CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA PILI
★★★★★★★★★★★★★★
Blandina aliingia barabarani na kukanyaga mafuta zaidi, akiwa kama yuko kwenye mashindano vile. Namouih alikuwa ameweka kiganja chake kifuani huku akitazama mbele kama vile amezubaa. Blandina alikuwa akitazama kioo cha juu ndani ya gari na cha pembeni nje ya mlango mara kwa mara, ili tu kuhakikisha kwamba walikuwa mbali na kitu walichotoka kuona muda mfupi nyuma.
Waliangaliana mara chache kwa nyuso zilizoonyesha utata sana, lakini hawakusemeshana chochote mpaka wanafika sehemu za mjini zenye shughuli nyingi zaidi. Blandina akapeleka gari sehemu ya kujaza mafuta, kisha mhudumu akafika karibu na mlango na yeye Blandina kumpatia elfu hamsini ili amwekee lita za mafuta ya bei hiyo. Namouih alikuwa ameegamiza kichwa chake kwenye mkono usawa wa kioo cha gari, naye Blandina akamwangalia usoni.
"Nani atatuamini tukimwambia?" Blandina akauliza kwa sauti ya chini.
Namouih akatikisa tu kichwa kwa njia ya kufadhaika.
"Unajua till a few moments ago nilidhani nimeua mtu, lakini... nilichoona leo... haki ya Mungu!" Blandina akaongea na kuinamisha kichwa chake kwenye usukani.
Namouih alikuwa akiyatafakari maneno yale kwenye tattoo aliyoiona mwilini mwa mtu yule asiyeeleweka kabisa. "LIVING IN MY HEART YOU ARE, SO YOU AREN'T DEAD," ilimaanisha "NDANI YA MOYO WANGU UNAISHI, KWA HIYO HAUJAFA." Akili yake yenye udadisi ilikuwa ikimwambia hicho alichokisoma kilikuwa na maana fulani kubwa, na jinsi mtu huyo alivyokuwa wa ajabu kukamfanya atamani kama ingewezekana, apate kujua kumhusu. Lakini hicho kilikuwa ni kitu hatari sana, na alilitambua hilo.
Mhudumu wa kituo hicho cha mafuta akasogea sehemu ya mlango na kumwambia Blandina kwamba angeweza kuondoka sasa, lakini pia akamwambia kuhusu jinsi sehemu ya mbele ya gari lake ilivyokuwa imekunjika kiasi, akionelea kwamba alikuwa amegonga kitu fulani. Blandina na Namouih wakatazamana kiufupi kama kujikumbusha sababu ya jambo hilo, kisha Blandina akamshukuru tu mhudumu na kuliondoa gari hapo.
★★
Hatimaye Blandina akawa amewafikisha nyumbani kwa Namouih. Walipokelewa vyema na msaidizi wake wa kazi aliyeitwa Esma, ambaye aliichukua mizigo waliyoileta na kuipeleka ndani mpaka jikoni. Nyumba ya Namouih ilikuwa kubwa na pana, yenye ghorofa lenye vyumba kadhaa, na ilipangiliwa vizuri sana kwa kuwa na vitu vingi vya gharama na samani zenye thamani. Alikuwa akifuga paka pia, mwenye manyoya meupe, na aliyemwita kwa jina Angelo. Angelo alifurahia sana kumwona mfugaji wake baada ya kuwa wamefika ndani, na kwa muda fulani Blandina akawa anacheza naye kwa kuwa yeye pia alimzoea.
Wakati Esma alipokuwa akiandaa mambo ya msosi kwa ajili yao, marafiki hawa walitumia muda mfupi kuzungumzia tukio lile ambalo ingekuwa ngumu sana kulisahau kwa siku hii. Kutokana na wao kuwa wanasheria, walikuwa wakiangalia jinsi hali zile zilivyojitengeneza mpaka ikawa bonge moja la onyesho. Blandina alikuwa akisema yaani ikiwa waandishi wa habari wangepata kuchukua tukio lile, basi ingekuwa taarifa moja kubwa sana ambayo ingezagaa nchi nzima kama ugonjwa wa malaria au popo bawa.
Angalau waliingiza na utani kiasi kwenye mazungumzo yao katika suala hilo, lakini pointi muhimu ilikuwa ni usalama wa watu wengine maeneo ambayo kiumbe yule angekuwa. Ikiwa mtu kama huyo angeendelea kuwa hadharani, na kama hakuwa mtu mzuri, basi ingekuwa hatari kwa wengi. Ila ni nani angewaamini hata kama wangejaribu kusema walichokiona bila kuwa na uthibitisho? Kwa hakika wangeweza kumwonyesha yeyote mkunjo mbele ya gari la Blandina, lakini hata hiyo haingethibitisha kwamba aligonga "mtu," halafu "mtu" huyo akanyanyuka tu kama kujipangusa vumbi na kuondoka. Kwa hiyo ikaonekana kuwa mwisho wa siku wangetakiwa tu kuigiza kana kwamba jambo lile halikuwahi kamwe kutokea, naye Blandina akajiahidi kuwa mwangalifu zaidi katika uendeshaji wa gari.
Esma alimaliza maandalizi ya msosi, kisha wote wakapata chakula kwa pamoja. Walifurahia kweli mlo huu, na baada ya kumaliza, marafiki hawa wakaingia kwenye ofisi ya Namouih ya hapo nyumbani kwake kupitia mambo machache pamoja huku wakifanya maongezi, kisha ukafika muda ambao Blandina alihitaji kuelekea kwake hatimaye. Bado alikuwa amekwazika kwa sababu kijana yule aliyemwahidi kumtafuta asubuhi ya leo hakufanya hivyo, naye Namouih akaona amtie moyo kwa kusema angepata tu mkali mwingine wa kutuliza mahitaji yake. Akamsindikiza mpaka kwenye gari lake na kumsihi awe makini sana barabarani, kisha wakakumbatiana kwa upendo na Blandina kuondoka.
