Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA NNE

★★★★★★★★★★★★★★


Asubuhi ilipofika, tayari Namouih alikuwa macho akishugulika na mambo kadhaa yaliyohitajika kwa ajili ya kumweka baba yake katika hali nzuri. Bwana Masoud alipoamka, Namouih akamsaidia kupata chakula chepesi, naye akatulia kidogo mpaka daktari alipofika na kuanza kuangalia hali yake. Akamsogeza Namouih pembeni na kumwambia jinsi alivyoyaona mambo, kwamba ingawa mzee wake alijitahidi sana kuonyesha yuko imara, alikuwa na maumivu makali sana. Muda si muda yangekuja kwa kasi zaidi na kusababisha mfumo wake wa upumuaji ukate, na habari hii ikamwongezea simanzi mwanadada huyu.

Daktari akamtia moyo pia kwa kumwambia Mungu ni mkubwa, hivyo ingetakiwa tu kusubiri mikono wake wa neema utue kwao, labda ingekuja njia ya kumwokoa. Kila kitu kilihitaji pesa, na kumsukuma mzee huyu aendelee kuishi kwa hizi wiki chache zilizopita ilitokana na dawa alizokuwa akipata, lakini bado ugonjwa wake uliendelea kumtafuna. Upasuaji wa gharama kubwa ndiyo uliokuwa suluhisho kwake. Akamwacha Namouih baada ya maongezi yao, na mwanamke huyu akarudi kwa mzee wake; akiketi pembeni yake.

Bwana Masoud alikuwa akimtazama Namouih kilegevu, macho yake yakionyesha kuchoka sana, lakini akaweza kuachia tabasamu dogo kumwelekea binti yake. Namouih akatabasamu pia, naye akakishika kiganja chake.

"Daktari alikuwa anakupiga swagger gani?" Masoud akauliza.

"Alikuwa ananiambia kuhusu hali yako. Anasema uko imara sana," Namouih akamwambia.

"Imara... imara kwamba ninajua ninakufa na nimelikubali hilo?"

"Baba usiseme hivyo. Bado una maisha marefu, na utayaishi..."

"Ahah... Namouih... kila mtu ana wakati wake...."

"Baba nimekwambia usiongee hivyo...."

"...ni lazima kuufikia tu. Roho inaniuma kujua kwamba umeacha baadhi ya mambo muhimu kwenye maisha yako ili kuwa hapa... Namouih... unapaswa tu kukubali hili pia, kwamba hautakuwa na mimi sikuzote. Wewe endelea na mambo mengine, jitahidi kuboresha maisha yako, yangu yanaelekea tamati yake...."

"Kwa sababu yangu. Ni kwa sababu yangu maisha yako yanaelekea tamati, na mimi siwezi kukaa kukuangalia tu...."

"Unamaanisha nini Namouih? Hujanisababishia lolote. Wewe ndiyo umenipa hii kansa?"

"Umekuwa ukifanya kazi hiyo kwa ajili yangu, ili nisome, nije kufanikiwa. Siwezi kuelewa ni nini umepitia huko migodini baba lakini naelewa kwamba ulikuwa unapigana kwa ajili yangu... kwa ajili yetu sisi sote. Sitaacha kupigana kwa ajili yako baba. Hili suala litakwisha. Nakuahidi," Namouih akasema kwa hisia.

"Mhm... una kichwa kigumu sana wewe. Utapoteza muda, pesa, na mambo mengine halafu bado mwisho wa siku nitaenda tu. Mimi sitajali hata nikifa Namouih. Nachojali tu kwa sasa... ni kuwa nawaona nyie wote kwa hizi siku chache nilizo...."

"Baba please..."

"...bakiza... usijali Namouih, usijali. Kila kitu kitakuwa sawa, na sitaki ulazimishe mambo yasiyokuwa na ulazima. Ninakujua vizuri sana. Niahidi hautafanya jambo lolote la kipuuzi. Niahidi hautaharibu maisha yako kwa sababu yangu... tafadhali..." Masoud akamwomba binti yake.

Machozi yalikuwa yameanza kumjaa machoni mwanamke huyu, naye akajikaza kutoyaruhusu yamwagike, kisha akaketi kwenye kitanda alicholala baba yake usawa wa kichwa chake, akikinyanyua kidogo na kukiweka kwenye paja lake.

