Sehemu ya 1.
Naitwa Rojaz na nimezaliwa kwa wazazi ambao baba na mama matamanio yao ni kuona watoto wao tunasoma kwa bidii ili kuweza kufikia malengo yetu na ndoto ambazo wao kama wazazi wanaziota juu yetu,natumaini ni ndoto ya kila mzazi kwa mtoto wake,hakuna mzazi anayesomesha mtoto na asitamani kuona anapata mafanikio katika masomo yake,kiufupi mimi nilikuwa ni mmoja kati ya watoto 6 katika familia yetu nikiwa ni mtoto wa tatu kuzaliwa.
Na nimejaaliwa kusoma mpaka kidato cha nne na sikufanikiwa kufanya vizuri katika matokeo yangu ya mwisho, ukiniuliza sababu ya matokeo yangu kuwa mabaya kiukweli sikuwa na jibu la moja kwa moja ila kiukweli hakukuwa na ugumu huo ila naweza kusema ni mimi mwenyewe kwa uzembe wangu na uzembe wa wanafunzi baadhi mnapokuwepo shuleni kutotambua nini kilichowaleta pale. Kuna wengine ambao wanatilia mkazo masomo yao matunda yake waliyaona na wale wakina wenzangu mie akili tunaielekeza katika michezo isiyo na tija, naeleza haya usidhani nilidharau elimu kwakuwa labda nilitokea katika familia bora, familia yetu ina uwezo wa kiuchumi la hasha kwani hata elimu yangu tokea kidato cha kwanza ni harambee ndio ilikuwa inatawala katika upatikanaji wa ada yangu, mara kachangia shangazi, mara mamdogo au mwana familia yoyote anayeonekana ana nafuu ya kipato kwa wakati huo. Kiufupi nilikulia katika familia duni.
Tulikuwa tumezaliwa watoto wengi na kila mtoto alikuwa na mahitaji yake kwa wakati husika. Sasa maisha ya mtaani bada ya kumaliza mchakato wa masomo tena ukiwa matokeo ambayo sio rafiki chamoto hujakiona, changamoto nyingi zinakuwa zinajitokeza na hapo unatakiwa kujiongeza ili kuweza kujikimu wewe na wanaokuzunguka ilimradi mkono uende kinywani. Katika kusaka tonge nikaanza kujichanganya kwa kuanza kutembea na mafundi hawa mafundi ujenzi nikiwa kama saidia fundi (kibarua msaidizi) na haikuwa kwa mafundi tu kwani pale mtaani kila aina ya kazi iwe kuchimba shimo,kukusanya mchanga (wakati wa mvua ule mchanga unaoletwa na maji), kubeba tofali, kusaidia mtu anayetaka kuhama na kadhalika mie kwangu ilikuwa twende kazi yaani kwa upande wangu maisha yalikuwa ni magumu sana sana sana na msalie Mtume yangu ni kujipenyeza katika harakati hizi, (nakuhusia ewe kijana ambaye umepata neema ya kupata nafasi ya kusoma chonde chonde usiichezee bahati hiyo uko mbele ni kugumu sana,soma kwa bidii maisha sio marahisi), maisha ya kukaa nyumbani yalikuwa na maneno maneno mengi yenye kuumiza roho, ukishamaliza shule hata andazi upewaji wake hauwezi kuwa kama mwanafunzi kwani ukigewa ujue utasindikizwa na neno la masimango hivyo sikuipenda hali hiyo nikawa najibidiisha katika videiwaka hivyo ili kuweza kupata mahitaji.
Siku zilisogea, maisha nayo yakawa yakienda yakibadilika kwani kama unavyojua siku hazigandi mahitaji yanaongezeka, vitu vinapanda bei na maisha yanavyosogea kwangu ndivyo maisha yakazidi kuwa magumu sana kwani ni jasho lako ndilo litakaloamua mustakbali wako.
