HADITHI: THE ODYSSEY OF GAVIN LUCA (LIONELA)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: [email protected]
AGE: 18+
********************
UKURASA WA TANO
SONGA NAYO................
Kwake taarifa hizo alizipokea vibaya kwa sababu alikuwa anamhitaji Gavin akiwa hai, alikuwa anataka alipe ushenzi ambao aliufanya baba yake kumuua Gustavo lakini hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo ila alibakia na mambo mawili kwenye kichwa chake, moja lilikuwa ni kupata shule na onyo kubwa kwenye maisha lakini jambo la pili lilikuwa ni kutafuta kitu ambacho alihisi ni haki yake ya msingi. Pesa.
Shule ambayo aliipata ni yale mambo ambayo aliyafanya Gavin Luca hali ambayo ilimfanya kuchukua tahadhari kubwa, sasa kwanini aliichukua hiyo tahadhari? Ni baada ya kugundua kwamba bwana yule alikuwa na familia lakini haikuwahi kujulikana tena kwamba familia hiyo ilipotelea wapi kwa kipindi chote hicho hivyo aliamini kwamba kama kuna binadamu alikuwa na zile nguvu basi kulikuwa na uwezekano mwanadamu mwingine akawa na nguvu za namna ile ile jambo ambalo huenda kwa baadae lingekuja kuwa hatari kwake yeye mwenyewe.
Baada ya kuligundua hilo ndipo aliamua kusafiri mpaka Japan na watu wake kadhaa, huko alienda kujitengeneza yeye na watu wake ili ikija kutokea siku akapata watu aina ya Gavin isijekuwa shida kuweza kupambana nao lakini wakati anafanya hayo yote ni kwamba kuna watu ambao aliwaweka kila sehemu ambao walikuwa wanaendelea kupeleleza kwa umakini kuhusu ilipokuwa familia ya mtu huyo ambayo alihisi ingemsaidia kukamilisha jambo lake ambalo alihisi ni haki yake yeye.
Kwenye kuitafuta familia hiyo jambo pekee ambalo alifanikiwa ama niseme tulifanikiwa ni kukupata wewe hapo. Kwenye ile orodha ya watu wote ambao walikuwa wanatafutwa na Gavin wengi kama sio wote walikufa huku zikibaki familia tu ambazo hazikuwa na hatia hivyo hata Gavin mwenyewe kama alikufa basi huko aliko anajua kabisa kwamba aliimaliza kazi lakini sisi tulitambua kwamba wewe bado unaishi jambo ambalo lilitushangaza kwamba wewe ulifanikiwa vipi kupona kwenye lile sekeseke? Ikawa sababu ya kuanza kuzitafuta taarifa zako zote hapo ndipo tukayagundua mengi ambayo ndiyo yamefanya hii leo mimi na wewe tufikie hapa.
Kwenye taarifa zile tuligundua kwamba wewe ndiye ulikuwa mtu wa karibu sana na raisi George kipindi kile lakini jambo hilo mlikuwa mkilijua nyie wawili tu. Wengi walikuwa wanajua kwamba bwana yule mtu wake wa karibu zaidi alikuwa ni mlinzi wake lakini haikuwa kweli, ulikuwa wewe hapo ambaye alikuwa anakutumia kukamilisha kazi zake nyingi ambazo asingeweza kuzikamilisha akiwa pale Ikulu kulingana na jina ambalo alikuwa nalo yeye na kuogopa kupata doa.
Wewe umehusika kwenye mauaji ya watu wengi kwa niaba yake, umehifadhi pesa nyingi ambazo zilikuwa zake na kila jambo ambalo yeye alihitaji ulifanye kwa ajili yake ulilifanya bila hata kuuliza. Tunajua kwamba pia alikuwa na sababu nyingine ya kuwa na wewe pembeni kwa siri kubwa kwa sababu alihitaji kuwapindua viongozi wake ambao pia hakuwa anawajua, raisi yule alikuwa anakutumia wewe uweze kuwatafuta watu hao kujua mfumo wao mzima kisha baada ya hapo angeweza kuwateketeza kisha yeye ndiye ajisimike kuwa kiongozi wa THE IMMORTALS lakini jambo hilo halikuwezekana kwa sababu kabla hajatimiza hayo yote ndipo alikutwa ameuawa wewe mwenyewe ukiwa hauna taarifa mpaka pale ulipokuja kuona kwenye vyombo vya habari.
Baada ya raisi kufa kwa sababu ulikuwa unazijua siri zake nyingi, kwa sababu ulikuwa unajua kila mambo yake ya siri zikiwepo akaunti zake za benki ambazo wewe ndiye ulikuwa ukizisimamia haukutaka kuishi kinyonge tena wala kuwa fala, uliamua kupotea na kila kitu ndipo ukaamua kuanza kuipambania nafasi ambayo mpaka leo upo nayo. Nafasi ambayo ulitumia pesa kuipata na hatimaye ukafanikiwa kuwa nayo, haya mambo hakuna wananchi wa huko nje ambao wanayajua zaidi ya sisi hapa ndiyo maana tukakutafuta kwa sababu taarifa hizi kama zikifika kwenye vyombo vya sheria ni lazima utahusishwa na kifo cha George.
Lakini baada ya kujua hilo kuhusu wewe tulijua kabisa wewe ungekuwa karata yetu ya mhimu kwa sababu unajuana na watu wengi lakini pia una taarifa nyingi za mambo ambayo yalitokea kipindi hicho hivyo tuliamini kwamba ungeenda kuwa msaada mkubwa kwetu ndiyo maana tuliamua kutumia njia yoyote kukupata. Sasa utajiuliza kwamba ni kwanini tumetumia njia hii?
