Chimera.
Mvua ilikuwa ni kubwa mno ndani ya jiji la Paris chini ya anga jeusi, minunurisho ya mwanga wa taa katika maji ilikuwa imesambaa kila mahali. Jiji hilo la kimitindo na la mapenzi lilibadilika ghafla.
Pembezoni mwa Bar moja ambayo inauza vinywaji kama bia na mvinyo alionekana mwanaume alievalia nguo nyeusi akiwa amesimama na mwanvuli wa rangi nyeusi.
Alikuwa amevalia koti refu lililovuka magotini( Trench Coat) la rangi nyeusi na kofia ya hat rangi nyeusi pia. Ukiachana na mwamvuli alikuwa ameshikilia kibegi kidogo cha leather rangi nyeusi , na muda ule alonekana kufungua kibegi kile na alitoa kitu kama mfuko wa nailoni hivi ambao umetuna na kuutupia kwenye ndoo ya takataka.
Baada ya kufanya vile , palepale hakujali mvua iliokuwa ikinyesha kwani na mwamvuli wake alitokomea katikati ya nyumba mbele yake.
Dakika moja mbele alionekana kijana mzungu mwenye nywele zilizojikunja kunja akitoka katika ile Bar akiwa amevalia Aproni.
Alisogelea ndoo ile ya takataka bila wasiwasi na kisha alichukua ule mfuko na kuingia nao ndani ya Bar ile.
Zoezi hilo lilifanyika ndani ya dakika mbili tu na kwa giza na mvua iliokuwa ikinyesha , ilionyesha hakuna mtu ambae ameshitukia.
Lakini upande wa mbele katika jengo refu kulikuwa na mtu alieshikilia darubini akiangalia jambo lile kwa umakini mkubwa bila ya kutoa sauti yoyote.
*****
Nusu saa mbele katika makao ya muda ya kikosi cha Malibu ndani ya hoteli.
Mkurugenzi wa kikosi cha Malibu kwa masuala ya kigeni , Balozi Rajabu , alionekana akiwa ameketi mbele ya tarakishi mpakato, alikuwa akivuta sigara lakini umakini wake wote ulikuwa ni kwenye monita ya tarakishi hio na alionekana kufikiria kwa kina pia juu ya kile anachoangalia.
Balozi Rajabu alikuwa mlevi wa sigara ndio maana alichagua chumba cha peke yake ambacho kingemruhusu kufanya kazi huku akiwa anavuta sigara
“Ding Dong!
Mara baada ya Balozi Rajabu kusikia kengere ya mlango haraka sana alifunga laptop yake.
“Nani?” Aliuliza
“Balozi , nimekuletea chakula”Alikuwa ni Rehema sekretari na msaidizi wake, na baada ya kumtambua Rajabu alisimama na kwenda kufungua mlango.
Rehema alionekana kuchoka kwa namna alivyokuwa akitembea na mkononi alikuwa ameshikilia mfuko ambao ulionekana kuwa na vyakula.
“Pole Rehema kwa kutembea na mvua na asante”Aliongea Balozi Rajabu huku akipokea mfuko ule na tabasamu.
Rehema aliishia kufuta maji ya mvua usoni mwake na kutingisha kichwa na tabasamu hafifu.
“Usijali balozi , hata mimi nilikuwa na njaa”Aliongea huku akimuonyesha mfuko wake wa chakula pia.
Wawili hao hawakupenda chakula cha kifaransa hivyo walienda kwenye duka ambalo lilikuwa likiuza vyakula ambavyo vinaendana na radha ya kibongo.
“Basi sawa, kwasasa unaweza kwenda kupumzika maana hakuna kingine cha kufanya , tutaonana asubuhi”
“Sawa! Usiku mwema Balozi”Aliongea Rehema na kugeuka.
“Hebu subiri kwanza!”Aliongea Balozi mara baada ya kuona Rehema anatokomea nje.
