Reader Settings

Hamza  alishangaa kidogo baada ya bwana huyo  kuwasogelea.

“Ndio mkuu , kuna tatizo?”Aliuliza.

“Mimi ni mpiga picha  wa jarida  maarufu la mitindo hapa Paris. Jarida letu  linahusisha utoaji wa  ripoti juu ya watu waliopendeza zaidi  kwa wiki ndani ya Paris. Nimeona huyu mwanadada mrembo  mbele ya Eifell tower  na  kudhania  macho yangu yananidanganya kwani ni kama kiumbe kilichoshushwa ghafla , hivyo nauliza kama naweza kuchukua picha zake kadhaa. Msiwe na wasiwasi picha hizi hazitotumika kwa ajili ya matangazo ya kibiashara na pia jina lako litafichwa ili tusivunje faragha yako”

Regina mara baada ya kusikia maelezo hayo alishindwa kujizuia aibu kumshika . Ingawa ameitwa sana mrembo tokea akiwa mdogo  lakini  sio kama kiumbe alieshushwa kutoka  angani tena katika ardhi ya ugenini.

“Ni wapi  picha hizi zitatumika katika jarida lenu?”Aliuliza Hamza

“Ni mbele ya jarida , lakini vilevile katika mitandao yetu ya kijamii  na ofisi za maonyesho”

“Sasa kama mkichukua picha ya mke wangu si itawavutia watu wengi na maana yake mtapata trafiki kubwa , ambayo huleta hela , kuna utofauti gani na kufanya biashara?”Aliuliza Hamza akiwa hajaridhika.

“Sir kwa kusema hivyo hatuwezi kupinga pia . Lakini jarida letu linadili zaidi na wanawake warembo  na hatuwezi kuchukulia  swala hili kwa namna ya kujinufaisha”Aliongea na Hamza aliishia kumwangalia Regina.

“Wife , vipi unataka kupigwa picha na kuonekana kwenye jarida lao?”

Regina alikuwa na aibu sana kupiga picha ndio maana hata mtandaoni hakufahamika sana , sasa inawezekanaje apigwe picha kwa malengo ya fasheni kwa ajili ya kuonekana katika jarida.

Lakini Regina aliona kama angekubali kupigwa picha  katika mazingira kama hayo itakuwa ngumu kusahaulika  na pia ingekuwa nzuri zaidi.

“Sioni shida  kupiga”Aliongea Regina baada ya kusita kidogo na Hamza alitingisha kichwa kukubaliana nae.

“Vipi utampatia mke wangu hela , namaanisha hela za umiliki wa picha yake?”

“Sire , tunachokifanya  ni kama interview ya mtaani , itakuwa ngumu kuweza kulipa  hela kila tunaeomba kumpiga picha. Kama  dada atakataa kupigwa picha  hatuwezi kumlazimisha pia”

“Yaani hamtaki  kunipa hata shilingi , halafu mnataka kumiliki picha ya mke wangu ? Mnaniona mjinga , kwanini niwagawie  mke wangu bila sababu?”

Regina alijikuta akichizishwa na maneno yake na kujiuliza huyu mtu anaongea nini ? Alishindwa kujizuia na kumfinya Hamza  kiunoni.

“Wewe unaongea ujinga gani? Kupiga picha kunafanana vipi na kunigawa?”Aliongea na kumfanya Hamza kucheka.

“Ndio hivyo , sitaki mtu mwingine akuone  kila siku ,  mimi peke yangu ndio mwenye kigezo cha kukuona wewe kila siku”Aliongea.

“Wewe , mbona unakuwa  kama mtoto” Regina hakujua anune au afurahi, lakini moyo wake ulijaa utamu.

Cameraman yule aliishia kutingisha kichwa chake kwa masikitiko  na kisha aliaga na tabasamu baada ya kukataliwa.

“Ipo hivyo , wewe ni wa  kwangu na nitakuwa kichaa kuacha wanaume wengine  waangalie picha yako kila siku”

“Yule ni msanii wa picha tu , kwanini unafikiria mbali. Jitu kubwa lakini  una mawazo ya kitoto”Aliongea Regina akitingisha kichwa kama kujutia kukosa nafasi ya kupigwa picha.

