Jitu la Chuma.
The long Table au Meza ndefu ndio kikao cha daraja la juu katika jamii ya siri ya Inferno tokea kuanzishwa kwake. Inferno ilitokea katika Clubs mbalimbali za kishetani ambazo zilianzishwa hapo mwanzo katika miaka ya 70, club hizi zilipewa jina la Hellfire Clubs. Watu wa Hellfire club walijaribu kuvumisha jamii yao hii kwa kuingiza katika filamu kubwa za kimataifa kama Marvel Comics , Stranger Thing na baadhi ya nyingine nyingi wakijaribu kuonyesha ushawishi wao katika kila sekta ndani ya dunia hii kwanzia katika maswala ya uchumi , jamii na hata tamaduni.
Hellfire Club walifahamika kama watu wanaomzihaki Mungu nchini Ireland katika miaka hio. Hii jamii ilikuwa ikifanana sana na Freemason au Iluminat na iliongozwa na Black Emperor au Mr Black.
Baada ya kufa kwa jamii hii kupitia vita takatifu ndio ikaibuka jamii nyingine ambayo ndio hii ya Inferno.
Waasisi wakuu walikuwa ni watu kumi na mbili ambao walitengeneza kikao cha hadhi ya Meza Ndefu ya siti kumi na mbili.
Maana yake ni kwamba vikao vya juu havikuzidi watu hao kumi na mbili tokea kuanzishwa kwake.
Iliwachukuwa miaka miwili tu kuingia katika daraja S katika ulimwengu wa giza ambapo ndio kipindi chote cha Vita takatifu , vita ambayo sio tu kumpa Hamza umaarufu lakini ilimpa ushawishi mkubwa.
“Mephistopheles hajafanikiwa kufika”Aliongea Azzle
“Sallisbury hajasafiri kwa ajili ya kulinda kisiwa cha Toharani”Aliongea Asmuntis na Hamza palepale aliinua juu kikombe cha mvinyo.
“Kikombe cha kwanza cha mvinyo huu ni kwa ajili ya kuwaenzi wale waliotuacha , Belzebuli , Abtoni , Samuel na Roffe , Jamaa zetu hawa wa nne licha ya kutokuwepo na sisi leo hii lakini nafasi zao zitaendelea kuwa wazi katika vikao vyote vya Long Table milele”Aliongea Hamza.
Katika meza hio kila mmoja aliinua glasi ya mvinyo wake na kisha alikunywa yote kwa ajii ya kuwaenzi washikaji zao wengine.
Hali ile ya huzuni na kutafakari ilipita baada ya awamu hio ya kwanza ya mvinyo. Hamza alitaka kunywa na washikaji zake mpaka kesho , kunywa kujigalagaza kabla ya kwenda kushiriki katika baraza la maksi. Lakini muda ule simu ya Azzle ilianza kuita.
“Kuna nini na naongea na nani?” Aliuliza Azzle huku akiwa amekunja sura.
“Kapteni! Sitaki kuwasumbua katika kikao chenu na Mkuu wetu , lakini kuna kitu kimetokea hapa , watu wetu wanashambuliwa na watu wa Wimbi la chuma”
“Metal tide!” Azzle alijikuta akishangazwa na habari ile huku akiinua macho yake na kumwangalia Asmuntis
Asmuntis hata yeye uso wake ulibadilika mara moja baada ya kusikia mwenzake anataja Metal tide na aliishia kumwangalia Hamza kwa wasiwasi.
“Nimesikia vibaya?”Aliongea Mameni kwa sauti kubwa.
“Metal tide wanathubutu vipi kushambulia watu wetu , hawajui mtu ambae yupo nyuma ya Barhamu ni bosi “Aliendelea kuongea Mameni.
“Mhh! Bosi inaonekana kutoonekana kwako kwa miaka mingi , hawa watu washaanza kujihisi wapo juu. Kwanini tusiwaonyeshe kile wanachohitaji”Aliongea Leviathani na kisha akaendelea “Sasa hivi tumezidi kuwa na nguvu , tukiungana mimi , Mhunzi hapo na Mchafu na watu wake ni swala la kufumba na kufumbua tushalizima kundi lote la watu wa Wimbi La Chuma”Aliendelea kuongea Leviathani akiwa katika hamasa kubwa sana.
