Reader Settings

DYLAN

Story by Elton Tonny

Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

(R-rated 18+)

Enjoy!


★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA TISA

★★★★★★★★★★★


"Hospitali gani?" Fetty akauliza kwa presha.

Kisha akaishusha simu kutoka sikioni na kumwangalia Dylan usoni kwa hofu.

"Vipi Fetty?" Dylan akauliza kwa kujali.

"M..mdogo wangu... amegongwa na gari!" akasema huku akianza kulia.

Dylan akashangaa sana.

"Nahitaji kwenda Dylan... asante kwa kila kitu..." Fetty akasema huku akianza kuondoka.

"Subiri kwanza Fetty. Siwezi kukuacha uende mwenyewe, ninakuja nawe. Wamempeleka hospitali gani?" Dylan akamuuliza huku anamwita mhudumu kwa kiganja.

Baada ya Dylan kulipa pesa ya chakula ambacho hata hawakuwa wamemaliza, walianza kuondoka kutoka hapo upesi sana na kuingia kwenye gari, kisha kuanza safari huku Fetty akimwelekeza hospitali ilipokuwa. Binti alikuwa na wasiwasi sana, naye Dylan alijitahidi kuendesha kwa kasi ili waweze kuwahi kule. Ilikuwa sehemu ya mbali kiasi kwa kuwa iliwachukua dakika kama 30 kufika huko. Fetty alishuka upesi kutoka ndani ya gari na kukimbilia mule ndani ya hospitali, Dylan akimfuata kwa nyuma. 

Mwanadada huyu alimkuta mama yake, mvulana mwingine mdogo, mwanaume fulani mwenye umri mkubwa kidogo kumzidi Fetty, pamoja na kijana fulani wakiwa eneo la nje ya chumba cha matibabu. Mama yake Fetty alikuwa analia, na baada ya kumwona binti yake akazidi kulia na kumfata. Fetty akamkumbatia na kuanza kuuliza hali ya mdogo wake aliyegongwa na gari.

"Wamekataaaa... hh... wamekataaa..." mama yake akawa anasema huku analia.

"Wamekataa nini? Mama..." Fetty akasema kwa huzuni.

"Wanasema hawawezi kumfanyia matibabu kwa sababu hatuwezi kulipia!" yule mwanaume akamtaarifu.

"Nini?! Yaani... wamesema... kwa hiyo Sophia... Sophia wamemwacha tu?!" Fetty akauliza huku analia.

"Eee..."  mwanaume huyo akajibu.

"Ameumia vibaya sana Fatuma... wanataka hela ili kulipia mambo yatakayohitajika kumtibia... na ni hela nyingi sisi hatuna... aaahahaaaa.... nitafanyaje mama anguu mimi... Sophia atakufaaa!" mama yake akaendelea kulia kwa uchungu mwingi.

Fetty alichanganyikiwa. Hakujua afanye nini, kwa sababu hakutegemea jambo hili hata kidogo la sivyo angekuja hata na hela kidogo alizotunza. Dylan alikuwa pembeni anasikia kila kitu, na hapo hapo akaja daktari na muuguzi mmoja. Mama yake Fetty akawafata na kuanza kulia sana akiwaomba wamsaidie ili binti yake asipatwe na madhara, lakini daktari huyo akasisitiza kwamba ni LAZIMA Sophia alipiwe KWANZA ndiyo apewe matibabu.

Dylan alimshangaa. Alijiuliza ikiwa hapo palikuwa ni hospitali kweli au kituo cha biashara! Yaani kuna msichana ambaye bila shaka alikuwa mdogo sana hapo na alikuwa anapambania maisha yake, lakini hawa watu walichojali ilikuwa pesa tu. Akamfata daktari huyo na kumgeuza ili amtazame.

"Nisikilize. Ninataka madaktari wote waliopo hapa waje kumhudumia huyo msichana kimatibabu haraka. Sasa hivi!" Dylan akatoa amri.

