Reader Settings

SEHEMU YA 210.

Mchawi wa wafu(Necromancer).

                                                                               

Muda ulionekana kusimama kwa muda , mara baada ya kusikia jibu lake . Regina macho yake yalioyaa maji  yalimwangalia Hamza kama vile alikuwa amepotelea katika mawazo.

Hategemea kabisa  jibu  la Hamza lingekuwa  la moja kwa moja na jepesi. jepesi kiasi kwamba alishindwa kuelewa  ni nini hasa mwanaume huyo anajaribu kumaanisha.

Mara baada ya dakika moja  yote, Hamza aliona mwanamke huyo hakushituka , hivyo aliishia kutoa tabasamu na kunyoosha mkono wake kumgusa  Regina usoni.

“Silly wife, unaota nini  mchana wote huu? Ingia kwenye gari”

Muda huo ni kama sasa Regina alishituka katika mawazo yake , na alipiga hatua moja kurudi nyuma huku akiongea  kwa sauti hafifu;

“Wewe ni mjinga , nilikuwa nikikudanganya lakini bado tu unaniamini”

“Wewe ndio unaejua kama unaigiza au  ni kweli , lakini kwangu mimi  sijali kabisa  kama wewe  ni halisi au feki. Napenda unavyoonekana na napenda unachokifanya , kila kinachohusiana na wewe nakipenda . Na kingine  kama utaendelea kuniigizia kwa maisha  yako yote  unadhani  unachokifanya kitaendelea kuwa maigizo?”

Regina kusikia hivyo alijikuta akishangaa , aliishia kumwangalia  mwanaume huyo mwenye uso wake mweupe  ulivyokuwa katika hali ya utulivu  na kuishia kuuliza kiwasiwasi.

“Unapanga kuishi na mimi maisha yako yote?”

“Ndio , nimekuoa maana yake nitaishi na wewe milele”Aliongea Hamza.

“Lakini nimekudanganya” Regina alishindwa kuelewa.

“Wife nadhani unashindwa kuelewa kitu kimoja , tokea  mwanzo sikujali kama ulikuwa ukidanganya kuhusu Helena . Kama ulipanga kumchukua  Helena kama mtu wako , hilo ni  juu yako. Naona anafaa pia maana ana mafunzo ya hali ya juu , ni muaminifu na  tabia  nzuri na kingine ni  mwanamke . Chaguo lako ni sahihi  na hata sijaliwazia sana”Aliongea Hamza

“Lakini kwanini? Sasa  hivi tu ulionekana ku…”

“Niache nimalize….”

“Nimefikiria kwa kina na  kugundua wewe ni mfanyabiashara.  Na  kama mfanyabiashara kama ungekuwa mwepesi kiasi cha kuitwa mtu mwenye roho nzuri  basi kampuni ya Dosam isingekuwa hai mpaka sasa h ivi . Ukweli  wakati tunakutana  sikukuona kama mwanamke mpole. Kwangu mimi ulionekana  kama mwanamke ambae una mtazamo wako binafsi kwenye mambo mazuri na mabaya”

Regina kusikia hivyo alishindwa kuongea na  kufanya mikono yake kugang’ania gauni lake kwa nguvu.

“Pia nilikuwa na wasiwasi unaweza kuwa mtu mwenye roho  nzuri kupitiliza na  siku moja kujiingiza katika matatizo . Lakini sasa hivi kuona mpango wako juu ya Helena , nimepatwa na amani , kwa kuona angalau mke wangu sio mjinga  bali ana akili  kuliko nilivyotegemea. Ila nisiwe mnafiki  sijapenda namna ulivyoniigizia na kunifanya nione kila kitu ni kweli”

“Mwisho wa maneno yote bado unaonekana kunichukia kwa kile nilichyofanya…”Aliongea Regina akikunja sura.

