Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

 

Ilikuwa imepita miaka mitano tangu familia ya Mr Jonson Malisaba iweze kuuawa na watu wawili wasio julikana na mtoto mmoja ambaye ni Lenovatus Jonson kuweza kuokolewa na mtu asiye julikana na kutokomea nae gizani usiku wa siku ile. Ndani ya ardhi ya matajiri wa chakula nchini ni katika jiji la Mbeya pembezoni kabisa mwa nchi katika wilaya ya Kyela inayo patikana kusini magharibi mwa nyanda za juu kusini mwa Tanzania. Ni wilaya ambayo utafanya makosa makubwa sana bila kusifia ukarimu mkubwa wa watu wake Wanyakyusa, ni watu wakarimu sana walio bahatika kuwa na utajiri mkubwa wa chakula kikitawaliwa na kilimo cha mpunga na kokoa ambazo zinawaingizia kipato kikubwa sana kwa watu wa hii wilaya.

Mida ya saa tano za usiku walionekana watu wawili wakiwa na mtumbwi wao wakionekana kabisa ni wavuvi wazoefu ndani ya hilo eneo, waliamua kurudi mapema sana baada ya kuona hali ya hewa imebadilika ghafla sana mvua zimeanza kunyesha, kuendelea kuwepo ndani ya ziwa hili kubwa lijulikanalo kama ziwa nyasa ingekuwa ni hatari kwao. Walifanikiwa kufika nje ya maji hayo wakiwa wamelowa miili yao yote, ni mzee mmoja wa mwenye takribani umri wa miaka 48 akiwa na kijana aliye onekana kuwa na umri wa miaka 21 hivi kwa mwonakeno wake. Walikuwa ni wavuvi wazoefu wa hili eneo la Matema Beach Kyela ndani ya hili ziwa licha ya kurudi mapema walifanikiwa kupata kitoweo cha siku ya kesho siku yao haikuwa mbaya sana. Walikuwa wakiishi pembezoni kabisa mwa safu za mlima Livingstone. Baada ya kukusanya mizigo yao walianza kuondoka taratibu kuelekea kwenye kijumba chao kidogo cha nyasi ambacho kilitengenezwa kwa miti na udongo pembeni ya jiwe moja chini kabisa ya safu za mlima huo, kabla ya kufika nyumbani kwao hapo waliifuata njia ya mlimani mvua ikiendelea kunyesha kwa nguvu hata hawakuijali kabisa.

 

Kuna mahali walifika walikimbia kwa spidi sana mpaka karibia na kileleni mwa mlima walikunja njia ya kushoto mita kumi kutoka hapo kuna sehemu katikati ya mawe mawili kulikuwa na sehemu nzuri yenye uwanja mdogo ulio onekana kuwa ni uwanja ulio tengenezwa kwa ajili ya mazoezi japokuwa haikueleweka mjenzi wa huo uwanja wa mazoezi ni nani sehemu kama hii tena ikionekana kuwa ni kwa usiri mkubwa. Hakuna aliyekuwa ameongea neno lolote tangu watoke ziwani kwa sababu kila mtu aliujua wajibu wake kwa usahihi, kila mtu alirusha kikapu chake cha samaki juu ya mti kwa kasi ya kutisha zilipita dakika kumi kukiwa kuna ngumi kali za mauaji zinapigwa miongoni mwa hao watu wawili ambao walikuwa hawaongei chochote kile. Kijana wa miaka takribani 21 alionekana kuwa hatari baada ya kuanza kumuelemea mzee mzima wa takribani miaka 48 na kuendelea, aliacha baada ya kuona ngumi ilikuwa inaenda kumpiga huyo mzee kwenye maeneo ya kichwani alibaki amesimama tu ghafla bila taarifa yoyote.