“Kuna tatizo mheshimiwa!?”
“Hebu nenda kaangalie kama Mboma yupo kwenye hii hoteli , nipe taarifa baada ya kuhakikisha”
“Okey!”
Mara baada ya Rehema kutoka , Balozi aliweka chakula mezani na kuanza kula taratibu na dakika tatu mbele alipokea simu kutoka kwa Rehema.
“Vipi Rehema , yupo?”
“Chief Mboma hayupo , msaidizi wake Juma anasema ametoka tokea saa kumi na mbili kwenda kukutana na marafiki zake”
“Okey! Asante kwa taarifa , nenda kampumzike sasa”
“Sawa Balozi”
Mara baada ya simu ile kukatwa , Balozi alifungua tarakishi ile ya mapakato na kisha aliangalia kilichokuwa kikionekana na palepale alionekana kuingia katika fikra nzito.
******
Ndani ya chumba cha hadhi ya raisi katika hoteli ya Four Season , Regina mara baada ya kusikiliza mapigo ya moyo ya Hamza kwa muda , sura ilimjaa aibu.
‘Sitaki tena kusikia , unaongea sana ila sikuamini”Aliongea Regina
“Wife nilichoongea ni kweli , mimi ni mpiganaji na ni kawaida kuweza kudhibiti mapigo yangu ya moyo. Hata wakati ninapopambana na jeshi kubwa mapigo yangu hayabadiliki namna hii . labda tu iwe nimefanya mazoezi makali sana . Lakini nikikukumbatia na kukukiss nashindwa kabisa kudhibiti mapigo yangu ya moyo. Ni aina ya hisia ambazo zijawahi kuzipata tokea niwajue wanawake”
“Wewe umejuaje! Maana sio kama umekutana na wanawake wote kwenye dunia hii . Unajuaje pengine siku moja utakutana na mwanamke mwingine ambae anafanya mapigo yako yaende mbio”
“Ah! Unataka nikutane na kila mwanamke dunia nzima , ili kujihakikishia nani anayabadilisha mapigo yangu ya moyo . Si itakuwa ni kupoteza muda na kama ingekuwa hivyo basi watu wasingeoa na kuolewa”
“Ila mimi sijawahi kupenda hapo kabla , sijui hata mapenzi yakoje… najuaje kama unanipenda kweli?”Aliongea Regina na kumfanya Hamza kuishia kunusa harufu ya marashi ya nywele ya Regina.
“Hata mimi sijawahi, likija swala la hisia hakuna kipimo maalumu, hata mtu aseme mapenzi ni sawa na kujumlisha moja na moja na kisha kupata mbili, ukiuliza kanuni ya kuja na hesabu hio hutopata majibu . Kitu pekee ninachojua ni kwamba nikiwa na wewe hata kama unifokee , uwe na hasira za haraka na kununa siwezi kukuchukia , haijalishi upoje bado nakupenda. Unajua kumpata mtu unaempenda na anaekupenda ni kazi ngumu sana , kwanini unafikiria sana?”
“Jiangalie sasa ulivyokosa aibu , una wanawake kibao lakini unasema unanipenda , unaniona mjinga eh! Mimi najua umenioa kwasababu unajua mimi ni mjinga kati ya wanawake wote uliokuwa nao na ni rahisi kukubali kila unachofanya. Unajua fika kama ungewaoa wengine wasingekuvumilia”
“Wife wewe sio mjinga, una busara kubwa na IQ yako ni kubwa vilevile , kwanini uwe mjinga?”
“Mh! Lazima utakuwa unaniona mimi mjinga mtu rahisi kudanganyika na kukubali kila kitu”
“Wife kwanini unafikiria mbali hivyo , kama ni kweli kulikuwa na haja gani ya mimi kukuoa sasa?”
