HADITHI: THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA (LIONELA)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: [email protected]
AGE: 18+
********************
UKURASA WA NNE
SONGA NAYO................
“Kwa sababu zipi?”
“Alikuwa na familia tayari, siku zote mwanaume sehemu kubwa ya moyo wake inakuwa upande wa familia yake hivyo huenda hayo yote aliyafanya ili kuhakikisha familia yake inakuwa salama muda wote kwani yeye alijua kabisa kwamba kuna watu wanaweza wasiwe na nia nzuri kwa familia yake”
“Tunaanzia wapi na hii kazi kwa sababu umesema kukupata wewe umekuwa mwanzo wa mafanikio ya hii safari ambayo ninaifanya ya kuitafuta hii familia?”
“Hilo ni kweli kabisa lakini mimi binafsi siwezi kufanya kazi na watu ambao siwafahamu hivyo nahitaji kuwafahamu kwanza ndipo tujue tunaanzia wapi kuifanya kazi hii”
“Unataka kunifahamu mimi?”
“Sio wewe tu mpaka hao ambao wamekutuma wewe uje hapa”
“Hili jambo litakuwa hatari sana kwa upande wa usalama wako na maisha yako”
“Mpaka sasa sipo salama hivyo unaweza kuniambia tu nijue aina ya watu ambao naenda kuyaweka maisha yangu hatarini kwa ajili yao wapoje ili nisije kuwa napoteza muda wangu bila sababu zozote za msingi”
“Unalikumbuka jina la Gustavo Gaviria?”
“Unamaanisha yule muuza madawa ya kulevya ambaye aliwahi kutamba ndani ya mitaa ya PEENUGA kabla ya ujio wa Lucas Antony?”
“Ndiye huyo huyo”
“Hakuna mtu ambaye hamkumbuki yule bwana kwa sababu kwa kiwango kikubwa alifanya vijana wengi wakatamani kuingia kwenye hiyo biashara kwakuwa waliamini kwamba ndiyo ilikuwa njia rahisi ya kuweza kutoka kimaisha”
“Sasa huyo ndiye sababu kubwa ya sisi kuwepo hapa leo kuzungumza na wewe kuhusu jambo hili”
“Bado sijakuelewa unacho kimaanisha”
“Sio rahisi kunielewa ila nisikilize kwa umakini sana tena zaidi ya ambavyo unafikiria kwenye ubongo wako wa sababu hizi taarifa ambazo naenda kukupa hapa zinaweza kuyabeba maisha yako muda wowote kuanzia siku ya leo itategemea na namna ambavyo wewe utazipokea na kwenda kuzitumia.
Gustavo Gaviria aliuawa na DEA agent kutoka Marekani ambaye alipewa taarifa na mtu wa siri kuhusu uwepo wake kwa yule hawara wake ambako alikuwa anaenda kwa siri kubwa bila watu kufahamu lakini Gustavo kwa wakati ule alikuwa anamuamini mtu mmoja tu pekee ambaye ndiye huyo Lucas Antony ambaye ndiye alikuwa anakuwa na taarifa zake zote juu ya wapi atakuwepo, kitu gani ambacho atakifanya kwa muda fulani na biashara zote ambazo walikuwa wanazifanya, kiufupi ni kwamba hakuwa msaidizi wake tu bali mtu ambaye alimuamini kwa maisha yake yote.
Sasa wakati anaondoka usiku ule inadaiwa kwamba mtu ambaye alikuwa na taarifa za wapi atakuwepo alikuwa ni huyo msaidizi wake japo jambo hili limekuja kujulikana kwa baadae sana wengi hawakuwahi kulifahamu. Kabla ya hilo kutokea ni kwamba huyo msaidizi wake ndiye alikuwa amemtafuta huyo DEA Agent Rakeem ili amuuze Gustavo kwao kwa sababu walikuwa wakimtafuta kwa biashara yake ya madawa ya kulevya na nina uhakika unalitambua hilo namna Marekani wanavyo yapiga vita madawa ya kulevya kwa gharama ya namna yoyote ile.
