SEHEMU YA 205.
Gonzalezi alimwangalia Hamza alivyokuwa akimsogelea na palepale alijua ni kwa namna gani tatizo limekuwa kubwa. Akiwa na damu mdomoni , aliishia kusaga meno kwa nguvu na kisha akaongea;
“Wewe.. ulifanya makusudi kuniigizia sio?”
“Iwe nimekuigizia au vyovyote sio suala langu hilo, kama usingenisumbua hili lisingetokea”
“Lucifer kabla haujafanya chochote kwanini usiangalie kushoto kwako eneo F kwenye siti?”Aliongea Gonzalez akiwa na mwonekano wa uovu kwenye macho yake.
Hamza alijikuta akikunja ndita na kusimama kwanza huku akigeuka na kuangalia upande ambao Gonzalez alikuwa akiongelea na ile kugeuka tu sura ya kwanza kuiona ilikuwa ni ya Regina aliekuwa amevalishwa mavazi ya jeshi la Metal Tide.
Wawili hao waliishia kukutanisha macho kwa umbali . Hamza alishituka wakati huo Regina alijikuta akijawa na wasiwasi na kuishia kukunja ngumi yake tu.
Hamza muda ule ni kama makelele ya watu kumshangilia yalimpotea ghafla na sio makelele tu ni kama watu wote walitoweka na alibakia yeye aliekuwa kwenye steji na kipenzi chake Regina aliekuwa katika siti za juu.
Kulikuwa na hisia nzito sana zilizopita katika kichwa cha Hamza.Hakudhania uhalisia wake ungeweza kufahamika kwa Regina kwa namna hio tena katika Baraza la maksi.Alijikuta akishikwa na hisia nyingi mchanganyiko ambazo alitamani kuziweka wazi. Lakini katika muda huo alijihisi kuwa katika hasira zaidi ya kumdhibiti Gonzalez.
Hamza aligeuza macho yake na kumwangalia Gonzalez katika mwonekano wa ukauzu zaidi. Macho yake yalikuwa ni kama ya mnyama mkali ambae anajiandaa kumrarua mtu.
“Umethubutu kumteka mke wangu?”Aliongea Hamza kwa sauti nzito sana. Muda ule ndio sasa anajua taarifa ambayo Huge alitaka kumwambia ilikuwa ikihusiana na jambo hilo , alijikuta akimtukana ndani kwa ndani huku akigeuza uso wake na kumwangalia kwa macho mabaya.
“Unaongea ujinga gani? Ninachokuonyesha ni kwamba watu wangu pia wananisaidia . Nitapigana na wewe kwa uwezo wangu wote kujiheshimisha na kuheshimisha watu wangu”
Gonzalez asingekubali kama yeye ndio alieruhusu Regina kutekwa. Vinginevyo hata kama akishinda asingepata ujasiri wa kukalia kiti cha Ugwiji.
Lakini watu waliokuwa ndani ya eneo hilo walikuwa wakiangalia kila tukio kwa uelewa wa hali ya juu sana na baada ya kumuona Hamza mwonekano wake ukibadilika walihisi kabisa kuna kitu hakipo sawa.
Kuhusu Magwiji licha ya eneo hilo kuwa na mekelele mengi lakini walikuwa na uwezo wa kumsikia Hamza na Gonzalez kwa urahisi kabisa.
“Gonzalez kamteka mke wa Lucifer? Huge unajua kuhusu hili swala na umekaa kimya”Aliongea Oleg.
“Hatutoi taarifa bila ya kupata kitu , hio ndio sheria yetu”Aliongea Huge akiwa na tabasamu.
“Oh! Kumbe Lucifer kaoa?” Silvia alionekana kushangaa.
Nyakasura aligeuza macho yake na kuangalia upande wa mashabiki na kweli alifanikiwa kumuona Regina.
“Ni kweli ni mke wake. Hili furushi la chuma ni lishenzi kweli”
“Mpaka hapa kama Gonzalez akishindwa hatoweza kuvumilia aibu”Aliongea Mika.
