Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

SEHEMU YA NNE

Hakutaka hata kukaa tena, alihitaji kuona kwamba ni kipi ambacho kilikuwa kinaenda kutokea hata kwa wale wanne ambao walikuwa wamebaki pale. Hao walimchangia wote, uzembe mdogo tu uliwapoteza wenzao wawili kiwepesi mno hali ambayo hawakuwa tayari kuendelea kuiruhusu iweze kutokea hata kwao. Ujio wao ulikuwa mzito sana, walimpiga ngumi nyingi sana mwanaume yule kiasi kwamba alishindwa kuhimili hivyo alidondoka mpaka chini ambapo alitua kwa mkono mmoja na alipo nyanyuka alikuwa ameukunja mkono wake mmoja na sindano yake kwenye mkono wa kushoto.

Alifanya mauaji ya kikatili sana kwa watu hao ambapo aliwaua makomando watatu kwa kuwachana chana sehemu za shingoni huku komando mmoja akimzamishia sindano hiyo kwenye mdomo wake na kuisindikiza na ngumi kali ambayo ilimfanya mwanaume huyo kuimeza sindano hiyo kwa lazima. Alihangaika sana akiwa anapiga kelele lakini aliishia kujichomeka kwenye nondo ambayo ilikuwa ukutani akiwa anakimbia kimbia kila sehemu kutokana na maumivu makali ambayo alikuwa ameyapata hivyo mmoja ndiye pekee alikuwa amebakia hapo.

Mwanaume huyo alijisachi kwenye kiuno chake, hakuwa na kitu zaidi ya kisu kimoja tu na hapo ndipo akakumbuka kwamba aliyekuwa na bastola ni mmoja tu ambaye alikuwa wa kwanza kufa. Aliangalia umbali wa ile bastola ilipokuwa imeangukia, hesabu ziligoma asingeweza kuiwahi maana adui yake ambaye walimfuata hapo ndiye alikuwa karibu zaidi na hiyo bastola. Njia pekee ambayo alikuwa amebakiwa nayo ni kumvamia mwanaume huyo na kisu ambacho kilikuwa kwenye mkono wake.

Alisogea nacho kwa spidi lakini mwenzake alikuwa amempigia hesabu za muda mrefu sana kwani wakati anakaribia mwanaume huyo alichomoa bastola kwenye kiuno chake kisha aliipigiza kwa nguvu kwenye buti lake kuikoki vizuri na alipokuja kuinyanyua tena, risasi sita ziliishia kwenye kichwa cha komando ambaye alikuwa amebakisha hatua moja tu kumfikia mwanaume huyo. Baada ya kuhakikisha amewaua wote sita, aligeuki sehemu ambayo bila shaka hakujua kama kuna kamera, akakitoa kitambaa ambacho kilikuwa kimemfunika uso wake.

Sura ambayo Luka Gambino aliiona ilimshtua sana. Alikuwa ni Remy Claude, mwanaume ambaye muda mchache uliokuwa umepita yeye ndiye alikuwa amempokea ili aanze kuitumikia miaka yake sitini akiwa ndani ya hilo gereza ambalo lilikuwa linatajwa kutokuwa kabisa na haki za binadamu, mtu akiwa huko hakuwa na thamani yeyote ile na wala hakuna mtu hata mmoja ambaye alikuwa anaruhusiwa kuweza kumuona eneo hilo kwa namna yoyote ile. Huo ndio ulikuwa utangulizi wa Remy kwa mkuu wa gereza la Dominic, gereza ambalo haikujulikana kwamba ni kwanini lilikuwa linamtoa machozi mwanaume huyo ambaye kwenye video alionekana kutokuwa na ubinadamu ndani yake. Huyo ndiye mtu ambaye alisisitizwa kwamba asije akamtoa kwenye hiyo minyororo bila kuwa na uhakika na usalama wake binafsi lakini pia na usalama wa watu wote ambao walikuwa wanapatikana ndani ya eneo hilo.

Mfungwa huyo alikuwa anatakiwa kuja kutoka gerezani akiwa na miaka tisini na sita kwa hukumu yake ya miaka sitini ilivyokuwa inajieleza. Remy Claude, The Menace.

SNIA HEAD QUARTERS

Nje kabisa ya mji, yalipokuwepo makao makuu ya shirika la usalama la nchi ya Tanzania, kulikuwa na kikao kizito sana ambacho kilikukwa kinaendelea. Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo madam Cleopatra Gambo alikuwa na kikao na msaidizi wake pamoja na vijana wake ambao walikuwa ni mhimu sana hususani kwa kazi kubwa ambayo walikuwa wametoka kuifanya muda sio mrefu. Alikuwa nao hapo kwa ajili ya kujadili hatua ambazo walikuwa wamezipiga na kujua ni kipi ambacho kilikuwa kinatakiwa kufuata kwenye huo mpango wao.

"Tumefanikisha kazi kubwa sana ya kuweza kumkamata mtu ambaye alikuwa anadaiwa kuwa hatari mno kwa hili taifa, maisha ya wananchi wetu yalikuwa yanayategemea maamuzi yetu magumu ili kulifanikisha hili na kwa pamoja niseme kwamba tumefanya kazi nzuri sana. Nitumie nafasi hii kuweza kumpongeza kila mmoja wenu kwa kukamilisha kazi hii na kwa sasa nawapeni likizo ya mwezi mmoja kila mtu akaitumie ndani ya nchi anayo ipenda au na familia yake. Kuna swali?" mama huyo aliyatoa maelezo yake kwa watu sita ambao walikuwa wanamwangalia mbele yake.

Mmoja alikuwa ni msaidizi wake Henry Mawenzi, huku wengine watano ambao walikuwa wamebakia ni kikundi cha kutisha ambacho hakuna mtu alikuwa anaujua uhalisia wake HOLY TRINITY maarufu kama TULIKUFA TUKIWA HAI. Hicho ndicho kikosi ambacho kilifanikisha ukamatwaji wa mwanaume aliyepata kuitwa Remy Claude, walikuwa ni vijana wapelelezi ambao walikuwa wanafanya kazi ndani ya idara ya usalama wa taifa chini ya mkurugenzi Cleopatra Gambo.

"Kiongozi mimi sioni kama kuna muda wa kupumzika, kwa sababu nina mashaka sana na kitu ambacho kimefanyika, nadhani kuna sehemu sisi hatupo sawa na kama tutakuwa sawa basi ni wazi kuna mambo tumeyafanya bila kuweza kuujua uhalisia wake na huenda kwa baadae inaweza kuwa tatizo kubwa sana kama tusipo chukua hatua stahiki mapema" msaidizi wake aliongea akiwa kama mtu ambaye hakuridhika na hatua zote ambazo zilikuwa zimefanywa mpaka kumfikisha mwanaume yule gerezani.

"Kitu gani kinakupa mashaka sana kiasi hicho bwana Henry?"

"Kuna vitu vingi sana, kwanza kwa maelezo ambayo yametolewa kwenye historia ya mtu huyu sidhani kama tungefanikiwa kumpa kiwepesi sana namna hii. Mtu ambaye tumemtafuta kwa miaka kumi bila kufanikiwa kumtia nguvuni, unahisi inawezekana vipi kumkamata kienyeji tu namna hii? Simaanishi kwamba nina wasiwasi na kazi nzuri ambazo vijana wameifanya hapana, bali najaribu kupima aina ya mtu ambaye tumemkamata na namna tulivyo mkamata na namna mambo yalivyo fanyika mpaka wakati huu"

"Bado sijaelewa pointi yako ya msingi iko wapi"

"Nahisi huyu mtu atakuwa amejikamatisha mwenyewe"

"Una uhakika kabla ya kuja hapa haujanywa hata kidogo?"

"Sijawahi kutumia pombe wala kilevi chochote kwenye maisha yangu na unalijua hilo kiongozi"

"Sasa kwanini unaanza kuongea mambo ya ajabu kama unaota? kwa uelewa wako unahisi mtu mwenye akili timamu anaweza kujikamatisha akiijua kabisa adhabu ya hatari kama ile ambayo ilikuwa mbele yake? alijua kabisa kwamba mambo yakienda mrama anapelekwa ndani ya lile gereza ambalo halizijui hata haki za wanadamu ndiyo maana wanapelekwa watu wa aina yake, kwahiyo unataka kuniambia kwamba yote hayo aliyafanya makusudi? Unaweza ukaniambia ni kitu gani hasa kimekufanya uweze kufikiria mambo kama hayo?"

"Kiongozi najua ni furaha kubwa sana kumkamata mtu wa aina hii, hili litatupa sifa kubwa sana nchini na hata nje ya mipaka ya nchi akiwemo mheshimiwa raisi lakini tumejiuliza sababu ya msingi na lengo la msingi la kumkamata mtu huyu limetimia? jibu linaweza kuwa hapana. Kumkamata huyu mtu ni jambo moja na kukamilisha malengo yetu ni suala jingine kabisa. Huyu mtu historia ya maisha yake ina kona kona nyingi sana mpaka anakuja kuwa kiongozi wa hilo genge, ukiangalia ni aina ya mtu ambaye alikuwa anachagua hata watu wa kuwaua na sio kila mtu hivyo tunaweza kusema hakuwa hatari kwa taifa bali alikuwa ni hatari kwa maisha ya watu fulani pekee, sasa swali ni kwanini?"

"Kama nadharia yangu itakuwa sahihi basi huenda bado hakuna kitu ambacho tunakijua kuhusu huyu mtu na kama tutakijua basi tunaweza kuijua sababu nzuri zaidi ya kwanini yeye aliishi maisha haya na kwanini alimuua kiongozi wa kwanza wa hilo genge kisha akaingia yeye. Hapo mnaweza kuja kuniamini kwamba huenda huyu mtu alikuwa na ajenda zake kuweza kufanya haya yote ambayo sisi tunahisi ndiyo tumeyafanya. Tunaweza kuwa tunahisi kwamba tumefanikisha kazi kumbe tunaishi kwenye mtego wake yeye na tunaifanya ni kazi yake mwisho wa siku akatugeuza sisi wajinga"

4 inaishia hapa.

Previoua Next