Hii ikiwa ni mida ya saa tano ya saa sita usiku sasa, Namouih akaamua kwenda tu chumbani kwake ili hatimaye ajipumzishe. Alipanda kitandani, akimwacha Angelo amepanda kwenye kagodoro kake pia hapo kwa chini. Akajilaza huku akiperuzi mitandao ya kijamii kuangalia mambo ya hapa na pale, na ndipo wazo lile likamwingia. Ile tattoo. Mgongoni kwa jamaa. Waliyemgonga kwa gari. Alikuwa anawaza kwamba maneno yale yalikuwa na maana fulani, kama fumbo, naye akajaribu kutafuta maana zozote zile kwenye Google zinazohusiana na maneno hayo.
Alipata misemo na maana tofauti-tofauti, lakini hakukuwa na chochote chenye kuendana na hali aliyojionea leo kilichomridhisha. Msemo wa karibu zaidi ulioendana na maneno yale ni kutoka kwa Thomas Campbell, lakini hata na hapo hakuona kama kuna ulingano wa kutosha kuleta maana fulani iliyofichika. Alikuwa karibu kuiweka simu yake pembeni baada ya kumaliza hayo ili aanze kuutafuta usingizi, pale ilipoanza kuita. Akaangalia jina la mpigaji kwa ufupi, kisha akapokea hatimaye.
"Hallo..." akasema Namouih.
"Hey sweety... how are you?" ikasikika sauti upande wa pili.
Alikuwa ni mume wake, aliyekwenda kwa jina la Efraim Donald.
"Am good. Za huko?" akajibu Namouih.
"Serene. Lakini nakukosa sana mpenzi..."
"Mimi pia..."
"Usijali my dear, tutakuwa wote soon..."
"Mikutano haijaisha bado?"
"Ndiyo tumemaliza, nilikuwa nimeboeka sana. Niliposema soon nilimaanisha tomorrow soon," Efraim akamwambia.
"Oh! Unamaanisha kesho ndiyo unakuja?"
"Yep!"
"Ahah... okay. Nafurahi sana. Natamani kesho ifike ndani ya dakika mbili yaani, uwepo wako huku pamoja nami ni wa muhimu mno Efraim..."
"Wewe pia. Yaani vitanda vyote navyolalia vina baridi tupu kwa sababu joto lako ndiyo linakosekana..."
"Mhmhm... bado hujaachana na mashairi eeh?"
"Kwako hayazimi... nakupenda mke wangu..."
"Nakupenda pia husband... niko nakusubiri..."
"Asante sana. Uwe na usiku mwema eeh?"
"Kwako pia..."
Namouih akamalizia maongezi hayo mafupi, na kisha simu ikakatwa. Akaiweka simu yake kifuani na kutulia kidogo, akitafakari mambo kadhaa kuhusu ndoa yake hii iliyokuwa imemaliza mwaka mmoja tu sasa. Kuna vitu vingi vilivyokuwa vikiendelea tokea alipoolewa na Efraim Donald, na hakuhisi kama alitakiwa kuwa na sababu yoyote ya kutoridhika na maisha aliyokuwa amefanikiwa kuyapata akiwa naye, lakini bado kuna jambo fulani lililomfanya ahisi kuvunjika moyo kila alipomfikiria mume wake.
Akaona isiwe kitu cha kumpa msongo mwingine wa mawazo kwa wakati huu, hivyo akaiweka simu yake pembeni, kisha akaufunika mwili wake kwa shuka na kuanza kuutafuta usingizi.
★★★
Alikuja kuamka na kukuta kuna giza, ikionekana bado ni katikati ya usiku, naye akaamua kuchukua simu yake ili kutazama saa na kukuta ni saa kumi usiku. Alihisi kiu kiasi cha kumtaka atoke na kwenda kule chini ili kupata kikombe kimoja cha maji, pale alipoanza kusikia sauti za vishindo, bila kutambua vilitokea wapi. Zilisikika kama hatua za mtu anayetembea. Akajaribu kuiwasha taa ndogo iliyokuwa pembeni na kitanda, lakini ikawa haiwaki. Ajabu.
Akawasha tochi ya simu yake na kuanza kuielekeza huku na huku, akifikiria kunyanyuka kwenda kuwasha taa ukutani, na mwanga wa tochi hiyo ukatulia kwenye muundo fulani kama mtu aliyeinama kwenye kona ya chumba hicho. Akapiga kelele kidogo kwa hofu na kuidondosha simu yake chini, na hiyo ikasababisha izimike baada ya kudondoka vibaya. Akaanza kujitahidi kuiokota ili kuiwasha upya, lakini ni hapa ndiyo akakumbuka kwamba kwenye kona ile kulikuwa na stendi ya kutundikia makoti, na bila shaka alichokiona hapo ilikuwa ni koti refu jeusi lililotundikwa.
Akashusha pumzi kwa kupata utulivu kiasi. Tochi ya simu yake ilikuwa imezimika ndiyo, lakini akatambua kuwa chumba hiki kilikuwa na mwangaza fulani hafifu kutokea nje. Haukuwa ule mwanga wa taa za nje, ilikuwa ni kama mwanga wa mapambazuko. Akajiuliza ikiwa tayari asubuhi ilikuwa imefika, lakini akakumbuka aliangalia simu yake na kuona kweli ni saa kumi usiku. Sasa ni nini kilichokuwa kikifanya chumba kiangazwe?
