Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

SEHEMU YA KWANZA

GEREZA LA DOMINIC 

Kiza totoro kilizalisha nyota za kuvutia sana angani ikiwa ni usiku sana. Dunia ilikuwa imetulia sana hususani yale maeneo ambayo watu walikuwa wanautegemea mwanga wa jua kufanya mijongeo ambayo haikuwa na mwisho bali mwanzo ambapo ungeona watu wanatoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya utafutaji na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Hali ilikuwa ni tofauti sana kwa usiku huo wa manane ambao ulikuwa umezongwa zongwa na kiza kinene, shukrani kwa taa za umeme ambazo ziliufanya mji uendelee kuvutia na kupendeza huku mvua zikiwa zinashuka kwa wingi na kufanya mijongeo ya watu kuwa michache sana.

Usiku huo ndio wakati ambao msafara wa gari tano za jeshi ulikuwa barabarani kwa spidi huku madereva wakionekana kuwa makini sana kuhakikisha kwamba wanafika salama mahali ambapo walitakiwa kuwepo usiku huo. Gari hizo za jeshi zilikuwa zinalilinda gari moja la wafungwa ambalo lilikuwa katikati ya gari zingine na kuufanya msafara huo kuwa na jumla ya gari sita ambazo zilikuwa kwenye mwendo wakati huo.

Msafara huo ulikuwa unaelekea nje ya mji, sehemu ambayo kadri muda ulivyokuwa unazidi kwenda ndivyo kiza kilivyokuwa kinazidi kuwa kingi kwani nje ya mji hakukuwa na taa za kusema kwamba zingemlika kila sehemu hususani zile ambazo hazikuwa makazi ya watu.

Gari hiyo ya wafungwa ndani yake ilikuwa na cage ndogo ya chuma ambayo ndani yake alikuwa amehifadhiwa mfungwa huku kwenye mwili wake akiwa amewekewa minyororo kila sehemu. Hakuonekana kuwa mtu mwema sana wala kuwa mtu wa kawaida sana ndiyo maana licha ya uwepo wa makamanda wa jeshi wa kuaminika bado hawakumpa mtu huyo nafasi ya kuweza kuwa huru hata kidogo zaidi ya kumfunga minyororo karibia sehemu yake kubwa ya mwili.

Ndani ya hiyo cage ndogo kwenye hilo gari la wafungwa, alionekana mwanaume mmoja kwa mbali sana kutokana na uhaba wa mwanga ambao ulikuwepo usiku huo. Kipara kilichokuwa kinang'aa sana kilionekana kwa usahihi kabisa, mwili wake ambao ulikuwa umegawanyika vipande vipande ulijichora vyema sana ndani ya gari hiyo huku akionekana wazi kwamba aliyafumba macho yake kama sio kulala usingizi.

Haikujulikana mwanaume huyo alikuwa amefanya kitu gani hasa kwenye maisha yake mpaka kuwekewa ulinzi mkali sana namna hiyo huku makamanda wa jeshi wapatao sita wakiwa ndani ya gari hiyo na silaha zao walizielekezea kwa mwanaume huyo kiasi kwamba kama angefanya jambo lolote baya basi risasi zilitakiwa kumhusu moja kwa moja.

Baada ya safari ya muda mrefu gari hizo zilisimama ghafla sana hali ambayo ilimfanya mwanaume huyo kuyafumbua macho yake. macho yalikuwa yanawaka moto kwa kumtazama mwanaume huyo kwa mbali, ni macho ambayo yalionekana kuongea lugha nyingi sana za hisia zenye maumivu makali sana ambayo hayakujulikana nini kilikuwa chanzo chake hasa mpaka akaishia kwenye hiyo minyororo.

Mbele ya sehemu ambayo gari hizo za jeshi zilisimama kulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa sana ambao ulionekana wazi ulikuwa umejengwa kwa uimara mkubwa kwa muda mrefu sana. katikati ya kuta hizo kulikuwa na lango kubwa sana la vyuma ambalo baada ya msafara huo kufika hapo lilifunguliwa taratibu na ndipo wanaume hao wakaingia na gari zao.

Juu kabisa ya hilo lango kubwa kulikuwa na maandishi makubwa sana ambayo yalikuwa yameandikwa GEREZA LA DOMINIC. Lilikuwa ni gereza la kuogopeka zaidi ndani ya nchi ya Tanzania, gereza ambalo hakuna mfungwa aliwahi kutamani kuingia huko hata kama angekuwa na kosa gani kubwa. Yote ni kwa sababu ya taarifa ambazo zilikuwepo zikidai kwamba lilikuwa kinyume kabisa na haki za wanadamu na wananchi wengi sana walikuwa wakilipigia kampeni gereza hilo liweze kufungwa kwani hakuna mtu aliwahi kupelekwa huko halafu akafanikiwa kutoka akiwa hai na mzima wa afya. Huko ndiko ambako mwanaume huyo aliweza kupelekwa usiku huo na msafara wa kijeshi.

