Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA (LIONELA)

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA 

STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER 

WHATSAPP: 0621567672

EMAIL: [email protected]

AGE: 18+

 

********************

UKURASA WA PILI

SONGA NAYO................

 

Jaji alishtuka baada ya muda kupita, ubaridi ndio ambao ulimshtua kwani mwili wake haukuwa na ushirikiano kwa sababu baada ya kushtuka tu alianza kutetemeka. Aliamshwa na maji ya baridi isivyokuwa kawaida ambayo ndiyo yaliufanya mwili wake kuwa kwenye ile hali ambayo alikuwa nayo wakati ule. Macho yake yalikuwa mazito, mwili ulikuwa umechoka huku akiwa na njaa kali ila haikuwa sababu ya kuyarudisha nyuma yote ambayo yalikuwa yametokea kule mahakamani.

Kumbukumbu zake zilirudi vizuri ndipo alishtuka baada ya kugundua kwamba hakuwa salama mpaka wakati huo, jambo hilo ndilo lilimfanya atahayari na kuanza kuangaza ndani ya hilo eneo ili kuweza kujua mahali ambapo alikuwepo kwani alijiona kabisa kuwa kwenye hatari kubwa ya kuyapambania maisha yake. Chumba ambacho alikuwepo kilikuwa kitupu kabisa zaidi ya sehemu tu ambayo yeye alikuwa ameketi, hakuona mtu hata mmoja na ndio wakati ambao akili yake ilirudi kwenye lile tukio ambalo lilikuwa limetokea ndani ya mahakama yake tukufu.

 

Moyoni alihofu kwa sababu hakujua kwamba ni nani alikuwa amemfanyia jambo lile, hakujua kabisa kwamba yule mtuhumiwa alikuwa ni nani haswa. Alishangazwa na bwana yule kufanya jambo lile mbele ya mahakama na kuua watu namna ile, hali hiyo ndiyo ilizidi kumpatia hofu kubwa kwenye moyo wake. Alitamani kuweza kumjua bwana yule kwamba alikuwa ni nani haswa kwenye maisha yake mpaka kuishia kwenye hali kama ile lakini hakufanikiwa kulipata jawabu lake kwa sababu muda huo haukuwa rafiki sana kwa upande wake akabaki na maswali ambayo hakuwa na uwezo wa kuyapatia majibu akiwa mwenyewe.

Ule ujasiri wa kufanya tukio kama lile tena mbele ya mahakama haukuwa wa kawaida, ulikuwa ni ujasiri ambao walikuwa wanauweza wanadamu wachache kwenye haya maisha ya kawaida. Hata walinzi wa mahakama walimshangaza, ilikuwaje wao ndio wakashiriki kwenye kutekeleza tukio kama lile? Maana yake ni kwamba walikuwa wanashirikiana na hao watu kwa muda mrefu? Hao watu ni akina nani na kulikuwa na nini haswa mpaka wakafanikiwa kuwafanya watu hao kukubali kulisaliti taifa lao na kufanya kazi na hao mabwana ambao bila shaka hakuwajua kabisa? Jibu lilibakia kuwa kizungu mkuti kwani alikuwa mwenyewe hata mtu wa kumuuliza hakuwepo humo ndani.

Jambo kubwa ambalo liliendelea kumtia hofu zaidi bwana huyo ni juu ya usalama wake na hatima yake kwa ujumla, aliletwa ndani ya hilo eneo asijue alikuwa anatakiwa kufanya jambo gani au kwanini alibakishwa akiwa hai. Huenda ni kazi yake ya kuhukumu watu ndiyo ilikuwa imemponza? Lakini kwanini iwe kwa mfungwa kama huyo ambaye aliua watu wengine wote? Ndipo aligundua kwamba jambo pekee la yeye kuweza kuijua sababu ya kuwa hilo eneo ni kusubiri mtu yeyote ambaye angekuja hapo ili aweze kuongea naye japo hakujua jambo hilo litawezekana kwa muda gani.

 

Akiwa anaendelea kujuta kwa mateso makali ambayo alikuwa anayapata hilo eneo ndilo mlango ulifunguliwa, kufunguliwa kwa mlango huo alimuona yule bwana mtuhumiwa wake akiwa anaingia ndani ya hilo eneo akiwa amezungukwa na wanaume wawili. Bwana huyo alikuwa amevaa suti ya blue lakini wale wengine wawili ambao wote walikuwa wamekaa upande wake wa kulia na kushoto, wao walikuwa ndani ya suti nyeusi ambazo ziliendana vyema na miili yao. Bila shaka alitambua kwamba huenda walikuwa ni walinzi wake.

“Unajua kwanini upo hapa mheshimiwa jaji?”

“Bila shaka sipo hata kuuawa kwa sababu mimi na wewe wote tunajua kwamba kama nilitakiwa kufa mpaka sasa nisingekuwa napumua”

“Huenda upo sahihi lakini kuishi kwako pia itategemea na aina ya mazungumzo ambayo utakuwa nayo hapa muda huu mheshimiwa”

“Unataka nini kutoka kwangu?”

“Kwanini unahisi nataka kitu kutoka kwako?”