Ile ndiyo sababu ambayo ilimfanya Rakeem kumuua Gustavo na ikaonekana kwamba lilikuwa ni jambo la kawaida tu. Ila kuna kitu Gustavo aliamua kuishi nacho moyoni kwa muda mrefu na ni watu wachache walikuwa wanakijua na watu hao walikuwa ni wanafamilia ambao hakuwa kwenye maelewano nao mazuri hivyo yeye siku zote alikuwa anjitangaza kwamba hakuwahi kuwa na ndugu. Hilo lilikuwa na faida zake na hasara zake, faida yake ni kwamba aliifanya familia yake kuwa salama muda wote kwa sababu hakuna mtu ambaye aliingia kuitafuta kwa namna yoyote ile kwani hawakuwahi kujua kwamba ilikuwa yake.
Lakini hasara yake ni kwamba alikufa akiwa mpweke bila ndugu yake yeyote yule kuhusika kwenye mazishi yake kwani yalisimamiwa na serikali. Sasa siri ambayo alikuwa nayo kwenye moyo wake ni kwamba bwana huyo alikuwa na mtoto ambaye alizaa na mwanamke mmoja ambaye alikuwa anajiuza huko kwao. Mwanamke yule aliwahi kumfuata Gaviria na kumpa taarifa ya mimba lakini aligoma kwa sababu ingeonekana kuwa aibu kwake kuweza kuzaa na mwanamke ambaye alikuwa anajiuza tena mtaani huku akiwa amefanya naye mapenzi kwa bahati mbaya tu tena akiwa amelewa.
Hali ile ilimfanya yeye kumpatia mwanamke yule pesa nyingi ili aweze kuitunza siri ile lakini alitakiwa kwenda kuitoa ile mimba hivyo makubaliano yao yakawa ni hayo ila mambo yalienda tofauti na yeye alivyokuwa amepanga kwani mwanamke yule hakuweza kabisa kuitoa ile mimba, aliamua kuitunza. Jambo hilo alilifanya kwa siri mpaka pale ambapo alijifungua na mtoto akaanza kukua ndipo alikuja kumtafuta Gustavo kwa mara nyingine na kumpatia taarifa ambazo zilimshtua sana ila hakuwa na namna kwa sababu jambo hilo lilikuwa limetokea na hakuwa na uwezo wa kuweza kulizuia tena.
Aliamua kukubaliana na hali kwa kuomba mwanamke huyo asije akavujisha habari hiyo yeye angemsaidia kwa kila kitu mpaka mtoto huyo anakua. Kwahiyo akawa ana mtoto kwa siri kubwa kiasi kwamba hakuna mtu ambaye alijua kuhusu hilo mpaka siku ambayo alikuja kufa ndipo wanafamilia wachache waliokuwepo wakazipata hizo habari baada ya mama wa mtoto kumpelekeka mtoto ili awafahamu ndugu wa baba.
Yeye baada ya kufika alihitaji kukutana na baba yake ndipo akapewa taarifa za kifo chake huku akiambiwa kwamba aliuawa na mtu ambaye jina lake baadae lilikuja kuwa maarufu sana. Kijana huyo hakukubaliana na hali hiyo alihitaji yeye na familia kwa ujumla waweze kumtafuta bwana huyo na alipe kwa yale ambayo alikuwa ameyafanya hivyo akatakiwa kufa kwa namna na kwa gharama yoyote ile.
