Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

 

Jamal hakuhitaji maswali mengi kwa hao watu akijua wazi wapo hapo kwa ajili ya kumchukua na hakuwa tayari kuweza kuruhusu hiyo hali iweze kutokea hakutaka kuishi mbali na baba yake ni kitu alicho jiwekea ahadi tangu siku ya Kwanza kuweza kujitambua akiwa ndani ya Kyela. Baada ya kuwafikia wale wananaume wanne aliwapita juu kwa sarakasi moja maridadi sana akatua nyuma yao mmoja alipokea teke la mgongo lililo mzoa mpaka kwenye ukuta wa nyumba moja iliyokuwa jirani na hapo, ni kama bahati hiyo nyumba ilikuwa imejengwa kwa tofali za simenti vinginevyo ingeweza kubomoka hata hivyo huyo mwanaume alijinyanyua na kujifuta vumbi lililokuwa limeshika kwenye nguo zake baada ya yeye kudondoka pale chini.

 

"Bwana mdogo ebu acha hiki unachotaka kukifanya ni hatari mno kwa mtoto mdogo kama wewe ebu ongozana nasisi upande kwenye gari tuweze kuondoka hili eneo kwa amani tu bila kuumizana, wewe ni kama mdogo wangu usinilazimishe kufanya kitu kibaya kwenye mwili wako huo" umbo la Jamal nadhani lilimdanganya sana kiongozi wa hawa wanaume, hakuwa mdogo sana mwili wake ulikuwa umepasuka na kuvimba kwa mazoezi magumu ya mlimani hata hivyo umbo lake alionekana bado ni mdogo sana alikuwa na miaka 21 tu pekee.

 

"Sawa kama ni rahisi sana namna hiyo niko hapa njoo unichukue" Jamal hakuwa mtu wa kuongea ongea sana hasa kwa mtu ambaye hakumjua kabisa kwenye maisha yake, kauli yake ilimfanya yule mwanaume aliyedondokea ukutani kuja kwa hasira akitaka kulipiza, mkono wake ulikamatwa kwa nguvu alipigwa na buti maeneo ya sehemu za siri mpaka wenzake walianza kumcheka namna alivyotia huruma kwa kupigwa na mtoto mdogo namna hiyo. Walijikusanya wote wanne ili wamkamate kiurahisi ila ilikuwa ni tofauti sana na walivyokuwa wakimdhania alicho kuwa anakifaya hapo wote kiliwashangaza, alionekana kuwa sio wa kawaida hata kidogo miaka minne aliyoweza kuishi ndani ya safu za mlima Livingstone na baba yake alikuwa ameivishwa vya kutosha mifupa yake ikiwa mikavu bila maji ilikomaa sana.

 

Hiyo sehemu ilichafuka kwa mapigano makali ya hao watu wanne dhidi ya kijana mdogo mmoja tu, hakuna mwananchi yeyote wa Buguruni aliyetamani kukatiza kwenye hayo maeneo licha ya maeneo hayo kusifika kuwa na wahuni wengi wa kutosha, wote walikuwa wamejifungia ndani wengine waliokuwa karibu zaidi wakiifunga vyema milango ya nyumba zao wasije kuyakatisha maisha yao ambayo yanasemekana kuwa mafupi mno kwa mwanadamu wa kawaida. Dakika kumi za vita vikali ziliisha baada ya Jamal kuchomwa sindano ya usingizi shingoni iliyo mlevya na kulala usingizi mzito. Walifanikiwa kumpata lakini wanaume hao walikuwa wapo hoi kwa kipigo wakichokuwa wamepewa na kijana Jamal hakikuwa cha kawaida hata kidogo. Walimbeba haraka haraka na kumpakiza kwenye gari lao lililokuwa lipo karibu na hapo huku wakichechemea, waliondoka hayo maeneo na kupotelea kusiko julikana.