“Mimi sijui , lazima uliona kwasababu ya ujinga wangu sitokusumbua na kujihisi ni kama upo bachela tu”
“Unachofikiria sio sahihi mke wangu”
“Utajua mwenyewe , muda umeenda na nataka kuosha uso kuondoa makeup”Aliongea Regina akijiondoa kwa Hamza.
“Wife kwani umepaka make up! Mbona haionekani?”
“Wewe ni mjinga! Unadhani kwa sherehe ya leo ningeenda bila ya kujipodoa , huwezi kuona ndio lakini nilijipaka foundation kidogo ili macho yangu yaonekane vizuri. Macho yamenikauka sana , nitaenda kununua lensi nyingine nzuri ili yawe mazuri”Aliongea huku akifikicha macho yake na muda huol Hamza aliishia kucheka baada ya kuona Regina anataka kupendeza macho na lenzi.
“Wife unajua una macho mazuri sana, ni kama umechanganya damu ya mzungu na mwafrika kama mimi”
“Wewe mshenzi huaminiki! Unasema unanipenda lakini umeshindwa kujua nimepaka makeup. Hujali mwonekano wangu kabisa wewe , hebu toka chumbani kwangu kwanza”
“Wife ni kwasababu ya uzuri wako ndio maana sizingatii kabisa mabadiliko madogo”
“Kamdanganye mtoto wa darasa la tatu ndio atakuamini sio mimi”
“Kweli mke wangu , umejaliwa uzuri na silika nzuri, ukiachana na uzuri wako wa sura namna ulivyo tu inatosha kuwapiku wanawake wengi”
“Nilivyo kivipi?”aliuliza Regina.
“Mwonekano wako umegawanyika katika matabaka kadhaa ,yaani kawaida sio kawaida , ni kama upo katikati ya kila aina ya uzuri , ukivaa vizuri ndio unabadilika kabisa , Aura unayosambaza ni kama vile ni malkia kutoka falme ya kufikirika”
“Kadri unavyoongea ndio unavyoonekana muongo , unanisifia kama vile umekula asali, kwa taarifa yako siwezi kulainika kwa kuzidisha kunisifia,hebu toka kwanza nataka nioshe uso”
Hamza aliishia kujiambia moyoni , kwani amemzuia kuosha uso au ndio hivyo tu hataki kukaa uchi mbele yake , lakini alijua fika Regina hakutaka kutengeneza mazingira ya kugawa kitumbua chake.
“Wife usiku mwema , mimi naenda”.Aliongea Hamza huku akipiga hatua na Regina aliishia kumwangalia tu huku kwa namna flani akijisikia vibaya.
“Kesho sitoenda kazini” Aliongea Regina baada ya Hamza kufikia mlango na baada ya kusikia sauti hio aligeuka.
“Basi nitakutoa out kesho tukatembee!”
“Sawa! Asubuhi tutaongea vizuri. Uwe na usiku mwema”
“Na wewe pia mke wangu”
Hamza aliongea akiwa na furaha na kisha alitoka na kufunga mlango.
Hamza mara baada ya kutoka nje alijikuta akihema kwa nguvu , ukweli ni kwamba kipindi cha nyuma hakufikiria sana namna ya kuongea anapokuwa na mrembo , lakini ilikuwa tofauti na alipokuwa na Regina , alijitahidi akili yake ifanye kazi kwa kiwango kikubwa , Lakini hata hivyo aliridhika na namna alivyomsifia.
Hamza alijihisi ni kama amegeuka kichaa ambae anayafurahia maumivu Regina anayomsababishia, maana kadri Regina anavyomwekea ngumu na kumfanya ajisikie vibaya ndio alivyozidi kumpenda.
Hamza hakuwahi kuyafurahia mapenzi na ndio kwa mara ya kwanza alijihisi kupenda kweli, alijua alikuwa amependa kweli maana alivyokuwa akijisikia akiwa na Eliza na Dina ni tofauti sana alivyokuwa na Regina.
Ijapokuwa aliona sio haki kwa wanawake wengine kuchanganywa na mwanamke mmoja , lakini hakuweza kujizuia kufurahia hisia hizo.
