DYLAN
Story by Elton Tonny
Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa
(R-rated 18+)
Enjoy!
★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KUMI
★★★★★★★★★★★
"Najua mambo ni mengi, lakini tunahitaji kwenda hospitalini... mama anasubiri," Dylan akasema kwa upole huku akiwa bado amemkumbatia Fetty.
Kisha akamwachia na kumwambia angemsubiri nje ili avae nguo alizohitaji kuvaa. Baada ya kubadili nguo, Fetty akaenda pamoja na Dylan kwenye gari na kuelekea mpaka hospitali. Njia nzima ni kama Dylan alikuwa anaongea mwenyewe, kwa kuwa Fetty alijibu kifupi tu au kuwa kimya mpaka ikabidi Dylan akaushe tu.
Walipofika kwenye chumba alicholazwa Sophia, mama yake Fetty alimuuliza kwa nini hakuwa akipokea simu wakati anampigia, naye binti akajibu kuwa aliiacha kwa jirani ili ipate chaji kwa kuwa umeme kwenye nyumba yao ulikuwa umeisha. Baada ya hapo mama yake akaondoka, akiwaacha wawili hao kwenye chumba hicho. Fetty aliketi kwenye kiti kidogo pembeni huku sura yake ikiwa bado inaonyesha ana huzuni.
"Ulikula?" Dylan akaanzisha maongezi.
"Ndiyo. Nimekula," Fetty akajibu bila kumwangalia.
"Hey mbona hivyo? Usinitendee kama boyfriend wako yule," Dylan akasema kimasihara.
Fetty akamwangalia, kisha akasema, "Samahani Dylan. Nimepatwa na stress tu basi, ila siyo kwamba..."
"Fetty relax. Natania tu," Dylan akamtuliza.
Fetty akashusha pumzi na kuangalia chini.
"Sam umekuwa naye kwa muda gani?" Dylan akauliza.
Fetty akamtazama tu bila kutoa jibu.
"Haina haja ya kubeba mzigo huu mwenyewe. Mimi ni rafiki yako, tambua niko hapa kwa ajili yako," Dylan akasema kwa upole.
"Samwel ni... nilikuwa natoka naye kimapenzi, lakini..." akashindwa kuendelea.
"Kwa hiyo mliachana au?" Dylan akauliza.
"Aa... hapana. Ni muda mrefu sana yaani... baada ya muda unajua tu kwamba unahitaji kukua... nilihitaji muda wa kuwa mwenyewe... nafasi ya kuyajenga maisha yangu..."
"Okay, okay, nimeelewa. Ulihitaji muda wa kuyajenga maisha yako hivyo mahusiano ukaona uyaweke pembeni... lakini ukashindwa kumwambia jamaa hivyo," Dylan akasema.
"Siyo kushindwa Dylan, yaani... nilimwambia kabisa kuwa ninahitaji muda, sema... aahh jamani..." Fetty akaongea kwa kuvunjika moyo.
"Inaeleweka. Lakini, bado siyo fresh kumzungusha. Kama utaendelea naye mwambie, kama huwezi tena... sema. Ukifanya hivyo unakuwa unamwonea kwa kiasi fulani na bichwa lake lile," Dylan akasema.
Fetty akacheka kidogo na kumwangalia usoni. Dylan akatabasamu kidogo baada ya kumwona binti ameonyesha itikio zuri. Mrembo alijua alichosema Dylan kilikuwa sahihi na alihitaji afanye uamuzi haraka, kwa kuwa Sam alikuwa akisubiri kwa muda mrefu sana.
"Kesho nafungua rasmi restaurant yangu," Dylan akamwambia.
"Kweli?" Fetty akauliza kwa shauku.
"Ndiyo."
"Eh, hongera. Uliniambia utaiitaje kweli?"
"Dy-Foods."
"Dah, haya bwana. Kwa hiyo kesho kutakuwa na pilau ya sherehe?"
"Pilau ya nini? Nafungua ili watu waanze kazi, siyo wacheze dansi."
"Umeshaweka na watu tayari? Umewaajiri lini wakati hujaufungua bado?" Fetty akauliza.
Dylan alianza kumwelezea jinsi alivyopangilia mambo mengi vizuri kwenye suala la mgahawa wake mpya. Fetty alipendezwa sana na werevu mwingi wa Dylan. Akatambua pia kwamba Dylan hakuwa aina ya mtu mwenye pesa anayejivuna sana, bali alikuwa mwenye usawaziko na mkarimu, ijapokuwa alikuwa mwenye utundu mwingi mno. Fetty akaahidi angekwenda kuuona wakati ambao angepata nafasi. Wakaendelea kupata maongezi huku wakimwangalia Sophia, na baada ya muda Dylan akaondoka.
