Reader Settings

DYLAN

Story by Elton Tonny

Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

(R-rated 18+)


★★★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA KUMI NA NNE

★★★★★★★★★★★★★★★


"Cammy... bado hujalala?" Jaquelin akamuuliza.

Camila akameza mate na kusema, "Aa... yeah. Sijalala bado..."

"Nimesikia kama ulikuwa unaongea mtu," Jaquelin akasema.

Camila akazidi kuingiwa na wasiwasi, lakini akajitahidi kujidhibiti. "Aam... yeah. Nilikuwa... nilikuwa naongea na simu," akadanganya.

"Ahaaa... sawa."

Camila akamtazama kifupi Dylan na kuona jinsi alivyojitahidi kujikaza pale juu. Jaquelin akaongeza hofu ya Camila baada ya kuanza kuingia chumbani akimfata. Dylan akasema kwa sauti ya chini 'shit!' maana alijua vizuri kwamba endapo kama mama yake angegeuka, basi angemwona. Jaquelin akafika karibu zaidi ya Camila akiwa anatabasamu.

"Alikuwa Felipe bila shaka," akasema Jaquelin.

Camila akatabasamu kihofu-hofu tu.

"Nilikuwa nataka kuuliza, huwa anapenda lobsters (kaa)? Kuna maduka huku makubwa wanauza. Ikiwa na yeye anakula hizo, basi kesho niagize," Jaquelin akasema.

"Ndiyo... huwa anakula. Anapenda," akajibu Camila.

"Ahah... sawa. Dylan asingekuwa anaondoka angekula pia. Anazipenda sana."

Wakati wakiendelea kuongea, Dylan akaona aanze kushuka taratibu bila kutoa sauti yoyote. Alitumia umakini sana, na Camila akatumia akili kwa kuuliza mambo fulani ili kumkengeusha Jaquelin asigeuke nyuma. Dylan akawa amefika chini bila kutoa sauti, na sasa akaanza kuelekea nje ya mlango taratibu mno ili atoke kimya kimya. Baada ya kufanikiwa kutoka ndani hapo, akajibanza kwa nje na kushusha pumzi ya utulivu, kwa kuwa mapigo ya moyo yalimdunda kwa nguvu. Akacheka kidogo kutokana na jinsi jambo hilo lilivyosisimua, kisha akarejea chumbani kwake.

Alikaa kitandani kwa dakika kadhaa, akiwaza kuhusu kilichokuwa kimetokea chumbani kwa shangazi yake. Alijua kwamba jambo sahihi ilikuwa kumwachia Camila kutoka moyoni mwake, lakini bado roho ilimuuma kwa sababu hisia zake kumwelekea mwanamke huyo zilikuwa zenye nguvu sana. 

Kimahusiano, Dylan alikuwa amepita kwa wasichana kadhaa ambao mwisho wa siku walimtendea kwa njia yenye kuvunja moyo ijapokuwa alijitahidi kuwaonyesha upendo mwingi. Kwa hiyo kwa kutegemea mambo aliyopitia kutokea kwa mpenzi wake wa kwanza mpaka kufikia kwa Harleen, tayari alikuwa ameshaondoa wazo la kufatilia mwanamke mdogo kwa kuwa wana mambo mengi mno ambayo yalifanya kipimo chake cha imani kuwaelekea kipungue. 

Lakini alimjua Camila vizuri sana. Aliupenda utu wake. Na kiukweli, ni kama vile alikuwa anatafuta mtu aliye kama Camila ili awe naye, lakini hakuona bado, ijapokuwa Fetty alikaribia. Kwa hiyo hisia zake kwa shangazi yake bado zilikuwa zenye nguvu mno, ila hali waliyokuwa ndani yake haikuruhusu aweze kuzishiriki pamoja naye.

Kijana akaona asiendelee kukazika sana kiakili kuhusiana na jambo hili kwa kuwa haingekuwa na faida yoyote. Akatazama muda na kukuta ni saa nane usiku tayari, hivyo akajilaza na kuanza kutafuta usingizi.


