Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Ysiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA PILI

★★★★★★★★★★★★★


Mshtuko mfupi niliopata ukanifanya nimeze kinywaji na kuvuta pumzi puani kwa wakati mmoja, nami nikapaliwa. Nikakohoa na kudondosha 'juice' kiasi kutoka mdomoni mwangu, kitu ambacho kilifanya wale wanawake wakubwa washtuke na kunitazama kwa kujali. Nikaendelea kukohoa kwa nguvu, nami nikasimama kabisa nikijitahidi kujizuia lakini nikawa nashindwa. 

"Hee... pole kijana wangu... umepaliwa?" akaniuliza yule mwanamke mweusi.

"Akh... kkhh... koh... koh..." nikaendelea kubanja.

"Zawadi, mfatie maji..." akasema hivyo mwanamke huyo.

Nafikiri Zawadi ndiyo lililokuwa jina la mwanamke huyu mweupe, naye akaenda upesi kule jikoni huku mwenzake akinisogelea na kunipiga juu ya mgongo kwa kiganja chake. Aisee nilikuwa nimepaliwa vibaya. Machozi yalinitoka, kooni nikihisi kama vile kimiminika kimeunganisha bomba la pua na mdomo kwa pamoja, nami nikawa namwangalia yule mwanamke mlangoni pale aliyenikata jicho la hasira. Maji yakaletwa, huku binti yule aliyelala sofani bado akiwa anatafuna tu vidole vyake kama vile hayupo. Nikaanza kunywa maji, na kikohozi cha kupaliwa kikawa kinafifia japo kooni palivurugika sana. Nikamwangalia yule dada pale mlangoni, aliyekuwa amesimama kwa utulivu tu, nami nikahisi aibu na kuangalia pembeni. 

"Uko sawa baba?" Zawadi mweupe akaniuliza.

"Akh... ndiyo... niko sawa..." nikajibu huku koo imenibana. 

"Pole sana baba... pole..." Zawadi akanibembeleza.

"Miryam... karibu mwanangu. Za huko?" yule mama mweusi akamuuliza mwanamke aliyesimama mlangoni.

Ke! Huyo ndiyo alikuwa Miryam? Nimekwisha.

Miryam mwenyewe alionekana kutaka kunipasua kabisa kwa jinsi alivyokuwa ananiangalia, lakini akaacha kunitazama na kumwambia mama huyo, "Ni nzuri. Shikamooni?"

"Marahaba," wakajibu wanawake hawa kwa pamoja.

Mpaka sasa nilikuwa nimesimama kwa ukaribu na Zawadi mweupe, akiwa anausugua mgongo wangu taratibu, nami nikamtazama mwanamke yule aliyetakiwa kuwa ndiyo mwenye nyumba wangu. Kufikia hapa ningeweza kutambua tu kwamba dili lilifeli, na alikuwa na kila haki ya kunikasirikia maana nilimtendea kama mtoto mdogo vile kule tulipotoka. Ah yaani mambo mengine haya! Eti ilipaswa tu kuwa yeye kati ya maelfu ya watu wote walioishi Dar!  

Mwanamke huyo ambaye sasa nilijua aliitwa Miryam, akafunga mlango na kusogea usawa wa sofa alilolalia yule binti, nami nikamwona akimshika sehemu ya shingo taratibu na kuibonyeza kidogo. Binti huyo, Mariam bila shaka, akanyanyuka upesi huku akiwa anatabasamu kwa furaha na kumkumbatia Miryam kwa nguvu sana, utadhani alimpamia. Huyo Miryam akatabasamu pia na kukishika kichwa cha mdogo wake kwa upendo. Kuwaangalia namna hiyo kukanifanya sasa nitambue kwa nini mwanzoni binti huyo aliponitazama nilifikiri sura yake haikuwa ngeni sana. Ni kwa sababu kwa kadiri kubwa alifanana na dada yake, mtu ambaye nilikuwa nimemwona siku hiyo. Binti akamwachia dada yake na kumwangalia usoni huku akicheka kwa pumzi za kujirudia-rudia kama mtoto vile, na dada yake akaingiza mkono ndani ya mkoba aliokuwa amebeba na kutoa boksi refu la biskuti na kumpatia. Akalipokea kwa furaha sana na kukaa kwenye sofa, naye akaanza kulifungua ili ale biskuti zake. 

Macho ya Miryam yakarudi upande wetu tena. Kiukweli, kiukweli, huyu mwanamke alikuwa mrembo. Hata mara ya kwanza tulipokutana niliona hilo lakini hasa baada ya kujua sasa kwamba alikuwa mrangi ndiyo ikawa wazi zaidi ni kwa nini. Alikuwa mrefu kwa kadiri iliyomfaa mwanamke, mwenye mwili mzuri ulionawiri, kiuno chembamba na miguu mirefu yenye unene wa chupa ya Dompo. Alibeba mapaja manene kiasi yaliyoitesa sketi aliyovaa kwa kuivutisha zaidi kila pande, na hapo bado sikuwa nimemchora huko nyuma vizuri ila nilijua kuna hazina matata iliyokuwa imetunishwa huko. Alionekana kuwa mwanamke makini sana asiyependa mchezo, na ndiyo jambo ambalo lilifanya nisikazie fikira sana masuala ya uanamke wake zaidi ya masuala yaliyonileta huku; ukitegemea tayari nilikuwa na kesi ya mkosaji kwake.

