SONGA NAYO................
Saa kumi na dakika tano usiku msafara ya kiongozi mkuu wa usalama nchini ulikuwa umeingia Moshi karibu kabisa na yalipokuwa makazi ya Sarah Martin. Walishuka walinzi kuangalia mazingira na baada ya dakika chache ndipo mheshimiwa mwenyewe aliruhusiwa kuweza kushuka ili kukutana na mwanamke huyo. Sauti ya helikopita hiyo ikiwa inashuka ndani ya uzio mrefu ambamo ilikuwepo nyumba hiyo ndiyo ambayo ilimshtua Sarah pamoja na mama yake.
Wakati inatua aliiona vizuri na alikuwa anazijua aina za helikopita hizo kwamba zilikuwa zinatumiwa na watu gani, jambo hilo lilimuongezea hofu kubwa kwani aliamini kwamba kile ambacho kilitokea kwenye ule msitu huenda kingemuwinda na kumfanya asiwe salama kwenye maisha yake yote ambayo yalikuwa yamebakia. Alimtoa mama yake hofu na kumhakikishia kwamba watu hao walikuwa ni wa kazini na kuja hapo lazima kulikuwa na jambo la mhimu hivyo alihitaji kwenda kuwasikiliza. Alitoka nje kwa tahadhari ambapo aliona mwanaume huyo mtu mzima akiwa amesimama nyuma ya watu wake ambao walimtaka yeye asimame kwanza, walimkagua kwenye mwili wake ndipo walimpisha kiongozi wao ambaye moja kwa moja aliongoza sehemu ambayo ilikuwa na bembea za kukalia ili wafanye maongezi.
Sarah kwenye maisha yake yote hakuwahi hata siku moja kukutana na mtu huyo zaidi ya kuishia kumuona kwenye picha tu siku ambayo mheshimiwa raisi alimteua kuwa mkurugenzi kwenye kitengo hicho nyeti. Baada ya hapo hakuwahi kusikia lolote kuhusu mtu huyo wala historia yake ya maisha haikuwa ikifahamika sana na hilo alitambua kwamba lilifichwa kwa sababu za kiusalama hivyo alianza kuogopa kwa kutembelewa na mtu mzito namna hiyo kwenye taifa, mkurugenzi asingejisumbua kwenda sehemu kama kusingekuwa na shida kubwa au uhitaji wa taarifa za mhimu na za haraka.
"Bila shaka utakuwa haunifahamu bibie na pole kwa kukuvamia na usiku wote huu ambao unatakiwa kupumzika lakini wote tunaelewa kwamba maisha yetu sisi taifa linakuja mbele kwanza kabla ya kila kitu hivyo pia sitakiwi kukuomba msamaha kwenye hilo kwani ni jukumu lako pia kuipigania nchi yako kwa namna yoyote ile"
"Ndiyo mheshimiwa, nimefurahi kupata bahati ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wewe na natumai kuna jambo la mhimu ambalo naweza kusaidia" mheshimiwa alikuwa amemkazia macho mwanamke huyo kupitia taa za mwanga ambazo zilifanya eneo hilo kuwa jeupe huku walinzi wake wakizunguka kila upande kuhakiki ulinzi hususani baadhi ya maeneo ambayo yalionekana kuzungukwa na migomba mingi.
"Upo sahihi, mpaka nafika hapa basi unajua ambacho kimenileta ila wakubwa zako ndio hawajui kama nipo hapa. Usiku huu nimepokea simu moja kwa moja kutoka kwa mkurugenzi wa NIS Kenya ndiyo maana nipo hapa, nadhani unajua kile ambacho kimetokea ndani ya msitu wa Mau na jambo hilo linaenda kutuchafulia jina kwa kiasi kikubwa kwa sababu limefanyika jambo bila ruhusa ya wenye mamlaka kule hivyo kuna gharama ambazo kiusalama kama taifa lazima tuingie lakini hilo linaweza kuisha endapo utanijibu maswali yangu matatu tu Sarah" hakushangaa kiongozi huyo kuwa na jina lake kwenye kinywa chake ila kilicho muogopesha ni hayo maswali matatu.