Pale nyumbani tulikuwa tunaishi kifamilia na mama yangu yeye alikuwa anajishughulisha kwa kufanya biashara, alikuwa anafanya biashara za sokoni (mchuuzi mdogo mdogo) na baba yangu yeye kwa muda mwingi alikuwa yupo tu nyumbani (misheni town) na sana alikuwa kama dalali kimtindo ingawa haukuwa ule udalali wa moja kwa moja yaani kama kuna chumba yeye anadalalia kupata mpangaji na anapewa kamisheni au mtu ana mali yake anauza au anatafuta kitu yeye anamsaidia kuweza kufanikisha jambo husika.
Kwahiyo egemeo kubwa la familia lilikuwa ni mama,mama yeye alikuwa anaenda sokoni uko akaemee ndio akirejea watu wanapata afadhali, siku zilisogea na kusogea mama yangu pekee aliendelea kuwa mkombozi wangu kwani hata nikiwa nimepungukiwa nauli alikuwa ananipa lakini alikuwa ananambia akinikumbushia kwa kusema "Nilikupa nafasi ya kusoma ukachezea unaona unavyopata tabu? Yaani wewe unaniomba mimi nauli? Utagewa nauli hadi lini?"
Lakini pamoja na maneno yote mama yangu mpenzi alikuwa ananipa mtoto wake
Ikafika wakati mama yangu mpendwa akapata maradhi,akaumwa sana, aliumwa sana yule mama na kama nilivyotangulia kueleza awali mama ndio alikuwa nguvukazi na wakati alipopata maradhi akawa yupo kitandani tu na baba yetu ndio hivi mara apate pesa, mara siku asikutane nayo yaani utokaji wake haukuwa na uhakika wa kurudi na kitu yaani ni bahati nasibu tu, mama alikuwa ana utaratibu wa kudunduliza pesa kama akiba kwa ajili ya maendeleo na kutokana na changamoto iliyojitokeza zikaanza kutumika kwa ajili ya kumuuguza yeye na kutatua changamoto za nyumbani kwani pia nilikua na ndugu zangu ambao walikuwa wanasoma.
Maisha yalikuwa magumu sana huku mimi nikizidi kupambana ili kuweza kujikwamua na umaskini uliokuwa umetuzunguka. Dah! Majira na nyakati
yalikuwa yamefika, mama yangu kipenzi, mama yangu nimpendae, mboni ya jicho langu akaaga dunia!
Tulifanya mazishi kuweza kumpumzisha mama yetu kipenzi katika nyumba yake ya milele, kiukweli huu ulikuwa msiba mzito sana kwetu kwa sababu hakuna asiyejua kuanzia majirani hadi ndugu wa karibu kuhusu nafasi ya mama yetu katika familia, mama alikuwa kinara, alikuwa mpambanaji katika familia yetu kwahiyo kuondoka kwake woga ulituvaa miilini mwetu kwa namna ya kuikabili kesho yetu yaani hasa mimi nikajiuliza tutafanyaje?
Hii kauli hata wadogo zangu waliweza kuitamka na kujiuliza tutaishi na kusoma vipi? Lakini maisha lazima yaendelee na tukakamilisha kipindi cha maombolezi ya mama yetu kipenzi.
Siku zikasonga nikiwa nayakumbuka mengi ambayo mama alikuwa akinishauri alikuwa akiniambia
"Rojaz soma mimi leo nipo kesho sipo, kesho baba yako yupo kesho hayupo mkombozi wako ni elimu, tizama ndugu zako wanasoma, hivi vipesa ninavyokupa visikubweteshe kesho nitakopokuwa sipo utapata tabu mwanangu, dunia hii ni ngumu sana ukiwa hauna cha kufanya dunia ni ngumu sana naomba ulitambue hilo",
Nazikumbuka hizi kauli kwani uwa zinanijia sana,zinanijia pale nina shida, pale napokuwa sina kazi yakuweza kunipatia riziki, unajua sie masaidia fundi ni pale fundi apate kazi ndio akwambie njoo, kama hajapata nawe ujue imekula kwako!
Kaka yangu mkubwa alikuwa ana rafiki yake ambaye ni dereva taksi, nakumbuka nilimfata kaka na kumwambia, "kaka huku kwenye ujenzi ni pagumu sana, kaka kama unaweza hata kuniunganisha kwa rafiki yako niweze kukaa hata kijiweni naweza kupata chochote kitu"
Kaka yangu alicheka na akanambia
"sasa wewe ukakae katika kijiwe wakati gari huijui, yaani hujui chochote kuhusu gari pale sio wanakaa tu, wanakaa watu wenye idea na hivyo vitu yaani ukakae kijiweni na haujui lolote? Au unatakaje? Unatakaje mdogo wangu?"
Nikamwambia, "nataka kujua hiyo gari sasa ndio maana nataka kukaa na wenye magari". Akasema, "Ntaongea naye na atakaporidhia utaambatana nae lakini ngoja nizungumze nae kwanza".
Siku zikapita toka nimueleze kaka kuhusu hili jambo na nilikuwa nikimkumbusha mara kwa mara yeye alikuwa akinijibu kuwa amesahau lakini nashukuru siku moja niliwakuta wote wawili kaka na rafiki yake wakiwa pamoja nikamwambia kaka
"Kaka naomba umwambie hapahapa maana uwa unasahau naomba umwambie sasa hivi", nashukuru Mungu kaka alimwambia huyu rafiki yake ambaye anaitwa John, naye akajibu, "Hakuna shaka kama yeye anapenda hata kama hajui chochote atajua tu, wengi walifika pale hawajui chochote kuhusu gari na sasa wanajua, atakuwa akitazama tunavyofanya na tutamfundisha atajua"
Maisha yakasogea na nilifurahi sana kwa ombi langu hili kukubaliwa, nilianza kwenda pale kijiweni na kwa nyakati hizi biashara ya taksi ilikuwa na mzunguko sana, wateja walikuwa wengi kwani kulikuwa hakuna mambo mengi kama mabodaboda au hizi Uber yaani taksi ndio ulikuwa mpango mzima.
Basi nikafika kijiweni nikakutana na John na alinambia wewe utajumuika nami katika safari iwapo mteja atakuwa ameridhia, utakaa unatazama namna ninavyopiga gia na pia siku za Jumapili John alikuwa hafanyi kazi hivyo alikuwa ananichukua na kwenda katika uwanja wa wazi na kunifundisha gari na kwa sababu mimi nilikuwa na nia na ninapenda kwangu haikuwa ngumu kujua tena kaka John alinipa maneno ya hamasa sana
"Sio ngumu mdogo wangu weka nia tu kuna wenzako wengi wametoka vijijini uko leo wanawaendesha mabosi na maisha yao yanasonga, wanakula vichwa kwahiyo wewe pambana bwana, pambana mdogo wangu".
Kweli nikapambana hadi ikawa tena kwenye vile vibarua vya saidia fundi siendi nikawa napenda gari napenda gari kweli kweli, ikifika asubuhi mie wa kwanza kijiweni utasema kama vile mie ndio nimekabidhiwa taksi kumbe bado deiwaka, namsubiri bro John basi mishemishe zinaendelea.
Taratibu nikawa najenga imani kwa John na John akanambia sasa siku mojamoja nitakuwa nakupa nawe uwe unakula vichwa, yaani siku ambazo anakuwa yuko sehemu ametulia ananiachia chombo nakula vichwa, yaani alikuwa ametokea kunikubali sana nami nikawa napiga mishe kila kaka John anaponikabidhi chombo, sasa nikawa dereva namudu kukiongoza chombo maana kijiweni tena John awepo au asiwepo mi naburuza tu, maisha ya udereva yakaendelea na bro John akawa ananitoa toa mara buku tatu, mbili hadi tano, kwa kipindi iko ilikuwa ni kubwa, elfu tatu kwangu ni kubwa tena ukitilia maanani natokea nyumbani akinipa elfu tatu, akinipa elfu mbili niliona safi sana kwa sababu nikitu nilishaanza kukipenda.
Huyu John kwa muda mchache niliokaa nae nilimsoma nilimgundua ni mtu anayependa sana mabinti (mtu wa totozi) yaani yeye ikifika jioni tu kile kigiza cha kwanza tu anapotea kijiweni anaenda kujificha na binti aliyemteua siku hiyo. John alikuwa mwenyeji sana katika nyumba za wageni na ukitilia maanani alikuwa na wateja sana katika biashara yake ya taksi yaani kwa watu wa taksi saa 1 hadi saa 2 usiku ndio kunakuwa kumekucha lakini yeye hauwezi kumkuta muda huo anakuwa maeneo yake yakujidai kwani muda huo kibunda kishanona hapo ananiambia dogo nishaondoka kwenda kujipumzisha na shemeji yako, kiufupi alikuwa mzee wa bandua bandika.
Kwa hiyo muda mwingi alikuwa ananiachia funguo sababu alikuwa ameshaniamini kama deiwaka wake nami nikawa napiga kazi hadi mida flani nampigia bro nshamaliza naye ananielekeza alipo namkabidhi chombo narudi nyumbani
Siku moja John akanambia "mdogo wangu sasa wewe umeiva, umekwisha iva inabidi tufanye mpango upate leseni usije kukutwa barabarani huna chochote hii ni hatari kwakuwa ushakuwa uko vizuri katika uendeshaji, lakini pia uweze kujua sheria za barabarani"
Kwahiyo nikafanyiwa mpango wa kupata leseni na John akanitimizia nikapata leseni sasa nikawa kamili gado kama wasemavyo watoto wamjini! Na akanambia sasa upo kamili na hata akitokea tajiri anaweza kukukabidhi gari ukawa unapeleka hesabu, uko vizuri na hii ukiichukulia serious itakutoa dogo" Nikamwambia
"Asante bro kwa wema wako nakuahidi sitakuangusha na hata hizi dakika chache unazonipa naamini kijiweni michongo ni mingi ntatoka tu"
Aliendelea kunielezea "Hapa kijiweni kweli kazi ni nyingi tena waweza akatokea mtu akazingua na tajiri akatafuta dereva anaweza akakukabidhi wewe chombo, komaa dogo hao wengi unaowaona kijiweni si kama wewe tu wamekabidhiwa rasmi vyombo bali madeiwaka we kuwa mvumilivu tu".
Kiukweli alinipenda kwakuwa mimi nilikuwa mchangamfu, mwepesi kuelewa jambo ninaloelekezwa, kazi nilitokea kuipenda na zaidi sikuwa muongo yaani zile za kumdanganya labda nimebeba mteja alafu nimwambie sijabeba au nimebeba ila nikawasilisha pesa pungufu kiukweli sikuwa na utundu huo, kwahiyo ndio sababu bro John akaniamini sana.
Safari ikaendelea maisha yakasogea nikiwa sasa ni dereva kamili wa taksi na nikawa najivunia na kufurahia kazi yangu ya udereva ingawa katika mambo yote bado nilikuwa namtegemea John lakini nilikuwa nimepata ujuzi mkubwa kutoka katika kitu nilichokuwa sikijui kabla, kadri siku zilivyokuwa zinaenda nami nikawa naanza kuzoeleka na kujulikana kwa wateja mmoja mmoja, siku moja tukiwa kijiweni alikuja dada, huyu dada alipofika John akanambia, "Huyu dada ni mtoto wa mwenye hii gari ambayo mimi nimekabidhiwa"
John alinieleza haya kwakuwa huyu dada alitaka kuleta mazoea yaliyopitiliza, yaani ni mara mbili tu ndio nimepata kukutana na huyu dada, mara ya kwanza nikiwa na bro John alipokuwa akipeleka hesabu ya gari kwao kwahiyo John akanitambulisha kwao mimi kuwa ni mdogo wake, siku ya pili ndio hii tunaonana hapa kijiweni lakini ile siku ya kwanza huyu dada alikuwa akiniwekea ishara ambazo mimi sikuzielewa, unajua mimi tangu ninasoma hadi kufikia hatua hii sikuwa na ukaribu wa kivile na akina dada kama hivi yaani kiufupi sikuwa na masuala ya mahusiano na akinadada kwa sababu mazingira ya shule na nyumbani hayakuwa rafiki katika mambo hayo yaani hakukuwa na nafasi ya zile za kikombolela au michezo ya kujificha vichakani.
Huyu binti kwanza alikuwa na mtindo wa kunikonyeza nami nikawa namshangaa tu na haya mambo hakuna aliyekuwa anaona zaidi yangu mimi ile siku ya kwanza tulipoenda kwao na John na siku ya pili ndio hii amekuja hapa kijiweni na alipofika kwanza aliniulizia sisi tukiwa tumegeuza migongo tumekaa hapa kijiweni tumegeukia kwingine mimi na huyu bro. Alikuja moja kwa moja na kuniulizia akitaja jina langu yaani huwezi kuamini jina langu alilishika kwelikweli, siku ya kwanza tu kulisikia akalishika akaulizia, "Yuko wapi Rojaz?"
Wakamuuliza "Rojaz wa John?"
Akajibu "eeh, yuko wapi?
Akaelekezwa mpaka nilipo na dada yule akaja yaani wala hakuwa na woga sijui yuko vipi,akaanza kusema,
"Jamani toka siku ile hata haunitafuti"
Mbele ya John akawa anayatamka maneno hayo "Hunitafuti? Mbona umekuwa hivyo? Au haujui mambo ya mjini? Haya mambo ya mjini we huelewi? Basi mi nikabaki nashangaa shangaa nikiwa nimeweka mikono hivi tukipiga stori na John akaja yaani akanikumbatia kwa kuniwekea mikono yake juu yangu akiwa amenikumbata kutokea nyuma akanambia
"Nimekumiss sana, nimekumiss mno, nyumbani umekuja siku moja tu nimekufahamu haukuja tena,au John amekwambia usije? Nikamwambia "hapana mbona tunakuja sana labda uwa tunapishana wakati sisi tunakuja wewe unakuwa haupo"
Akanambia "kama tunapishana si uniulizie?". Pale ni nyumbani kwetu ulizia flani yuko wapi utaniona, siku hizi tunaenda kwa simu sasa mpaka unione tena wewe huna hata simu nikamjibu "sina simu"
John akawa anamtizama tu, anatutazama tu na si kama alinivuta pembeni ni mbele ya huyu John, akasema "Basi itabidi utafute simu, ntakutafutia simu". Basi yule binti akaondoka zake mi nikiwa nimeshikwa na butwaa, wakati anaondoka akanambia "Mbona hata haunisindikizi?
Wakati ananambia hivyo John akawa ananinng'oneza kitaratibu
"mwache aondoke zake"
Akaendelea kunambia
"Katika vitu ambavyo unatakiwa ukae navyo mbali kimojawapo ni huyu binti, huyu binti achana nae kabisa hii ni hatari unaweza kupigwa risasi ya kichwa,achana nae asikuzoee"
Nilimwambia John "Kaka wala usiwe na wasiwasi na mimi kuhusu yule binti kwani ugumu wa maisha ambao nimeupitia haitaweza kutokea, kwanza sina mahusiano nae na kama ulivyosikia ameniulizia kama nina simu nimemdanganya kuwa sina na hayo anayonieleza akili yangu wala haiko huko na kwakuwa umenisisitiza nitakuwa mtiifu kwako wala sitajihusisha nae, mimi nitakaa kimya"
Akanambia "ndio hivyo unatakiwa ufikirie maisha sasa mambo lazima yaendelee, hawa mabinti wa mabosi watakuja kukuletea matatizo mbeleni achana nao kabisa".
Nikamsikiliza kaka yangu na baada ya muda kanambia "leo usiku kunaweza kukawa kuna dili tunaweza kulifanya na kwa sababu umeshakomaa sasa wewe ni dereva mzuri" Nikamwambia "hakuna shida, kuna abiria?
Kaka John akasema "yes,kuna abiria ila mimi ntaenda kupumzika nina kitu changu(mpenzi) bwana si unajua? Mimi bwana sinywi pombe, mi sio mshabiki sijui wa vitu gani gani lazima nitulie sehemu na mtoto mzuri tule raha, mimi nitakupa mchongo muda ukifika".
Basi nikakaa tayari kwa huo mchongo, akaniachia funguo naye akaondoka zake lakini sehemu alienda mimi sikuijua (sikujua ni guest gani) lakini aliniambia tu kaa tayari, usiku nikaona muda umeenda na kwa sababu nilifanyafanya kazi kwa toka muda ule alionieleza hili swala jioni ilishaingia ilikuwa mida ya saa 11 hivi, nikapigapiga kazi mpaka kwenye majira ya saa 3 usiku nikajiuliza bro yuko wapi? Nikipiga simu yake hapokei, nikajua huyu kashakuwa katika uwanja wake wakujidai tena basi nikajiondokea zangu nyumbani kujipumzikia, gari nikaenda kuipaki palepale tunapoipaki, nikaenda zangu nyumbani nikijua mteja ameaghirisha hilo zoezi, nilipofika nyumbani nikaoga zangu na kula chakula nikijiandaa kwa kulala, wakati nimeshajipumzisha mara simu yangu ikaita na kutizama ni bro John akanambia, "Nakupgia muda mwingi naona namba yako inatumika au ulikuwa unaongea na yule mtoto?
Nikamwambia, "Hapana bro siongei na huyo mtu kwanza nimemwambia sina simu na wewe shahidi ulisikia pale nikimwambia, sina hata namba yake wala namba yangu hana, nafatisha ushauri wako kama ulivyonambia niachane nae nami nafanya hivyo"
Bro akanambia "vizuri, sasa lile dili liko tayari limeshakaa mkao wake,kuna abiria utaenda kumchukua". Nikamuuliza "namfata wapi?"
Akanambia "palepale gari ilipo yeye tayari atafika hapo na atakapofika hapo ataingia kwenye gari na utamsikiliza wapi unapompeleka"
Nikamuuliza "ina maana gari ilipo yeye anapajua? Akanambia "anapajua tena ukichelewa unaweza kushangaa yeye ameshafika kabla yako wewe lakini sitaki wewe umkute jitahidi uanze kufika wewe na ukifika milango ya gari aikute iko wazi, yaani yeye akifika akute milango haijakomewa yeye atafungua na ataingia ndani mtazungumza akiwa ndani ya gari huku ukiwa umewasha gari,ni mteja wetu mzuri, anatoa pesa nzuri kwahiyo wewe kale kichwa".
Basi mimi nikanyanyuka na kujiandaa, nikatoka zangu kuelekea pale tunapolaza gari, ile nimefika tu nafungua gari na kuweka mazingira vizuri garini basi kweli mtu huyu akaja, alionekana ni kijana ila alionekana amenizidi umri kidogo lakini ni rika la kijana, alikuwa anashabihiana kiumri kiasi kama bro John hivi lakini sema yeye alikuwa ni mrefu, akaja akaingia garini na akakaa siti ya nyuma, ujue tena taksi hizi, akanambia, "Naomba endesha twende huku" Nikamwambia "wapi? Akanambia "wewe twende ntakuelekeza,taarifa zangu si John amekupa? Nikamwambia "ndio"
Akasema "sawa sasa twende".
Nikawasha gari tukaanza kuondoka huku yeye akiwa ndio muelekezaji njia mara pita hivi, kata hapa lakini akanambia "wewe ni dereva mzuri sana John amenambia ni dereva mzuri alafu ni mzoefu barabarani sasa tupite short cut"
Kwakuwa nilishakuwa na gari muda mrefu na mzoefu katika njia tofauti tofauti ni kawaida yetu kumsikiliza mteja matakwa yake, nikapita njia alizozitaka basi tukawa tunachanja mbuga, nikamwambiab"Bro kwani tunaelekea wapi?" Akanambia "wewe twende"
Huyu kaka alikuwa amebeba kibegi, kibegi hiki ni vile unaweza kukiweka kwenye mabega si begi kuubwa ni kibegi cha mkanda mmoja ambacho alikuwa kakigeuzia kwa mbele, baada ya muda nikaingia kwenye lami kwani hakukuwa na ujanja tena ni lazima ilikuwa tuipate njia kubwa kutokana na eneo ambalo anakwenda, tuliposhika barabara kubwa kama dakika kumi mbele tuliona kama magari yanakuja upande wetu, unajua tena barabara kubwa magari hayaepukiki, mara yakawa yanapiga honi kwa nguvu, jamaa akanambia "nakuomba ongeza spidi"
Nikamwambia "kwanini niongeze spidi kwani kuna shida gani acha wapite hao" Akanambia "nisikilize mimi hao watu wanatufuata sisi" Nikastuka sana na nikamuuliza "wanatufuata?" Akasema "eeh wanatufuata inabidi uongeze spidi"
Nikamuuliza "wanatufuata kwani tumefanya kosa gani? Akanambia "nisikilize mimi kijana acha ubishi we ongeza spidi tu hao watu wananifata mimi" Ikanibidi nitii nikaongeza spidi na akanambia "hawa watu wakitukamata hawatataka kujua wewe ni nani yaani wote tutapigwa risasi za vichwa na uwe ndio mwisho wetu,ongeza spidi".
Nilitii na kuongeza spidi hatimaye wale watu hatukuwaona tena tukawa tunaelekea njia kama vile nje ya mji akawa ananisisitiza "kazana, kazana"
Na kwa sababu kiasi nilikuwa najua njia za mikato tukawa tunapita hizo tunarudi njia kuu lakini ukiniuliza kwanini alikuwa ananiambia niongeze spidi mimi sijui kabisa kwani hata nilipokuwa nikimuuliza jibu lake kwangu lilikuwa "Haya mambo wewe hayakuhusu, hao watu wananifata mimi"
Nakumbuka kweli nyuma kukawa shwari hakuna watu wanaotufuata, tukafika sehemu moja nje sana ya mji yaani ni mbali sana sikuwahi kupata abiria wa kuja huku kabla, tukafika mpaka uko sasa akanambia "Basi sasa mimi nashuka", Yaani kwa sababu nilikuwa nimeacha vioo wazi ile nataka kusimamisha gari huyu kaka aliruka, yaani alichoropoka kama panya,aliruka na kibegi chake. Nikamwambia "Bro si utaumia" Akasema "sasa basi we geuza uende zako na hakikisha hawa watu haukutani nao na ukikutana nao ujue watakuua"
Nikamuuliza "kwanini bro?" Akasisitiza
"unaporudi tafuta njia yakuweza kuwakwepa wale la sivyo watakuja kukuua hao sio watu wazuri watakuja kukuua amini hivyo"
Mimi mpaka hapo sikujua lolote,sikujua kwanini alikuwa ananiambia maneno hayo, sijui alikuwa amefanya kitu gani, sijui walikuwa wamekoseana nini,nikageuza gari kuanza kurudi wakati huo nikawa nampigia simu bro kumjuza kuwa nimekutana na kitu ambacho kinanitisha, nikawa napiga simu ya bro John na simu yake ikawa haipatikani hewani, simu yake haipatikani na mbaya zaidi hata namba ya simu ya huyu mtu niliyempakiza pia sikuichukua kwa sababu ilikuwa kuachana ni chapchap halafu yupo kama kuna kitu flani ananificha namimi sijui lolote, uoga ulitanda ndani ya moyo wangu,amani ilinipotea kabisa.
Nikageuza gari kinyonge na kuanza kurudi, nikarudi nikiwa na tahadhari maana niliambiwa hawa watu nisikutane nao au wasinione, kumbe hii ilikuwa ni siku mbaya kwangu, ilikuwa siku mbaya, mbaya, mbaya sana, wakati niko barabarani mara ghafla hawa watu sijui walitokea wapi, sijui hata kama walikuwa wanajua kama mimi ninarudi niko barabarani gari moja nyeusi na nyingine yakawa yananifuata kwa kasi, ni lile lile la mwanzo na la pili nayaona yakijia upande wangu kiukweli niliogopa mno, niliongeza spidi lakini hawa watu walikuwa spidi zaidi yangu, yaani ukiniuliza nilikuwa nakimbia nini kiukweli hata mie nilikuwa sijui lakini lazima nikimbie kwani nilisisitizwa kukimbia kwani nikisimama nitapigwa risasi, mimi sijafanya kitu nilimbeba tu huyu abiria na wala sijui lolote.
Kila nilipokuwa nikimpigia bro John nikawa simpati hewani, namba ya huyu mtu sina yaani nimejikuta ninaucheza mziki nisioujua kiukweli sikujua ntakuwa mgeni wa nani mie....
Comments