Reader Settings

DYLAN

Story by Elton Tonny

Familia, Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Unyanyasaji, Usaliti, Visasi, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

(R-rated 18+)

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA TANO

★★★★★★★★★★★★★★★


Dylan aliendelea kudondoka kuelekea chini kwa kasi, huku mwili wake ukizunguka-zunguka ovyo ovyo sana. Alikuwa akijaribu kuishika kamba ya kuvutia parachuti ili lifunguke kutoka kwenye begi, ambalo bado lilikuwa mgongoni kwake, lakini akawa anashindwa kuipata kutokana na upepo kuirusha huku na huku. Alianza kuona kuwa alikaribia chini zaidi sasa, na kwa ustadi akajikunja na kujibinua angani hapo ili aweze kuuweka mwili wake sawa, kisha akafanikiwa kuishika kamba hiyo na kuivuta kwa nguvu. 

Parachuti lilifunguka, lakini kutokana na kasi yake lilipofunguka, ilifanya mwili wa Dylan urudi juu kidogo kwa kushtukiza, hivyo kasi yake ya kudondoka ikapungua, lakini tatizo lingine likatokea. Kwa kuwa hakuwa ameifunga mikanda ya begi kifuani, ilifanya mikono ya begi iteleze kutoka mabegani kwake na hivyo begi hilo kumtoka mgongoni!  Alikuwa amekaribia chini sana, na baada ya begi kumtoka, akaanza kuanguka huku anapiga kelele za hofu.

Mwili wake ulidondokea kwenye kamba nene iliyokuwa ya kivuko/daraja refu la kamba, ambalo lilikuwa juu katikati ya miamba miwili mikubwa ya bwawa pana sana la maji yenye kina kirefu. Baada ya kujigonga hapo, akaanza kuangukia chini huko na kudumbukia ndani ya bwawa kwa nguvu sana, na mwili wake ulipokuwa unazama chini, kichwa chake kikajigonga kwa nguvu kwenye jiwe kubwa ndani ya maji hayo.

Upande wa helicopter, rubani alijitahidi sana kurudisha chombo hicho kwenye utaratibu mzuri, lakini jitihada zake zikaendelea tu kugonga mwamba. Helicopter iliendelea kuzunguka na kwenda ovyo ovyo, na kwa dakika kadhaa baadaye, ikaishiwa nguvu yote na kuanza kuelekea chini kwa kasi sana; hapo ikiwa imevuka mikoa michache toka ilipoanza kuleta shida. Kwa kusikitisha sana, iliangukia sehemu ya mbali ambayo ilikuwa na mlima, na yote ikalipuka.


★★★


Huzuni, simanzi na majonzi vilitawala familia nzima ya Dylan baada ya kuwa wamepata taarifa kuhusu ajali iliyompata kijana huyo. Walisafiri haraka kuelekea mkoa ambao helicopter iliangukia, na baada ya kufika huko, waliweza kuonyeshwa miili mitatu ambayo ilikuwa imeungua sana na kuwa myeusi yenye kutisha. Gilbert alikumbuka kuwa, Dylan alipanda helicopter pamoja na mwanaume mwingine wa kampuni yao, hivyo ukijumuisha na rubani bila shaka walikuwa watatu. Kwa hiyo kwa haraka wote wakajua kwamba Dylan pia alikuwa amepoteza maisha kwenye ajali hiyo. Walilia sana.

Camila pamoja na mchumba wake walikuwepo pia, naye alimwombolezea mpwa wake kwa uchungu mwingi sana moyoni, ukitegemea hawakuwa wameachana kimtazamo mzuri.

Walifanya msiba baada ya siku chache, kukiwa na ndugu na marafiki wa karibu waliofika kuwafariji. Aliyepoteza matumaini kabisa alikuwa ni Jaquelin. Hakula vizuri, hakuongea, angelia mara kwa mara na kuanza kupiga-piga vitu walipokuwa nyumbani, na hakutoka nyumbani kwa siku nyingi. Muda mwingi angelala tu kitandani akiwa anaangalia picha za Dylan huku analia kwa huzuni, na mambo yote haya yalimvunja sana Gilbert.