★★★


Ilikuwa ni asubuhi yenye pilika-pilika upande wa Fetty kulipokucha. Aliwahi mgahawani mapema na kuanza kazi kama kawaida; kusafisha vitu mbalimbali hapo, kusaidia mapishi, na kuhudumia wateja. Kwa kuwa walikuwa na kawaida ya kuwapelekea wateja fulani vyakula sehemu mbalimbali za karibu mjini hapo, alisaidizana na wenzake kufanya hivyo pis. 

Ilipofika mida ya saa nne, Dylan akampigia simu kumkumbusha kuwa alipaswa kumpelekea chakula ofisini, kitu ambacho Fetty hakuwa amesahau. Alimwambia angefika ndani ya dakika 15 tu, hivyo akakata simu na kuanza kumwandalia rafiki yake chakula na kukiweka kwenye makontena madogo na masafi sana. Fetty alikuwa mwenye bidii, na hakutaka nafasi hiyo ya kupata pesa impite hata kama aliyemwagiza alikuwa rafiki yake na ilikuwa mbali. Baada ya kuviweka kwenye mfuko, akawaaga wenzake wa hapo mgahawani na kuanza kuelekea huko. 

Ilimchukua dakika kadhaa kufika maeneo ya kampuni yao Dylan. Akamlipa dereva wa bajaji, kisha akaanza kuelekea ndani kule, akipendezwa na urefu na umaridadi wa jengo la kampuni hiyo. Akiwa anaelekea juu, alipishana na watu kadhaa ambao walisalimiana naye vizuri, naye akaelekea mpaka kwenye lifti na kuingia ndani. Alikumbukia jana walipokuja na Dylan hapa, mwanaume alibonyeza kitufe chenye namba 7, yaani ghorofa la saba, hivyo akanyoosha kidole chake ili abonyeze kitufe hicho. 

Lakini wakati akiupeleka mkono wake hapo, simu yake ikaanza kuita na kumfanya aangalie kuielekea ilipokuwa mfukoni mwa suruali yake; kitu kilichofanya kidole chake kikosee pa kubonyeza, na kubonyeza namba 6 badala ya 7. Milango ya lifti ikafunga, nayo ikaanza kumpeleka juu, akifikiri alibonyeza 7. Akaitoa simu yake mfukoni na kukuta anayepiga ni Dylan, naye akatabasamu kisha kupokea.

"Nini kinakutafuna wewe? Mbona hufiki tu?" Dylan akalalamika.

"Ahahahah... nakaribia bwana," akasema Fetty kwa furaha.

"Umeweka nyama kama zote?"

"Kama zote."

"Okay. Unapakumbuka ofisini kwangu?"

"Ndiyo. Napakumbuka. Si nitakukuta humo?"

"Yah. We' ukifika ingia tu, sawa?"

"Haya."

"Haya. Waisha hizo nyama."

Fetty akacheka, na kisha Dylan akakata simu. 

Lifti ilipofunguka, Fetty alianza kutembea akivipita vyumba kwa kuhesabu jinsi alivyokumbuka chumba cha ofisi ya Dylan kilipojipanga. Alijua kilikuwa mwishoni, hivyo akapita moja kwa moja mpaka mwisho huko na kuufikia mlango. Kulikuwa na watu wachache hapo, na wengi hawakumkazia uangalifu, hivyo akausukuma mlango na kuingia ndani. Alianza kwa kuchungulia, lakini hakuona mtu. Alipoingia ndani zaidi, aliona ni kama vile mwonekano wa ofisi hii ulikuwa tofauti na jinsi alivyoikumbuka ofisi ya Dylan. Hakukuwa na mtu hapo, naye akawaza huenda amekosea ofisi, au Dylan anamfanyia mchezo.

Alitembea taratibu kuelekea mlango ambao ulikuwa wa chumba chenye makolokolo mengi ya kiofisi. Akafungua mlango na kuingia kuchungulia humo, lakini hakukuwa na mtu. Kwa haraka akawaza bila shaka alikuwa amekosea ofisi, na sasa akataka ageuze ili kurudi nje. Lakini ile anageuka nyuma, akaona mtu anaingia ndani ya ofisi hii, akiwa amevalia suti nyeusi na miwani ya macho. Alikuwa ni Mr. Bernard mwenyewe.