"Tesha amerudi?" Miryam akauliza.

Sauti yake nzuri ikanifanya nikumbuke namna alivyoniongelesha kwa kujali sana kule tulikotoka.

"Hapana, bado hajaja," mwanamke yule mweusi akamwambia.

Kwa jicho la pembeni, niliweza kumwona Zawadi mweupe akimwonyesha Miryam kwa ishara ya macho kuwa niko hapo, na mwanamke huyo akaniangalia. Alinitazama kwa umakini sana, naye akapiga hatua tatu nne kunielekea huku bado nikiwa nimesimama. Nikaweka uso tulivu tu, nikihisi labda hata natakiwa kusema "shikamoo."

"Ndiyo wewe?" 

Miryam akaniuliza hivyo, na kama angekuwa ni mtu ambaye amefika akiwa na malengo mengi ya kumfikisha hapo, basi nisingeweza kujua aliuliza hivyo kuelekea lengo lipi. Lakini langu lilikuwa ni moja. Kuja kupangishwa hapo, basi. 

Hivyo nikielewa swali lake lililenga ishu hiyo, nikajibu, "Ndiyo."

Sikuendelea kukohoa tena, na wakati huu nilijivika tu ujasiri wangu wa kiume ingawa bado nilihisi vibaya kwa nilichokuwa nimemfanyia. Baada ya kumpa jibu hilo alinishusha na kunipandisha kama kuonyesha haamini vile, nami nilielewa sababu kuwa yeye kutopendezwa nami. Haingejalisha tena kuhusu yaliyotokea ikiwa tu ningemwomba samahani, na kama asingeikubali basi 'fresh,' ningetafuta tu sehemu nyingine ya kukaa. 

Nikawaangalia mama zake kwa ufupi, ambao walitutazama sisi wote kwa umakini, nami nikamwangalia Miryam usoni na kusema, "Naomba kuongea nawe Miryam... kibinafsi."

Aliniangalia machoni bila kukwepesha hata kidogo, na wanawake wale wawili wakaendelea kunitazama.

"Kama ni sawa. Twende chumbani, halafu tuzungumze," nikamwambia hivyo kwa sauti yenye uhakika.

Akanikazia macho yake na kuuliza, "Unataka... nikupeleke chumbani?"

"Ndiyo. Nionyeshe chumba... ili tuongee pia," nikamwambia hivyo.

Nilikuwa namwonyesha kwa lugha ya macho kwamba nilihitaji tuzungumze kuhusu tatizo letu, lakini aliniangalia utadhani amechanganyikiwa. Akawatazama wale wanawake kwa mshangao fulani hivi, na hata mimi nilipowaangalia nikaona wananitazama kimaswali kiasi.

Lakini Zawadi mweupe akaachia tabasamu na kusema, "Ni sawa tu... nyie nendeni mkaongee... sisi tutakuwa hapa hahah..."

Nikamwangalia Miryam usoni na kuona ni kama vile anashangazwa na mimi, na nilichukulia hiyo kuwa kwa sababu labda hakutaka kunipeleka chumbani. Lakini akaangalia pembeni kiasi na kushusha pumzi, kisha akaanza kutembea taratibu kuuelekea upande ambao bila shaka ungefikia vyumbani. Sikuhitaji kupewa agizo, hiyo ilikuwa ishara tosha kwangu. Nikawapa tabasamu hafifu wanawake hao wawili na kubeba begi langu, kisha nikaanza kumfata mwanamke yule. Sijui ni kwa nini lakini eti wakawa kama vile wanashangaa kuona nimelibeba na begi kabisa. Ah ugeni huu! Bora nisingelazimisha kutafuta huduma ya aina hii maana hali yote ya hapa ilizidi kunichanganya. Kumfata mwanamke huyo kulinipeleka upande wa nyumba hiyo uliokuwa na korido fupi lenye milango mitatu ya vyumba vya kupumzikia, na kona nyingine iliyopeleka mtu kwenye choo na bafu. Angalau sasa niliweza kulichora umbo lake huko nyuma, na alikuwa amebarikiwa kubeba mzigo wa maana! 

Yeye akaingia ndani ya mlango wa chumba cha mwishoni, na nilipofika hapo nikakuta amesimama mlangoni kama kuniruhusu niingie, nami nikampita na kuingia. Bado alikuwa akinitazama kimashaka fulani hivi, lakini baada ya mimi kuingia ndani humo mashaka yangu ndiyo yakapanda zaidi. Chumba hicho kilikuwa kizuri; kizuri mno. Lakini ulikuwa uzuri ambao ulimfaa mwanamke, si mwanaume. Vitu vingi sana vilikaa kimaua-maua tu, kuanzia mashuka yaliyotandikwa mpaka kabati la nguo lililopambwa kwa maua, na hata upande mmoja kulikuwa na meza ya kujipambia mwanamke iliyo na kioo kirefu pamoja na vipodozi na manukato! Nikatembea na kuingia ndani zaidi nikiwa nakiangalia kwa umakini, fikira zikiwa kwamba huenda kuna mwanamke aliyekuwa akikaa humo na sasa hakuwepo, ndiyo mimi ningechukua nafasi yake. Siyo kuchukua nafasi ya kuishi kike, ila nafasi ya kulala kwenye chumba!

"Umekuja na begi kabisa?"