"Swali la kwanza ni nani aliua wale watu, swali la pili nipe sababu ya msingi ya kwenda kumuulia yule mtu kwenye ule msitu, na swali la tatu ni kwanini wauawe watu wote kisha wewe uachwe hai?" ni maswali yaleyale ambayo alihisi kwamba ndiyo ambayo yanaweza kuja. Sarah hakusita kumpa mheshimiwa ile stori yake ya kusadikika ambayo aliirekebisha baada ya kushauriwa na Nick lakini bwana Micho aliishia kucheka kwa sababu alijua kabisa binti huyo anamdanganya.
"Binti kitu ambacho tunakizungumzia hapa ni usalama wa taifa kwa ujumla na mamilioni ya watu wake, nipo kwenye kazi za usalama kwa miaka zaidi ya thelathini sasa hivyo usinione mimi kama hao wanajeshi wenzako ambao unaweza kuwauzia stori za kitoto hizo. Nina mamlaka ya kuondoka na wewe muda huu ukawa mshtakiwa namba moja na habari zikafika kwa wakubwa zako na unajua kabisa nikiamua kukuchunguza ni masaa matano tu yatatosha mimi kujua kila kilicho tokea kule au tunaweza kuyamaliza hapa kwa wewe kuniambia ukweli na kunijibu hayo maswali yangu" Sarah alibaki ameganda njiapanda kwani mzee hakuonyesha urafiki licha ya kucheka, alionekana hakuwa mtu wa kupenda kupotezewa muda wake kabisa.
"Kwakweli sababu za msingi za mimi kuachwa hai mpaka sasa sizijui, alikuwa na nafasi ya kuweza kuondoka na maisha yangu lakini akaamua kuniacha tena kwa kunipa onyo kubwa. Sababu ya kumuulia yule mtu kule ni kwa sababu ndiko ambako alikuwa anaishi kwa siri kwenye nyumba moja ambayo ilionekana kutelekezwa eneo lile kwa muda mrefu bila kujulikana sababu ya msingi ya nyumba ile kujengwa lile eneo. Kuhusu mtu ambaye ameua wale wenzangu wote kule simjui na kama ningekuwa namjua kiundani basi nisingekwambia mheshimiwa, nisamehe sana kwa kusema hivi kwa sababu mtu huyu anaijua vizuri mpaka familia yangu hivyo kufungua kwangu mdomo ingemaanisha ni mwisho wa familia yangu yote" alimsikiliza mwanamke huyo kwa umakini mkubwa akiwa anaongea na kuyapima maneno yake kwa kumkazia macho.
"Ni nani ambaye mlienda kumuua kule?" lilikuwa swali lingine gumu lakini hilo alipaswa kulijibu.
"Gavin Luka"
"Gavin Luka ni nani?" ilionekana kabisa kwamba ilikuwa mara ya kwanza kabisa mheshimiwa kulisikia hilo jina kwenye maisha yake yote.
"Kiukweli mimi nilitajiwa tu jina, sikuwahi kumjua huyo mtu kabla mtu ambaye alikuwa na taarifa zote za mtu huyu alikuwa ni kiongozi wa msafara wetu Michael ila kwa bahati mbaya amekufa pale pale.
"Umeiona sura ya mtu huyo" Mr Micho aliuliza tena akiwa amemkazia macho Sarah akicheza na mboni za macho yake kuona kama zinamdanganya au zinasema ukweli. Sarah alimeza mate kwa shida akiwa kwenye mstari mgumu wa kufanya maamuzi, maneno ya mwanaume yule yalikuwa yanajirudia kwenye kichwa chake, akakumbuka mpaka namna mtu huyo alivyofika hapo kwake na kuacha barua pamoja na pesa nafsi ilimwambia huenda bado mtu huyo anamfuatilia kila hatua ambayo alikuwa anaipiga hivyo alipaswa kuwa makini isivyokuwa kawaida.