★★★
Upande wa Mr. Bernard, mipango yake pamoja na yule mtu mwingine ya kumwangusha Gilbert ilikuwa nyendoni. Mr. Bernard alikuwa mtu wa kutekeleza tu kile alichoambiwa na mtu huyo, kwa sababu yeye hakuwa mwanaume mwenye subira sana. Lakini mtu huyo alikuwa amemwambia wasubirie wakati mwafaka ili waweze kupiga hatua yao kwa umakini wa hali ya juu, na sasa wakati huo ukawa umewadia. Walichokuwa wanasubiri tu, ni ndege wao kuingia mtegoni, halafu wao waufyatue.
★★★
Ilikuwa ni furaha kubwa sana upande wa Fetty, kwa kuwa sasa Sophia alikuwa amerejesha fahamu tena! Binti huyo aliamka siku mbili kutokea usiku ule ambao Dylan alikutana na boyfriend wa Fetty, Samwel. Baada ya kupata taarifa, Dylan alikwenda hospitali upesi siku hiyo kumwangalia. Alimkuta mama yake Fetty pamoja na Fetty pia, nao wakamwambia Sophia kwamba wa kumshukuru kwa matibabu yake ni Dylan. Lakini Dylan hakutaka kuelekezewa sana fikira, na kwa busara akasema tu kwamba alisaidia kama mama na dada yake walivyosaidia pia.
Sofia alikuwa amewekewa kifaa cha kuizuia shingo yake isishtuke, kwa kuwa ilihitaji muda mrefu wa kukaa usawa mmoja ili kupona, hivyo hangeweza kuigeuza. Mguu wake mmoja ulikuwa umevunjika kwa ndani na hivyo kuwekewa vifaa vya kuusaidia unyooke tena; ukizibwa kwa muhogo mnene sana kuanzia kwenye goti mpaka nyayoni. Hakuweza kutoa sauti vizuri, hivyo Dylan akampa njia ya kuwasiliana kwa kumwambia atumie macho kujibu walipomsemesha; mfano kama akikubali kitu, anafumba na kufumbua, lakini akikataa, asifumbe macho hata kidogo.
Baada ya muda fulani, mama yake Fetty akasema kwamba Japhet, aliyekuwa kule nyumbani kwao, aliomba sana aje huku kumsalimia dada yake baada ya mama yake kumwambia ameamka, hivyo mama Fetty akasema angeondoka ili kumfata. Lakini Dylan akamwambia haikuwa na haja ya kwenda, bali yeye mwenyewe angemfata ili mama huyu awe na binti yake hapo. Fetty akasema angekwenda pamoja naye pia, hivyo wakaondoka na kuanza kuelekea nyumbani huko.
Kufikia sasa Dylan alikuwa ameshaufungua rasmi mgahawa wake wa Dy-Foods, na ulikuwa wa kisasa zaidi wenye kuvutia wengi. Ijapokuwa mwonekano wa mgahawa huo ulikuwa wa kifahari kwa kadiri fulani, hiyo haikumaanisha kwamba ulikuwa kwa ajili ya wenye pesa tu, kwa kuwa watu wote walikaribishwa pale. Alikuwa ameajiri wahudumu sita, wapishi wanne, na mwanaume fulani aliyeitwa Tony ambaye alikuwa kama msimamizi hapo (manager). Alikuwa anataka kuajiri mtu mwingine awe ndiyo msimamizi msaidizi (assistant manager) hapo, na wa kwanza kwenye akili yake hakuwa mwingine ila Fetty.
Dylan alijua Fetty alikuwa na uzoefu pia kwenye masuala ya migahawa, hivyo bila shaka jambo hilo lingemsaidia, kama Fetty alivyosema kipindi kile, kuyajenga vizuri maisha yake. Hakuwa mwanamke aliyetaka vitu maishani kwa njia ya mkato, bali kuvifanyia kazi, kwa hiyo Dylan alihisi hiyo ingekuwa njia nzuri ya mwanzo ya kumsaidia kwa kadiri fulani. Wazo hili alimpatia wakati wakielekea kule kwao, naye Fetty alionekana kutokuwa na uhakika ikiwa angeweza. Lakini Dylan alimhakikishia kwamba aliamini aliweza, hivyo aamue ikiwa angekubali ofa hiyo. Fetty akamwambia angelifikiria kwanza suala hilo, naye Dylan akaridhia kwa kusema angesubiri jibu.