Wote waliokuwepo hapo walimshangaa. Daktari akamwangalia kwa njia ya kujiuliza ni nani huyo, naye Dylan akamtazama muuguzi.

"Nenda kawaite wote wanaohitajika hapa na waje na madude yao yote ya kumsaidia, haraka sana. Pesa yote nalipia mimi," akasema kwa uhakika.

Muuguzi akabaki kumwangalia tu kama kachanganyikiwa.

"Harakisha!" Dylan akafoka.

Muuguzi huyo akatoka hapo haraka na kwenda kufanya alivyoagizwa. Daktari huyo akashusha pumzi kisha kwenda upesi kwenye chumba alichokuwepo Sophia, mdogo wake Fetty. Mama yake Fetty alimtazama sana Dylan kwa matumaini, naye akamsogelea na kuanza kumshukuru sana kwa jambo hilo, ijapokuwa hakumfahamu. Dylan alimwonea huruma sana mama huyo, kwa kuwa alilia kwa njia iliyomfanya kijana ahisi simanzi nzito ndani yake. 

Sekunde chache tu, madaktari wawili na wauguzi kadhaa wakapita hapo kuelekea kile chumba, wakiwa wamebeba vifaa mbalimbali vya kimatibabu. Fetty alikuwa analia bado huku anamwangalia sana Dylan, na mama yake akawa amemkumbatia yule mvulana mdogo huku anasali ili Mungu asaidie binti yake awe salama.

Hospitali hii haikuwa kubwa, hivyo Dylan alijua wazi matibabu ya hapo yangekuwa na kikomo fulani, kwa hiyo ingekuwa muhimu binti huyo akipelekwa kwenye hospitali kubwa ili apate matibabu mazuri zaidi. Lakini kwa kuwa alihitaji uangalizi fulani baada ya kuachwa tu muda wote huo, Dylan aliona ni sawa wakimshughulikia kwanza, ili akiwa kwenye uafadhali kutoka hatarini, basi wamwamishe. Dylan akatoka hapo ili kwenda sehemu ya malipo, naye Fetty akamfata. 

Walipofika kule, waliuliza gharama iliyohitajiwa, na baada ya mahesabu kupigwa ya kila jambo lililohitajiwa, wakasema ni kwenye laki nne. Fetty aliona ni kama walikuwa wanafanya wizi, lakini hangeweza kusema lolote na kubaki kumtazama tu Dylan. Mwanaume akatoa wallet yake na kuchomoa kadi ndogo ya benki, kisha akampatia mhusika wa malipo na kusema atoe laki tano kamili. 

Baada ya kukamilisha hilo, akachukua kadi yake na kumwangalia Fetty, ambaye alikuwa anamtazama sana machoni. Binti akaanza kumshukuru mno na kumwambia angefanya yote awezayo kumlipa siku moja, lakini Dylan akakanusha na kumwambia hakuhitaji kufanya hivyo, maana alitoa msaada si kwa kutarajia malipo. Ndipo wote wakarejea kwa wengine kule walikowaacha, na baada ya Fetty kumwambia mama yake kwamba Dylan alilipia, mama huyo akaanza kumshukuru mwanaume huku akilia. Dylan akamtuliza kwa kumkumbatia, kitu ambacho kiliufariji sana moyo wa Fetty. 


★★


Waliendelea kukaa hapo mpaka inafika saa sita usiku. Mama yake Fetty alikuwa amewasimulia kilichompata Sophia. Binti huyo, alikuwa ameagizwa na mama yake kufata mzigo fulani kwa rafiki yake kwenye mida ya saa tatu, ndipo akapigiwa simu baadaye na kuambiwa binti yake aligongwa na gari. Kwa hiyo kwa kiasi kikubwa mama huyo alijilaumu kwamba ni makosa yake bintiye kugongwa kwa kuwa ni yeye ndiye aliyemtuma, lakini Fetty na yule mwanaume mwingine wakawa wakimwambia asijilaumu na kumtia moyo kwamba Sophia angekuwa sawa. 