“Haha.. nahisi huu ni ujinga ila napenda radha yake”Aliongea Hamza mwenyewe huku akijicheka.
Hamza alijiambia njia rahisi ya kumega tunda ni kuharakisha zoezi la kumchumbia Regina , lakini aliona zoezi hilo lazima lifanyike kitaalamu zaidi. Vinginevyo matokeo yanaweza kuwa tofauti kwa mrembo huyo.
Wakati akiendelea kufikira , bila kujijua alikuwa ashafika kwenye mlango wa chumba chake na kabla ya kupitisha kadi alihisi kuna mtu alikuwa amefika kumtembelea na aliishia kutoa tabasamu la kifedhuli na kisha bila kujali chochote alipitisha kadi na kufungua mlango na kuingia ndani.
Mara baada ya kuingia ndani aliweza kuona kivuli cha mtu kikiwa kimekaa kwenye kiti dirishani. Mtu huyo nywele zake ndefu zilikuwa zimefunika uso wake na mavazi yake machafu yalionekana kuloa na maji ya mvua.
“Aah! Mchafu ya nini kuja kwenye chumba changu usiku wote huu kuniogopesha”Aliongea Hamza akijifanyisha kushituka baada ya kuwasha taa.
Alikuwa ni Asmuntis , kama ninja namba moja duniani kuingia katika chumba kama hicho bila ya kuwa na ufunguo ilikuwa ni rahisi sana kwake.
“Bosi , uko sawa!”Aliuliza Asmuntis huku akiruka kutoka kwenye kiti.
Hamza aliishia kutoa tabasamu na alisogea mpaka kwenye kimeza na kutoa sigara kwenye pakti na kumpatia Asmuntis na kisha alimsaidia kuiwasha.
“Naona umenitembelea usiku usiku?”Aliongea Hamza muda huo akiwasha ya kwake sigara na kufungua mlango wa kutokea kwenye balkoni na wote waliangalia upande wa nje ya jiji.
“Nani mwingine kajua kuhusu mimi?”Aliuliza Hamza , haikuwa na haja ya kuuliza kwanini Asmuntis amefika hapo.
“Ni watu wa Metal Tide. Inaonekana Gonzalez amekosa uvumilivu wa kutaka kupata cheo cha Ugwiji. Isitoshe vikao vya magwiji ni adimu sana kama hivi , nadhani anataka kutumia nafasi hii kuthibitisha mbele ya watu wote kwamba ana hadhi ya kuwa katika orodha ya magiwji kumi wa dunia”
“Kama ana shida sana na cheo hicho ningemwachia tu , kulikuwa na haja ya kutuma watu kunijaribu?”
“Bosi hatuwezi kuruhusu Gonzalez kuchukua cheo cha hadhi yako . Hata kama umepoteza uwezo wako wa nishati , sisi tupo . Inferno ni jamii iliokamilika, wewe ndio uliotutoa kutoka kuwa Clubs na kuwa umoja. Nimekwisha kuwasiliana na Azzle, tutakusindikiza kwenda kuhudhuria kilele cha magwiji . Muda ukiwadia tutakuwa chini ya maagizo yako na kupigana kwa ajili yako. Hatuwezi kumruhusu Gonzalez kushinda”Aliongea Asmuntis akiwa sirasi mno.
“Pepo mchafu , nashukuru sana kwa kunijali . Kwa muda mrefu nilikuwa nikidharau sana hiki cheo , ila kama ndio hivyo basi nipo tayari kuwakaribisha wakibisha hodi. Ukweli mpango wangu ni kustaafu moja kwa moja katika ulimwengu wa siri na kuishi kama binadamu wa kawaida anaeonekana na mke wangu na wapenzi wangu na mengine yatajidhihirisha yenyewe. Malengo yangu mengine ya kimaisha ni kumuamsha malaika , kuhusu mengine yote sitaki kuyazungumzia”
“Bosi bado tu hujamkatia tamaa Malaika?”Aliuliza Asmuntis akiwa amekunja sura.
