Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA TATU

★★★★★★★★★★★★★★


MWAKA MMOJA NA NUSU ULIOPITA


Tunarudi miezi mingi nyuma kupata kujua mambo kadhaa kuhusu maisha ya mwanamke mrembo sana, Namouih. Jina lake halisi ni Namouih Alhaji Masoud, na yeye ndiye aliyekuwa mzaliwa wa kwanza katika familia iliyobarikiwa kuwa na watoto wanne.

Baba yake aliitwa Masoud Alhaji, mwanaume mwenye ngozi nyeupe na mwenye nguvu aliyefanya kazi migodini kwa muda mrefu. Alikuwa ni mtu wa Pemba, naye alikuwa mstaarabu na mchapakazi sana, aliyejitahidi kuiandalia familia yake mahitaji yao mengi licha ya kufanya kazi ngumu mno zilizomwathiri kwa njia mbaya ndani ya miaka aliyozifanya. Hakuwa mtu mwenye makuu, na sikuzote alimwongoza vizuri Namouih kwa kumwambia asome kwa bidii kwa sababu elimu ingemsaidia aweze kuboresha maisha yake baadaye. Aliipambania sana familia yao, naye alikuwa na umri wa miaka 54.

Mama yake Namouih aliitwa Zakia Masoud, aliyekuwa na miaka 48 wakati huu, naye alikuwa mweupe pia, mwenye sura nzuri na umbo namba nane kama wengi waliitavyo japo kwa njia yenye unene kiasi. Alikuwa ni mtu wa Arusha, naye alipenda sana mambo ya urembo na kujishughulisha na ususi kwenye saluni za wanawake na urembaji wa maharusi. Alikuwa mwongeaji sana, mkali, na ambaye sikuzote alipenda kujitanguliza kwanza kwa mambo mengi ingawa aliipenda familia yake kwa ujumla.

Wadogo zake Namouih walikuwa ni Sasha, Nasri na Nasma. Sasha alikuwa binti mwenye miaka 18, mweupe na mrembo, mrefu kumkaribia Namouih, na mwenye umbo zuri sana la kike. Wakati huu alikuwa anaelekea kumaliza kidato cha nne, naye alikuwa mpole sana na mwenye akili kama tu dada yake kwa kuwa alifanya vizuri sana kwenye masomo. Aliyefuata alikuwa ni Nasri, lakini mvulana huyu alipoteza uhai wake alipokuwa na miaka 6 kwa kuliwa na mnyama hatari wa porini, ingawa mpaka kufikia wakati huu haikueleweka alikuwa mnyama gani. Alikuwa mvulana mjanja sana aliyependa michezo, na kama angekuwa hai bado basi wakati huu angekuwa na miaka 13. Nasma ndiyo alikuwa wa mwisho, binti mdogo mwenye miaka 10, naye alikuwa anaendelea na elimu ya msingi wakati huu. Wote walibarikiwa kwa sura nzuri na weupe, ingawa Sasha hakuwa mweupe sana kama watoto wengine wa familia hii.

Familia yao ilikuwa na mgawanyiko mdogo wa kidini, kwa sababu Masoud alikuwa mwislamu na alipokutana na Zakia kabla ya kuitengeneza familia, mwanamke huyo alikuwa mkristo, na alikwenda kwa jina la Christina. Walipendana, na wakiwa bado vijana wadogo wakaonyeshana upendo wao na kusababisha Christina apate ujauzito wa Namouih wakati akiwa anasoma sekondari bado. Watu wa kiukoo wa Christina walikasirishwa sana na jambo hilo, nao wakamfukuza kutoka nyumbani kwa sababu ya jambo hilo. Wakati huo Masoud alikuwa amepanga chumba kimoja tu, akifanya biashara za hapa na pale, hivyo akampokea Christina na kumwahidi kwamba wangemtunza mtoto wao pamoja.

Kulikuwa na upinzani mkubwa kutoka pande zote za familia zao kwa sababu ya jambo hilo, lakini Masoud alikuwa na msimamo imara, naye akaendelea kupambana haswa ili amtunze mpenzi wake na mwanaye mtarajiwa. Ndiyo baada ya muda fulani kupita, Christina akawa amebadili jina lake na kujiita Zakia, ili kuendana na hali ya uislamu ya Masoud ingawa hakubadili dini kabisa, ndiyo wakafunga ndoa kwa misingi hiyo baada ya Namouih kuwa amezaliwa. Walitengwa na ndugu zao wengi, na hata mara ambazo walipitia magumu kiasi cha kujaribu kuomba msaada kwa ndugu, hawakupata chochote zaidi ya masimango tu, hivyo ilikuwa ni kupambana wao kama wao. Wawili hawa kwa pamoja hawakuwa na baba wala mama, mayatima, kwa hiyo hawangeipata huruma kutoka kwa wanaukoo walioendekeza chuki dhidi yao.