“Nilitaka kupata picha  moja nzuri , angalia ulizopiga zilivyo mbaya”

“Basi kama ni hivyo nitaenda kutafuta  mtaalamu wa hali ya juu wa kupiga picha. Lakini mke wangu picha yako  itawekwa nyumbani tu ili mimi niwe naingalia mwenyewe  vinginevyo nitashikwa na wivu eti” Regina alishindwa kujizuia na kucheka.

“Wewe umekuwa mtoto kweli na vituko vyako.. nishakata tamaa sitaki picha  tena”

“Haha.. mke wangu labda utakuwa hujasikia tu , Mwanaume  siku zote  ni kama mtoto mbele ya mwanamke anaempenda. Mwanaume akiwa hakupendi mbingo zake zitakuwa ni za kibaba baba tu. Hivyo mke wangu nipo hivi kwasababu nakupenda  kutoka uvungu wa moyo wangu”

“Lione, sitaki kukusikia tena . ninunulie basi kitu chochote kitamu cha kula”

“Sawa mke wangu , ngoja nikupeleke ukale kitu utakachopenda”

Hamza alimchukua mrembo wake na kununua vitu  na kisha walienda kupanda kwenye Ferris Wheel. Ijapokuwa  hawakuwa na mengi ya kufanya  pamoja , lakini kuwa  kama hivyo , kama wapenzi wa kawaida  iliwafanya  ukaribu wao kuzidi kuongezeka.

Baada ya kutumia siku nzima kutembea na kucheza kama wapenzi  Hamza alimuaga Regina kwamba siku tatu zitakazofuatia kuna  vitu anaenda kufanya hivyo hatoweza kuwa nae.

Regina hakuhitaji maelezo mengi kujua Hamza anaenda kufanya nini , alikuwa na vitu vingi ambavyo hakuwa akijua kuhusu Hamza hivyo aliishia kumkubalia. Walikubaliana tu  akisharudi huko anakoenda wataanza safari ya kurudi Tanzania.

Hamza upande wake alijua hatokuwa na muda wa kununua  zawadi , hivyo  aliingia mtandaoni na kuchagua vitu vingi  kama zawadi na  kumtumia Mzee Pino kuviandaaa kwa ajili ya Eliza, Yulia na  Dina.

Wanawake hao watatu walikuwa  ni warembo wake , kuhusu  Prisila alimchukulia kama mdogo wake  na  Irene kutokana  na bado kuwa mwanafunzi aliona asimpatie zawadi  maana atamfanya azidi kuchizika.

Muda huo Hamza alishindwa kujizuia  na ghafla tu mawazo  juu ya Yonesi yalimvaa palepale. Kama bado angekuwa na mawasiliano na mrembo huyo angemnunulia pia zawadi.

*****

Ni ndani ya mji mdogo unaofahamika kwa jina la Limours , uliokuwa  kusini Magharibi  mwa jiji la  Paris , uliozungukwa na vilima vidogo vidogo  vyenye  msitu.

Ni sehemu ambayo ilikuwa na utulivu mkubwa na mahali ambapo  ni rahisi  kuficha siri   kwa watu wa ulimwengu wa nje. Hivyo Baraza la maksi lilipangwa kufanyikia katika mji huo.

Eneo la uwanja wa ndani wa mpira wa miguu , ndio mahali ambapo paligeuzwa kuwa Venue  kwa ajili ya Set Conference.

Katika siku hizo , kwa watu wote ambao walifika  nchini Ufaransa kwa ajili ya kushiriki baraza hilo la maksi walikuwa wamejazana katika  mji huo wa Limour , karibia katika kila hoteli na gesti zote.

Kulikuwa na  wanajeshi wengi pamoja na polisi ambao wametumwa na serikali kwa ajili ya kutoa ulinzi ili kuepusha  machafuko.

Hamza  sasa alifika ndani ya mji huo akiwa ametangulizana na  Asmuntis na Black Fog kupitia  gari aina ya Hummer.