Fetty aliumia sana. Alihisi ni kama mikosi kwake isingeisha kamwe. Dylan alikuwa ni kitu kizuri sana kuwahi kuingia kwenye maisha yake. Kuna msemo wa kwamba mtu huwa hatambui umuhimu wa kitu alichonacho mpaka anapokuja kukipoteza, naye Fetty alihisi ni kama msemo huo ulimfaa yeye kwa sababu ijapokuwa nafasi ilikuwepo kabisa ya kuwa pamoja na Dylan kimahusiano, hakupiga hatua hiyo. Hivyo alijilaumu kwa kuona alikuwa akichezea muda tu wakati angekuwa ameshamwambia mapema kuwa alimpenda. Kutokea hapo, mwanadada huyu hakuwa na furaha tena moyoni, kwa kuwa kitu kilichompatia furaha kilikuwa kimepotea.

Camila alirudi Brazil na mchumba wake baada ya miezi mitatu. Hawakuwa wamepanga kukaa muda mrefu hivyo, lakini baada ya mambo hayo yasiyotazamiwa kutokea, Camila alihitaji kuwa na ndugu zake karibu zaidi. Lakini kwa kuwa walihitaji kuendelea na kazi, ilibidi warudi Brazil sasa; Camila akimuahidi Jaquelin na Gilbert kuwa angeendelea kuwasiliana nao kila siku.

Kufikia wakati huu, Gilbert alikuwa anaendelea kujitahidi kuweka mambo sawa kwenye kampuni, kwa kuwa baada ya Dylan "kufa," mipango mingi iliyokuwa ikiendeshwa naye iliharibika. Ijapokuwa Gilbert alijitahidi sana kuongoza mambo vyema, vizuizi vya kimakusudi kutoka kwa watu waliotaka aporomoke vilimrudisha nyuma; na wakati huu ilikuwa ni kama anapoteza mwelekeo kwa kuhisi yuko mwenyewe. Jaquelin alianza tena kwenda kwenye kampuni, lakini akili yake haikukazia fikira kabisa kazi, bali ni mwili wake tu ndiyo ulikuwa pale.

Maisha ya wawili hao yaliendelea kuwa yenye misukosuko zaidi kadiri siku zilivyoendelea kwenda, na haikuonekana kama wangeweza kupata kitulizo tena.


★★★


Dylan anafumbua macho yake taratibu, akiwa anahisi kama ametoka kwenye usingizi mzito. Anatazama sehemu aliyopo na kutambua ni ndani ya chumba fulani. Anapojaribu kugeuza shingo, anahisi maumivu yanayofanya akunje sura yake kwa hisia za kuumia. Kichwa chake kinamuuma sana, naye haelewi kwa nini iko hivyo.

Kisha anasikia sauti pembeni yake ikisema, "Ameamka... nyie... ameamka..." 

Anatambua sauti hii ni ya mvulana mdogo, lakini hawezi kumwona kwa kuwa hawezi kuigeuzia shingo yake upande huo. 

"Emmy, kamwite dokta..."

Anasikia sauti hiyo nyingine ikisema hivyo. Hii ni ya mwanaume mtu mzima, lakini hatambui ni nani. Kisha hapo hapo mwanaume fulani anasogea karibu na uso wake na kuanza kumwangalia-angalia usoni mwake. Hamtambui hata kidogo, kisha anakuja mwanaume mwingine na kuanza kumkagua usoni; analimulika jicho lake kwa tochi ndogo, anatumia kifaa cha kusikilizia mapigo ya moyo kusikiliza ya kwake, kisha anamuuliza Dylan anahisije mwilini.

Dylan akaanza kuzungusha macho huku na huku bila kutoa jibu lolote. Mwanaume huyo, daktari, akaanza kuongea na yule mwanaume mwingine pembeni. Alikuwa anamwambia kwamba mgonjwa anaonekana kuwa na shida kwenye ubongo, hivyo angehitaji kupelekwa hospitali kubwa zaidi. Dylan akamsikia mwanaume huyo mwingine akimwambia daktari kuwa hana pesa ya kumgharamia na kumpeleka kwenye hospitali kubwa, kwa kuwa alimpata tu akiwa kwenye hali mbaya, hivyo akamsaidia na kumleta hapo kwenye zahanati hii.