Misukosuko mingi waliipitia pamoja, na kwa miaka yote bado waliendelea kuwa pamoja mpaka kufikia wakati huu, ila sasa kukawa kumezuka tatizo kubwa. Namouih ndiyo alikuwa amemaliza masomo ya chuo kikuu na kupata digrii ya sheria, na ndiyo alikuwa mwanzoni tu kwenye masuala ya kazi akijijengea maisha yake na ili aendelee kuisaidia familia yake pia, pale alipopata taarifa kwamba baba yake ana ugonjwa mbaya sana, na alikuwa amepelekwa hospitali kupatiwa matibabu lakini hakuwa na muda mrefu sana wa kuendelea kuishi endapo kama hangefanyiwa upasuaji maalumu uliokuwa ghali mno.

Ugonjwa wake ulikuwa ni saratani ya mapafu. Ulisababishwa na vumbi kali lenye madini fulani ambayo yalimwathiri kwa kipindi kirefu sana alichokuwa akifanya kazi, na saratani hiyo ilikuwa ndani yake kwa kipindi kirefu bila yeye kujua, na hivyo sasa ilikuwa imefikia hatua mbaya na ndiyo maana ikamzidia ghafla na kudhoofisha mwili wake. Zilikuwa ni habari zenye kushangaza kwa sababu bwana Masoud alionekana sikuzote kuwa na afya nzuri, na ikawa wazi kwa wengine kuwa huenda alijua kabisa kwamba anaumwa lakini akakaa kimya tu na kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili aikimu familia yake. Na alikuwa amewafanyia mambo mengi sana.

Namouih alihuzunika mno. Yaani aliacha mambo mengi na kwenda hospitalini ili kuweza kufanya lolote kuokoa uhai wa baba yake. Alitumia pesa zozote alizokuwa nazo, na rafiki yake, Blandina, alikuwa pamoja naye katika hilo pia. Lakini kila jambo alilofanya lilikuwa njia tu ya kusaidia kumwongezea bwana Masoud siku za kuishi, siyo kuliondoa tatizo lake kabisa. Kama angepata pesa ya kutosha, basi mzee wake angefanyiwa upasuaji huo, lakini jinsi siku zilivyozidi kwenda ndiyo ambavyo Masoud angeendelea kudhoofika, ingawa dawa alizopewa zilisaidia kumsukuma kimaisha, na zilikuwa za gharama SANA. Mwanamke alikuwa ametumia njia zote kuhakikisha anakusanya pesa hizo, lakini zilizohitajika zilikuwa nyingi mno, na hasa kwa sababu angehitaji kuendelea kumsaidia baba yake apate dawa, ilimhitaji atoe pesa ambazo alitunza.

Familia yake ilimfahamu Blandina kuwa rafiki wa karibu sana wa Namouih kwa kipindi kirefu, hivyo naye alikuwa huku hospitalini mkoani kwao kuwapa mchango (support) wake wote alioweza. Yeye Blandina alikuwa na ndugu yake mwingine huku hivyo alikaa kwake kwa muda wakati akiendelea kuwa karibu na Namouih. Bwana Masoud angeongea mara kwa mara na binti yake kumwambia kwamba asisumbuke sana kutafuta njia za kuokoa uhai wake kwa sababu angepoteza hela nyingi na mwishowe mzee angekufa tu, lakini hilo ni jambo ambalo Namouih hangesikiliza kamwe. Alimpenda sana baba yake, naye alikuwa amejiahidi kufanya kila kitu alichoweza ili kumwokoa.

Kufikia kipindi hiki, Masoud na Zakia walikuwa na nyumba yao kabisa. Ilikuwa ya kawaida tu yenye vyumba kadhaa, ikipakana na zingine za majirani, na Namouih pia alikuwa anasaidia sana kuwawekea mambo mengi mazuri na ya kisasa ili ipendeze zaidi. Ni kwa jitihada zao na kutokata tamaa ndiyo vitu vilivyowafikisha huku ingawa ndugu zao wengi waliwatupa, na hata kuna baadhi yao walianza kujipendekeza kwa familia hii baada ya kuona vitu fulani vinanyooka kwao lakini Zakia hakutaka kabisa familia yake ijihusishe nao kwa lolote.