 

"Huo ujinga ndio utakao kufanya uje kufa kipumbavu sana nilisha kuambia ukiwa kwenye uwanja wa vita haitakiwi ujiulize mara mbili kumvamia adui ukimpa nafasi ya kizembe namna hii anakuua ilitakiwa hiyo ngumi uifikishe kwanza ndipo mengine yangefuata" alifoka kwa jazba huyu mzee akiwa anamwangalia kijana wake aliyekuwa mbele yake.

 

"Bora nife siwezi kumpiga baba yangu mzazi ngumi ya hatari hii ambayo inaweza kumletea matatizo kichwani siwezi utanisamehe kwa hilo" huyu kijana ambaye bado hakufahamika jina lake alikuwa nani aliongea akionyesha anamaanisha alichokuwa anakisema, mzee alitabasamu sana kuona thamani anayopewa na huyo kijana ilikuwa ni kubwa kuliko hata alivyokuwa akifikiria.

 

"Kitanda hakizai haramu, na kondoo hawezi kuzaa chui hata siku moja nakupenda mwanangu najivunia sana kuwa baba yako kwenye hii dunia" mzee aliongea akicheka kwa nguvu na kwenda kumkumbatia huyo kijana kwa furaha kubwa meno yote yakiwa nje kama mzazi ilimpa amani ya moyo kuona kijana wake anamthamini kiasi hicho.

 

"Lakini baba kuna kitu mimi huwa sikielewi kwanini tunafanya sana mazoezi kiasi hiki na unanihimiza kila siku ikiwa ni mwaka wa nne sasa nafanya haya mazoezi ya hatari ambayo yanaweza kuchukua hata uhai wangu? Ni kipi kinakufanya mtu mwenye nguvu kama wewe uliamua kuja kuishi huku wakati ulinambia mama alikufa mimi nikiwa bado mdogo sana maeneo ya Dar es salaam huko japo sikujui ila nadhani kwa nguvu na uwezo wako ungekuwa mtu tajiri sana huko mjini kuna nini kinaendelea na hatima ya kunifundisha mazoezi makali sana namna hii kwa miaka hii minne ni ipi?" Kijana alikaa nalo moyoni kwa takribani miaka minne lakini leo aliamua amuulize baba yake swali ambalo lilionekana kumshtua sana mzee huyu hakulitegemea kwa muda kama huo ilikuwa ni ghafla sana, miaka minne ndio muda ambao huyo kijana alikuwa anaukumbuka kwa usahihi kuwepo kwenye hilo eneo mengine hakuonekana kuyakumbuka vizuri hivyo alihitaji jibu la sababu ha msingi ya mzee hatari mwenye nguvu kama baba yake kuja kuishi maisha ya kubangaiza huku wakiishia kuwa wavuvi na kilimo kidogo cha mpunga kilicho wapa chakula cha kujikimu wao wenyewe wawili tu wakati kwa uwezo wa huyo mzee alikuwa na uwezo wa kwenda sehemu yoyote ile akatengeneza pesa nyingi sana. Huyu mzee alitulia kwa umakini kama dakika mbili akiwaza amjibu nini mwanae ili asije akaharibu maada hapo kwani alimpenda sana huyo mtoto hakuwa na ndugu yeyote zaidi ya huyo mtoto, ndiye aliyekuwa rafiki yake mkubwa kila muda walikuwa wote wakipambana na maisha ya mji wa watu wastaarabu huo pamoja lakini hakuwahi kuruhusu yeye wala mtoto wake kuwa na rafiki wa aina yoyote ile ndani ya hilo eneo na hakutaka mtu yeyote awajue kivyovyote vile kwa sababu za msingi alizokuwa nazo yeye mwenyewe.

