Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

 

SONGA NAYO................

"It's him, it's him" Ni mwanamke mmoja alikurupuka kutoka kwenye ndoto ya kweli ambayo haikuwa njema kwake akiwa anasisitiza kwamba ni yeye, ni yeye. Aliyekuwa anaota ndoto hiyo alikuwa ni yule mwanamke ambaye ndiye pekee alifanikiwa kuishi na kuachwa hai kule msituni. Ni masaa mengi yalikuwa yamepita lakini tukio lile halikufutika kwenye kichwa chake ndiyo maana hata alipo shtuka wakati huo alitoka kulikumbuka lile tukio huku akiwa anapiga makelele kutoka kwenye kitanda ambacho alikuwepo. Sarah ndilo lilikuwa jina lake halisi mwanamke huyo, ndiye pekee aliishi miongoni mwa wale wanajeshi wote ambao walikuwa wametumwa kuweza kumtafuta mwanaume yule ndani ya msitu ule mzito.

Mwili wake ulikuwa unatoka jasho kila mahali kiasi kwamba alilowanisha mpaka shuka ambalo alikuwa amelalia. Bado hakuwa na utulivu, alikuwa akitetemeka na kila alipo likumbuka tukio lile alizidi kuwa na wasiwasi zaidi ya mwanzo. Alijipapasa kila sehemu ya mwili wake na kugundua kwamba alikuwa salama kabisa lakini mwili wake ulikuwa na maumivu makali ndani yake ambayo bila shaka aliyapata kutoka kwa mtu yule. Akiwa kwenye kitanda hicho alihisi kuna hatua za mtu zinamsogelea kwa sababu alikuwa anashangaa yuko wapi wakati huo, bado akili yake haikuwa imetulia vizuri.

Mbele yake alimuona mwanajeshi mmoja ambaye hawakusafiri naye kwenda kuifanya ile kazi ambayo iliwapeleka ndani ya ule msitu. Mwanaume yule alikuwa na kikombe cha maji mkononi mwake ambapo alimpatia Sarah aweze kunywa ili kutuliza akili yake. Aliyagida maji yote na kutua kikombe chini akiwa anahema.

"Maneno ambayo umeyaongea hapa nimeyasikia mimi pekeyangu, hakuna mtu mwingine yeyote yule hivyo nahitaji uniambie ukweli kwamba ni nani huyo ambaye amekujia ndotoni kiasi kwamba umeogopa namna hiyo?" Sarah alishtuka, hakutarajia kukutana na swali kama hilo kwa wakati huo, lilikuwa ni jambo la hatari kama ukweli ungejulikana kwamba mhusika wao hakuwa amekufa bali alikuwa hai na mzima wa afya kabisa.

"Hakuna kitu ni ndoto ya kutisha tu Nick"

"Sio kweli, kwa mwanajeshi kama wewe huwezi kuota ndoto ya kufikirika ikakupa hofu namna hiyo na ukumbuke wewe ndiye pekee ambaye umekutwa upo hai ndani ya ule msitu. Unataka kuniaminisha kwamba mhusika ambaye amefanya tukio hili alifanya makosa ya bahati mbaya kukuacha wewe pekeyako hai na wengine wote wakauawa tena kikatili namna ile? Kumbuka kwamba baada ya hapa unaenda kwenye chumba cha mahojiano ili ukaeleze nini kilitokea kule kwa sababu mtu ambaye mlimfuata alikufa, sasa huyo ambaye aliua watu wote kasoro wewe alikuwa nani na kwanini ni wewe pekee ndiye ambaye ulifanikiwa kuishi kule? Niambie ukweli ili nijue namna sahihi ya kuweza kukusaidia" Sarah alimwangalia kwa umakini bwana huyo tena kwa utulivu wa hali ya juu.

"Unahisi kuna nini labda Nick?"

"Hakuna utulivu nadhani taarifa imefika mpaka kwa mkuu wa majeshi juu ya kilicho tokea, kila mtu anahitaji kujua ni jambo gani lilifanyika mpaka kufikia hatua ya yale yote kutokea nje ya mpango ambao ulikuwepo" Sarah bado ni kama alikuwa gizani, alitamani kumsimulia bwana huyo juu ya kile ambacho kilitokea lakini nafsi yake ilikuwa inagoma, aliikumbuka kauli ya yule mwanaume ambaye alimuacha hai kule msituni alivyo mpa maelekezo kama angeweza kusema jambo hilo mahali popote na kile ambacho angekifanya! Nafsi yake iligoma kabisa kuwa shahidi na kuelezea kwamba alimuona mtu wa aina kama ile akifanya tukio la namna ile.