 

Wakati matukio yote hayo yanafanyika Daud Hauston baba yake na Jamal alikuwa amesimama juu ya daraja lililopo katikati ya bara bara kubwa ifahamikayo kama Mandela Road, alikuwa juu kabisa majira hayo ya saa mbili akiwa anashuhudia kila kilichokuwa kinaendelea, alivyo hakikisha wamefanikiwa kumkamata Jamal japokuwa waliteseka sana aliondoka hilo eneo kwa kuruka kutoka juu ya daraja hilo dogo ambalo watu wengi huwa wanalitumia kupumzika usiku hasa kupata upepo kupunguza adha ya joto ambalo linapatikana kwenye hili jiji, watu walimshangaa mzee huyo kwani juu mpaka chini palikuwa ni mbali sana halafu ni kati kati ya barabara muda wote magari yalikuwa yanapita ilikuwa ni hatari kufanya hicho kitu hivyo hawakuelewa kwanini asitumie njia za kawaida tu kushuka, hakuwajali kabisa aliingia vichochoroni na kupotelea mahali pasipo julikana kabisa.

 

"Niache naondoka mimi, mwanaume gani huwezi kumsikiliza mkeo kila siku unaiamini halmashauri ya kichwa chako tu kwa sababu unajua nakupenda sana ndo unapata kiburi eeh, ndio Kwanza nina mtoto mmoja tu basi unataka nife nikiwa bado mdogo hivi hapana baba Precious mimi siwezi naenda kwetu maisha gani haya" ni ndani ya mitaa hiyo hiyo ya Buguruni mtu na mkewe walikuwa kwenye ugomvi mzito sana ulio onekana kusababishwa na mume mtu kuwa na kichwa kigumu sana kwenye kuchanganua mambo.

 

"Mke wangu nilikwambia mapema hili nitalifanyia kazi mapema tu nadhani wiki ijayo nitakuwa nimeshalimaliza mama Precious wangu nakupenda siwezi kuishi mwenyewe bila wewe mke wangu nadhani hilo unalijua vizuri kwahiyo usifanye hivyo" ni maneno ya mume mtu ambaye ni baba Precious akimbembeleza mkewe ambaye alikuwa ana miaka minne tu tangu amuoe alimpenda sana huyo mwanamke aliye mheshimisha baada ya kuimbwa sana mtaani kwamba hawezi kuzaa. Alikuwa ameyashikilia mabegi ya mkewe ili asiweze kufanya haya maamuzi mtoto akiwa zake kwenye kochi akicheza na mdoli wake asielewe kinacho endelea kwa wazazi wake.

 

"Kila siku matukio hayaishi hii mitaa mimi naogopa kuendelea kuishi huku nakwambia kila siku tuhame hutaki, ona watu wanapigania kwenye ukuta wa nyumba kabisa mpaka ndani nasikia vipi kama wangebomoa au wangeingia ndani si ningekufa mimi na mwanangu?" Mama Precious aliendelea kulalamika huku akimpiga piga mumewe, mapigano ya akina Jamal yalifanyika nyuma ya nyumba yake na hata yule mwanaume aliyepigwa na Jamal alidondokea kwenye huo ukuta hiyo ilimpelekea mwanamke huyu kuwa ma wasi wasi kubwa sana ya kuendelea kuishi ndani ya maeneo hayo akihofia uhai wake na mwanae, mumewe alimkumbatia kwa kumbembeleza akimpiga piga mgongoni basi yaliisha akamsamehe mmewe ambaye aliahidi kuhama baada ya wiki moja mbele.

 

Ile sindano aliyouwa amechomwa Jamal alikuja kuamka kesho yake majira ya saa sita za mchana akiwa kwenye chumba kikubwa na kizuri tofauti na maisha aliyokuwa ameyazoea yeye, alitaka kuuliza yuko wapi ila aliona atakuwa mjinga kwani humo ndani alikuwa yupo peke yake, alijivuta kwa uchovu mpaka lilipokuwa dirisha kubwa la kisasa lililuwa wazi pakiwa pametandazwa pazia kubwa lililo mfanya asiweze kuona nje, alilitoa pazia hilo alicho kiona nje kilimfanya arudi nyuma kama hatua mbili kwa uoga, nje walikuwa wanaonekana watu walio vaa kombati za jeshi wakiwa na silaha nzito wakizunguka zunguka karibu na hiyo nyumba kwa umakini sana, mara ya Kwanza alihisi atakuwa jela lakini aliwaza hata Kama hajawahi kwenda jela kwa jinsi ambavyo huwa anasimuliwa jela haiwezi kuwa nzuri namna hiyo, hata hivyo hilo wazo alilipinga kwa sababu kubwa mbili aende jela kwa kosa lipi alilolifanya? Pia alijua baba yake angekuwa amekuja kumtembelea hapo.