Walifika kwao binti baada ya dakika kadhaa, kisha wote wakashuka na kuelekea usawa wa nyumba yao. Dylan akamwambia Fetty aende tu ndani kumpanga dogo na yeye angemsubiri hapo nje. Binti akaingia ndani na kumkuta Japhet pamoja na mjomba wake wakiwa wamekaa, naye akaanza kuwaambia kuhusu hali ya Sophia kule hospitali. Akamwambia Japhet aende kujiandaa haraka ili waondoke, kisha akamuuliza na mjomba pia ikiwa alitaka kwenda, lakini akakanusha na kusema alihitaji kufanya jambo fulani, hivyo angeenda kesho.
Basi, baada ya hapo Japhet akawa amerudi, akiwa amevaa nguo nyingine pamoja na viatu, kisha yeye na dada yake wakamuaga mjomba wao na kuanza kuelekea nje. Walipofika nje tu, Japhet akasema amesahau kitu chumbani, hivyo dada yake akamwambia awahi kukifata na angemkuta nje anamsubiria. Fetty alimkuta Dylan akiwa ameketi kwenye benchi dogo huku anatazama upande mwingine pale nje. Alipomwangalia vizuri, aliona Dylan akicheka peke yake na kumfanya ajiulize ni nini kilichomchekesha. Akamfata mpaka hapo alipokuwa amekaa.
"Dylan..." Fetty akaita.
Dylan akageuka na kusimama baada ya Fetty kusogea karibu.
*Vipi... mbona unacheka mwenyewe?" Fetty akauliza.
Dylan akaachia tabasamu na kutazama upande ule aliokuwa anaangalia.
Baada ya Fetty kuangalia huko pia, aliweza kuona mtoto mdogo wa jirani, mwenye miaka kama miwili hivi, akiwa amevaa chupi iliyotera kwa nyuma kufikia chini ya mapaja, huku akiwa anachukua michanga chini na kujimwagia kwa kuigiza kama anaoga! Fetty alishangaa na kuanza kucheka, kisha akamwita mama ya mtoto huyo kwa sauti kubwa, ambaye alikuwa jikoni akipika, na kumwambia amzuie mwanaye. Mwanamke huyo akafika hapo na kumtoa mwanaye haraka.
"Yaani Dylan, badala umsaidie mtoto we' unamcheka!" Fetty akamwambia.
"Ahahah... dogo alikuwa ameweka show nzuri hapo, lakini siyo yeye tu ndiyo amenifanya nicheke," Dylan akasema.
"Kilichokuchekesha ni nini sasa?" Fetty akauliza.
"Nilikuwa nakuwaza... umekuzwa huku pia kwa hiyo... nikapigia picha kwamba ulivyokuwa mtoto ulikuwa unafanana na vile huyo dogo amepauka," Dylan akasema kiutani.
Fetty akacheka na kumwambia, "Nilikuwa zaidi ya hapo."
"Kweli?! Ahahah... sipati picha jinsi enzi hizo ulivyokuwa kachafuuu... afu leo mishebeduo kama yote..." Dylan akamtania.
"Em' toka hapa!" Fetty akamwambia huku akicheka.
Ni wakati huu ndipo Japhet akawa amerejea.
"Sh'kamoo..." kakamsalimu Dylan.
"Aam... mahaba," Dylan akaitikia.
Fetty akacheka. "Yaani hujui hata kuitikia shikamoo?" akamuuliza.
"Sijazoea," Dylan akasema.
"Nani alikulazimisha ukasome nje ya nchi? Ni mama yako eti?" Fetty akauliza.
"Umesema kwa usahihi, lakini umeotea," Dylan akajibu.
"Ahahah... eti nimeotea!" Fetty akasema.
"Okay, kwa hiyo... ndani mambo yako fresh?" Dylan akauliza.
"Ndiyo. Tuondoke sasa," Fetty akasema.
"Sawa."
Walirudi kwenye gari na kuanza kuelekea hospitalini. Njiani Dylan alinunua vyakula mbalimbali vizuri sana ili waende kukamua pamoja kule hospitali. Kiukweli mambo yote Dylan aliyofanya yalizidi kuongeza upendezi ambao Fetty alikuwa nao kumwelekea, bila kupenda! Wakafika hospitalini mida ya saa kumi na mbili jioni, naye Japhet akapelekwa hadi kwenye chumba cha dada yake. Sophia alifurahi sana kumwona mdogo wake tena, na wote wakaanza kumtuliza kwa kuwa alikuwa akilia kwa furaha baada ya kuwaona watu aliowapenda wakiwa hapo.
