CHANGE
A Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA KWANZA
★★★★★★★★★★★★★★
Ni usiku usiojulikana saa, giza ni zito haswa, ndani ya eneo lililo na uoto mwingi wa asili. Kuna mtu anakimbia ndani ya eneo hili, kukimbia kwake ni kwa njia ya woga mwingi alionao kwa sababu anakimbia ili kuokoa uhai wake. Lakini hawezi kuona vizuri mbele kwa sababu ya giza, naye anaanguka mara kwa mara kwa sababu ya kuhisi uchovu mwingi, maumivu mengi, na kizunguzungu kizito kichwani kwake. Anajaribu hata kupiga kelele, lakini anashindwa kwa kuwa mdomo wake unadondosha damu nyingi sana. Hana ulimi. Mtu huyu ni binti mdogo mwenye miaka kumi na kitu tu, naye amejikuta ndani ya janga ambalo akili yake inatamani lingekuwa ni ndoto mbaya tu, lakini anaelewa wazi kwamba siyo ndoto, na kifo kiko nyuma yake. Anajaribu kuokoa uhai wake ingawa anaelewa wazi kwamba anachokikimbia, yaani kinachomfuata, kiko karibu naye sana, lakini ni kama kinafanya mchezo pamoja naye kwa kuwa kinajua hawezi kufika mbali.
Hatimaye nguvu zinamtoka kabisa binti huyu, naye anaanguka chini na kubaki amelala tu huku akihisi ni kama kuna vitu vizito vimemlemea kwenye mwili wake, na hawezi tena kujongea. Anafumbua macho na kuyafumba kwa uzito sana, na kwa sekunde hizo chache, anahisi mwili wake ukishikwa sehemu ya kiunoni na kugeuzwa taratibu, ili awe kama amelala chali. Amelegea mno, akiona vitu mara mbili-mbili kama vile macho yenye makengeza yanavyoona. Kilichokuwa kimesimama katikati ya mwili wake uliolala chini hakikuwa kitu cha kibinadamu kabisa, na ingawa msichana huyu aliogopa sana, alikuwa amechoka mno kuonyesha hilo.
Kiumbe hiki kilisimama tu na kumwangalia kwa njia ya kikatili sana. Msichana huyo alipopata nafasi moja tu ya kukiona usoni ingawa ilikuwa gizani, aliona namna ambavyo macho ya huyo kiumbe yalikuwa mekundu na yenye lenzi zilizofanana na zile za macho ya nyoka mwenye sumu, na mdomo wake ulikuwa umechanika pande za pembeni kuruhusu meno makali na mengi sana yatokeze nje huku yakidondosha udende mzito wa damu nyeusi. Kisha likaanza kuupanua mdomo wake huku likitoa sauti ya kukwaruza kwa chini, halafu ghafla likaishika miguu ya msichana huyo na kuanza kumburuza kurudi upande aliokuwa ametoka, na kisha kutokomea naye gizani.....
★★★★
Moja kwa moja mpaka ndani ya jiji kuu; jiji kubwa sana kimaendeleo nchi nzima. Kama kawaida ya majiji makubwa, sikuzote huwa hakukosekani jambo fulani muhimu kwenye taarifa za habari, iwe kubwa au dogo, ni lazima tu liwepo. Wakati huu, kulikuwa kumetokea ajali mbaya sana siku ya Jumamosi, iliyohusisha gari kubwa la kubeba mizigo na basi dogo la abiria (Costa), iliyosababisha vifo vya watu 17 na kuwajeruhi wengine 36; hiyo Costa ilikuwa imejaa, siyo mchezo. Taarifa za maafa hayo zilisambaa upesi, na hata baadhi ya watu walikuwa wamechukua video eneo la tukio kwa simu zao na kuanza kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii, na ndipo zikawafikia watu wawili muhimu sana ndani ya kisa hiki.
Blandina Sospeter. Mwanamke mrembo mwenye umri wa miaka 30. Sura na umbo zuri ni kati ya vitu vinavyomfanya mwanamke atamanike, lakini Blandina hakuwa tu na sura na umbo zuri, bali akili nyingi pia. Alikuwa na urefu wa wastani tu kawaida ya mwanamke, yaani si mfupi si mrefu sana, mwenye ngozi laini ya rangi ya maji ya kunde. Mwili wake ulikuwa umenawiri vya kutosha lakini hakuwa mnene sana, bali alibeba mapaja manono na hips zilizochoreka vyema kila mara alipovaa nguo zilizoubana mwili wake. Alikuwa na kalio kubwa vya kutosha hata kutikisika sana kwa nyuma endapo angevaa kijora, na alikuwa na sura nzuri, fupi yenye midomo mizuri, macho madogo kiasi kama ya mchina wa Tanzania ya mbali, na alipendelea kusuka nywele za rasta ndefu au zenye muundo kama nywele laini za wazungu. Alijua sana kupendeza.
Kisha tunakuja kwa Namouih Donald Masoud. Ukisikia wale wanawake wanaoukaribia uzungu wa kiarabu au kihindi kwa mionekano yao, ndiyo alikuwa huyu sasa. Namouih alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 32. Alikuwa mrembo ajabu. Alikuwa mrefu, yaani urefu unaopita urefu wa kawaida kwa mwanamke, na alikuwa na ngozi nyeupe sana. Siyo kwamba labda alizaliwa kama chotala, hapana, ni kwamba tu ngozi yake ilikaribia weupe wa uzungu, na hata jinsi alivyoonekana usoni ilikuwa kwa njia hiyo pia ingawa wazazi wake wote walikuwa ni wazawa. Umbo lake lilikuwa zuri, akiwa siyo mnene wala siyo mwembamba sana, na hips zake zilinawiri na kutokeza mlima mnene kiasi huko nyuma uliofanya mwonekano wake wa kike uvutie zaidi. Usoni alikuwa mrembo mno; macho yenye mchanganyiko wa uarabu na uchina fulani hivi, na alikuwa na nywele ndefu na laini, ambazo mara nyingi alizibana au kuzisukia mitindo tofauti, na angeziachia kama angekuwa nyumbani. Kwa ufupi ni kwamba hawa wanawake kwa pamoja walibarikiwa kwa uzuri.