Fetty akaingiwa na wasiwasi sasa, naye akajirudisha ndani ya chumba hicho kidogo. Akashindwa kujua afanye nini maana ameingia kwenye ofisi ya mtu bila ruhusa, huenda hata angeitwa mwizi. Lakini alijua ilikuwa ni kimakosa tu kwamba ameingia hapo, na akawaza kama angemweleza, basi angeelewa.

Bado Mr. Bernard hakuwa amemwona Fetty kwa sababu binti alikuwa ndani kidogo ya chumba kile kingine, akijifikiria atoke ili aongee na huyo mtu mzima. Wakati anataka kutoka, akamwona Mr. Bernard amesimama usawa wa mlango wa chumba hiki alichokuwa ndani yake, akiwa ameweka simu sikioni huku amempa mgongo. Ikabidi Fetty atulie kwanza.

"Ndiyo..." 

Sauti ya Mr. Bernard ikasikika.

"... hakikisha kila kitu kinakwenda kama tulivyopanga... umeelewa?" akaendelea kusema kwa sauti yenye mkazo.

Fetty akaendelea kumsikiliza.

"Vizuri. Itakuwa kwenye mida ya saa sita. Hakikisha hakuna mtu hata mmoja anayetoka..."

Fetty akakunja uso wake kimaswali. Hakuweza kuelewa mwanaume huyo alikuwa anazungumzia nini, lakini hakikuonekana kuwa kitu kizuri. Akamwona ameshusha simu yake kutoka sikioni.

"Your downfall begins now, Gilbert (Kuanguka kwako kunaanza sasa, Gilbert)," akasema Mr. Bernard kwa sauti ya kikatili.

Fetty alishangaa sana, na alijiuliza maswali mengi mno. Hakuwa na ma-degree ya kisomi lakini alielewa vizuri kile ambacho Mr. Bernard alisema. Alielewa jina hilo la Gilbert ni la baba yake Dylan, na bila shaka mwanaume huyu alipanga kufanya jambo fulani ambalo lingemdhuru baba ya rafiki yake. Kilichokuwepo ilikuwa ni kuhakikisha anamfikishia Dylan jambo hili ili kumwonya kuhusu hatari ambayo ingeweza kumkabili baba yake.

Mr. Bernard akaelekea mezani kwake na kupitia mafaili fulani, bila kutambua kulikuwa na mtu ofisini kwake. Fetty akaendelea kutulia humo humo ndani, akiombea jambo fulani litokee ili mwanaume huyo aondoke, ili naye aweze kutoka. Ilikuwa ni kama Mungu alijibu sala yake, kwa kuwa ndani ya dakika chache, Mr. Bernard alitoka ofisini hapo na kuelekea alikojua yeye. 

Bila kupoteza wakati, Fetty akatoka kwenye chumba hicho na kwenda mpaka mlangoni. Akachungulia nje, na hakuweza kumwona Mr. Bernard, hivyo akatoka haraka na mifuko yake akielekea upande wa ngazi za jengo. Akatulia hapo na kutoa simu yake, kisha akampigia Dylan. Akamwambia alikuwa amefika lakini alisahau ofisi yake ilipokuwa, hivyo Dylan akamwelekeza vizuri, na sasa Fetty akaelewa cha kufanya.

Haikuchukua dakika nyingi, naye akawa amefika ofisini kwa mwanaume. Alimkuta ameketi kwenye sofa lake huku anaangalia muziki wa kilatini (aina ya reggaetón), na baada ya kumwona Fetty, Dylan akanyanyuka akiwa anatabasamu.

"Finally!" Dylan akasema kwa shauku.

"Ahah... pole nimechelewa. Nilipotea," akasema Fetty.

"Si nilikuuliza kama bado unapakumbuka ukasema 'ng'weee,' kilichokupoteza nini sasa?" Dylan akamtania.

"Ahahahah... lione kwanza," Fetty akamwambia na kumpiga ngumi nyepesi begani.

"Mmmm... hapa nitakamua mpaka nisahau kula siku nzima," akasema Dylan baada ya kuvitoa vyakula.

"Kwa hiyo kweli ilikuwa lazima ule chakula hiki?" akauliza Fetty.

"Ndiyo. Nilikuwa nataka nikuone na wewe pia," Dylan akasema bila kumtazama.

