HADITHI: THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA (LIONELA)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: [email protected]
AGE: 18+
********************
UKURASA WA KWANZA
ANZA NAYO................
MAHAKAMANI
Ndani ya mahakama kuu ya taifa kulikuwa na kesi nzito ambayo ilikuwa inaendelea siku hii maalumu kwa ajili ya kusikiliza na kumhukumu mwanaume mmoja ambaye alikuwa ametenda uhalifu usio elezeka kwa lugha ya kawaida na kila mtu akaweza kuielewa kwa usahihi.
Ndani ya mahakama ni watu wengi ambao walikuwa wamefika mapema wakiwa wanaisubiri kesi hiyo ambayo ilikuwa gumzo kwenye kila kona ya mitaa. Walikuwa wamejiandaa vyema huku wakiwa wanamsubiria mhusika mwenyewe ambaye ndiye kesi hiyo ilikuwa inamhusu aweze kufika ili kesi ianze. JOPA MAGOMA, ndiye mwanaume ambaye alikuwa anasubiriwa ndani ya mahakama tukufu ili aweze kusomewa mashtaka yake mazito ambayo yalileta msisimko mkali ndani ya jamii ndiyo sababu kesi yake ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na watu wengi kila pembe.
Ndani ya muda mfupi, msafara wa gari za polisi na gari moja ambayo ilikuwa inatumika kubebea wafungwa iliwasili ndani ya mahakama hiyo huku kukiwa na ulinzi mkali mno kiasi kwamba hakuna mtu alikuwa anasogelea kirahisi ndani ya eneo hilo. Hata waandishi wa habari walijaribu kupenya penya na kupiga picha za kuibia ila hakuna ambaye alipewa uhuru wa moja kwa moja kufanya ambacho walikuwa wamemikusudia ili kuweza kuuza habari zao kwa ukubwa.
Kwenye ile gari ya wafungwa, alishushwa mwanaume mmoja ambaye alikuwa pande la mtu, alijazia vyema, afya haikuwa mgogoro kwa upande wake. Bwana yule kichwani alikuwa amenyoa upara ambao ulikuwa unang’aa isivyo kawaida huku akiwa na ndevu za kutosha kwenye mashavu yake na kidevuni, bila shaka zilitunzwa vyema.
Wakati wanamtoa mle ndani ya gari ndipo yalipatikana majibu sahihi kwamba huenda hakuwa mtu wa kawaida kama ambavyo wengi walikuwa wanamhisi. Alikuwa amefungwa minyororo mizito kwenye miguu yake huku kwenye mikono yake akiwa na pingu ambazo zilifungwa upande wa mbele. Kila baada ya hatua moja kulikuwa na askari wenye silaha nzito ambao walihakikisha bwana huyo anafika mahakamani salama na kupata kile ambacho alikuwa anastahili kukipata kwa yale ambayo aliyafanya.
Wakati anaingia ndani ya chumba cha mahakama, watu wote waligeuka kumwangalia bwana yule huku akiwa hana muda nao, alipelekwa mpaka kwenye kizimba, mahali ambapo alitakiwa kuwepo mpaka pale ambapo kesi yake ingefika mwisho. Bwana huyo hakuonekana kabisa kujali yale yote ambayo yalikuwa yanaendelea ndani ya lile eneo kwani aliona kama wanapoteza muda tu. Licha ya mawakili wake kujitahidi kupambana kuweza kumtetea lakini ilishindikana ila jambo la kushangaza ni kwamba yeye alikubali kwa mdomo wake kwamba mashtaka yote ambayo alikuwa ametajiwa pale, ni kweli alihusika nayo mwenyewe lakini hakuwa tayari kuomba msamaha jambo ambalo lilileta hisia zingine mpya ndani ya mahakama hivyo kazi ikabaki kwa jaji kufanya maamuzi ya mwisho kwani kila kitu kilikuwa wazi.
“Jopa Magoma, usiku wa tarehe kumi na tano ulihusika kwenye tukio la kumbaka mwanamke mwenye miaka kumi na tisa kisha ukamuua, unakubali mashtaka yako?”