Hamza alijikuta akiishiwa na usemi , aliishia kunyoosha mkono wake kwa ishara ya kuzuia pendekezo la Leviathani.
“Msiniingize mimi huko tena , nilishawaondolea wasumbufu wote lakini bado tu mnataka kunichosha?”Aliongea Hamza.
Upande wa Azzle na Asmuntis walikuwa na hali zisizoelezeka katika nyuso zao , walifikiria kuona Leviathani na wenzake hawakuwa na taarifa ya Hamza kupoteza uwezo wake wa nishati za mbingu na ardhi.
Ukweli ilikuwa tofauti kwa wenzao , walikuwa wakifahamu Hamza hakuwa na tatizo lolote kuhusu uwezo wake maana alishawasiliana nao na hata kukutana nao siku kadhaa zilizopita.
“Bosi timu yetu ya Barham inaonekana kupambana na watu wa Wimbi la Chuma hapa Limour . Mimi nitaelekea huko nikadili na hili suala,sitoungana na nyie kuendelea kunywa”Aliongea Azzle na kusimama.
“Hey! Mhunzi , hili swala limeamsha shauku yangu. Kwanini tusiende wote kuangalia. Nataka kumuona Jitu Chuma uwezo wake ni mkubwa kiasi gani”Aliongea Mameni huku na yeye akisimama.
“Ndio bosi , hujaonekana kwa muda mrefu na hawajakukaribisha kwenye kikao cha kilele cha Magwiji . Ukijionyesha sasa hivi asilimia kubwa ya watu watakuwa mashabiki zako”Aliongea Berlly.
“Mashabiki wa nini? Unadhani nimekuwa msanii?”Aliongea Hamza.
“Kwa mtazamo wangu haina haja. Bosi huna haja ya kwenda ,kama bosi akienda si kama tunawaheshimu sana ? Mimi na Mhunzi peke yetu tunatosha kudili na hii hali”Aliongea Asmuntis.
Hamza aliishia kusinyaza macho baada ya kuona Azzle na Mchafu wanamtetea asiende kwasababu wanadhani hana uwezo wowote. Hamza alifikiria kidogo na palepale aliona haina haja ya kuwaambia ukweli kwanza, kwasababu alijua anachofanya Gonzalez ni kutaka kumtega yeye. Gonzalez alikuwa akitafuta tu ugomvi , lakini ukweli ni kwamba makundi yote mawili yaani Barham na Wimbi la Chuma walikuwa ni daraja A hivyo wasingeenda mbali.
Alipanga pale ambapo Gonzalez atakuja moja kwa moja kwake ndio atadili nae na atatumia nafasi hio kumkamata na kumshikisha adabu.
“Tutaenda wote , ila sitojitokeza. Ijapokuwa Barham kwasasa ipo chini yako lakini bado nina hisia na jina lake , nisipoonekana itawavunja moyo vijana wetu”Aliongea Hamza.
“Bosi kwasababu umeongea hivyo , basi twendeni pamoja”Aliongea Azzle
Asmuntis alishindwa kufanya lolote mpaka hapo lakini maneno ya Hamza yalikuwa na mantiki. Kama kila mtu yupo ndani ya Limuour na kitu kibaya kikatokea vijana wao na Hamza hajajitokeza itawafanya kuvunjika moyo na pia ingeibua minong’ono.
“Twendeni , sitaki kuchelewa tena , ni bora Gonzalez akajitokeza mwenyewe nimpasue kichwa chake”Aliongea Leviathani huku akisimama.
“Haha.. Ngisi huna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya hilo , tupo nchi kavu na huwezi tumia matamvua yako kirahisi. Ni kheri ukawaacha Mchafu na Mhunzi kudili na hili swala”Aliongea Mameni.
Wakati wakiwa wanaongea walitoka ma kwenda moja kwa moja mjini Limour kupitia magari yao ya kifahari.
