Sehemu ya 04
Nilipokutana naye sikujua kama maisha yangu yangekuwa tofauti namna ile. Ilikuwa siku ya Jumamosi, jua kali linawaka juu ya anga la Dar, vumbi la barabara likipanda juu kila gari lilipopita, na mimi nilikuwa nimekaa pembeni mwa duka la Mzee Rashid nikikunywa maji ya baridi baada ya kazi nzito ya kupakua mifuko ya saruji. Nilihisi miguu yangu imeishiwa nguvu, mikono imejaa jasho, na mwili wangu unataka kupumzika kabisa.
Wakati niko pale, kijana mmoja alipita. Alikuwa na umri wa karibu na mimi, labda miaka 21 au 22. Alikuwa amevaa t-shirt nyekundu yenye maandishi madogo, suruali ya jeans yenye viraka, na viatu vya raba vilivyokuwa vimechakaa vibaya. Lakini cha ajabu, uso wake ulikuwa na tabasamu kubwa sana, kana kwamba hana tatizo lolote duniani. Alisimama ghafla, akaniangalia, kisha akasema:
"Bro… mbona unaonekana umechoka vibaya? Nimekuwa nakuona siku kadhaa unafanya kazi hapa duka la Mzee Rashid, una nguvu sana lakini uso wako kila mara una huzuni."
Nilishangaa, nikamjibu kwa aibu: "Ndio kaka… maisha Dar sio mchezo. Nilitegemea nikija huku nitapata mwanga, kumbe giza ndio limekuwa kubwa zaidi."
Akanitabasamia tena, kisha akajikalia jirani yangu. "Mimi naitwa Kelvin, ila marafiki wengi wananita Kido. Nimetokea Morogoro mwaka jana. Nilikuja hapa Dar nikiwa na ndoto kubwa kama zako. Nilianza vibaya sana, nililala hata stendi ya mabasi kwa miezi mitatu bila pa kuishi. Nililaumu kila kitu, lakini baadaye nikajifunza kitu kimoja – ukiishia kulalamika Dar, utakufa njaa. Dar ni mji wa vichwa, siyo misuli pekee."
Nilimsikiliza kwa makini. Alizungumza kwa urahisi, si kwa kujidai, bali kwa uzoefu wa kweli. Nilihisi kama namwona ndugu ambaye sijawahi kuwa naye mjini.
Akaendelea: "Maxwell, maisha Dar ni magumu, lakini kila mtaa una fursa zake. Kuna watu wamefanikiwa kwa kuuza maji tu. Kuna watu wamepata maisha bora kwa kupiga picha na simu ndogo ndogo, wakawa wapiga picha wa harusi. Kuna wengine walikuwa kama sisi – vijana wasio na kitu – leo hii wanamiliki maduka. Suala ni kujiamini na kuanza na kidogo ulicho nacho."
Nilimwangalia nikiwa na maswali mengi kichwani. Nikamwambia: "Lakini kaka, mimi sina chochote cha kuanzia. Hata hela nikipata, naitumia kula tu. Sina ndugu wa kunisaidia, sina elimu kubwa zaidi ya kidato cha nne."
Alitulia kidogo, kisha akasema kwa sauti ya chini: "Hata mimi nilikuwa hivyo. Nilianza kuuza karanga kwa mkopo. Nilimshawishi mama mmoja alinipa karanga nuzile, nikaanza kuuza mtaani. Nilipata faida ndogo, nikarudisha pesa yake, nikabaki na hela kidogo ya kula. Siku ya pili nikajikaza tena. Leo hii nimesogea kidogo – siwezi kusema nina maisha mazuri sana, lakini angalau siishi njaa tena."
Nilihisi machozi yanataka kunitoka. Sikuwa nimezoea mtu wa umri wangu kuniongelea kwa ukweli na moyo safi kiasi hicho. Kido alionekana si mtu wa kujigamba, bali mtu wa kuzungumza kile alichopitia. Niliona uhalisia wa maisha yake machoni pake – alama za njaa, shida na pia ushindi wa kidogo.