Fetty akamwangalia kwa hisia sana. Aliyapenda sana maneno ya Dylan, na kila siku ilikuwa kama mwanaume alikuwa anampa sababu ya kuvutiwa naye hata zaidi. Akawa anauangalia uso wake, huku Dylan akitoa chapati na kuikunja, kisha akaichovya kwenye supu na kuanza kula kwa hamu kubwa. 

"Mmmm... delicioza (tamu)," akasifia.

"Ahahah..." Fetty akacheka huku anamwangalia.

"Nitabeba na nyama kwenye helicopter. Nikifika kule nazila zote," akasema Dylan.

"Wacha! Unaenda kwa helicopter kumbe?"

"Yeah. Usingechelewa ningekula huku nimekaa."

"Kwani unatakiwa uondoke saa ngapi?"

"Ilikuwa niondoke saa sita, ila ratiba imebadilika. Chopper inatua hapa saa tano... ikiwezekana nitarudi leo leo," Dylan akatania, kwa kuwa asingerudi kwa siku kadhaa.

"Saa sita?" Fetty akauliza.

Dylan akatikisa kichwa kukubali na kubugia nyama.

Kitendo cha Dylan kusema saa sita kilimkumbusha Fetty kuhusu Mr. Bernard. Aliongelea kuhusu jambo fulani ambalo lingetokea saa sita pia, na lilihusiana na Gilbert. Akatambua huu ulikuwa muda mwafaka wa kumwambia Dylan alichosikia.

"Dylan..." akamwita.

"Mm..." jamaa akaitika huku anakunywa supu.

"Wakati ule... wakati nimepotea ofisi... niliingia kwenye ofisi ya..."

"Umeingia kwenye ofisi ya mtu? Ahahahah... usiniambie umetimuliwa!" Dylan akamtania.

"Ahah... hapana. Hakuniona. Nilijificha."

"Wewee! Ilikuwa ofisi ya nani?"

"Simjui... ni mbaba mtu mzima. Ni... mnene kiasi, mweusi afu'... amevaa miwani ya macho hivi... ana kipara..."

"Aaaaa unamwongelea Mr. Bernard," Dylan akamjuza.

"Nafikiri ndiyo huyo."

"Huwaga ananikera na kitambi chake huyo! Ni vizuri hajakuona maana angeanzisha timbwili."

"Well... nilimsikia alikuwa anaongea kwenye simu... na mtu fulani sijui nani..." Fetty akaanza kufunguka.

"Mm-hmm..." Dylan akatega sikio kwa makini.

"Walikuwa wanaongelea kuhusu..."

"Mr. Dylan..."

Sauti hiyo ikamkatisha Fetty ghafla. Wote wakatazama mlangoni na kumwona Mr. Bernard akiwa amesimama hapo. Fetty aliingiwa na wasiwasi kiasi, huku Dylan akimpuuzia mzee na kuendelea kula. Mr. Bernard akaweka tabasamu la bandia na kuwasogelea. Fetty akarudi nyuma kidogo ili kuwaachia nafasi.

"Nani huyu?" Mr. Bernard akauliza.

"Ni rafiki yangu. Unasemaje?" Dylan akamuuliza.

"Aam... najua unaondoka, nilikuwa nimekuja kukuaga," Mr. Bernard akasema kinafiki.

"Kila mara nikiondokaga ofisini huwa hauniagi, kulikoni leo?"

"Ahahahah... ni kwa sababu unaenda mbali Mr. Dylan."

"Okay. Asante. Kuna kingine?"

"Aaaa... kuna paperwork nyingi sana za kufanyia kazi kutokana na mambo uliyoyaingiza hapa, sanasana insurance certificates na material orders. Process ziko slow, kwa hiyo..."

"Kampuni kufanya kazi primarily paperless ni kitu ambacho mlikuwa mnatakiwa kuwa mmefanya kitambo sana. Mbona ziko njia na system nyingi za ku-deal na document management, iwe ni categorization, due dates, project deadlines... tsk... acheni uvivu... em'... niache tu kwanza maana napata msosi hapa! Kadili na hayo masuala mwenyewe," Dylan akamwambia kwa kukereka.

Mr. Bernard alichukizwa sana na Dylan, kwa kuwa alihisi kwamba Dylan ni mtoto mdogo sana kuweza kumzidi akili namna hiyo, na hasa kwa sababu hakuwa ameitumikia kampuni kwa muda mrefu kama yeye. Akatoa tabasamu bandia, akijifanya mwema sana.