Wauguzi walitoka na kuingia mara kwa mara kwenye chumba hicho bila kusema lolote kuhusu hali ya binti, kisha baadaye madaktari watatu wakatoka pia.

"Dokta, dokta, mwanangu anaendeleaje?" mama yake Fetty akauliza baada ya kuwafata.

Daktari mmoja akaondoka, akiwaacha wawili hapo; mmojawapo akiwa ni yule wa kwanza kabisa kufika.

"Tumejitahidi kuzuia damu zisiendelee kuvuja na tumeziwekea mihogo sehemu za shingo na mguu wake mmoja kwa kuwa zimevunjika. Bado amepoteza fahamu lakini tutaendelea kumwangalia ili kuhaki...."

"Nani anamwangalia sasa hivi wakati wauguzi wote wameondoka?" Dylan akamkatisha daktari huyo kwa uthabiti.

Madaktari hao wakamwangalia kwa hisia kali.

"Huyu ndiyo aliyekuwa anafoka hapa?" daktari yule wa pili kuingia kwenye chumba cha Sophia akamuuliza mwenzake kwa kiburi.

"Siyo kufoka... mlichokuwa mnafanya hakikuwa sahihi," Dylan akamwambia.

"Kijana nisikilize. Hii ni hospitali na ina sheria zake. Hautakiwi kuongea vitu usivyovijua. Bila sisi unajua huyo binti hangekuwa salama..."

"Nyie mlichokuwa mnajali si ni pesa tu? Inamaanisha mngemwacha tu mpaka akafa!" Fetty akasema kwa hisia za huzuni.

"Fatuma usiongee hivyo..." yule mwanaume akamwambia.

"Haujui mambo vizuri dada. Sehemu hii ina sheria zake za kufata kama sehemu zingine, na ni lazima tuzifate tu. Kama hamjui, ni kwamba mgonjwa hawezi kuhudumiwa ikiwa hawezi kulipia. Hilo ni jambo halali hata kisheria... kwa hiyo hakuna njia yoyote ya kuweza kutulaumu hata kama nini kingetokea," daktari akasema.

"Nyie ndiyo mnaokosea! Sheria za wapi hizo zinazowaruhusu mmwangalie tu mtu aliye hatarini eti kisa hawezi kulipia?" Dylan akauliza.

"Ni mambo ambayo sisi tumebobea... wewe huwezi kuelewa. Kwa kuwa umeshatoa hela endeleeni kusubiria tu, sisi ndiyo tunaojua mambo vizuri zaidi ya NYINYI," daktari yule mwenye kiburi akasema.

"Wewe ndiyo unajifanya unajua sana lakini hujui lolote!" Dylan akamwambia kwa uthabiti.

"Basi jamani, inatosha. Haina haja ya kulaumiana," mama yake Fetty akawaomba.

"Kwa hiyo we' ndiyo unajua sana sheria za hospitali? Hebu nielezee..." daktari huyo akamwambia Dylan.

"Najua ndiyo kwamba huwa inahitajika hospitali na madaktari wapewe malipo mgonjwa anapohitaji huduma, na mnaruhusiwa kukataa kutoa huduma ikiwa mgonjwa hawezi kulipa. Lakini hamruhusiwi kukataa IKIWA kufanya hivyo kutamsababishia madhara makubwa," Dylan akawaambia.

"Ndiyo unavyojidanganya?" daktari huyo akamwambia Dylan.

"Wewe ndiyo unajidanganya. Madaktari wanatakiwa wawe watu wanaohangaikia hali za wanaoumia siyo tu kwa sababu ya kupata pesa, bali kwa sababu wanawajali. Unapotambua kwamba mtu ana UTI mbaya sana kwa mfano, halafu ukakataa kumsaidia... ni lazima utawajibika kisheria ikiwa tatizo hilo litaongezeka na kuidhuru figo yake. Huyu hakuwa mgonjwa, alikuwa amejeruhiwa vibaya ghafla sana. Mnakosa hata ubinadamu kweli? Ikitokea huyu msichana akapatwa na madhara kwa sababu ya ujinga huu ninawaahidi lazima nitawafungulia kesi kwa sababu mnafanya medical malpractice kwa kisingizio kisicho na kichwa wala miguu." 