Akatoka kitandani vizuri zaidi na kujaribu kupapasa chini ili aichukue simu yake, lakini hangeweza kuiona, na akashindwa kuipata. Akatoka alipokuwa na kuanza kutembea kuelekea sehemu ya ukuta yenye soketi za kuwashia taa, lakini alipowasha, hazikuwaka. Akafikiri kuwa huenda umeme ulikata, ingawa bado wazo la taa za nje kuwaka lilikuwa akilini lakini ikawa kama vile halijalishi sana, hivyo akaamua kuelekea nje ya chumba kwa uzoefu tu wa kuijua nyumba yake mpaka alipofika kwenye korido lililoelekea kwenye ngazi ili ashuke kule chini.
Mwangaza ule ni kama ulizidi kuijaza sehemu hiyo, na ni hapa ndipo akajiuliza swali hili: ikiwa alichoona kwenye kona muda ule kilikuwa koti, basi ni nini kilichokuwa kinatoa sauti zile za vishindo baada ya yeye kuamka? Akaendelea kupiga hatua chache mbele, lakini akahisi kitu fulani. Akasimama. Akageuka taratibu na kutazama nyuma yake. Aliweza kuona kitu chanye muundo wa mtu fulani, kama kivuli, lakini kikiwa kimesimama, na kilikuwa kimevaa moja ya makoti ya mume wake aliyotumia kwa ajili ya kuvaa kazini. Hakuweza kuuona vizuri uso wa kitu hicho kilichoonekana kama kivuli kilichosimama, lakini alitambua kwamba kilikuwa kinatoa tabasamu.
Mapigo ya moyo wake yalidunda kwa nguvu sana kwa hofu kubwa iliyomwingia, kana kwamba moyo wake ulitaka kuruka kutoka kifuani kwake. Akaanza kukimbia kama kichaa, akigeuka nyuma ovyo ovyo mpaka alipofikia sehemu ya mwanzo ya kushuka kwa ngazi, naye akaanza kuzishuka upesi sana. Ilikuwa kwa tukio zuri kwamba hakuanguka kwa kushuka haraka-haraka, kwa sababu ingawa mwangaza ule ulimwonyesha baadhi ya vitu, bado ilikuwa hatari kushuka ngazi jinsi alivyozishuka.
Akafika chini na kuanza kuelekea upande wenye mlango wa kutokea, lakini hakuelewa kwa nini alikoelekea palibadilika na kumfanya aufikie ukuta wa eneo hilo la chini. Akajigonga hapo kidogo na kugeuka nyuma. Ilikuwa ni kama vitu vyote viliondolewa sehemu hiyo, lakini tena kama vile bado vilikuwepo. Mwangaza uliomzunguka ukaanza kuwa kama moshi mzito, naye akafikiria kukimbia tena, lakini hofu yake ikafanya miguu iwe kama imenasa hapo hapo alipokuwa, kwa hiyo akashindwa kutoka.
Akatazama huku na huku asijue la kufanya, na ni hapa ndiyo akahisi akishikwa kwa mikono miwili mabegani kutokea nyuma. Hakugeuka haraka, kwa sababu mtetemo uliopita mwilini mwake ulimfanya ahisi ni kama amepigwa shoti kali mwili mzima. Alipokuwa amesimama, nyuma yake kulikuwa na ukuta. Mikono iliyomshika ilitoka wapi? Akajitahidi kujitoa hapo na hatimaye kugeuza mwili wake, na ndipo akaona kinywa chenye meno mengi makali na marefu kikifunguka na....
"Aaaaaaaah!"
Alipiga kelele kwa sauti ya juu sana na kujinyanyua kuketi. Alikuwa anapumua kwa presha sana, huku mwili wake ukitoa jasho. Alipojitazama, akatambua kwamba alikuwa kitandani, upande ule ule aliokuwa amelala na kuamka usiku mpaka kisa hicho kilichoonekana kuwa ndoto kumpata. Hapo hapo msaidizi wake wa kazi akaingia bila hodi, akiwa anaharakisha sana na kumfikia karibu.
"Dada... vipi? Kuna shida gani?" Esma akamuuliza.
Namouih akamwangalia usoni kwa umakini, asijue la kumwambia hata kidogo.
"Ulikuwa unaota ndoto mbaya?" Esma akamuuliza kwa kujali.
Namouih alipoangalia kwenye kona ile yenye stendi ya kutundikia nguo, akaona kwamba koti la mume wake lilikuwa hapo bado. Akatazama huku na huko kwenye chumba chake, na kila kitu kilikuwa kwenye mpangilio wake mzuri.
"Dada?" Esma akamwita tena.
Namouih akamwangalia na kusema, "Aam... ndiyo... ilikuwa ndoto mbaya."
"Oh pole. Pole sana. Nimeshtuka yaani umesikika hadi chini..."
"Nimepiga kelele kwa nguvu sana?"
"Sana, yaani mpaka nikaogopa..."
"Okay, usijali niko sawa. Ni saa ngapi?"
"Nafikiri saa mbili."
"Okay. Angelo ume..."
"Eh ndiyo nimeshampa maziwa. Chai tayari... nimekuwekea mezani."
"Asante..."