Dylan aliondoka baadaye kwenye mida ya saa mbili, akiwaacha wote pale baada ya kushiriki nao chakula alichowaletea. Japhet alimtania sana Fetty kwamba 'amepata mchumba,' na kwa kiasi fulani maoni hayo yalimkosha moyoni huyu dada ijapokuwa alikanusha mara nyingi kwa kusema walikuwa ni marafiki tu. Bila wao kujua, Dylan alikuwa amefanya mpango wa kumlipia Sophia huduma ZOTE alizohitaji hospitalini hapo mpaka wakati ambao angeachiwa na kwenda nyumbani. Hiyo ilikuwa ni pesa ndefu kwa sababu alitaka Sophia atendewe kama vile ni mtoto wa mfalme hapo hospitalini.
★★
Baada ya Dylan kufika nyumbani, alienda zake chumbani kuoga, na kisha akarudi tena sehemu ya sebule na kuketi. Mama yake hakuwa amefika bado, lakini baba yake alikuwa hapo ameketi tu kwenye sofa. Dylan akamuuliza Gilbert mama yake yuko wapi, naye akamwambia ametoka na rafiki yake mmoja ila yuko njiani kurudi. Dylan akataka kuondoka apande juu kwenda kwenye chumba chake, lakini Gilbert akamwambia aketi ili waongee kidogo.
Ijapokuwa sasa hivi walifanya kazi za kampuni pamoja, bado uhusiano wao haukuwa wa karibu sana, hivyo kwa kiasi fulani Dylan aliona hii ingekuwa na uajabu. Lakini akatii na kukaa ili amsikilize mzee wake.
"Ulikuwa hospital?" Gilbert akauliza.
"Yeah," Dylan akajibu.
"Anaendeleaje huyo binti?"
"Ndiyo ameamka tu. Bado baadhi ya viungo vyake havijakaa sawa lakini... with time, ata-heal," Dylan akajibu.
"Sawa. Nafurahi sana kujua kwamba unatoa msaada kwa mtu namna hiyo."
"Asante."
"Unajua... nilienda kumwangalia jana," Gilbert akasema.
Dylan akakunja sura kimaswali.
"Yeah. Nilimkuta mama yake, na huyo msichana... Sophia... alikuwa bado hajaamka," Gilbert akamwambia.
Dylan alishangaa kiasi. "Kwa nini ulifanya hivyo?" akamuuliza.
"Nilitaka tu kumwona. Umekuwa... adamant sana kutaka kumsaidia, na sasa naelewa ni kwa nini."
"Unamaanisha nini?" Dylan akauliza.
"Kwa sababu ya dada yake... Fetty, si ndiyo?" Gilbert akauliza kichokozi.
Dylan akashindwa kujizuia kutabasamu kwa kustaajabishwa na hili.
"Ni ukweli, usikatae," Gilbert akasema.
"Ahah... yeah actually, namjua Sophia kupitia kwa dada yake... na ninamsaidia kwa kuwa ni rafiki yangu," Dylan akajibu kwa unyoofu.
"Rafiki?" Gilbert akauliza.
"Ndiyo."
"Kweli?"
"Ahahah... unataka kusema nini?"
"Nothing. I found something to be very interesting. Medical bill zake zote unazilipia wewe... na umelipia mpaka wakati ambao ataruhusiwa kwenda nyumbani."
"Yeah, so?"
"Hiyo ni pesa nyingi sana Dylan. Sidhani ikiwa 'rafiki logic' ni ya kweli."
"Ahah... kwani siwezi kutoa msaada kwa mtu mpaka awe ni zaidi ya rafiki?"
"Hapana. Nachotaka kukwambia ni kwamba... usiogope hisia zako mwenyewe. Unahitaji kupanua moyo wako Dylan kutambua kwa nini unafanya vitu... siyo kukazia fikira kile unachodhani ndiyo sababu," Gilbert akamshauri.
Dylan akabaki kimya akiyatafakari maneno ya baba yake. Aliongea kwa fumbo, lakini alimwelewa kwa asilimia zote.
"Unaonaje ukimleta "rafiki" yako hapa siku moja... atutembelee?" Gilbert akamwambia.
Dylan akatabasamu, na kisha akasema, "Ni wazo zuri."
Gilbert akatabasamu pia.
Huyu ndiyo Gilbert ambaye Dylan alimpenda sana akiwa mdogo. Nyakati hizi ambazo walikuwa mbali kiukaribu wa mahusiano, ilionekana ni kama alikuwa amebadilika, lakini sasa Dylan akapata kuona kwa kiasi fulani kwamba Gilbert bado ni yule yule; ijapokuwa bado hangeweza kusitawisha ukaribu kama waliokuwa nao zamani.