Dylan aliongea yote hayo kwa mkazo sana. Wote walikuwa wakimwangalia kwa makini, hata madaktari wakabaki kumtazama tu kwa kushangaa jinsi alivyosema mambo kwa uhakika. Baadhi ya watu wachache walikuwa wamesogea hapo kuangalia malumbano hayo, hivyo Dylan akaondoka ili asije akatenda kwa njia ambayo isingependeza. Fetty alimwangalia kwa hisia sana hadi alipoishia kwenye kona na kutokomea.

"Huyo mwanaume anajiona yeye ni nani?" daktari akawauliza waliobaki hapo.

Fetty akamwangalia tu, kisha akaondoka ili amfate Dylan. Alimtafuta huku na kule bila kumwona, kisha akaamua kutoka hadi nje na kumkuta akiwa amesimama pembeni ya gari lake; akionekana kuongea na mtu fulani kwenye simu. Fetty akamwangalia sana kwa sekunde kadhaa hadi alipomaliza kuongea na simu, naye akamfata pale alipokuwa amesimama.

"Dylan..." akaita baada ya kumkaribia.

"Fetty..." Dylan akasema baada ya kumwona.

Fetty akasogea karibu yake na kumtazama tu.

Dylan akashusha pumzi na kusema, "Samahani Fetty... sija... sijatenda kwa njia nzuri mule ndani."

"Acha masihara basi! Yaani isingekuwa wewe kuwaambia ukweli mimi hata ningepigana nao kabisa," Fetty akasema.

"Ahahah... kweli?"

"Ndiyo. Wamezidi sana kutuonea yaani... kwa sababu tu hatuna hela wanatutendea kama hatufai. Kuna kipindi mmama mmoja jirani yetu, mwanaye aliumwa sana. Akamleta akiwa amembeba mgongoni akiwaomba wamsaidie lakini wakawa tu wanamweka pembeni. Kakaa kusubiri analia, analia, analilia msaada... wapi. Mtoto wake akafa akiwa mgongoni kwake!" Fetty akasema kwa huzuni.

Dylan alitikisa kichwa kwa kutoamini kabisa. Hakuelewa watu hawa walikuwa na mafunzo ya aina gani ya kutoa huduma kwa wagonjwa, lakini ni wazi watu wengi waliumizwa na vitendo hivyo. 

"Dylan, ninaomba nikushukuru tena kwa kutusaidia. Ninakuahidi, nitajitahidi...."

Dylan akamkatisha kwa kuweka kidole mdomoni mwake. 

Fetty akabaki kumwangalia tu usoni.

"Na mimi ninakuomba usije kurudia tena kusema utanilipa. La sivyo sitakusemesha milele," Dylan akamtania kidogo.

Fetty akatabasamu kwa kufarijika, naye Dylan akamkumbatia. Kumbatio hili lilikuwa la faraja kutoka kwa Dylan, kwa maana yeye alizoea sana vitu kama hivi vya wazungu-wazungu kwa sababu ya kuishi muda mrefu Brazil. Lakini kwa Fetty, liliamsha hisia fulani kumwelekea Dylan ambazo kwa kiasi fulani alikuwa akijaribu kupingana nazo, ila ni kama zikawa zinakita mizizi tu. 