"Kitu cha mwisho ninacho kikumbuka ni kwamba nilikuwa napigwa na kiongozi wangu kule msituni mpaka nikapoteza fahamu" alidanganya

"Sijakuelewa bado, yaani kwamba Michael ndiye ambaye alikuzimisha wewe?"

"Ndiyo"

"Hili linawezekanaje?"

"Tulipishana nilipo mwambia kwamba kile ambacho tunakifanya hakikuwa sahihi, yule alikuwa binadamu mwenzetu hivyo tungetumia njia nyingine kumuua sio ile na hatukuwa na uhakika asilimia miamoja kama kweli alikuwa na mtuhumiwa wetu hapo ndipo ugomvi ulipo anzia" mwanaume huyo ambaye alijulikana kama Nick alitabasamu kwa sababu Sarah alikuwa anamdanganya mchana kweupe.

"Sarah kama ulizimia maana yake hukuona kile ambacho kilitokea, nilipo kueleleza kuhusu mauaji ya wenzako haujaonyesha hata mshtuko ikiwa na maana kwamba ulishuhudia kilicho tokea na huenda ndicho ambacho kimekupa hofu namna ile. Najua unanidanganya lakini kwenye mahojiano usije ukafanya huo upumbavu kwa sababu utaingia kwenye matatizo mazito, itengeneze stori yako vizuri ili ukaeleweke, wanajeshi waliokufa ni wengi hivyo usitegemee kwamba itakuwa kirahisi tu namna hiyo lazima watataka kujua kila ambacho kilitokea na siku ambayo utakuwa tayari kuniambia kilicho tokea basi nitafute nitakusikiliza na kuangalia namna ya kukusaidia" Nick alimpiga piga begani Sarah kwa sababu alijua kabisa anamdanganya hivyo alimpa msaada wa kutaka aitengeneze vizuri hadithi yake hiyo ili asije kujiingiza kwenye shimo baya. Sarah alihema kwa nguvu, jambo hilo hakuwa tayari kumwambia mtu yeyote yule kwa gharama na namna yoyote ile.

 

******************

Sarah Martin, ndilo lilikuwa jina lake mwanamke pekee ambaye alifanikiwa kupona ndani ya ule msitu ambako wenzake wote waliuawa kikatili. Msitu wa Mau, upatikanano nchini Kenya ndiko ambako mambo yote hayo yaliweza kutokea, msitu wa Mau ndio msitu mkubwa na mnene zaidi ndani ya nchi ya Kenya na ndiko ambako mambo yote hayo yaliweza kufanyika. Sarah baada ya kuzimishwa ndani ya ule msitu baadae alikuja kuzinduka hali yake ikiwa ni mbaya ndipo alipoamua kupiga simu makao makuu kuweza kuomba msaada na kuelezea kwamba hakuwa na uhakika kama kuna mwingine alikuwa amepona zaidi yake.

Msaada ulifika lakini ilikuwa ni baadae sana, kitu ambacho kilishuhudiwa ndani ya hilo eneo kilikuwa kinatisha kwa sababu yalikuwa ni mauaji tu pekee ambayo yalitamalaki na mtu ambaye alikuwa hai alikuwa ni huyo mmoja tu pekeyake. Sarah wakati huo ndipo aligundua sababu halisi ya muuaji yule kuweza kumpiga namna ile kiasi kwamba alipoteza mpaka fahamu. Kuwa kwenye hali kama ile haikuwa sababu pekee ya kufanya jambo hilo liishe kirahisi, ilikuwa ni lazima afanyiwe uchunguzi wa kutosha pamoja na kuhojiwa kwa kina ili aweze kueleza kinaga ubaga kwamba ni jambo gani lilitokea huko wakati ni wazi mhusika wao walifanikiwa kumkamata na kumuua na ushahidi wote wa picha na video ulikuwepo.

Baada ya kuzinduka tu Sarah ndipo alikutana na mwenzake huyo Nick ambaye alimpa ushauri wa kuweza kuitengeneza vizuri hadithi yake ya uongo hiyo kwani kama wakubwa wake wangegundua kwamba kuna kitu anakificha basi alikuwa anapewa kesi nzito ya kuwauza ama kuwasaliti wenzake. Alijua yeye kuumia pekee na ndiye ambaye alipona isingekuwa rahisi kuwaaminisha wakubwa zake kwamba lile tukio yeye hakuelewa lilitokeaje, alitakiwa kulidadavua kwa kina Sarah ila abadani hakuwa tayari kuelezea uhalisia wa namna tukio hilo lilivyo fanyika.