Namouih na Blandina walikuwa kama mapacha waliozaliwa na mama tofauti. Walikuwa marafiki wa karibu, wa karibu sana, tena kwa muda mrefu mno. Walikutana chuoni, na hasa kwa sababu wote walifuatilia aina moja ya kozi, kifungo chao cha urafiki kiliendelea kuimarika mpaka walipokuja kumaliza chuo na kuanza kazi. Wote walikuwa wanasheria. Lakini kulikuwa na utofauti baina yao katika ngazi zao kikazi, yaani, Namouih alimzidi Blandina cheo katika nyanja za utumishi ndani ya uanasheria. Namouih alikuwa mwanasheria mkuu (attorney), ilhali Blandina alikuwa mwanasheria wa kadiri/msaidizi wake (paralegal). Hii inamaanisha kwamba kuna mambo ambayo Namouih angeweza kufanya lakini kwa Blandina yalikuwa na mipaka, ingawa bado naye angeweza kutimiza majukumu mbalimbali ya kisheria kwa kusaidizana na rafiki yake. Kwa mfano, ikiwa kungekuwa na kesi, cheo cha Blandina kilimruhusu yeye kufanya kazi kama vile kuwasiliana na watu wao wa kesi ili kuwapa taarifa mbalimbali na kupitia taarifa zao, kuzipangilia, kutayarisha mambo yanayohitajika katika kesi, kuwahoji watu wao wa kesi na mashahidi, na kumuunga mkono mwanasheria wake mkuu katika kazi anazochukua na kuendesha mahakamani. Namouih akiwa kama mwanasheria mkuu, yeye alikuwa na uwezo wa kufanya mambo yote hayo kama Blandina, lakini vitu kama kuwapa ushauri wa moja kwa moja wa kisheria watu wao wa kwenye kesi, kukubali au kukataa kupokea kesi, kuwasimamia watu kwenye kesi mahakamani, na kusema kiwango cha malipo wanayotaka ili kusimamia kesi ya mtu, ni mambo ambayo yeye peke yake ndiye angeweza kushughulikia, na si Blandina.
Ingeweza kusemwa Namouih alikuwa kama "boss" kwa Blandina, ingawa Namouih hakumwona kama mfanyakazi wake bali kama msaidizi wake wa karibu sana. Na alipenda sana kufanya kazi pamoja naye kwa sababu walitoka mbali na bado hawakuwa wameachana mpaka kuanza kufanya kazi kwenye kampuni kubwa ya kibinafsi; Namouih akiwa ndiyo mwanasheria mkuu hapo. Kipato walichokipata kilikuwa kizuri, na wao ndiyo waliozitegemeza familia zao zilizoishi mikoa tofauti-tofauti.
Blandina alikuwa mwanamke mchapakazi, mbunifu, na mchangamfu sana. Alipenda kujiachia na kula bata kila mara aliyopata nafasi, kwa kuwa alikuwa na sera ya kibinafsi ya kwamba maisha ni mafupi hivyo ni bora kuyaishi kwa kujifurahisha. Siyo kwamba hakuishi kwa akili, ila angalau alijua kuponda raha. Alipenda sana watu wenye tabia na mionekano mizuri, siyo kumaanisha alikuwa mbaguzi lakini, hivyo alikuwa mwenye kupendeka sana. Tofauti naye kiasi, Namouih alikuwa mkali. Yaani hakupenda michezo ya kijinga-kijinga kabisa, na sikuzote alitaka kuhakikisha mambo yanafanywa kwa mpangilio na ukamili. Hiyo haikumaanisha kwamba hakupenda kujifurahisha, ni kwamba tu akili yake sikuzote ilikazia fikira mambo muhimu kwanza kabla yake yeye mwenyewe, hivyo alikuwa na utu wa kivyake mno kama vile haijali dunia inayomzunguka. Ni akili yake nyingi na umakini wa hali ya juu ndiyo vitu vilivyomsaidia asiwahi kupoteza kesi hata moja tokea alipoanza mlolongo wake wa uanasheria (career). Alipenda hasa kushughulika na kesi zilizohusisha mambo kuelekea haki za wanawake na watoto, ingawa mara nyingine alichukua kesi za mambo mengine, na zote alishinda. Na ni Namouih pekee ndiye aliyekuwa ameolewa, tena na mwanaume mwenye pesa sana, na aliyempenda mno.
Sasa, siku hii ya Jumamosi baada ya taarifa za tukio lile la ajali kusambaa, ikawa imefika kwa utambuzi wa wanawake hawa kwamba mmoja wa rafiki zao alikuwa ameathiriwa na hiyo ajali. Yaani, rafiki yao mwingine mwanamke aliyeishi maeneo ambayo ajali hiyo ilitokea, alikuwa ameathiriwa nayo kwa sababu mume wake na mtoto wake walikuwa miongoni mwa abiria ndani ya Costa iliyogongwa, nao walijeruhiwa vibaya sana na kuwahishwa hospitalini. Rafiki yao huyo aliitwa Mwantum Ramadhan, ambaye walisoma pamoja naye chuo kipindi cha nyuma ingawa kwa kozi tofauti. Hivyo wakawa wamewasiliana naye na kumpa pole kwa yaliyotokea, nao wakamwambia wangekwenda huko siku ya kesho ili kuwa pamoja naye na kumpa faraja. Blandina, akiongea na Namouih baada ya kumaliza mawasiliano na Mwantum, alimsifu sana Mungu kwa kuwaepusha watu wa familia ya rafiki yao na kifo katika ajali hiyo, na Namouih akamwambia Blandina hayo yalikuwa ni mambo yasiyotazamiwa tu na wala si mipango ya Mungu, kwa kuwa bado kuna watu waliokuwa wakiomboleza vifo vya wengine kwenye ajali hiyo hiyo. La muhimu lingekuwa tu kutoa mchango wao katika kuipatia faraja familia ya Mwantum kwa ujumla.
Wakakubaliana kukutana kesho asubuhi ili kuondoka kwa pamoja kuelekea kule kwa rafiki yao.
★★★
Ni Blandina ndiye aliyempitia Namouih asubuhi ya saa mbili ili waianze safari. Mwanamke huyu alikuwa na gari zuri jeupe aina ya Toyota Crown, na kwa sababu wangeondoka wakiwa pamoja, Namouih hakuona haja ya kuendesha gari lake mwenyewe, hivyo akaingia kwenye hilo la Blandina na wote kuondoka. Nyumba yake Namouih ilikuwa kubwa na ya kifahari sana, naye Blandina akawa anamwambia namna ambavyo siku moja atakuja kununua kubwa zaidi ya hiyo; huku na maongezi mengine yakiendelea.