Basi, siku fulani ndani ya kipindi hiki ambacho bwana Masoud alikuwa amelazwa, Namouih akawa nyumbani pamoja na mama yake, wakifanya mambo ya hapa na pale kabla ya kujiandaa kwenda hospitalini kumwona mzee, kisha wakaketi kwenye masofa ili kula na kupumzika kidogo. Kule hospitalini alikuwepo Sasha kwa wakati huu. Zakia alikuwa anamwangalia sana Namouih wakati mwanamke huyu alipokuwa anafanya miamala fulani kwa simu yake, na kwa kutambua kwamba mama yake alikuwa anamtazama mno, Namouih akamuuliza shida ni nini, naye Zakia akaangalia tu pembeni kwa njia ya kukwazika.

Namouih akaweka simu chini na kumwangalia vizuri, kisha akasema, "Litakuwa jambo zuri ukiniambia shida ni nini maana unaniamgalia kwa njia inayoonyesha kuna tatizo."

"We' unaonaje? Hakuna matatizo?" Zakia akamuuliza.

"Kwa upande wako sijajua," Namouih akasema.

Zakia akamwangalia kwa ufupi, kisha akauliza, "Hii hali ya baba yako itakuwa na suluhisho, au ndiyo tunasubiri msiba tu?"

"Mama!" Namouih akasema hivyo kwa ukali kiasi.

Zakia akaangalia pembeni.

"Maneno gani hayo?" Namouih akauliza.

"Naongelea hali halisi. Masoud yuko vibaya, gharama ni kubwa, inahitajika jambo la haraka la sivyo...."

"Unapendekeza tufanye nini?" Namouih akamkatisha.

"Nimekutafutia mchumba mwanangu," Zakia akasema.

"Nini?" Namouih akauliza kama vile hajasikia vizuri.

"Ndiyo. Kuna... mwanaume fulani... rafiki yangu, aliniambia kwamba huyo mwanaume kijana anakupenda sana na anataka kukuoa pia," Zakia akamwambia.

"Ahah.... acha masihara basi!" Namouih akashangaa.

"Sikutanii."

"Unataka kuniozesha kwa mtu ambaye simjui?"

"Utakuwa na muda wa kukutana naye, kujuana naye vizuri,..."

"Mama, sina muda wa kuolewa kwa sasa. Mambo ni mengi, vitu vingi vinaniangalia mimi na wewe, unawezaje tu hata kunipangia jambo kama hilo bila me kujua? Tuko India hapa?"

"Hapana nisikilize. Ni kijana mzuri, ni mtaratibu..."

"Naona bado hujanielewa. Hilo suala sitaki kulisikia tena. Mama... napigana kwa ajili ya baba na wadogo zangu halafu unaniambia masuala ya kuolewa? Ndiyo yatasaidia kuleta hilo suluhisho unalotaka?" Namouih akauliza kwa uthabiti.

Mama yake akabaki kumtazama tu. Namouih akatikisa kichwa kwa njia ya kukerwa, kisha akanyanyuka na kuanza kuondoka kutoka hapo.

Zakia akasimama pia na kusema, "Namouih... Namouih nisikilize kwanza... ana pesa..."

Namouih akasimama, kisha akamgeukia mama yake. "Nini?" akamuuliza.

"Ana hela. Ukiolewa naye, kila kitu kitakuwa safi," mama yake akamwambia.

"Unamaanisha nini?"

"Ikiwa utaolewa naye, hautapaswa kuwaza kuhusu wadogo zako, sijui tiba ya baba yako... atakusaidia kwa hayo yote."

Namouih, akiwa ameweka uso ulioonyesha maswali mengi, akamsogelea mama yake karibu zaidi.

"Mama... unataka kuniuza?" akamuuliza kwa hisia.

"Hapana siyo kihivyo... namaanisha... baba yako anahitaji sana msaada, hali yake ni mbaya, na mimi nimefungwa mikono. Mkopo wako wa chuo bado unalipia, Nasma bado yuko shule unamlipia, na kuna huyo mdogo wako mwingine tunayemlipia..."

"Unashindwa nini kumwita kwa jina mama...."

"Nisikilize!" Zakia akamkatisha kwa ukali.

Namouih akaangalia pembeni.

"Hapa ni moja tu, hakuna mbili. Kwa muda mrefu tumemtegemea zaidi baba yako, na mimi biashara zangu haziendi, mambo ni magumu. Ingekubidi ukatishe mwaka wako wa mwisho... yaani... Namouih... wewe ndiyo uliyebaki kuwa tegemeo kuu hapa...."

"Mama... lakini..."

"Hata kama akikuoa, haimaanishi utaacha kufanya mambo unayotaka. Niamini, huyu mwanaume anakupenda, na siyo kwamba nataka tu akuoe kwa ajili ya faida, hapana. Ila kwa sasa ndiyo njia ya haraka itakayo...."

Namouih akawa anatikisa kichwa kukataa na kusema, "Mama... hapana. Naweza kuongea naye ukitaka, ni... nimweleze hali... labda hata anaweza kutusaidia, lakini siyo...."

"Tumia akili wewe binti! Nani sasa hivi atakupa vya bure?!" Zakia akamkatisha kwa ukali.

"Mama!" Namouih akashangaa.

"Kaa ukitambua hili. Ikiwa baba yako atakufa... akifa, Namouih... basi itakuwa ni makosa yako," Zakia akamwambia.

Namouih akabaki kutikisa kichwa kwa njia iliyoonyesha alifadhsishwa sana na njia ya mama yake ya kufikiri. Zakia akaondoka sehemu hiyo akimwacha binti yake anatafakari vitu vingi. Hiki ni kitu ambacho moyo wake ulipinga kabisa kuwa suluhisho la tatizo walilokuwa nalo. Akiwa anahitaji kutuliza akili yake kidogo, akaamua kumpigia rafiki yake kipenzi ili amsaidie kutoa misongo kwa kadiri ambayo ingetosha.

★★

Muda mfupi baadaye, mwanadada Namouih akawa ameondoka nyumbani na kwenda upande wa mji huo uliokuwa na harakati nyingi zaidi za hapa na pale. Blandina alikuwa ameshafika sehemu fulani waliyoahidiana kukutana mjini huko, ikiwa ni ya starehe kiasi kwa wengi, ili kupata kinywaji na maongezi pia. Baada ya Namouih kufika, kama kawaida macho ya wengi yalikuwa kwake, lakini yeye alipuuzia watu na kwenda kuketi kwenye meza alipokaa rafiki yake. Alikuwa amevalia baibui lenye rangi nyeusi na hijab iliyoacha sehemu ya uso wake wazi, na Blandina alikuwa amevaa gauni jeupe lenye maua-maua lililoubana mwili wake vyema.

Rafiki yake aliona wazi kwamba Namouih alikuwa na mkazo sana. Akamwitia mhudumu na kumwambia amletee kinywaji fulani kimoja mwanamke huyu alichopendelea, na mhudumu huyo akakileta na kwenda zake. Namouih akaanza kumwelezea Blandina namna mama yake alivyoongea muda fulani siku hiyo, akiona kwamba alikuwa amevuka mipaka yake kama mzazi na kumtaka afanye jambo hilo kwa kumbebesha yeye Namouih hatia kwa hali iliyokuwa imempata baba yake. Ilimtia huzuni sana, kwa sababu alihisi sasa kwamba alikuwa ameshindwa kumsaidia kabisa baba yake.

Blandina akawa anamtia moyo kwa kusema mambo yangekuwa sawa tu, na ndiyo akauliza kuhusu huyo mwanaume ambaye Namouih alitafutiwa na mama yake ili aolewe naye. Namouih akamwambia hata hakujua jambo hilo lilitokea wapi, yaani lilikuja ghafla sana, na ilimkera sana kujua mzazi wake angefikia hatua ya kumshauri afanye kitu kama hicho ambacho hakingekuwa na utofauti na kujiuza ili kupata pesa.

"Kwani me wanaume siwaoni? Ni wangapi wenye pesa waliotaka kuwa nami lakini nikawakataa? Sitaki mwanaume mimi kwenye maisha yangu, niliyopitia yanatosha. Sasa sa'hivi natakiwa tu kuwa na mtu kwa kuwa eti ana pesa, ili amsaidie baba yangu... nisipompenda? Mimi sijabumbwa kwa njia hiyo kabisa aah," Namouih akawa anaongea kwa hisia.

Blandina akatulia kwa ufupi, kisha akauliza, "Kwa hiyo... unamaanisha kwamba ingekuwa bora baba yako akifa kuliko wewe kuolewa ili kumsaidia?"

Namouih akamwangalia kwa macho makali.

"Samahani, namaanisha kwamba... najua yule mzee amewapigania sana kipindi cha nyuma. Kama kuna chance ya kuweza kumtoa kwenye teseko lake Nam... ni bora kuichukua nafasi hiyo haraka..."

"Teseko ndiyo nini? Sijawahi kusikia hilo neno..."

"Namouih..."

"Hivi kweli Blandina, na wewe unakubaliana na wazo la mama? Niende tu, nikutanishwe na mtu, anioe, halafu nimwombe sasa hela, 'baba yangu anaumwa, mlipie matibabu kwa sababu umenioa,' does that make sense?" Namouih akauliza kwa hisia sana, mpaka machozi yakawa yanakaribia kumtoka machoni.

"Ninajua hali mliyo nayo ni ngumu, na sikushauri ufanye kile ambacho moyo wako unakataa. Lakini umeshajaribu mambo mangapi rafiki yangu? Na muda unazidi kwenda. Sitaki kusema vibaya, lakini, mama yako...."

"Ninajua anataka tu niolewe na huyo mwanaume kwa sababu ya pesa, wala siyo kwamba baba ndiyo sababu kuu. Anautumia ugonjwa wake kama kigezo tu..."

"Usimhukumu vibaya namna hiyo, ingawa sipingi hilo. Lakini jaribu tu kuangalia uwezekano wa kupata suluhisho haraka kwa njia hiyo hiyo..."

"Unamaanisha nini?"

"Siyo lazima mpaka akuoe. Unaweza kumkubalia mama yako, akakuunganisha naye, halafu mkishajuana, wewe utampanga huyo mwanaume... yaani... Nam mpaka nashindwa nifanye nini kukusaidia rafiki yangu," akasema Blandina kwa hisia.

"Nimpange? Kwamba nimpe kitu fulani ili nipate pesa, kama hivyo si ndiyo?" Namouih akauliza kiupole.

Blandina akabaki kimya tu na kutazama chini.

Namouih akafumba macho yake kidogo, kisha akaangalia pembeni, akionekana kutafakari.

"Nikuagizie kinywaji kingine?" Blandina akauliza.

Namouih akatikisa kichwa kukanusha, kisha akatoa simu yake na kumpigia mdogo wake, yaani Sasha. Akamwambia kwamba angeelekea huko huko hospitalini muda si mrefu, hivyo ajiandae tu kuondoka na yeye ndiye angefika kukaa na baba yao. Baada ya kumaliza kuongea na Sasha, akamwambia tu Blandina anataka kuondoka, hivyo kama yeye bado alitaka kuendelea kubaki hapo basi ingekuwa sawa. Lakini Blandina akamwambia angeenda pamoja naye huko huko hospitalini, ili aweze kumsalimu baba yake Namouih pia.

Wawili hawa wakaanza kuondoka hapo baada ya kulipia, na giza lilikuwa limekwishaingia. Wakiwa wanaelekea upande ambao wangechukua usafiri, mvua ikaanza kunyesha. Ilianza taratibu tu, na walikuwa wanajitahidi kuharakisha ili kuwahi usafiri kabla haijawa kubwa, lakini ikaongezeka sana na kuwafanya waamue kujikinga usawa wa maduka lli kuepuka kulowana. Watu kadhaa walionekana kujikinga pia hapa na pale, huku wengine wakikimbizana na mvua hiyo, nayo ikazidi kuongezeka na kuwa kubwa zaidi.

"Jamani, mambo gani tena haya!"

Blandina akamsemesha Namouih kwa sauti kubwa ili asikie, naye Namouih akatikisa kichwa huku akijishika pande za mikono yake ili kusitiri baridi ndogo iliyomwingia. Alipotazama upande mwingine wa eneo hilo, aliweza kuona sehemu ya mbali kiasi iliyokuwa na jengo dogo, na hapo kulikuwa na mtu amesimama. Mwonekano wake kwa umbali huo ungemfanya yeyote adhani kwamba alikuwa amejikinga tu kutokana na mvua hiyo, lakini baada ya mwanga wa radi kumulika vyema kufikia upande huo, Namouih akatambua kwamba uangalifu wa mtu huyo ulielekezwa sehemu aliyokuwa amesimama yeye na Blandina. Hakuweza kumwona vizuri kutokana na giza ingawa mianga ya taa za nje ilimulika vyema, lakini Ilikuwa ni kama anawaangalia.

Namouih akampuuzia mtu huyo na kuangalia tu chini, na ni hapa ndiyo Blandina akamwambia ingekuwa bora zaidi wakizima simu zao kwa kuwa alihofia radi zingeweza kusababisha tatizo. Akaitoa yake na kuizima, na ile alipopeleka macho yake upande ule, akakuta mtu yule bado amesimama tu kwa njia ile ile. Yaani, kwa wakati huu, Namouih aliamua kutokwepesha macho yake na kumtazama moja kwa moja, na ilikuwa ni kama anaangalia sanamu kwa sababu mtu huyo hakutikisika hata kidogo. Ni hapa ndipo aliweza kutambua kwamba mwilini mwa mtu huyo kulikuwa na jaketi kubwa lililofunika mpaka kichwa chake, uso wake ukifichwa kama vile wote umeingia ndani ya kifuniko cha kichwani cha jaketi hilo.

Jambo hili likamfanya akerwe kiasi na kutazama pembeni tu, lakini hangejizuia kupeleka macho yake upande huo mara kwa mara, na alichokiona mwanzo kilibaki kuwa namna hiyo hiyo tu. Ilianza kumfanya ajiulize ni mtu wa aina gani angesimama namna hiyo, bila hata kujigeuza kidogo huku na huko. Mvua iliendelea kunyesha kwa nguvu, zikiwa zimepita kama dakika kumi, naye Blandina akasema ingekuwa bora kama wangekuja na miamvuli kwa kuwa hakupenda kusubirishwa namna hiyo.

Namouih akamshika mkono rafiki yake kwa chini na kumsogelea mpaka karibu na sikio, naye akamwambia kuhusu jambo hilo aliloona upande ule mwingine. Akamwambia amtazame mtu yule, kwamba alikuwa anawaangalia sana na hakutikisika hata kidogo.

"Wapi?" Blandina akauliza.

"Kule hivi ambako kuna gari dogo limepaki mbele ya duka, amesimama hapo," Namouih akasema bila kuangalia huko.

"Hakuna mtu hapo mbona?" Blandina akamwambia.

"Ah... we naye, unataka mpaka nimnyooshee kidole. Basi sa..."

Namouih alikuwa akisema hivyo huku akigeukia tena upande ule, lakini maneno yake yakakata baada ya kukuta kweli sehemu ile haikuwa na mtu kabisa.

"Wapi kuna nyani amesimama?" Blandina akamuuliza kiutani.

Namouih akawa amebaki kuangalia huko kwa umakini.

"Au ni kwingine?" Blandina akauliza.

"Hamna. We hukuona labda mtu anatoka hiyo sehemu?" Namouih akauliza.

"Hamna sijaona. Macho yako tu," akasema Blandina na kuangalia kwingine.

Kwa dakika chache, jambo hilo likawa limeichanganya kiasi akili ya Namouih, lakini mwishowe akapotezea na kuendelea kusubiri mvua ikate.

★★

Mvua ilipungua taratibu mpaka kufikia hatua ya kudondosha matone madogo madogo, na sasa zilikuwa zimekwishapita dakika zaidi ya ishirini wanadada hao wakiwa wamejikinga hapo. Wakaanza mchakato wa kuondoka eneo hilo, wakiwa waangalifu kwenye mwendo wao kwa kuwa barabara ilikuwa na utelezi kwa chini kutokana na ardhi kuwa tope pia. Wakafanikiwa kuifikia barabara ya lami, na kwa pande zenye mitaro barabarani hapo yalionekana maji mengi yakiwa yamejaa na kusonga kuelekea upande mmoja. Wakapata taxi na kuingia pamoja, kisha wakaanza sasa kuelekea kule hospitalini.

Walipofika, wakaelekea mpaka kule alikolazwa bwana Masoud, na hapo wakamkuta Sasha pamoja na Zakia. Namouih alikuwa ametarajia kumkuta mama yake huku, na baada ya Sasha kuwaona wawili hawa akawafata na kuwasalimu, kisha akamwambia dada yake kwamba mama yake pia ndiyo alikuwa amefika tu muda siyo mrefu. Blandina akaenda kumsalimia Zakia na kuuliza hali ya mgonjwa, na mama huyu akamwambia kwamba bado hali yake haikuwa nzuri na madaktari walisema watarajie lolote lile kwa muda wowote. Namouih alijua vizuri sana kuwa mama yake alisema hivyo ili kumuumiza, naye Blandina akampa tu mama huyu pole na kusema yuko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Namouih akampatia pesa Sasha na kumwambia atangulie nyumbani ili kuwa pamoja na Nasma, naye Sasha akatii kisha kukusanya vitu vichache vya kwenda navyo huko.

Baada ya Sasha kuondoka, Namouih akamsogelea baba yake na kumwangalia kwa hisia sana, kisha akakishika kiganja cha mama yake. Zakia akamwangalia binti yake kwa njia fulani iliyoonyesha ni kama amemkasirikia, lakini Namouih akamwambia alihitaji kuzungumza naye, hivyo watoke nje mara moja. Blandina akasema angebaki hapo pamoja na mgonjwa wakati huo, hivyo Namouih akatangulia nje, akifuatwa na mama yake nyuma. Wakaelekea mpaka sehemu iliyokuwa njia ndefu ya hospitali iliyoelekea pande mbalimbali, nao wakasimama kwenye kingo ya chuma; Namouih akimwangalia mama yake, lakini Zakia akitazama chini.

"Umekuja mvua imeshaanza kunyesha?" Namouih akaanzisha maongezi.

"Imenikuta njiani," Zakia akajibu.

"Baba alikuwa ameshalala ulipofika huku?" Namouih akauliza.

"Alikuwa macho," Zakia akajibu bila kumwangalia.

"Amekula angalau?"

"Mdogo wako anasema hakula chochote, alikuwa anasumbua. Nimefika nikampa juice. Amekunywa, ndiyo akalala..."

"Bado dawa za maji zinahitajika, si ndiyo?"

"Kila siku. Leo tu imekatika laki mbili, na mifuko inaisha, hela inakata. Ikifikia hatua pesa ikakosekana ndiyo basi tena."

"Usijali, nitapata tu ya kusukuma kwa wiki za mbeleni..."

"Utapata wapi?" Zakia akasema huku sasa akimwangalia.

"Kuna ishu ninafuatilia. Kilichopo tu ni kusubiri haitachukua muda mrefu na...."

"Ingekuwa afadhali kama ungechagua kazi inayolipa kwa uhakika na siyo kwa kubahatisha, maana kukaa kusubiri kitu ambacho hauna uhakika nacho inamaanisha Soud atakuwa ameshakufa kufikia muda huo..."

"Mama usiongee hivyo tafadhali..."

"Ni ukweli. Namouih nisikilize. Baba yako huyu amefanya kazi ngumu sana kukujengea maisha mazuri, na najua hakuwa na... matarajio labda tuseme... uje ulipie. Najua umefuata ndoto zako, lakini zinachukua muda sana kutimia ili wewe angalau uwe msaada kwetu. Ndugu zetu wametutenga tokea zamani, siwezi hata kufikiria kuwaomba msaada maana wanajua kabisa hali aliyonayo Masaoud lakini wametuacha... yaani tukome..."

Namouih akatazama tu chini.

"Baba yako ni mtu mzuri sana Namouih, anastahili kuishi maisha marefu, na kama kuna nafasi ya kumwokoa tunapaswa kuichangamkia. Kwa huu muda wote ambao tumejitahidi kupigana, ni kama jitihada zetu zinaelekea mwisho sasa... tunahitaji suluhisho la kudumu. Namouih me sitaki baba yako afe. Au wewe unataka afe?"

"Mama..."

"Najua unampenda pia. Lakini utapaswa kuonyesha hilo kwa kuzuia hatma hii. Mimi naipinga kabisa. Amebakiza wiki chache sasa, na angekuwa ameshaenda mapema tu. Unajua ni kwa nini bado yupo? Bado anataka kuishi Namouih. Anataka kuishi, kuziona sura zetu, kufurahia siku za mbeleni akiwa pamoja nasi. Kwa nini tumnyime hilo?"

Maneno ya Zakia yalimchoma sana binti yake, kwa kuwa alikuwa akimfanya ahisi hatia moyoni kwa kufikiria kwamba alishindwa kufanya jambo fulani kumsaidia baba yake. Ilikuwa wazi mama yake alitaka afanye nini, na kwa sekunde chache akabaki kimya tu akitafakari vitu vingi.

"Hapa hakuna msaada zaidi kwa baba yako, ni ubabaishaji tu yaani wanakula hela zetu kwa ajili ya dawa lakini hata wewe unajua hizo hazitasaidia lolote, anahitaji tiba nzuri.... ni kama wanamsogeza zaidi kwenye...."

"Okay, mama inatosha. Tafadhali," Namouih akamkatisha kwa ustaarabu.

Zakia akatazama tu pembeni.

Namouih akashusha pumzi, kisha akauliza, "Anaitwa nani?"

Zakia akamwangalia.

"Huyo mwanaume... anaitwaje?" Namouih akauliza tena bila kumwangalia.

Zakia akatabasamu kwa mbali, kisha akavishika viganja vya Namouih akionekana kufurahi. "Anaitwa Donald. Ni kijana mzuri sana Namouih, anakupenda sana," akamwambia.

"Una uhakika gani? Mtu anawezaje kunipenda halafu asijaribu hata kunitafuta?"

"Hapana, siyo hivyo. Huyu rafiki yangu aliyeniambia kumhusu ni Mage, unamkumbuka aunty Mage?"

Namouih akatikisa kichwa kukubali.

"Eee... yeye ndiye aliniambia. Huyo kaka inaonekana ameanza kukufatilia kwa muda mrefu. Mage yeye anafanya kazi kwenye moja ya maduka ya huyo kaka yaani anamiliki kampuni na maduka mengi... ndiyo alikuja kumsikia siku moja anakuongelea kwa rafiki yake, alikuwa anamwonyesha picha yako. Alikuwa anasema yaani kama ni kuoa anakuoa wewe tu... ndo' Mage akaja kuniambia sasa," Zakia akaelezea.