Msaidizi wake akatoka na kumwacha akiwa ameketi tu bado kitandani. Kitu kilichokuwa kimetokea muda mfupi nyuma hakikuonekana kama ndoto, kilikuwa halisi kabisa kwake. Akajiuliza mambo mengi sana kuhusu "ndoto" hiyo, lakini hakupata majibu. Akaamua tu kuacha kuitafakari na kujiondoa kitandani ili kwenda kuusafisha mwili wake. Hakukuwa na shida tena baada ya yeye kumaliza kuoga na kuanza kujiandaa kwa ajili ya kazi, na hata kuifikiria ndoto hiyo hakukumsumbua kama jinsi ilivyomsumbua wakati alipoamka.
Akatia mwili wake vazi refu lenye kubana, kama gauni, lililokuwa na rangi nyeusi na nyeupe kulizunguka, likiwa la mikono mirefu mpaka kwenye viganja na kuacha uwazi katikati ya kifua chake ulioonyesha mstari wa kati wa matiti yake kwa mbali. Nywele zake alizibana vizuri nyuma ya kichwa, na usoni alipendeza sana kwa kupaka lipstick yenye rangi ya maroon-nyeusi mdomoni. Viatu vyeupe vya kuchuchumia alivyovaa viliongezea zaidi urefu wake, na baada ya kumaliza kupata kiamsha kinywa akamwachia Esma maagizo machache, kisha akaondoka hatimaye.
★★
Baada ya kufika ofisini, Namouih alianza kushughulika na mambo kadha wa kadha ya kikazi, na ndipo Blandina akaingia hapo na kuanza kumsemesha kuhusiana na ile kesi ambayo wangeishughulikia kesho, akimwambia pia kwamba alilipeleka gari lake kufanyiwa matengenezo asubuhi hiyo. Ofisi ya Namouih ilikuwa pana na yenye mwonekano wa gharama sana, ikizungukwa na vitu vingi na samani za vioo; yaani meza yake pana, viti vya humo na madirisha mapana yalikuwa ya vioo vizito. Pembeni ilikuwepo sehemu yenye masofa mawili na meza ndogo ya kioo pia.
Lakini kwa muda wote ambao Blandina aliongea toka ameingia ndani hapo, Namouih hakusema mambo mengi, na alionekana kuwa makini kupita kawaida, kitu kilichofanya Blandina ahisi rafiki yake alikuwa na tatizo.
"Vipi wewe?" Blandina akauliza.
"Bee... vipi nini?" Namouih akauliza pia.
"Nilikuwa nakwambia kuhusu Mwantum. Biashara yake haimlipi sana tokea mwezi juzi mpaka leo, na nahofia anaweza akakosa njia za kujikwamua zaidi maana sa'hivi mambo mengi yatamwangalia. Tunamsaidiaje?" Blandina akamwambia.
"Jamani Mwantum si alisema jana kila kitu kiko sawa? Hayo ya kumsaidia yanatoka wapi?"
"Siyo lazima mpaka aseme nawe, yule anaweza kufa na tai shingoni kabisa na hajaomba msaada. Ila nimefatilia nikagundua vitu vingi vinampiga vibaya dear, hasemi tu. Namwonea sana huruma," Blandina akasema kwa hisia.
"Haina shida. Kitakachohitajika we' tu unaniambia, sawa?" Namouih akaongea kibaridi sana, bila hata kumtazama rafiki yake.
Blandina akamtathmini kwa sekunde chache, kisha akauliza, "Una tatizo gani Nam?"
Namouih akaacha kubofya keyboard na kumwangalia. "Unamaanisha nini?" akauliza.
"Nimekwambia kitu cha muhimu sana lakini unaonyesha ni kama haujali vile. Umekuwaje?"
Namouih akabaki kumtazama tu.
"Bado ajali ya jana inakusumbua akili?" Blandina akauliza.
"Hapana."
"Sasa shida ni nini?"
Namouih akaitazama tena kompyuta yake, kisha akasema, "Efraim anakuja leo."
Blandina akatabasamu huku akitikisa kichwa chake na kumtazama rafiki yake kiutundu. "Oooh... kumbe kitunguu maji anarudi leo?" akauliza kiutani.
Namouih akatikisa kichwa kimasikitiko kiasi.
"Ahahahah... kwa hiyo, ndiyo uko tense kihivyo kwa sababu mumeo anarudi?" Blandina akauliza.
"Nimefurahi. Nimefurahi kwamba anarudi... hii ni kawaida every time, atarudi, mambo yatakuwa safi..."
"Kweli? Sasa mbona uko hivyo?"
Namouih akakaa kimya tu.
"Najua ni maisha yako binafsi lakini lazima niwe advocate wako kwa hili. Nam, itabidi uongee naye. A woman has needs. Hai-make sense hata kidogo, yaani, mwaka mzima amekuoa halafu...."
"Basi Blandina, tuachane na hayo. Nitakuwa sawa. Nitakuwa sawa," Namouih akamkatisha.
"Utakuwa sawa ya kwamba utatafuta suluhisho, au ndiyo utabaki kimya tu?" Blandina akamuuliza.
Namouih akachukua makablasha fulani na kumpatia, akisema, "Mpelekee Edward ayatie saini."
"Unakwepa swali langu, si ndiyo?" Blandina akamuuliza.
Namouih akamkazia macho kama kumwambia afanye alichomwambia.
"Yes ma'am..." Blandina akasema na kuyachukua, kisha akatoka ofisini hapo.