Wawili hawa walikuwa wamepanga kupita kwenye duka kubwa jijini ili kununua vitu kadhaa kwa ajili ya kumpelekea Mwantum na wagonjwa, hivyo wakafika kwenye sehemu iliyokuwa na jengo kubwa la soko la kisasa (mall), nao wakaenda ndani huko kuanza kutafuta bidhaa walizohitaji. Blandina alivaa suruali ya kubana ya rangi ya khaki, blauzi nyepesi yenye rangi nyeusi na viatu vya kike vya masai, huku akizibana nywele zake za rasta juu ya kichwa na usoni akivalia miwani ya urembo. Namouih yeye alibana nywele zake kwa mtindo wa kuacha njia kadhaa kichwani ili ziunde kama matuta-matuta mazuri sana, na alivaa gauni fupi lenye kubana la samawati, lililooshia magotini kwake. Sehemu za ngozi yake nyeupe zilizoonekana zilivuta macho ya wengi waliovutiwa na urembo aliobarikiwa kuwa nao. Blandina alipenda sana kujua kwamba waliua macho ya wengi, ingawa Namouih hakukazia sana fikira mambo hayo.
Wakiwa wanatoka ndani huko sasa kuelekea nje kwenye gari baada ya kununua vitu walivyohitaji, Blandina akawa anaongea na Namouih kwa utani kuhusu namna ambavyo mhudumu mmoja alikuwa anakosea kulisema jina la rafiki yake baada ya kulisoma. Namouih alikuwa ameandika jina lake kwenye karatasi ya cheki aliyompatia mhudumu huyo kwa ajili ya malipo, naye akawa analitamka kwa kumwita "Namoi" badala ya kulitamka "Namuuy" kama ilivyotakiwa, hivyo Blandina akawa anamwita rafiki yake "Namoi" ili kumuudhi. Namouih yeye alikuwa ameshamzoea rafiki yake kupenda kumchokonoa sana, hivyo akawa anamwacha tu aendelee na masihara yake. Walipofika eneo la nje ya hilo soko, Blandina akapamiana ghafla na mtu mwingine ambaye hakuwa amemwona akija upande wake. Walipamiana kwa nguvu sana kiasi kwamba Blandina akaweweseka na kudondosha mifuko ya vitu alivyonunua, lakini hakuanguka kutokana na mwili wa Namouih kumkinga. Sauti za vifaa vilivyokuwa ndani ya mifuko zikasikika, na ikawa wazi kwa haraka sana kwamba kuna kitu kilipasuka.
"Oh... sor... samahani... samahani sana dada..."
Blandina akamtazama mtu huyo aliyepamiana naye na kubaki amemwangalia tu kama anamshangaa. Namouih naye akamtazama kwa kuudhika sana. Alikuwa mwanaume kijana, mrefu kumpita Namouih kiasi, na mwenye mwili mpana uliojengeka kiume. Alivalia T-shirt ya rangi ya blue-nyeusi, kaptura fupi kufikia magotini, na viatu vyeupe kama raba. Shingo yake ilizungushiwa "headphones" nyeupe, na alionekana kuwa mtu wa mazoezi kwa sababu kifua chake kilikuwa kimetuna na hata T-shirt yake kumbana hasa kuzunguka mikono yake imara. Lakini Blandina alikuwa akimwangalia zaidi usoni. Alikuwa na sura nzuri; ndevu hafifu kutokea kwenye timba zilizochongwa vizuri, na macho yake hasa ndiyo yaliyomvutia haraka mwanamke huyu, yaani Blandina. Nywele za kichwa cha mwanaume huyu zilikuwa fupi kwa kukatwa sawa kichwa kizima, laini za kubrashi. Alikuwa na ngozi iliyoonekana kuwa kama weupe ulioukimbia weusi. Na kama ni kitu kingine ambacho kiliinyakua haraka akili ya Blandina kumwelekea jamaa, basi ilikuwa ni harufu yake. Alinukia vizuri sana.
Mwanaume huyo akachuchumaa na kuanza kujaribu kukusanya vitu vilivyokuwa vimeanguka. "Pole sana dada..." akasema hivyo.
"Hivi kweli jamani watu mnashindwa kuangalia mnakoenda!" Namouih akaongea kwa ukali.
"Samahani yaani...."
Mwanaume huyo akasema hivyo, na ni hapo ndiyo akawa ameishika chupa ya chai ikiwa imepasuka mtungi wake wa ndani.
"Umeona sasa! Tayari umemtia hasara mtu kwa sababu tu ya kuwa careless," Namouih akasema.
Mwanaume huyo akamtazama Namouih kutokea chini hapo kwa umakini.
"Basi Nam, inatosha, haina shida," Blandina akasema.
"Haina shida?" Namouih akamuuliza.
Mwanaume huyo akasimama na kusema, "Nimemwomba samahani, siyo kwamba nimefanya makusudi. Ilikuwa tukio baya."
"Tukio baya wapi, kwani kuna giza sasa hivi? Na samahani inasaidia nini wakati umemvunjia vitu vyake vipya kabisa?" Namouih akamuuliza.
"Nam!" Blandina akamwita kumzuia.
"Kwa hiyo ukinilalamikia hivi vitu ndiyo vitarudi kuwa vipya?" mwanaume huyo akamuuliza kwa uthabiti pia.
Kuna watu kadhaa walikuwa wameanza kusimama na kuangalia kisa hiki kilichoongezeka utata.
"Mtu umemtia mtu hasara halafu bado unajifanya mkali," Namouih akamwambia.
Blandina alikuwa ameshindwa hata kusema lolote na kubaki kumtazama tu mwanaume huyo.
"Dada, naomba samahani tena. Hii chupa si umeinunulia huku?" akamuuliza Blandina.
"Ndiyo, lakini usi...."
"Hapana, tafadhali nisubiri nikakuchukulie mpya. Nakuja sasa hivi," mwanaume huyo akasema kwa ustaarabu.
Kisha akaelekea ndani kule kwenye maduka, akionekana kuharakisha.
Blandina akamwangalia Namouih na kumuuliza, "Hivi mbona nawe unakuwa hivyo?"
"Nakuwaje? Mtu kakutia hasara halafu unaendekeza unyonge?" Namouih akamjibu.
"Hata kama, usiwe mkali kihivyo bwana. Kaka mwenyewe anaonekana mstaarabu tu."
"Mh... Yaani wewe nimeshakusoma, hauna lolote. Ustaarabu, ustaarabu gani ananifokea wakati yeye ndiyo mwenye dhambi? Ah-ah..." Namouih akaongea kwa kuudhika.