 

Ilimlazimu kurudi tena kitandani ili atulize akili kukumbuka yupo ni wapi, baada ya dakika moja usingizi ulikata kichwani akakumbuka matukio ya jana yake akagundua alikuwa ameshikwa na watu ambao walionekana kabisa kuwa na taarifa kutoka kwa baba yake, basi aliamua kusubiri kuona nini kinaenda kutokea humo ndani. Baada ya dakika kumi na tano kupita mlango wa hicho chumba aliingia mwanaume mmoja akiwa pekeyake bila presha yoyote mikono yake kaiweka nyuma, sura ilikuwa ni ngeni kabisa hakuwahi kumuona mtu kama huyo kwenye maisha yake yote, ila hakuwa anajua kama mtu mwenye sura kama hiyo alikuwa ni baba yake na alikuwa anaishi naye karibia kila siku tatizo la huyo mzee alikuwa anaishi na sura bandia ambayo haikuw yakwake lakini hicho kitu Jamal hakuwahi kukijua wala kukihisi hata siku moja.

 

"Utakuwa una maswali mengi sana kuhusu wewe kuwepo hapa, kwanini baba yako ameruhusu hili liweze kukutokea wewe hapo, unatakiwa ujue tu kwamba haya yanatokea kwa sababu anakuandalia maisha yako halisi ya baadae na namna ya kuweza kuukabili huu ulimwengu kwa siku chache zijazo mbeleni. Sitakuwa na jibu la swali lako lolote mimi nitafanya yale ambayo napaswa kuyafanya kwako basi, ila ujue tu kwamba hapa mbele yako aliye simama ni mkuu wa majeshi ya nchi ya Tanzania" maelezo ya mwanzo yote yalimzalishia maswali mengi sana ndani ya kichwa chake Jamal ila hili la mwisho lilimtisha kiasi kwamba akaanza kutetemeka alielewa mkuu wa jeshi ni mtu mkubwa ndani ya nchi hivyo alikuwa na wasi wasi mkubwa kusikia hayo maneno hakuelewa yeye na mkuu wa majeshi wanahusiana vipi mpaka aweze kuletwa mbele ya huyo mwanaume. Jamal hakupewa nafasi ya kuongea tangu huyo mwanaume aweze kuingia humo ndani sasa ndo alipata wasaa wa kuufungua mdomo wake.

 

"Shikamoo mkuu" ilimlazimu kusalimia kwa ukakamavu baada ya kugundua yupo mbele ya mkubwa wa wanajeshi na makomando wote wa nchi, mkuu wa majeshi alitabasamu baada ya kugundua kwamba huyo kijana alikuwa mstaarabu sana kwa aina ya uongeaji wake ulivyokuwa.

 

"Unajijua kwa jina moja tu kama Jamal ila wewe unaitwa Jamal Hauston, hizo hapo ni passports zako na kadi ya benki namba ya siri ni 0101, ishike vizuri hiyo namba ya siri ina uhusiano mkubwa sana na maisha yako ya nyuma, kwenye hiyo account kuna bilioni kumi za kitanzania zitumie utakavyo kwa muda utakao upo mbali ila usisahau kuufunga mdomo wako kwa kila kitu unacho kijua kwenye maisha yako na usimwamini mtu yeyote yule popote pale utakapokuwa pia usije ukamueleza mtu kuhusu uwepo wa baba yako kama ikitokea hata viongozi wakubwa wanakuuliza waambie mimi sina wazazi ni yatima walishakufa miaka mingi sana huko nyuma hapa nipo kwa sababu ya kuiwakilisha bendera ya nchi yangu ya Tanzania". Maneno yalikuwa mazito sana kwa Jamal hakuelewa anawezaje kusema yeye ni yatima wakati baba yake ni mzima wa afya aliona anaenda kumkosea sana baba yake ila huenda hawa watu walikuwa na maana kubwa sana ambayo yeye hakuwa anaijua kabisa kwa sababu hakuonekana kujua kitu chochote kile, alilazimika kuuliza wakati huo mkuu wa majeshi alikuwa ameshaanza kuondoka akiwa amemuacha njiapanda sana.