Sauti yake Miryam iliyouliza swali hilo ikanifanya nimgeukie na kumtazama. Bado aliniangalia kana kwamba hanielewi hata kidogo, na mimi kiukweli nilikuwa nimeanza kuchanganyikiwa.

"Chumba ndiyo hiki?" nikamuuliza.

"We' unakionaje, ni sebule?" na yeye akaniuliza.

"Hapana, namaanisha... kina mwonekano wa kike sana. Ama ndiyo mnavyopamba siku hizi kwa ajili ya wageni? Nikilala humu nitajihisi kama princess," nikasema.

"Kulala kivipi?" akaniuliza.

"Kulala kulala. Si ndiyo nitalala humu?"

"Hakuna chochote kilichopangwa, unanielewa? Huwezi kulala humu."

Njia aliyotumia kunisemesha ilijaa kisirani sana, na tayari nilijua sababu kuwa nilimuudhi kwa hiyo nikachukulia yote hayo kuwa majungu tu. Nikaweka begi chini na kusogea mpaka kufikia aliposimama, naye alikuwa ananitazama usoni kwa umakini mno.

"Sikiliza dada. Najua hatujakutana kwenye mazingira mazuri, na ndiyo maana nimeomba uje nami humu ili nikuombe tu samahani. Huna sababu ya kuendelea kunikasirikia, mimi siyo mtu mbaya... muda ule nilihitaji tu msaada, lile eneo sikulifahamu, na usiku ulikuwa unaingia... ndiyo maana nikafanya vile..." nikamwambia hivyo kwa sauti ya chini.

Akaangalia pembeni na kubana midomo kwa njia fulani ya kukerwa.

"Hayo ya saa zile tuyasahau. Me napenda amani, halafu na hapa nimepapenda. Nataka nikae hapa," nikamwambia.

Macho yake mazuri yakarudi tena kwangu, akinitazama kama vile bado hanielewi, naye akasema, "Na wewe nisikilize. Sipendi michezo isiyo na faida. Umeanza kunifanyia michezo huko nyuma, na umeileta mpaka hapa. Kuna lolote lililopangwa kukuruhusu ulale chumbani kwangu?"

Nikakunja uso kimaswali kiasi. Chumbani kwake? Sikuelewa vizuri.

Akashusha pumzi kiasi kama kujipa utulivu, kisha akaanza kusema, "Nisikilize Festo..."

A-ah! Festo gani tena? Mbona alikuwa ananichanganya?

"Mimi sitakuwa mwongo kwako. Hili suala haliwezi kufanikiwa. Ni sawa wakubwa wetu wanataka kutusaidia lakini siko tayari kuanzisha mahusiano na wewe, achilia mbali kuolewa..."

Eh! Nikabaki kinywa wazi kiasi huku namwangalia kwa umakini, kwa sababu kiukweli alikuwa ameniacha Mbezi.

"Kama wewe ni mtu mzima naweza kuamini kwamba utanielewa, na ndiyo maana niliyaruhusu haya yote ili tukutane, niweze kukwambia wewe kama wewe. Ndoa ni jambo zito, na bado... bado siko tayari. Sijui hata Shadya aliwaza nini kudhani mimi na wewe tungeendana kwa kweli... kwanza unaonekana kabisa ni mdogo kwangu. Mimi kwa ombi hilo... makubaliano yote ambayo amefikiri tunaweza kufanya... siko tayari. Nadhani inaeleweka kaka'angu..." akayasema hayo kwa sauti tulivu. 

Niliinamisha uso kiasi nikiwa natafakari yote aliyosema, na sasa kila kitu kikawa kimeeleweka kwangu. Hawa wanawake walikuwa wanamsubiria mtu mwingine tofauti na mimi, ambaye labda alikuwa na mipango ya kuja kumchumbia huyu dada. Shadya ndiyo alikuwa mshenga, muunganishi wao. Kwa hiyo mimi nilipofika hapa, wale wanawake wawili walifikiri mkwe ndiyo kafika, na kwa kweli hali nyingi zilikuwa zimeingiliana kwa njia iliyofanya nijikute natendewa kwa njia ambayo aliistahili huyo Festo aliyetarajiwa kufika. Mpaka wali wake na nyama niliula! Nikajikuta naachia tu tabasamu na kutikisa kichwa kwa kutoamini jinsi hali hii ilivyonifikisha mbali namna hiyo.

Miryam alipoona natabasamu, akaniuliza hivi, "Nilichokisema kimekupa furaha, au?"

Nikamwangalia, nami nikashindwa kujizuia kucheka kidogo kwa pumzi, kisha nikasema, "Ndiyo, ndiyo, sawa."

"Usiseme sawa, nimekwambia hapana," akasema.

"Ndiyo, sawa imemaanisha hapana..." nikasema hivyo.

Akaniangalia kama vile hanielewi.

"Pole dada. Kuna mwingiliano umeingiliana hapa... mimi siyo unayemdhania," nikamwambia.

"Nini?" akauliza kwa sauti ya chini.

"Mimi nimekuja huku kwa...."

Maneno yangu yakakatishwa baada ya kumwona Zawadi mweupe akiwa amefika nje ya chumba hicho, na Miryam akageuka kumtazama pia. Uso wa mama huyo ulionekana kutatizika kiasi, naye akaendelea kusimama hapo huku akiniangalia kimaswali. Miryam akamsogelea karibu na kumuuliza kuna nini, naye akamwambia kwamba Shadya alikuwa amefika, pamoja na wageni. Wote kwa pamoja wakanitazama tena usoni, nami nikalifata begi langu na kulibeba tena, kisha nikawasogelea na kuwaomba turudi pamoja sebuleni, nao wakakubali. 