Blandina akaangalia upande ule alikoelekea jamaa, lakini hakumwona.
"Huyo kashakimbia dada, umeliwa. Hapa kilichopo turudi huko ndani tununue nyingine, maana hatuwezi...."
"Huyo hapo anakuja," Blandina akamkatisha.
Namouih akatazama huko na kumwona jamaa akija huku ameshikilia mfuko mdogo uliobeba kitu, bila shaka chupa.
"Siyo kila mtu yuko kama unavyofikiria dada yangu," Blandina akamwambia Namouih.
Namouih akamnyakua Blandina funguo za gari na kuondoka tu hapo akionekana kuudhika, naye akatangulia kwenye gari akimwacha Blandina anamsubiri "kaka mzuri." Mwanaume huyo alipomfikia Blandina, mrembo wetu akaachia tabasamu hafifu, naye akapewa mfuko huo uliokuwa na chupa aina kama ile ile iliyopasuka.
"Samahani tena, eti?" mwanaume huyo akamwambia kiupole.
"Usijali, ondoa shaka kabisa kaka'angu," Blandina akamwambia.
"Hiyo utahitaji kuitupa, siyo? Leta nitakusaidia kuiwe...."
"Hapana usijali. Nitaitunza tu kama kumbukumbu," Blandina akamkatisha.
Mwanaume huyo akatabasamu huku akimwangalia kwa njia iliyoonyesha kwamba hakuwa amemwelewa vizuri.
"Naitwa Blandina," akajitambulisha huku akitabasamu.
Mwanaume huyu kijana akatulia kidogo, kisha akasema, "Naitwa Draxton."
"Draxton. Jina zuri sana, kama wewe," Blandina akaanzisha uchokozi.
"Ahah... okay. Aa... nisikucheleweshe, tafadhali unaweza tu ku...."
"No, hapana, haunicheleweshi. Kiukweli, ningependa kama hii haingekuwa mara ya mwisho tunaonana... kama ikikupendeza," Blandina akamwambia, huku akimtazama kwa macho fulani hivi ya uvutio.
Mwanaume huyu akamwangalia kwa ufupi, kama vile anatathmini maneno ya mwanamke huyo, kisha akatazama upande mwingine na kumwangalia tena.
"Okay. Ungependa kuniona lini tena?" Draxton akamuuliza.
Blandina akacheka kwa haya kiasi, kisha akasema, "Unaonaje nikikupa namba?"
Bila hata kutoa jibu, jamaa akachukua simu yake kutoka mfukoni mwa kaptura na kumpatia Blandina ili aiandike namba yake mwenyewe. Blandina alikuwa akifurahi sana, lakini hakutaka ionekane kupita kiasi. Akamaliza kuandika na kumrudishia jamaa simu.
"Utani-text?" Blandina akauliza.
"Sure," Draxton akajibu kwa njia ya kawaida tu.
Alionekana kuwa aina ya mwanaume makini sana, na ni moja kati ya mambo mengi yaliyomvutia Blandina haraka. Mwanaume huyo akaanza kurudi nyuma taratibu huku akimwangalia Blandina kwa umakini, naye Blandina akawa ameibana midomo yake huku akimtazama pia. Jamaa akageuka na kuanza kuelekea upande mwingine akimwacha Blandina anamsindikiza kwa macho, kisha naye akaelekea mpaka ndani ya gari lake na kumkuta Namouih akiwa amekaa kwa kumsubiri.
Blandina alipomwangalia tu, Namouih akasema, "Tafadhali, please, na tafadhali sana, naomba usiniambie lolote kuhusu...."
"He's so hooot!" Blandina akamkatisha kwa kusema hivyo.
"Naomba uwashe gari twende," Namouih akaongea kwa kuudhika.
"Hahahahah... honey! Hilo HB limetokea wapi?" Blandina akauliza.
Namouih akabaki kimya tu.
"Ahahahah... Namoi bhana, unayumba sana. Mwenzio nimeombwa na namba on the first go, chezea msupu huu wewe!" Blandina akajisifia.
"Nimekwambia usiniambie, mtajuana wenyewe. Mtu mwenyewe hayuko care utakuja kumwingiza kwako ndani ya sekunde mbili nyumba imeungua," Namouih akasema.
"Anaitwa Draxton. Yaani unalitamka kizungu baby 'Drax-ten.' Aaah... walahi hapo najua sijakosea," Blandina akaendelea kuongea huku akiwasha gari.
Namouih akabaki tu kimya kwa kuwa alijua ikifika kwenye suala la wanaume Blandina alikuwa haambiliki.
"Halafu amesema nikwambie una bichwa kubwa," Blandina akamwambia kiuchokozi.
Namouih akamkata jicho kali sana, kisha akasonya na kuangalia pembeni huku akiwasha simu yake, kitu kilichofanya Blandina acheke sana. Akaligeuza gari kutoka hapo na kuwaondoa eneo hilo huku akiendelea kumchokonoa Namouih kama kawaida yake.
★★
Baada ya mwendo wa zaidi ya dakika arobaini, marafiki hawa wawili wakawa wamefika kwenye hospitali ambayo mume na mtoto wa rafiki yao wa karibu walikuwa wamelazwa. Walitakiwa kuivalisha miili yao khanga kwa chini ili kuwa na mwonekano wenye kusitirika kwa taratibu za hospitali, nao wakavaa na kuelekea kule ndani. Mume wake Mwantum aliitwa Selemani, na mwanaye aliitwa Islam. Blandina na Namouih walikuwa wamejitahidi kufika huko muda ambao hospitali ingeanza kuruhusu watu kuingia ili kuwaona wagonjwa, nao wakamtafuta Mwantum na kufanikiwa kumpata. Mwanamke huyo alikuwa pamoja na watu wachache wa familia yake hapo na marafiki waliofika kuwatembelea wapendwa wake, naye akaingiwa na simanzi baada ya kuwaona Namouih na Blandina mpaka akaanza kulia. Namouih na Blandina wakampa pole kwa kumkumbatia kwa pamoja, kisha wakaketi naye na kuanza kumtia moyo. Kwa sababu ya tukio lile la ajali kuwa kubwa, sehemu hiyo ilikuwa na watu wengi, na hata baadhi ya watu kutoka kwenye vyombo vya habari walikuwa hapo pia, na ilisemwa kwamba Waziri Mkuu wa Serikali alikuwa njiani kuja huku kufanya uzuru na kutoa pole zake pia.