Mwanaume huyo akamuuliza daktari shida ya mgonjwa kwenye ubongo ni nini, naye daktari akasema atahitaji kumfanya mgonjwa aongee ili aweze kuwa na uhakika zaidi, ndipo atoe jibu. Dylan alisikia vizuri walichokuwa wanasema, lakini HAKUELEWA kilichokuwa kinaendelea. Daktari akamsogelea tena, halafu akanyanyua vidole viwili mbele ya uso wa Dylan huku anamwangalia kwa makini.

"Hii ni ngapi?" daktari akauliza.

Dylan akaukazia macho mkono wa daktari, kisha akasema, "Mbili."

Daktari akafurahi kuona ameweza kuongea na kutoa jibu kwa usahihi, kisha akamwangalia macho tena kwa kuyavuta-vuta.

"Unaitwa nani?" daktari akamuuliza tena huku anamwangalia.

Dylan akafungua mdomo ili ajibu, lakini akabaki ameachama bila kutoa neno lolote. Akaanza kupeleka macho huku na huku, akionekana kutafuta jibu. Daktari akarudia tena kumuuliza jina lake ni nani, lakini Dylan akawa amekunja tu uso huku anaonyesha kutangatanga kiakili. Daktari akamtuliza kwa kumwambia asijilazimishe maana kichwa kingeanza kumuuma, kisha akamgeukia yule mwanaume aliyemsaidia Dylan.

"Inaonekana atakuwa amepoteza kumbukumbu," daktari akamwambia.

"Mh! Sasa itakuwaje?" mwanaume huyo akauliza.

"Tumchukue tumpeleke nyumbani," akajibu mvulana yule mdogo.

Mwanaume huyo akamwangalia Dylan kwa wasiwasi. "Sasa dokta, ikiwa anaweza kukumbuka namba mbili, anashindwaje kukumbuka jina lake?" akauliza.

"Aa... kumbukumbu ni pana. Na mara nyingi kwenye visa vya kupoteza kumbukumbu, watu husahau hasa mambo mengi kuhusu maisha waliyoishi, lakini vitu vichache walivyofundishwa mara nyingi hubaki kwenye ubongo. Ndiyo maana unaona hajasahau kiswahili," daktari akaeleza.

"Ee ndiyo baba. Ndo' maana unaona anaweza kuongea, la sivyo asingesema chochote," akasema binti ya mwanaume huyo, aliyeitwa Emilia.

"Hahah... angekuwa kama litoto anafanya bhabhabha..." akasema mvulana yule, na wote wakacheka kidogo (isipokuwa Dylan).

"Nini kinaendelea? Nimefikaje hapa? Kwa nini sikumbuki vitu?" Dylan akauliza kwa wasiwasi.

Daktari akamsogelea na kusema, "Pole sana. Inaonekana ulipatwa na ajali, na sasa... ukaangukia vibaya jiwe kubwa na kukipiga kichwa chako kwa nguvu. Kwa hiyo sehemu kubwa ya ubongo wako iliyotunza kumbukumbu imevurugika," daktari akaelezea.

"Ajali? Jiwe? Mbona sikumbuki?" akasema Dylan kwa kuchanganywa.

"Usijali. Tatizo hili litaisha baada ya muda fulani kupita. Atahitaji dawa za kusaidia maumivu ya mishipa ya shingo, nitakuandikia," daktari akamwambia mwanaume yule.

Kisha daktari akaondoka kwenda kwa wagonjwa wengine, akiwaacha wote hapo.

"Sasa baba, kama amepoteza kumbukumbu atarudije kwao?" Emilia akamuuuliza baba yake kwa sauti ya chini.

"Nitamsaidia kupatafuta alikotokea. Nafikiri kuna watu eneo hili wanaomfahamu," baba yake akajibu.

Dylan alikuwa anaangalia huku na huku kwa wasiwasi, akijaribu kuvuta picha ya mambo mengi, lakini anashindwa kukumbuka. Mwanaume huyo akamsogelea na kuketi kitandani akimwangalia, naye Dylan akamwangalia pia.

"Hujambo? Naitwa Baraka, mimi ndiyo nilikusaidia na kukuleta hapa," mwanaume huyo akasema.

"Asante. Nini kilinipata?" Dylan akauliza kwa hisia.