“Kama ni hivyo , sitokuja kumchokoza Lucifer”Aliongea Sebastiani.
“Wewe Popo Mzee , si Madhabahu yenu ya giza ina ushirikiano na watu wa kuzimu. Kwanini usisaidie kumuokoa mke wa Lucifer?”Aliuliza Oleg.
“Ingawa ni kweli sisi ni marafikii , lakini sio kihiivyo. Halafu huu mchezo ni kati ya watu wawili , tukiingilia haitokuwa vizuri. Mkumbuke hata kama mbinu ya kuteka ni ya kishenzi lakini ni sehemu ya mbinu za kivita.Magwiji pia wana udhaifu la sivyo kungekuwepo na magwiji wengi ambao wapo hai” Aliongea Sebastiani na kisha akaendelea
“Jamani eh! Nimehudhuria mabaraza mengi ya maksi tokea kuanzishwa kwake na nimeshuhudia marafiki zangu wengi wakipoteza maisha hapa hapa . Ni matumaini yangu nitaendelea kuwaona katika mikutano ijao”Aliongea Sebastiani.
Sebastiani ndio Gwiji wa muda mrefu sana , ambae pia amehudhuria vikao vingi vya baraza la maksi. Hakuna mtu wa kupinga maneno yake kwa namna alivyoyaweka.
Uwanja wa vita ni kupigana kufa na kupona na kwasababu hio mbinu nyingi zinatumika na hakuna sheria rasmi ya kimbinu, iwe ni kuteka au mbinu nyingine jambo la kwanza ni kushinda mengine yanavumilika.Hivyo ilikuwa juu ya Hamza kuweza kulimaliza swala hilo bila ya msaada wowote.
Mara baada ya kauli ya Sebastiani, magwiji wengine wote walikaa kimya wakiwa hawana nia kabisa ya kutoa msaada na walimwangalia Hamza kwa shauku ya kutaka kujua ni jambo gani ataenda kufanya kumdhibiti Gonzalez na pia kumuokoa mke wake.
Chini ya steji Azle na wengine waliweza kusikia maneno ya Hamza na walijikuta wakipandwa na hasira mno.
“Damn it! Metal Tide ni kundi la wanahatamu , wanathubutu vipi kumteka shemeji yetu?”
“Nilikosea . Nilipaswa kumuwekewa ulinzi shemeji tokea mwanzo”Aliongea Asmuntis akijilaumu.
“Bosi wetu aliwachukulia wanawake kama chombo cha sterehe tu . Ila sasa hivi tuna shemeji hakuna mwenye uzoefu kati yetu.. tulikosea kimahesabu”Aliongea Leviathani.
“Kwahio tunafanyaje sasa? Usiniambie bosi atakubali kushindwa hili pambano kwa sababu hii?”
“Hebu acha kuongea ujinga na fikiria namna ya kumuokoa shem kwanza”Aliongea Mameni.
“Mimi naweza kufanya nini sasa kama sio kunionea tu” Berly alijikuta akilalamika.
“Master unaonaje nikienda mimi kumsaidia”
“Haiwezekani. Anaemlinda pale ni Helena, kwa uwezo wake kabla hujamfikia tayari atakuwa ashamuua. Hatupaswi kukurupuka katika hili vinginevyo hatutofanikisha lolote”Aliongea Asmuntis.
“Kwahio tutafanyaje sasa.. Bro sidhani kama ..” Black Fog alitamani kulia, akiogopa Hamza anaweza kupatwa na tatizo kwasababu hio.
Muda huo kwenye steji , Gonzalez aliweza kumuona Hamza akisita kumshambulia tena na alihisi uhakika wa kujipanga upya , hivyo palepale alisimama kwa kuchechemea na kutema damu.
“Lucifer , kwasababu kwa nia ya dhati kabisa unataka kuona uwezo wangu wote basi sina haja ya kuwa mpole tena. Nina kwenda kukuonyesha leo hii kwanini naitwa Goliathi”
Mara baada ya kuongea hivyo , Gonzalez palepale alichanua mikono yake juu huku akivuta pumzi nyingi na kupumua. Mara baada ya pumzi chache alibweka kwa sauti kubwa.