Hamza alitabasamu na kisha alimsogelea Regina na kumkumbatia  kiwepesi  na kisha palepale alimgeuza na kwenda kumwegamiza kwenye  gari.

“Wewe … unataka kufanya nini?”

Mikono yote ya Regina ilikuwa imajishikiza katika kifua cha Hamza kumzuia , alihisi  hofu na aibu kwa wakati moja.

“Wife kwanini unashindwa kuelewa? Mimi sijali kile  unachokifanya , kwasababu unachofanya ndio utashi wako. Kama unao uwezo wa kunidanganya  basi huo  ni uwezo wako maana  mimi pia sio mwepesi kudanganyika kutokana na  uwezo wangu wa akili . kitu pekee ninachotaka angalau kujua ni kuhusu hisia zako kwangu kama ni za kweli au lah , kwasababu hisia zangu kwako ni  za dhati kabisa..”

Regina kusikia hivyo alijikuta akishituka  na kuacha kuleta ukinzani  huku akimwangalia  Hamza na macho yake  yaliojaa maji.

Wawili  hao walijikuta wakiangaliana  na mara baada ya kuangaliana kwa kitambo kirefu. Hamza alishusha lipsi zake  na kupokelewa na Regina na walijikuta wakidendeka kwa hisia  kali.

Ingawa haikuwa mara yao ya kwanza kukiss , lakini  picha waliotengeneza katika eneo hilo  pembeni mwa hospitalini , ilikuwa ya aina yake . Baada ya mgogoro  wao dakika chache zilizopita , Regina mara baada ya lipsi zake kukutanisha na za Hamza alihisi  shoti za umeme zikisambaa mwili mzima.

Aliishia kutoa macho huku  mwili wake laini  ukitingishika  zaidi ya mara mbili. Alitaka kutoa kilio mara baada ya kuhisi joto na hisia kali kutoka kwa  mwanaume  huyo,  alijihisi ni kama anazamishwa majini na kuibuliwa.

Baada ya kushindana na hisia zake  na  zikamdhibiti kisawasawa , alijikuta akifumba macho yake yaliojaa machozi na kufanya yatengeneze mfereji wa maji. Alijikuta bila kuelewa amekwisha kupitisha mikono yake  na kuizungusha katika mgongo wa mwanaume  huyo huku akimvutia kwake kwa nguvu.

Hakuna aliekuwa akijua ni kwa muda gani walikuwa wamegandana , mara baada ya  kuhisi pumzi zinataka kumwishia. Hamza  hatimae alimwachia  mrembo wake.

Hamza mara baada ya kumwangalia mwanamke huyo na kuona jinsi macho yake yalivyokuwa mekundu na  kuonekana kama amekosewa sana, alijikuta akishindwa kujizuia na kuachia kicheko.

“Haha.. Wife mbona unalia?” Aliongea Hamza huku akinyoosha mkono wake na kumfuta Regina machozi kutoka kwenye mashavu yake.

Regina alijikuta akihema kwa nguvu  na kisha  kuinua kichwa chake na kumwangalia Hamza  na  kisha akiwa siriasi aliongea;

“Na mimi hisia zangu kwako ni  za dhati , siwezi kudanganya kuhusu hisia zangu”

“Najua,  kwa  namna ulivyonikumbatia kwa nguvu inatosha. Kwangu mimi ili mradi uwe mkweli juu ya hisia zako , mambo mengine sitojali”Aliongea Hamza akiwa na tabasamu.

“Sikutaka kukudanganya kuhusu Helena, ni kama ulivyosema ni utashi wangu… nili..”Alionekana kukosa neno  zuri la kuongea;

“Na mimi nilitaka  kuwa na nguvu  haraka iwezekanavyo ili kupunguza gepu  lililopo kati yetu. Ndio maana nilitaka kumchukua Helena , isitoshe  anao uwezo wa kuniambia kila kitu  kuhusu ulimwengu wa Giza”Aliongea Regina  kwa sauti hafifu.