Tulipofika pale sebuleni, watu walikuwa wameongezeka, isipokuwa binti yule mdogo niliyemwacha akila biskuti ndiye ambaye sikumkuta kwa wakati huu. Wageni niliowakuta hapo walikuwa watu wazima wanne, wanawake wawili, wanaume wawili. Wanaume walikuwa watu wazima kwa pamoja kufikia miaka 40 hivi, pamoja na mwanamke mmama mwenye kama miaka 60 hivi. Wote walisimama kukaribiana na masofa baada ya kumwona Miryam. Ukijumuisha na yule mwanamke mweusi pia, sasa kila mtu hapo akawa amesimama. Kwa wale wageni waliofika, mwanamke mmoja mwenye umri mkubwa kufikia miaka 45 hivi aliyevalia baibui na ushungi, aliniangalia kiudadisi sana, kama kujiuliza mimi ni nani. Kila mmoja wao alielekeza umakini wake kwangu isipokuwa Miryam, ambaye alisimama tu kwa utulivu baada ya kuwaamkia wawili wa wageni wale ambao walimzidi kiumri. Mimi pia nikawaamkia wote, nao wakanijibu vizuri kasoro mwanamke huyo aliyevaa ushungi.

"Huyu ni nani?" mwanamke huyu aliyevaa ushungi akauliza.

Wanawake wale walionikaribisha wakanitazama tu kama vile wanasubiri mimi ndiyo nitoe jibu, na kwa kutumia akili ya haraka, nikamuuliza mwanamke huyo, "Wewe ndiyo Shadya, eti?"

Huyo mvaa ushungi akatikisa kichwa kukubali.

"Aaa sawa. Aisee... kuna mabiti yame-mix vibaya sana hapa ahah... nimejichanganya kidogo," nikawaambia. 

Wote sasa wakawa wananiangalia.

"Mimi natokea Sinza, nimekuja Mbagala leo kuna hii nyumba nilikuwa natakiwa kufikia, sasa... ramani imenileta mpaka hapa, nikafikiri ndiyo penyewe, sijui nimekosea wapi..." nikawaambia.

"Ulikuwa unaenda kufikia wapi kwani?" Shadya akaniuliza.

Ongea yake ilikuwa 'sharp,' akionekana kuwa mswahili mkomavu, nami nikasema, "Kuna nyumba inafanyiwa upangishaji mpya wa vyumba... niliwasiliana na aliyetoa tangazo, sasa tukakubaliana nije ili... nikae hapo."

"Lakini ramani ikakuleta hapa?" akauliza mwanamke yule mweusi, ndugu ya Miryam.

"Ndiyo," nikamjibu.

Zawadi mweupe akaonekana kutafakari kitu fulani, naye akaniuliza, "Umesema nyumba ya kupangishwa?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Ahaa... hiyo nyumba ni hapa hivi pembeni, kwa huyu jirani yetu. Ankia si alikuwa ameshatuambia anataka kupanga na mtu juzi juzi?" Zawadi akawasemesha wakina Miryam.

"Eeeh ndiyo..." akajibu yule mwenziye nisiyemjua jina, la sivyo labda na yeye ningemwita Zawadi mweusi.

"Baba ni hapo hivi... ukivuka huu ukuta wetu," Zawadi mweupe akaniambia.

"Hii nyumba ya pembeni kumbe?" nikauliza.

"Eee..." akaitikia.

"Ina maana hukuwa umewasiliana na Ankia akwambie nyumba yake ilipo?" Shadya akaniuliza.

"Tuliwasiliana kwa WhatsApp, nikamwambia nitakuja siku yoyote wiki hii, sema nimechelewa tu kidogo leo... kuna katatizo kalitokea," nikasema hivyo na kumtazama Miryam.

Alikuwa ananitazama usoni kwa umakini, nami nikaangalia pembeni.

"Kwa hiyo alipofika hapa mkafikiri ndiyo Festo?" Shadya akawauliza wale wamama huku akimwonyeshea huyo Festo kwa kiganja chake.

Nikamwangalia jamaa. Alikuwa mmoja wa wale wanaume wawili waliosimama hapo, mrefu kiasi kunipita, mweusi, na mwenye mwonekano nadhifu wa kiutu uzima. Alikuwa na sura tulivu tu, na ndevu nyingi kidevuni pekee, na kwa kumtazama upesi ningeweza kukisia alikuwa mtu mwenye pesa. Bila shaka wale wengine waliokuwa naye walikuwa ndugu zake ama wazazi, nami nikamtazama Miryam na kuona ameangalia chini tu.

"Eee ndiyo, tukafikiri ni yeye. Jamani! Haya ni makubwa... naombeni radhi sana," Zawadi mweupe akasema hivyo.

Nilijihisi vibaya kiasi ukitegemea na ukweli kwamba wanawake hao walinitendea kwa ukarimu sana. Shadya akawa ananiangalia kama vile hanitaki, yaani hataki niwe hapo, na kiukweli sikutakiwa kuwa hapo. Huenda hata ningesababisha wadhani mchumbiwa ameshaliwa! 