"Sijui kwa kweli. Nilikuwa kwenye mtumbwi na mwenzangu, tukijaribu kuvua dagaa wachache bwawani. Nikakuona ukiwa chini ya maji kwa sababu ya shati lako jeupe... kwa hiyo tukakutoa, na ulikuwa umepoteza fahamu. Kichwa chako kilikuwa kimevimba kwa nyuma huku damu zinakutoka, kwa hiyo tukakuwahisha hapa kwa sababu bado ulikuwa hai..." Baraka akaelezea.

Dylan akanyanyua mkono wake na kujishika kichwani. Akatambua alikuwa amefungwa bendeji kuzungukia kichwa chake, kisha akafumba macho kwa huzuni.

"Haukumbuki kitu chochote kabisa?" akauliza Emilia.

Dylan akafumbua macho na kumtazama Emilia. Aliweza kumwona akiwa amesimama pembeni kidogo, huku akiwa ameikunjia mikono yake kifuani.

"Kuna vitu najua. Najua wewe ni msichana... najua hiki ni kitanda... najua hapa tuko hospitali... aam, zahanati..." Dylan akasema.

Baraka akatabasamu kwa kutambua kuwa Dylan alikuwa mwerevu.

"Lakini vitu vingi vya maisha yangu sivijui... aah... ni hisia mbaya sana," akasema Dylan.

Wote walimwonea huruma sana.

"Usihofu. Kama dokta alivyosema, usijilazimishe... itarudi yenyewe. Jipe tu muda," Baraka akamtia moyo.

Dylan akashusha pumzi taratibu, kisha akauliza, "Nimekuwa hapa kwa muda gani?"

"Siku... sita. Tokea tulivyokutoa kwenye maji," Baraka akajibu.

"Haionekani kwamba nilikuwa humo muda mrefu?" Dylan akauliza.

"Hapana. Inaonekana ulidumbukia siku hiyo hiyo tuliyokutoa, la sivyo tungekuta umekufa," Baraka akamwambia.

Dylan akatulia kidogo.

"Hawa ni wanangu. Huyu ni Emilia, na huyu mdogo ni Steven," Baraka akawatambulisha wanaye kwa Dylan.

Dylan akatabasamu kidogo, na watoto wa Baraka wakatabasamu pia kirafiki.

Waliendelea kukaa na Dylan kwa muda fulani, kisha wakaondoka na kumwacha chini ya uangalizi wa wauguzi.


★★★


"Hivi kweli baba Leila... unawezaje kufanya uamuzi huo?" 

"Kwa hiyo unataka nimwache tu kijana wa watu?" akajibu Baraka.

"Ina maana hana familia? Waje wamchukue! Wewe unataka kutuletea hapa mtu ambaye hatumfahamu hata kidogo. Unajua vipi tabia zake? Je kama ni jambazi?" 

"Mama Leila, usiwe hivyo. Yule kijana anahitaji msaada. Hana pa kwenda kwa sababu hakumbuki maisha yake. Siwezi kumwacha tu mpaka nimsaidie arudi kwao..."

"Lakini si kuna watu maalumu wa kumtafutia? Kwa nini wewe? Umemmwokoa asizame, umempeleka zahanati, umemtolea hela ya matibabu ambayo tungetumia hapa nyumbani, inatosha. Sasa sa' hivi unataka tena kumleta hapa ili iweje? Aagh..."

Haya yalikuwa ni maongezi kati ya Baraka na mke wake. Ilikuwa imepita wiki moja sasa tokea Dylan alipoamka, na daktari alisema yuko vizuri kimwili kuweza kutoka zahanati hapo. Lakini shida ilikuwa kwamba Dylan hakukumbuka vitu, kwa hiyo hangekuwa na pa kwenda. Baraka alikuwa ametumia muda huo wa wiki kuulizia sehemu za maeneo yao ikiwa kuna kisa cha mtu kupotea, lakini hakupata mtu aliyeonekana kufahamu upotevu wa Dylan.

Baadhi ya watu waliofahamiana na Baraka walikuwa wameenda pamoja naye zahanati ili kumwona Dylan, lakini wote hawakumtambua hata kidogo. Sasa kijana huyo angetakiwa kuondoka zahanatini kesho, na Baraka alikuwa anafikiria kumpa hifadhi nyumbani kwake wakati wakiendelea kutafuta watu ambao wangemfahamu. Jambo hill lilikuwa limemkera sana mke wake, ambaye aliona ingekuwa kuongeza mzigo tu kwenye maisha yao ikiwa wangemleta Dylan hapo.