Watu wa kawaida walipangiwa  kuishi  katika hoteli  kwa kipindi chote  cha  baraza hilo  lakini ilikuwa tofauti kwa Hamza. Watu wake wasingemruhusu kukaa hotelini  na watu wa kawaida hivyo walikodisha  nyumba nzima kando ya shamba.

Ukweli ni kwamba  Magwiji wakubwa kama wangejitokeza  ama kufahamika mbele ya watu wa kawaida ingeleta  msisimko na aina flani ya ukinzani. Hivyo hoteli haikuwa maeneo sahihi kwao kuishi.

Mara baada ya kufika   katika nyumba iliozungukwa na shamba kubwa la Farasi , ijapokuwa eneo lilikuwa limejitenga lakini lilikuwa limeboreshwa ulinzi wake kwa teknolojia ya hali ya juu  na kulikuwa na vyanzo mbalimbali vya starehe.

Ndani ya uzio wa shamba hilo kulikuwa na magari kadhaa ya kifahari yaliokuwa yameegeshwa. Ikionyesha mtu ambae sio wakawaida alikuwa ametangulia kufika.

“Bosi nasikia sauti ya  kugongelea chuma”Aliongea  Asmuntis  wakati akitoka nje ya gari.

“Hata mimi pia , ngoja tukajionee huyu mhunzi  ni kitu gani anatengeneza tena”Aliongea  Hamza.

Mara baada ya kuzunguka nyuma  ya banda la Farasi , waliweza kuona mwanaume akiwa ndani  akigongelea chuma na nyundo kubwa.

Kipande cha juu cha mwili wa mwanaume huyo kilikuwa cha rangi ya kahawia  na misuli mikubwa iliotuna  iliweza kuonekana. Kila msuli ulionekana kuwa mgumu kama jiwe.

Alikuwa na  nywele fupi zilizojikunja kunja, alikuwa ametoboa masikio na  kuvalia heleni kubwa za dhahabu.

Dang , Dong , Clang!

Sauti hio ya kugongelea chuma , ilikuwa ni kama inatoka kwa mpangilio maalumu wa kutengeneza mziki.

Mara baada ya kumuona mwanaume huyo wa mita moja na  nukta tisa , midomo ya Hamza na Asmuntis  ilicheza kwa kuonyesha tabasamu.

“Uncle Azzle , kwanini kufika tu unaanza kugongelea chuma?”Aliongea Black Fog

Mwanaume huyo wa rangi ya zambarau alikuwa  ni Azzle mkuu wa  kundi la Kimasenari   la Barhams, Maarufu kama Ares  of Arabian Peninsula.

Azzle  mara baada ya kugeuka na kumuona Hamza , haraka sana aliweka  kile chuma   kwenye dimbwi la  maji.

Siziiiii! Mvuke wa maji ulipanda ukipoza chuma kile  na palepale aliweka nyundo yake chini na kisha  alishuka chini na goti moja huku akiweka mkono kifuani.

“My Prince!”

Alimsalimia Hamza kwa mbali na kisha akasimama na kumwangalia  Asmuntis kwa macho makali.

“Wewe Mtu mchafu kwanini umechelewa kumleta bosi  hapa?”

“Kwahio kama nimechelewa inakuhusu nini? Bosi  alipaswa kuwa na shemeji yetu kwanza”Aliongea Asmuntis.

“Oh Tena nimekumbuka , bosi  mbona simuoni  shemeji?”Aliuliza Azzle.

“Wewe mzee wa Stroke , unavyoongea tu  ni kama  mzimu uliofufuka , halafu unataka nije na mke wangu, Unataka  umtishe? Ni muda mrefu tokea  tuonane mara ya mwisho   nipokee hata kwa kicheko basi”Aliongea na kumfanya Azzle kutabasamu.

“Bosi nilijizuia tu , ila jana nilitaka kuja Paris kukutafuta , lakini baada ya kufikiria nikaona nije hapa mapema kuona maandalizi yakoje. Ni Berrly alieagiza  hii sehemu iwe wazi  kwa ajili  yako , si unajua alivyo  mvivu  ndio maana nikaona nijihakikishie.  Unapenda kuendesha  Farasi ndio maana na kutengenezea viatu hapa”Aliongea.

