Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

SEHEMU YA PILI

Mkuu wa gereza alimsogelea mwanaume huyo huku akiwa anatabasamu sana lakini baada ya kufika na kumkagua mtu huyo aliikunja sura yake vibaya sana akiwa anaukunja uso wake kwa ghadhabu kubwa.

"Wewe ndiye mpuuzi mmoja ambaye umenifanya mpaka usiku huu nishindwe kulala na mwanamke wangu nikae nikikusubiri hapa? Siwezi kuacha hili lipite, nakuhakikishia lazima ukalipe kwa hili mpuuzi mkubwa sana wewe. Niliwahi kuapa kwamba watu ambao walikuwa kwenye gereza hili walikuwa wanatosha na sikuwahi kuhitaji kuletewa mtu mwingine ila wewe umefanya kosa la aina ile ile ambalo sikuwa nahitaji litokee na hatimaye umeletwa huku sehemu ambayo hatakiwi kuhifadhiwa mwanadamu wa kawaida, je unajua ni kipi kitakupata kwenye maisha yako bwana mdogo? niamini mimi ni bora wakati wa kiangazi ungeenda kuishi jangwani sehemu ambako hakuna hata maji ila sio kuletwa sehemu kama hii" aliongea akiwa anamzunguka mwanaume huyo ambapo alimtwisha rungu la chuma mgongoni lakini mwanaume huyo alibaki ameganda tu hivyo hivyo bila kutamka neno lolote lile wala kutikisika.

"Una familia?" kwa mara ya kwanza mwanaume huyo aliitoa sauti yake ambayo ilikuwa nzito sana na ya kukwaruza kwa mbali akionekana wazi kwamba alikuwa anamlenga ni kiongozi huyo wa hilo gereza. Alihisi aliisikia vibaya kiasi kwamba akawageukia vijana wake lakini aligundua kwamba mwanaume huyo alikuwa amemlenga ni yeye mwenyewe. Alishikwa na hasira kali mno kitu ambacho kilimfanya atoe bastola yake na kumpiga risasi mbili za kwenye mapaja mwanaume huyo mpaka akashindwa kusimama na kuishia kupiga magoti huku akiwa anauma meno kwa maumivu makali sana ambayo alikuwa anayapata wakati huo.

"Mpuuzi mkubwa wewe kijana, wewe hapo ndiye mtu ambaye unathubutu kuliingiza jina la familia yangu kwenye huu upuuzi wako? ulitakiwa kuisoma historia ya maisha yangu ya nyuma. Nina historia mbaya sana ya haya maisha mpaka leo kuwa kiongozi kwenye gereza kama hili ni bahati nasibu sana kwa sababu mimi nilitakiwa kuwa miongoni mwa wafungwa ambao wangekuwa wanayaishi maisha magumu sana ila mimi ndiye kiongozi kwenye sehemu kama hii. Ukajifunze maana ya jina langu la pili la Gambino nililipataje, kaisome familia yenye historia ya jina hilo huko Marekani kisha utagundua kwamba umefanya kosa sana kunijibu nikiwa naongea" aliongea kwa hasira huku akiwa anairudisha silaha yake kwenye mfuko wake kisha akawageukia vijana wake.

"Hatakiwi kulala kwa masaa arobaini na nane, apitie mateso makali sana ila hakikisheni hafi na hizo risasi atakaa nazo kwa siku mbili mwilini akili imkae ndipo ataelewa kwamba huku sio kwa ajili ya watoto wa mama ambao wakiguswa tu wanataka kuwalilia mama zao na kuhitaji kunyonya. Akimaliza hiyo adhabu ndipo aanze kupatiwa matibabu kidogo kidogo" alitamka huku akiwa anageuka na kuelekea kwenye ofisi yake, muda ulikuwa umeenda sana hivyo alihitaji kurudi ili akajiandae kupumzika maana kazi ya kumpokea mfungwa huyo ilikuwa imekamilika tayari.

Mwanaume huyo akiwa ndani ya maumivu makali kwenye mwili wake, aliunyanyua uso wake ambao haukuwa na nuru hata kidogo kuangalia juu ya ukuta wa kuingilia kwenye vyumba ambavyo walikuwa wanahifadhiwa wafungwa mbali mbali, huko aliona maandishi makubwa tena yakiwa yameandikwa GEREZA LA DOMINIC. Baada ya kuliona jina hilo, kuna picha nyingi sana zilikuwa zinapita kwenye kichwa chake kwa kasi sana kiasi kwamba zilianza kumuumiza sana mpaka akayafumba macho yake, alipokuja kushtuka wanaume walikuwa wapo nyuma yake wakimnyanyua kwa nguvu huku wakimpiga na vitako vya bunduki zao kumtaka aelekee sehemu ambayo yangekuwa makazi yake mapya kwa wakati huo.

Luka Gambino baada ya kufika kwenye ofisi yake alisogea mpaka kabatini ambako alitoa chupa ya pombe na kuanza kuinywa kwa pupa sana akionyesha kutoridhika na kauli ya mwanaume ambaye muda mfupi uliokuwa umepita alitoka kumpokea kwa makamanda wa jeshi. Akiwa anainywa hiyo pombe yake aliingia msaidizi wake akiwa na bahasha mkononi mwake.

"Kuna kingine umesahau?"

"Ndiyo bosi"

"Sikio langu ni lako" alimaanisha anamsikiliza.

"Kuna hizi taarifa za mtu huyu zimefika muda sio mrefu sana, kuna mtu amezileta inaonekana zilisahaulika, pia kuna frashi ndogo inasemekana kwamba kuna taarifa zote za mtu huyo hivyo itakuwa ni jambo la busara kama tutafanikiwa kuweza kuzipitia na kuweza kumjua kiundani ukiachana na zile taarifa fupi ambazo zilikuja mwanzo" mheshimiwa baada ya kumsikia kijana wake anaongea hayo maneno, alisogea kwenye kiti na kumpa ishara kijana huyo kuelekea ukutani ambako kulikuwa na skrini kubwa ili aweze kumchambulia taarifa hizo na maelekezo yake yaliyokuwepo ndani.

"Remy Claude ndilo jina lake linalo daiwa kuwa la kuzaliwa lakini jina lake ambalo linafahamika sana kwa watu wake ni Menace likiwa na maana ya muuaji wa hatari sana. Mwaka huu anaingia mwaka wa thelathini na sita tangu azaliwe, hakuna alama yoyote ambayo inaonyesha kwamba alizaliwa wapi na lini ila taarifa zilizopo ni kwamba ni mtoto wa mtaani ambaye maisha yake hayana mwanzo bali mwisho wake utakuwepo."

"Ni kiongozi wa genge la hatari sana la kihalifu ambalo linajulikana kwa jina la SARAFU KUMI NA TANO (FIFTEEN COINS). Hizo sarafu kwa mujibu wake ni kwamba zilishapotea hivyo anazitafuta na haijulikani kwamba hizo sarafu zina maana gani kwa sababu jina la genge hilo linaonekana lilibadilika baada tu ya yeye kuanza kuliongoza"

"Watu ambao alikuwa anawaongoza kwenye genge hilo wanadaiwa kwamba kwa sasa wote wamekufa kwa kuuawa na mtu pekee ambaye amefanikiwa kuishi ni yeye ambaye ndiye alikuwa kiongozi. Ni genge la kimafia ambalo limesababisha athari kubwa sana kwa taifa yakiwepo mauaji ya kutisha, kuliyumbisha taifa kiuchumi lakini ilidaiwa kwamba pia genge hilo lilikuwa likisambaza madawa ya kulevya mitaani na kuwatumikisha vijana wengi sana kwa kuwaachisha masomo na kuwaingiza kwenye biashara hiyo huku wote ambao walikuwa wanapingana na genge hilo walikuwa wanaishia kuuawa na wanawake kubakwa hovyo hovyo" msaidizi wa mkuu wa gereza aliacha kwanza kuichambua na kuisoma taarifa hiyo huku jasho likiwa linamtoka kwenye uso wake. Yalikuwa ni maelezo ya juu tu lakini yalikuwa ni maelezo mazito sana ambayo hayakuwa na usalama mkubwa kwa walikokuwa wanaelekea. Alikunywa maji na kuikuza picha kubwa ya mwanaume ambaye walikuwa wanamuongelea hapo akiwa ndani ya suti safi sana na begi lake huku kwenye kichwa chake akiwa na nywele nyingi za kutosha kisha akaendelea tena.

"Baada ya jambo hili kutokea na kuwa kubwa sana mtaani ndipo serikali ilitengeneza mazingira ya kuweza kumkamata mtu huyu. Kumkamata haikuwa kazi rahisi sana kwa sababu alikuwa ni mtu mwenye pesa sana na jina hivyo ulikuwa unahitajika ushahidi wa kutosha ili kumpata kwani kazi yake alikuwa anaifanya kwa usahihi na umakini sana. Hali hiyo ilipelekea maafisa wengi sana kupoteza maisha kwa wale ambao walikuwa wanaingia kwenye njia zake ili kuweza kumtafutia ufumbuzi mtu huyo na ndipo shirika la usalama la nchi lilipo amua kumvalia njuga kisawa sawa baada ya kukerwa na kupotea kwa maofisa wengi sana ambao walikuwa wanapewa kazi ya kuweza kumfuatilia mtu huyu"

"Sentinel Nexus Intelligence Agency (SNIA), shirika letu la usalama wa taifa chini ya mkurugenzi Cleopatra Gambo lilimteua mwanamke mrembo Anelia Baton kuweza kuifanya kazi ya kufanikiwa kumuweka karibu mwanaume huyo ili kujua njia zake zote ambazo alikuwa anazitumia kwenye biashara yake kwa ujumla lakini bila kusahau kuweza kuungamiza mtandao wake wote ili ikiwezekana akamatwe ama kuuawa japo serikali ilikuwa ikimhitaji zaidi awe hai kwani angekuja kuwa na msaada mkubwa sana kwa taifa hapo baadae"

Sehemu ya pili inafika mwisho.

Previoua Next