"Mimi ndiye nitakayewajibika kwa ajili yake. Wewe niamini mimi," Baraka akamwambia.

"Maisha yetu kama unavyojua ndiyo hivyo... hayaeleweki. Wewe kuanza kujifanya msamaria mwema kutaongeza tu..."

"Aagh mama Leila! Nimeshasema anahitaji msaada, na nitamwajibikia mimi. Hebu acha basi kulalamika... agh!" Baraka akamwambia akiwa ameudhika.

"Sawa, utajua mwenyewe," mke wake akamwambia kwa kukerwa.

Akatoka hapo kwenye kochi walilokuwa wameketi na kuelekea chumbani akiwa amekasirika. Baraka akabaki sebuleni akitafakari mambo kwa makini, bila kujua kwamba binti yake mkubwa, Leila, alikuwa akiwasikiliza kutokea pembeni akiwa amejibanza.

Baraka alikuwa na familia yenye mke mmoja na watoto watatu. Binti yake wa kwanza ndiye aliyeitwa Leila, na alikuwa na umri wa miaka 22. Binti yake wa pili aliitwa Emilia, naye alikuwa mwenye miaka 18. Mwana wake wa tatu aliitwa Steven, naye alikuwa na umri wa miaka 11. Jina la mke wake lilikuwa Shani, lakini alizoea kuitwa mama Leila na wengi.

Baraka alikuwa mwanaume mstaarabu sana. Alikuwa ana ujuzi wa masuala ya makarai; alitengeneza majiko ya vyuma, mageti, nguzo za chuma, na alirekebisha mambo mengi yaliyohusisha vyuma. Hii ndiyo iliyokuwa kazi yake tokea zamani sana ambayo ilimpatia kipato kidogo kwa ajili ya kutegemeza familia yake. Eneo waliloishi lilikuwa mbali kutokea na sehemu aliyofanyia kazi, ambayo ilikuwa kama soko dogo la biashara, ambako watu wengi walifanya kazi zao.

Mke wake, Shani, alikuwa mwanamke mwenye kujiamini na mkali kiasi. Mara nyingi ungekuta akiwafokea-fokea watoto wake kwa vitu vidogo vidogo tu, nao walikuwa wameshamzoea. Alikuwa anafanya kazi ya upishi, yeye kama maman'tilie, kwenye mgahawa wake mdogo eneo la soko lile la biashara. Alikuwa mwenye mwili mnene kiasi, lakini haukuwa na manyama mengi, bali uliofanya umbo lake lionekane vyema kwa kutokeza kalio lake kubwa vizuri kwa nyuma. Alipenda sana kuvaa nguo za kujiachia na kujiremba; ili kufanya aonekane kama binti mdogo bado!

Leila, binti mkubwa wa Baraka, alikuwa mwanamke mwenye kujiamini, mkaidi, na mwongeaji sana. Alikuwa amemaliza kidato cha nne miaka kadhaa nyuma na kwenda kwenye chuo cha ufundi, lakini akaachana na masuala ya shule ili akazie fikira biashara. Kwa kukosa kutengeneza mazingira mazuri ya biashara, alianza kufanya kazi kama mhudumu kwenye mgahawa fulani, tofauti na wa mama yake, na aliendelea kuwa hapo kwa miezi kadhaa. Leila alikuwa mwenye umbo zuri, nene kidogo lakini lililojikata kike sana, na hips na kalio lake vilitokeza vyema. Alikuwa na uso mzuri, naye alipenda kusuka rasta za kuchanganya rangi, na nguo nyingi alizopendelea kuvaa zilikuwa ni dera. 

Emilia, binti wa pili, alikuwa msichana mstaarabu, mpole na mwenye akili sana. Wakati huu alikuwa kidato cha nne, akikaribia kumaliza masomo ya sekondari. Alikuwa mzuri pia kisura na kitabia, huku umbo lake lililonona pia likiwatamanisha wanaume wengi, ambao walikuwa wamejaribu sana kupita hapo ila binti akawagomea. Alikuwa anajiheshimu, na alipatana vizuri sana na baba yake.

Kisha kuna dogo Steven, ambaye ni mwana, na mtoto wa mwisho wa Baraka na Shani. Alikuwa mvulana mjanja, mtundu, mwongeaji, na mwerevu pia. Alikuwa darasa la sita wakati huu, na alisoma kwa bidii pia ili afanikiwe kuingia darasa la saba mwaka ujao.

Hiyo ndiyo ilikuwa familia ya bwana Baraka. Alikuwa amejenga nyumba ya kawaida yenye vyumba vinne ndani; kimoja kama sebule, kimoja cha kulala yeye na mke wake, kimoja cha kulala Leila na Emilia, na kingine cha kulala Steven. Walikuwa na jengo lingine dogo kwa nje ambalo lilitumiwa kama jikoni, na choo na bafu vilikuwa nje pia.

Walikuwa na shamba kwenye eneo hilo hilo ambalo walipanda mazao fulani waliyotumia kama chakula na kufanyia biashara kwenye kazi ya Shani. Nyumba za majirani wengi hapo zilikuwa kwa umbali fulani kutoka kwa moja na nyenzake, hivyo hawakubanana hata kidogo. Ilikuwa ni eneo kwenye mwinuko mkubwa sana, ambao ulikuwa na bwawa kubwa sehemu za mbele, lililotenganisha mwamba wa eneo hilo na mwamba mwingine kufikia upande wa pili wa mtaa huo; ambao ndiyo ulikuwa wenye eneo la biashara.

Katikati ya bwawa hilo, kutokea kwenye kingo za miamba hiyo, lilijengwa daraja refu la kamba na shaba ngumu kama kivuko kufika upande mwingine, lakini kivuko/daraja hili lilikuwa limeharibika katikati kwa muda mrefu sasa, na halikuwa limetengenezwa. Wenyeji wa upande huu wa eneo hili waliloishi familia ya Baraka walikuwa wameshajaribu kuomba msaada kutoka kwa diwani wao, lakini kwa sababu fulani hakuwa ametoa msaada na kuwapuuzia tu. 

Ni daraja hili ndiyo ambalo Dylan aliangukia juu ya kamba yake ya kulishikilia siku ile aliporushwa nje kutoka kwenye helicopter, na wakati amedumbukia bwawani, Baraka alikuwa pamoja na rafiki yake kwenye mtumbwi wakitafuta dagaa kwa ajili ya chakula, ndiyo akaweza kumtoa baada ya kumwona kwenye maji.

Baada ya muda fulani, Baraka pia akaelekea chumbani ili kupumzika, baada ya kuwa amekorofishana na mke wake kuhusu kumleta Dylan hapo kwao. Ilikuwa ni usiku, hivyo walijua watoto walikuwa wamelala, pasipo kujua Leila alikuwa anasikiliza maongezi yao.


★★★


Asubuhi ilipofika, Baraka alielekea zahanati ili kumfata Dylan. Dylan angeweza kutembea vizuri, lakini kwa uangalifu sana ili asitie kichwa chake mtikiso ambao ungemuumiza, kwa kuwa alikuwa na kidonda kikubwa bado kichwani kilichofanya sehemu kubwa ya kichwa chake kufunikwa kwa bendeji. Baraka alimtoa huko na kumpeleka kwake, wakitembea mwendo mrefu sana. 

Alimkaribisha vyema kwake, kisha akamwekea maji ya kunywa, na baadaye ya kuoga. Akamwelekeza chumba ambacho angetumia, nacho kilikuwa kile alicholalia Steven. Kwa kuwa Baraka alikuwa na godoro la ziada, alimwambia Dylan kuwa angelala chini, kwa sababu hakukuwa na kitanda, na kitanda cha Steven kilikuwa kidogo. Dylan akasema hakuna shida, na kwamba anapenda kulala chini. 

Baraka akabaki anamwangalia kwa makini. "Umejuaje kwamba unapenda kulala chini?" akamuuuliza.

Dylan akamtazama Baraka, akiwa hajatambua kwamba alisema kitu fulani kuhusu utu wake bila kukaza sana fikra.

"Amm... sijui. Ahah... hiyo ni ishara nzuri, siyo?" Dylan akasema kwa shauku kiasi.

Baraka akatabasamu na kusema, "Ndiyo. Pole kwa pole... kumbukumbu yako itarudi."

Dylan alimshukuru sana Baraka kwa msaada wake wote aliompatia. 

Baada ya hapo alienda kuoga, kisha akarejea na kupata chakula. Baraka alikuwa amempatia baadhi ya nguo zake ili awe anavaa, naye alimwelezea Dylan kuhusu watu wa familia yake, na baadaye kijana akapata kuwatambua vizuri baada ya kuwa wamerudi. Emilia na Steven walimwonyesha Dylan roho ya ukarimu kwa kumkaribisha vizuri, lakini Shani pamoja na Leila hawakuonyesha upendezi wowote kumwelekea Dylan. 

Ijapokuwa alitambua kwamba siyo wote wangempokea vyema, alijitahidi kuwa mtaratibu na mwelewa; akitumaini kuweza kukumbuka maisha yake ya zamani haraka ili asiwabane tena.

"Kaka haitatosha baba. Tumtungie jina," akasema Steven, wakati wote wakiwa wameketi sebuleni pamoja.

"Ahahah... tumtungie jina gani sasa?" akauliza Baraka.

"Lolote tu. Kumwita kaka haifai kwa sababu siyo kaka yao," akasema Shani kwa njia yenye kuvunja moyo.

Leila alikuwa bize ku-chat tu, nao wengine walitambua Shani alisema hivyo kwa nia mbaya.

"Achague Steven. Ungependa uniiteje?" Dylan akasema.

"Mmmm... jina gani, jina gani, jina ganiii.... Tumwite ISHENGOMA!" akasema Steven kwa uhakika.

Wote wakacheka, huku Dylan akishangaa jina hilo.

"Ishwegwama?" Dylan akauliza.

"Ahahahah... kwa nini unataka tumwite hivyo?" Emilia akamuuuliza Steven.

"Jina la kibabe. Kama yule Ishengoma mvuta bangi kule sokoni," akasema Steven, na wote wakacheka.

"Ahah... kumbe nafanana naye?" Dylan akauliza.

"Hamna, wewe mzuri. Yeye ana sura ngumu, huwa tukimwona tunakimbia. Sema ana marasi kama wewe, ndiyo maana nikaona tukuite hivyo," Steven akajibu.

"Mhm... linamfaa," akasema Leila kikejeli huku akiendelea ku-chat.

"Hamna bwana, baya. Tutafute la kizungu," akasema Emilia.

"Ili iweje?" akauliza Shani.

"Tumwite... Brian," akasema Baraka ili kumpotezea Shani.

"Mm-mm," Emilia akakataa.

"Kendrick?" akasema Baraka.

"Mm-mm."

"Sebastian?" akasema Steven.

"Mm-mm."

"Sasa we' unataka lipi?" Shani akamuuuliza Emilia.

"Ishengoma," akajibu Leila, na wote wakacheka.

"Hamna bwana," Emilia akasema.

Dylan alikuwa anamwangalia Emilia huku anatabasamu.

"Basi wewe mchagulie, maana unayajua majina ya wazungu kuliko hadi wazungu," Leila akamwambia Emilia.

"Ndiyo, Emilia. Nichagulie jina," Dylan akamwambia.

Wote wakamtazama Emilia, naye akawa anamwangalia Dylan kwa makini, kama anatafakari jina ambalo litamfaa.

"Mmmm... Ethan. Tumwite Ethan," akasema Emilia.

Dylan akatabasamu.

Leila akasonya kidogo na kusema, "Me nikafikiri labda utasema Pipindopolupsykapolis."

Baraka akacheka kidogo, kisha akasema, "Ni zuri. Tutakuita Ethan mpaka utakapokumbuka jina lako."

"Na asipolikumbuka milele?" Shani akauliza.

"Haiwezekani. Saa zile alikumbuka kwamba huwa anapenda kulala chini. Atakumbuka vitu vingine tu taratibu," Baraka akasema.

"Kweli?" Steven akauliza.

"Ahahah... ndiyo," Dylan akajibu.

Akamwangalia sana Emilia huku akitabasamu, naye binti akatabasamu pia. Kisha akamshukuru kwa kumpa jina zuri, na kuanzia sasa, Dylan angeanza kufahamika kama ETHAN.


★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★

Previoua Next