“Kupunguza gepu! Kuna utofauti gani kwani na sasa?”

“Kuna haja hata ya kuuliza? Wewe ni Gwiji  na una madaraka makubwa , mimi ni mfanyabiashara mdogo tu kutoka nchi masikini , naona wasiwasi nitakuangusha …Na mimi pia nataka kuwa na nguvu haraka iwezekanavyo. Hata kama siwezi kuvuna nishati za mbingu na ardhi. Ila kwasababu  asili  yangu ni  kutoka kwa watu wa Bondeni  familia ya  urithi wa damu. Nataka  kutumia  fursa hii  kukirudisha kitengo cha Binamu  na teknolojia ya jicho  la Anga katika himaya yangu , nikifanikiwa najua hautonichoka” Hamza  kusikia hivyo  alijikuta akishangaa na kukosa usemi juu ya  namna Regina anavyoyachukulia mahusiano.

“Wife sijawahi kuwaza nitakuja kukuchoka kwasababu ya ulivyo , kwanini unafikiria sana? Kama unataka  kumiliki  teknolojia ya jicho la Anga  itakuwa ngumu sana  , maana  Huge sio mtu mwepesi , alitengeneza  kitengo cha Binamu kwa ajili ya kujilinda kimadaraka kutoka kwa  Babu na Bibi yako”

“Lazima nifanikishe , wewe unaweza usijali mimi nilivyo , ila kwa marafiki zako ni tofauti , wakiendelea kuniona  wa kawaida  watasema sistahili kuwa na wewe  na kadri watakavyoonyesha hisia zao utajisikia vibaya na pengine baada ya muda utaniona  sina maana”Aliongea Regina katika hali ya kuchukia.

Hamza aliona mwanamke huyo alikuwa akifikiria sana,  alijiambia kwanini afikirie kuhusu watu wanavyomuongelea mke wake.

“Wife acha kufikiria mbali , ikitokea mtu akakuongelea vibaya  na kusema hustahili kuwa na mimi  atakula kibano”

“Mimi sitaki hivyo , sitaki muda wote niwe nakutegemea kwenye kunilinda. Nataka kuwa na nguvu haraka iwezekanavyo  na kuajiri watu wengi.. Ukweli sikutaka kukudanganya, ilikuwa ni wasiwasi wangu  utaniona ni mtu  mwenye hila na mitego mingi  kwasababu unapenda mwanamke mpole  na mwenye utoto  utoto, sikutaka  kuharibu picha yangu iliojijenga  ndani ya moyo wako..”

Aliongea Regina akiwa na aibu  kiasi cha kuinamisha kichwa chini,upande wa Hamza baada ya kusikia maneno hayo alijikuta akishindwa kujizuia na kutoa kicheko kikubwa.

“Hahahaha… Haha.. Wife . haha.. kumbe una vituko namna hii. Kwahio ndio  unavyojiona , kama  mwanamke mpole na  mwenye utoto? Haha.. dah!”

Hamza alicheka mpaka  kufikia  hatua alianza kushika tumbo lake.

“Wewe unacheka nini vyote hivyo?”

Regina hata yeye aliona maneno aliongea  hayakuwa ya kawaida  na kufanya sura yake kuiva  kutokana na aibu nyingi  huku akipiga piga miguu chini  kwa hasira.

“Wewe usicheke  tena  nakuambia”

Hamza alicheka  sana kiasi cha kufanya machozi kuanza kumtoka . Aliishia kuinua macho yake juu angani   huku akivuta pumzi nyingi huku akiongea

“Mungu baba  kwanini umenipa mwanamke mjinga kama mke wangu? Inakuwaje kukawa na mwanamke wa hivi dunia hii?”

“Umekuwa chizi! Mimi nina tatizo gani? Au nyie wanaume mnapenda wanawake wenye mambo ya  kuficha ficha?”