Sarah baada ya mahojiano alikuwa amerudi nyumbani kwao, kambi yao ilikuwa ndani ya jiji la Arusha lakini yeye alikuwa amejenga ndani ya Moshi ambako ilikuwa ni asili ya mama yake mzazi. Kwenye jumba lake alikuwa akiishi yeye, mama yake pamoja na mdogo wake mmoja ambao walikuwa wakimtegemea yeye kwa kila kitu kuanzia kuvaa mpaka kulala. Majira ya jioni alikuwa amerudi nyumbani kwao baada ya kupata nafuu na kupewa likizo kambini, kurudi kwake nyumbani kulimpa nafasi ya kutuliza akili yake na kutafakari mambo mengi ambayo yalikuwa yametokea. Aliwahi kuwepo kwenye baadhi ya mataifa ambayo hayaishi vita kila siku na mauaji yalikuwa yanafanyika kwa wingi ila jambo ambalo alilishuhudia kwa wenzake lilimtisha na kumfanya kila akilikumbuka mwili wake kuanza kutetemeka kwa nguvu kiasi kwamba ikawa kama ni ndoto mbaya kwake ambapo kuna wakati ilikuwa inamfanya atetemeke.

Alikuwa dirishani juu ya nyumba yake hiyo ya ghorofa moja akiwa amelifunua pazia na kuuangalia kwa mbali mlima mkubwa na mrefu zaidi ndani ya bara la Afrika ambao ulikuwa unavutia na kuifanya mandhari hiyo kuwa bora na ya kupendezesha kwenye macho yake, fahari ya mlima Kilimanjaro. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha kahawa ili kuweza kushindana na baridi kali ambalo lilikuwepo huko Moshi. Mkono wake ulikuwa unatetemeka kiasi kwamba yeye mwenyewe akawa anajishtukia, alishtuka baada ya kusikia sauti nyuma yake kiasi kwamba mpaka kile kikombe kikataka kumponyoka! Ilikuwa ni sauti ya mama yake.

"Una shida gani binti yangu? Sijawahi kukuona una wasiwasi kiasi hiki kwenye maisha yako tangu siku umezaliwa, nini kinakusumbua mama yangu?" ilikuwa ni ghafla na hakutarajia kitu kama hicho hivyo alipata wasiwasi mno kiasi kwamba alikosa jibu la haraka la kumjibu mama yake. Alijichekesha ili kumtoa wasiwasi mama yake lakini hali ya mkono ndiyo ambayo ilikuwa inamdhalilisha, ilimlazimu kukitua chini kikombe hicho kwenye meza ndogo ambayo ilikuwa karibu na dirisha kisha akasogea kumkumbatia mama yake.

"Nawaza kuhusu kazi mama, kazi yetu hii imebeba hatima ya maisha ya watu wengi kwenye mikono yetu hivyo kila wasaa nawaza nisije kufanya kosa la namna yoyote ile nikashindwa kuyaokoa maisha ya watu wengi" 

"Binti yangu wewe ni moja kati ya wazalendo wakubwa kwenye taifa hili, tangu ukiwa mdogo siku zote umekuwa ukijitoa kwa watu kwa ukubwa hata kama wewe utaumia na ndiyo maana kwenye kabati lako umejaza zawadi za mfanyakazi bora ambazo ulikuwa unapewa na viongozi wako hivyo mimi nakuamini kuliko mtu yeyote yule na unatakiwa kujua kwamba wewe ni bora kwa kila kitu" mama yake alimpa maneno mazito na yenye ujumbe ulioshiba kumpa tumaini mwanae.

"Asante mam...." hakuimalizia sentensi yake alihisi kuna kitu hakipo sawa, alichomoka kwenye mkono wa mama yake na kukimbilia nje akiwa anaichomoa bastola kwenye kiuno chake. Haikuwa kawaida kuhisi jambo zito namna hiyo huku moyo ukiwa unamuenda mbio kwa nguvu, ni hisia ambazo zilimpa hali hiyo akajua kabisa hapakuwa sawa kwenye hiyo nyumba yao lakini baada ya kufika nje aliona kivuli kikiwa kinaishia kwenye mti fulani ambao ulikuwa karibu na uzio mrefu wa fensi. Alitamani kumfuatilia mtu huyo lakini alisita baada ya kukutana na begi hivyo akalifungua haraka kujua kulikuwa na nini ndani yake, hakuwa na wasiwasi ya kukutana na kitu cha ajabu kwa sababu hakuwahi kuwa kwenye ugomvi na mtu yeyote yule na hakuna mtu ambaye alikuwa anajua ni wapi yeye anaishi.

 

Ni nani tena huyu ambaye amemtembelea Sarah mpaka nyumbani kwake ikiwa ndo kwanza amerudi? Alikuwa na lengo naye lipi? Unatamani kujua kwamba lile begi lilikuwa na kitu gani ndani yake?

 

Kwa leo sehemu ya tatu inaishia hapa, tukutane ndani ya sehemu ya nne wakati ujao.

 

FEBIANI BABUYA.

Previoua Next