Nje ya Bar moja mjini Limour, kulikuwa kumejazana watu. Walikuwa ni wanaume na wanawake , wazee na vijana na karibia kila mmoja amevaa staili yake. Ndani ya eneo hilo kulikuwa na taasisi mbalimbali kutoka pande karibia zote za ulimwengu ambazo zimetuma wawakilishi kwa ajili ya kushiriki katika baraza la Maksi.
Sasa ndani ya hii Bar, ndio vurugu ilipokuwa imetokea baina ya watu wa Wimbi la Chumba na masenari wa kundi la Barham. Ilikuwa ni pata shika.
Kitendo cha kufanya watu wengi kusimama nje kuangalia mapigano hayo, ilifanya watu wengi kusogelea eneo hilo.Licha ya kwamba vita ilikaribia kuisha lakini hali ya Bar hio haikuwa ikitamanika tena , kwani meza na viti vilikuwa vimeharibika na kusambaa kila sehemu huku chupa nyingi zikiwa zimepasuka chini.
Upande mmoja katika Bar hio lilionekana kundi ambalo lilikuwa limevalia mavazi ya kijeshi ya rangi ya kijivu na isignia za mchoro wa mawimbi kwenye vifua vyao na mabegani.
Upande mwingine lilikuwa ni kundi lililovaa mavazi ya kijeshi rangi ya jangwa wakiwa na isignia za nembo ya nyota kifuani na mabegani.
Masenari hao wote walikuwa katika mavazi yao ambayo yalikuwa yamechafuka kwa damu. Na walikuwa wamesimama pande zote mbili wakiangaliana huku wakihema kwa nguvu.
“Nini kinaendelea hapa?”
Muda huo mwanaume na mwanamke alieongozana na kundi la wanajeshi wa kimasenari walijipenyeza katika kundi la watu waliosimama nje ya bar na kuingia ndani.
Baada ya kusikia sauti hio watu wa upande wa kundi la Wimbi la chuma walikakamaa miili yao.
“Ripoti kwa Afande Gray. Ni hili kundi la Barham limejaribu kutuletea vurugu. Kwa ajili ya kulinda hadhi ya kundi letu tukaamua kupigana nao”Aliongea.
Mwanaume na mwanamke alieingia hapo alikuwa ni Gray na Helena. Baada ya ripoti hio Gray aliwaangalia Masenari saba wa kundi la pili na kisha akatabasamu.
“Marafiki , Mnaweza kuwa watawala katika peninsula ya Uarabuni , lakini hapa ni Ufaransa”
“Mh ! Kama sio watu wako kutuchokoza tusingekuwa na muda na nyie”Aliongea mwanajeshi wa Kimasenari wa kundi la Barham huku akitema mate chini.
“Oh! Walimuongelea vibaya Lucifer nini?”Aliongea Gray huku akiwaangalai watu wa kundi lake.
“Sir tulikuwa tukiongelea kuhusu Lucifer kupotea baada ya kupigana na Black Emperor . Je tumekosea wapi?”
“Mshenzi! Mlikuwa mkimuongelea vibaya bosi wetu na kusema baada ya vita alipotea baada ya kupoteza uwezo wake ndio maana mpaka leo anaoagopa kujitokeza. Dunia nzima inajua ni Prince aliemuua Black Empor kwa ajili ya amani ya dunia. Kwa ajili ya kuifungua katika minyororo ya giza aliamua kupigana vita takatifu na kuwaachia huru waliofungwa gizani na Mahakama takatifu. Master ni mtu wa haki ndio maana hata baada ya kushinda aliamua kutawanyisha watu wa Inferno ili wasijikusanyie umaarufu na ushawishi kuingilia mambo ya ulimwengu wa kawaida. Hata viongozi wetu wa Barham ni watu wa haki. Unatoa wapi ujasiri wa kumuongelea Master vibaya?”Aliongea Mwarabu huyo na kumfanya Helena kucheka.
“Nyie watu wa Barhams, siku hizi mpo sensitive sana. Tunajua mnamwabudu bosi wenu lakini kuna haja ya kupaniki baada ya kusemwa kidogo tu?”Aliongea Helena.