Baada ya kumwachia, wakarudi ndani pia, kukuta mama yake na yule mvulana mdogo wamekaa huku wakisinzia. Yule mwanaume aliyekuwa hapo, akamwambia Fetty kwamba alihitaji kurudi nyumbani, na angekuja kesho kuangalia hali ya Sophia. Akaondoka pamoja na yule kijana mwingine, na ni hapa ndipo Fetty akamjulisha Dylan kwamba huyo mwanaume alikuwa mdogo wa mama yake, yaani mjomba wake Fetty, na yule kijana alikuwa ni mtoto wa rafiki yake aliyekuwa akiishi kwake. Mvulana yule mdogo aliyekuwa amelala hapo pamoja na mama yake ni mdogo wake Fetty pia, aliyeitwa Japhet. Dylan akapendekeza kwamba itafaa kama akiwapeleka nyumbani mama yake na mdogo wake, halafu yeye na Fetty wakae hapo hospitali mpaka asubuhi.

Wakawaamsha, na ijapokuwa mwanzoni mama yake aliweka kipingamizi cha kutotaka kurudi nyumbani, Fetty alimshawishi kwa kumwambia alihitajika kuwa na Japhet nyumbani pia kwa kuwa ni mdogo, hivyo yeye angebaki kumwangalia Sophia ili wenyewe wakapumzike. Baada ya kukubali, Dylan akambeba Japhet na kutangulia naye nje, na ni hapa ndipo mama yake Fetty akamuuliza binti yake Dylan alikuwa ni nani hasa. Fetty akamweleza ni rafiki yake tu mzuri na mkarimu sana, na baada ya hapo wakaenda nje pia mpaka kwenye gari la mwanaume. 


★★


Fetty yeye alibaki hospitalini, kwa hiyo Dylan alifanikisha kuwapeleka mama yake binti na mtoto nyumbani kwa kuelekezwa na mama huyo. Hapakuwa mbali mno, mwendo wa dakika kama saba hivi ulitosha kuwafikisha, kisha Dylan akarejea hospitalini tena; ikiwa ni saa saba usiku sasa. Alimkuta binti akiwa ameketi tu kwenye benchi, naye akaenda kukaa pamoja naye. Aliuliza kama kulikuwa na jipya, naye binti akakanusha. 

"Uko sawa Fetty?" Dylan akauliza kwa kujali.

"Ndiyo. Niko sawa," Fetty akajibu kwa hisia.

Dylan akatulia kidogo na kuuliza, "Sophia ana miaka mingapi?"

"Kumi na nane."

"Anasoma?"

"Amemaliza kidato cha nne. Amefaulu vizuri unajua... ndiyo najitahidi kumtunzia ili aendelee... lakini sikuzote maisha yana njia ya kunifanya nivunjike tu moyo," Fetty akasema huku machozi yakianza kumtoka.

Dylan akaanza kuusugua-sugua mgongo wake kwa njia ya kubembeleza.

"Baba yetu alikufa nilipokuwa naingia chuo... siyo kikuu... nilikuwa tu nimemaliza form four nikaona niende chuo kwa kuwa sikutaka kupita kule juu kote... niliona mizunguko ingekuwa mingi. Yeye ndiyo alikuwa ananilipia... kwa hiyo kifo chake kilifanya isiwezekane kuanza. Lakini mama, na kazi yake ya ushonaji, alijitahidi kutusaidia sisi wote watatu tuendelee na elimu... na mimi nikawa nafanya shughuli ndogo ndogo nilipopata nafasi. Baadaye nikaanza chuo... nika... nilipenda sana sheria... nikasoma kwa miezi michache, ndipo tukagundua mama'angu ana shida fulani... kiafya..." 

Yote haya Fetty aliyasimulia huku analia kwa kujikaza sana, naye Dylan akawa anamtazama kwa simanzi kadiri binti alivyoendelea kufunguka.

"... hhh... alihitaji kutibiwa... na pesa haikutosha... hata zile ndogo ndogo nilizopata hazikufikia kiwango kilichohitajiwa. Kwa hiyo ikabidi niachane tu na chuo... nikaanza kufanya kazi... za ndani. Karibu kila sehemu niliyofanya, walioniajiri walinitaka kimapenzi... nami nilijua wazi wangenitumia tu Dylan... sikuwa na akili chafu ya kutaka kukubali vitu hivyo... kwa hiyo ilikuwa ni kutoka hapa, kufukuzwa, kwenda hapa, kwenda kule, kufukuzwa... ahhh...."