Kwenye moja kati ya vyumba vikubwa na bora zaidi ambavyo vilikuwepo ndani ya jengo hilo, alikuwa ameketi mwanaume mmoja ambaye gwanda lake lilikuwa na nyota za kutosha akiwa anapata chai taratibu huku kwenye mkono wake akiwa ameshika kishikwambi na kuendelea kusoma habari ya mtu ambaye muda mchache ujao alitakiwa kumpokea kwenye mikono yake.

Huyo ndiye alikuwa mkuu wa hilo gereza la Dominic, Luka Gambino ndilo lilikuwa jina lake. Mwanaume huyo aliwahi kuwa kanali wa jeshi kabla ya kuja kuipata nafasi hiyo na historia yake ya nyuma haikuwa nzuri sana. Akiwa hapo anapitia pitia taarifa za mwanaume huyo, mlango wa ofisi yake ulikuwa unagongwa ambapo alitoa ruhusa mgongaji aweze kuingia na wakati huo huo aliingia msaidizi wake.

"Mkuu mtuhumiwa amefika tayari, inasubiriwa amri yako tu" ndiyo kauli ambayo aliitamka iliyo mfanya kiongozi huyo kutoa tabasamu hafifu kwenye uso wake.

"Hii ndiyo habari kubwa zaidi ambayo mimi nilikuwa naisubiri kwenye maisha yangu. Kufanikiwa kumhifadhi mtu kama huyu eneo hili kutanipa sifa kubwa sana nchini na kila mtu atatamani kuhitaji kunifahamu mimi kwa undani kwamba ni nani hasa na hapa ndipo nitamuonyesha huyo bwana mdogo kwamba dunia sio sehemu salama sana hususani kwa watu wa aina yake. Naapa huu utakuwa mwisho wake mbaya sana atatamani ni bora angefanikiwa kujiua kabla hajaingia ndani ya jengo hili. Nipeleke huko waliko sasa hivi" aliongea kwa msisitizo huku akiwa anachora alama ya X kwenye picha ya mwanaume huyo ambaye haikujulikana alikuwa amefanya kosa lipi mpaka watu waweze kumpania sana kiasi hicho.

Mwanaume ambaye alikuwa amefungwa ndani ya gari hiyo ya wafungwa alionekana kuwa kwenye mawazo makali mno baada ya kugundua kwamba alikuwa ameingia ndani ya kuta za gereza hilo.

Maumivu yalionekana kuutafuna sana moyo wake kiasi kwamba chozi lilikuwa linashuka kwenye mashavu yake huku likikosa mfutaji au mtu wa kuweza kulipa sehemu ya kuelekea. Haikuonekana kuwa sehemu njema sana kwenye maisha yake ndiyo maana alikuwa anatoa machozi, hiyo sehemu alionekana kuwa na historia nayo kubwa sana kiasi kwamba nafsi yake ilikuwa inamuenda mbio sana baada ya kuifikia.

Aliyafumba macho yake kwa hisia sana na alipokuja kuyafumbua tena machozi hayakuwepo tena kwenye macho yake na gari zilikuwa zinasimama kwa kasi sana kiasi kwamba aliyumba kidogo na kujigongesha kwenye nondo moja ya chuma ila hakuonyesha mshtuko wa aina yoyote ile kana kwamba kwake lilikuwa jambo la kawaida tu. Walishuka wanajeshi wengi sana na kuisogelea ile gari ambayo yeye alikuwepo na baada ya hapo wanaume sita ambao walikuwa wanamlinda walifumgua milango mikubwa ya gari hiyo na kuitoa cage ambayo alikuwepo mfungwa huyo nje.

Wakati huo wote walitoa heshima kwa kiongozi mkuu wa gereza hilo ambaye alikuwa anafika wakati huo ndani ya hilo eneo. Mtu mzima wa miaka karibia sitini ndiye ambaye alikuwa anakuja kumpokea mfungwa huyo akiwa ndiye kiongozi mkuu wa gereza hilo. Alisogea mpaka walipokuwepo makamanda hao ambapo mmoja wao aliyekuwa kiongozi alimsogelea na kumpa heshima kisha akampa maelekezo ambayo alitakiwa kuyapata kabla ya kumpokea mfungwa wake.