"Kwa hiyo inamaanisha kumbe hujawahi hata kukutana naye? Mbona ulisema umenitafutia mchumba kana kwamba mnajuana, wakati bado hata hujaongea naye?"

"Mage ndiyo ilibidi amwambie kwamba anakujua, na amesema kwa sababu kuna mambo mengi ya kikazi hapo nyuma Donald alikuwa bize, ila akaniambia kwamba amepanga kukutafuta. Mage alikuwa anataka kukuunganisha naye haraka lakini hakuwa na namba yako, na mimi sikuona inafaa kumpatia kabla hatujaongea. Namouih, ukiolewa na huyu kaka itakuwa jambo zuri sana kwa familia yet- kwa baba yako... na wadogo zako pia," Zakia akasisitiza.

"Nahisi ni kama nitajiweka kwenye hali mbaya nikijaribu kuchukua hayo maamuzi," Namouih akaongea kwa hisia.

"Hapana mwanangu, usifikirie hivyo. Huyo kaka atakufaa. Mage ameniambia ni mtu mmoja mstaarabu sana, hata aliponi-boost kidogo hela kwa ajili ya baba yako ni kwa sababu analipwa vizuri sana na Donald..."

"Ungekuwa ndiyo mimi ungeolewa naye hata sasa hivi kabisa eeh..."

"Ahah... Namouih acha mambo yako. Bahati imekuangukia wewe. Nataka tu uitumie vizuri ili kumwondolea baba yako mateso. Mambo mengine yatajipa tu, amini hilo," Zakia akaongea kwa ushawishi huku akikishika kichwa cha binti yake.

Namouih akatulia kidogo, kisha akasema, "Sawa. Fanya umpe rafiki yako namba yangu, ampe huyo Donald, anitafute. Tutaangalia na jinsi mambo yatakavyokuwa."

Wakati alipokuwa akisema hayo, Zakia alikuwa ameachia tabasamu lililoonyesha dhahiri kabisa kwamba alifurahi kupita maelezo. Uso wa Namouih ulionyesha hali ya hisia za kawaida tu, kwa kuwa alisema hayo kwa kinywa lakini hayakutoka moyoni. Ni kwamba tu katika pambano hili la kutaka kumwokoa mzee wake, ilionekana suluhisho lililokuwa limebaki ni yeye kutumiwa ili achune pochi ya mwanaume mwenye pesa ili kupata njia nzuri ya kumtibu baba yake. Ni jambo ambalo lilipingana kabisa na aina ya mambo aliyotaka kwenye maisha yake, lakini badiliko hili la hali lilifanya iwe lazima kwake kuchukua uamuzi huo; akiona jukumu la kuokoa maisha ya bwana Masoud lilikuwa lake.

Mama yake akamkumbatia kwa furaha, na kwa utani akamwambia kwamba anajua asingemwangusha maana alikuwa amezaa "pisi kali." Namouih hata hakutoa itikio la furaha ya kujilazimisha, naye akasema tu warudi kule ndani kuwa pamoja na baba yake. Walimkuta Blandina akiwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa bwana Masoud, akiwa anapitia mambo fulani kwenye simu yake. Wakaendelea kukaa hapo kwa dakika kadhaa huku wakiangalia mahitaji ya mgonjwa, kisha Zakia akaaga kwenda nyumbani, kwa kuwa Namouih ndiyo angebaki hospitali kwa usiku huo.

Baada ya mama mtu kuondoka, Blandina aliuliza ikiwa kila kitu kilikuwa sawa, naye Namouih akamwambia sasa kwamba aliamua kumtafuta huyo Donald ili wayajenge, na kama ikiwezekana aweze kumwomba amsaidie baba yake. Bado huyu dada aliliona jambo hilo kuwa lenye kutatiza sana; hakutaka kabisa kufanya hivyo. Lakini alikuwa amekwishaishiwa mawazo mazuri na ya haraka ya kusuluhisha tatizo la mzee wake, kwa hiyo ingekuwa lazima kuvaa moyo wa chuma ili jambo ambalo mama yake alitaka afanye litimie. Blandina akamtia moyo tu kwa kusema asiwaze sana, na kusema kwa utani kwamba angetakiwa kuonyesha mautundu yake mengi kwa huyo jamaa ili apagawe na kumwaga mamilioni. Angalau ni Blandina ndiye aliyeweza kulifanya tabasamu la Namouih lionekane kidogo kwa maneno yake yenye utani.

Muda uliposonga zaidi, Blandina alirudi kule alikokaa kwa wakati huu pia akimwacha Namouih hapo. Kama kawaida, mwanadada huyu akaendelea kukaa pembeni ya mzee wake mpaka usingizi ulipomchukua na kumpeleka kwenye ulimwengu wa ndoto.

★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next