Akainamisha uso wake na kuufunika kwa viganja vyake. Dylan akaanza kuzilaza-laza nywele zake kwa wororo ili kumbembeleza. Kisha taratibu Fetty akaunyanyua uso wake na kutazama mbele.

"Nimejitahidi sana. Mambo mengi yalikuwa yanakatisha tamaa lakini nilijua sikupaswa kufanya hivyo. Familia yangu ilinihitaji sasa, kwa hiyo nilijua lazima nifanye yote kujitoa kwao... lakini siyo kwa njia za mkato. Angalau nilikuja kupata kazi kama hii niliyonayo sasa, nikatunza na kumsaidia mama... na wadogo zangu pia. Kwa hiyo... kwa muda fulani niliona niliweke suala la chuo pembeni ili... niitegemeze familia yangu pia. Ndugu zetu wa ukoo hawakujali kuhusu afya ya mama hata kidogo, ukitoa huyu mjomba wangu, angalau ni yeye tu ndiye aliyetusaidia mpaka kuhakikisha tunamsaidia mama... yaani Dylan wakati mwingine nahisi kushindwa sana... sana. Nina miaka ishirini na tano sa' hivi, na kilichopo akilini mwangu ni hali nzuri tu ya familia yangu... basi. Mdogo wangu huyu... I wanted her to have a bright future... and she's so intelligent... nini hiki sasa? Ah..."

Fetty aliongea kwa simanzi nzito mno mpaka Dylan akadondosha chozi. Dylan hakuwa mzuri sana wa maneno ya kufariji, hivyo akazungushia tu mkono wake mpaka kwenye bega la Fetty na kumvutia kwake, naye Fetty akalaza kichwa chake kwenye sehemu ya juu ya kifua cha mwanaume, akiruhusu amfariji kwa njia hiyo kwa muda mrefu hapo. 

Mpaka asubuhi inafika wawili hawa hawakusinzia hata kidogo. Dylan alikuwa ametafutwa mara kadhaa na Jaquelin, aliyeuliza kijana wake huyo alikokuwa, naye Dylan akasema tu alilala kwenye ile nyumba yake nyingine. Alimwambia huenda angechelewa kufika kazini, hivyo mambo ambayo angehitajika kushughulika nayo angeyafanya baadaye. 

Ilipofika mida ya saa mbili asubuhi, madaktari walikuja kumwangalia Sophia, kisha wakawataarifu wawili hao kuwa inaonekana matibabu waliyompa jana yamesaidia kwa kuwa alionekana kutoka kwenye hatari. Dylan akawauliza ikiwa itakuwa sawa kumtoa hapo na kumpeleka kwenye hospitali nyingine, na wote wakamshangaa kwa kiasi fulani. Walijibu kuwa ndiyo inawezekana, lakini mpaka apelekwe kwa kutumia ambulance, na hata kabla hawajamaliza kuelezea, Dylan akatoka tu nje upesi. 

Madaktari walimwona Dylan kama mtu fulani mwenye kujisikia sana, lakini kihalisi hilo halikuwa kweli. Alitoka na kumpigia simu Harleen. Alimweleza kwamba alihitaji msaada wake kwa kuwa rafiki yake alikuwa ameumia, hivyo angetaka apatiwe uangalizi bora kwenye hospitali kubwa kama aliyofanyia kazi Harleen. Harleen akakubali na kumwambia afanye mpango ili ampeleke huko haraka, hivyo bila kuchelewa akaenda sehemu ambayo angefanya mipango ya kuchukua ambulance ili wamtoe Sophia pale haraka.

