Reader Settings

Part 2


Naendelea kuelezea mikasa niliyokumbana nayo katika harakati zangu za utafutaji na kama nilivyowaelezea awali niko katika harakati za kuwakimbia wale watu ambao hadi wakati huu sijawajua kiundani hawa ni wakina nani,sijui ni majambazi ama ni polisi mi kikubwa nilichoamua ni kukimbia kadri nitakavyoweza ili kuwakwepa hawa watu.

Niliongeza spidi ya lakini hawa watu walikuwa wanakimbia zaidi na hofu ilizidi kunitanda moyoni mwangu,nikawa nawaza peke yangu aliyesababisha yote haya ameshashuka na gari hili siwezi kulitelekeza njiani kwani bro John amenikabidhi mimi je ntaenda kumueleza nini kama ntalitelekeza? Mawazo kiukweli yalinitinga sana na ukitilia maanani namba za simu za bro John zilikuma hazipatikani hewani muda wote huo,mbio za sakafuni huishia ukingoni ikanilazimu kusimamisha gari na wakaniamuru kutelemka garini tena katika eneo lenye giza nene ni mwanga tu wa taa za gari ndizo zilikuwa msaada wa kuweza kuonana,nikatii amri zao ila nikawauliza
"mbona siwafahamu nyinyi ni wakina nani?"

Hiyo ndio ilikuwa sentensi yangu ya kwanza kwao,kabla sijapata jibu mmoja kati ya wale watu alinipiga ngumi moja ya uso, yaani katika maisha yangu toka nizaliwe sijawahi kupigwa ngumi kama ile,watoto wa mjini siku hizi wangeiita Ndoige,ngumi iliniyumbisha na kunipeleka mweleka mpaka chini,kiukweli kila nikitizama hili eneo nilikuwa silielewi hata kidogo kwani ramani ilinipotea nikawa najiuliza peke yangu ni wapi hapa? na ukitilia maanani ule mfukuzano na hawa watu hata sikuelewa niko eneo gani,nakumbuka niliwauliza tena
"Mbona mnanipiga,mbona mnanipiga mimi nimefanya kosa gani?"
Mmoja wao akasema kwa kufoka
"mshkaji ameshatutoroka huu ni uzembe wa hali ya juu sana,hatukutakiwa kufika hapa na kama tungefika mapema tusingefika hapa"

Lakini mwingine akasema "huyu anajua alipo" nikamjibu
"Mimi simjui huyo mtu mnayemtafuta mimi nilimbeba kama abiria tu na mimi nilimpakia akaanza kunambia kuna watu wanamfata"
Mmoja wao akasema "nyamaza,nyamaza wakubwa wanapozungumza,ameelekea wapi huyu mtu?
Nikawajibu mi simjui huyu mtu mimi ni dereva tu na hii gari mi si ya kwangu mi ni Deiwaka tu"
Ghafla nikapigwa ngumi nyingine
"Tumekwambia tulia"

Waliingia kwenye gari wakawa wanasagula sagula sasa kwa sababu mimi sikuwa najua wanachotafuta ila kwakuwa niliambiwa nisizungumze chochote nikawa natizama tu tena nikikumbuka zile ngumi mbili nilizotwangwa nikawa mdogo nisije nikaongweza nyingine zikaweza kuniletea kizaazaa mwilini,taa za gari yangu zikiwa zinawaka,taa za gari nyingine zikiwaka na za gari nyingine pia zikiwaka nikaamrishwa
"Kaa chini,kaa chini,kaa chini"
Sasa kwakuwa nimeona hawa watu idadi yao ni kubwa na mimi nipo peke yangu hata wakiamua kunifanyia vitendo vibaya nani atakayejua? Wakiamua kunipoteza ndugu yangu gani atakayejua? Nililala kifudifudi na nakumbuka kaka mmoja kati yao alikuwa amevaa kiatu kizito kwelikweli kama buti akaja akanishindilia si unajua mtu akikukanyaga kwa nguvu mgongoni nikawa nahangaika akawa ananambia "tena nakwambia utulie,utulie,utulie hapo wakati tunawatafakali"

Mmoja kati ya hawa walioniweka chini ya ulinzi akawa anawaambia wenzake "kwa kupitia huyu kijana tutampata huyu mshkaji wala hakuna haja yakupaniki,huyu huyu atatupeleka mpaka mlangoni kwake"
Lakini mwingine akasema "huyu hajui lolote si unamuona? Hajui chochote na kama angekuwa anajua mi ningeshajua hapa tunapoteza muda tu"
mwingine akasema "huyu ni kijana na tena ni Deiwaka mwenye gari hii atatupa taarifa za huyu mtu,mwenye gari hii atatupa taarifa za huyu mtu,kwahiyo chakufanya hapa tufanyaje?"

Wakawa wanajadili hapa huku mimi nimelazwa kifudifudi,mmoja akasema "tuondoke na hii gari" wakanambia "inuka" yaani ni watu wa milaba minne wameshiba haswa wakaniamrisha kuinuka na kuniuliza "wewe umesema ni Deiwaka haya mwenye hii gari ni nani? " kiukweli sikuweza kuficha nikawaeleza mmiliki wa gari kuwa ni kaka yangu ambaye ananiachia mara kwa mara na sijui chochote,wakaniuliza anaitwa nani? Mi nikawatajia jina lake
"Mpigie simu sasa hivi,taja namba yake"
Nikawajibu "kiukweli huyu mtu hapatikani,nimempigia muda mrefu hapatikani"

Kiukweli naikumbuka sana siku hii,katika harakati zangu zote za kufanya kazi ya udereva sitaisahau hii siku,niliwaambia "mimi sifahamu chochote nawaomba msinifanye jambo baya lolote huyu ni mtu tu nilimbeba kama abiria"
Mmoja wao akanambia "huna sababu ya kujieleza utaondoka mazingira haya kama ulivyo na vitu vyako vyote utaviacha hapa"
Nikaacha kila kilichostahili kuacha na kile kisimu changu nilichokuwa nacho na kwa kutizama mazingira haya jinsi nilivyo na ukitilia maanani ulikuwa ni usiku niliona ni bora nitafute njia ya kutoka kuliko kuendelea kubishana na hawa watu nikaukumbuka msemo wa wahenga mwenye nguvu mpishe nami sikuweza kuendelea kung'ang'nia visivyowezekana,nikaondoka nakujisemea moyoni kama ni gari kaka atashughulikia acha nitoke kuliko kuendea kuwa katika mazingira hatarishi,nilipopewa ruhusa ya kuondoka katika mazingira haya sikujali giza,sikujali ninamjua nani,sikujali naelekea wapi ilikuwa mimi ni kukimbia kutafuta mpenyo wa kuweza kupata msaada,nilikimbia sana na giza hili sikugeuka nyuma nilikimbia hadi nikakutana na mazingira ambayo niliona naweza kupata msaada,nakumbuka nilienda katika nyumba moja na kugonga ili kupata msaada majira haya ya usiku,Tanzania ni nchi nzuri na yenye amani sana,nilibisha hodr na kuomba msaada nikafunguliwa na wenyeji wangu wakaniuliza nilikuwa nimetoka wapi isitoshe usiku ulikuwa mkubwa,nilikuwa natokwa na jasho jingi,wakawa na taharuki na waliendelea kuniuliza maswali kujiridhisha kama ni mtu mwema nami nilijieleza kadri ya uwezo wangu ili niweze kupata msaada,walinambia sijui twende kwa mwenyekiti wa mtaa nikawaambia "naombeni angalau tu nipumzike na huko kwa mwenyekiti tungeenda kutapopambazuka" kwa imani waliniamini na wakanipa msaada na kulipopambazuka nikafanya utaratibu wa kurudi nyumbani huku nikiwa sina simu,sina chochote,sijui kaka yupo wapi na sijui ntakapomueleza atayapokeaje haya ambayo namwambia.

Hatimaye nikafika nyumbani na kuwaeleza ndugu zangu kile kilichotokea,wao wakapigwa na mshangao na kuniuliza "si umeondoka hapa mkiwa mnaongea imekuwaje tena hapatikani? Huyo uliyembeba alikuwa amebeba nini? Maswali yalikuwa lukuki lakini mimi nikawa sina majibu ndipo kaka mkubwa ambaye yeye ndiye alikuwa anafahamiana zaidi na huyo kaka alisema atamtafuta,alitafutwa hapatikani,alifatiliwa mahali ambapo anaishi huyu kaka John ambaye alinifundisha mimi udereva hakupatikana nyumbani kwake kwahyo hata mimi nikawa sina jibu la ya chochote katika kile kilichotokea,simu nimeacha,gari nimeacha na kaka huku anatafutwa hapatikani kwahiyo ishu ni kama inaishia hapo lakini kaka alinambia ni vyema twende kituo cha polisi kutoa hizi taarifa kwa akiba lakini mimi nikamjibu sawa tunaweza kwenda lakini kaka John akisikia tumeenda uko anaweza asipendezwe na kwanini tusizungumze nae kwanza alafu tuweze kujua anatushauri vipi,tunaweza kwenda polisi tunaweza kujikuta tunamuharibia yeye pia na kumbe ni mambo ambayo anayafahamu pia,mimi nilishauri hivyo na hata kaka akasema ni kweli lakini hatuwezi kujua watu hawa ni wakina nani wanaweza kuendelea kukuwinda wakati wewe hauelewi chochote,mambo haya tulizungumza kama familia lakini ilibidi tuwe wapole kumsubiria bro John kujua atakuja kusema nini kuhusiana na hiki kilichotokea nami nimueleze gari yake mazingira ambayo nimeiacha kule kwa wale watu ambao walinikamata.

Tumekaa siku nne toka lile tukio kutokea kwahiyo tukawa katika hali ya ukimya tu na kuruhusu maisha mengine yaendelee,nakumbuka niko tu home kwa sababu hata ile mood ya kufanya kazi ilikuwa imekata kwa changamoto hizi nilizokutana nazo,kaka alikuja (kaka yangu huyu kabisa) akanambia "kuna tatizo,yaani nimepata taarifa ambayo sio nzuri tena sio nzuri hata kwa upande wetu sisi pia"
Sikujua zinamuhusu nani lakini kaka akasema "nasikitika mpaka sasa hivi mshkaji hapatikani,hajulikani wapi alipo"
Nikamwambia kaka "taarifa gani?
Kaka akanambia taarifa ambazo anazo ni kuhusiana na mimi,kaka anasema kuwa leo leo nakuja kukamatwa
"Kuhusu nini? Kaka mbona unanambia mambo ambayo siyaelewi? Kaka akanambia "unatakiwa utulie na unisikilize kila ntakachokisema,ile ishu iliyotokea siku ile,ile ishu iliyotokea usiku ule haijawa nzuri ndio maana nilikwambia twende kituo cha polisi tukatoe taarifa na hata niliuliza kuna mshkaji alinambia nendeni kituo cha polisi mkatoe taarifa mambo kama haya msinyamaze nayo nyumbani"
"Kaka nini kilichotokea kwanini unanitishia maisha?kwanini unambie mambo nusunusu? Akanambia "yule kijana ambaye siku ile alipanda gari yako amepatikana ameuwawa,nikamjibu "kama amepatikana na ameuwawa mimi nahusika vipi hapo? Yaani kwanini uone hii kwangu ni taarifa mbaya? Alishuka akaenda zake mimi najua nini na nani alikwambia hizo taarifa za uongo,nani alikwambia?"

Mimi nilipokea taarifa katika mazingira haya lakini kumbe kaka alikuwa na taarifa zaidi ya hizi alizonieleza kuwa ni kweli yule kaka ambaye nilikuwa nimembeba ambaye sikuwa namfahamu zaidi ya kuambiwa na kaka ambaye alinifundisha udereva kuwa nikambebe na hata nilipotaka namba yake alinambia wewe nenda uko uko garini utamkuta yeye hii gari anaijua,sasa kama amepatwa na matatizo mimi sasa nahusika vipi na matatizo yake?
Mambo kumbe hayakuwa mepesi kama nilivyokuwa nikiyawaza kichwani mwangu au nilipokuwa nawaza yaliponitokea kwamba kaka atafanya utaratibu atapata gari yake,sikuwaza hasa kuhusiana na yule kijana kwanza alishatoka na kukimbilia uko akisema ana mzigo ingawa mimi niliona kipochi sijui mzigo ni mzigo gani,ni kweli mimi nilikuja kufatwa na askari polisi "wewe ni Rojaz?
"Ndio"
"unamfahamu flani?"
Sasa mimi majina ya yule mtu hata siyajui
"Mara ya mwisho wewe ndio ulimchukua kwenye gari yako na hakuonekana na alipoonekana tayari ameshakuwa katika hali ya umauti,tunakuhitaji kituo cha polisi"
" Yaani mimi Deiwaka nisiyekuwa hata na gari jamani,nimepigiwa simu nikambebe abiria leo matatizo ya mtu mnataka kunitwisha mimi kwa sababu gani? Mi sijui chochote"

Unajua katika hali ya taharuki unapopewa taarifa kama hii unaweza sema "mi simjui huyo mi simjui"
"Aah sasa kwani sisi tumesema wewe umetenda? Sisi tunachojua mara ya mwisho ulikuwa nae kwahiyo tutakapokwenda kule kituo cha polisi utaenda kupata maelezo zaidi,bila kutumia nguvu basi fuata utaratibu tunaokueleza" kaka alikuwepo wakati huo akanieleza "ni kweli mdogo wangu haujui chochote,sheria iko hivyo,ni kweli humjui jina lake nawe ni Deiwaka kama unavyosema nami najua hivyo lakini lazima uende kituo cha polisi" nikamwambia kaka "mimi kituo cha polisi siendi,siendi mimi kituo cha polisi" polisi walinizoa mzobe mzobe kunitoa pale wakinambia wananichukua ili kuweza kunihoji ilikuwaje mara ya mwisho,kwanini akutwe na hili jambo ndio walivyonieleza,nilipofika kituoni kile walichoniahidi kule nyumbani kilikuwa tofauti kabisa yaani kwenda kituo cha polisi ni rahisi lakini kuondoka katika hayo mazingira sio rahisi,nikajikuta katika mazingira hayo nikiwa sielewi nini nitafanya,taharuki pia ilitokea kwenye familia yetu lakini aliyenifundisha udereva,yeye ambaye alinituma mimi nikamchukue huyu mtu hajaonekana toka siku ile mpaka mimi nimefight nimerudi nyumbani basi nae atafutwe aelezwe kuhusu hili,hapatikani mpaka sasa hivi!

Kwahiyo mimi nikawa nimeshikiliwa kituo cha polisi "niachieni mimi nirudi zangu nyumbani,niachieni mimi nikaendelee na maisha yangu mimi sijui chochote,mi sijui chochote" habari ya kwamba hujui chochote mpaka ije ithibitishwe kuwa hujui chochote ni lazima hapo wafanye kazi yao inabidi utulie na kaka aliniambia "tulia usiongee sana,usiongee sana haya ni mambo ya kisheria ndio maana tulishauriwa tutoe taarifa kituo cha polisi kwa sababu tutaulizwa kama hayo yaliyotokea mliripoti wapi? Tutajibu nini? Ina maana tuna vitu tunavijua,hakuna muda wa kulaumiana ni kufata taratibu za kisheria zinavyosema,mambo yatakaa sawa"

Kwa upande wangu kilio ndio kilikuwa kimeshika hatamu nikiwaza toka nizaliwe nilikuwa sijawahi wekwa lock up leo nimekutwa na mkosi gani huu,mi ni kijana ambaye naishi kwa amani na wenzangu na nafanya kazi zangu bila ya zengwe lolote lile,sijawahi kupora mtu,sijawahi kumfanyia hila mtu yoyote yule mi napiga mishe zangu najipatia chochote cha kujikimu maishani leo naambiwa "sasa utapumzika hapa" Nini hasa kilichotokea hata mimi nilikuwa natamani kujua kwa sababu sijui chochote na walionikamata pengine wanahisi nina maelezo zaidi nitasema lakini sijui chochote yaani kama wao wanavyojiuliza nami mwenyewe najiuliza sijui chochote,mtu huyu ameuwawa vipi wakati alinambia "hakikisha unatoka katika mikono ya hawa watu,wakikukamata watakuua"unaona na yeye ndio aliniambia "unaona huu mwendo tunaoenda nao? Ukisema ujisalimishe hapa,usimamishe gari tutapigwa risasi za vichwa hatutapata hata nafasi ya kujieleza,utajieleza mbele ya safari" na mimi hofu,taharuki ndicho kilichonikimbiza mpaka nipo hapa kizuiani sina nafasi ya kufanya chochote wala kujitetea kwa loloje.

Previoua