"Hapana, alikuwa amevaa kitambaa usoni sikufanikiwa kumuona kwa sababu hata nilipotaka kumhoji kutaka kumfahamu alinipiga mpaka nikazimia na wakati nazinduka hapakuwa na mtu zaidi ya maiti za wenzangu zikiwa zimezagaa na ile nyumba ikiwa imechomwa tayari" mkurugenzi alitabasamu, macho ya Sarah ni wazi yalikuwa yanadanganya lakini hakutaka kulisema jambo hilo.
"Tutakutana wakati mwingine nikikuhitaji" aliongea mkurugenzi na kusimama kisha akaanza kuzitupa hatua zake kwenda kwenye helikopter mpaka pale ambapo helikopiter hiyo ikapotea maeneo hayo. Sarah bado alikuwa haamini kuachwa kirahisi tu namna hiyo, moyo wake ulikuwa unapiga mbio isivyokuwa kawaida. Baada ya mheshimiwa huyo kuondoka, alianza kupokea simu nyingi za majirani wakitaka kujua kama kuna usalama hapo kwake kwani waliona helikopiter inaingia na baada ya muda ikatoweka. Aliwatuliza kwa kuwaambia yalikuwa na mambo ya kazini tu hakukuwa na tatizo lolote lile.
Gavin Luca huenda kweli lilikuwa jina geni kwa mkurugenzi au ni yeye tu aliamua kumdanganya mwanamke huyo. Asubuhi ya mapema kabisa wakati kumepambazuka mheshimiwa huyo alikuwa kwenye gari akielekea Bunju nyumbani kwa mkuu wa majeshi wa Tanzania Medrick Savato. Ni muda mchache alitoa taarifa ya kuweza kufika ndani ya hilo eneo ikiwa ni muda mchache tangu atoke Moshi kuonana na Sarah Martin. Alifika kwenye jumba kubwa la kiongozi huyo ambalo lilikuwa linalindwa isivyo kawaida na wanajeshi wengi, taarifa za ujio wake zilikuwa zinafahamika hivyo aliingia bila kizuizi chochote, walishuka vijana wake ambao mavazi yao meusi yaliitambulisha vyema kazi yao na kwenda kumfungulia mheshimiwa mlango huku mkuu wa majeshi akiwa amesimama na walinzi wake kumsubiri kiongozi mwenzake huyo mkubwa wa usalama nchini.
Watu hao walipeana mikono na kwenda moja kwa moja kwenye chumba maalumu ambacho kilikuwa kwa ajili ya wageni wa mhimu kufanya mazungumzo yao huku kahawa ikiletwa pale walipokuwepo.
"Haujawahi kuja kunijulia hali hapa kwangu hata siku moja Micho, leo mpaka umefika hapa basi natarajia kwamba utakuwa una jambo kubwa ambalo limekuleta"
"Upo sahihi, mimi na wewe hatujawahi kuwa na ukaribu wowote wala urafiki kwenye maisha yetu na mara nyingi ukiona tumekutana kama hivi basi ujue kabisa kwamba kuna jambo la msingi lipo nyuma ya mambo haya bila shaka unaelewa hilo"
"Ni vyema ukienda kwenye pointi ya msingi kwa sababu najua kabisa haujaja hapa ili kunijulia hali"
"Safi, nahitaji kujua ni kipi ambacho kimetokea ndani ya msitu wa Mau bila kuacha pointi hata moja kwenye maelezo yako"
"Msitu wa Kenya huo, sasa mimi nahusika nini na mambo kama hayo?"
"Tusipoteze muda kuelezea jambo ambalo limefanyika chini ya usimamizi wako, kama ulivyotaka kwenda kwenye pointi ya msingi na ndicho hicho hata wewe unatakiwa kukifanya hapa"
Sehemu ya tano inafika tamati, sehemu ya sita ndiyo inafuata, tukutane huko.
FEBIANI BABUYA
Comments