Hazikupita dakika nyingi sana na mtu mwingine ambaye alikuwa ni rafiki ya wanawake hawa watatu akawa amefika. Huyu alikuwa ni mwanaume hodari, aliyefanya kazi ya upelelezi kwa masuala ya kiaskari, naye aliitwa Felix Haule. Alikuwa mrefu kuufikia urefu wa Namouih, mweusi, mwenye mwili imara na mpana, naye kwa wakati huu alivalia kwa unadhifu kama mtu wa ofisini. Alifika hapo pamoja na chakula kidogo na vifaa kadhaa alivyonunua kwa ajili ya kumletea Mwantum na wagonjwa. Namouih na Blandina walijua kwamba Felix angekuja, nao wakaridhika baada ya kumwona. Wanne hawa kwa pamoja walisoma chuoni, na kabla ya kuachana miaka mingi baadaye walikuwa wamejenga urafiki wa karibu sana, kwa hiyo walipendana mno. Mwantum ndiye aliyekuwa wa kwanza kufunga ndoa kati yao wote, kisha Felix, halafu Namouih, na sasa alikuwa amebaki Blandina tu. Felix alikuwa na watoto watatu, na alikuwa na umri wa miaka 37.
Wakaingia ndani ya chumba alicholazwa Selemani, ambaye alikuwa amevunjika mguu na kuwekewa muhogo, na bendeji nene kuzungukia kichwa chake, huku usoni akivimba sana kwa kujeruhiwa vibaya, nao wakampa pole ingawa hakuweza kurudisha shukrani kwa mdomo. Wakaonyeshwa na Islam pia. Mtoto huyo mwenye miaka 13 alikuwa ameumia ubavuni na kuwekewa muhogo mkononi pia, huku shingoni akizungushiwa bendeji nene kuzuia maumivu pindi ambapo angeigeuza, nao wakampa pole na kumwachia zawadi nyingi. Baada ya saa za kuwaona wagonjwa kuisha, Namouih, Blandina, Felix na Mwantum wakatoka pamoja kwenda nje kupata chakula kidogo kwenye mgahawa mmoja.
Mwantum alikuwa na miaka 34, mwanamke mwenye mwili mnono uliokaribiana na wa Blandina, mweusi wa maji ya kunde, na kwa ukawaida alivalia nguo zenye ushungi wa kuzungushia kichwani kama hijab. Alikuwa mstaarabu tu, na alifanya kazi mbalimbali zilizohusiana na masuala ya mitindo kuanzia ushonaji wa nguo mpaka upambaji wa shughuli kubwa kubwa. Yeye hakusomea mambo magumu magumu kama wenzake, lakini alikuwa na kichwa chepesi na mchapakazi. Alifurahi sana kuwa pamoja na hawa rafiki zake ijapokuwa ulikuwa wakati mgumu sana kwake, naye akawashukuru sana kwa msaada wao wote waliompatia. Walikuwa wamempa kiasi kingi sana cha pesa kwa ajili ya kumtegemeza angalau, nao wakasema wangeendelea kuwa pamoja naye bega kwa bega. Yeye Mwantum akawa ameshiba sasa na kusema angerudi kule ndani, na marafiki zake wakamwambia wangeendelea kuwa hapo mpaka muda wa kuruhusiwa kuwaona wagonjwa tena ili waweze kwenda ndani ya hospitali pia.
Mwantum akanyanyuka na kuelekea hospitalini tena, na sasa Felix, Namouih na Blandina wakaendelea kula taratibu na kushushia juice huku wakiongelea masuala ya kikazi.
"Nyie wapelelezi mna jipya gani?" Blandina akamuuliza Felix.
"Hakuna jipya wala. Kila kitu doro tu," Felix akasema.
"Vipi ile ishu uliyosema mmeifatilia kwa muda mrefu? Mlifanikiwaga?" Namouih akauliza huku akinywa juice.
"Hamna, bado Namouih. Huwezi kuamini yaani mpaka leo bado tunachunguza tu, halafu inazidi kuwa...." Felix akaishia tu hapo na kuendelea kula.
"Inazidi kuwa nini? Mbaya?" Namouih akauliza.
Felix akatikisa kichwa kukanusha huku akitafuna tonge kubwa.
"Ni ishu gani?" Blandina akauliza.
"Hakuwahi hata kuniambia ni nini, alisema tu ni ngumu saaana..." Namouih akasema.
"Si useme na we' naye," Blandina akamwambia Felix.
"Ah, potezea hiyo bwana. Nyie niambieni. Duo ya wanasheria mahiri mkoa mzima. Mnapiga kesi gani sa'hivi?" Felix akawauliza.
"Ya ubakaji," Namouih akasema.
"Kwa hiyo mnashughulika nayo kwa pamoja wakati huu?" Felix akauliza.
"Yeah, yaani mizungusho mingi kweli lakini ingetakiwa kuwa imeisha siku ya kwanza tu... Namouih yeye anataka iendelee, si unajua anavyopenda anasa za kesi," akasema Blandina.
"Siyo hivyo bwana, ila nataka tu challenge maana mpaka leo hakuna aliyeni-beat, na hii tutashinda tu so... kidogo inaboa ingawa ni nzuri," Namouih akasema.
"Aahahah... ni ya nani?" Felix akauliza.
"Kuna msichana amebakwa... tena na mtu aliyekuwa boyfriend wake," Blandina akasema.
"Mh? Kivipi?" Felix akauliza.
"Yaani... waliachana, kwa njia ya kuzinguana, ndiyo jamaa akamlala kinguvu. Afu' ukimwona ni mdogo tu anaonekana mstaarabu huwezi dhani anaweza kufanya kitu kibaya namna hiyo kabisa. Ila sura hazitudanganyi sisi... anakula miaka 30 jela," Namouih akamwambia.
"Halafu unajua haya mambo yenu huwa nayapenda sana lakini yananichanganya... em' nielezeeni hizo process zinaendagaje," Felix akawaambia.
"Zinaendagaje... hahahahah kwa kisukuma zaidi..." akasema Blandina.
"Wewe hautaki kutuambia mambo yenu halafu unataka maelezo ya mambo yetu?" Namouih akamuuliza Felix.
"Ni kaujuzi tu kidogo bwana, acha kubania. Ya kwetu mazito mno... na top secret," akasema Felix.
"Ahah... haya bwana. Mwambie paralegal wangu akuelezee," Namouih akasema huku akiendelea kula.
Felix akamtazama Blandina.
"Sawa nitakuelezea. Kwa shi'ngapi lakini?" Blandina akamuuliza Felix.