"Sawa nimeelewa.... boss," akasema Mr. Bernard kikejeli.

Dylan akamtazama kwa ukali, naye Mr. Bernard akageuka na kumwangalia Fetty. Akamshusha na kumpandisha, kisha akatoka ofisini hapo akiwa ameudhika. 

Dylan akatikisa kichwa chake na kuendelea kula. "Si ndiyo huyo weasel uliyekuwa unamsemea?" akamuuliza Fetty.

Fetty akasogea karibu zaidi na kukubali.

"Anajifanyaga anajua sana huyo. Yaani huwa namnyoosha, mpaka nitahakikisha hicho kitambi kinaporomoka," akasema Dylan.

"Ndiyo, anaonekana ni mwenye hila sana. Nilikuwa nakwambia..."

"Sir Dylan... helicopter imefika." 

Fetty akakatishwa tena na sauti hiyo nyingine mlangoni pale. Alikuwa ni mfanyakazi wa hapo.

"Already?" Dylan akashangaa.

"Ndiyo sir."

Dylan akashusha pumzi kwa kukwazika, kisha akasema, "Okay fine, nakuja. Nenda waambie ninakuja."

"Okay sir."

Mfanyakazi huyo akaondoka, kisha Dylan akamwangalia Fetty.

"Time's up (muda umekwisha)," Dylan akasema huku anatabasamu.

Fetty akawa anamwangalia machoni kwa hisia.

"Asante kwa chakula. Nimefurahia ijapokuwa hawa wahuni wananiwahisha mno," akasema Dylan huku anatoa wallet yake.

Akampatia Fetty laki moja. 

Binti akashangaa. "Dylan, nini hiki?" akamuuliza.

"Najua, najua. Haijafika milioni moja uliyosema jana. Usijali nikirudi nitamalizia deni," Dylan akatania.

"Lakini Dylan... mbona unapenda kuchezea pesa sana?" Fetty akauliza.

"Sijazichezea. Nimekupa wewe. Ikiwa huzitaki fanya lolote lile unaloona ni sawa, maana siyo zangu tena... ni zako," Dylan akamwambia huku anachukua simu yake.

Fetty akakosa cha kusema. 

Dylan akamshika shavu lake la kushoto, kisha akambusu la kulia. "Tutaonana tena my friend... ngoja niwahi," akamuaga.

Fetty alikuwa anamtazama kwa hisia nyingi sana. Hata lile wazo la kumwambia kuhusu alichosikia Mr. Bernard anasema kwenye simu, likatoweka. Akili yake na hisia zake zilikuwa zimesharuka mbali kutokana na kupenda sana mambo yote Dylan aliyoyafanya kwa ajili yake. Mwanaume akachukua rimoti na kuzima TV, kisha akaelekea mlangoni na kumgeukia Fetty, akiachia tabasamu la kirafiki. 

"Usipotee tena ukitoka," Dylan akasema, kisha akaondoka sehemu hiyo.

Fetty alibaki ofisini hapo, akiwaza kuhusu jinsi Dylan alivyokuwa mwenye kumfanya ajihisi wa pekee sana. Akajishika shavu lake, akikumbukia jinsi midomo ya jamaa ilivyolipiga busu laini iliyomsisimua kwa kiasi fulani. Akakusanya vyombo vyake, kisha akaondoka kutoka kwenye jengo hilo ili arudi kule mgahawani.

Njia nzima kurudi huko alimfikiria tu Dylan, na sasa jambo moja likawa wazi kwake. Alimpenda. Akatabasamu kwa hisia nyingi sana za upendo wa dhati aliohisi kumwelekea, akijishauri akilini mwake kuwa pindi ambapo mwanaume huyo kijana angerudi, angemfunulia kilicho moyoni mwake.


★★


Upande wa juu kabisa wa ghorofa, helicopter ilisimama hapo huku chuma lake la juu likizunguka kwa kasi. Dylan akawa amefika hapo na kumkuta baba yake, Gilbert, akiwa pamoja na wanaume wengine watatu. Wakaongea naye kuhusu safari hiyo, wakimtakia mkutano na kazi njema huko ambako angeenda. Akaagana na baba yake pia, akimwambia amfikishie heri zake mama yake pia, ambaye alikuwa bize na mambo fulani.