Ukweli ni kwamba wewe ni miongoni mwa watu wagumu mno kukupata, mara kadhaa umekuwa ukionekana ukitokea Ikulu, jambo hilo limefanya tuchelewe sana kuweza kukufikia na ukiacha hilo, hata baadae baada ya kuyajua makazi yako, ilionekana wazi kwamba ni mtu mwenye ulinzi mkali mno kwa sababu serikali masaa ishirini na manne inaangalia usalama wako kwahiyo ingekuwa ni kazi kubwa kukupata na hata kama tungekupata kwa kule basi lazima kuna watu ambao na sisi tungewapoteza wengi na hatukutaka kufika huko kwa sababu tungekuwa tumetangaza vita vya moja kwa moja lakini pia tungeweza kutambulika kirahisi sana.
Hesabu ambazo zilikuja mezani ilikuwa ni kukupata ukiwa mahakamani kwa sababu ndiyo ilionekana kuwa njia rahisi zaidi kukamilisha jambo hili tena kwa haraka kubwa ndiyo maana tulianza kutengeneza mazingira mapema ya mimi kuwa na kesi kwa kuamini kwamba ungekuja pale mahakamani sasa mahakamani tungekukamata vipi? Ukiwa kwako au nje ya mahakama huwa unakuwa na ulinzi mkali zaidi ambapo kunakuwa na ule wa serikali lakini wakati huo huo unakuwa na ulinzi wako binafsi lakini pale mahakamani kunakuwa na ulinzi wa serikali tu pekee.
Urahisi ulianzia hapo baada ya kuanza kupandikiza watu wetu kwenye mfumo ili tukupate wewe ndiyo maana baada ya kuvamia pale umeona askari karibia wengi wamekugeuka na ambao walibaki ndiyo wale wamekufa mheshimiwa jaji. Mimi ndiye nilitakiwa kuifanya hii kazi ya kuhakikisha tunakupata na kufanya mazungumzo na wewe ya moja kwa moja kama hivi ili ujue umuhimu na ukubwa wa hili jambo kiasi kwamba kuna roho za watu zimetoka ili kuweza kufanya hili litokee, kamwe usije ukalisahau jambo hilo kwenye akili yako kwa sababu inaweza kukukosti.
Na jambo ambalo ulilifanya ni kwamba wewe una familia mbili ambapo moja mkeo mkubwa hajui kwamba una familia ya siri. Kwa sababu ulijua ni ya siri basi haukuipa ulinzi mkubwa ndiyo maana imekuwa rahisi mimi kuwapenyeza watu wangu mle ndani ila tambua kama utafanya jambo lolote la kijinga basi hakutakuwa na mazungumzo mengine ya amani kama ambayo umebahatika kuyapata leo kwa sababu watu ambao unaingia nao kwenye hii kamari sio watu wa kawaida bwana jaji hivyo hakikisha unayakumbuka maneno yangu kwa usahihi sana.
Nadhani nimekwambia jambo moja tu pekee la bwana huyo kuchukua tahadhari, lakini jambo lingine la pili ambalo alihisi ni haki yake kulipata ndiyo sababu amewekeza pakubwa kwenye kuitafuta hii familia ni kwamba ule utajiri wote unastahili kuwa wake kwa sababu ulipatikana kwa msaada mkubwa wa baba yake. Anataka kuhakikisha kama kuna wanafamilia wamebaki ahakikishe anawateketeza wote kisha baada ya hapo abebe fedha zote za hiyo familia ndipo anaweza kuhama moja kwa moja ndani ya taifa hili ila bila ya hivyo nadhani muda umefika sasa anaweza kuanza kuyaonyesha makucha yake hadharani. Nadhani ulidai kwamba unataka kutufahamu, umeweza kutujua kiufupi tu kuhusu maisha ya hapo nyuma na sababu za mhimu ambazo zimefanya mimi na wewe tupo kuongea hapa muda huu”
Mheshimiwa jaji alibaki ameduwaa, watu hao walikuwa wanafanya kazi kwa data ndiyo maana Jopa alimpa taarifa mpaka za kwake yeye mwenyewe ambazo zilikuwa za siri mno na aliamini kwamba siri hizo alibakia nazo mwenyewe tu kwenye kifua chake ila haikuwa kweli. Mheshimiwa jaji ndiye alikuwa mtu wa siri wa raisi George ambaye alikuwa anatumika kuweza kukamilisha kazi nyingi za bwana huyo hivyo baada ya George kufa iliaminika kwamba siri zote alibakiwa nazo yeye tu pekee kiasi kwamba akaamua kuzizika kwenye moyo wake lakini siku hiyo alikuwa anapewa taarifa za hizo siri. Alichoka.
Alihema na kushusha pumzi ndefu baada ya kusikia hiyo simulizi kutoka kwa bwana Jopa Magoma.
“Na vipi kama sitakuwa tayari kufanya kazi na nyie?”
“Utaziponza familia zako kisha wewe utawekwa mahali ukiwa hai ila utatamani ni bora ungekufa”
“Nahitaji kuonana na huyo kiongozi wako”
“Hilo ni jambo ambalo haliwezekani mpaka siku ambayo ataamua yeye kufanya hivyo ila kwa sasa utakuwa unawasiliana na mimi hapa kwa muda ambao nitakuwa nakutaka ama kama utakuwa na taarifa za mhimu kuweza kunipa”
“Umeniambia kwamba hata huyo bosi wako anazihitaji hizo pesa mbazo hata mimi nimepoteza miaka nikiwa nazitafuta, itakuwaje kuhusu nafasi yangu kwenye hizo pesa?”
Ukurasa wa tano unafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.
Comments