Baada ya kurudi chumbani kwa Sophia, alimkuta Fetty humo na kumwambia kila kitu alichofanya, akimwacha binti anashangaa. Fetty alihofia gharama, lakini Dylan akamwambia asiwaze kabisa kuhusu hilo. Hivyo ikabidi Fetty ampigie mama yake ili kumjulisha yaliyojiri, na mama huyo akamwambia Fetty amshukuru sana Dylan kwa niaba yake. 

Muda fulani baadaye, Sophia alipelekwa taratibu mpaka kwenye ambulance ili safari ianze kuelekea hospitali kuu ya jiji. Wakati huu mama yake alikuwepo pia, naye alikuwa amewaambia kwamba alimwomba mdogo wake yule mwanaume awe kwake pamoja na Japhet kwa muda ambao angekwenda pamoja na Sophia kule hospitali kuu.


★★★


Zilipita siku tano baada ya Sophia kuhamishwa kutoka kwenye hospitali ile, na bado alikuwa kwenye usingizi wa kupoteza fahamu (coma). Kwenye hospitali hii kulikuwa na madaktari wenye uzoefu wa hali ya juu, dawa za kila aina na vifaa vingi vyenye ubora, hivyo binti alihudumiwa vizuri sana. 

Sophia alilazwa kwenye chumba cha peke yake ghorofa ya tano ya jengo la hospitali hii, na ni Dylan ndiye aliyekuwa akilipia matibabu ya msichana huyo hapo hospitalini. Mama yake alikuja kila siku kwa usafiri ambao ni Dylan aligharamia nauli pia, ili aje kumwona binti yake na kurudi nyumbani pia wakati ambao angehitaji kuwa pamoja na Japhet. Ratiba ya Fetty ilimruhusu kwenda hospitalini kwenye mida ya saa kumi na mbili au saa moja jioni pindi ambapo angemaliza kazi, hivyo ni muda huo ndiyo mama yake angerudi kule nyumbani kwake.

Mama yake Fetty alitaka sana kujua ikiwa Fetty alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na Dylan, kwa kuwa aliona msaada huo wote ambao kijana huyu aliwapatia haukuwa bure. Mara zote Fetty alimhakikishia kwamba wao ni marafiki tu, tena wamejuana kipindi cha karibuni tu. Mama yake alipendezwa sana na Dylan, hivyo alikuwa akimshawishi Fetty amzuzue jamaa (seduce) ili waweze kuwa pamoja, lakini Fetty hakuafikiana na wazo hilo. Hakutaka kufanya hali hii ionekane kama alitakiwa kujitoa namna hiyo kwa Dylan kwa sababu tu amemsaidia; aliona ingekuwa ni kama anajiuza kwake. Mama yake alikuwa mwenye nia nzuri tu, lakini bado binti akayapiga chini matarajio yake.

Dylan alikuwa akija pia kila jioni kumwona. Mara kwa mara alikutana na Harleen hapo, nao wangetazamana sana kisha Dylan angempa tu tabasamu na kuelekea upande mwingine. Bado roho ilimuuma sana Harleen, na mpaka wakati huu hakuwa ameachana na Alex, kwa sababu kihalisi alimpenda. Lakini tatizo lilikuwa kwamba alimpenda Dylan pia, hivyo hakujua jinsi ya kupima uzito wa upendo wake kwa wanaume hawa, na ni hicho ndicho kilichomfanya apoteze amani ya moyo kabisa.

Jioni hii sasa Dylan alipokuja hapo hospitali kwenye mida ya saa moja, alimkuta mama yake Fetty akiwa mwenyewe kwenye chumba cha Sophia. Mara zote alipofika alikuta Fetty tayari yupo, lakini leo haikuwa hivyo. Akamuuliza mama yake kama amewasiliana naye, lakini akamjibu kuwa amempigia sana simu ila binti yake huyo hakupokea hata mara moja. Dylan pia akampigia, lakini hakupokea simu yake pia. Akapiga simu kwa rafiki yake kumuuliza kama bado wako kazini, lakini akamjulisha kwamba Fetty aliondoka mapema tu ili awahi nyumbani kujiandaa kwenda hospitalini. Hivyo Dylan akamwambia mama yake Fetty kuwa angemfata binti yake kule kule ili arudi pamoja naye upesi.