 

"Samahani kwani natakiwa kwenda wapi?" Jamal alihisi kama wanamchanganya kichwa chake walikuwa wanamwambia vitu nusu nusu alikuwa haelewi.

 

"Ooooohps nilisahau, kwa sasa unaelekea Cuba, kule unaenda kama komando wa nchi ya Tanzania ambaye unaenda kuchukua mafunzo ya hali ya juu zaidi ya makomando wakubwa duniani, haukutakiwa kwenda huko kwa sababu haupo kwenye orodha ya wanajeshi wala hujawahi kuhudumu ndani ya jeshi la nchi, nimefanya hivi kwa heshima ya baba yako tu ambaye ni rafiki yangu wa muda mrefu. Kwa sasa wewe unaenda kuwa komando halisia kabisa wa nchi yako na hilo unatakiwa kuliweka kichwani unaenda kuilinda nchi yako kwa maisha yako yote haijalishi umeenda kwa bahati mbaya au kwa kupanga ukishaingia huko ni moja kwa moja unalazimika kuitumikia nchi yako. Popote unapokuwa zikumbuke rangi nne za bendera ya nchi yako Blue ikimaanisha maziwa, mito, bahari,na vyanzo vyote vya maji, Nyeusi ikiwa inawakilisha kwamba sisi ni Waafrika, Kijani inasimama kwa niaba ya uoto wa asili uliopo nchini na ya mwisho ni Njano hii inawakilisha utajiri wa madini tulio nao nchini mwetu. Haujui sheria za jeshi vizuri ila baba yako amekufanya umekuwa mwanaume imara hivyo tumia uzoefu na kufuata kanuni zote za mafunzo uwapo huko hautapata tatizo lolote ila kama kuna kitu utakuwa unakihitaji utaelekezwa sehemu ya kwenda ukiwa kule namimi nitakuwa napata taarifa,jiandae baada ya masaa mawili wanakuja kukuchukua na kukupeleka huko" mkuu wa majeshi baada ya kumalza maelezo yake alitoka humo ndani na kuufunga mlango, Jamal alikaa chini kabisa kwenye sakafu aliishiwa nguvu zote hakuwa anajua lolote kuhusu hicho kitu leo ghafla hivi anaambiwa anaenda kwenye mafunzo ya kikomando kuja kuilinda nchi yake pendwa ya Tanzania, aliona kama baba yake hajamfanyia wema kwa hilo alitakiwa amuulize Kwanza kama alikuwa yupo tayari kuifanya hiyo kazi, alifikiria sana ni kipi kilikuwa kinaendelea kwenye maisha yake ambacho yeye binafsi hakuwa na uelewa nacho?, Alianza kuhisi kwamba huenda yalikuwa yapo mambo mazito mno nyuma ya pazia ambayo alikuwa anatakiwa aweze kuyajua, kuna picha zilianza kujirudia rudia kwenye kichwa chake kumbu kumbu zilikuwa zinakuja na kupotea kichwa kilianza kumuua sana, alipiga makelele mazito humo ndani akiwa hapo sakafu, baada ya dakika tano alitulia na kulala hapo hapo chini ya sakafu.

 

Ukurasa wa 4 natia nanga, endelea kufuatilia kisa hiki chenye utulivu kabisa wa kukupatia madini ya ubongo.

 

Bux the story teller.

 

Previoua Next