“Ndio! Ni swala ambalo siwezi tu kuliacha. Nimekuja kugndua kupitia Earth Axis ambayo serikali ya Tanzania imeshikiria , kuna tumaini kubwa la kumuamsha malaika na hata kumfahamu mzee. Ndio maana nimekuwa na ukaribu na kitengo cha Malibu”
“Bosi Kama kweli Malaika ataamka , ataweza kukulinda kwa hakika na unaweza kupata majibu ya maswali yako mengi” Aliongea na Hamza alitingisha kichwa.
“Angalau leo mchafu umeongea vizuri. Halafu vipi kuhusu huyu msichana wetu.. nini kimetokea juu ya hii mbinu ya Hundred Shadow?” Asmuntis mara baada ya kusikia kauli ile macho yake yaliwaka.
“Ametumia hundred Shadows?”
“Usiwe na wasiwasi , kaniambia nisikwambie lakini mimi na wewe hatuna haja ya kufichana ndio maana nasema sasa hivi mbele yako. Yule ni kama mdogo wangu wa kike hivyo nataka kumsaidia , hivyo kabla sijachukua hatua nataka kusikia kutoka kwako na mtazamo wako juu ya mbinu hii ya hundred Shadows”.
“Bosi ukweli mimi niliishia kumfundisha tu , lakini kuhusu uwezo aliopata sina uhakika kama unatokana na mbinu yenyewe , ni kama vile ni kitu ambacho amezaliwa nacho”
“Duh! Unataka kumaanisha nini? Mbona hata mimi sijui . Hundred Shadows ni mbinu ya kumuwezesha mtu asionekane katika macho ya kawaida , lakini alichopata kupitia hii mbinu ni spidi kubwa kitu ambacho ni ngumu wewe kumfundisha. Hebu niambie unachojua kuhusu chimbuko la Rhoda kwa ujumla”Aliongea Hamza.
“Wakati nilivyomuokota na kuamua kumlea . hakuwa akikumbuka wala kuelewa chochote zaidi ya jina lake tu. Miaka kadhaa iliopita baada ya kufikia daraja la juu la mafunzo nilimpa ruhusa ya kufuatilia chimbuko lake. Baadae alikuja kujua ufunuo aliopata baada ya kufika levo ya nafsi, ilikuwa ni asili ya ufunuo uliokuwa ukifundishwa katika shule moja iliofahamika kwa jina la Night Shadows. Ajabu ni kwamba watu ambao walikuwa wakivuna nishati kwa ajili ya kugeuka vivuli, kambi yao imeteketezwa yote na mtu ambae alitumia shambulizi la radi na inaonekana katika shambulizi hilo ni Rhoda peke yake alisalimika mpaka mimi kuja kumuokota na kumwasili”
“Unasema wanafunzi wote wa mafunzo ya Black Shadows waliuliwa?”
“Ndio na muuaji alitokea nyakati za usiku wa mvua kubwa kama hivi na hakujulikana ni nani. Mama yake Rhoda pengine alikuwa ni ninja na pengine ni yeye aliemuokoa”
“Lakini bado mpaka sasa nina swali , kwa nilichosikia kutoka kwa Rhoda ana asili ya ki Afrika na Ugiriki , ilikuwaje ukamuokota Japani?”Aliuliza Hamza.
“Hata mimi nilijiuliza hivyo mwanzo! Ila baada ya kufuatilia kwa umakini niliweza kupata habari za biashara ya viungo iliokuwa ikiendelea kutoka bara la Asia na Afrika , wanawake wengi kutoka Afrika walikuwa wakisafirishwa kwenda Asia. Pengine mama yake alikuwa ni moja ya Wa afrika waliongizwa Japani”
Hamza hatimae aliweza kuelewa mbili tatu , ndio maana Rhoda alikuwa akikwepa kuongea kuhusu chimbuko lake.
