Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

SEHEMU YA TATU

"Mwanamke huyo ambaye alikuwa na urembo usio elezeka na umbo ambalo dunia ilipata kustaajabu ule urembo wa asili usio na kasoro yoyote ile kwa mwanadamu, mwanamke ambaye alikuwa na taaluma ya udaktari ndiye mpelelezi ambaye aliwekwa chambo mezani kuweza kumpata mhalifu Remy Claude. Taarifa za siri kuhusu mwanamke huyu (confidential information) hazitaji wazi kwamba alitumia njia gani kuweza kuingia huko ila ni kwamba njia hii iliweza kuzaa matunda kwa ukubwa sana na kufanikiwa kuliangusha genge hili hatari sana hapa nchini. Penzi likaliokoa taifa kutoka kwenye hatari ya kuweza kuyumbishwa na kuteketezwa na genge hilo" mkuu wa gereza baada ya maelezo hayo aliguna kidogo na kumtaka msaidizi wake aweze kumuonyesha picha ya mwanamke ambaye alikuwa anaongelewa hapo.

Alisimama kutoka pale alipokuwa ameketi na kusogea mpaka kwenye ile skrini, aliigusa na kuikuza ile picha ya huyo malaika ambaye alikuwa anazungumziwa hapo, hakuamini alichokuwa anakiona, bado hakuwa kwenye fahamu zake kuweza kuamini kwamba taifa la Tanzania lilikuwa na mwanamke mrembo wa namna hiyo, hilo ni jambo ambalo kwake lilikuwa ni gumu kuamini.

"Unataka kuniambia huyu binti ni mzaliwa wa hili taifa?"

"Ndiyo bosi, kama sio hivyo wasingeweza kumtumia kwenye kazi nyeti sana namna hii"

"Mhhhh natamani sana nipate bahati ya kuja kuutumia hata usiku mmoja kitandani na mwanamke huyu. Baada ya hapa hakikisha unamtafuta kwa gharama yoyote ile"

"Lakini bosi, japo taarifa zake zinadaiwa kuwa za siri huyu mwanamke lakini kuna sehemu hapa inaonyesha alama ya X kwenye picha yake ikiwa ni kama tafsiri ya kwamba huenda alishakufa"

"Hapana, mpaka tuhakikishe hilo, kama angekuwa amekufa basi wangeonyesha moja kwa moja kwenye hizo taarifa huyu atakuwa yupo hai na anaishi mahali kwa starehe kabisa"

"Sawa bosi, nitafanya hivyo"

"Ebu malizia maelezo ya huyu mtu kisha mimi nikalale, umekuwa usiku mrefu sana leo"

"Baada ya mwanamke huyo kufanikiwa kutoa taarifa zote za mtu huyu ambaye serikali ilikuwa inamtafuta kwa miaka kumi kumtia mbavuni bila mafanikio hatimae kikosi maalumu kiitwacho HOLY TRINITY (UTANO MTAKATIFU) huku wao wakipenda kujiita TULIKUFA TUKIWA HAI, kilitumwa kwenda kumchukua mtu huyu sehemu ambayo walielekezwa kwamba alikuwepo"

"Hicho kikosi umewahi kukisikia au unakifahamu?" mkuu wa gereza alishtuka kusikia jina kama hilo kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupata kulisikia jina la namna hiyo ndiyo maana aliamua kuingilia maelezo ya kijana wake.

"Hapana bosi, imeandikwa (Disclosed) hizi taarifa zao hakuna mtu ambaye anatakiwa kuzijua wala kuwajua, nadhani wakubwa ndio watakuwa na majibu sahihi kwamba hiki kikosi ni kipi na kilianzishwa kwa ajili ya jukumu lipi"

"Endelea"

"Watu hawa wapo watano tu ambapo kiongozi wao ni mwanamke, hawa ndio ambao walifanikiwa kumkamata mwanaume huyu baada ya pambano la muda mrefu na baada ya hapo walimzidi nguvu kwa sababu inadaiwa kabla alikula chakula chenye sumu ya kulegeza mwili hivyo walifanikiwa kumkamata na kuteketeza watu wake wote na ndipo alipelekwa mahakamani kwa kosa la kuua watu kumi kwa makusudi pamoja na uhalifu wa hilo genge lake, akahukumiwa miaka sitini jela. Akiwa kwenye gereza la kwanza aliua askari watano na wafungwa wenzake kumi na watano na ndipo ikaamuliwa aletwe huku baada ya kupata kipigo kikali sana kutokana na ujeuri ambao alikuwa nao" 

Habari ya mwanaume huyo namna alivyoweza kukamatwa na utambulisho wake uliokuwa mezani ulikuwa umeishia hapo, uliletwa ili mkuu wa gereza aweze kujua mtu ambaye alikuwa amemuweka kwenye mkono wake alikuwa mtu wa namna gani. Baada ya kufanikiwa kumaliza maelezo hayo na kuangalia picha ambazo zilikuwepo kwenye frashi ambayo walikuwa wamepewa waliiona video moja, ilikuwa ni video ya dakika mbili tu ambayo walitakiwa kuiangalia kwa umakini sana kabla ya kuacha kila kitu ambacho kilikuwepo.

Kwenye video walikuwa wanaonekana wanaume sita ambao kwa mwonekano tu walikuwa ni makomando kutokana na magwanda ambayo yalikuwa kwenye miili yao wakiwa wamemzunguka mwanaume mmoja ambaye alikuwa amejifunika uso wake huku akiwa ameipa kamera mgongo na kwenye mwili wake akiwa amevaa mavazi meusi. Kwenye mkono wake mwanaume huyo alikuwa ameishika sindao ya kushonea viatu huku komando mmoja akiwa amemuweka chini ya ulinzi.

Katika moja kati ya makosa makubwa ambayo komando huyo aliyafanya ni kumsogelea karibu mtu huyo ambaye alifanya jambo la ajabu na la kushtua sana. Aliugeuza mkono ambao ulikuwa na sindano kwa nguvu sana wakati anageuka baada ya kupiga mahesabu na kugundua kwamba mtu ambaye alikuwa na silaha alikuwa na uwezo wa kumfikia pale alipokuwepo. Komando huyo baada ya kupata mshtuko aliachia risasi ambayo alichelewa kuiachia kwa sababu mtu huyo alikuwa amefika karibu na usawa wa bunduki hivyo risasi ikaenda hewani wakati huo mkono wake uligeuzwa vibaya sana ambapo alichomwa chomwa sindano nyingi sana kwenye mkono wake ambazo ziliishia shingoni.

Alichanwa chanwa shingo vibaya kisha sindano ikazamishwa ndani ya shingo na ilipokuja kutolewa, koromeo halikuwa likifaa kabisa. Alishuka chini taratibu akiwa amejishika shingoni hata silaha yenyewe hakuwa na uwezo wa kuishika tena, hali yake ilikuwa mbaya mno na dakika za yeye kuwa hai zilikuwa zinahesabika muda wowote alikuwa anaenda kupoteza maisha yake. Hata wenzake walibaki kwenye mshangao mkubwa sana maana lilikuwa ni jambo ambalo lilifanyika kwa haraka kiasi kwamba hawakuwa na uwezo wa kuzuia jambo hilo.

Waligadhabika sana kwa hali ambayo ilikuwa imemtokea mwenzao, alijifyatua mmoja kwa kasi na buti lake zito ambalo lilimpata mwanaume huyo kifuani lakini hakutetereka wala kurudi nyuma. Komando yule alitua mguu wake chini na kuirusha ngumi kali ambayo ilimpuliza mwanaume yule kwenye uso wake kisha akageuka na mateke ambayo yalikuja mfululizo. Ni teke moja tu lilizama tena kifuani ila lingine wakati linakaribia mwanaume huyo alilizuia kwa kutumia sindano ambayo ilikuwa kwenye mkono wake.

Sindano hiyo iliuchana mguu wake kwa maumivu mno kiasi kwamba wakati anataka kugugumia kwa hayo maumivu makali alijisahau, alipigwa ngumi mbili za haraka sana kwenye kifua chake. Alibaki amesimama tu akiwa ameyatoa macho yake kiasi kwamba hakuwa na uwezo wa kujongea, kuhema wala kuongea. Mkuu wa gereza aliisimamisha video hiyo kwa mshangao mkubwa sana akasogea karibu zaidi ili kuweza kuangalia kwa usahihi kwamba ni kipi kilifanyika. Alicho kishuhudia ni kwamba ngumi ambazo zilitua kwenye kifua cha yule komando zilimletea madhara kiasi kwamba moyo wake ulisimama kufanya kazi hivyo akawa hana namna ya kuishi. Video ilipo ishia pale ambapo ilikuwa imefikia, komando yule alidondoka chini akiwa tayari ni wa juzi

Sehemu ya 3 niseme baaasi.

Previoua Next