"Vipi kuhusu kesho kutwa? Mipango inakwendaje?" Gilbert akauliza.
"Oh yeah... aaam... mkutano utafanyika. Wamesema watatuma taarifa ya eneo husika, lakini najua haitakuwa ndani ya huu mkoa. Ninaona uvivu kwenda," Dylan akasema.
"Ahahah... ni must Dylan. Unajua kwamba wewe sasa hivi ndiyo the face of the company," Gilbert akamwambia.
"Sitaki ifike mbali kote huko. Itanipa tu furaha nikiendelea kusaidia kwenu huku nauendesha mgahawa wangu pia," Dylan akasema.
"Ahahah... yeah, hongera sana kwa hilo pia. Nafikiri... kesho nitapita pale ili nipate msosi," Gilbert akasema.
Dylan akacheka kidogo, kisha akamwambia, "Karibu sana."
Wawili hawa hawakuwa wametengeneza maongezi yenye kufurahisha kama haya tokea Dylan aliporudi kutoka Brazil. Pindi hii ilimfariji sana Gilbert, kuona Dylan ameweza kumpa itikio zuri sana kwenye maongezi yao. Dylan yeye akanyanyuka tu na kuelekea chumbani, akijitahidi kupotezea jambo hilo. Lakini alishindwa kuacha kufikiria maneno ya baba yake kuhusu hisia zake, kwa sababu ndani ya moyo wake alijua mzee wake alichoongea ni kweli. Akakaa kumtafakari Fetty kwa kina, ili aone kama kweli alikuwa tu akizizuia hisia zake za upendo kumwelekea.
Kila alipowaza kuhusu mambo mengi yenye kuvunja moyo aliyopitia kwenye mahusiano, alijikataza asipaparukie mapenzi tena, kwa kuwa hakutaka kuangukia pua. Isitoshe, alijiaminisha kuwa Fetty tayari alikuwa na mtu ampendaye, yaani Samwel, ijapokuwa uhusiano wao haukuwa kwenye mstari ulionyooka. Hivyo wazo la kumwelekezea Fetty fikira za kimapenzi akaliweka pembeni yake, na kuendelea kumwona tu kama rafiki mzuri.
★★★
"Yaani watu siku hizi jamani! Mtoto wa watu mzuri kweli, nilienda kumwona ile juzi pale na Fetty," akasema dada fulani aliyeitwa Patricia.
"Kwa hiyo mpaka sasa hivi hajaweza kunyanyuka eeh?" akauliza mwanamke mwingine; mmama.
"Ndiyo. Itachukua muda ila tumeambiwa atarudia hali yake ya kawaida," Fetty akasema.
"Inshaallah Mola amjalie apone," akasema mwanamke huyo.
Yalikuwa ni maongezi kati ya wanawake hawa waliofanya kazi kwenye mgahawa aliofanyia kazi Fetty, ikiwa ni asubuhi ya mapema. Huyo mwanamke mwislamu ndiye aliyekuwa mwenye mgahawa, na hapa ilikuwa ni asubuhi wakiongelea kuhusiana na ajali iliyompata mdogo wake Fetty huku wanaendelea na kazi kadha wa kadha sehemu ya jikoni. Akaja dada mwingine aliyefanyia kazi hapo pia.
"Fetty, yule kaka amekuja... anakutaka," huyo dada akasema.
"Yule mkaka wa Fetty handsome handsome?" akauliza Patricia.
Wote wakacheka na kisha dada yule akakubali.
"Hivi ulimfanyaje maana kila akija lazima aagize wewe tu," huyo mama akamwambia Fetty.
"Haka si kachawi tu... kanatumia unga wa ngano, sijui upupu!" Patricia akatania.
"Hamna, ni tako tu hilo," yule dada aliyekuja akasema.
Wote wakacheka.
"Nenda kamsikilize mteja wako, halafu ndiyo utaenda sasa," huyo mama akamwambia Fetty.
"Haya," Fetty akajibu.
Fetty alikuwa amemwomba mama huyo ambaye ni mwajiri wake ruhusa ya kwenda mapema hospitalini kwa Sophia. Kwa hiyo hapo alivyomwambia kwamba akimaliza kumhudumia Dylan ndiyo angeenda, alimaanisha hospitalini. Binti akatoka na kwenda kule ndani, akimkuta Dylan ameketi huku anatabasamu baada ya kumwona mrembo akija. Kulikuwa na wateja wengine wakipiga misosi yao ya asubuhi hapo, naye Fetty akapita meza kadhaa na kumfikia Dylan.