Baada ya Blandina kuondoka, Namouih akampigia simu yule msichana ambaye ndiyo alikuwa anamtetea kwenye kesi hii ya ubakaji, aliyeitwa Agnes, akimuuliza ikiwa alikuwa tayari kwa kesho, na kwa jinsi mambo yalivyokuwa, ilionekana kwamba kusingekuwa na mengi mno ya kufanya kwa sababu wangekuja tu kusikiliza hukumu ya yule jamaa endapo kama kufikia kesho angekuwa bado hajapata mwanasheria wa kujaribu kutetea upande wake. Agnes akamwambia kwamba hakusahau hilo, na kesho angefika mahakamani kwa muda uliopangwa. Akamuuliza Namouih ikiwa huyo Japheth angefungwa na kulipa faini kesho, naye Namouih akamwambia hayo yalikuwa mambo ya uhakika, kilichokuwepo ni kusubiri kesho ifike.
Alipomaliza hilo, akakaa kwa utulivu kwanza akifikiria yale ambayo Blandina alikuwa ametoka kusema muda mfupi nyuma. Maneno yake yalikuwa ya ukweli, na kuna sababu iliyofanya yawe kweli. Kuna kitu fulani ambacho kilikuwa kikisumbua akili ya Namouih toka Efraim Donald alipomuoa, na kwa kipindi kirefu alikuwa amejaribu kujifanya kwamba angeweza kupuuzia na kuendelea na mambo mengine tu, ila kwa wakati huu alihisi kuchoka. Sasa leo kwa kuwa Efraim angerudi, Namouih akawa amekusudia "kutafuta suluhisho," kama vile Blandina alivyopendekeza.
★★
Baada ya muda fulani, Namouih akajiunga na mkuu wa kampuni hiyo, yaani Mr. Edward Thomas, kwenye mlo wa mchana, wakiwa pamoja na watu wengine maalumu kutoka kampuni za mikoa tofauti kuzungumzia masuala ya kikazi yaliyohusisha mambo mengi. Namouih alikuwa hapo kama kichwa kikuu cha masuala ya sheria kutokea upande wao, nao wakafanikiwa kufikia makubaliano mazuri katika kuendeleza misingi imara ya kimaendeleo na kisheria kwenye kampuni zao na watu waliotaka kuwasaidia. Blandina yeye alikuwa amepewa mgawo wa kusaidizana na mwanasheria mwingine wa kampuni yao kusuluhisha tatizo ambalo lilikuwa mzozo mkubwa baina ya pande mbili zilizodai kupewa haki ya umiliki wa mali; pande moja ikidai kupewa mali zote, na nyingine ikipinga hilo kwa kutaka igawanyishwe kwa usawa. Walikuwa ni wanandoa waliotalikiana kipindi hiki hiki, hivyo kulikuwa na mzozo mkali baina yao.
Kwa hiyo marafiki hawa wakawa bize kwa mambo mengi muhimu ya hapa na pale mpaka walipokuja kukutana mida ya jioni, nao wakaamua kwenda sehemu fulani kama hoteli na bar waliyopendelea kwenda mara nyingi kupata kinywaji kimoja au viwili ili kujiliwaza kidogo. Kama kawaida ya Blandina, alikuwa akitazama sehemu hiyo kuona ikiwa angepata mwanaume ambaye angefaa kutoka naye, lakini hakuna hata mmoja aliyeona anafaa.
"Ridiculous... lame... too short... too sweaty..." Blandina akawa anawabagua wanaume hao kwa kuwahukumu namna hiyo.
"Ahahahah... unaiga maneno ya kwenye George of the jungle eeh?" Namouih akasema.
"Aaih... Draxton wangu amekwenda wapi jamani? Nimejaribu hata kuwatafuta ma-Draxton wote FB lakini sura yake sijaipata. Bora tu kama mimi ndiyo ningechukua namba yake jana, ona anavyonitesa..."
"Usihofu sana Blandina. Atakuja tu. Nina uhakika atatokea maana Mungu aliwakutanisha, kwa hiyo usipoteze matumaini. Amini tu mtaonana tena," Namouih akamwambia.
"Kweli eti?" Blandina akauliza.
"Hapana," Namouih akasema.
Blandina akasonya na kunywa kileo chake.
Namouih akatabasamu na kuuliza, "Vipi kesi yenu?"
"Aaagh, yaani kuna watu wanachosha! Mgogoro wenyewe wa mali utafikiri ni Bangalore kumbe nyumba ya mabati sita tu!"
"Hebu acha masihara bwana. Niambie umefanya nini kusuluhisha..."
"Hakukuwa na tabu. Tumewafanya wakakubaliana kugawana pasu maana huyu wa kwetu alitaka share yake aitumie kujiendeleza na masomo..."
"Na huyu mwingine si ni mume wake?"
"Alikuwa. Alikuwa mume wake. Talaka ndiyo inamwasha huko chini, alikuwa mgumu vibaya mno. But you know me, hakuna chai ngumu mbele ya mkate wangu," Blandina akajisifia.
Simu ya Namouih ikaanza kuita alipokuwa akitabasamu kidogo kutokana na maneno ya rafiki yake, naye akapokea na kuiweka sikioni. Blandina akamuuliza kwa ishara ya mdomo "ni Donald?" naye Namouih akatikisa kichwa kukanusha. Akaongea na mtu huyu wa upande wa pili, akionyesha umakini kiasi, kisha baada ya hapo akaishusha simu kutoka sikioni.
"Well, angalau kesho haitaboa sana," Namouih akasema.
"Kwa nini? Kuzurura na Edward leo kumekuboa sana?" Blandina akauliza.
"We' acha tu, alikuwa amening'ang'ania kweli..."
"Ahahahah... nani huyo?" Blandina akauliza na kunywa kinywaji chake.