“Ni lini nilikuambia napenda kuendesha farasi. Nakumbuka  ilikuwa ni miaka sita iliopita tukiwa Argentina Pampas Height, kipindi kile niliendesha farasi sio kwasababu napaenda bali ni kwasababu nilikuwa nikifukuzia mtu nilietaka kumuua”

“Ni kwasababu bosi  wewer ni tajiri tayari  hivyo sijui ni kipi naweza kukupatia kama zawadi , nimeona kutengeneza horseshoes itakuwa na maana zaidi” Hamza mara baada ya kuona jitu siriasi namna hio linataka kumfurahisha aliguswa.

Washikaji zake ambao  alikuwa nao kwa muda mrefu , wengi wao  wanaishi kwa kuamini  wana deni kubwa  kwake  na kila siku wanajribu kutafuta namna ya kumlipa.Lakini ukweli ni kwamba kuweza kuishi katika ulimwengu wa giza  na kufanikiwa  ni swala la kutegemeana.

Hivyo Hamza hakuwahi kuwaza mafanikio yake yametokana na uwezo wake pekee  bali ni kwasababu ya kuwa na marafiki wengi. Hivyo hata baada ya kustaafu na kuachia maeneo aliokuwa akiongoza wayasimamie wao hakujutia wala kujisikia vibaya.

“Wewe Mhunzi  nashukuru sana  unaonekana kunijali  lakini  haijalishi kama napenda kuendesha farasi au lah . Ila kwasasa nataka tukae chini na tupate  kinywaji pamoja  na kupiga stori . Naamini umekuja na mvinyo mzuri , maana mpaka kuwa Mshauri mkuu wa mfalme  naamini wanatumia hela zao za mafuta kukulipa vizuri”

“Bosi niseme tu ukweli sijaja na mvinyo wowote , Berly  pia  ni mbahiri mno sijaona  mvinyo wowote hapa , ngoja nimpigie  mtu simu atuletee..”Mara baada ya kuongea , sauti nyingine ilisikika kutoka chini.

“Pumbavu zako Azzle , ushaanza kunisnitch tayari kwa bosi.Mimi Berly  naweza nisikupe wewe wine  lakini mimi ni mtiifu kwa bosi wangu na nimemuandalia  kitu roho inapenda. Huko ardhini nina chumba kizima cha  mapipa ya wine kama haya, sikutaka kukuonyesha mlevi kama wewe”Aliongea  huku akiwa ana kohoa  mfululizo , akiwa anatoka  ndani ya eneo  la chini kama shimo, ilionekana eneo hilo lilikuwa na vumbi mpaka kumfanya kukohoa.

Berly alikuwa ndio  mwanaume mtanashati  kuliko  wenzake wote , alikuwa amevalia shati  la maua maua na cheni  shingoni , huku nywele zake akiwa amezisuka. Muda huo alikuwa amebeba pipa la kuozeshea mvinyo na haraka sana alilitua chini na kumsogelea Hamza na kumkumbatia.

“Bosi , hatimae umefika. Nilikumisi sana. Katika miaka mitatu yote nilikuwa nikikuota wewe tu . Hatimae nimekuona tena”Aliongea huku akiwa amemkumbatia lakini Hamza aliimshia kumsukuma

“Hebu acha kuniganda kama mwanamke”Aliongea Hamza.

Berly alikuwa tofauti  sana , ilikuwa ngumu kuamini alikuwa akijihusisha na ulimwengu wa giza, katika ulimwengu  wa nje alikuwa ni msanii , DJ  na Playboy ambae  maisha bila kuzungukwa na wanawake hayaendi. Alijua sana kuhonga na kila  jiji alilopita aliacha alama.

Kubwa zaidi ni kwamba alikuwa na ushawishi mkubwa sana katika  tasnia ya mziki , watu wengi  alikuwa akifahamiana nao  na  alikuwa  hata na ushaiwshi wa nani apewe tuzo na nani asipewe na hio ilimfanya kuwa maarufu sana.