Tulikaa pale kwa saa kadhaa, tukizungumza mambo mengi. Aliniambia namna Dar ilivyo mji wa mitihani – unaweza ukawa na pesa leo, kesho ukawa huna chochote. Lakini pia, Dar iliyoileta ndoto kwa wengi waliokuwa wavumilivu.
Kido alinialika nikatembelee geto lao, lililokuwa chumba kidogo kilichojaa vijana wanne waliokuwa wanalala pale. Nilipoingia, niliona godoro moja limewekwa chini, na wengine wamelala kwa zamu. Harufu ya jasho na chakula kilichopikwa jana ilijaa humo, lakini kwa namna ya ajabu nilijisikia nyumbani. Vijana wale walinipokea kwa mikono miwili, walinichekesha, wakaniambia “Karibu geto, huku ndio Dar yenyewe!”
Usiku ule tulikula ugali na maharage yaliyopikwa kwenye sufuria ndogo. Tuliweka sufuria katikati, kila mmoja akashika kijiko chake. Tulicheka, tukasema stori, na kwa mara ya kwanza tangu nifike Dar nilihisi upweke wangu unapungua.
---
Baada ya siku ile, Kido akawa rafiki yangu mkubwa. Tulianza kukutana mara kwa mara, mara nyingine nikimaliza kazi duka la Mzee Rashid, alinikuta na twende tukatafute vibarua vya ziada kama kufagia barabara au kubeba mizigo sokoni. Wakati mwingine tulitembea tu mitaani tukipiga stori, tukijiuliza maisha yetu yatakuwaje miaka michache ijayo.
Kido kila mara alikuwa akinisisitiza: "Max, unajua akili yako ndio mtaji mkubwa kuliko kila kitu? Usijidharau. Umefaulu kidato cha nne, hiyo ni kitu kikubwa. Hata kama hujaendelea shule, elimu uliyo nayo inaweza kukusaidia kwenye kila jambo."
Nilianza kuamini maneno yake. Nikaanza kuona kwamba Dar si lazima nikae nikisubiri mtu anipe kazi kubwa – labda na mimi naweza kuanza na kile kidogo nilicho nacho.
Lakini pia Kido alinifungua macho upande wa pili wa maisha ya Dar. Alinionyesha vijana waliokuwa wakiishi maisha ya haraka – wengine walijiingiza kwenye madawa, wengine kwenye wizi, wengine wakajiuza miili yao. Aliniambia: "Max, ukiwa huna msimamo, Dar inaweza kukumeza. Usiingie kwenye hizo njia. Bora ule mihogo kwa chumvi kuliko kula kwa wizi."
Maneno hayo yalinigusa sana. Nikaanza kumheshimu Kido sio tu kama rafiki, bali kama ndugu wa damu. Tulishirikiana shida na furaha. Wakati mwingine nilipokuwa sina hata mia moja mfukoni, alinipa ugali wake nusu. Wakati yeye alikuwa hana kitu, nilimgawanya kilichokuwa changu. Tulijua maisha Dar sio ya mtu mmoja, bali ni ya kushirikiana.
---
Kadri muda ulivyokuwa unasonga, nilianza kugundua kuwa urafiki wetu ulikuwa zaidi ya urafiki wa kawaida. Ulikuwa ni msaada wa kiroho. Kila nilipokata tamaa, Kido alinifanya nicheke. Kila nilipohisi giza, alinipa mwanga.
Lakini pia ndani yangu, nilianza kuhisi kitu kipya – ndoto kubwa zaidi. Niliwaza: je, inawezekana kweli mimi, kijana kutoka Nguruka Kigoma, nikawa mtu wa maana hapa Dar es Salaam? Nilipojiangalia usiku, nikajiona bado masikini, bado naishi kwenye chumba kisicho na umeme, bado navua viatu vya raba vilivyochoka. Lakini nilipoangalia ndoto moyoni mwangu, niliona picha kubwa – picha ya kesho yangu ikiwa na maana.
Na hapo ndipo safari yangu na Kido ikaanza rasmi. Safari ambayo baadaye ingetufundisha sote kuwa Dar es Salaam sio tu mji wa shida, bali ni uwanja wa mapambano, ambapo washindi sio wale wenye nguvu pekee, bali wale wenye moyo wa kuamini hata kwenye giza zito zaidi.
Comments