"Mtu fulani sijui nani, alikuwa ananifahamisha kwamba huyo Japheth amepata mwanasheria atakayemsimamia kesho... so tunaingia trial," Namouih akajibu.
"Wacha! Kwa hiyo unapiga prosecution ya nguvu kesho eeh?"
"Ndiyo maana yake. Uzuri ni kwamba ushahidi tunao, mashahidi watakuwepo, kwa hiyo..."
"Ulichokuwa unalilia umekipata..."
"Yeah. Haijalishi sana, maana huyo Japheth ni lazima nihakikishe anafundishwa somo kwa alichomfanyia Agnes. Kwa hiyo nafurahi kwamba amepata mtu wa kujaribu kuutetea upuuzi wake ili niwakomeshe wote," Namouih akasema.
"Ahahahah... atakuwa anafanya kazi yake tu bwana, lakini inaonekana jamaa hajasoma kujua anapingana na wewe..."
"Hamna kikubwa hapo. Ni kesho kuingia mahakamani, mimi kushinda, Agnes apate haki anayostahili, na mbakaji wake afungwe hata milele. Mwanasheria anayemtetea mpumbavu ili tu kupata pesa sikuzote namwona kama mpumbavu, ingawa hatutakiwi kujaji hivyo," Namouih akaongea.
"Hakukuwa na namna maana unajua majaji wasingekubali Japheth achukuliwe hatua bila kupata mwanasheria. Ilikuwa kama wote wamemkimbia," akasema Blandina.
"Yaani!" Namouih akasema hivyo na wote kucheka.
"Donald anaingia home saa ngapi?" Blandina akauliza.
"Amesema atakuwa ameshafika kwenye saa mbili. Tena nataka niwahi kurudi nyumbani ili anikute kabisa," Namouih akasema.
"Eeeh... akukute kabisa! Utakuwa umekaa style gani kwenye sofa?" Blandina akauliza kiutani.
Namouih akacheka kidogo.
"Ile ya spoon? Au ile ya lamba ubweche? Ama panua memory card 4GB?"
"Ahahahah... hebu acha mambo yako bwana. Nataka tu kumwandalia bonge la msosi. Nime-miss kula pamoja naye," Namouih akasema, huku sura yake ikionyesha hisia sana.
"Leo hakikisha kinaeleweka. Akikataa niite kukusaidia tumuue pamoja, umenielewa?" Blandina akamwambia.
Namouih akatabasamu tu, naye Blandina akanyanyua chupa yake kumwelekea, kisha Namouih akachukua yake pia na kuigongesha hapo, nao wakaendelea kushusha vinywaji vyao taratibu.
★★
Wawili hawa walikuja kuachana kwenye mida ya saa kumi na mbili jioni, Blandina akielekea kule ambako alipeleka gari lake lirekebishwe, na Namouih akielekea nyumbani. Alikuwa amempigia yule Agnes kwa mara nyingine tena kumjulisha kwamba kesi ya kesho ingekuwa na upinzani, na ingawa aliona hilo halingekuwa na shida, akamtaka awe tayari kujibu maswali kwa uhakika endapo angeulizwa vitu vingi vilivyompata kwenye mkasa wake wenye kusikitisha.
Alifika nyumbani na kuvalia kwa njia ya kawaida, kisha akaanza kusaidizana mapishi na Esma, wakitengeneza vyakula vizuri sana kwa ajili ya ujio wa mume wake. Walipomaliza, wakaandaa meza ya chakula vyema, kisha Namouih akaelekea chumbani tena ili kujiweka sawa hata zaidi. Ilikuwa ni kama vile hawajaonana kwa miezi mingi ingawa zilikuwa ni wiki tatu tu ndiyo hawakuonana. Hakuhitaji kujiremba sana, alijiweka sawa katika maana ya kwamba mume wake angefurahia zaidi kumwona akiwa "fresh," na yeye alipenda sana mara zote ambazo Efraim alimsifia kuwa mzuri sana.
Ilifika saa mbili na dakika kadhaa hatimaye, na nje ya geti ikasikika horn ya gari. Mlinzi wa getini, aliyeitwa Alfani, alikwenda kufungua geti hilo na gari aina ya Range Rover Vogue nyeusi kuingia na kuelekea mpaka sehemu ya maegesho. Kwenye sehemu ya mwingilio wa nyumba yao alisimama Namouih, akiwa anaangalia upande huo wa gari hilo kwa subira, na mlango wa mbele wa dereva ukafunguka, akishuka mwanaume aliyekuwa dereva-baunsa wa mume wake, aliyeitwa Suleiman. Akafungua mlango wa nyuma wa gari hilo, na hapo akatoka Efraim Donald mwenyewe. Alikuwa amevalia shati lenye mtindo fulani kama batiki yenye rangi ya samawati, suruali nyeusi, na viatu vyeusi pia. Machoni alikuwa amevaa miwani nyeusi ya mitindo, na kichwani kofia iliyozungukia pande za kichwa chake (aina ya fedora).
Namouih akatabasamu kwa furaha, naye Efraim Donald akaanza kuelekea pale mke wake aliposimama huku akifuatwa na Suleiman kwa nyuma. Akamfikia karibu na kuitoa miwani yake machoni, naye akamkumbatia mke wake kwa upendo. Walipoachiana, miili yao bado ilikuwa imegandana pamoja, Namouih akimwangalia kwa njia fulani ya kudeka, naye Efraim Donald akambusu kwenye paji la uso. Kisha wakaanza kuongozana kuelekea ndani huku wakishikana viunoni, na wakiongea kwa furaha sana kuhusu mambo mengi ambayo yalitokea kwao ndani ya hizi wiki tatu ambazo hawakuwa pamoja.