“Inawezekana , ndio maana wakati unamuokota alikuwa mdogo sana, lakini spidi yake ya kuvuna nishati ni kubwa sana kiasi cha kunishangaza”
“Bosi kuna swala lingine pia sikukuweka wazi, pengine ndio linalochochoa uwezo wake wa kuvuna nishati”
“Swala gani?”
“Rhoda ni Chimera”
“Chimera! Unamaanisha ana wazazi watatu?”Aliuliza Hamza kwa mshangao. Kama mtu mwenye mafunzo ya utabibu alikuwa akijua nini maana ya Chimera au Chimerism , mtoto ambae anakuwa na baba wawili kwa wakati mmoja , ni binadamu adimu sana wa namna hio ambae hutokea baada ya mwanamke akiwa katika siku za hatari kuzalisha mayai mawili kwa wakati mmoja kutoka katika ovari zake na hayo mayai hutungishwa na mbegu za wanaume wawili tofauti na baadae ya hapo mayai hayo huungana na kutengeneza mtoto mmoja na kumfanya mtoto kuwa na vina saba vya wanaume wawili kwa wakati mmoja , ukijumlisha na Mama anakuwa mtoto mwenye wazazi watatu. Mtoto wa aina hio huitwa Chimera.
Kwa lugha nyepesi unaweza kumpima Rhoda vinasaba vya damu kwa kulinganisha na vya Hamza akafanana kwa asilimia kubwa na ukapima damu yake tena kwa kulinganisha na Asmuntis pia ikaonyesha ni baba yake, japo pia inategemea na aina ya kipimo.
“Ninachomaanisha bosi ana chimbuko la watu wa damu ya Aikido , pengine ndio maana spidi yake ya kuvuna nishati ni ya juu sana”Aliongea Asmuntis.
“Inawezekana pia , ukijumlisha na changamoto alizopita , moyo wake umejaa moto , pengine ni wa kisasi ya juu kilichotokea.”Aliongea Hamza.
“Nadhani pia linaweza kutokuwa swala zuri , kuna hisia zinaniambia pengine mtu ambae alihusika na kuimaliza kambi hio , sio mtu wa kawaida kudili nae”
“Haha , mara nyingi ikifikia hatua kama hii , wewe kama mwalimu huna chakufanya zaidi ya kumwelekeza mwanafunzi wako nini chakufanya”
‘Sidhani kama anaweza kupokea maelekezo yangu , mimi namjua vizuri”
“Basi sawa , tutaongelea kuhusu hili vizuri . Vipi kuhusu taarifa juu ya watu tuliowaweka kufuatilia wanajeshi wa kitengo cha Malibu?”Aliuliza Hamza.
“Ni kama ulivyotea bosi , mtu ambae ulimshuku anaonekana kuwa tatizo lakini kuna zaidi ya watu wawili ndani ya Malibu ambao wana matatizo”
“Ni hivyo , basi napaswa kukusikiliza kwa umakini ..”
*****
Katika anga moja , kulikuwa na jengo kubwa lenye bango kubwa la chuma ambalo limebandikwa juu kabisa ya jengo hilo.
Bango hilo la chuma lilionekana kama la pembe sita lenye mchoro wa ishara ya dhoruba.
Sehemu hio ndio yalikuwa makao makuu ya kundi la kimasenari kwa nchi ya Mafuvu maarufu kama Metal Tide. Katika Command Room alionekana jitu kubwa la miraba minne na urefu wa mita mbili akiwa amesimama mbele ya dirisha akiwa amevalia koti.
Ingawa ngozi ya nguo zake ilikuwa imefunika mwili wake vyema , lakini haikutosha kuficha namna misuli ya mwili wake ilivyotuna.