Wakati huo bwana yule Rakeem alikuwa amerudi kwao Marekani lakini haikuwa tatizo la kumfanya aishi salama kwenye maisha yake. Mtoto wa Gustavo alidhamiria kumfanya mtu huyo apate mateso makali kwa kuipoteza familia yake aone jinsi maumivu yalivyokuwa makali, wakati huo naye alikuwa amefungua genge lake la siri kupitia jina la baba yake ili awe na nguvu kubwa naye akajikuta anaingia kwenye hiyo biashara huku moyoni akiwa ana shida kubwa na Rakeem aweze kulipa kwani aliamini kumpata Agent huyo ilimhitaji kuwa na watu kadhaa kwenye serikali ya Marekani na kuwa na watu wa namna hiyo inamhitaji mtu awe na mfuko mrefu, sasa kuhakikisha kwamba anakuwa na mfuko mrefu ndipo akaingia kwenye hiyo biashara akiamini kwamba ingempa pesa za kutosha.
Kwenye biashara alifanikiwa kwa kiwango kikubwa mno akawa anaingiza pesa nyingi ndipo sasa akatengeneza mfumo wake ndani ya Marekani ili kumpata bwana yule ambaye jina lake lilikuwa limepata thamani kubwa kwa kuweza kumuua muuza madawa ya kulevya maarufu ambaye taifa lake lilikuwa likimtafuta kwa kipindi kirefu.
Baada ya muda mrefu kupita alifanikiwa kuipata familia ya Rakeem ambapo alimtaka bwana huyo ampe taarifa za mtu aliye msaliti baba yake ili aweze kuiacha familia yake. Kama ulivyo nena hapo mwanzo kwamba sehemu kubwa ya moyo wa mwanaume upo kwenye familia ndivyo ilikuwa hata kwa Rakeem pia, hakuwa tayari kuona familia yake inauawa hivyo akalazimika kufanya jambo ambalo lipo kinyume na taratibu za kazi yake, kumtaja mtu ambaye alimpatia taarifa.
Sasa hapo ndipo kwa mara ya kwanza lilikuja jina la Lucas Antony kwenye masikio ya bwana huyo, jina ambalo lilikuwa la raia kutoka Tanzania. Licha ya Rakeem kuweza kutoa taarifa hizo lakini bwana huyo alimuua yeye na familia yake kwa sababu hakumuona kama ni mtu aliyekuwa anastahili kuwa hai kwa namna yoyote ile, alitakiwa kufa tena kwa mkono wake ndiyo maana aliua familia hiyo yeye mwenyewe huku akiwa tayari anajua hatua ambayo alitakiwa kuifuata kwenye karatasi yake ya maandishi ambayo ilikuwa inamuongoza wapi pa kwenda na nani wa kuweza kumfuata kwa wakati ambao alikuwa na uhitaji na ulazima wa kuweza kufanya hivyo.
Ndipo kwa mara ya kwanza alipo anza rasmi kutafuta taarifa za Lucas Antony, kumbuka kwamba wakati anafanya hayo yote muda ulikuwa umepita mrefu hivyo aligundua kwamba bwana huyo alikuwa mfu lakini kulikuwa na taarifa za uwepo wa familia yake na mwanae ambaye aliulaghai ulimwengu kwamba alikuwa amekufa.
Kwenye kufanya utafiti huo pia aligundua kwamba mwanae huyo alikuwa na nguvu za ajabu ambazo kwa mara ya kwanza zilikuwa ndani ya upanga ambao mpaka leo haujulikani upo mahali gani hivyo hapo akawa amedhamiria kumpata Gavin Luca. Ulitumika muda mrefu mpaka kupatikana kwa taarifa za bwana huyo lakini alifanikiwa kuzipata zote kwenye mkono wake hivyo akafanya maamuzi ya kuja Tanzania mwenyewe kwa mara ya kwanza kumtafuta mtu huyo lakini ndipo ikaja taarifa kwamba hakuwa hai, alikuwa amekufa japo taarifa hizo hazikuwahi kuwa na uthibitisho na ushahidi wa moja kwa moja.
Ukurasa wa nne unafika mwisho.
FEBIANI BABUYA
Comments