Efraim Donald alikuwa mwanaume mwenye miaka 40, mweusi, mrefu kuendana na urefu wa Namouih Ingawa nywele au viatu virefu vingefanya Namouih aonekane mrefu kidogo kumzidi. Alikuwa mtu mstaarabu na mkarimu sana, aliyefanya mambo mengi yaliyompa mafanikio na hivyo kusaidia watu wengine wengi waliomzunguka. Alijulikana zaidi kwa kumiliki kampuni kubwa sana iliyohusiana na biashara za magari; usafirishaji au uingizaji wa magari ndani na nje ya nchi, akishirikiana kwa ukaribu sana na kampuni za nchini Dubai. Alikuwa mtu wa safari mara kwa mara, yaani kila mwezi angetoka na kwenda sehemu au mkoa mwingine kushughulika na mambo ya kikazi, na ndiyo kurudi kwake kungekuwa namna hii baada ya siku au wiki chache. Alipenda kumtendea mke wake kwa njia nzuri sana hasa mara zote ambazo angekuwa naye, na Namouih alikuwa anamwamini sana na kujitahidi kumwonyesha upendo katika njia nyingi.
Baada ya Efraim Donald kuwa amefika sasa kutoka kwenye mikutano yake, Namouih akampakulia chakula, nao wakala pamoja na Suleiman na Esma. Mlinzi alikuwa na kawaida ya kula chakula chake ndani ya nyumba ndogo ya nje ambako ndiyo alitunza vitu vyake na kupumzikia huko. Walifurahia maongezi mpaka muda ambao walimaliza kula na kwenda tena kukaa kwenye masofa ili wapatane zaidi, kisha ukafika muda ambao Efraim Donald alihitaji kwenda juu chumbani kujimwagia maji ili kuutoa uchovu. Kulikuwa na vyumba kadhaa vya wageni, naye Suleiman akaenda zake kujipumzisha pia. Mwanaume huyu alikuwa kama mlinzi wa Efraim Donald, na alimfanyia kazi kwa kipindi kirefu, hivyo alionwa kuwa kama sehemu ya familia hii ndogo.
Efraim Donald alikwenda kujimwagia maji na kuutoa uchovu wa mwili kweli, kisha akarudi sehemu ya chumba na kuishia kusimama sehemu ya mlango wa kuingilia ndani ya bafu lao pana. Alikuwa amevalia taulo kiunoni, na macho yake yalielekea upande ambao kulikuwa na kitanda cha ndoa; kikubwa sana. Hapo alikuwepo Namouih. Jinsi alivyokaa ndiyo jambo ambalo lilimfanya Efraim Donald awe kama amezubaa.
Mwanamke alikuwa amekaa kwa kuegamia mwanzoni mwa kitanda hicho kulipoundwa kuta fulani ya sofa laini (ya kitanda) iliyopendeza sana, akiwa amenyoosha mguu wake mmoja na mwingine kuukanyagisha kitandani karibu na huo aliounyoosha. Mwili wake mweupe sana haukuwa na nguo zozote isipokuwa sidiria nyekundu iliyoficha matiti yake yaliyotuna kuelekea mbele, na chupi ya mikanda laini na nyekundu pia iliyoonekana kubanwa kiasi na sehemu ya kati ya mapaja yake manono. Sura yake nzuri, laini, na nyeupe sana ingefanya hata mapigo ya moyo ya mwanaume yeyote gaidi yasimame kwa jinsi ilivyotamanisha. Alikuwa anamtazama Efraim kwa njia iliyoonyesha wazi kwamba alitaka afatwe hapo kitandani ili ashughulikiwe haswa, naye Efraim Donald akaachia tabasamu dogo na kuanza kukielekea kitanda.
Mwanaume akamfikia karibu na kuketi usawa wa ubavu wake, huku akimtazama kwa njia iliyoonyesha wazi kwamba alimtamani sana. Namouih akapeleka kiganja chake kifuani kwa mume wake, akimwangalia kwa upendo mwingi sana, kisha akaifata midomo yake na kuanza kumbusu kimahaba. Efraim Donald aliipokea busu ya mke wake vizuri, lakini baada ya sekunde chache, akajitoa mdomoni mwake na kumshika pande za mikono yake.
"Tulale mpenzi... sijihisi vizuri sana."
Namouih akamtazama usoni kwa njia fulani ya kawaida tu, lakini Efraim alijua wazi kabisa kwamba jambo alilosema lilimkwaza mke wake. Mwanamke alikuwa amejiandaa vizuri kabisa kumpatia kitu kitamu kuliko hata chakula, lakini yeye akaona kulala ndiyo jambo bora zaidi. Efraim Donald akanyanyuka kutoka hapo na kuifuata kabati kubwa yenye nguo zao nyingi, huku Namouih akimwangalia tu, naye akavaa kaushi na bukta nyepesi, kisha akatoa nguo ya kike ya kulalia (night dress) na kumsogelea tena Namouih, aliyekuwa amekaa vile vile.
"Chukua... vaa. Usingizi ni mzito sana honey... tutatafuta muda mwingine ku...." Efraim akaishia tu hapo.
"Lini?" Namouih akauliza.
Efraim Donald akamwekea tu nguo hiyo mapajani na kugeuka nyuma ili azungukie upande mwingine wa kitanda.
"One year!"