Ukiachana na kuimba hakuwa na kazi maalumu , alichofanya siku  nzima  ni kula bata kwenye mayatcht ya kifahari  na kupiga milegezo. Hakujali kabisa swala la mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi  na ilikuwa ngumu kuamini mtu kama huyo alikuwa na ukaribu na Hamza.

Lakini alikuwa mtu muhimu sana kwa Hamza , anaweza asiwe na  nguvu ama na uwezo kama Asmuntis , lakini kipindi  alipokuwa na Hamza alikuwa ndio mtu pekee aliekuwa akiongoza kwenye  vita ya maneno , alikuwa  na kipaji cha kuongea na mtu yoyote na  akakubali kile anachomwambia , hivyo alifanikisha mambo mengi kwa ajili ya Hamza.Lakini mbaya zaidi aliatumia  uwezo wake wa ushawishi kuwakopa wenzake.Alikuwa anakula bata kwa kukopa marafiki zake.

“Bosi usinilaumu  wakati wewe ndio uliniacha mwenyewe , nina picha yako nyumbani na muda wote naingalia kila nikikukumbuka . Kuna muda mwingine hadi nalia’

“Tangu lini ukawa  na nyumba ya  kuamkia kila siku wewe, Si unaamkia mahotelini na kwenye maboti  wewe. Imepita miaka  mingi lakini tabia yako ya  kudanganya hujaacha tu”Aliongea Hamza huku  asijue acheke ama alie.

“Bosi nilipomuambia atukodishe hili shamba , aliniambia tumlipe  Euro milioni mbili. Jamaa ni mbahiri sana   kwa sisi washikaji zake ila mbele ya mbususu  anakuwa kama chizi kwa kuhonga tena kwa hela zetu”

“Azzle acha kunisnitch , ndio maana muda wote unanuka mafuta ya taa  na petroli. Niliemkodisha shamba  kaniuzia na mvinyo , kuomba Euro milioni  mbili unaona  nyingi sana?”

“Nakudai Dollar milioni mia moja zangu , ulizonunulia private Jet. Nakupa mwaka mmoja , usiponilipa nitayafanya maisha yako kuwa magumu”Aliongea Azzle.

“Wewe Mhunzi , kwanini unashindwa kujali ushikaji  wetu. Bosi ashawahi kusema upendo na haki ni zaidi ya thamani ya dhahabu.  Hela kidogo hio ila makelele meengi”Aliongea Berly kwa sauti

“Berly hata mimi nimekumbuka nakudai dolla milioni moja na hamsini, mimi nirudishie  tu  milioni mia , zinazobaki nimekupunguzia”Aliongea Hamza.

“Bosi mimi ni shabiki wako namba moja , kwanini  unanikandia? Nyie wote naona  hamtaki niwe na amani . Yaani nimewatafutia eneo zuri kama  hili kwa ajili ya kukutania baada ya kunipa shukrani mnaanza kunidai madeni. Hela zote hizo  natoa wapi , sijui kupigana , sijui kuuza siraha , sijui  kuua watu , ninachojua ni kuwakopa tu bila kujua namna ya kulipa”Aliongea huku akijitilisha huruma na kuigiza alikuwa  akilia huku amekaa chini kama mtoto.

Baada ya  kuona anachokifanya  Berly  iliwaacha midomo wazi na walishindwa kujizuia na kucheka.

“Mnanifanya hata binamu yangu Roda ananidharau . Kuna haja gani ya mimi kuendelea kuishi , sina thamani kabisa hata ya kuwa mbele yenu na bosi ..”Aliongea kama mkiwa.

“Bosi  mbona kuna makelele mengi huko ndani , mnamfanya nini huyo mwehu. Hebu tokeni kwanza huko ndani mje tucheze raundi boja la sivyo Leviathani ataniua kwa kipigo”

Mara baada ya kusikia sauti hio , kila mmoja alijua ni nani  na palepale waligeuka na ndio muda walioweza kumuona mwanaume bonge kama Rickross akiingia

Boss!