"Elezea kwanza, hela ipo tu," Felix akasema.
"Okay. Yaani, mtu akishakamatwa kama hivyo anapelekwa kwa jaji. Jaji anamwelezea mashtaka yake na kwamba kama hawezi kugharamia mwanasheria, basi atapewa mmoja ili amsaidie. Baada ya hapo ndiyo tunaingia kwenye hiki kitu kinaitwa preliminary hearing, yaani mahojiano ya awali, au niseme usikilizwaji kesi wa mwanzo kabisa. Hapo jaji anasikiliza ushuhuda kwa mashahidi na ushahidi uliopo kutoka pande zote za wanasheria. Jaji akiona kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha mtuhumiwa amefanya maovu, ndiyo tunaingia kwenye kitu kinaitwa trial sasa..." Blandina akaeleza.
"Eeeh kwenye kurushiana maneno haswa..." Felix akasema.
"Ahahah... kama mahakama ndogo hakijaeleweka inapelekwa mahakama kuu. Lakini kabla ya siku ya trial, jaji anasema tarehe ambayo mtuhumiwa atasomewa mashtaka tena, ili achague kujitetea ikiwa anaona hana hatia, au kama atakubali ana hatia. Hiyo tunaiita arraignment..." Blandina akaendelea kueleza.
"Eh, hapo umeniacha... areement..." Felix akasema.
"Ahahaah... ni arraignment..." Namouih akamwambia.
"Okay... n'taicheki kamusini. Kwa hiyo... kama tuseme mtuhumiwa akikubali ana hatia kwenye hiyo arraignment... nini kinafanyika?"
"Trial inaahirishwa. Jaji atasema tarehe ambayo mtuhumiwa atapelekwa mahakamani kusomewa hukumu kutokana na kile kilichopatikana kufikia hapo..." Blandina akasema.
"Hiyo ndiyo mnaita sentence..." Felix akaongea.
"Pigia mstari..." Namouih akasema.
"Na mnapoingia trial ndiyo kwenye majibizano sasa... napendaga sana hiyo, full drama," akasema Felix.
"Yeah, sasa... huyu kijana aliyebaka, anaitwa Japheth, alikuwa amepewa mwanasheria kutoka serikalini amsaidie. Ushahidi tuliokuwa nao sisi una nguvu, lakini kwenye tarehe ya arraignment akatoa plea ya kwamba hana hatia, kwa hiyo tunaenda trial... kwenye majibizano huko. Sasa mwanasheria wake ghafla tu sijui amefanyaje eti sijui kameza kijiko... hataweza kumsimamia, mambo ya dharura, kwa hiyo anapaswa kuchukua mwanasheria mwingine. Anataka mwanasheria ambaye atamtetea ili ashinde maana amekazania kusema hana hatia, lakini kila mtu anajua hiyo haiwezi tokea... kwa hiyo mpaka sasa hivi tunasubiri trial hajampata mwanasheria mwingine," Blandina akaeleza.
"Si ulisema jaji anaweza kumpa wa serikalini?" Felix akauliza.
"Ndiyo hataki sasa huyo kijana. Anafikiri akipewa yeyote tu atashindwa, so anataka atakayemsaidia kushinda," Namouih akasema.
"Heh... kwa Namouih ni kugonga mwamba tu hata akimtoa mwanasheria Marekani," Blandina akaongea.
"Na ndiyo challenge nayotaka, sema haiji," Namouih akasema na kuwafanya wote wacheke kidogo.
"Haya hela yangu..." Blandina akamwambia Felix.
Felix akatoa elfu kumi na kumpatia Blandina, naye Blandina akaanza kujipepea nayo.
"Kinapenda hela hiki," Felix akasema huku akila.
"Ndiyo sehemu ya kazi, hatuangalii urafiki wala undugu," Blandina akamwambia.
Namouih akacheka kidogo.
"Ila Felix nawe acha uzongaji bwana, si useme tu nini kinaendelea kwenu? Au unafikiri sisi ni Radio Free Africa?" Blandina akasema.
"Siyo hivyo. Ila... niseme tu ni mambo ambayo...."
"Felix we' tuambie. Usiwaze kabisa kuhusu taarifa mbaya kusambaa, unajua sisi hatunaga porojo," Namouih akasema.
"Mmm?" Felix akafanya mguno huo kwa njia ya kejeli.
Blandina akacheka kidogo.
"Okay. Hayo mambo tuliyokuwa tunafatilia hayajaleta matokeo mazuri... tena ni mabaya sana. Kwa muda mrefu wasichana wadogo kwenye miaka ya kumi na, kumi na, wamekuwa wanapotea na bila kupatikana... na kutokea mwaka jana idadi ilipungua, tofauti na miaka miwili nyuma. Tumefukua na kufukua sana mpaka tukaanza kuwapata baadhi yao... lakini wengi walikuwa wameshaoza..." Felix akaanza kuwaambia.
Jambo hilo likawafanya wanawake hawa wawe makini sana.
"Unamaanisha walikuwa wameshakufa?" Blandina akauliza.
"Ndiyo. Tena kwa muda mrefu. Kila mara tulipowapata kwa kweli tulihuzunika sana, ilikuwa ngumu hata kuziambia familia zao lakini haikuwa na jinsi. Kila mara tulipompata msichana angekuwa ameshakufa. Lakini vifo vyao vimekuwa vikisababishwa na mtu au watu fulani. Kila msichana tunayempata... tunakuta alama ya kukatwa na kisu tumboni..."
"Kukatwa?" Namouih akauliza.
"Kuchanwa yaani... sehemu ya chini ya kitovu kidogo. Kila mmoja wao," Felix akasema.
Namouih na Blandina wakatazamana kimaswali.
"Wengi mliwapatia wapi?" akauliza Blandina.
"Wengi tumewapata wakiwa wamefukiwa sehemu tofauti-tofauti... na haikuwa rahisi kuwatambua mpaka miili yao ilipofanyiwa vipimo vya DNA. Lakini kwa hii miezi michache ya nyuma idadi yao ilipungua, ila tukaanza kuwapata wengine tena. Zamu hii imekuwa ni mmoja mmoja, na hawakuwa wakifukiwa kama kipindi cha nyuma lakini bado waliuawa kwa njia zile zile za kukatwa tumboni kwa kisu huku wakiwa na majeraha mengine mwilini. Njia moja tu. Ni mambo yanayosikitisha sana yaani... na mbaya zaidi ni kwamba...." Felix akaishia hapo na kuangalia chini.