"Niimbie basi," Masoud akamwambia akiwa amefumba macho.

"Ahah... nikuimbie hapa?"

"Ndiyo. Niimbie kale kawimbo kazuri ulikokuwaga unamwimbia Nasri..."

"Mhmhm... bado unaukumbuka mpaka leo?"

"Siwezi kusahau sauti yako ilivyo nzuri..."

Namouih akavuta pumzi kiasi, kisha akaanza kumwimbia mzee wake kwa sauti ya chini lakini iliyosikika vyema kwa Masoud. Baba yake akatabasamu tu kwa furaha aliyohisi kuona jinsi binti yake alivyompenda sana, naye akafumba macho akisikilizia jinsi sauti tamu ya Namouih ilivyoikonga nyoyo yake, na hii ikamfanya ahisi amani sana.

Muda mfupi baadae, Zakia akawa amefika hapo pia na vifaa kadhaa, na moja kwa moja akaanza kumweleza Namouih kuhusiana na suala la Donald. Akamwambia kwamba tayari alikuwa amempatia Mage namba yake, na Mage pia alikuwa ameshaanza mipango ya kumuunganishia kwa boss wake huyo ili mambo yatie tiki. Kwa hiyo Zakia akawa anamshawishi sana bintiye kwamba pindi ambapo mwanaume huyo angemtafuta, afanye juu chini ili amzuzue zaidi na hatimaye aweze kupata faida ambayo itasaidia kuokoa uhai wa baba yake haraka.

Namouih hakuonyesha hisia yoyote ile kuelekea shauku kubwa ya mama yake, naye akasema tu angeondoka kwenda kununua dawa zaidi za maji ili kuja kumwekea mzee kwa ajili ya siku hii. Hata Zakia alijua wazi kwamba binti yake alikubaliana na jambo hilo kwa shingo upande, lakini aliona ilikuwa bora kuliko kama angekataa kabisa. Akawa tu anaombea kwamba asije kuvuruga mambo wakati alikuwa amemtengenezea vizuri sana mitambo hiyo.

★★

Ilipofika mida ya saa 7 mchana, tayari Namouih alikuwa ameshaondoka hospitalini kule kwenda kufanya mizunguko ya hapa na pale mjini. Kwa muda huu baba yake alikuwa chini ya uangalizi wa wauguzi hospitalini huko, na mama yake kama kawaida alikuwa kwenye shughuli zake pia, wadogo zake wakiwa shuleni. Ni wakati alipokuwa ndani ya taxi kuelekea nyumbani pale alipopata ujumbe kutoka kwenye namba ngeni.

'Habari yako.'

Ulisomeka hivyo. Namouih akawa amekisia kwamba huyu bila shaka ndiyo angekuwa mwanaume tajiri aliyemtaka, hivyo akajibu ujumbe huo kwa salamu pia. Mwenye namba ngeni akajitambulisha kwa jina la Efraim Donald, akisema ameipata namba ya Namouih kupitia kwa "shangazi yake," yaani yule Mage, rafiki yake Zakia. Namouih akamkaribisha vizuri, na hapo ndiyo mwanaume huyo akasema alihitaji sana kupata nafasi nzuri ya kuja kuonana naye kwa sababu kuna mambo mengi alitaka waongee.

Akaomba samahani kwa kwenda moja kwa moja kwenye hilo kwa kuwa Namouih hata hakumfahamu, naye akamwambia angependa waendelee kufanya mawasiliano ili wajuane vizuri zaidi, na hata akitaka basi angemrushia picha zake ili amwone. Mwanzo ingekuwa kwamba wanatakiwa tu kufahamiana na kujenga urafiki, ili mwishowe wakija kukutana basi aweze kumwelezea hayo "mambo mengi," kwa sababu alikuwa na hamu kubwa sana ya kuzungumza naye.

Namouih kama Namouih hakuwa na kipingamizi, kwa kuwa tayari hili ni jambo lililokuwa limepangwa. Ingekuwa kwamba limekuja kwa kushtukiza angempiga "block" ya nguvu mwanaume huyo. Kwa hiyo Namouih akamwambia tu kwamba yeye yuko huru muda wote, hivyo atakapotaka kumtafuta afanye hivyo, na ili kuweka hali fulani ya mazoea kiasi, akasema ana hamu ya kukutana naye pia. Mwanaume huyo akasema angemtafuta baadaye kutokana na kuhitaji kumalizia kazi fulani, hivyo angeshukuru kama Namouih angeitunza namba yake. Mwanamke akamwambia mwanaume asiwaze, na baada ya hapo wakaagana.