Walisalimiana vizuri, kisha Dylan akamwambia Fetty amletee chai ya maziwa, chapati mbili, na supu ya nyama yenye nyama nyingi kama alivyopenda. Sikuzote hata kama angeagiza nini, lazima malipo yalikuwa ni elfu kumi kamili; bila kujali chenji iliyobaki. Hivyo, Fetty akaondoka kwenda kumfatia vitu hivyo, huku wanaume hapo wakiangalia jinsi kalio lake lilivyonesa-nesa kila alipopiga hatua. Hata Dylan mwenyewe alipenda sana.
Baada ya dakika chache, akarudi akiwa amebeba sinia pana lililowekewa vyakula alivyoagiza Dylan. Akaviweka mezani huku anatabasamu, naye Dylan alikuwa akimwangalia tu kiunoni. Yaani jinsi mwili wa Fetty ulivyokuwa mnono kutokea kiunoni na ulivyojichora kulimdatisha sana Dylan, lakini akajizuia tu asipitilizishe mawazo yake mpaka mbali mno.
"Nikuwekee vingapi?" Fetty akauliza.
Alikuwa anamaanisha amwekee vijiko vidogo vingapi vya sukari kwenye chai yake.
"Viwili tu vinatosha. Sitaki chai yangu iwe tamu mno kukuzidi wewe," Dylan akatania.
Fetty akamwangalia kwa upendezi mwingi, kisha akamuuliza, "Ulishawahi kunionja?"
Tabasamu lililokuwa usoni mwa Dylan likafifia taratibu, naye akaanza kumwangalia Fetty kwa kushangazwa na maneno yake kiasi. Binti yeye akawa anakoroga tu sukari kwenye chai huku akitambua kwamba Dylan anamtazama sana, kisha akabeba sinia lake na kuondoka bila kumwangalia wala kusema lolote, akimwacha Dylan anamsindikiza tu kwa macho.
Dylan akabaki anayatafakari maneno yale. Yeye kumtania vile ilikuwa masihara tu kutokana na jinsi alivyo, lakini maneno ya binti yalikuja kivingine kabisa. Yaani ilikuwa ni kama Fetty alimpa ujumbe fulani usio wa moja kwa moja, lakini bado akawa tu anaizuia akili yake isifike huko kwa kuwa alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake wote kujidhibiti.
Alipomaliza kula, Fetty alirudi tena, naye akampatia pesa ya malipo. Binti akashukuru huku akimtazama jamaa kwa njia fulani ambayo kwa Dylan ilikuwa ngeni. Hakuwahi kumtazama jinsi alivyomtazama sasa.
"Fetty..." akamwita.
"Bee..." akaitika.
"Nataka leo nikutoe... out. Ungependa?" Dylan akauliza.
Fetty akaangalia pembeni na kutabasamu, kisha akauliza, "Saa ngapi?"
"Jioni. Ukimaliza kazi si unaenda hospital baadaye?"
"Actually... ninaondoka sasa hivi kuelekea hospitalini. Nimeomba ruhusa," Fetty akamjulisha.
"Oh kumbe! Basi, twende pamoja nikupitishe hospitalini."
"Si unaenda kazini lakini?"
"Ndiyo. Nakupeleka huko, halafu nageuza. Baadaye ndiyo nitakupitia kwa ajili ya outing," Dylan akasema huku ananyanyua nyusi zake kichokozi.
"Sawa. Kwenye mida ya saa ngapi kabisa?"
"Kwenye mida ya saa moja au mbili... ni wewe tu," Dylan akasema.
"Mmmm... hiyo inamaanisha hakutakuwa na mtu kwa Sophia maana mama ataondoka," Fetty akamkumbusha.
"Usijali kuhusu hilo. Nitaweka muuguzi maalum ili awe naye karibu," Dylan akamwambia.
"Sawa basi. Tutaenda. Ni wapi?" Fetty akauliza.
"Utapaona. Utapapenda sana. Pendeza mtoto," Dylan akamwambia.
Fetty akatabasamu.
Alifurahi mno moyoni mwake na kuwa na matarajio mengi mazuri. Ijapokuwa Dylan alijiaminisha kwamba alifanya haya yote kirafiki tu, furaha aliyohisi pia ilipita hisia za kawaida za urafiki. Alitazamia kwa hamu 'date' hii kwa kuwa alipanga kumpeleka sehemu ya muhimu. Baada ya hapo, Dylan akakaa kama dakika tano hivi akimsubiria Fetty apange mambo yake hapo, kisha wote wakaondoka pamoja.
