni cha wapi..."

"Hakuna... ni mafundi mwashi... haina wingi..."

"Hamna... washa simu uangalie kamusi Google..."

"Na nikikuta niko sahihi?"

"Basi mimi ndiyo nitalipia hiki chakula chote."

Dylan akacheka.

"Na tukikuta hauko sahihi, utapaswa...."

Kabla Fetty hajamaliza kuongea simu yake iliita, na alipoitoa, akakuta ni mama yake ndiyo anapiga. Akamwambia Dylan atafute Google aone, kisha akapokea huku Dylan akiwa anamwangalia tu na tabasamu.

"Halloo... Mama, mama, nini... subiri sikuelewi, nini kimetokea?"

Dylan alianza kumwangalia kwa makini baada ya kutambua kulikuwa na tatizo upande wa mama yake.

Fetty akasimama ghafla na kuuliza kwa sauti ya juu, "NINI?!"

Dylan alishtushwa kiasi na jambo hilo. Yeye pia akasimama taratibu, huku sasa pumzi za Fetty zikianza kuongezeka kasi.


★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★

Previoua Next