Mwanaume huyo mwenye mwili mweusi alitembea  huku akitawanya upepo na kwenda kumkumbatia Hamza.

Kama Hamza asingekuwa na nguvu angedondoka nae chini  maana sio kwa uzito huo.

“Mameni  kila ulipo unawaza kucheza kamari tu , utaacha lini?”Aliongea Hamza huku akicheka.

Mameni ukiachana na kuwa Taikuni wa kuuza siraha , lakini vilevile alikuwa  ni mlevi mkubwa wa michezo ya kamari na kubeti.

“Ndio kitu kinachonipa furaha, hili eneo lilivyokauka kamari ndio starehe pekee iliobaki”aliongea huku akicheka

“Twendeni zetu tukacheze , Azzle huna haja ya kuendelea kutengeneza hicho chuma”Aliongea Hamza na Azzle alikubali.

Mara baada ya kuona kila mtu anaondoka bila kujali huzuni yake , Berly aliekaa  chini  alianza kulia tena.

“Bosi vipi kuhusu mimi! Unanitelekeza masikini kama mimi”

“Njoo na hio pombe”Aliongea Hamza  na kumfanya Berlly furaha kumvaa na haraka haraka aliinuka na kubeba  pipa lile.

Wote walitembea na kwenda kuingia katika nyumba  iliokuwa katikati ya shamba hilo ,  kwa nje haikuwa nzuri sana , ila ndani ilikuwa imepambwa vizuri tu na kupendeza.

Katika eneo la Dining kwenye meza ndefu alionekana Leviathani akiwa amekodolea macho kararata.

Mara baada ya kumuona Hamza akiingia Leviathani haraka haraka alisimama na kumpa Hamza heshima yake.

“Wewe ngiri kwanini  unang’ang’ania kucheza  na Mameni! Unaishi baharini  halafu unataka kumfunga?”

“Sikutaka kukubali ndio maana nikampiga, kwanini kila saa yeye ndio anashinda tu” Hamza muda ule aliweza kuona Leviathani alikuwa amenyoa kipara na alishangaa.

“Wewe Ngiri hicho kipara umekitoa wapi kwanza?”

“Haha.. binti yangu anasema rasta zangu zinamuumiza  kila ninapomkumbatia ndio maana nikaamua kunyoa kipara”

“Kumbe hata shetani mkubwa wa baharini ana upande mwingine  mlaini ,  Ajabu iliooje hii”Aliongea Berry  na kauli y ake  ile ilimfanya Leviathani haraka haraka amsogelee  na kumkwida tai.

“Wewe takataka ni lini utanilipa milioni zangu therathini  ninazokudai na dhahabu ulizochukua?”Aliongea akiwa siriasi.

“Ngisi hebu acha kuwa hivi  basi , ijapokuwa tunalingana umri lakini  nimekuzidi mwezi mmoja , hivyo mimi ni kaka yako  na uache kuniabisha, kama ni hela nitalipa tu  nikipata..”

Mara baada ya kusikia hivyo  watu wote walijikua wakianza kucheka , huku Leviatahni akishangaa , maana hakujua ni kipi kimewafanya kucheka.

Mara baada ya kuongea kidogo , kila mmoja alikaa kwenye nafasi yake . Hamza alikaa katika kiti cha heshima  na kumfanya awe anawaangalia kupitia pande zote mbili. Ndani hapo  karibia marafiki zake wakubwa wote walikuwepo , akiwemo Azzle , Asmuntis , Mammeni, Livotani , Berly na wengine. Black Fog hakuthubutu kukaa , aliishia kuwamiminia  mvinyo huku akiwa amesimama nyuma ya Asmuntis.

Muda huo  wote walitulia na Hamza hakuongea neno wala Berly  muongeaji sana hakuongea neno . Kila mmoja alikuwa na mwonekano  mzito ,  wakiwa katika  takafakari ya kukumbukia mambo yote  yaliopita.

Mpaka dakika kumi kupita hatimae Hamza aliwaangalia mmoja baada ya mwingine na kisha akaongea.

Kunani huko kwenye Baraza la maksi?

Previoua Next