“Ndiyo mheshimiwa jaji”
“Usiku mwingine wa tarehe ishirini tena ukahusika kwenye ubakaji na mauaji ambapo ulimbaka binti wa miaka kumi na sita kisha baadae ukambaka mama wa miaka arobaini na tano na haukuishia hapo tu ukafanikiwa mpaka kuwaua. Jopa Magoma, unakubali mashtaka haya?”
“Ndiyo mheshimiwa jaji”
“Una lolote la kusema kwa kile ambacho umekifanya kama kuwaomba msamaha ndugu na watanzania kwa ujumla kwa matukio yako yasiyo faa ambayo umeyafanya kiasi kwamba yameacha mapengo yasiyoweza kuzibika na maumivu makali kwa ndugu wa hao ambao umewafanyia ukatili?”
“Hapana, wote waliokufa walistahili kufa na kubakwa kama ambavyo nimefanya. Sijutii na wala siwezi kuomba msamaha mheshimiwa jaji”
“Mahakama imekukuta na hatia za kubaka na kuua kwa kukusudia ukiwa na akili timamu hivyo mahakama inakuhukumu kifo ambapo kabla ya kufa utapitia mateso makali ili iwe fundisho kwa watu wengine” jaji aliongea akiwa anaimaliza kesi hiyo huku akiinyanyua nyundo yake ili aweze kuigonga kuweza kuhalalisha hukumu ambayo alikuwa ameisoma mbele ya mahakama lakini ndipo ukatokea mshtuko mkubwa baada ya umeme kuzima ghafla.
Jopa, alikuwa ni mwanaume mwenye jeuri mbele ya mahakama, bwana huyo alihusika kwenye ubakaji wa wanawake watatu pamoja na kuwafanyia mauaji lakini akiwa mbele ya mahakama alikubali mashtaka yote na kugoma kuomba msamaha jambo ambalo lilifanya aipate hukumu ya kifo tena kwa mateso makali kabla ya kufa. Jaji mkuu akiwa yupo kwenye harakati za kuigongesha nyundo yake ndipo umeme ukakata.
Zilipita sekunde kumi tu umeme ukawa umerudi tena lakini wakati umeme unarudi, mwanaume yule hakuwa kwenye minyororo wala pingu. Jopa alikuwa huru kabisa akiwa amesimama nje ya kile kizimba mahali ambapo aliwekwa kwa mara ya kwanza. Kuwa huru halikuonekana kuwa jambo jema mle ndani, kila mtu alibaki ameduwaa asijue ni kitu gani kilikuwa kimetokea kwa wakati ule. Jaji alitoa amri ya kukamatwa kwa Jopa, ni kwa bahati ambao haikuwa upande wao.
Bwana yule hakuwa wa kawaida ndiyo maana alifungwa vizuri tangu mwanzo, alitua mguu wake mmoja kwenye kile kizimba kama anakipanda, alipinda kwa sarakasi ya nyuma ambapo alitua kwenye shingo ya askari aliyekuwa karibu yake akimjia kwa kasi, wakati anashuka naye chini aliivunja shingo yake mpaka ndani ya mahakama kukazuka kelele za hofu watu wakianza kuogopa. Alijivuta kwa nyuma na kugeuka kwa mguu wake ambao ulitua kwenye uso wa askari aliyekuwa pembeni akajibamiza ukutani kichwa kikapasuka.
Askari walianza kuongezeka mahali ambapo alikuwepo bwana huyo, mmoja alikuwa ameshika kiti cha mbao, alikirusha kwa nguvu zake zote ila kiliishia kupasukia kwenye mikono ya huyo bwana ambaye alimvuta askari huyo na kumtwisha ngumi yake moja kwenye shingo, shingo ilipinda akamtupa. Mwanaume mmoja ambaye alisimama kama shahidi wa upande wa bwana huyo alikirusha kisu kidogo kwa nguvu kuelekea kwa yule bwana na wakati anakidaka kilitua kwenye shingo ya askari mmoja ambaye alimkata kata kama karoti.
