SEHEMU YA 203.
Kabla ya mc kumaliza kuongea , makelele mengi ya kushangilia yaliweza kusikika . Mashabiki wengi damu zilionekana kuwachemka . Kuna mpaka ambao walikuwa wakifuta machozi kwa furaha zao.
Yalikuwa ni makelele ya kulitaja jina la Divinirth mwanzo mwisho huku wengine wakitamka maneno ya kiapo yanayomtambulisha mfalme wa kuzimu.
Azzle na wenzake pia walisimama na kuanza kupiga makofi mengi wakiuungana na watu waliokuwa wakishangilia huku macho yao yakiwa yamejaa unyevunyevu.
Nyakasura ambae alikuwa juu ya jukwaa aliishia kupindisha midomo kwa kuchukia.
“Ana kitu gani cha upekee mpaka kuwa na mashabiki wengi hivi. Wajinga kweli”Aliongea lakini licha ya hivyo kulikuwa na kitu kigeni kilichokuwa kikionekana katika macho yake.
Regina alijikuta akihisi ni kama vile nafsi yake imekuwa na shimo ghafla. Macho yake mawili yalichanua huku akiwa ametoa amepanua mdomo kwa mshangao.
Alijihisi ni kama pumzi zinampotea mara baada ya kusikia jina la Lucifer likitajwa na kujua moja kwa moja jina hilo lilimhusu nani.
Ukweli siku ya kwanza aliposikia jina hilo kutoka kwa Leibson aliona ni jina baya ambalo hakulipenda kwa kuona limekaa kishetani zaidi , lakini mara baada ya maelezo ya mshereheshaji kusikika juu ya sifa za Hamza alijikuta kuwa katika hali ya kuchanganyikiwa.
Hakuamini mwanaume ambae alikutana nae kwa njia ya kuweka tangazo mtandaoni ili kuigiza kuwa ni wapenzi na uhusiano wao kubadilika na kuwa mkubwa hata kufunga ndoa.Mwanaume ambae alijifanyisha kusoma chuo na kuishi maisha ya kimasikini huku akifanya kila aina ya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato. Mpaka dakika hio Regina alijihisi mambo mengi ambayo yametokea kuhusu Hamza yalikuwa ni ya kumfanya apatwe na ugonjwa wa moyo.
Hatimae wakati watu wakishangilia kwa nguvu , Hamza aliweza kuonekana akitokeza kwenye mlango na kupanda jukwaani.
Viongozi wa Set na baadhi ya viongozi wawakilishi kutoka nchi mbalimbali walisimama na kuanza kupiga makofi ya kumkaribisha.
Hamza mara baada ya kumulikwa na mwanga , aliishia kuinua kichwa chake juu na kuzunguka kuangalia watu waliokuwa wakimshangilia na kwa jinsi watu walivyocharuka aliishia kutoa tabasamu tu.
Ijapokuwa alijua alikuwa maarufu kwa yale ambayo amefanya katika ulimwengu wa siri , lakini kwa namna moja alijikuta akiguswa kuona kwamba alikuwa na wafuasi wengi.
Hamza alijikuta akijionea aibu baada ya kukumbuka alikuwa ameamua kustaafu na sasa alikuwa akiishi nchi ndogo huko Afrika na kuajiriwa na mwanamke.
Hamza hakusimama sana katika eneo moja na badala yake alitembea na kwenda kwenye jukwaa la magwiji.
Baada ya kukaa chini , mc alisubiri zaidi ya dakika kumi kwa ajili ya watu kutulia na kisha ndio akaanza taratibu za kuita mtu wa mwisho.
Mtu wa mwisho alikuwa ni kiongozi mkuu wa watu wa Bondeni , pamoja na mtendaji mkuu wa Binamu, Master Mathias Huge.
Watu wengi hawakuwa wakimjua sana kutokana na aina ya sekta aliokuwa akisimamia , kuna hadi wengine ambao walionekana kutomfahamu kabisa . Hata hivyo Huge hakuonekana kujali sana na badala yake alienda moja kwa moja kwenye jukwaa.
