HADITHI: THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA (LIONELA)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: [email protected]
AGE: 18+
********************
UKURASA WA TATU
SONGA NAYO................
“Kwa maana hiyo hakuna umuhimu wa wewe kuwa hai na familia yako kwa sababu hauna msaada wowote ambao utautoa kwangu”
“Hilo ndilo kosa ambalo hautakiwi kulifanya kwa sasa kwa sababu umepata mwanga wa kile ambacho unakitafuta. Hauwezi kuua watu wengi namna ile na kujiweka hadharani sura yako huku ukijua kabisa kwamba unaenda kutafutwa na taifa zima, haujaishia hapo umemteka jaji mkuu wa taifa halafu unataka kipuuzi tu uipoteze hii nafasi ambayo umeipata kusikilizwa na mimi?”
“Kama unahisi maisha yako yana thamani kubwa namna hiyo basi uanze kuongea mara moja na kunipa majibu ya jambo ambalo nimekuuliza”
“Ni miaka zaidi ya ishirini sasa tangu kwa mara ya mwisho familia hiyo ilipo onekana, kuipata tena haiwezi kuwa rahisi namna hiyo. Tangu yatokee yale matatizo ya mwanzo kama raisi kuweza kujiua na viongozi wengine wakubwa kufa ndipo ilikuwa mara ya mwisho familia hiyo kuonekana na kusikika. Miaka yote hii nimeitumia kuitafuta kwa udi na uvumba lakini sikufanikiwa kuipata ila kwa sasa nimeanza kuona mwanga wa kuwapata siku za hapa karibu”
“Umetumia miaka ishirini kuitafuta?”
“Unayo izungumzia hapa ndiyo familia tajiri zaidi ndani ya bara zima hili kwa miongo karibia mitatu sasa, unahisi inakuwaje rahisi kuwapata kwa namna ambayo unataka wewe?”
“Sababu ni ipi haswa ya wewe kuitafuta sana familia hiyo bwana jaji?”
“Sijajua ila huenda mimi na wewe wote tuna sababu moja ya kuweza kuitafuta, mimi nina shida na ule utajiri, ninataka kuzipata zile pesa zote ziwe kwenye mkono wangu kwa sababu najua nikiwa nazo basi nitakuwa mtu mwenye nguvu zaidi ndani ya bara zima. Nikiwa mtu mwenye nguvu maana yake ni kwamba kila mtu atakuwa chini yangu na kunisikiliza kwa kila jambo ambalo nitaliongea hivyo nataka niwe na hiyo nafasi ya kufanya ambacho nakitaka kwa muda niutakao mimi”
“Kwahiyo miaka yote hiyo umeipambania kwa ajili ya kutafuta utajiri tu kutoka kwao?”
“Ndiyo ndugu yangu, pesa ni kila kitu kwenye haya maisha. Pesa inatafutwa kwa miaka mpaka kuna watu wanazeeka bila kuwa nayo, unanishangaa vipi mtu ambaye nimeitafuta kwa miaka ishirini tu? Tena pesa ambayo ipo ni mimi kufanikiwa kuwapata wahusika tu ndipo niipate” maongezi ya jaji ndiyo yalimfanya Jopa naye kusogea kwenye kiti na kukaa, alionekana kuanza kuvutiwa na maelezo ya jaji ambaye alikuwa akijiamini mno.
“Ni kweli kwamba Gavin Luca mwenyewe alikufa?” swali la Jopa bila shaka jaji hakuwa amejiandaa kulipokea, lilimshtua kwa namna yake ikamlazimu kujifuta kwanza usoni maana jasho lilianza kumtoka.
“Unajua kwanini naishi haya maisha ya siri sana wakati naitafuta hii familia Jopa?” mwanaume huyo aliishia kumwangalia tu, ilikuwa ni ishara kwamba alitakiwa kuendelea na maongezi yake ambayo yalikuwa kwenye kichwa chake.
“Kwa sababu najua kosa moja tu liyatabeba maisha yangu”
“Nina uhakika haukuwa na taarifa yoyote juu yangu na watu wangu, sasa ulikuwa unahofia nani atayabeba maisha yako?”
“Kwa sababu mpaka sasa hakuna mtu ambaye ana uhakika kwamba Gavin Luca alikufa?”
“Unamaanisha?”
“Inawezekana kwamba bado yupo hai”
“Ilitangazwa kila sehemu kwamba amekufa, nimekuuliza ili nipate uhakika kwako kwa sababu ulikuwa karibu na mazingira ya watu wale wakati hayo mambo yanatokea kwa taarifa ambazo nimezipata awali”
“Hilo ni sahihi, nilikuwa karibu nikiwa gizani kiasi kwamba hakuna mtu alijua uwepo wangu ndani ya ule mzunguko kwa sababu niliwaza kwamba yangetokea yale ambayo yalitokea na mimi ningekufa kama ningetaka sifa za kujulikana lakini kuishi kwangu gizani ndiko ambako kumenifanya mpaka leo umenikuta nikiwa na afya njema. Dunia nzima ilitangaziwa kwamba amekufa lakini jambo la kushangaza ni kwamba haujawahi kupatikana mwili wake wala sehemu ambayo alizikwa bwana huyo. Kuna namna watu wanaiamini mitandao na mitandao ndiyo huwa inatumika kuwapumbaza watu hususani watu wapumbavu hivyo usije ukakaa na ukaamini kwamba Gavin Luca alikufa”
“Na vipi kama yupo hai?”