“Sio kuhusu hilo . Kuwa mke hupaswi kujitahidi kujua kila kitu. Najua  kila ulichofanya ulitaka  kunivutia. Ila kilichonichekesha ni namna ulivyoongea  kile kilichopo ndani ya moyo wako  kwa usiriasi mkubwa.  Niimehisi umeongea kijinga sana ..hahaha”

“Nimekudanganya hukupenda , nimekuambia ukweli unaniona mjinga. Mbona unakuwa mgumu hivyo kueleweka ? Mimi nina hasira , sitaki  kuwongea na wewe tena , nenda mwenyewe kwenye  mkutano” Regina alihisi kushikwa na aibu na kugeuka kutaka kuondoka.

Hamza palepale alimsogelea na kumkumbatia kwa nyuma  huku akiongea kwa kumnong’oneza katika sikio lake.

“Mke wangu usiwe na   hasira  ni kwa jinsi ulivyokuwa cute ndio maana nilicheka na sio kwamba nakuchukia wala nini. Ukweli  huna haja ya kunifanya nikufikirie vipi  katika moyo wangu , wewe unaweza kufanya  unavyotaka. Ni kama kipindi kile ulivyomtafuta  Lamla ili kurudi  nyumbani , nina uhakika   hujategemea  kupata kitu chochote kutoka kwako , si ndio?”

Regina  mara baada ya kusikia hivyo , aligeuza kichwa chake na kumwangalia.

“Kuna vitu vingi unafanya sio kwamba unaigiza , kwa mfano namna unavyoonekana ukiwa unakula donati , ni kwasababu unazipenda kweli. Ninachomaanisha siwezi  kuwa mnafiki  kwako . Watu tunazaliwa na  tabia nyingi sana , nyingine  zimejificha na zinaibuka kadri tunavyongeza umri , pengine hata mimi nina tabia  ambazo huzijui na mimi pia bado sizijui , lakini  je  kwasababu ya  upande wangu mwingine  inatufanya tuachane?”

Regina mara baada ya kusikia hivyo , alijikuta akipata ahueni  baada ya kuona mwanaume huyo alikuwa akimwelewa vyema.  Alijikuta furaha ikimjaa  na moyo wake kuhisi utamu kama sukari.

“Muda wa kwenda kwenye mkutano ushafika , twende zetu”Aliongea  Hamza na Regina alitingisha kichwa , lakini muda ule alihisi  kitu  hakipo sawa.

“Vipi nibadilishe nguo? Hizi nguo nimevaa tokea jana”

“Kwanini , mbona ziko sawa tu”

“Wewe ni maarufu , nikionekana kurudia rudia nguo kwa siku nzima  si  nitaonekana wa kawaida?”

“Wife  uzuri wako haupo kwenye nguo unazovaa bali kwa  urembo wako wa sura. Kama ukivaa  vizuri kupitiliza  si itawafanya vidume   kukumezea mate , unataka kuniongezea maadui?”Aliongea  na Regina kusikai hivyo alishangaa kidogo.

“Kweli?”

“Ndio , sipendi kabisa  watu kumkodolea macho mke wangu”

“Oh, so you’re that petty … haya basi twende” Aliongea Regina ambae alikuwa katika mudi nzuri  na  kuingia kwenye gari.

Ingawa  lisaa limoja la maongezi nje ya hospitali kutokuwa kawaida. Lakini  ni mazungumzo ambayo yaliwafanya  kuwa karibu zaidi  na kuimarisha  uhusiano wao.

Hamza aliweza kuona Regina  kila alichofanya kilitokana na hisia zake  na hiko ndio alichotaka kuona. Lakini suala lingine  lilingiia akilini na hilo ni juu ya Regina  kutaka kurudisha  nguvu zake ndani ya Binamu na kumiliki teknolojia ya jicho la Anga. Mpango wake huo ulimfanya Hamza kuwa na wasiwasi mkubwa , lakini hakutaka kumzuia vilevile na alijiambia  atajitahidi kwenda nae hatua kwa hatua.