 

"Mwanangu haya maisha kuna muda furaha ni kitu cha msingi sana kuliko hata pesa wala maisha mazuri ambayo wewe unayataja hayo, pesa ni nzuri sana unavyo simuliwa na pale unapokuwa nayo ukiwa mwenye furaha ila pesa ni kitu cha hatari sana ukitumia njia za hovyo kuipata, haya sio maisha yako mwanangu na pengine haustahili kuishi sehemu kama hii, unisamehe tu baba yako ipo siku utajijua kiundani zaidi wewe ni nani hasa kuna sababu za msingi sana mpaka wewe ukaitwa Jamal" kwa mara ya kwanza alilitaja jina la mtoto wake aliye fahamika kama Jamal wakati anamjibu kwa utulivu mkubwa sana swali lake wakati huo mvua ziliendelea kuongezeka lakini hawakuzijali pamoja na radi zilizokuwa zinapiga.

 

"Baba mbona sijakuelewa umesema nikijijua? kwahiyo sijijui au unamaanisha mimi ni nani?" Jamal alishangazwa kidogo na maelezo ya baba yake alihisi huenda ameelewa tofauti na mzee huyo alivyokuwa amemuelekeza.

 

"Muda ni dakitari mzuri sana kwenye maisha mwanangu, muda huwa unaamua ni nani ni mtu sahihi kwenye maisha ya mwanadamu, muda huwa unatibu matatizo mbali mbali yanayo wafanya watu wanalia kila siku lakini pia muda huwa unakuja kutengenisha uhalisia na kitu kilichopo ndani ya giza(akaguna). Hakikisha unakitunza hiki kidani kama ambavyo huwa unayalinda macho yako pale yanapokuwa yanavamiwa na kitu chochote kama jiwe na vingine, hiki kidani usije ukathubutu kumpa mtu yeyote yule hata kama siku ikitokea mimi sipo, hiki kidani kina majibu sahihi ambayo yataamuliwa na muda, zingatia sana haya maneno hiki kidani hapaswi kukigusa mwanadamu mwingine yeyote kwa sasa zaidi ya wewe pekeyako hata ungekuwa umeoa mkeo na watoto wasingeruhusiwa kukigusa hicho kimeshikilia maisha ya watu wa nchi hii" maneno mazito ya mzee huyu akiwa anamwambia mwanae huyo Jamal huku akiyatoa kwa uchungu mkubwa sana akiwa anamvalisha kijana wake kidani ambacho hakuwahi kukiona hata siku moja ikionekana wazi anayaongea kwa maumivu makali na ndani ya moyo wake alionekana wazi kuwa na siri moja nzito sana ambayo ilikuwa ni siri ya kifua chake hakuhitaji mtu yeyote aijue zaidi ya yeye pekeyake.

Aliogopa Sana Jamal kukabidhiwa kitu ambacho kilisemekana kimeshikilia maisha ya wananchi karibia wote wa nchi hii ilimuogopesha mno alibaki anajiuliza maswali mengi bila kuyapatia majibu yake kwamba yeye ni nani hasa mpaka aweze kupewa kitu chenye thamani namna hiyo ila hakuyatilia maanani maneno ya baba yake kwani hicho kidani chenyewe kilikuwa cha kawaida tu tena cha zamani halikuwa na mvuto wowote kusema kwamba kitaweza kumfanya mtu avutiwe nacho, alitaka kuuliza kitu ila kichwa chake kilianza kumuuma ghafla na hii ilikuwa ni hali ya kawaida kwa takribani miaka minne sasa kila akiwa na mawazo au akionekana anataka kukumbuka baadhi ya mambo kichwa huwa kinaanza kumuua kama dakika mbili hivi ndipo anakuwa sawa. 