"Watu wenu wanaficha hayo mambo, si ndiyo?" Namouih akauliza.
"Hawataki watu wa-panick kabla ya kujua tatizo ni nini. Aaah... yaani ni kero sana, nimeingia kwenye huu upelelezi tangu mwaka jana na bado hatujajua shida iko wapi. Hakuna viashirio vyovyote vinavyopatikana kwenye miili ya hao wasichana kwa hiyo hatuna lead yoyote ile," akasema Felix.
"Mh, jamani! Naonaga kwenye vipindi tu wanamsema fulani kapotea na nini... kumbe kati yao kuna hao wanaofanyiwa hayo?" Blandina akasema kwa sauti yenye huzuni kiasi.
"Yeah, ndiyo kama hivyo," Felix akajibu.
"Sasa kuficha jambo kama hilo si inamaanisha litaendelea kimya kimya tu bila watu kuwa na tahadhari? Inakuwa ni kama mnamlea muuaji," Namouih akasema.
"Waambie hivyo mabosi sasa," Felix akasema.
"Au ni wenyewe ndiyo wanafanya hayo?" Blandina akauliza.
"Ahahah... ningehakikisha wanaiona kuzimu kabisa. Ila msichana wa mwisho tuliyempata ilikuwa mwezi uliopita. Tulikuta yaani hana ulimi... ah alikuwa mdogo jamani! Yaani wakati mwingine nashindwa kuelewa watu wanaweza vipi kuchukua hatua za namna hiyo, ni unyama mkubwa sana! Lakini hapana. Nitafanya yote niwezayo kuhakikisha huyu mtu anakamatwa. Naombeni msimwambie yeyote kuhusu haya," Felix akasema.
"Usijali Felix, tunaelewa. Lakini unajua ni jambo la kuwaza... mimi nina mdogo wangu wa kike yuko huku anasoma... ni muhimu nimpe tahadhari, lakini sitamwambia hayo yote. Eh, yaani umenifanya nimeanza kuwaza sana," Namouih akasema.
"Ndiyo maana sikutaka kusema. Siyo kitu kizuri... basi tu," Felix akaongea kwa hisia.
Marafiki hawa wakaendelea na maongezi yao mengine huku wakimalizia vyakula na vinywaji, kisha baada ya hapo wakaenda kutembea-tembea maeneo ya karibu na hapo, halafu wakarejea tena kule hospitalini ili kuwa pamoja na rafiki yao kwenye muda wa kutembelea wagonjwa ilipofika saa kumi na moja. Bado Mwantum na baadhi ya watu wa familia yake walikuwepo huko, na marafiki hao wakakaa kwa muda wote wa matembezi kwa wagonjwa mpaka walipokuja kuachana hatimaye na kutawanyika ili kurudi nyumbani. Felix aliondoka kwa gari lake kwanza, kisha Namouih na Blandina wakaondoka pia baada ya kumtia moyo Mwantum.
★★
Namouih na Blandina wakawa njiani sasa kurejea mjini kwao baada ya kutoka kuwatembelea wagonjwa na rafiki yao. Blandina mpaka sasa alikuwa akijihisi vibaya kwa sababu tofauti na matarajio yake kutokea asubuhi, kijana yule kwa jina la Draxton hakuwa amemtumia ujumbe wowote kwa simu kama alivyoahidi. Kama kawaida ya Namouih alikuwa akimshurutisha rafiki yake aachane na habari za kijana huyo na waangalie mambo mengine muhimu zaidi, kama vile shughuli zinazohusika katika kumaliza kesi ile ya ubakaji kwa ushindi. Blandina hakuwa akiwaza kuhusu hayo kabisa na kuendelea tu kulalamika kwa nini hajatafutwa, hivyo Namouih akaona ampuuzie. Ikiwa imekwishaingia mida ya saa mbili sasa, walikuwa maeneo ambayo barabara ilikuwa katikati ya mapori mapori mengi pembezoni, wakiwa ndiyo wanaelekea kuingia sehemu za mjini kwenye majengo zaidi. Blandina ndiye aliyekuwa akiendesha, na kwa sehemu hizo hakukuwa na magari mengi waliyopishana nayo.
"Ikiwa huyu Japheth hatakuwa amepata mtu wa kumtetea naona ni kama wamenipotezea tu muda wangu," Namouih akawa anaongea.
"Kwa nini?" Blandina akauliza.
"Sasa faida gani kupatiwa kesi niishughulikie halafu mpinzani hana mwanasheria wa kumtetea?"
"Ih! Badala ufurahi tu kwamba huyo jamaa atapelekwa jela kwa alichokifanya bila usumbufu we' tena unalalamika... na hela si umeshalipwa?"
"Siyo hivyo, ni kwamba tu haeleweki. Jumanne kesho kutwa tu, siku ya trial. Bado sijataarifiwa kama ameshapata mwanasheria au la. Niko najiandaa vizuri kuishinda hii kesi halafu itokee akakosa mtu wa kumtetea, si nitakuwa nimejisumbua kujitayarisha?"
"Haina shida. Paycheck nene si unaipata?"
"Hata kama, me ningependa sana kupeleka hii kitu trial. Nime-miss," akasema Namouih.
"Ahahahah... unapenda mno kujibizana na watu mahakamani. Ila unajua nafikiri wanasheria wengine wanaogopa," Blandina akasema.
"Waogope nini?"
"Mtu tu akisikia hii ni kesi ya kubaka, halafu wewe ndiyo unamsimamia mtoa mashtaka aaaa... wanageukia mbali... maana unajulikana sana kwa kutowahi kupoteza kesi hata moja," Blandina akamwambia.
Namouih akacheka kidogo. "Well, akiachwa bila wa kumtetea basi atatakiwa kulipa maana ametoa ahadi fake... na bado miaka 30 jela ataila," akasema.
"Nina hamu sana ya kumuonja huyu jamaa, hajui tu," Blandina akasema.
"Aliyebaka?"
"What... no, namaanisha Draxton..."
"Hivi bado unaendelea tu na huo upuuzi? Wote ambao umeshawahi kuwaonja wana ladha gani tofauti na ya huyo mvunja chupa ambaye hata haumjui vizuri?" Namouih akasema.
"We' utajuaje Namouih, maana una kama muongo mzima hujatekenywa," Blandina akamwambia kiutani.
"Unataka nikutukane eti?" Namouih akasema.
Blandina akamwangalia huku akicheka.