Kati ya Masenari hao , kuna mmoja ambae alikuwa amekaa , mwanajeshi aliekuwa na nyota kwenye bega lake. Alikuwa ndio kiongozi wa kundi hilo la Barham. Mara baada ya kuona Helena anacheka kwa dharau alisimama na kusogea mbele.
“Wewe Gray na Helena watu wa kundi la Wimbi la Chuma nimeyasikia sana majina yenu lakini sijawahi kudhania watu wa sifa zenu mtakuwa kichefuchefu namna hii. Ijapokuwa mimi Kent ni Kiongozi wa kikosi tu najua heshima za msingi zidi ya watalaamu wa daraja la Ugwiji , nje na ndani ya kundi letu. Bosi wetu sio mtu wa kuongelewa na mtu mwenye mdomo mchafu kama wewe. Hata kama alituacha kwa muda mfupi , yeye ndio kiongozi wetu , mtu wa imani pekee tuliekuwa nae . Kama ujasiri unao , tangaza vita na kundi letu hapa hapa. Nyie kumi na mbili mtashambuliana na sisi saba na hamtoweza kutushinda. Kwa uwezo wenu mdogo hata mwanajeshi wetu wa daraja la chini hamuwezi kumshinda”
“Haha.. Majigambo meengi. Kama tusingewaonea huruma mnadhani mngeendelea kusimama?”Aliongea mwanaume wa upande wa Metal Tide.
“Eti mmetuonea huruma. Kama mmetuonea huruma mngekuwa na nundu usoni?”Aliongea Kent.
“Nyie , mmeshinda si kwasababu mlitutega , mlikuwa na siraha na sisi hatukuwa nazo’
“Kuna chupa kibao haba ambazo mngeweza kutumia kama siraha lakini mkashindwa , msilaumu kwa uzembe wenu. Haishangazi ndio maana kwa miaka mingi mmebakia kuwa kundi la daraja A. Moja ya mafunzo ya mkuu wetu anatusisitizia; kufanikiwa zaidi ni kukubali kushindwa na kuyatambua mapufungu yako”Aliongea Kent.
“Damn it! Sir Gray wanaendelea kutudhalilisha tu”
“Jina lako ni Kent sio? Maneno yako uliongea yametukosea sana. Piga magoti chini na uombe msamaha , la sivyo usije kutulaumu kumdhalilisha Master wako Azzle”Aliongea Gray.
“Nipige magoti!?” Kundi lote la Barham walitunisha vifua huku wakikamamaa miili kwa kujiamini, “Hata mkuu wetu Azzle hawezi kutuambia tupige magoti. Sisi Barham ni watiifu kwa Mfalme wa kuzimu pekee” Mara baada ya kuongea hivyo aliwapa ishara vijana wake na kuanza kupiga hatua kutoka katika Bar hio lakini Gray alisogea na kusimama mbele ya Kent.
“Usipopiga magoti na kuomba msamaha , usifikirie kabisa kuondoka hapa kirahisi”
“Pisha njia” Kent alikuwa na hasira mno. Palepale alikusanya nishati ya mbingu na ardhi na kumsukuma Gray.
Ingawa hakukuwa na mabadiliko sana , lakini katika vita halisi , tena vita mchanganyiko kama hivyo utofauti wa nishati ya mbingu na ardhi ulikuwa na faida kubwa. Ilikuwa ni vita ya kifo , unapigana ukiwa na nafasi ya kushinda na kama hakuna njia rahisi ni kuondoka ndio maana Kent aliongoza watu wa kundi lake kuondoka.
Gray mara baada ya kuona Kent anajitutumua haraka sana alikunja ngumi yake na kumrushia Kent.
“Bang!
Gray alikuwa ni mpiganaji ambae pia alifikia katika daraja la Ukaidi wa asili na mwanzo wa ufunuo wa mwili mpya , hivyo kwa namna flani alichukuliwa kama mbobezi.
Ngumi yake ambayo ilikuwa imeambatana na nishati ya mbingu na ardhi ilikuwa nzito kiasi kwamba ilimfanya Kent kutetemeka mwili.
Arghhhh!
Mfupa katika mkono wake ulipinda mara baada ya kujaribu kupangua ngumi ya Gray, uliumia na kumfanya ashindwe hata kukunja ngumi tena.
Kundi la nje ambalo walikuwa wakiangalia waliona Kent alikuwa akijikadiria kwa viwango vya juu kutaka kupigana na mtu kama Gray ambae hakuwa katika daraja sawa la uwezo.
“Unadhani sisi watu wa kundi la Metal Tide hatuna uwezo? Piga magoti na omba msamaha kabla ya kufikiria kuondoka”
Kent aliishia kusaidiwa na wenzake wawili kusimama juu na hakuonekana kukubali kushindwa kirahisi.
“Mwanajeshi wa daraja la ukaidi wa asili , kushambulia mtu kama mimi ambae ni kiongozi wa kikosi ni sawa na kujidhalilisha. Lakini hata kama tutakufa hapa hapa sisi Barham hatuwezi kupiga goti na kuomba msamaha kwa watu washenzi kama nyie”
“Umeongea vyema!”Sauti ilisikika kutoka nje ikiambatana na makofi.
Muda huo kundi lilitawanyika baada ya wanajeshi waliojazia miili wa Barhampton Empire kutengeneza njia kwa ajili ya Azzle alievalia kombati za kijeshi na Asmuntis alievalia jacketi la kijani kibichi kupita.
Watu baada ya kuona wanajeshi hao wawili , walijihisi ni kama miili yao imetawaliwa na presha kubwa na kufanya wahisi woga.
“Oneni sana , yule ndio Bwana wa Vita. Marshall wa kundi la Barham, Kapteni Azzle mwenyewe”
“Msisimko anao toa ni wa ajabu mno. Inafanya watu kuwa na wasiwasi kwa kuangaliana nae usoni tu. Kama ilivyokuwa inasemekana moja kati ya mashetani kumi na mbili wa Inferno waliosalimika katika vita takatifu hawa ni moja wapo”
“Hey! Achana na Azzle , angalia alieambatana nae , yule ndio Asmuntis mwenyewe, Assassin namba moja duniani! Bosi na mmiliki wa kundi la wauaji la Baffodil DayDreamers! Ni adimu sana kujianika hadharani”
“Mungu wangu! Inamaana umoja wa Inferno unajikusanya upya, wanapanga kushiriki katika Baraza la Maksi au?”
“Inawezekana , Lucifer hajulikani alipo , hivyo ni kawaida kwa Baffodil na Barhampton kuja kushiriki”
Kundi lote la washiriki wa Baraza la maksi waliokuwa katika eneo hilo walikuwa wakiongea wao kwa wao kwa kile walichokuwa wakifahamu , lakini Azzle na Asmuntis wala hawakujali kabisa
Azzle aliwapita Gray na Helena na kwenda kusimama mbele ya Kent akimwangalia.
“Vipi umeumia?”
Kent na wenzake mara baada ya kuona kiongozi wao amefika , walijikuta wakipatwa na ahueni na kufarijika kwa wakati mmoja.
“Report kwa Kapteni! Ni majeraha madogo tu”Aliongea akijikakamua na Azzle alitingisha kichwa na kisha aliwageukia Gray na Helena.
“Umemuumiza mtu wangu. Ni mkono upi ulioutumia , uvunje mwenyewe kabla sijachukua hatua”
Kauli hio ni kama vile Gray alikuwa amekuhukumiwa kifo , hakuweza kuleta ukinzani tena.
“Kiongozi Azzle nakuheshimu sana. Wewe ni mwanajeshi mwenye nguvu na hadhi kubwa , lakini huna mamlaka ya kuniamrisha kufanya chochote. Kundi letu ni la daraja sawa na la kwako. Kwanini usianze kwanza kujua nini kimesababisha haya yote?”
“Haina haja kwani vijana wangu hawawezi kufanya kosa kwasababu wanajua matokeo yake ni nini ikiwa wamekosea”
“Hapa sio Uarabuni. Wewe ni maarufu tu kama Ares wa Peninsula ya Uarabuni , lakini huwezi kuziba anga lote na mkono. Gray tuondoke , Kapteni anatusubiria”Aliongea Helena na Gray alitingisha kichwa kukubali
“Tuondokeni”Aliongea Gray akiwapa ishara vijana wake.
Mara baada ya agizo hilo , wanajeshi wa kundi la Metal Tide walianza kutembea kutaka kutoka , lakini Azzle na mwili wake kama wa tembo alienda kusimama mbele ya Gray na Helena kuwazuia.
“Kubali kupoteza mkono au ufie hapa hapa . chagua moja”Aliongea Azzle akiwa siriasi kiasi kwamba macho yake ni kama yamejaa moto wa kuzimu, kusudio lake la kuua lilikuwa limetawala Bar nzima.
Gray na Helena waliishia kuangaliana na bila kupenda walijikuta wakipiga hatua mbili kurudi nyuma. Na muda ule ghafla tu walisogea kwa spidi katika pande mbili tofauti na kuanza kumshambulia Azzle kushoto na kulia.
Ukweli ni kwamba walikuwa wakijua ni ndoto ya mchana kuweza kumshinda mtu wa daraja la Azzle kwa kupambana mmoja mmoja , hivyo waliona angalau wakishambulia kwa wakati mmoja wanaweza kufanikisha.
Hawakutaka kukimbia pia kwani ingewafanya watu kuwadharau. Lakini bado mtu wanaepambana nae alikuwa ni hatari mno , mtu kuwa moja ya sehemu ya watu wa karibu wa Hamza halikuwa swala rahisi hata kidogo.
Azzle hakuonyesha mabadiliko kabisa , mara baada ya kuona shambulizi la Helena na Gray limekaribia shingo yake , palepale alifyatua mikono yake yote miwili kwa wakati mmoja na kupangua mashambulizi yale.
Bang Bang!
Kwa wepesi kabisa aliweza kuyapangua na kwa wakati mmoja alinyoosha mikono yake akijaribu kuwakamata wote wawili . Lakini Gray na Helena haraka sana walifyatuka wakimkwepa baada ya kuona mashambulizi yao hayakuzaa matunda.
Baada ya hapo wote wawili walikuwa wakishambulia kitahadhari wakimkwepa Azzle asiwakamate.
Azzle alikuwa amesimama katika eneo moja , hakuwa amesogea hata kidogo na ni mikono yake tu ndio iliokuwa ikicheza , alikuwa na nguvu za mikono kiasi kwamba alionekana kama sio binadamuwa kawaida. Licha ya kushambuliwa, Gray na Helena ni kama walikuwa wakigusana na chuma kwani hawakumwathiri hata kidogo.
Asmuntis upande wake aliishia kusimama tu akiangalia , huku akiwa hana nia ya kusaidia.
Kundi lote nje lilijawa na hamasa na shauku katika kuangalia pambano hilo , asilimia kubwa ni wanajeshi waliokuwa katika daraja la chini kabisa katika mafunzo ya nishati za mbingu na ardhi hivyo waliokosa ujuzi na ufunuo, hivyo kwa pambano kama hilo wasingeweza kulimudu.
Mara baada ya kumshambulia kwa dakika kadhaa , Azzle ni kama alikuwa akiwasoma muda wote na alionekana kugundua udhaifu wao . Ghafla tu Azzle alipiga hatua kubwa mbele na kumshika Gray mkono wake mmoja. Gray ambae alikuwa akitaka kushambulia alijikuta akigutushwa na shambulizi hilo na kutaka kusogea lakini sasa kabla haja sogea Azzle alikuwa tayari asharusha ngumi kwa kulenga bega lake.
Kwa namna alivyofyatuliwa ni kama alikuwa mpira , kwani alipaa hewani na kwenda kutua mbele ya Helena , na mwanamke huyo hakuwa na jinsi zaidi ya kumkwepa Gray na ile alipotua kilichosikika ni Kwacha.
“Arghhhhh!!
Gray alitoa ukulele mkubwa baada ya mkono wake mmoja kuvunjika
“Nilikuambia vunja mkono wako au kufa ila hukunisikiliza”Aliongea Azzle.
Shambulizi lile liliwafanya watu wengi kushangaa baada ya kuona licha ya Azzle kushambuliwa na watu wawili , lakini hakupata jeraha hata moja
“Muue . haina haja ya kumuacha akiendelea kuishi”Aliongea Asmuntis aliekuwa pembeni.
Gray na Helena walijikuta akiwa katika mshituko mkubwa , hata Gray ambae alikuwa katika maumivu alijikuta yakipotea kutokana na kauli ya Asmuntis.
“Ngoja niwaache , kesho ni ufunguzi wa baraza la maksi . Haina haja ya kulikuza hili swala . Sitaki kuona sura zenu hapa tena , waambie watu wako wakae mbali na sisi”Aliongea Azzle akimuonya Helena.
“Mhunzi , wapo hapa kutafuta ugomvi tu , kuwaacha hai ni kuwapa kiburi cha kutuchokoza zaidi”
Azzle alikuwa sio mjinga , mara nyingi katika tukio kama hilo ilikuwa ni mtego umewekwa . Metal tide wametuma watu dhaifu ili kuibua ugomvi ili baadae Gonzalez akiingilia mwenyewe na hata Hamza kujitokeza na kupigana , watu wa baraza wasingemhukumu kwa kusema anajitafutia sifa.
Sasa kwasababu walijua Hamza ni dhaifu kama kweli atapigwa na Gonzalez basi moja kwa moja ingekuwa rahisi sana kwa bwana huyo kupata hadhi ya Ugwiji.
Ki ufupi ni kwamba mtego huo alikuwa amewekewa Hamza ili aingie kati na Gonzalez achukue hatua.
“Kama unataka kutuua tuue tu. Sisi ni wanajeshi sio Maninja”Aliongea Gray.
“Mhunzi!” Aliita Asmuntis huku akijua kwa tabia ya kizamani ya Azzle asingechukua hatua ya kuwaua. Lakini Asmuntis yeye kama muuaji hakujali watu watamfikiria nini kama atawaua hivyo alipiga hatua kusogea.
Gray na Helena mara baada ya kuona kweli Asmuntis anasogea walijikuta wakianza kupaniki.
Watu waliokuwa nje walijikuta pia wakishangaa , wakiwa hawaamni kama kweli Asmuntis kiongozi wa wauaji wa kundi la Bafodili anakwenda kuua wanajeshi wa kundi la kimasenari la Metal tide.
Kama angefanya hivyo maana yake ni kwamba kabla hata ya baraza , Baffodil ingejiingiza katika ugomvi na Metal Tide .
“Inasemekana aina ya mauaji ya King of killers , Asmuntis hayajawahi kukosa sababu ..Na kama akichukua hatua huwezi hata kujua namna unavyokufa”Watu walianza kuongea wao kwa wao.
“Kwa uwezo huo si hao watu wameisha tayari”
“Lakini mkumbuke huyu ni muuaji wa siri, yaani Assassin , lakini hapa si hadharani, Sidhani kama atamuua Gray na Helena kirahisi”
Wakati maneno yakiibuka kati ya kundi hilo la watu waliokuwa wakiangalia , upande wa Gray na Helena ulikuwa ni wa kutia huruma. Hisia zao zilisimama pia kwa presha kubwa iliokuwa ikiwasogelea kutoka kwa Muuaji namba moja duniani.
Asmuntis aliishia kusimama mara baada ya kutembea kwa hatua kadhaa huku akiwaangalia , hakuwa mrefu sana wala hakuwa na mwonekano wa kupendeza , lakini msisimko aliokuwa akitoa ulikuwa ni wa baridi na kufanya wahisi ni kama wanachomwa na vichomi vya baridi mwilini.
“Uchokozi wenu ni wa kijinga sana”Aliongea Asmuntis.
Kabla ya Gray na Helena kujibu ghafla tu walishuhudia Asmuntis akipotea mbele yao na ile anatokea kwa mara nyingine kilichosikika ni;
‘Clang!!’
“Haaa !”
Kundi lote la watu lilipiga kelele ya mshangao , waliweza kuona Asmuntis alikuwa amekwisha kumfikia Gray alipokuwa akitaka kumchinja na kisu, lakini matokeo yake hakufanikisha baada ya mkono uliokuwa mgumu kama chuma kuzuia shambulizi lile.
Comments