Nikalivuta begi langu vizuri mgongoni na kusogea usawa wa Zawadi na mwenzake, nami nikasema, "Asanteni sana, japokuwa tumekutana katika mazingira yenye kuchanganya lakini... nashukuru kwa ukarimu wenu. Msosi ulikuwa mtamu sana."

Zawadi mweupe akatabasamu kiasi na kunishika begani, na mwenzake akatikisa kichwa tu kuonyesha uelewa.

Nikawatazama wageni, ambao bado walikuwa wamesimama wakiniangalia, nami nikasema, "Jamani, msiendelee kusimama, kaeni. Karibuni mkae."

Shadya akaanza kuwaambia wageni wakae kweli, na nilipomwangalia Miryam nikakuta amenikazia sura. Najua alikuwa ananishangaa kwamba mimi si mwenyeji hapo lakini nawaambia wageni wakae kana kwamba palikuwa kwetu, nami nikatabasamu kidogo na kisha kuuelekea mlango. Nikaufungua na kuwapungia mkono kuwaaga, na akina mama wale wakanipa heri na usiku mwema. Nilipomwangalia Miryam tena, alikuwa amenikazia tu jicho lake kwa umakini, na sijui ni nini tu lakini njia yake ya kununa ilimfanya apendeze sana kiasi kwamba sikuweza kujizuia kutabasamu kila nilipomwona namna hiyo, nami nikafungua tu mlango na kutoka ndani humo. 

Nikaanza kuondoka hapo huku nikiwaza jinsi bahati ya leo ilivyokuwa ikipingana sana na mimi, kuanzia kuharibikiwa na daladala mpaka kuingia kwenye sebule ya mhusika nisiyetakiwa kukutana naye. Ila huyo Miryam alikuwa ameifanya jioni hii iburudishe sana siyo siri. Nikatoka zangu mpaka nje ya geti, na hapo nje lilikuwepo gari aina ya Volkswagen Touareg nyeusi, bila shaka ikiwa ni ya mchumba Festo. Nikawaza ikiwa Miryam alimaanisha kweli kile alichokuwa ameniambia alipofikiri mimi ndiyo nimekuja kumchumbia, basi hata huyo Festo angerudi kwao mikono mitupu. Ila kuna kitu chochote kile ambacho pesa haiwezi kubeba siku hizi? Aa wapi! 

Nikavuka tu nyumba hiyo na kwenda ya pembeni. Kwa nje, kulikuwa na duka la bidhaa, na ndani niliweza kumwona mwanamke mwislamu akiwa ameketi huku akinyanyua kichwa chake kunichungulia kutokea ndani humo, nami nikapapita tu na kuingia ndani ya geti jepesi la vyuma vyembamba kama milango ya gereza. Lilikuwa wazi, nikaelekea ndani zaidi ya upande huo, na ukuta ule uliozitenganisha nyumba hizo ulikuwa na... niseme urembo labda, urembo wa matundu manene kuuzungukia ulioruhusu kuiona nyumba ya akina Miryam kwa nje, pale ndani ya geti lao. Nikaenda mpaka kwenye mlango wa nyumba hii sasa. Ilikuwa pana pia, lakini si sana kama ya akina Miryam. Kulikuwa na uvaranda mpana uliojengewa matofali madogo-madogo ya simenti yenye mtindo wa urembo, nikaona jengo lingine dogo kwa nje lenye milango miwili kwa ukaribu; bila shaka choo na bafu, sinki fupi la kuoshea vyombo likiwa limejengwa kutokea ukutani, na kamba za kuanikia nguo kwa juu. Hakukuonekana kuwa na watu wengi hapa na inawezekana aliye ndani tayari alikuwa amejifungia kwa ndani maana ilikuwa saa nne hii, ila nisingeweza kujua. 

Nikaugonga mlango mara tatu na kusimama kwa kusubiri. Haikuchukua muda mrefu sana na mlango ukafunguliwa, na hapo mbele yangu alisimama mwanamke mtu mzima ambaye kwa haraka ningeweza kukisia alikuwa kwenye miaka ya thelathini hivi. Alikuwa na mwili ulioukimbilia unene, mwenye uso wa duara na midomo mikubwa ya denda nzito. Macho yake yakiwa ya kungu kiasi, sura yake ilipendezeshwa kwa weupe fulani hivi uliotokeza sana, nadhani wa mapodozi, kwa kuwa rangi ya mikono yake haikuwa nyeupe namna hiyo. Alivaa kilemba kilichofunika nywele zake ama labda kipara, dera pana mwilini, lakini bado liliuchora mwili wake vyema kuonyesha kwamba alikuwa na mapaja na miguu minene, na puani aliweka pini ndogo ya urembo. Alinitazama kwa macho fulani... laini, kama vile hajiulizi nilikuwa nani, lakini tena akisubiri kujua mimi ni nani.

Ingawa alionekana kuwa mkubwa kwangu, nikamwambia, "Mambo vipi?" kwa sauti tulivu.

"Poa," akajibu hivyo na kubana midomo yake.

"Wewe ndiyo mwenye mji?" nikamuuliza.

"Ndiyo. Wewe ni nani?" akaniuliza.

"Mimi ni yule kijana tuliyewasiliana WhatsApp, kuhusu ile ishu ya kuishi kwa kulipa kodi kwenye nyumba yako..." nikaeleza.

"Aaaa, ndiyo wewe?" 

"Ndiyo."

"Sawa. Karibu, karib... karibu ndani," akanikaribisha.