Namouih alikuwa anamtazama kwa ukali wa kimasihara pia, pale kona ya jicho lake ilipoona jambo fulani kwa mbele na kumfanya atazame huko upesi. Ilikuwa ni kama mtu au kitu fulani kinapita haraka sana barabarani, kikiwa kinavuka kutoka upande wa kushoto wa barabara kwenda wa kulia, naye Namouih akashtuka sana.
"Blandina!"
Namouih akaita kwa sauti ya juu na kumfanya Blandina ashtuke na kutazama mbele, ambaye kwa sekunde hizo chache alikuwa bado amemwangalia rafiki yake. Akakanyaga breki kwa nguvu sana, na wakati huo taa za gari lake zilikuwa zimemulika vizuri zaidi umbo la kitu hicho kuwafanya wanawake hawa watambue kwamba ilikuwa ni mtu. Lakini tayari gari lilikuwa limemfikia na kumgonga kwa nguvu sana wakati ambao matairi ndiyo yalikuwa yamefika ukomo wa kusimama kwa ghafla. Gari likasimama kwa upande kiasi katikati ya barabara baada ya Blandina kuwa amezungusha usukani kidogo kutokana na mwili kutenda kwa mshtuko, na marafiki hawa wakaona vizuri jinsi mtu huyo alivyorushwa hewani na kudondokea chini kwa nguvu, na mwili wake ukaviringika mara chache, na kisha kutulia tuli. Namouih akaweka kiganja chake mdomoni huku akiwa ametoa macho kwa mshangao sana, huku Blandina naye akishangaa na pumzi zake kuongezeka kasi.
"Mungu wangu! Nam... Nam... Nam nime...."
Blandina akashindwa hata kuendelea kuongea na kubaki amemwangalia rafiki yake.
"Okay, okay, tulia. Tunaenda kumsaidia haraka, hatuko mbali sana na hospitali, okay? Kila kitu kitakuwa sawa," Namouih akamwambia kumtuliza.
Blandina akawa anatikisa kichwa kujipa matumaini kwamba kweli kila kitu kingekuwa sawa, naye Namouih akamwambia aligeuze gari vizuri kutoka barabarani hapo ili kulisogeza karibu na upande ambao mtu yule aliangukia, kisha washuke kwenda kumtoa mtu huyo hapo chini kumwahisha hospitali. Wazo la kwamba huenda ajali hii ndogo ilisababisha kifo halikuwa mbali na akili za wanawake hawa, lakini ilikuwa rahisi zaidi kujipa moyo kwamba mtu aliyegongwa alikuwa mzima ili kuweza kuiondolea mbali hatia ya kuua; hata kama hawakukusudia. Wakiwa wameshuka sasa na kuanza kumwelekea mtu yule, ni Namouih ndiye aliyekuwa kwa mbele kidogo kumtangulia mwenzake, kwa kuwa kwa kiasi kikubwa Blandina aliogopa. Mtu huyo alikuwa ameangukia pembezoni zaidi kutokea barabarani, hivyo kwa upande huo mwanga wa taa za gari haukumulika vyema kutokana na Blandina kulisimamisha kwa upande wa milango. Namouih akawasha tochi ya simu yake, akimmulika mtu yule pale chini, na wote wakabaki kushangaa kwa kile walichoona.
Mtu huyo waliyemgonga hakuwa na nguo hata moja mwilini mwake. Ulikuwa tupu kabisa! Ngozi yake ilikuwa nyeupe, weupe kama wa mzungu. Kwa haraka waliweza kutambua kwamba ilikuwa ni mwanaume, ingawa alilalia tumbo lake, huku mkono wake wa kulia ukionekana kuvunjika kutokea kwenye kiwiko na kuzungukia kwa nyuma, yaani ulikuwa umepindia mgongoni. Kichwa chake kilikuwa kimelala kwa uso kugusa ardhi, hivyo hawangeweza kuuona. Ingawa hivyo, nywele za kichwa chake zilionekana vyema, nazo zilikuwa ndefu kiasi na laini, zenye rangi nyeupe... rangi nyeupe pe. Marafiki hawa ni kama walitulia kidogo wakitathmini mwili wa mtu huyo, na sauti za magari kama mawili matatu yakipita pale barabarani zikasikika, lakini umakini wao wote ulikuwa hapo chini. Mwili wa waliyemgonga ulionekana kuwa imara sana, na kwa sekunde chache Namouih akawa ametambua kwamba sehemu ya juu kwenye mgongo wa mtu huyo kulikuwa na tattoo ya maneno fulani ambayo yalisomeka, "LIVING IN MY HEART YOU ARE, SO YOU AREN'T DEAD."
Blandina akamshika mkono mwenzake na kuuliza wafanye nini, maana hali aliyokuwa nayo mtu huyo hapo chini ilitatiza. Akasema ikiwa wangeita msaada, basi hata kama jamaa bado alikuwa hai angekufa kwa sababu ya muda mrefu kupita, na yeye alikuwa anahisi asingeweza kuwa na ujasiri hata wa kumshika tu. Namouih akaendelea kummulika akijishauri cha kufanya, lakini ghafla mkono ule uliokuwa umekunjikia kwa nyuma wa mtu huyo ukajinyoosha kwa kasi na kushika chini! Blandina akashtuka sana na hata kupiga kelele kidogo, naye Namouih akaingiwa na hofu pia, kisha wote wakalifata gari lao, Blandina akiwa wa kwanza kuingia ndani. Kabla Namouih hajaingia pia, akaangalia sehemu ile, naye akashangaa kumwona mtu huyo akinyanyuka mwenyewe na kusimama, akiwa amempa mgongo. Uajabu wa hali hii ulifanya asahau hata kufungua mlango wa gari na kubaki amepigwa na butwaa, huku Blandina akiwa anamwangalia "mtu" huyo kwa hofu kutokea ndani ya gari lake pia. Huyo alikuwa ni mtu, au kiumbe wa aina gani?
Alisimama hivyo kwa sekunde chache, kisha akaonekana akianza kugeuka nyuma.
"Nam, Nam, Nam, Nam, Nam, ingia, harakisha!"
Blandina akaongea hivyo kwa hofu huku akiliwasha gari lake, na hakukumbuka hata ikiwa alilizima kabisa. Namouih akaingia upesi pia kwenye gari, huku akitazama upande ambao "mtu" yule alikuwepo. Lakini akashangaa kutomwona sehemu ile tena, ikiwa ni kama alitoweka ghafla kabisa, na ni wakati huu ndipo Blandina akawa amekanyaga mafuta na kuliondoa gari lake hapo upesi sana.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments