SEHEMU YA 01..
Ni saa moja dakika saba katika website maarufu ya JamiiForum linaonekana tangazo katika jukwaa la Connect , tangazo ambalo limetolewa na ID yenye jina la Ngwena.
Ajira: Boyfriend anatafutwa.
“Husika na kichwa cha tangazo, mimi ni msichana wa miaka ishirini na nne natafuta mwanaume ambae ataigiza kuwa boyfriend wangu kwa mkataba wa mwaka mmoja, vigezo ninavyovitaka ni mwanaume wa miaka 20 mpaka 30 awe ni mwenye kujiamini, dini yoyote, Mwonekano wowote lakini ukiwa mtanashati ni kigezo cha ziada, Elimu angalau ya chuo cha kati kuendelea, mshahara kwa mwezi si chini ya laki tano na maongezi yapo, kuhusu mimi zaidi utanifahamu baada ya kukidhi vigezo, Kama umevutiwa na kazi hii njoo PM jielezee kwa ufupi na weka mawasiliano yako”
Jukwaa la Connect mara nyingi hutumika kuunganisha watu ambao wanatafuta kuingia katika mahusiano ya aina mbali mbali aidha yale ya urafiki wa kawaida au yale ya kupelekea uchumba hadi ndoa, hivyo mwana jukwaaa mwenye ID ya Ngwena alitumia haki yake kuweka tangazo la namna hio , ijapokuwa tangazo limekaa kibiashara au kiajira lakini kwa namna moja ama nyingine lilikuwa likihusisha mahusiano.
********
Sifa yake kubwa ni mkimya lakini sio mpole, ni mtu mwenye kufikiria kila neno analolisikia na kulisoma mahali kwa kutumia akili nyingi, Hamza anaamini kuna zaidi ya maana katika kila neno analotamka binadamu na hii inampelekea kuwa kati ya watu ‘Overthinker’ sana , kwa mfano Hamza unaweza kumtania ila ule utani yeye akauchukulia siriasi , ijapokuwa hakukasirika lakini utani ataugeuza na kuanza kujitafakari kwa nini ametaniwa hivi na vile.
Hakuwa mchangiaji wa mada , lakini alipenda kusikiliza michango na maoni ya wengine , hakuwa mpenzi sana wa kuanzisha mada kwenye mitandao ya kijamii , lakini alipenda sana kusoma maoni ya wengine na mada za wengine , huku akiamini kwa kupitia maoni yao angeweza kufahamu tabia za watu mbalimbali kwa kuchanganua zaidi ya maana kwa kila maoni ya mtu mmoja mmoja , hayo ndio maisha ya Hamza na alipenda sana mtandao wa Twitter na JamiiForum.
Hakupenda kujichanganya na watu wengine, lakini alipenda sana mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa sana huku akijiaminisha kwamba mitandao ya kijamii ndio sehemu ambayo watu wanaweza kuwakilisha uhalisia wao kwa urahisi kupitia maandishi kwani hawakuwa wakionekana kwani wengi wao walitumia utambubulisho feki,Kwa tabia yake hio unaweza kumuita Jasusi wa mtandaoni.
Licha ya hayo yote lakini Hamza ni moja wapo ya vijana ambao unaweza kusema ni wenye moto unaowaka ndani , moto wa upambanaji, moto wa kutodharau fursa iliopo mbele yake, ni kwamba tu kila fursa aliokutana nayo haikuwa kubwa ya kumtajirisha lakini ilimfanya kusongesha maisha yake.
Sasa Hamza ndio moja wapo ya watu walioweza kuona tangazo la ajira ya kuigiza kama boyfriend, ilikuwa ni majira ya usiku wa kwenda saa mbili na baada ya kusoma Tangazo hilo alivutiwa sana , akiamini lazima kutakuwa na Maoni ya kuchekesha na ndio alichokutana nacho.
Ni kweli Tangazo lilikuwa likijipambanua kwamba ‘Boyfried’ wa maigizo anahitajika kama ajira isio rasmi, lakini tangazo lilikaa sana kitapeli kwa watu wengi , nani anaweza kuamini mwanamke wa kitanzania kuajiri mwanaume kwa kumlipa malipo ya laki tano kwa mwezi kwa kuigiza kuwa boyfriend, ni jambo ambalo sio kawaida kabisa , hivyo maoni mengi ya wachangiaji ilikuwa ni matusi na dhihaka huku ID(jina la utambulisho) feki ya jina la Mnyoo ukiongoza kwa dhihaka lakini upande wa mtoa mada hakujibu chochote ni kama alitoa tangazo na kisha akapotea,watumiaji wa mtandao huo wanayo kauli ya kusema Uzi unatembea kwa kasi mno na hiko ndio kilichokuwa kikiendelea ,wachangiaji wengi wakiwa ni wale wenye ID za kiume.
Hamza aliendelea kusoma maoni huku mengine yakimchekesha sana, hakuwa na mpango wa kutoa maoni lakini watu walivyocharuka ilimfurahisha sana , baada ya kusoma karibia maoni yote alirudia upya kusoma tangazo lenyewe na kuanza kulitafakari kama ilivyokuwa tabia yake ya kutafuta zaidi ya maana kwa kila mtu anachoongea au anachokiandika kwenye mitandao, ndio tabia yake ambayo kwa umakini aliokuwa akitumia kuchambua mawazo na maandishi ya watu ungedhania analipwa alichokuwa akitafuta ni kujua kwanini mtoa mada alikuwa akidhihakiwa kwa kiasi kikubwa.
Hamza katika siku zote alizokutana na matangazo ya ndoa na kutafuta wenza hili kidogo lilikuwa na upekee , aligundua kulikuwa na zaidi ya maana , zilikuwa ni hisia ambazo hata yeye mwenyewe alishindwa kuzielewa , lakini ile tabia ya kufatilia maoni ya watu na mabandiko ilimwongezea utashi(Instinct) wa kuelewa hisia za watu kwa haraka zaidi kupitia kile wanachokiandika na wanachokitolea maoni na ndio alichokutana nacho , wakati akiendelea kusoma kwa kurudia rudia hilo Tangazo ujumbe wa meseji kwenye simu yake ya Tecno Spark 5 uliiingia , aliufungua haraka sana na kuona ni muamala wa pesa.
“Huyu Mzee leo kanikumbuka” Aliongea mwenyewe bila furaha huku akiangalia ile meseji, sababu moja ya kutokufurahia ule mwamala ni moja tu , hela iliotumwa haikuwa ikimtosha kwa matumizi kabisa achana na madeni ambayo alikuwa akidaiwa chuoni.
Kila ikifikia hio tarehe ndio siku ambayo alikuwa akipokea muamala kwa mwanaume anaemfahamu kwa jina la Mzee.
Miamala ambayo Mzee alikuwa akituma ni kwa kiasi anachojisikia yeye mwenyewe atume shilingi ngapi , mbaya zaidi ni kwamba Hamza hakuwa na uwezo wa kumpigia simu Mzee na kumwambia amwongezee kidogo.
Tusichokijua kuhusu Hamza ni kwamba alikuwa ni Yatima na kuna stori kubwa ya maisha yake iliomtokea mkoani Rukwa huko Sumbawanga ambayo ndio ilimfanya kuwa mtoto Yatima lakini pia kumkutanisha na mtu aliefahamika kwa jina la Mzee.
Maisha yake yote tokea kupatwa na janga la ajali huko Sumbawanga iliopelekea kupoteza ndugu zake na mzazi wake mtu ambaye alimsaidia mpaka kufikia katika umri huo ni huyo Mzee..
Mbaya zaidi kuhusu Mzee ni kwamba alimuona mara moja tu na ilikuwa ni usiku wa mvua kali na wakati huo alikuwa na miaka tisa akiwa darasa la nne na mpaka wakati huu akiwa na miaka ishirini na tisa hakuwahi kumuona tena, miaka ya mwanzoni aliwasiliana na mzee kwa barua , lakini mara baada ya ujio wa simu aliwasiliana nae kwa jumbe za meseji tu na siku zote Mzee angemtumia Hamza ujumbe kwa ‘Private number’(Namba ambayo huwezi kurudisha jibu) tena ikiwa ni nyakati za usiku pekee.
Kwa maneno marahisi ni kwamba Hamza alisaidiwa kimaisha na Mzee ambaye hakuwa akimfahamu kwa sura yake halisi na ndio maisha yake yalivyokuwa mpaka kufikia umri huo,
Mzee alikuwa akimsaidia vitu vingi lakini hakuwahi kujionyesha kwake.
Hamza baada ya kupatwa na hasira kwa kiasi kile kidogo cha pesa alichopatiwa na Mzee alijikuta akirusha pembeni simu yake kwenye godoro ndani ya chumba chake alichopanga katika eneo la Gongo la mboto jijini Dar es salam.
Chumba chake hakikuwa na vitu vingi kabisa , kilikuwa na godoro dogo kama yale ya wanafunzi, mtungi wa gesi na baadhi ya vyombo vichache pamoja na chandarua.
Alikuwa pia na mabegi mawili , moja kubwa kidogo la wastani na lingine ni la saizi ya kati ambalo hutumia kuwekea nguo zake, maisha yake yalikuwa ya chini sana huenda kuliko mwanafunzi yoyote anaesoma ndani ya chuo cha FEMU(Future Enterprise and Monetary University).
Baada ya kujilaza kwenye godoro lake alijikuta akipotelea usingizini na alikuja kushituka ni siku nyingine kabisa ya jumatatu , alijiandaa haraka haraka kwa ajili ya kwenda Chuo.
Baada ya kutumia zaidi ya lisaa limoja na nusu kujiandaa kutokana na kusubiria zamu yake ya kuingia bafuni kufikia , hatimae aliweza kusogelea vituo vya daladala kwa ajili ya kupanda ambazo zingemwezesha kufika chuoni.
Njia ilikuwa na foleni na kwa bahati nzuri aliweza kupata siti ya kukaa , hivyo alitoa simu yake mfukoni na kuendelea kuperuzi peruzi mtandaoni huku Earphone zikiwa masikioni.
Hamza ni aina ya watu ambao hawakupenda kabisa kusikiliza maongezi ya abiria kwenye daladala na miezi hio habari za uchaguzi zilikuwa zikijadiliwa sana kwenye magari kwani ilikuwa ndio mwaka wa uchaguzi na ilikuwa kama miezi mitatu tu hivi siku ya wananchi wa taifa la Tanzania kupiga kura , lakini kwa upande wake yeye hakuwa hata na mpango wa kupiga kura, kwanza hakuwa na chama na wagombea wote hakuna ambaye alikuwa akimvutia japo mmoja wapo ya wagombea aliweza kusikia akijinadi kwamba atakwenda kupambana na rushwa pamoja na Madawa ya kulevya nchini, kauli hio kidogo ilikuwa ni sera iliojitosheleza kulingana na hali ya taifa kwa ujumla lakini Hamza kwa mtazamo wake hakuwa na uhakika kama sera hio ingeweza kutekelezeka.
Katika kipindi cha miaka mitano iliopita madawa ya kulevya yalikuwa yameathiri sana vijana wa kitanzania , haikueleweka nini kinaendelea nchini kutokana na kuongezeka kwa wimbi la wagonjwa ambao wana uraibu wa madawa ya kulevya katika hospitali zenye vituo maalumu vya kusaidia wagonjwa hao.
Takwimu za kiserikali zilikuwa zikionyesha kwa wastani wa siku hospitali ya rufani ya Muhimbili hupokea zaidi ya wagonjwa wa tano wapya wanaofikishwa kwa ajili ya kutibiwa uraibu wa madawa ya kulevya.
Inawezekana ikawa idadi ndogo lakini kimahesabu ni idadi kubwa sana na hilo lilimaanisha kwamba kuna zaidi ya wagonjwa wenye uraibu huo uraiani ambao hawakufikishwa hospitalini.
Sasa Hamza kutokana na kuishi uswahilini alikuwa akikutana na watu wa aina hio wanaotumia madawa ya kulevya kwa kiwango kikubwa , ndio maana sera ya mgombea mmoja wa chama fulani cha kisiasa baada ya kutaja vipaumbele chake ni kupambana na dawa hizo aliona angalau ana mantiki lakini kwasababu anazozijua yeye aliona ni sera ambayo ni ngumu sana kutekelezeka.
Hamza akiwa kwenye gari kama hivyo huwa ni mwenye kuyafikiria mapito yake na asubuhi hio alipokuwa akielekea chuoni alijipa muda wa kufikiria nia ya mzee katika maisha yake.
Ukweli ni kwamba maisha yake yote ni kama yameshikiliwa na huyu mtu anaejiita mzee ndio maana alikuwa akiwaza na alijiambia huenda kama sio Mzee angetafuta uelekeo mwingine wa kimaisha na kuacha kuendelea kuishi maisha ya kimaskini yaliojaa maigizo ndani yake.
Tatizo moja tu kuhusu Mzee ni kwamba alikuwa anamtishia sana maisha yake pale tu asipotii maagizo yake, kwa upande wake huenda mtu ambaye anamuogopa katika maisha yake ni huyo Mzee.
Kilichomfanya kumuogopa zaidi ni kwamba ukiachana na kumsaidia kimaisha mpaka kufikia umri aliokuwa nao Mzee hakuwa akionekana na hata mawasiliano yake yalikuwa ni nyakati za usiku lakini kutokuonekana kwa Mzee mbele yake haikumaanisha hakuwa na nguvu, alikuwa na nguvu kubwa ambayo Hamza mwenyewe ameweza kuishuhudia kwa macho yake katika kila hatua aliopiga katika maisha yake akiwa chni ya uangalizi wa Mzee.
Kuhusu swala hilo lilikuwa likimfikirisha sana miaka na miaka na kujiuliza kuna siri gani ya huyu mtu anaefahamika kwa jila la Mzee kumtafuta tu usiku.
Hamza akiwa kwenye daladala ambayo ilikuwa kwenye msongamano wa magari , palepale alijipa muda wa kufikiria maisha yake ya nyuma namna alivyokutana na mzee.
Comments