Aliacha uwazi zaidi ili nipite, nami nikaingia mpaka sehemu ya sebule huku nikisikia anaufunga mlango. Sebule hii haikuwa pana sana, lakini ilipambwa vizuri mno. Vigae sakafuni, vilivyofunikwa kwa kapeti zito jekundu lililobeba meza ndogo ya kioo, masofa mawili marefu na moja lingine dogo yaliyopangwa kuizunguka meza hiyo, feni kwenye kona moja ya ukuta, na TV ya 'flat screen' iliyobebwa kwa vyuma vyake vilivyounganika na ukuta juu kiasi. Kulikuwa na mapambo ya midoli kwenye meza ile ya kioo na masofa yalipambwa kwa kutunikiwa vitambaa; bila shaka kuficha zaidi ngozi zake zenye nyufa nyingi kutokana na kuchanika. Niliona upande mwingine wa mbele zaidi wenye ukuta uliokuwa umetenganisha milango miwili, bila shaka ya vyumba, na upande mwingine ulionyesha sehemu ya jikoni ambayo haikuwa na mlango. Palinukia ile harufu ambayo wanawake waislamu hupenda kuivaa, sijui manukato ya kuchomwa, kitu kama hicho. Lakini huyu hakuonekana kuwa mwislamu. 

Nikamgeukia mwenyeji wangu, ambaye alikuwa anasogea upande wangu huku amevibana viganja vyake kwa mbele, na akiniangalia kwa macho yenye subira. Nikamwangalia kwa macho yenye upendezi, naye akatabasamu kwa haya kiasi na kuangalia chini. Athari niliyonayo kwa wanawake!

"Kwa hiyo... nimefika sehemu sahihi?" nikamsemesha.

"Eeeh... ndiyo hapa," akajibu.

"Najua hukutarajia nije leo, halafu usiku sana..."

"Hapana, mbona bado mapema? Hamna shida. Karibu sana," akasema kwa sauti yenye kuvutia.

"Asante. Uko mwenyewe?" nikamuuliza.

Akatikisa kichwa mara moja kukubali, kwa njia ya shau.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Poa, basi... nionyeshe chumba af' tuongee mengine."

Akanipita tu na kuuelekea mlango wa mbele zaidi kati ya ile miwili, nami nikamfata. Ningetaka kumuuliza upesi kwa nini aiishi peke yake kwenye hiyo nyumba, ikiwa alikuwa na familia labda, ama kama haikuwa yake yeye na alikuwa mtunzaji tu, lakini hayo yangepaswa kuja baadaye. Hapa suala lililokuwepo ni kwamba ningeishi kwenye nyumba hiyo pamoja na mwanamke bila mtu mwingine kuwepo, kwa hiyo ya kutegemea yalikuwa mengi. Yale mambo yetu yale! Mwanamke mwenyewe alikuwa anatembea kwa kutikisa kweli maana na yeye alikuwa na zigo tenteme, nami nikaingia pamoja naye ndani ya chumba hicho. 

Kilikuwa na mwonekano safi na mpangilio mzuri wa vitu vichache tu vilivyokuwemo. Kulikuwa na kitanda chenye ukubwa wa nne ya sita, kilichotandikiwa shuka jeupe na safi sana. Mito miwili ilikipendezesha zaidi, na neti ilifungwa juu kwenye 'ceiling board' kukielekea, ama kwa kiswahili tulivyozoea kuiita, basi ni singibodi. Kulikuwa na kabati la kuwekea nguo ukutani, na uwazi mpana kiasi sakafuni kutokea mwisho wa kitanda ambao ungeniruhusu kuwekea vitu vyangu vingine kama viatu. Na palinukia harufu yake huyo mwanamke. Nikapatazama kwa kuridhishwa sana kwa kuwa palifanana na jinsi nilivyotaka pawe kabisa, kawaida, patulivu, angalau kwa jinsi palivyoonekana. Nikamgeukia mwenyeji wangu na kukuta ananiangalia tu usoni, lakini ndiyo akakwepesha macho yake baada ya yakwangu kugongana na yake. 

Nikashusha pumzi na kusema, "Pazuri. Pametulia."

"Ndiyo. Huku hamna makelele yaani unalala vizuri kabisa," akasema.

"Na mbu kama wote..."

"Ahahah... unachoma tu dawa, af' unashusha neti. Hawasumbui. Hata usiposhusha neti, ukishachoma tu dawa wanaisha, unalala kwa amani."

"Sawa. Tutakuwa tunaishi kinyumbani zaidi kwa hiyo mengi ya hapa utanielekeza ili niendane vizuri na mazingira, au siyo?"

"Hamna neno."

"Kwa hiyo, utataka nikulipe kila tarehe ya mwanzo wa mwezi, ama mwishoni?" nikamuuliza.

"Wewe tu," akaniambia hivyo huku akiangalia pembeni.

"We' ndiyo uniambie, si ndiyo mwenye nyumba wangu?"

"Ahah... ni wewe tu, me... hata ukilipia sa'hivi au mwishoni mwa mwezi sawa tu."

"Mh! Mbona kwenye tangazo ulisema malipo kwanza? Je nikikwambia nitakulipa mwishoni halafu nikakimbia kabla mwezi hujaisha?" nikamuuliza kichokozi.