Mtu huyo ndio mwanzilishi wa kundi hilo la kimasenari la Metal Tide. Alikuwa pia ni mtaalamu wa kimapigano ambae alikuwa akikaribia kuingia katika daraja la Ugwiji, Aliitwa Jitu Chuma au Gonzalez.
“Kwahio unasema mwanzo mwisho mtu aliezuia mashambulizi ya kumuua Lucifer ni Black Fog?”Aliuliza mtu huyo kwa sauti ya chini.
Nyuma yake alikuwa amesimama mwanaume na mwanamke. Walikuwa ndio viongozi wakubwa wa kundi hilo , watu ambao Hamza alikutana nao yaani Helena na Gray.
“Ndio, Kapteni. Nadhani sio suala la kawaida kwasababu kwa kile nilichoona Lucifer hakushituka kabisa”
“Halafu pia tumeweza kugundua maninja kutoka Baffodil wameingia mjini . Makisio yetu ni kwamba wapo kwa ajili ya kumpa ulinzi Lucifer”Aliongea Gray.
Gonzalez aligeuka na misuli mingi ilionekana katika uso wake kama vile ni mizizi ya mti uliozeeka.
“Kipindi kile baada ya Lucifer kuondoka , nilijua tu kuna kitu hakipo sawa . Kimsingi baada ya kumuua Mr Black angejitokeza hadharai kupata sifa zake , lakini akaamua kwenda kujificha , ili nichanganya na kuona ni mtu gani ambae ana sifa nyingi namna hii kuamua kwenda kuishi maisha ya kawaida? Lakini naona yote haya ni kwasababu hana nguvu yoyote iliobakia katika mwili wake. Sasa mtu hana nguvu na anajaribu kutaka kushiriki katika Baraza la maksi. Hizi ni dharau na sisi Metal Tides hatuwezi kuchukulia hili kiwepesi .
Nataka kuona nani atasogelea kundi letu baada ya kuwatia uvilema mashetani wote wa Inferno! Natamani kuona namna watu watakavyoniangalia baada ya pambano”
“Hongera sana Master , hatimae ndoto yako ya kubeba cheo cha hadhi ya nyota kumi , inakwenda kutimia”Aliongea Helena na Gray huku wakiwa na msisimko wa hali ya juu sana kwa kiongozi wao.
Muda ule mwanga wa radi ulitokea na kufanya sura ya Gonzalezi iliofunikwa na giza kuonekana , alikuwa katika tabasamu la uovu na halikumlenga mtu mwingine bali Hamza.
******
Saa tatu kamili za asubuhi Hamza na Regina walimaliza kupata kifungua kinywa na kuanza safari ya matembezi kuzunguka jiji hilo la Paris.
Hamza alikuwa mzoefu wa jiji na alikuwa akijua historia ya maeneo mengi , hivyo alikuwa kama tour guide kwa siku hio na uwezo wake wa kuongea kifaransa ulimpa maksi nyingine.
Mara baada ya kufika katika Eiffel Tower , waliweza kuona wapenzi wengi wakipiga picha , hivyo na yeye alitoa simu akitaka kupiga picha na Regina.
“Wife ngoja tuweke kumbukumbu”Aliongea Hamza huku akimshika Regina bega na kuanza kupiga selfie , lakini Regina alionekana hataki.
“Wewe hujui kupiga picha vizuri, unanifanya naonekana mbaya”
“Mke wangu kwa uzuri wako huo , unaogopaje kupiga picha? Vipi kufanananisha na hawa wengine ambao ni wakawaida lakini wanajitahidi kuonekana wazuri?”
Hamza hakujali ubishi wa Regina na alimshika kwa nguvu na kuanza kupiga selfie za kutosha.
Muda huo , mwanaume alievalia katika mavazi ya mtindo wa mpiga picha aliwasogelea , akiwa na tabasamu pana usoni.
“Excuse me, may I bother you two for a few minutes?”Aliongea yule mwanaume kwa lugha ya kingereza , huku akiwaangalia Regina na Hamza.
Comments