Alifika nje ya ile nyumba alikopanga Fetty, naye akaelekea moja kwa moja mpaka mule ndani akitumaini angemkuta. Kulikuwa na vyumba kadhaa vilivyopangiliwa kwa mzunguko, naye akapata kumwona mwanamke fulani hapo nje akiwa ameketi huku anakuna nazi. Akamsogelea na kumsalimu, kisha akauliza chumba cha Fetty kilikuwa ni kipi, na kama Fetty alikuwepo. Mwanamke huyo akakubali kwamba yupo, na baada ya kumwonyesha Dylan chumba hicho kilipokuwa, akakifata na kukuta mlango uko wazi kidogo. Akamwita Fetty huku anausukuma mlango na kuingia, na hapo akasimama kwa kutotarajia alichokikuta.

Fetty alikuwa amesimama huku akimtazama, na kulikuwa na mwanaume mwingine mweusi na mrefu humo akimtazama pia, bila shaka wote wakiwa wameshtushwa na Dylan baada ya yeye kuingia tu humo ndani. Ilionekana ni kama walikuwa na maongezi, naye Dylan akajisikia vibaya kiasi kwa sababu aliingilia ubinafsi wa watu. Akatambua haikuwa adabu hata kidogo.

"Oh... samahani jamani. Ngoja nisubiri hapa nje..." Dylan akasema.

Fetty akamfata na kumshika mkono ili asiende nje.

"Haina haja... tumeshamaliza kuongea," Fetty akasema.

"Huyu ni nani?" mwanamume huyo akauliza.

"Ni rafiki yangu, anaitwa Dylan. Dylan... huyu ni Sam," Fetty akawatambulisha.

"Vipi kaka?" Dylan akamsalimu jamaa.

"Aaaa... kwo' kumbe ni huyu ndiyo anafanya unanitendea hivi, eti?" Sam akasema kiukali huku akianza kumwelekea Dylan.

Dylan akashangaa.

"Sam, Sam... siyo hivyo. Huyu ni rafiki yangu. Agh... me sitaki hayo mambo bwana, unajua sipendi," Fetty akasema kwa hisia kali.

"Kama umeshaanza kubemendwa na mtu mwingine si useme tu? Unanizingua kisa nini sasa?" Sam akasema kwa hisia.

"Sam nakuomba uende... tutaongea wakati mwingine, nimeshakwambia nataka kwenda hospitalini, mbona huelewi?" Fetty akamwambia.

Dylan alikuwa ameachwa njia panda kwa kuwa hakuelewa nini kinaendelea, lakini kwa akili ya haraka akatambua mwanaume huyo bila shaka alikuwa na uhusiano wa kimapenzi pamoja na Fetty. Sam akamwangalia Fetty kwa mkazo sana, kisha akampita na kumpamia Dylan kimakusudi kabla ya kutoka nje na kuondoka. Dylan akatikisa kichwa chake huku akicheka kidogo kwa kutoamini, kisha akamwangalia Fetty, ambaye alionekana kutangatanga sana kiakili.

"Hivi ni kwa nini sikuzote wanawake wazuri lazima muwe na watu wenye akili kama za yule mwigizaji Zimwi?" Dylan akatania.

Bado Fetty alionyesha kutangatanga sana, hivyo, kwa huruma Dylan akamfata na kumkumbatia ili kumtuliza. Fetty alijibana kwenye mwili wa Dylan akijihisi vizuri sana kuonyeshwa na Dylan kwamba alimjali, huku pia bado akiwa na huzuni kwa sababu ya mambo yaliyotokea kati yake na Sam, naye Dylan akaendelea kumpa mwanamke huyu kumbatio hilo la faraja.


★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next