 

"Acha kukiumiza kichwa chako mwanangu nakwambia kila siku muda utafika kichwa chako kitakuwa sawa, jiandae kesho asububi sana tunaondoka hii sehemu tunarudi Dar es salaam" maneno ya baba yake yalimpa maswali mengi ila yalimfurahisha mno, alikuw na hamu sana ya kufika ndani ya hili jiji ambalo alikuwa akisimuliwa na baba yake kwamba maisha yake ndiko yaliko anzia huku alihitaji kufika ili aone kama huenda wana ndugu wengine huku alichoka kukaa mwenyewe na baba yake pekee, alichukua kikapu chake cha samaki akiwa na kidani chake shingoni akaanza kumfuata baba yake nyuma kwa furaha kubwa baada ya kuambiwa asubuhi walikuwa wanawahi Dar es salaam kwa wazaramo japokuwa hakuelewa nauli wanatolea wapi kwa maisha waliyokuwa wanaishi yalikuwa ya kawaida sana hakuwa na imani kama baba yake atakuwa na nauli ila aliweza kumuamini baba yake hakuwahi kumdangaya.

 

Walifika kwenye kijumba chao hicho cha nyasi ambacho ndani kilikuwa na kitanda pamoja na vyombo vichache vya kupikia vilivyo onekana kutumika kwa muda mrefu kidogo, baba yake alipika ugali wakala kisha wakaenda kulala, kabla ya kufanya hivyo alishangaa kumuona baba yake ananyanyua upande mmoja wa kitanda hicho akakitoa kisu chake na kuchimba chini kidogo alitoa pesa mabunda matano yaliyo jaa pesa nyingi zikiwa ni pesa za kitanzania, dola za kimarekani pamoja na simu ndogo.

 

"Baba hizi pesa umezitoa wapi na umezihifadhi kwa muda gani pesa zote hizo?" Alikuwa na mshangao Jamal pesa zilikuwa mabunda matano yaliyo jaa vyema zilifungwa kwenye rubber band zikionekana hazikuguswa kabisa tangu siku wanazitoa Bank.

 

"Hahahaha hizi ni pesa zetu mwanangu usijali nimechoka saivi acha nipumzike tutaongea kesho tukiwa njiani"maelezo ya baba yake yakimtia wasi wasi sana hakuwahi kumuona mzee huyo akifanya kazi yoyote ile ya kumpatia ujira wowote zaidi ya uvuvi wa samaki wa chakula na kilimo cha mpunga kinacho wapatia chakula cha kujikimu alianza kuhisi huenda kuna mambo mengi sana hayajui kuhusu baba yake, alikigusa kidani chake kwa umakini akakiangalia kisha akalala.

 

Saa kumi kamili alfajiri ndio muda ambao Jamal aliamshwa na baba yake akiwa kwenye usingizi mzito.

"Hutaki kwenda Dar es salaam!" Baba yake alikuwa akimuuliza mtoto wake kwa tabasamu huku akimrushia mtoto wake suti moja ya bei kali sana, kwa mwanga mdogo wa kibatari kilichokuwa humo ndani kilimfanya Jamal azione nguo hizo kwa umakini, tangu aanze kujitambua hakuwahi kuvaa nguo za bei hata siku moja, alikuwa na maswali mengi juu ya huyu mzee wake lakini akaamua kukaa kimya akisubiri muda mwafaka wa kumuuliza ufike, hawakuhitaji mtu yeyote ajue kama walikuwa wanaondoka walizima kibatari chao na kubeba kila kilichokuwa cha mhimu wakakifunga kibanda chao hicho kwa nje.

 

"Huenda miaka niliyo kaa hapa ikawa ndiyo miaka yangu bora zaidi kuwahi kuiishi kwenye uhai wangu" Baba yake Jamal alitamka haya maneno akiwa amesimama anatazama vilele vya safu za mlima Livingstone, Jamal aliishia kutabasamu tu kisha wakaondoka hiyo sehemu wakianza harakati za kuweza kusafiri mpaka ndani ya jiji la Dar es salaam.

 

Jamal ni nani, huyu baba yake ni nani? Huko Dar es salaam wanaenda kutafuta nini?

 

Sehemu ya pili ya hadithi hii inafika mwisho huenda sehemu inayofuata ikatupatia majibu zaidi.

 

Bux the story teller.

Previoua Next