Sasuti yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba iliziumiza ngoma za masikio za watu waliokuwa ndani ya eneo hilo na kutengeneza mwangwi. Muda ule kupitia sauti yake tu eneo hilo lilianza kutingishika kama vile tetemeko la ardhi linatokea.
“Clang , clank!”
Steji ile ilianza kuporomoka na kufanya mpaka Magwji kusimama wakishangazwa na kile kinachoonekana mbele yao.
“Nini kinaendelea , kwaninii steji imeharibika ghafla?”Watu walijiuliza kwa msahngao.
“Ni Gonzalez ana meng’enya chuma na kufanya elementi za madini mengine kushindwa kuhimili uzito ndio maana steji imedondoka”Aliongea mmoja wapo na kufanya watu kuelewa kinachoendelea.
Upande wa Gonzalez ni kama alikuwa akipandiwa na wadudu ambao wanajigandisha katika mwili wake kwa spidi ya hali ya juu mno.
Eneo la tumbo lake palipokuwa pamebonyea palianza kuvamiwa na madini ya chuma kwa kasi kubwa na kuanza kupona. Ndani ya sekunde chache tu aliweza kurudi katika hali yake ya kawaida kabisa.
Haikuwa kupona tu bali gamba la chuma liliongezeka upana wake tabaka baada ya tabaka na kufanya mwili wake kuwa mkubwa na wenye nguvu zaidi.
Mara baada ya kumeng’enya karibia madini yote ya chuma yaliotengenezea steji , kilichobakia ni baadhi ya madini mengine dhaifu tu na kufanya jukwaa na Skrini kudondoka chini. Gonzalez hakumeng’enya madini katika juktwaa la magwiji kwa kuhofia kuwakasirisha.
Lakini hata hivyo chuma alichoweza kusharabu kilitosha kabisa kufanya mwili wake kuwa mgumu mno na mkubwa.
Mwanzo mwisho Hamza alikuwa akiangalia tukio hilo bila kufanya chochote , akiwa amesimama mbali na Gonzalez , hukua akimwangalia na macho yaliojaa ukauzu.
Licha ya Gonzalez kuendeleza kunyonya chuma Hamza hakuwa na nia ya kumzuia kabisa.
Magwiji pia walijikuta wakishangaa baada ya kuona jitu likiwa limesimama chini.
“Tsk tsk , huyu Gonzalez anaonekana kuwa na vimbinu vyake pia. Hilo gamba lake si mchezo”Aliongea Oleg.
“Kama ataweza kuhimili uzito wa mwili wake na kuwa na spidi ileile , basi nitakubali uwezo wake sio wa kawaida”Aliongea Mikaeli.
“Uwezo huo anao , vinginevyo asingeendelea kunyonya chuma na kuwa mkubwa zaidi”Aliongea Huge na aliungwa mkono na wengine.
“Kwahio kuwa vile ndio nini! Kama ni mimi ningemuunguza na kumgeuza kifusi cha urojo”Aliongea Nyakasura kwa kajeli.
“Kipenzi wewe pekee ndio unaeweza kumuunguza , wengine wote hatuwezi”Aliongea Silvia akicheka.
“Sijui Lucifer anapanga kufanya nini , ila anaonekana kutokuwa na wasiwasi”Aliongea Sebastiani.
Muda huo kimya kilitawala , hata wale waliokuwa wakimshangilia Hamza walikaa kimya wakiangalia kwa shauku kile kinachokwenda kutokea. Kila mtu alikuwa na hofu kutokana na mabadiliko aliokuwa nayo Gonzalez.
“Kweli hili ni jitu chuma , lakini atawezaje kupigana na mwili wote huo?”
“Namuona kama kifaru tu! Kwa haraka haraka uzito wa mwili wake ni tani kadhaa pale”
“Mimi kwangu naona Lucifer ana hali ngumu , kwa mwili ule hata umlipue na bomu ni kama kumtekenya tu”
Watu waliendelea kujadili na wasimamaizi wa Baraza la maksi walijikuta wakiwa katika hali ya wasiwasi , maana hawakutegemea hali ingefikia hatua hio. Angalau walipata ahueni mara baada ya Gonzalez kuacha kunyonya chuma zaidi.
“Lucifer sasa nipo katika nishati zangu zote za mwili , huu ndio muda wa pambano la uhakika sasa. Awamu hii nakuruhusu uanze kushambulia hahahaha..”
Gonzalez alicheka kama kichaa huku akipiga hatua moja mbele na kufanya Venue yote kutikisika.
“Huyu jamaa sio wa kawaida , kwa ukubwa wa miguu yake na mikono nani anaweza kuhimili uzito wa ngumi yake?”Aliongea Berly
“Bosi hana nishati za mbingu na ardhi ila Gonzalez ana ulinzi mkubwa wa mwili wake. Sio rahisi kudili nae”
“Bosi! Usimdharau huyo”Aliongea Mameni kwa sauti ya juu.
Watu wote wa upande wa Hamza hisia zao zilikuwa juu mno. Mkandamizo wa Gonzalez ulikuwa umefikia habari nyingine.
Wanajeshi wa kundi la Metal Tide walirudiwa na hali ya furaha na kuanza kumshangilia bosi wao.
“Lucifer bado tu unashangaa , hutaki kushambulia? Usipo anza nitakukanyaga na kukugeuza chapati”
Hamza aliishia kutoa pumzi nyingi , huku akigeuza sura yake na kumwangalia Regina.
“Nadhani utakuwa hujui ni mtu gani unamjaribu?”Aliongea Hamza kwa sauti yenye kitetemeshi.
“Oh!”
Gonzalez aliishia kuchezesha mboni za macho yake huku akihisi kuna kitu hakipo sawa.
Muda huo huo ghaflt tu mwili wa Hamza ni kama unachemka na kufanya utoe msisimko ambao hakuna aliewahi kuuhisia.
Ni kama vile muda wowote dhoruba kubwa itatokea na kuwafunika watu wote waliokuwa katika eneo hilo.
Muda ule Hamza mwili wake ulionekana kutawaliwa na kivuli kikubwa na kumfanya aonekane kama jitu, haikuwa hivyo tu misuli ya mwili wake ni kama ilikuwa ikituna na kusinyaa kama moyo.
“Nini kile!!” Mikaeli alijikuta akibung’aa.
Magwiji wengine pia walijikuta wakishindwa kuelewa , mabadiliko yale ya Hamza hususani kivuli cheusi kilichozingira mwili wake na kufanana nae.
Ilikuwa ni Nyakasura pekee ambae hakuonekana kushangaa , na hio yote ni kutokana na kuonja uwezo huo wa Hamza wa ajabu.
“Mwili wake ni kama umetawaliwa na mnyama mkali .. hapana ni kama kivuli cha jini” Sebastiani alijikuta akichanganyikiwa.
“Incredible!” Auland aliishia kuongea kauli hio huku akilinganisha uwezo wa Hamza na Gonzalez na kutoa mchanganuo wake.
“Inaonekana kupotea kwa Lucifer kwa zaidi ya miaka mitano , amerudi na mbinu mpya..”Aliongea Oleg huku akicheka.
Hata kwa Mchawi mkuu Skeletoni , ambae hakuongea neno tokea afike hapo alijikuta akishangazwa na kiwingu cha umbo la mtu kilichomzingira Hamza.
Kama magwiji tu walikuwa katika mshangao , haikuwa hata na haja ya kuelezea kuhusu watu wengine waliokuwa wakiangalia.
Watu wa upande wa Hamza walijikuta wakiwa katika bumbuwazi , hakuna aliethubutu kupepesa macho wakiogopa watakosa maelezo muhimu.
“Mmeona kile kivuli cheusi .. ni kama vile kimemfanya kuwa na nguvu zaidi”
“Achana na kivuli , mwili wake haujaongezeka sana” Watu walijikuta wakipagawa.
Upande wa Hamza palepale alitoa kilio kama vile amepandwa na wazimu na ni kauli moja tu iliosikika.
“Mgawanyiko!”
Hamza aliacha kusita, mbinu mgawanyiko mwanzoni ilikuwa ikimletea shida na kumfanya ajione ni kama yupo katika ile ndoto , lakini mara baada ya kuibobea wakati akipambana na Nyakasura hakuogopa tena kuitumia. Ikumbukwe mbinu hii ni ileile ambayo haikukamilika alioipata kutoka kwa Yonesi na alivyoanza kujifunza aliona sura ya mwanamke aliekuwa akimuota ndotoni , mwanamke mchawi.
Gonzalez aliweza kuhisi miguu yake ni kama inamtetemeka , licha ya kuwa na mwili chuma lakini msisimko ambao alikuwa akiusikia ulitawala kila pande ya mwili wake na kuanza kuhisi kuwa mdhaifu na kushindwa kutawala gamba la chuma nje ya mwili wake.
Alipanga kumuacha Hamza afanye shambulizi kwanza , lakini muda huo hakujali tena kwa hofu ya kuona jambo ambalo halikutabiliwa lingemtokea.
Gonzalez palepale alijikuta akipiga makelele mengi na kumsogelea Hamza huku akiinua mkono wake mzito wa chuma akielekezea ngumi kumlenga Hamza.
Angle aliotumia ililenga kutumia muunganiko wa mwili wake wote ili iwe na nguvu ya kusambaratisha. Watu waliokuwa wakiangalia mara baada ya kuona shambulizi lile la ngumi waliona ilikuwa na uzito mara nyingi zaidi kuliko ile ya mwanzo.
Mpaka hatua hio ilikuwa ngumu kwa watu kutabiri nani anakwenda kushinda katika hilo pambano , lakini sasa ile kila mtu akiwa amekakamaa mwili wakijua Hamza anakwenda kujeruhiwa vibaya , Hamza alikuwa ni kama radi , kwani palepale alikanyaga chini kwa nguvu huku akiwa amekunja ngumi yake na kumsogelea Gonzalez na kwenda kugonganisha nayo mkono kwa mkono , ngumi kwa ngumi na kufanya watu washindwe kuona kinachoendelea kutokana na Hamza kuzibiwa na mwili wa Gonzalez lakini vilevile vumbi la hatua za Gonzalez.
Boss!!
Watu wa upande wa Hamza walijikuta wakiita kwa sauti kubwa huku wakiwa wameshikisha vidole vya mikono yao kwa nguvu kutokana na wasiwasi.
Ilikuwa ni muda mchache sana wa shambulizi hilo lakini kutokana na wasiwisi ni kama ilikuwa ni mwaka. Ila sasa ile wakiwa na wasiwasi na kupiga makelele ghafla tu Gonzalez aliekuwa akionekana kutawala alitoa ukulele mkubwa.
Mkono wa Gonzalez ulionekana kusinyaa na kuwa mdogo huku matabaka ya ngozi ya chuma yakiachia kama magamba ya mti.
Clang ! Clang! Clang!”
Hamza alionekana kusukumiza ngumi yake katika mkono wa Gonzalez akiwa hajarudishwa nyuma hata kwa inchi moja na alikuwa akisambaza nguvu ya uharibifu na kufanya kile kivuli cha ajabu kilichomzingira kuzingira mkono wake.
Gonzalez alionekana kukosa mhimili na kufanya mwili wake kunesa nesa ukionekana unataka kudondoka huku upande wa Hamza alionekana kutopoa.
“Clank!”
Kishindo kizito kilisisikika na hio ni mara baada ya Gonzalez kupoteza balansi na kudondoka chini kama furushi la chuma.
“Haaaaa!!!”
Jambo lile lilifanya watu kutoa ukulele wa juu mno wakionekana kupagawa na kutoamini.
Comments