Mara baada ya kufika  nje ya ukumbi , Regina alipokelewa na  washikaji zake na kisha yeye alichukua uelekeo wa VIP kama kawaida. Muda ambao aliingia katika  chumba cha mapunziko  aliweza  kumuona Khalid akiongea na Huge.

“Sir Luciger , umekuja katika muda  muafaka . Nipo hapa kuwajulisha  kwamba hamtaondoka mapema kwasababu  leo Kikao cha Magwiji  kitafanyika pia”

“Kikao chetu ni leo? Kama ni hivyo kwanini tunaendelea kukaa kwenye  jukwaa? Si  leo ni mkusanyiko wa ajenda za  kitaasisi na  wawakilishi?”

Hamza aliona haikuwa na  muhimu  sana  kwa wao   kukaa jukwaani kwasababu  ajenda za siku hio hazikuwa zikiwahusu. Ukweli kama isingekuwa suala la  kitengo cha Malibu angemchukua Regina kwenda Shopping.

“Ukweli ni kwamba , kuna tatizo lingine ambalo linahitaji utatuzi  katika baraza hili la maksi . Sir Luciger nadhani utakuwa na  uelewa wa kutosha kuhusu  mwanasayansi maarufu duniani , Dokta Genesha  ambae alipotea”Aliongea Khalid.

“Dokta Genesha! Mbona alishakufa  na ni mimi niliemuona kwa macho yangu  kabisa na  sio hivyo tu  nilimchoma na kumwaga majivu yake baharini”

“Nini! Dokta Genesha amekufa ?” Khalidi alionekana kushangaa na Hamza aligeuza sura yake na kumwangalia Mathias Huge.

“Vipi na wewe huniamini au? Nadhani utakuwa na  taarifa juu ya hili kama sikosei?”Aliongea Hamza akimlenga Huge.

“My information is not free.”Aliongea akimaanisha taarifa zake sio za bure.

“F*ck , inachosha sana kudili na mtu kama wewe , kwanini unapenda sana hela  kuliko mimi?”Aliongea Hamza huku akimpotezea na kumgeukia Khalid.

“Ni kama nilivyosema bwana Khalidi ,  Genesha amefariki , ni juu yako kama utaamini  au lah , lakini  kwanini umemtaja?”Aliuliza Hamza na kumfanya  Khalid kushangaa kidogo kabla ya kujibu.

“Ni hivi , ukweli ni kwamba taasisi yetu imekuwa ikifanya  kazi  pamoja na Dokta Genesha.. Alikuwa ni mshauri wetu mkuu kwenye masuala ya kitafiti . Kabla ya kupotea aliweka Safe box kwenye umoja  wetu  na alitoa maekelezo  ifunguliwe  wakati wa Baraza la maksi”

“Ni kitu gani amehifadhi katika hicho kiboksi?”Aliuliza Hamza.

“Niwie radhi,  siwezi kufahamu  kutokana na  nafasi yangu. Lakini  moja ya sababu ya kualikwa kwa magwiiji wote kumi ni kwa ajili ya kuonyesha kilichopo ndani ya  hio safe box. Kwasababu  Dokta Genesha alikuwa akifanyia utafiti juu ya  Ankh , teknolojia  ya dawa ya kuzuia kifo , tuna kila sababu ya kuamini alichoacha kinahusiana na  dawa hio”

“Na kama ndivyo , basi litakuwa suala linalohusisha utajiri mkubwa,  kama  tusingekuwa na wataalamu  wengi ndani ya baraza letu basi  tusingethubutu kufungua hiki kiboksi wala kukitaja kabisa”

Hamza aliishia kuguna ndani kwa ndani ,   kabla Dokta Genesha anafariki alimwabia kabisa  hakuna dawa ya kuzuia kifo   zaidi ya  uwepo wa nadharia tu ambazo  nyingine zilihusisha  tafsiri ya kitabu  ambayo alipaswa kuifanyia kazi , ukweli ni kwamba hata kama utafiti huo ungemalizika  bila ya elementi  maalumu  isingeweza kufanikiwa .Lakini alijiuliza kwanini akaamua kuweka kiboksi muhimu katika Baraza la Maksi? Au kuna kitu kingine hakuwa akijua tofauti na Ankh alichokuwa akifanyia kazi?”