Maneno hayo ya Namouih yakamfanya Efraim asimame tuli huku akiwa amempa mgongo, kwa kuwa yalisemwa kwa njia iliyomwambia kwamba mke wake alitaka kusema mambo mazito.
"Mwaka mmoja Efraim! Mwaka mzima umepita... every time... unakuwa umechoka?" Namouih akauliza.
Efraim Donald akaanza kupiga hatua kuzungukia kitanda mpaka alipofikia upande wake wa kulala, naye Namouih akaikunja miguu yake na kuketi huku anamtazama kwa hisia kali.
"Si naongea na wewe?" Namouih akasema.
Efraim Donald akamtazama kwa ufupi, akiwa amesimama sasa, kisha akasema, "Unajua mambo ni mengi... nikikwambia nachoka ujue nachoka kweli."
"Kuchoka kivipi Efraim? Kunichoka mimi au?"
"Siyo hivyo, usiongee namna hiyo bwana..."
"Unataka niwaze vipi? Efraim umenioa kwa zaidi ya mwaka sasa, lakini haujawahi kushiriki nami haki yetu ya ndoa! Una shida gani?!" Namouih akauliza kwa hisia.
"Sina shida yoyote Namouih, nimekwambia nimechoka tu..."
"Efraim naomba usicheze na akili yangu. Tafadhali. Kama kuna kitu fulani juu yangu kinachofanya usitake kunigusa ni kheri kuniambia ili nijue... nirekebishe... siyo kunifanyia hivi. Ndoa yetu ina maana gani kama hatutimiziani mahitaji yetu muhimu?"
Efraim Donald akapanda kitandani na kuanza kulifungua shuka ili aufunike mwili wake, lakini Namouih akalichukua kwa nguvu na kulitupa chini!
"Namouih ni nini laki...."
Efraim Donald akaishia hapo baada ya kumwangalia Namouih usoni na kukuta anakaribia kuanza kulia.
"Namouih..." akamwita kwa upole.
"Niambie Efraim... nataka uniambie kwa nini unanitendea hivi. Sina chochote cha kulalamikia kwa sababu umekuwa mume mzuri kwangu, na kwa kipindi kirefu niliona nikuache tu kwa kudhani labda ulihitaji muda... lakini kwa ajili gani? Kuna kasoro fulani unayoiona kwangu au?"
"Namouih tafadhali... nina uchovu wa...."
"Kesho utanipa kisingizio gani? Kichwa kinauma? Unafata utaratibu wa mazoezi? Sukari imepanda? Au kuna sehemu unawahi, na ukirudi tena umechoka?"
Efraim Donald akaangalia pembeni.
"Hhh... mara ya kwanza tumekutana uliniambiaje? 'Namouih... sitaki na sitaki kukuona unaumia.' Kwa nini sasa unaniumiza wakati huu Efraim? Ikiwa hii ni adhabu yangu kwa sababu mwanzoni sikukukubalia...."
"Hapana, siyo hivyo Namouih..."
"....basi nimekuelewa, na ninafikiri muda umepita vya kutosha kulisamehe hilo. Kwa nini basi unifanyie hivi? Mimi ninakuhitaji Efraim... ninahitaji kujua kwamba unanihitaji pia," Namouih akaongea kwa hisia sana.
Efraim Donald akajaribu kumvuta ili akilaze kichwa cha mke wake kwenye kifua chake kumpa bembelezo, lakini Namouih akaweka mgomo kabisa na kunyanyuka kutoka hapo, kisha akaenda bafuni na kujifungia.
Hii ndiyo iliyokuwa hali halisi ya ndoa yake. Efraim Donald alikuwa mume mzuri kwa Namouih; alimpenda, alimpa mahitaji yoyote ya kifedha na kihisia na hata vitu ambavyo Namouih hakutaka kupewa, na mambo mengi na makubwa sana kipindi cha nyuma alikuwa amemtimizia, lakini tangu alipomuoa, kulikuwa na jambo moja ambalo hakuwahi kumpa, yaani, haki yake ya ndoa. Mwanamke kama Namouih, hakuwa na papara, na sikuzote aliacha tu mambo yawe namna yalivyo kama hangeelewa vizuri kwa nini yako hivyo.
Lakini huyu alikuwa ni mume wake. Kilikuwa kitu ambacho hakingefikirika kwa yeyote kwamba Efraim hakuwahi kabisa kufanya mapenzi na Namouih, na mwanamke huyu alijitahidi kuacha tu hali hiyo ipite kwa muda fulani lakini sasa na yeye alikuwa anamhitaji sana mume wake. Efraim Donald hakuwahi kumpa mke wake sababu yoyote kwa nini hakushiriki naye mapenzi, na ni kitu kilichomuumiza sana Namouih kwa kumfanya ahisi labda haonwi kama mwanamke anayeweza kumtosheleza mwanaume. Namouih alikuwa amepitia kwenye hali ngumu kabla ya kukutana na Efraim Donald, na ni mwanaume huyu ndiye aliyemsaidia sana, kwa hiyo alitaka amwonyeshe jinsi alivyomthamini sana lakini yeye akawa anakataa kupokea moja kati ya mambo ambayo Namouih alitamani sana kumfanyia.
Akiwa bafuni baada ya jaribio lake muda mfupi nyuma kushindwa kuzaa matunda, Namouih akawa amesimama tu sehemu yenye kioo kipana sana, akijitazama hapo kwa huzuni. Sura nzuri alikuwa nayo. Mwili wenye mvuto alikuwa nao. Akili alikuwa nazo. Na uaminifu kwa mume wake licha ya yeye kutompa haki yake alikuwa nao. Shida ilikuwa wapi?
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments