Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

HADITHI: BADO NINAISHI (ASHRAFU NDILO JINA LANGU)

MWANDISHI: FEBIANI BABUYA

EMAIL: [email protected] 

WHATSAPP: 0621567672

AGE: 18+

SEHEMU YA TANO

"Henry why?"

"Wakati tunaendelea na hii kesi nilikuwa nafuatilia kwenye kila hospitali hapa nchini na rekodi za majina ya watoto ambao wamezaliwa tangu uje utaratibu wa kuwasajili majina watoto ambao wanazaliwa kila siku. Hakuna mtoto yeyote ambaye amewahi kuzaliwa nchi hii anaitwa Remy Claude, ni mtoto mmoja tu ambaye jina lilikuwa linashabihiana na lake aliyekuwa akiitwa Claudia Remy lakini yeye alikuwa ni wa kike na alikufa miaka ishirini iliyopita kwa ajali ambayo alikuwa na familia yake. Ndiyo maana namtilia mashaka sana mtu huyu kwa kuhisi hata majina ambayo anayatumia sio yake ndipo inakuja hii nadharia ya kwamba huenda huyu mtu anayaishi maisha ya mtu mwingine na maisha yake sisi hatuyajui kabisa" 

"Whaaaaaat?" maelezo ya Henry Mawenzi yalimshangaza kila mtu na kumshtua sana mkurugenzi wa shirika la usalama la Tanzania. Habari ilikuwa mpya sana kwenye masikio yao kumhusu mwanaume ambaye dunia ilimtambua kama Remy Claude kiongozi wa genge la kihalifu la FIFTEEN COINS.

“Bosi najua hili jambo ni lazima limekushtua sana kwa sababu limekuwa ni ghafla mno lakini naomba unipe ruhusa yako niweze kulifanyia utafiti na muda sio mrefu nitakuja na majibu ambayo ni kamili na sahihi kuhusu uhalisia wa maisha ya huyu mtu"

"Unataka kufanya nini?"

"Nataka nimtume kijana mmoja huko gerezani akafanye utafiti juu ya hili jambo"

"Una uhakika na hiki unacho hitaji kukifanya?"

"Ndiyo bosi"

"Basi lifanye hili jambo kwa umakini sana na nitaihitaji ripoti yako. Kwa sasa naondoka inatakiwa nikutane na mheshimiwa raisi niweze kuiwasilisha hii ripoti kwake"

"Sawa bosi"

Mwanamama huyo alitoka ndani ya chumba ambacho walikuwa wanafanyia mkutano huku naye msaidizi wake akiwa anaelekea ndani ya ofisi yake kuweza kuanza kutekeleza jukumu ambalo lilikuwa mbele yake la kuanza kumchunguza Remy Claude mwanaume ambaye ilionekana kwamba maisha yake yalikuwa na utata mwingi sana"

Sehemu hiyo, kwenye vyumba vya chini kabisa ya ardhi, ndani ya chumba kimoja kizuri sana na cha siri alikuwa anaonekana mwanamke mmoja mrembo sana. Rangi yake ilikuwa sawia kabisa kuweza kuyavutia kila macho ambayo yangefika kwenye mwili wake, ngozi yake laini na rangi yake ilikuwa inamuongezea umaridadi na kumfanya aendelee kuonekana mrembo wa kufikirika vichwani mwa wanaume wengi.

Kwenye mwili wake alikuwa amevaa pajama la kulalia huku miguu yake ikiwa peku kwenye kapeti la manyoya ambalo lilikuwa linampa burudani kila akilikanyaga. Mwanamke huyo alikuwa ameketi karibu na kabati ndogo ya kisasa ambayo ndani yake walifugwa samaki wa mapambo. Licha ya kuketi karibu kabisa na kabati hiyo lakini macho yake hayakuwa hapo.

Macho yake yalikuwa pembezoni mwa hiyo kabati ambapo palikuwa na picha kubwa sana ya watu ambao walionekana kuwa kwenye mahaba mazito. Mwanamke kwenye picha hiyo alikuwa ni yeye mwenyewe lakini picha ya mwanaume ilikuwa ni picha ya Remy Claude ambayo kwa wakati huo alikuwa ameyaanza maisha ya jela tayari. Kuna mambo mengi sana yalikuwa yanaendelea kwenye kichwa cha mrembo huyo, kila alipokuwa anaiangalia picha hiyo alijikuta anachukua pombe ambayo ilikuwa pembeni yake na kuanza kuigida kwa pupa kama anakimbizwa huku akionekana kuwa na hasira sana.

"Unampenda?" sauti ambayo hakuitarajia kwa wakati huo ilipenya kwenye masikio yake kwa usahihi sana. Haikuwa sauti ngeni kwake kwa sababu alikuwa na uhakika kwamba alikuwa ni bosi wake jambo ambalo lilimshtua sana kwa sababu hakuhitaji bosi huyo aweze kujua kama yeye alikuwa anajisikia vibaya kwa sababu ya mtu huyo.

"Hapana bosi"

"Anelia nimekujua tangu ukiwa binti mdogo, acha kuniongopea. Unampenda?"

"Siwezi kusema ndiyo au hapana kwa sababu sina uhakika na jambo lolote lile. Yeye ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuniangalia mimi machoni na kunisikiliza kile ambacho mimi nilikuwa nakitaka. Yeye ndiye mtu pekee ambaye alikuwepo wakati wote ambao mimi nilikuwa naihitaji faraja ila mwisho wa siku mimi ndiye nimeyateketeza maisha yake yote"

"Unajuta kufanya hivyo?"

"Hapana bosi"

"Hivyo ndivyo unavyo takiwa kuwa. Umefanya jambo jema sana ambalo linaenda kuyaokoa maisha ya maelfu ya watanzania. Huwa sio vibaya sana kufanya jambo sahihi kwa kutumia njia mbaya hususani ya kuyatoa sadaka maisha ya mtu mmoja ili kuokoa maisha ya wengi. Taifa linakupongeza sana kwa jitihada zako za kutusaidia kufanikiwa kumkamata mhalifu mkubwa kama yeye, kwa hili hata mheshimiwa raisi atahitaji kuonana na wewe"

"Raisi ahitaji kuonana na mimi kwa sababu zipi?"

"Umefanya jambo kubwa sana unastahili kupongezwa hivyo mimi naenda kuonana naye na baada ya hapo nafikiri siku yoyote utaalikwa Ikulu"

"Mpaka lini nitaendelea kuishi hivi bosi?"

"Kwa sasa watu hawatakiwi kujua kama wewe upo hai kwa sababu kwenye kila taarifa tumeacha kiulizo juu ya jambo hili ili watu wasiwe na cha kuongea kuhusu wewe"

"Kwanini?"

"Kama wakijua upo hai inaweza kuwa hatari kwenye maisha yako kwa sababu hatujui ni nani na nani ambao huenda walikuwa na huyu mtu kwa siri hivyo kama habari zikija kuvuja kuhusu wewe basi unaweza kuwa kwenye mazingira hatarishi kitu ambacho mimi binafsi siwezi kuruhusu kiweze kufanyika nikiwa kama kiongozi wa usalama wa taifa"

"Asante sana kwa kujali uwepo wangu"

"Kwa sasa ukikutana na raisi utahitajika kwenda nje ya nchi kwa muda mpaka pale nitakapo kupatia taarifa ya kuweza kurejea tena nchini"

"Sawa bosi" mwanamama huyo baada ya kuongea na mwanamke Anelia Baton ambaye ndiye alifanikisha kwa ukubwa sana zoezi la kukamatwa kwa Remy Claude alitoka ndani ya hicho chumba na kuondoka huku akimuacha mwanamke huyo kwenye msongo mkubwa sana wa mawazo. Alificha ficha sana mbele ya bosi wake lakini ukweli macho yake yalikuwa yanazungumza na kumsuta kwamba alikuwa amempenda sana mwanaume huyo licha ya kumsababishia matatizo ambao huenda yangemfanya maisha yake yote aweze kuishia kwenye nondo za jela.

"Hivi haya ambayo yalikuwa yanaongelewa hapa yana uhalisia wowote ule?" Suzane ambaye alikuwa kiongozi wa kundi hilo hatari la TULIKUFA TUKIWA HAI aliuliza akiwa anawageukia wenzake kwa macho ya viulizo sana.

"Kazi yetu ilikuwa ni kuliteketeza genge la mtu yule na kumkamata yeye basi hayo mengine sisi sidhani kama yanatuhusu" alijibu mwanaume mmoja ambaye kwenye mkono wake alikuwa anamenya chungwa ila wenzake walimpotezea.

Sehemu ya tano inafika mwisho.

Febiani Babuya.

Previoua Next