“Kwa sababu kama ungekuwa unataka ni pesa usingetumia njia hii, wote tunajua hilo hivyo tufupishe mazungumzo, nenda kwenye hoja ya msingi moja kwa moja kwa sababu hapa nilipo nateseka na baridi na nina njaa kali sana natakiwa kwenda kula nyumbani”

“Mhhhh unawaza kwenda nyumbani?”

“Mimi ni mtu ambaye siku zote huwa nina amini kwamba lazima nipate njia ya kuishi hata kama nitakuwa kwenye mazingira ya namna gani, kwahiyo niambie sababu ya wewe kufanya haya yote ili uweze kukutana na mimi sehemu kama hii’

“Una kazi rahisi sana ya kuweza kuyaokoa maisha yako wakati huu ili nikuache hai, nahitaji unipatie jibu moja kwamba ipo wapi familia ya Gavin Luca”

“Samahani nahisi nimekusikia vibaya, umesema?” jaji alishtuliwa na jambo ambalo alilisikia kwenye kinywa cha huyo mwanaume kwa sababu lilikuwa jipya na kubwa mno kwake na hakutegemea kama angekutana na jambo la namna hiyo ndiyo maana waziwazi alionyesha hofu yake lakini bwana huyo hakuonekana kuwa na utani kwenye hilo jambo.

“Nina uhakika umenisikia vizuri, nina muda mchache wa kuwa na wewe kwenye hili eneo hivyo unaweza kunijibu haraka”

“Mhhhhhh naona mimi na wewe tuna mazungumzo marefu sana bwana Jopa, kama ungekuwa na namna nyingine basi usingeua watu wengi namna ile ili uweze kunipata mimi hapa, huenda nikawa msaada mkubwa kwako hivyo kwanza kabla ya kufungua rasmi haya mazungumzo, nataka unitoe kwenye hiki chumba na unipatie chakula ndipo tuongee kwa marefu juu ya jambo hili”

Jopa alimwangalia kwa umakini jaji huyo, alionekana kuwa mtu ambaye alijiamini ndiyo maana hakuwa na papara baada ya kusikia ambacho Jopa alitaka kukijua japo ni wazi kilionekana kumshtua kwa namna yake. Ilitolewa amri bwana huyo afanyiwe kile ambacho yeye alikuwa anakitaka kisha baada ya nusu saa maongezi yao yakawa yameanza upya kwa mara nyingine.

“Ni nani huyo ambaye anaitafuta hiyo familia?” lilikuwa swali la kwanza la jaji baada ya kuwa sehemu nzuri ambayo haikuwa inamuumiza kama ile ya kwanza.

“Mimi hapa”

“Hapana, nina uhakika sio wewe hapo, hakuna mtu ambaye anaitaka hiyo familia anaweza kuwa na jeuri ya kuonyesha sura yake hadharani tena kwa kujiamini namna ile. Ninajua kwamba wewe unatumika tu hivyo nataka kumfahamu huyo mtu ndipo tuendelee na haya maongezi”

“Una familia jaji, usifanye haya mambo kuwa magumu kwa sababu hivi ninavyo ongea na wewe, watu wangu wapo na familia yako muda wowote nitatoa amri hapa waue familia yako kwa sababu ya ujivuni wako ambao hauna umuhimu. Kuhusu nani kanituma au nafanya kazi kwa ajili ya nani hiyo sio biashara yako hivyo fanya yale ambayo yamekufanya wewe uwepo hapa vinginevyo sio muda mrefu utaanza kunipa lawama”

Mwanaume huyo wakati anaongea hivyo wote waligeukia ukutani sehemu ambayo ilikuwa imeunganisha na skrini kubwa. Ilianza kuonekana mijongeo ya video ikionekana watu kadhaa ambao walikuwa wamechangamana na walinzi wa jaji na hakuna mtu ambaye alikuwa amewashtukia nyumbani kwa bwana huyo jambo ambalo lilimpa wasiwasi mno hivyo alitakiwa kujibu kile ambacho aliulizwa, alimeza mate kwa shida, familia ilikuwa kila kitu kwake.

“Who are you people? (Nyie watu ni akina nani?)”

“Non of your business (Sio biashara yako)”

“Hiyo familia hakuna mtu hata mmoja ambaye anajua ilipo mpaka wakati huu ambao wewe unanihoji hapa”

“Whaaat?”

“Nina uhakika umekuja kwangu ukiamini utapata msaada jambo ambalo ulikuwa sahihi kabisa lakini huo msaada hauwezi kuupata kirahisi hivi leo leo kama ambavyo wewe unaonekana unatamani iwe japo mimi na wewe tunaweza kulifanikisha hili jambo pamoja”

“Nadhani bado haujanifahamu kwamba unadili na mtu wa namna gani bwana jaji ndiyo maana unayajibu maswali yangu kirahisi sana namna hii”

“Jopa hapa jambo la msingi sio mimi kujua kwamba nadili na nani bali ni aina ya taarifa ambazo wewe unazihitaji. Kufanikiwa kunijua tu mimi umefanya kazi kubwa sana ambayo ni hatua ya kwanza kwenye mafanikio yako ila jambo la kuipata hiyo familia ni jambo la pili ambalo linahusiana na mimi kwa udogo hivyo sio rahisi kama ambavyo huenda umepewa taarifa kwamba itakuwa”

 

Ukurasa wa pili unafika mwisho.

 

FEBIANI BABUYA.

Previoua Next