Wakiwa mwendoni, kwa mara ya kwanza kabisa ndiyo Dylan aliweza kumsimulia Fetty kuhusu maisha yake kule Brazil. Wakati wa nyuma alikuwa tu amemwambia kwamba alisomea nje ya nchi, lakini sasa akamwelezea kwa sehemu maisha yake ya huko. Sasa binti akaweza kuelewa zaidi ni kwa nini sikuzote aliiona lafudhi ya Dylan kuwa yenye utofauti, na sababu ilikuwa ni kukaa huko kwa muda mrefu. Alimwambia kuhusu mambo mengi mazuri ya kule, chuo alichosomea, na shangazi yake mdogo pia.
Wakiwa wanaelekea huko bado, Dylan alipigiwa simu kutoka kwenye kampuni yao na kujulishwa kwamba kulikuwa na makaratasi muhimu sana yaliyohitaji sahihi yake. Ni Jaquelin mwenyewe ndiye aliyemwambia aharakishe ili waweze kuyatuma yalikohitajika, hivyo Dylan akamwambia Fetty kwamba wangepita kwenye kampuni yao kwanza mara moja ili ashughulikie hilo, ndipo angempeleka hospitalini sasa.
Binti hakuwa na kipingamizi, na baada ya dakika kadhaa wakafika nje ya jengo la kampuni yao. Dylan akashuka na kumwambia Fetty waende pamoja, na ijapokuwa mwanzoni binti alisita, Dylan akamshurutisha kwa kumshika mkono na kwenda pamoja naye mpaka ndani. Ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kwa Fetty kuingia kwenye jengo hilo, naye alipendezwa sana na umaridadi wake. Alitazamwa mno na wafanyakazi wa hapo waliojiuliza alikuwa ni nani kwa Dylan mpaka aende naye hapo akiwa amemshika mkono. Dylan hakujali macho ya watu na kwenda moja kwa moja mpaka kwenye lifti pamoja na Fetty, kisha wakaelekea juu. Alimpeleka Fetty mpaka ofisini kwake na kumwambia amsubiri humo, kisha yeye akaenda kwenye ofisi ya mama yake upesi.
Baada ya muda mfupi, Dylan akarejea na kumkuta Fetty akiwa ofisini kwake bado, naye akamjulisha kuwa kazi yake ilikamilika hivyo wangeweza kuondoka. Wakatoka pamoja tena mpaka kwenye gari, kisha wakaendeleza safari yao ya kuelekea hospitalini. Alimfikisha binti na kuwasalimu Sophia na mama yao, na baada ya hapo akarejea tena kwenye kampuni akiiacha familia hiyo.
★★
Jioni ilionekana kufika haraka sana. Fetty aliwahi kuondoka hospitalini na kuelekea ghetto kwake kujiandaa vizuri. Alihisi uchangamfu mwingi mno kana kwamba alikuwa anatoka na mpenzi wake, na ni kama aliona mambo yangeelekea huko, ijapokuwa naye pia bado alijidhibiti. Alijisafisha vizuri sana, kisha akavaa kigauni chekundu kilichoyaacha mabega na mikono yake wazi, kilichoishia magotini, na kilichoubana mwili wake vizuri sana kulichora umbo lake matata vyema. Akazichana nywele zake vizuri na kuupamba uso kiasi, miguuni akivaa viatu vyekundu vya kuchuchumia vilivyoonyesha kucha zake zilizopakwa rangi nyekundu miguuni.
Hazikupita dakika nyingi akiwa anajiweka sawa mbele ya kioo, na simu yake ikaita. Akapokea baada ya kuona ni Dylan ndiyo anapiga, naye akamwambia alikuwa nje tayari anamsubiria. Binti akamjulisha kuwa anatoka muda siyo mrefu, kisha akakata simu. Akajipulizia manukato mtoto, na baada ya hapo akatoka na kuufunga mlango wake. Majirani wenzake walikuwa wanamsifia hapo nje kwa mwonekano wake, huku wengine wakiona wivu na kwenda kumchungulia mpaka alipoingia ndani ya gari la Dylan na kuondoka.
Dylan alimsifia sana kwa kupendeza, mpaka Fetty alihisi aibu. Yaani mwendo mzima jamaa alichoongelea sanasana ilikuwa ni mwonekano wa Fetty tu, hata ingawa binti alijitahidi kuzungumzia mambo mengine pamoja naye. Walifika hospitalini, naye mama yake Fetty alipendezwa na mwonekano wa binti yake. Fetty alikuwa mstaarabu lakini alijua kupendeza pia hata kwa hivyo hivyo vitu vichache alivyokuwa navyo. Dylan akamwambia mama yake Fetty kuwa walikuwa wanaenda sehemu fulani, hivyo wangeacha muuguzi maalum wa kumwangalia Sophia.
Mama yake alifurahi sana kujua walikuwa wanatoka pamoja, kwa kuwa matarajio mengi aliyokuwa nayo yalionekana kushika hatamu sasa. Akawatakia matembezi mema, kisha baada ya dakika kadhaa, Dylan akaenda kumpanga muuguzi yule aliyesema angemwangalia Sophia. Akarudi pamoja naye, kisha wawili hao wakamuaga mama Fetty na Sophia, nao wakaondoka hapo. Mama yake pia angeondoka muda siyo mrefu.
Ilikuwa ni saa moja jioni hivi tayari, naye Dylan akawa anamwendesha Fetty kuelekea sehemu ambayo binti hakutambua ni wapi. Matarajio yake mengi yalikwenda tofauti na alivyotazamia baada ya Dylan kulifikisha gari nje ya geti la nyumba kubwa sana na kupiga horn ya gari lake. Fetty akashangaa.
"Dylan hapa ni wapi?" akamuuliza.
"Karibu kwetu," Dylan akasema huku anatabasamu.
Fetty akatoa macho asiamini kama kweli Dylan alikuwa amempeleka kwao.
"Kwenu? Kwa nini umenileta kwenu Dylan?" akauliza kimashaka.
Ni wakati huu ndipo geti la nyumba yao likafunguliwa na mlinzi.
"Hukumbuki uliniambia ulitamani kupaona kwetu siku moja? Leo ndiyo hiyo siku sasa," Dylan akasema huku akiliingiza gari ndani.
"No... Dylan... nilikuwa natania tu... hivi kweli.... yaani umenileta kwenu... nimevaa hivi..."
Dylan akacheka.
"Dylan acha michezo yako bwana. Twende unirudishe sasa hivi," Fetty akasema.
Wakati huu, Dylan alikuwa amekwishaliegesha gari, lakini akawa anaangalia gari lingine hapo nje ambalo halikuwa la kwao. Akakisia kuwa huenda kulikuwa na mgeni mwingine tu amekuja.
"Tumeshafika. Shuka," Dylan akamwambia.
"Mm-mm... me sishuki," Fetty akagoma.
"Fetty come on..." Dylan akambembeleza.
"We' hujaniambia kama unanileta kwenu.... kweli Dylan unategeme..."
Dylan akakishika kiganja chake ili kumtuliza, naye Fetty akatulia kidogo na kumwangalia.
"Usiogope. Uko na mimi. Nakuahidi kila kitu kitakuwa sawa. Niamini," Dylan akamwambia kwa sauti ya upole.
Fetty akamwangalia tu huku akiwa na wasiwasi bado, naye Dylan akashuka na kuzunguka gari mpaka kwenye mlango wa siti aliyoketi Fetty. Akaufungua na kumnyooshea mkono ili amsaidie kutoka, naye Fetty akampa mkono na kutoka; kama wazungu wafanyavyo. Binti aliitazama nyumba yao Dylan, jinsi ilivyokuwa kubwa na yenye umaridadi wa hali ya juu. Akamwangalia Dylan kimashaka bado, naye mwamba akatabasamu tu na kumshika mkono, kisha akaanza kuelekea sehemu ya mlangoni pamoja naye.
Walipofika mlangoni, Dylan akamhakikishia Fetty kwamba kila jambo lingekwenda vizuri, kisha akaufungua mlango na kupiga hatua chache kuingia ndani. Ile anayapeleka macho yake pale sehemu ya sebule, tabasamu alilokuwa nalo usoni likageuka na kuwa butwaa kubwa sana baada ya kumwona mtu ambaye hakutarajia kumkuta hapo hata kidogo! Akabaki amesimama tu akishangaa, na sehemu hiyo walikuwa wameketi watu watatu kwenye masofa; Gilbert, Jaquelin, na nwanamke mwingine ambaye alimjua VIZURI sana.
Huyu alikuwa ni shangazi yake mdogo, yaani dada mdogo wa Gilbert, yule yule aliyekwenda kuishi naye kule Brazil. Alikuwa hapa wakati huu, na ni jambo ambalo Dylan hakuwa ametarajia kabisa. Baada ya Jaquelin kumwona Dylan, alisimama akiwa na uso ulioonyesha ana furaha sana.
"Hey Dylan... look who's here! (.. ona aliye hapa!)" Jaquelin akasema kwa shauku.
Shangazi yake akasimama pia baada ya kumwona mpwa wake huyu, akimtazama kwa hisia sana.
Dylan akabaki kumwangalia tu kimashangao, akiwa amerudiwa na kumbukumbu nyingi za wakati uliopita baada ya kumwona shangazi yake tena........
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Comments