“Kama kweli anaishi basi naweza nikakusihi kwamba kimbia kwa namna yoyote ile ambayo unaiweza wewe usije ukaonekana tena kwenye haya maisha”
“Unanitisha mimi?”
“Mimi sikutishi, unaongea haya mambo kirahisi sana kwa sababu hukuwahi hata kumuona mtu huyo namna alivyo. Sio binadamu ndugu yangu ni jini lile, napokwambia kwamba kimbia kwa namna yoyote ambayo unaweza namaanisha kwamba hakikisha asije kujua kwamba unaitafuta familia yake kwa sababu ataua mpaka kizazi chako chote ila mbali na hilo basi ombea kwamba taarifa juu ya kufa kwake ziwe za kweli”
“Mhhhhh unaonekana una mengi unayajua kuhusu huyu mtu japo nina uhakika haunifahamu mimi ndiyo maana unaniongelea kwa wepesi wepesi namna hiyo”
“Sina uhakika kama kuna ulazima wa kukufahamu wewe kiundani linapokuja swala la hicho kiumbe”
“Nipe mazingira yake ya mwisho mahali ambapo alikuwepo na ilikuwaje mwili wake usipatikane”
“Mara ya mwisho alienda kumuua kiongozi wa THE IMMORTALS ndani ya Kigamboni karibu na yale maeneo ambayo walala hoi huwa wanaponda kokoto kwa ajili ya kuzilisha familia zao. Ndani ya lile eneo alifanya mauaji ya kikatili mno kwa walinzi ambao walikutwa wamekufa waliokuwa wapo nje lakini ndani ya yale mapango ambamo ndimo yalikuwa makao makuu ya watu wale, eneo lile lilititia chini kiasi kwamba palifunikwa
Kwa taarifa za mwanzo ni kwamba bwana yule Gavin alienda lile eneo kuifanya ile kazi mwenyewe na eneo lile lilititia naye akiwa ndani hajatoka lakini jambo la kushangaza ni kwamba wakati wanafukua mle ndani, waliikuta miili ya watu ambao iliharibika na kupondeka pondeka vibaya kiasi kwamba ilikuwa haitambuliki kabisa hivyo kilicho fanyika ni kwenda kupima DNA ya ile miili ambapo wahusika walitambulika isipokuwa mtu mmoja tu DNA zake hazikuendana na mtu yeyote yule.
Hapo ndipo yalizaliwa maswali mengi, kwa asilimia themanini na tano wengi waliamini kwamba ule ndio ulikuwa mwili wa Gavin Luca kwa sababu DNA yake haikuwahi kupatikana popote pale kabla lakini asilimia kumi na tano kuna watu waliamini kwamba ule haukuwa mwili wake kwa sababu ya eneo ambalo ulikutwa wakati wanayatoa yale mawe makubwa ambayo yalikuwa juu ya ule mwili.
Sasa hapo ndipo ilizaliwa sintofahamu kwamba amekufa lakini watu werevu huwa tunazingatia kila taarifa hata kama itakuwa ndogo. Zile asilimia kumi na tano ambazo zilisalia ndizo zilimaanisha kwamba yupo hai, zile themanini na tano zilithibitisha kwamba amekufa na kwa sababu ndizo zilikuwa nyingi, ndiyo maana uliona wakitangaza kwa imani kubwa kwamba kile kiumbe kimekufa rasmi na ukurasa wake ukafungwa pale pale.
Mimi kwenye maisha yangu yote nimeishi na zile asilimia kumi na tano kwa zaidi ya miaka ishirini sasa nikiamini kwamba yule bwana bado yupo hai ndiyo maana huwa nafanya mambo yangu gizani kwa sababu sitaki ufahari wa kuja kujulikana nikawa mfano. Napiga hatua zangu taratibu ili hata siku nikigundua kwamba aliishi niweze kumuua kirahisi, kwa maana hiyo ni kwamba hakuna mtu mwenye majibu ya uhakika mpaka leo kama yupo hai kweli au alikufa ni wewe unachagua wapi pa kuamini”
Mheshimiwa jaji alionekana kuwa na taarifa nyingi za familia hiyo jambo ambalo lilimpa umakini Jopa kuweza kusikiliza ili aweze kumuelewa bwana huyo.
“Kama kweli alifanikiwa kuishi, kwanini mpaka leo haijawahi kuonekana hata alama tu ya uwepo wake?”
“Hilo hata mimi sijui, ndiyo maana nimekwambia hakuna mtu anajua kwamba yupo hai ama amekufa na kufahamu hilo ni mpaka lipatikane kaburi lake ithibitishwe kwa vielelezo maalumu ila bila hivyo basi itakuwa ni ngumu kuamini kwamba alikufa. Lakini kwa akili ya kawaida mtu kama yule hata angekuwa hai isingekuwa rahisi kuweza kupatikana namna hiyo”
Ukurasa wa tatu unafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.
Comments