SONGA NAYO................
Baada ya kufungua ndani ya begi hilo alikutana na mabunda mengi ya pesa yakiwa yamepangana lakini juu yake kulikuwa na bahasha moja ngumu ambayo ndiyo aliiona kuwa ya mhimu kwa wakati huo. Aliifungua hiyo bahasha ndipo ndani yake akakutana na karatasi nyeupe iliyokuwa imeandikwa kwa maandishi makubwa "Hizi pesa ni zawadi kwa mama, umefanya jambo kubwa kutosema kile ambacho ulikiona kule. Kuna siku nina uhakika maisha yatakuja kutukutanisha tena ila kwa kilicho tokea ndani ya ule msitu IDAIWE MAITI YANGU sio mimi. Hili jambo hakikisha unalifukia kwenye moyo wako, kila utakapo hitaji kulisema hadharani basi ikumbuke kwanza familia yako" Ujumbe huo uliishia hapo, ulimuogopesha na kumpa hofu, alikimbilia lile eneo ambalo aliona kile kivuli kinaishia akiwa na begi mkononi lakini hakuona kitu chochote kile.
Hali hiyo ilimuongezea hofu na kumpa ishara kwamba ina maana mtu huyo alikuwa akimjua vizuri kiasi kwamba hata kwake alipafahamu mpaka hivyo kama angetaka kumuua lingekuwa jambo la muda mfupi tu. Mpaka wakati huo alikuwa ana maswali mengi kichwani mwake kuweza kutaka kujua kwamba yule mtu alikuwa ni nani haswa na aliyekufa alikuwa nani? Alibaki anasonya na kuogopa kwa sababu asingeweza kujijibu hayo maswali hivyo akawa anarudi kinyonge ndani ambapo alikutana na mama yake lakini alimpisha bila kuongea jambo lolote lile.
**************
Saa nane na dakika kumi na tano usiku, simu ilikuwa inaita ndani ya jumba moja la kifahari ambalo lilikuwa maeneo ya Mbweni Dar es salaam. ulikuwa ni wakati wa kupumzika huo lakini ilionekana kuwa simu ya mhimu zaidi, hilo jumba lilikuwa linamilikiwa na mkurugenzi wa usalama wa taifa wa Tanzania Micho Othman. Simu ilipokelewa na aliyekuwa katibu wake yeye akiwa amepumzika lakini uzito wa simu hiyo ndio ambao ulifanya iwe lazima kwa mheshimiwa huyo kuamka ili kwenda kuisikiliza. Alikereka kuamshwa majira hayo ambayo alipenda kutulia na familia yake ila hakuwa na namna.
Simu hiyo ya majira ya usiku ilikuwa inatokea Kenya, ndani ya makao makuu ya shirika la kijasusi la nchi hiyo National Intelligence Service (NIS) yapatikanayo ndani ya jiji kubwa la Nairobi. Uzito wa mtu ambaye alimpigia hiyo simu ilionyesha kabisa kwamba kulikuwa na shida mahali kwa sababu isingekuwa rahisi kupigiwa simu na mtu huyo bila sababu za msingi za kufanya hivyo. Aliipokea simu hiyo na kuiweka sikioni
"Bwana Odhiambo ni usiku sana saivi na unajua kabisa muda kama huu inatakiwa nipate muda wa kutulia na familia yangu"
"Ni sahihi lakini sio kama kuna tatizo Micho na wote tunalijua hilo"
"Nakusikiliza"
"Unajua lolote juu la kilicho tokea ndani ya msitu wa Mau?"
"Hapana, huo ni msitu wako kwenye nchi yako sasa mimi nahusikaje na nchi yako Odhiambo?"
"Shida sio wewe kuhusika na msitu wangu shida ni kile ambacho kimetokea huku kinakuhusu hata wewe moja kwa moja"
"Ni usiku saivi ebu nenda kwenye hoja yako moja kwa moja unataka nini?"
"Kuna mauaji yamefanyika ndani ya huu msitu"
"Sasa mimi nahusika vipi?"
"Haya mauaji ni ya wanajeshi wa Tanzania" Micho alibakia kimya kwa muda kwanza asijue ni kipi ambacho alitakiwa kukijibu.
"Ni wanajeshi wangapi wamekufa?"
"Sina idadi kamili ila hawapungui kumi na watano"
"Unajua kilicho sabababisha mauaji yao na walikuwa wanafanya nini huko?"
"Kwa taarifa za awali inaonekana kwamba kuna mtu ambaye walikuja kumtafuta huku alikuwa anaishi kwa siri na baadae walifanikiwa kumpata wakamuua ila jambo la kushangaza ni kwamba wote wamekutwa wameuawa kasoro mtu mmoja tu ndiye amepona. Inanishangaza mkuu wa usalama nchini hauna hizi taarifa?" hilo swali ndilo ambalo lilimpa hasira kiongozi huyo wa usalama nchini, ni kweli hakuwa na hizo taarifa ina maana ni kwamba alifichwa na watu wawili, raisi pamoja na mkuu wa majeshi.