"Hahaah... hapana, huwezi. Kesho tunapaswa kwenda kwa mwenyekiti ukasaini pepa fulani la makubaliano. Kwa hiyo ukikimbia jela inakuhusu," akasema hivyo na kuniangalia kwa ufupi.

Alionekana kunionea aibu kiasi.

Nikamwambia, "Aaa, basi poa. Uko makini kumbe."

"Eee... lazima kuwa makini. Hapa mjini, ukizubaa unaachwa kweli," akaniambia huku akitabasamu.

"Safi sana. Ila usijali sitakukimbia. Na... nataka nikulipe sasa hivi ya miezi miwili kabisa," nikamwambia.

"Siyo lazima sasa hivi kaka, wewe... pumzika tu. Mengine hata kesho," akaniambia kwa njia fulani yenye kubembeleza hivi.

Dah! Haya bwana. 

Nikamwambia, "Asante. Jina lako Ankia, si ndiyo?"

Akaniangalia kimaswali kiasi huku akitabasamu, naye akauliza, "Umejuaje? Hatukuambiana majina WhatsApp. Ama umesoma kwenye namba jina la usajili?"

"Hamna, nimelijua leo, muda sio mrefu. Wakati nakuja nikapotea njia, nikaingia kwenye nyumba hiyo jirani nikifikiri ndo' kwako..." nikasema.

"Wewee!" akanena hivyo kimshangao kiasi.

"Ndiyo. Wakaniambia nimekosea, wakanielekeza hapa na jina lako ndo' nimelijua kutoka kwao."

"Aisee... hahaha pole mwaya," akaniambia huku akitabasamu.

"Sijui ingekuwaje kama ningeingia kwenye nyumba ya wanoa visu," nikamtania.

Akacheka kidogo na kusema, "Wangekunoa. Huku wahuni wengi unajua..."

"Na wewe ukiwemo?"

"Akhaa... mie nakulaga zangu za kistaarabu tu, hayo maisha ya waswahili tunawaachia wengine ndiyo wanayawezea..."

"Eti eh..."

"Eeeh."

"Wewe na nani mwingine?"

"Mimi na hao majirani zangu uliotoka hapo kwao, yaani hatuna zile shobo na watu wengi. Tunaishi kivyetu sana. Watu wa huku wakikuzoea mno ni mpaka nguoni."

"Hahah... hiyo iko kila sehemu," nikasema.

"Yeah, sioni kama inafaa. Kwa hiyo... wewe unaitwa nani?" akaniuliza.

"JC," nikamwambia.

Akatabasamu kidogo na kusema, "JC. Jina zuri."

"Asante."

"Ni kifupi cha?"

"Jina Chafu," nikamwambia kiutani.

Akacheka kidogo na kusema, "Sawa. JC ndiyo inafaa zaidi."

Nikaweka begi kitandani pale, na huwezi amini mpaka kufikia hapo bado nilikuwa nimelibeba. 

"Kuna joto," nikasema hivyo.

"Usipime yaani. Tunajimwagiaga kabla ya kulala angalau mwili unakuwa fresh," akasema hivyo.

Sikutoa itikio lolote kwa kauli yake, bali nikawa nafungua zipu ndogo ya begi ili nitoe baadhi ya vitu vyangu. Bado akawa ameendelea kusimama hapo hapo mlangoni kama vile kuna kitu alikuwa anasubiria, nami nikamtazama usoni.

Akaibana midomo yake na kuangalia pembeni kama vile anajishauri hivi, kisha akauliza, "Nikakuwekee maji... bafuni ujimwagie?"

Swali hilo likanifanya nitabasamu kwa mbali huku nikimwangalia kiumakini, naye akatabasamu kwa haya na kuangalia chini. Kiukweli... au basi tu! Pigo zake zilieleweka vizuri sana kwangu ingawa alikuwa mkubwa, na hayo madoido aliyoweka yalinifanya nijihisi kweli ni kama nimefika nyumbani kwetu kabisa. Chakula cha nguvu nilikula pale kwa akina Zawadi mweupe, na muda huu nikapewa ofa ya kutengewa maji bafuni. Hayo ndiyo mambo sasa! 

"Utakuwa umenisaidia sana, asante," nikamwambia.

Akatabasamu na kuibana midomo yake, kisha akaondoka kwenda kukamilisha zoezi hilo.

Nikacheka kidogo kwa pumzi na kutikisa kichwa, nami nikaendelea kutoa vitu vyangu. Ilikuwa wazi kwamba Ankia alivutiwa na mimi. Na kwangu hilo lilikuwa jambo la kawaida sana. Basi, nikatoa vitu kama vyote begini na kupangilia vingi kabatini, nikiweka viatu vyangu pea mbili sakafuni na kisha kuvaa sendo (sandals) ngumu za kimasai miguuni. Nilikuwa nimeshavua nguo za safari na kubakiza kaushi nyeupe na kaptura ya mazoezi, nami nikaweka taulo yangu ndogo begani ili niweze kuelekea bafuni kupunguza fukuto mwilini. Kabla hata sijafungua mlango kutoka kwenye chumba hicho, ukagongwa taratibu, nami nikimjua mhusika aliye hapo nikasema tu ingia, na Ankia akausukuma na kusogea ndani kiasi. 

Nilipomwangalia niliona akinitazama mikononi, ikiwa wazi alipendezwa na uimara aliouona, naye akasema, "Nimeshakuwekea maji bafuni."

Nikamwambia, "Asante."

Kisha nikachukua simu yangu pamoja na chaja na kusogea alipokuwa, naye akaanza kuelekea sebuleni huku nikimfuata nyuma. Tulipofika hapo, nikamwomba aniwekee simu ipate chaji, naye akaipokea na kwenda kuichomeka kwenye moja ya matundu ya 'extension' yake. Mimi nikaenda zangu bafuni, nikatumia dakika chache kujisafisha vizuri maana sabuni ilikuwemo mule mule, kisha nikarejea tena ndani. Nilimkuta mwanamke huyo akiwa amekaa sofani tu, akiikunjia miguu yake kwa pamoja huku akiwa makini kutazama tamthilia. Sikumsemesha na kwenda tu chumbani, nikajiweka vizuri, kisha nikaenda sebuleni tena huku sasa nikiwa nimebadili mavazi kwa kuvalia mepesi zaidi.

Nikamtazama mwanamke huyo. Aliniangalia pia upesi na kutabasamu kwa mbali, kisha akasimama na kusema angekwenda kuniwekea chakula. Lakini nikamzuia na kumwambia nilishiba, labda tu anipatie maji ya kunywa. Akatii kwa kuyafata na kuniletea, kisha akakaa tena huku mimi nikiyashusha kooni taratibu. Alikuwa amekaa kama vile ameshika tama, yaani akisikiliza kwa makini tafsiri za kiswahili kwenye tamthilia, nami nikamsemesha hatimaye. Tulianza kwa kuiongelea tamthilia, kisha kuhusu kilichofanya nichelewe kufika huku hadi kuingia kwa jirani yake, na mambo ya mitaa iliyozunguka eneo lote la Mzinga na tabia za watu, na nilijitahidi kufanya maongezi yaburudishe kwa kumchekesha kwa utani wa hivi na vile. Hatukuwa tumezungumza kuhusu maisha yetu ya kibinafsi, na ni kitu kilichofaa kwa mwanzo wa kujuana. Alikuwa ana nia ya kunichomea dawa za mbu chumbani lakini zilikuwa zimemwishia, na akasema kwa muda huo tayari duka la pale nje lingekuwa limefungwa hivyo asingeweza kwenda kununua zingine maana maduka mengine yalikuwa mbele huko. Nikamwambia aondoe shaka, ningelala ndani ya neti tu, kama yeye vilevile. 

Tamthilia ilipokwisha, akanyanyuka na kusema yeye pia angekwenda kujimwagia maji kabla ya kulala, kisha akaenda chumbani kwake. Hazikupita dakika nyingi sana naye akawa ametoka huko, nami nikamwangalia jinsi alivyokuwa. Alivaa khanga moja kutokea kifuani mpaka kufikia magotini, na mwili wake tepetepe ulinyumbulika kwa makusudi mengi sana alipopiga hatua kuja upande wangu ili atoke mlangoni na kwenda bafuni. Nikatazama tu runinga na kujitahidi kuweka utulivu, lakini tumawazo twingi twa kihuni kumwelekea tulikuwa tunanisumbua-sumbua sana kichwani. Akanipita na kutoka. Simu yangu ikaanza kuita, nami nikaichukua na kuona niibebe tu ili nikazungumzie chumbani; aliyekuwa ananipigia alistahili maongezi ya faragha zaidi, yaani mama yangu. Nilipenda sana kuonngea naye nikiwa sehemu tulivu. 

Nilitumia dakika nyingi kuzungumza naye kiasi kwamba sikutambua kama muda ulisonga mpaka nilipoona taa za sebuleni zikizimwa, nami nikaelewa bila shaka Ankia alikuwa amesharudi na sasa alijiandaa kwenda kulala. Nikamaliza maongezi ya kwenye simu na kuamua kutoka chumbani ili niifate chaja maana nilihitaji kuiweka simu ipigwe moto usiku mzima mpaka kukucha. Taa ya upande wa jikoni bado iliwaka kwa hiyo ndani hapo kuelekea sebule palikuwa na mwanga hafifu ulioruhusu kuona mambo vizuri, na ndiyo nilipofika sebuleni tu nikasimama ghafla baada ya kumkuta Ankia akiwa bado hapo. Nilifikiri labda tayari angekuwa chumbani kwake, lakini haikuwa hivyo. Sasa nilithibitisha kwamba alikuwa na nywele za kusukwa kichwani maana hakuwa na kilemba tena. 

Alikuwa amesimama usawa wa TV yake akionekana kuifunika kwa kitambaa. Kwa sababu TV ilikuwa juu kiasi, alinyoosha mikono yake kuiwekea kitambaa hicho huku akiinyanyua nyayo zake za miguu, na hivyo khanga fupi yenye kulowana aliyokuwa amevalia iliyaacha mapaja yake wazi na kulichora umbo lote la nyuma kwa njia iliyoamsha hisia zangu ghafla, na kwa nguvu mno. Inaonekana hakujua niko nyuma yake, ama labda alijua, lakini hakugeuka upesi, na alipomaliza tu kuifunika TV yake, bila kugeuka akawa ameifungua khanga yake ili airekebishe vizuri na kuifunga tena mwilini, na alipokuwa tu ndiyo anafanya kuirudisha mwilini akawa amegeuka. Kuna kitu chenye kusisimua kiliruka ndani yangu baada ya kuuona mwili wake wa mbele kwa kifupi sana, naye akaonekana kushtuka kiasi baada ya kukuta nimesimama hapo!


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next