“Hatukutangaza mapema kwasabu ya kuhofia mtu mwenye nia mbaya anaweza  kujaribu kuikwapua , lakini sasa hivi kwasababu ya uwepo wa Magwiji wote kumi  tunayo kila sababu ya kutangaza ,tunakwenda kuifungua  usiku wa leo”Aliongea Khalid.

Hamza alifikiria kwa muda , lakini hakuweza kudhania ni kitu gani ambacho Genesha ameweka katika hicho kisanduku cha usalama.

“Wewe si una jicho la Anga , unajua nini kipo ndani ya hicho kiboksi? Usiniambie unataka hela kunijibu swali langu?”Aliongea Hamza akimwangalia  Huge.

“Siri za mbingu hazitoki bure”Aliongea

“Kama isingekuwa inachosha kupambana na mtu kama wewe ningeshakupiga na kukushikisha adabu”Aliongea Hamza huku akitingisha kichwa chake.

****

Ajenda ya kikao cha  kwanza  ilikuwa ni juu  ya  masuala makubwa yanayoendelea  katika ulimwengu wa giza. Kulikuwa na mikinzano mingi inayotokana na  wanufaika  na kufanya  watu kuanza kurushiana maneno.

Moja ya  kitu kilichoibua  mapingano ni  juu ya Earth Axis , ambayo ipo chini ya mikono ya Watanzania , kila taasisi ilikuwa ikivutia upande wake kutaka kujumuishwa kwenye kujua siri za Earth Axis.

Lakini hata hivyo  Balozi Rajabu na wenzake  kama wawakilishi , walionekana kujiandaa vyema kwa  hali hio.

Ukiachana na hayo kulikuwa na masuala mawili ambayo yalikuwa muhimu zaidi , kwanza  Tanzania haikuwa ikijua  Earth Axis ni nini  na wala haikuwa na uhakika kama ni kitu kibaya kwa binadamu au kizuri  hivyo  halikuwa jukumu lao kugawa  taarifa za Earth Axis.

Hamza mara baada ya kusikiliza watu wa kitengo cha Malibu wakiweka mezani hoja zao , aliishia kukubali na kujiambia ndio maana  licha ya kutokuwa na uwezo wa mapigano lakini waliaminiwa  mno  kuja kuwakilisha taifa , walionekana kuwa vizuri mno katika  kujenga hoja.

Wakati wa mapumziko mafupi ya vikao, Balozi Rajabu na wenzake walimsogelea Hamza aliekuwa na  washikaji zake wa Inferno na kuwasalimiua kwa ukarimu. Alieonyesha uchangamfu zaidi alikuwa ni Mboma ambae mwanzo alionyesha kumdharau Hamza sana katika  kikao chao cha kwanza.

Hamza upande wake alijua watu hao walitaka  kuazima nguvu ya ushawishi wake  huku ughaibuni  ili kuwanyamazisha   watu wasitoe vitisho  kwa Tanzania.

Haikuwa hivyo tu Balozi Rajabu pia alionekana kuchangamkiana na Mathias Huge , akionyesha kumtega kwa maneno. Ukweli ni kwamba licha ya  Binamu kuongozwa na Huge lakini  teknolojia ya jicho  la Anga ilikuwa  ni miliki ya watu wa Bondeni ambao asili yao ni Afrika , hivyo ni sawa na kusema  Huge  ni mwafrika pia  ambae  asingeweza kuona Tanzania inaingia  matatizoni, licha ya kwamba  ana unafiki mwingi likija suala la kuuza taarifa. Hivyo uwepo wa Hamza , Nyakasura na Huge ilikuwa ni kama msingi wa kuilinda   Earth Axis ili mataifa yenye nguvu yasijaribu kushurutisha kugawa siri zake kwa nguvu.

Hamza mara baada ya kuona  watu hao wa Malibu walikuwa wakijiweza vyema katika vikao hivyo , hakuona haja ya kushiriki kwa kila kitu, alichopanga ni kutumiza nusu ya  yale alioomba rafiki yake  Himidu kuhusu kumjua msaliti ndani ya  kitengo.

Alikuwa na watu wake aliowaweka kutoka Baffodil na walikuwa wakiwachunguza  vigogo hao kwa umakini mkubwa.

Usiku wakati wa  chakula , Hamza alichomoka  kutoka nje ya ukumbi na kwenda kuingia kwenye gari moja hivi ya rangi nyeusi aina ya cadillac.

Mara baada ya kuingia aliweza kukutana na  Black Fog ambae  ndio aliekuwa dereva wa gari hio  na liliondoshwa mara moja.

“Una uhakika ndio yeye?”Aliuliza Hamza.

“Tumethibitisha ni yeye kabisa unaemtilia shaka. Ile siku wakati mvua ikiwa inanyesha  na alieiba  Nyaraka. Yote ilikuwa ni  mipango yake”

“Inasikitisha sana , kwanini asingekuwa mwaminifu tu”Aliongea Hamza huku akitingisha kichwa.

“Bro , nimekubali sana  uwezo wako wa kusoma watu , kama ingekuwa mimi mtu ambae ningemtilia shaka ni  Mboma”

“Mboma ni mtu anaependa  maisha ya starehe tu  na kuwa na uwezo mdogo wa kufikiria , lakini  hana ujasiri wa kusaliti nchi”Aliongea Hamza

“Karibia  ya watu wote wa kitengo cha Malibu wanaonekana kupenda starehe , tuliowafuatilia  karibia wote walihudhuria Casino  na wengine  walilala na makahaba kasoro yeye tu”Aliongea Black Fog na kumfanya Hamza kutabasamu  tu.

Mara baada ya Black Fog kuendesha gari kwa umbali kama wa  dakika kumi au ishirini hivi walikuja kusimamisha gari upande wa magharibi mwa mji wa Limour  katika makaburi.

Ni sehemu iliokuwa na mazingira mazuri sana ,   ukiachana na makaburi  yaliokuwa kwenye bustani safi , lakini vilevile kulikuwa na kanisa kubwa la Cathedral.

Kulikuwa na magari kadhaa  yalioegeshwa kando ya barabara  mkabala na kanisa   na  yalionekana sio ya waumini , bali ni wafanyakazi  wa  eneo hilo.

Black Fog na Hamza waliingia ndani ya kanisa , mlango ulikuwa wazi licha ya kuwa usiku na ile wanazama ndani waliweza kumuona mwanamke alievalia  nguo nyeusi na  hat kubwa ya rangi nyeusi pia , akiwa anasali mbele ya sanamu la bikra maria . Pembeni yake  alikuwa ameweka Briefcase. Alionekana ni kama  ndio  anamalizia  kusali  baada ya kuonyesha ishara ya msalaba  huku akitamka maneno.

“Mungu , ili mradi nifike salama  nchini America. Nitatumia muda wangu wote kukutukuza na kuliabudu  jina lako..”

Mara baada ya kumaliza kuongea maneno hayo , palepale  alishika ile briefcase na kusimama. Ile tu anataka  kuondoka  , alijikuta akiinua uso wake na kukutana na sura ya Hamza na Black Fog wakiwa katika eneo la kuingilia ndani ya kanisa .

“Ah! Hamza.. Mr Hamza!?”Alionekana kushituka mno.

Previoua Next