"Una jina la huyo aliyepona?"
"Sarah Martin"
"Unataka nini Odhiambo kulimaliza hili?"
"Ndicho ambacho huwa nakupendea, unajua kabisa kwamba taifa lako litatuletea picha mbaya kwa kuvamia kwenye msitu wetu bila kibali na kufanya mauaji huko hivyo itaonekana ni sisi tunaua raia wetu au wananchi wetu lakini kwa sababu wewe ni mtu mwenye busara unalielewa hili na lazima kuna gharaam zitumike ila leo sijakupigia kwa ajili ya kukwambia tunacho kitaka ili kulimaliza hili, leo nilitaka tu uwe na hizi taarifa. Kuna siku nitahitaji kitu kutoka kwenu na nitakupa taarifa mapema ya nini unatakiwa kukifanya"
"Kwanini hizi taarifa usingempatia mkuu wa majeshi au raisi maana sihusiki sana huku?"
"Mimi na wewe wote tunajua kwamba jeshi huwa linetekeleza tu ila jukumu la usalama wa nchi lipo kwenye mikono yako wewe hapo hivyo wewe ndiye ambaye unapaswa kuzungumza na hao watu wako huenda wakawa na majibu sahihi na mpaka walikuficha wewe basi kuna jambo halikuwa sawa kwenye kazi hiyo"
"Unamjua aliye waua watu hao?"
"Hapana ila zungumza na huyo binti atakupa majibu sahihi" simu ilikatwa, mkurugenzi aliketi kwenye kiti hata ile hamu ya kuendelea kulala iliisha kabisa. Alizihitaji taarifa za binti huyo ziletwe haraka mezani na kuweza kujua yuko wapi wakati huo kwani ilikuwa ni mhimu kuongea naye kabla hajaongea na mtu mwingine yeyote yule.
Sarah Martin, ana miaka 35 ni moja kati ya wanajeshi hodari na wenye mafunzo ya juu ndani ya jeshi la nchi ya Tanzania. Mwanamke huyu pia ni moja kati wa wadunguaji bora na wa kutegemewa jeshini. Amezaliwa Makongorosi Chunya ambako alianzia shule yake ya awali huko ila baada ya baba yake kufariki walihamia ndani ya jiji la Mbeya maeneo ya Nzovwe. Huko aliishi yeye, mama yake na mdogo wake ambapo baada ya kuhitimu elimu ya sekondari aliweza kujiunga moja kwa moja na JKT pale pale Nzonvwe ambapo safari ya maisha yake ilianzia hapo akiwa kama mwanajeshi.
Alikuwa ni miongoni mwa wanajeshi wenye umri mdogo kuaminiwa kufanya oparesheni ngumu za kijeshi ambapo ameenda kwenye nchi nne barani Afrika; Alienda Nigeria kubambana na kundi la Boko Haramu, alienda Congo kama sehemu ya wanajeshi ambao waliungana na Interpol kwenda kupambana na waasi. Alikuwepo kwenye ile oparesheni ya kupambana na Al-shabaab lakini pia alikuwepo Msumbiji kupambana na waasi ambao walisababisha hali ya hatari ambayo ilidhaniwa ingeweza kuupindua utawala ulipo madarakani.
Baada ya kutoka huko alipewa likizo kisha mwaka mmoja baadae akajumuishwa kwenye kikosi maalumu ambacho kilikuwa kinatambuliwa na mkuu wa majeshi na ndicho ambacho anafanya nacho kazi mpaka sasa. Japo alizaliwa Mbeya ambako ndiko asili ya baba yake lakini kwa sasa anaishi Moshi ambako ndiko iliko asili ya mama yake. Taarifa za mwanamke huyo zilikuwa zinasomwa na moja ya vijana wake usiku huo huo kwenye Ipad kubwa, zilikuwa zinajitosheleza kuujua uwezo wa mwanamke huyo ambaye alidaiwa kwamba ni pekee ambaye alifanikiwa kupona kwenye ule msitu huko iliko dhaniwa kwamba watu wengi walikuwa wamepoteza maisha.
"Kwa sasa yuko wapi?"
"Tumejaribu kudukua mawasiliano yake, inaonekana yupo Moshi muda huu"
"Andaeni helikopita nataka niende huko mwenyewe" mheshimiwa hakuwa na muda wa kusubiri kupambazuke, lilikuwa ni jambo la dharura na yeye ndiye ambaye angekuja kuzipokea lawama zote kama kuna kitu kingeenda vibaya hivyo aliona ulikuwa ni wakati sahihi wa yeye mwenyewe kudili na jambo hilo kabla ya kuwashirikisha watu ambao walimficha oparesheni nzima mpaka kufikia wakati huo.
Kuna mengi ya kuyafunua humu ndani, ndiyo kwanza sehemu ya nne, tukutane ndani ya sehemu inayo fuata.
FEBIANI BABUYA.
Comments