Kisha, Dylan akaongozana na mwanaume mmoja kati ya wale waliokuwa hapo mpaka kwenye helicopter na kupanda pamoja naye. Rubani alikuwa ni mwanaume mzungu, naye akasalimiana nao, kisha akaanza kuinyanyua helicopter angani. Gilbert akawa anampungia mkono mwanaye, na baada ya helicopter kufika mbali, akarejea kwenye ofisi yake.

Zilipita dakika chache wakiwa angani, nayo helicopter ikatua chini. Dylan akauliza mbona kama wamewahi sana, naye rubani akasema kuna mtu fulani alikuwa anampitia hapo. Na kweli akafika mwanaume mmoja, ambaye alijitambulisha kuwa rafiki wa rubani huyo aliyeelekea mkoa walioenda pia, hivyo wakamkaribisha vyema na helicopter ikarudi angani. Dylan alijitahidi kuongea nao na kuwafanya wapendezwe naye sana kwa kuwa alifurahisha mno. Wakaendelea kupiga story huku mara kwa mara wakiangalia jinsi mwonekano wa kule ardhini ulivyopendeza kutokea angani.

"Naona kama vile ni ngumu sana," akasema mwanaume wa kwanza.

"Hapana siyo ngumu wala," Dylan akajibu.

"Ulishawahi kujaribu?" mwanaume wa pili akamuuliza.

"Ndiyo tayari. Ni rahisi mno kama hauogopi kupita kiasi," Dylan akasema.

Walikuwa wanaongelea kuhusu jinsi ya kutumia parachuti. Mwanaume wa kwanza hakujua jinsi ya kutumia, na alifikiri ni ngumu sana.

"Hata humo kwenye hilo begi imo," akasema mwanaume wa kwanza.

"Ee ndiyo. Yaani unavaa, halafu... ngoja nikuonyeshe," akasema Dylan.

Kisha akafungua mikanda ya usalama aliyokuwa ameifungia mwili wake, na kulichukua begi la parachuti ili awaonyeshe mfano.

"Mr. Dylan, kuwa mwangalifu!" mwanaume wa kwanza akamwonya.

"Usihofu, niko sawa."

Akalivaa begi hilo.

"Okay, umeona... hizi kanda unazifunga tu ili kubana mwili wako na begi, halafu hiki kikamba ndiyo unachotakiwa kukivuta wakati unataka kulifungua parachuti," Dylan akawaelezea.

"Eeeh ndiyo naonaga wanafanya hivyo. Wanapovuta begi linakuwa kama linachanika," akasema mwanaume wa pili.

"Ahahah... siyo kuchanika, per say... yaani inakuwa ni kama inaifungua zipu ili parachuti litoke," akasema Dylan.

"Ahaaa... kwa hiyo unapovuta, inafunguka halafu inatoka?"

"Ndiyo. Kwa mabegi mengine inakuwa kama inaisukuma kwa juu, kwa hiyo ukivuta ina...."

Ghafla helicopter ikatoa kishindo cha nguvu sana kutokea juu! Wote walishikwa na taharuki kwa kutoelewa nini kilikuwa kinaendelea. Helicopter ikaanza kupoteza mwelekeo mzuri na kuanza kuzunguka bila mpangilio maalumu, huku rubani akijitahidi kuidhibiti bila mafanikio. 

Kwa kuwa Dylan alikuwa ameifungua mikanda maalumu ya usalama kutoka mwilini mwake, aliweweseshwa huku na huku, akijitahidi kujiweka sawa ili atulie sehemu moja, lakini akawa anashindwa. Wengine walipiga kelele wakiuliza nini kinatokea, na sasa kasi ya kuzunguka ya helicopter ikazidi. Hii ikasababisha lock ya mlango wa helicopter ijifungue na kumrusha Dylan nje kwa nguvu sana!

Kwa kuwa wengine walikuwa wamekazwa na mikanda kwenye siti zao, hawangeweza kutoka hapo hata kidogo. Walihofia sana kuhusu uhai wa Dylan, na usalama wao pia.


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next