Aligeuka kwa nguvu zote miguu yake ikatua kwa askari wawili ambao walikuwa wanamjia lakini kisu kile alikirusha mbali huku akianza kukimbia kwa nguvu ambapo alipita kwenye vichwa vya wananchi ambao walikuwa wamenza kunyanyuka huku wakipiga makelele. Ile sehemu ambayo aliirushia kile kisu kulikuwa na askari wawili wenye silaha, wakati anakirusha kisu kile askari mmoja alikuwa mbele ya mwenzake akiwa amenyoosha silaha kuelekea alikokuwepo Jopa ila alionekana kusita sita kuiruhusu kwa sababu asije akashambulia watu wengine ambao hawana hatia.
Kule kusita kwake ilikuwa hatari kwake na kwa mwenzake kwa sababu ile nguvu ambayo ilitumika kurusha kile kisu ilikuwa sio ya kawaida. Kilizama kwenye shingo yake na kupita mpaka kwa askari aliyekuwa nyuma yake ambaye yeye kilimbaraza kwenye kifua kwa sababu alikuwa mrefu kuliko ambaye alikuwa mbele yake. Muda ambao aliutumia kuhangaika kuweza kuuguza yale maumivu na kuweza kukitoa kwenye mwili wake ndio muda ambao Jopa aliutumia kutembea kwa kasi kumuendelea pale ambapo alikuwepo hivyo wakati anafanikiwa kukitoa mwanaume huyo alikuwa amemfikia.
Alikutana na ngumi ya uso askari yule akainama chini akakutanishwa na goti ambalo lilimuinua tena kwa lazima akiwa anapiga kelele za kuomba msaada lakini hakuna ambaye angemsaidia wakati huo. Mwanaume huyo alimdaka kwenye shingo na kuinyofoa vibaya kisha akakichana kifua chake na kuupiga moyo kwa ngumi kali kiasi kwamba ulipasukia mwilini. Ile hali ndiyo iliwafanya watu watawanyike kama wamechanganyikiwa ili kuweza kuondoka lile eneo, wengi walianza kujutia kuja ndani ya lile eneo hiyo siku lakini nani angejua? Muda wao ulikuwa umefika.
Wakati wanasogelea ulipokuwa mlango wa kuingilia ndani ndipo mlango ulifunguka nje wakatokezea watu ambao walivaa kama walinzi ambao walikuwa na silaha mkononi, raia wote walitandikwa risasi mpaka pale walipo isha ndipo risasi zikatulia. Jambo la kushangaza ni kwamba wale watu ambao waliwashambulia raia walikuwa ni miongoni mwa askari ambao walikuwa walinzi wa hiyo mahakama. Jaji alichoka.
Hakuwa mzee lakini umri wake kidogo ulikuwa umeenda jaji wa Tanzania, alikuwa amekaa pale pale kwenye kiti chake akiwa anashuhudia kila jambo ambalo lilitokea ndani ya mahakama yake. Tangu mambo yote yanatokea alikuwa ametulia tu kana kwamba hakuna jambo ambalo lilikuwa baya wakati huo. Utulivu wake ulisababisha yeye kuangalia kwa umakini hatua zote ambazo zilikuwa zimefanywa na watu hao.
“Usiendelee kufanya kosa lingine kij….” jaji hakupewa nafasi ya kuweza kuongea lolote, alipigwa na ngumu nzito kwenye shingo yake na mtu ambaye yeye hakumuona kwamba alikuwa amesimama nyuma yake mpaka akapoteza fahamu.
Wanaume hao ambao hawakujulikana kwamba walikuwa ni akina nani haswa na kwanini walikuwa wanayafanya hayo yote, walifanikiwa kufanya ukatili ndani ya mahakama kisha wakatoweka na jaji eneo hilo mahakama ikiwa wazi kwani wafanyakazi wote waliuawa, ni jaji tu pekee ambaye waliondoka naye akiwa mzima, ilionekana kabisa kwamba walikuwa wana uhitaji mkubwa na huyo jaji ndiyo sababu hawakuwa tayari kuweza kumuangamiza kirahisi.
Ndo kwanza kabisa tunaufunua UKURASA kwa kwanza wa simulizi hii. Tuna mengi ya kuyafahamu na kuweza kuyapatia majibu.
Twende sawa pamoja mwanzo mpaka mwisho.
Langu jina FEBIANI BABUYA.
Comments