"Mkuu kazi yetu ilikuwa ni kumfikisha hapa salama na kwa sasa kuanzia hapa itakuwa ni kazi yako. Wakubwa watakupa maelezo zaidi juu ya mtu huyu na kile ambacho unatakiwa kukifanya ila kuanzia sasa sisi tunageuza makao makuu. Usije ukafanya kosa la kumpa hata nafasi ndogo ya kuwa huru kwa sababu unaweza kuleta madhara makubwa sana ndani ya hili gereza ndiyo maana anatakiwa kuishi kwenye minyororo hivyo hivyo mpaka pale ambapo utakuwa na uhakika kwamba hatakuwa hatari tena kwa ajili ya maisha ya watu wengine ndani ya eneo hili"

"Hauna haja ya kuongea sana, najua aina ya mtu ambaye nimeletewa na nina uhakika pia hata wewe unajua aina ya eneo ambalo ameletwa hivyo yeye ndiye anatakiwa kuyahofia maisha yake kwani hii sehemu sio salama kabisa kwa mtu kama huyu na huenda akawa na maisha mafupi sana"

"Fanya yote ila usije ukamuua kwa sababu huenda akawa na matumizi kwa hapo baadae, ni mtu mhimu sana na anadaiwa kwamba huenda kuna taarifa za siri sana ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa taifa hili ambazo anazo"

"Waambie hatakufa ila atatamani ni bora angekufa huko mliko mtoa, kwanza mmefanya kosa kubwa sana kumnyoa nywele zake akiwa huko, mlitakiwa kumleta hapa nimnyoe mwenyewe kwa chupa, mpuuzi mmoja kama huyu hatakiwi kuishi kwa starehe sana namna hii"

"Tusamehe kwa hilo mkuu, sisi tunaondoka na tunakutakia bahati njema" mheshimiwa hakujibu kauli ya kamanda mkuu wa kikosi bali alitabasamu tu huku akitoa ishara kwa vijana wake kwenda kumtoa mwanaume huyo kwenye cage ambayo alikuwepo huku makamanda wakiwa wanaondoka na gari zao kwa kasi sana ndani ya hilo eneo kwa sababu kazi yao ilikuwa imekamilika na kuanzia hapo maamuzi hayakuwa yao tena juu ya nini cha kukifanya kwa mwanaume huyo.

Baada ya kutolewa kwenye chuma ambacho alihifadhiwa, akiwa na minyororo mkononi na miguuni ambayo iliunganishwa mpaka shingoni, mwanaume alikuwa anasukumwa kuelekea ule upande ambao alikuwepo Luka Gambino ambaye alikuwa kiongozi mkuu wa eneo hilo. Mwanaume mmoja ambaye hakuwahi kuujua ustaarabu wala kuelewa maana halisi ya neno huruma kwenye maisha yake, alikuwa ni mtu mkatili sana ambaye alikuwa anaogopwa na kila mfungwa au mtu ambaye alipata kumjua japo kwa uchache tu kwenye maisha yake.

Mjongeo wake wa lazima, uliweza kumsogeza zaidi sehemu ambayo ilikuwa na mwanga wa kutosha hivyo ukasaidia kuweza kumuonyesha vizuri sana. Mwanaume wa miaka isiyo pungua thelathini na mitano alikuwa anaonekana vyema, macho yake yakiwa makali na mekundu sana. Hakuonekana kuwa sawa kwenye mwili wake kwa sababu alikuwa anavuja damu. 

Kwenye mbavu yake ya kulia damu ilikuwa inatoka kwa wingi sana huku kisu kikiwa kimenasa eneo hilo kuonyesha kwamba kuna mtu alikizamisha na hakukitoa hivyo kikawa kinaendelea kumletea maumivu makali sana lakini hakuwa na muda nacho sana maana alivyokuwa amefungwa asingeweza kabisa kukichomoa. Miguuni alikuwa peku huku kila alipokuwa anakanyaga alikuwa anaacha damu, miguu ilitobolewa na misumari na nguo zake zilichakaa damu, paja lake la kulia likiwa na damu ya kutosha na nondo moja ambayo ilikatikia eneo hilo ikiwa bado haijatolewa. Ilionekana muda mfupi tu uliokuwa umepita mwanaume huyo alitoka kuchezea kipigo kizito sana kutoka kwa hao watu ambao walikuwa wamempeleka eneo hilo.

Ndo kwanzaaaaa tunaufungua ukurasa wa mwanza wa andiko hili.

Sitaki niongee sana, karibu kwa wakati mwingine tena tuweze kucheza na huu wino pamoja...

Next