“Haha..Huge watu hawakushangilii sio kwasababu hawakujui , bali wewe ni muuza siri za watu , hivyo watu wanakuchukia , muangalie mwenzako Lucifer namna alivyokuwa maarufu.. hahah”Aliongea Oleg Phantom.
“Phantom sisi watu wa binamu hatuuzi tu taarifa kwa kila mtu anaetaka , tuna vipaumbele vyetu vilevile. Hata hivyo mimi kama Msomi nishazoea kutofahamika , siwezi kujilinganisha na Bro Hamza katika swala la umaarufu”
“Ni usomi gani uliokuwa nao , kuongea maneno yaliojaa mafumbo ndio unaita usomi. Biashara yako ya kuuza taarifa za watu haina tofauti na biashara ya umbea ndio maana watu hawakupendi”Aliongea Nyakasura huku akivuta mdomo.
“Nyakasura kwanini unaongea kama vile tumekuwa maadui , ilihali hatujawahi kuonana kwa zaidi ya miaka miwili?”
“Kwani ninachoongea ni uongo? Najaribu kukuambia ukweli kama mtu ambae tunatokea ukanda mmoja”Aliongea Nyakasura.
“Tena ni kweli nimekumbuka nyie wote watatu mnatokea ukanda mmoja , mnaweza msiwe marafiki lakini maeneo mnayoishi yanapata faida kubwa kupitia mafanikio yenu”Aliongea Sebastiani.
“Sebastiani naona siku hizi unajua kuongea. Hatujaonana kwa muda mrefu , vipi hali yako?”
Moja ya sababu ya Baraza la giza kuungana na Hamza katika kushambulia watu wa mahakama ya nuru sio kwasababu ya ugomvi baina yao , lakini pia ni kutokana na ukaribu wa Sebastiani na Hamza.
Hata hivyo ni Hamza ambae aliomba Sebastiani na watu wake kumsaidia, baada ya kuona anazidiwa na maadui hivyo ni sawa na kusema Hamza alipigana vita bega kwa bega na Sebastiani.
“Baada ya vita nilienda zangu kwenye ngome ya kaburi kulala. Nimeamka katikati ya mwaka huu na ndio nilipopokea mwaliko wa kuja kushiriki katika baraza la maksi. Nikikujibu naendeleaje ki ufupi ni kwamba bado nina usingizi”
“Mhmm! Mavampire huwa mnashida kubwa sana , yaani umelala zaidi ya miaka miwili halafu unasema bado una usingizi. Staili yenu ya kimaisha inasikitisha sana”Aliongea Oleg.
“Hehe..Mimi namuonea wivu Sebastiani , wao kulala ndio namna ya kurefusha maisha yao na vilevile anao uwezo wa kuamka pale anapotaka. Sio kama sisi binadamu hatuwezi kulala muda mrefu na vilevile maisha yetu ni mafupi kutosha kutimiza ndoto zetu”Aliongea Silvia.
“Silvia na uwezo wako wa mafunzo ya nishati ya ufunuo wa uponyaji , huna haja ya kuwazia sana kuhusu miaka yao ya kuishi.”Aliongea Mikaeli.
Silvia na Madhabahu ya Nuru walikuwa na ukaribu mkubwa mno na hio yote ni kutokana na ufunuo wa mafunzo yao ulikuwa ukishabihiana sana licha ya kuwa na misingi tofauti. Watu wa nuru wao walitegemea zaidi maandiko na msingi wa kisheria kukuza nguvu za kiroho wakati upande wa Silvia na watu wake walitegemea maandiko pia kupanda levo katika kuvuna nishati za mbingu na ardhi tofauti ni kwamba tu katika kitabu kizima cha maandiko wanaweza kuamini mstari mmoja tu. Hivyo haishangazi kuona watu wa Silvia kuhudhuria ibada za madhahabu ya Nuru wakati ikiwa ni siku ya mahubiri ya mstari wanaotumia kuvunia nishati.
“Kama ni hivyo nakushukuru Mikael kwa kunitoa wasiwasi”Aliongea Silvia kwa tabasamu.
Ijapokuwa macho ya hadhira yalikuwa yakiwaangalia zaidi magwiji hao , lakini haikuwazuia kuongea wao kwa wao.
Ukweli sio kwamba magwiji hao walikuwa wakipatana , walikuwa na vinyongo lakini waliamua kuvificha kwa wakati huo.
Regina aliekuwa kwenye juktwaa la kundi la Metal Tide aliishia kurudi katika uhalisia mara baada ya kuhisi sio kama alikuwa akiota , bali kila alichokuwa akiangalia ni uhalisia. Aliishia kuvuta pumzi nyingi huku akishika kifua chake kujituliza.
Regina sasa aliona ndio maana Hamza alikuwa wa tofauti katika mambo mengi , mfano aliamini kwa uzuri wake ingekuwa rahisi kumtuliza mwanaume yoyote lakini kwa Hamza ikawa tofauti , kumbe yote hayo yalitokana na nguvu aliokuwa nayo.
Mwanaume siku zote akiwa katika kilele cha dunia yote , matatizo mengi ambayo watu wa kawaida wanayaona ni makubwa kwake ni ya kawaida sana.
Regina alikuwa na hisia mchanganyiko wakati huo na alishindwa kujizuia baada ya kukumbuka jambo.
“Kwahio nia yenu ya kuniteka ilikuwa ni kwa ajili ya kudili na Hamza?”
“Naona sasa umeelewa”Aliongea Helena huku akicheka.
“Mnao uwezo wa kudili nae?”Aliuliza Regina akiona ni kama watu hao wanajitafutia tu matatizo , lakini kwa Helena ilikuwa tofauti , kwani ukauzu ulimvaa.
“Kama angekuwa ni yule wa mwanzo tunaemjua tusingejaribu kufanya chochote , lakini huyu wa sasa alichokuwa nacho ni mwonekano pekee”
“Unamaanisha nini?”
Regina alijihisi kuwa katika hali ya mshangao na kutaka kujua lakini ghafla tu alinyamazishwa na sauti ya Raisi wa Baraza la Maksi , ambae alianza kutumia uwezo wake wa sauti kuongea.
“Jamani naombeni tuwe kimya. Tunakwenda kuanza mazungumzo ya kwanza rasmi”
Mara baada ya kuongea , mtu mmoja mwenye mwili mkubwa alisimama kutoka kwenye siti yake.
“Subiri kidogo ndugu raisi. Mimi Gonzalez nina jambo la kuongea”
Mara baada ya kumuona Gonzalez , watu zaidi ya elfu therathini waliohudhuria walijikuta wakipigwa na mshangao . Watu wachache walikuwa washasikia ugomvi uliotokea baina ya kundi la Metal tide na kundi la Barhams na pia nia ya Gonzalez kutaka kumchallenge Hamza.
Lakini watu wengi waliona Gonzalez alikuwa akijitafutia tu kifo , anatubutu vipi kujaribu kushindana na mtu kama Hamza.
Licha ya kwamba sio kawaida kwa mtu kutaka kuingilia kikao cha baraza hilo , lakini watu vilevile hawakumkasirikia na badala yake walishikwa na shauku ya kutaka kumsikia.
“Kapteni wa Metal Tide , ni jambo gani unataka kuongea?”Aliuliza Maxim huku akiwa na tabasamu lakini macho yake yalikuwa na ukali.
Gonzalez aliishia kutunisha kifua , huku akinyoosha shingo yake vizuri kujiweka katika namna ya heshima.
“Najiuliza kati ya magwiji kumi, ni wote wanaostahili kukaa pale”
“Oh?” Maxim alijikuta akisinyaza macho yake.
Haikuwa tu kwa Maxim alieshikwa na msahngao , lakini watu wote waliosikia kauli yake walishikwa na ajabu.
“Namimi nimejiuliza na kutamani kujua ni nani ambae unahisi hastahili kuwa pale?”Aliuliza Maxim.
Gonzalez alihisi kabisa kila mtu alikuwa akimwangalia na kutokana na hali hio alijisikia vizuri na sauti yake ilianza kusikika kwa kujiamini zaidi huku akinyoosha kidole chake uelekeo wa jukwaa la magwiji.
“Lucifer najua una mashabiki wengi lakini kundi langu la Metal Tide haliwezi kukubali kuchokozwa kirahisi. Mimi Gonzalez nina wasiwasi na uwezo wako. Ninaamini kabisa hauna vigezo vya kukaa kwenye jukwaa la magwiji tena”
Dakika ambayo maneno hayo yalimtoka , uwanja mzima ulizizima kwa mshangao.
Asmuntis , Azzle , Mameni na wengine walisimama wote huku wakimwangalia Gonzalez kwa macho makali.
“Gonzalez unajiona nani kuleta ukiburi wako mbele ya bosi wetu? Tushuke chini tuone mimi mzee nisipokuua”Aliongea Leviathani kwa sauti kubwa ya jazba.
Kundi kubwa pia la mashabiki wa Hamza lilianza kumnyooshea vidole Gonzalez kwa dharau zake.
Regina ambae alikuwa amekaa hatimae aligundua nini kinakwenda kutokea baada ya kuona tukio hilo na alishindwa kujizuia na kumwangalia Helena kwa macho yaliojaa ukali.
“Nyie watu mmenileta hapa kwa ajili ya kumtishia ili mpate umaarufu sio?”
“Ms Regina kuwa mpole, wewe ni mpango wa dharula tu . Ukweli hata tusipokutumia mume wako hawezi kumshinda kapteni wetu”Aliongea Helena huku akicheka.
“Huna aibu wewe!” Regina aliongea kwa hasira
“Tunafanya kinachopaswa kufanywa”
Regina uso wake ulijaa wasiwasi. Hakujua ni kitu gani kinakwenda kutokea na vilevile hakujua kati ya Hamza na hilo jitu nani ana nguvu zaidi.
Alijikuta akijilaumu kwa kutotilia mkazo mafunzo ya andiko la kimalaika. Lakini hata hivyo aliona hata kama angejifunza vipi ingekuwa ngumu kwake kutowazuia watu hao kumkamata.
Gonzalez upande wake hakujali kabisa juu ya hasira za watu na alimwangalia Hamza bila hofu yoyote.
“Lucifer nadhani nilikuambia jana kabisa kuwa leo nitahitaji maelezo! Vijana wangu walishambuliwa na watu wa kundi lako. Kama usipopiga magoti na kuomba msamaha , siwezi kuacha hili swala lipite”
Hamza upande wake alikuwa tayari ashaa washa sigara muda mrefu tokea Gonzalez aanze kuongea na sasa alikuwa akitoa moshi kama tanuru kutoka kwenye pua zake, huku akitingisha kichwa chake.
“Nipo kwenye mudi nzuri tu kwasababu leo ni siku ambayo nitawatunikia ndugu zangu tuzo . kuhusu swala lako kwanini tusiliache kwa leo na kutafuta siku nyingine?”
“Yaani unataka tubadili siku tena. Unaogopa nini kupigana na mimi mbele ya watu wa ulimwengu wa siri au unaamua kuficha udhaifu wako kupitia sifa ulizopewa?”
Malijendi waliokuwa katika jukwaa waliishia kumwangalia Gonzalez na mwonekano wa kichokozi. Hakuna hata mmoja ambae alikuwa na nia ya kuingilia hilo sakata.
Hamza aliishia kuipiga piga sigara yake na vidole kudondosha majivu huku macho yake yakitoka katika ukawaida na kuwa siriasi.
“Ulimuumiza Azzle jana nikakuacha lakini unaanza tena , hivi unajua nilipaswa kukufanya nini. Nadhani madini yako ya chuma yamekufanya kuwa na kichaa ndio maana unaamua kunichokoza. Kabla ya kunichokoza unapaswa kufikiria kuhusu wanajeshi wako , wataishije baadae”Aliongea Hamza.
Hali ya hewa ilizidi kuwa siriasi kutokana na maneno ya Hamza na watu wengi walianza kuingiwa na wasiwasi.
Hasira ya Infernal king ilikuwa ikijulikana na watu wengi tokea kipindi kile , watu wa Mahakama takatifu walimchokoza na hio sababu moja tu ilimtosha Hamza kuanzisha vita . Sasa leo hii kajikundi kadogo tu ka Metal Tide, kama Hamza akitaka kukazima ni jambo jepesi sana.
Upande wa Gonzalez yeye alihisi Hamza alikuwa akijigamba tu ila hana uwezo wowote.
“Huna haja ya kuongea kwa kujigamba , kama uwezo unao utumie acha maneno mengi”Aliongea Gonzalez na kisha alimwangalia Maxm.
“Prezdenti nadhani kuna sababu kubwa ya kuitisha mkutano mkuu wa Magwiji? Na kama ndio, sababu yenyewe ni kuuthibitishia ulimwengu kama magwiji kumi tunaowatambua wanastahili kuendelea kubaki katika nafasi zao. Si ndio”Aliongea Gonzalez.
“Ndio , ila hio ni sababu ndogo tu. Ni matumaini yetu kuona chini ya uongozi wa Magwiji wetu , amani na utulivu ndani ya ulimwengu wa giza inaendelea kudumu na kupitia ushirika wa nguvu zao ndio kitu ambacho tunahitaji”
“Haha.. upo sahihi lakini ziku zote Dhahabu halisi haigopi kusafishwa kwa moto! Leo hii mimi Gonzalez nakwenda kuwathibitishia unafiki aliokuwa nao mfalme wenu wa kuzimu. Sijawahi kupenda kuwa maarufu lakini nina mipaka yangu vilevile. Lucifer kama usiponishambulia nitakushambulia mimi!”
Kabla hajaendelea kuongea kauli nyingine ghafla tu kivuli cha mtu kilionekana mbele ya Gonzalez.
Shadow killer!
Watu walimaka mara baada ya kugundua mtu mwenye uwezo huo alikuwa ni Asmuntis , mbinu hio ilikuwa na uwezo wa kumpa spidi kubwa sana katika kufanya mashambulizi.
Gonzalez alionekana kutegemea jambo lile na kabla Asmuntis hajamshambulia na kisu chake , mkono wake uligeuka na kuwa chuma na kukinga shambulizi lile.
“Cliiiiii!!”
Kilichosikika ni mkwaluzano wa wa kisu kile na mwili wa chuma wa Gonzalez , ikionekana kimeshindwa kupita kabisa katika ngozi yake.
Muda uleule Gonzalez alitumia mkono wake mwingine na kumpiga Asmuntis na ngumi yenye uzito wa tani za kutosha na kumfyatua.
“Bam!”
Asmuntis alipigwa ngumi nzito sana ambayo ilimfyatua na kumfanya arudi nyuma nyuma huku akitema damu nyingi kwenye midomo yake.
“Master!”
“Mchafuuuu!!!”
Black Fog na Azzle haraka sana waliruka na kwenda kumsaidia Asmuntis kusimama, huku kundi la watu likimwangalia Gonzalez kwa macho makali.
Asmuntis mara baada ya kusimama aliishia kutema damu tena na kisha alitngisha kichwa kuwaonyesha kwamba alikuwa sawa.
“Asmuntis nishawahi kukuambia hutoweza katika maisha yako kuniua mtu kama mimi , mashambulizi yako ni kama kichekesho kwangu..”
Kabla hajaendelea kuongea alijikuta akihisi msisimko usiokuwa wa kawaida ukipita mgongoni kwake na kumfanya ahisi mwili wake kusisimka mno kama ameshikwa na maji ya baridi sana. Haraka sana alijikuta akigeuka na palepale ndio alipoweza kumuona Hamza akiwa amesimama huku macho yake ya ulegevu yakiwa yamebadilika na kuingia ndani huku yakiwa katika hali ya ukali mno, macho yake tu lilikuwa shambulizi lililomfanya kuhisi anakiona kifo kinamkaribia.
Comments