Ingekuwa rahisi kwa mwanamke mwingine kupata hata hisia za msisimko kwa kujua ndiyo alikuwa ametoka kuongea na mchumba mtarajiwa, lakini kwa Namouih haikuwa hivyo. Yaani hisia zake za moyoni zilikuwa zimefukiwa ndani sana, kwa kuwa kilichotawala mawazo yake ilikuwa ni baba yake tu. Akafika nyumbani na kushughulikia mambo kadhaa mpaka Nasma na Sasha waliporejea kutoka shuleni, naye akapumzika kidogo huku akisoma-soma mambo yake ya kisheria.

Ilipofika saa kumi jioni, akaelekea tena hospitalini kumwona mzee wake mpaka ilipofika usiku wa saa mbili ndiyo akarudi nyumbani tena. Blandina akawasiliana naye kuuliza mambo yalikwendaje, kwa kuwa yeye alikuwa bize kufuatilia mambo mengine kwa leo, naye Namouih akamwambia mambo yalikwenda kama kawaida, bila kugusia kuhusu Efraim Donald. Ni Zakia ndiye aliyekwenda kukaa na mume wake hospitalini baada ya kumaliza kuzurura, hivyo Namouih akawa ametulia ndani na wadogo zake.

Mida ya saa nne hivi usiku, Efraim Donald akamtumia ujumbe Namouih, akimsalimu na kutaka "wachati." Siyo kwamba Namouih alikuwa akisubiri ujumbe kutoka kwa mwanaume huyo, lakini akili yake ilimwambia kwamba hizo ndiyo njia za mwanzo ambazo zilikusudiwa kumwaminisha kwamba kweli ana nia naye. Hata ingawa alikuwa anapangwa akubali tu ikiwa mwanaume huyo ataomba wawe na mahusiano, hiyo haikumaanisha angekubaliana tu na kila jambo bila kudadisi vitu fulani. Hata akawa anawaza ikiwezekana amchune tu halafu amwache kwenye mataa, lakini hakuwa aina ya mtu mwenye viwango vya namna hiyo.

Walihamishia maongezi yao kutoka kwenye jumbe za kawaida kwenda WhatsApp, na hapo sasa ndiyo Namouih akaweza kumwona mwanaume huyo kwa sura baada ya ya kurushiwa picha yake. Picha ambayo Efraim Donald aliituma ilimwonyesha akiwa ameegamia gari jeupe aina ya Range Rover, akiwa ameshikilia simu huku akitazama camera ya mpigaji. Mwili wake ulikuwa mkubwa kiasi, yaani mpana, hata T-shirt aliyovalia kwenye picha ilimbana vyema, lakini haukuwa ule uliojikata sana kimazoezi ingawa alijaa kwa kadiri fulani. Alikuwa mweusi, mrefu, mwenye nywele fupi na ndevu zilizochongwa vizuri kutokea kwenye timba mpaka kidevuni, na alikuwa na macho makubwa kiasi.

Kumwangalia kwenye picha hiyo kulimfanya Namouih afikirie labda huyu jamaa alikuwa tapeli, naye akatabasamu tu na kutikisa kichwa chake kwa kujihisi kama mpuuzi kuendelea kufanya huu mchezo.

'Ndo wewe huyo,' Namouih akaandika baada ya kuiona picha sasa.

'Ndiyo mie,' Efraim Donald akamwandikia pia.

'Naona umenirushia picha uliyokaa karibu na gari kabisa. Impression ni kwamba?'

'Hahah we unadhan nataka kutoa impression gani?'

'Ndiyo uniambie'

'Napenda tu hiyo picha. Ninazo zingine kama utataka nikurushie'

'Sawa'

'Sijairusha hiyo kwa sababu ya gari, na hilo siyo gari langu'

'Kumbe'

'Ni la mteja ambaye ni rafiki yangu pia, hapo nilikuwa namuuzia ndiyo akawa anatwanga foto'

'Haya sawa. Kwa hiyo ulinijuaje mimi'

'Nilikuona ndotoni'

'Wapi?'

'Hahahah natania. Wewe siyo mpenzi wa utani eti?'

'Siyo sana'

'Ooh sawa, nanote hilo. Nilikuona mara ya kwanza kwenye conference fulani. Nafikiri ulikuwa kama intern wa mtu sijui maana ulivalia nadhifu sana na ulionyesha uko professional mno'

'Wewe ulikuwa unafanya nini hapo?'

'Nilikuwa kama mfadhili mdogo wa biashara zilizoendeshwa'

'Mdogo?'

'hahahaha napenda jinsi unavyoniuliza maswali, ikimaanisha unataka sana kuniingia'

'Hahaha.. siyo kihivyo. Ni kwamba me ni mwanasheria kwa hiyo maswali ni kitu yangu sana, samahani lakin'

'Oh no, nimekwambia napenda. Hiyo inamaanisha tutakuwa na mambo mengi sana ya kuongelea tukikutana. Ntakufanya uwe prosecutor wangu'

Namouih hakuweza kujizuia kutabasamu kwa kauli hiyo. 'Kwa hiyo kuanzia hapo ndo ukaanza kunifuatilia eeh?'

'Siyo kama stalker lakini ndiyo, nilijaribu kukutafuta ila nikakukosa. Baadae nikaja kupata picha yako. Nilikuwa naitazama kila siku yaani'

'Kwa nini?'

'Ulinivutia sana'

'Kwa nini?'

'Unaonaje tukija kukutana ili nikujibu vizuri zaidi'

'Lini?'

'Wakati wowote utakao'

'Wakati wowote nitakao? Nikikwambia uje sasa hivi?'

'Nimeshafika'

Namouih akazungusha macho kikejeli.

'Hizo swaga tu kaka'

'Ndiyo najua unajua hilo. Nataka tu uhisi kile ambacho nitasema kuwa kweli Namouih, na kwenye simu haitatosha. Najua unaelewa nitakakoelekea, lakini sitaki iwe kwa POV yako tu, bali yetu sote. Niambie kama unataka nitakuja hata kesho'

'Kweli?'

'Kabisa'

Namouih akatulia kidogo, kisha akamwandikia, 'Sawa, njoo kesho basi'

'Ondoa shaka, nitafika'

'Unajua pa kunipata?'

'Nimeshakupata tayari, so just relax, mimi ndiyo nitakuja kwako'

Namouih akacheka kidogo kwa kuguna, akiona mambo haya yote kuwa maigizo ya hali ya juu sana. Ni kwamba kuna ile hali tayari aliijua kuhusu jinsi wanaume wanavyokuwa wanapoanza kumshawishi mwanamke ili kupata watakacho, kwa hiyo kwake maneno hayo mazuri hayakulegeza ugumu wa moyo wake kuelekea jinsi alivyochukulia jambo hilo. Baada ya story fupi za hapa na pale, Efraim Donald akamtakia usiku mwema, akimwambia kwamba kesho angefika mjini kwao upesi ili wakutane na kuweza kuzungumza ana kwa ana. Akasema angepangilia kila kitu, hivyo kile ambacho Namouih angetakiwa kufanya ilikuwa ni kutulia tu. Wakaagana. Namouih akaingia kulala. Usiku ukapita.


★★★


Asubuhi na mapema, Namouih alikuwa ameamkia kufanya usafi nyumbani, akisaidizana na Sasha. Hii ilikuwa ni siku ya Jumamosi, hivyo Nasma alikuwa ameupiga usingizi tu kufidishia siku zote tano alizokuwa akiamka mapema sana kwenda shule, kama kawaida ya watoto wanaopenda usingizi. Sasha binti mrembo kama dada yake alikuwa na mpango wa kuandaa chakula kizuri sana kwa ajili ya baba yake siku hii, naye Namouih akampongeza na kumwambia yeye pia ana hamu ya kuja kukionja, kwa kuwa alijua angepika vizuri sana na baba yake angekifurahia. Kwa hiyo baada ya Namouih kumaliza mambo kadhaa hapo, akabeba chakula kidogo kwa ajili ya asubuhi ili yeye atangulie hospitalini, akimwacha Sasha anashughulika na vitu vingine baada ya Nasma kuamka.

Zakia bado alikuwepo hospitali Namouih alipofika, na mwanamke huyu akamkuta baba yake akiwa macho tayari na kuanza kumnywesha uji taratibu. Bwana Masoud alipenda sana Namouih alipomlisha, zaidi hata ya Zakia, kwa hiyo alijitahidi kumaliza wote na chakula chepesi cha asubuhi Namouih alichomsisitizia ale. Mama mtu alitaka kujua ikiwa Namouih alikuwa ameshaanza kuongea na Donald, akimuuliza bila Masoud kusikia, lakini Namouih akamwambia mambo hayo wangeyazungumzia baadaye. Akamwambia mama yake aende nyumbani kujiweka sawa kimwili ili baadaye aje tena pamoja na Sasha.

Zakia alikerwa sana na jinsi ambavyo binti yake hakutaka kufunguka haraka, kwa hiyo akaondoka hapo akiwa ameudhika, na Namouih alilielewa hilo vizuri. Akaendelea tu kukaa na mzee wake hapo, akipiga naye story moja mbili tatu zenye kufurahisha. Dawa alizokuwa akiendelea kupewa hapo zilimfanya Masoud asiihisi sana saratani yake ilivyomtafuna, lakini Namouih alijua kweli muda si mrefu mwili wa baba yake ungeshindwa kustahimili maumivu yaliyokuwa njiani kumpata.

Ilipofika mida ya saa nne asubuhi, Namouih akapigiwa simu na Efraim Donald. Ilimbidi atoke nje ya chumba cha wodi ya baba yake ili aweze kuzungumza kwa faragha. Baada ya kupokea, Efraim Donald akamwambia kwamba alikuwa ameanza kuja kutokea kwenye jiji alipokuwa, na ingawa Namouih alishangaa kiasi kuona jinsi jamaa alivyoonyesha hatanii, hasa kwa sababu ya jiji hilo kuwa mbali, hakuuliza. Efraim Donald akasema alikuwa tu anamtaarifu mapema ili akifika na kumfata asishtuke sana, naye Namouih akasema haikuwa na shida; angemkuta tu. Basi wakaagana, naye Namouih akarudi kwa baba yake. Alikuta usingizi ukiwa umempitia mzee wake, naye akabaki tu kumtazama akiwa anawaza jinsi ambavyo maisha yake yangebadilika kwa sababu ya uamuzi aliokuwa karibu kuuchukua.

★★

Muda ulisonga mpaka inafika saa saba mchana. Upande wa nyumbani kwake Masoud, Sasha alikuwa amemaliza kumpikia chakula kizuri sana baba yake, na ndiyo alikuwa tu akipangilia mambo yaliyobaki ili aambatane na mama yake kuelekea hospitalini. Nasma angekwenda pamoja nao pia ili kumsalimu baba yake, hivyo naye alikuwa amemaliza kujiandaa. Zakia akiwa anamsubiria Sasha, akafika mgeni hapo ambaye hakutarajiwa. Ilikuwa ni Blandina, naye Zakia baada ya kumwona akamkaribisha ndani.

"Za hapa mama?" Blandina akasalimu.

"Salama tu," Zakia akajibu.

"Shikamoo," Nasma akamwamkia Blandina.

"Marahaba baby. Umependeza kweli, unaenda wapi?" Blandina akamsemesha.

"Naenda kwa baba," kakajibu.

"Oooh mnaenda hospitali eeh? Ni vizuri maana na mimi nataka kwenda pia," akasema Blandina.

"Una mgonjwa kwani?" Zakia akauliza.

"A... ahah... hapana, namaanisha naenda pia kumsalimu ba Nam," Blandina akasema.

"Aaaa... sawa basi twende wote. We' Sasha... em' harakisha bana!" Zakia akaongea na kusema hivyo kwa sauti kubwa.

Blandina akatabasamu, na alipokuwa anataka kusema jambo fulani, Sasha akawa amefika hapo walipokuwa wamesimama.

"Ulikuwa unafanya nini nawe?" Zakia akaongea kabla ya Sasha kumsalimia Blandina.

"Nilikuwa na... nilikuwa..."

"Unajivuta mno wakati usafiri wenyewe unajua mgumu mwishowe usababishe mtu mwingine afe..." Zakia akasema hivyo na kusonya.

Kauli hii ilivuta umakini wa Blandina, na kwa sekunde akawa amemwangalia Sasha na kuona jinsi alivyoinamisha kichwa chake kwa njia iliyoonyesha huzuni. Blandina alielewa kwamba maneno hayo yenye chumvi yalimaanisha kuwa kwa kuchelewa, Sasha angesababisha Masoud afe, lakini Zakia kusema "mwingine" kulifanya Blandina ahisi mwanamama huyo alikuwa na maana nyingine.

"Twendeni tukachukue daladala sasa," Zakia akasema huku akianza kutoka.

"Oh, nimekuja na gari, haina haja ya kuchukua usafiri wa kulipa. Twendeni kwenye gari," Blandina akasema alichokuwa anataka kusema mwanzoni.

"Heh! Umenunua gari?" Zakia akamuuliza.

"Ahahah... hapana, ni la rafiki," Blandina akajibu.

"Mmmm la rafiki wapi?"

Zakia akamuuliza hivyo kichokozi huku akimbonyeza begani, na wote wakacheka isipokuwa Sasha. Wakatoka na kuelekea kwenye gari alilokuja nalo Blandina na kuanza safari kuelekea hospitalini. Njia nzima wanawake hawa waliongelea mambo kadha wa kadha, lakini Sasha hakujihusisha na maongezi. Haikumchukua muda mrefu Blandina kuelewa kwamba maneno ya mama yake yalikuwa yamemchoma sana binti huyo, lakini akawa anataka kujua kiundani zaidi sababu zilizofanya Zakia aseme maneno yale bila kujali hisia za mwanaye.

Walifika hospitalini na kumkuta Namouih akiwa hapo bado. Hii ikiwa ni saa ya kutembelea wagonjwa, sehemu nyingi zilikuwa na watu wengi waliokuja kuwatembelea wapendwa wao walioumwa, na hakuna kitu kilichompa furaha bwana Masoud zaidi ya kuiona familia yake yote ikiwa hapo. Nasma alipomlalia kifuani kwa njia ya kumkumbatia, Masoud alidondosha machozi utadhani ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kumwona baada ya kipindi kirefu. Kakaanza kumfuta machozi kwa upendo, naye Sasha akamkaribia zaidi na kuanza kumsemesha pia.

Baada ya wote kutulia, Sasha na Nasma ndiyo wakawa wanamlisha baba yao kwa zamu, huku na wenyewe wakila kidogo pia na maongezi ya mambo ambayo Nasma amekuwa akifanya yakiendelea. Zakia alikuwa pembeni na simu yake akionekana ku-chat na rafiki, naye Namouih alikuwa akiwaangalia wadogo zake na baba yao kwa upendo sana. Blandina, akiwa bado anafikiria kuhusu maneno ya Zakia kumwelekea Sasha, akamuuliza Namouih ikiwa alikuwa ameshakula, naye akakanusha na kusema angekula baadaye. Blandina akamwambia anataka waongee kidogo hivyo watoke nje mara moja, na mwanadada huyu akakubali. Wakawaacha wengine hapo na kwenda nje ya chumba hicho.

"Vipi mommy, unaendeleaje?" Blandina akamuuliza.

"Unamaanisha nini?" Namouih akauliza pia.

"Well, tulipoachana ile juzi ulisema ungemtafuta yule jamaa, lakini bado hujanipa ubuyu," Blandina akasema.

Namouih akatabasamu kwa mbali, kisha akasema, "Nilimtafuta."

Hii haikuwa kweli moja kwa moja kwa kuwa ni Efraim Donald ndiye aliyemtafuta yeye, lakini Namouih aliona yote kuwa yaleyale.

"Enhe, imekuwaje?" Blandina akauliza.

"Anakuja leo kuonana nami," Namouih akasema.

"Wewe... acha basi!"

"Sure kabisa..."

"Wow! Siku moja tu tayari amelewa mziki' wako eeh?"

"Hapana bwana... ahah... anakuja tu ili ndiyo uwe mwanzo wa kufahamiana vizuri. Ngoja nione itakavyokuwa..."

"Hii ikimaanisha haujapanga kumwambia kuhusu baba yako leo-leo, siyo?"

"Yaani hata sitaki kufanya hivyo kabisa."

"Lakini hamna namna, ikiwa kweli ana pesa huenda akakusaidia. Me naona ni bora umwambie kuhusu hii changamoto ili kama ni kukusaidia akusaidie mapema. Sidhani kama itakuwa busara kusubiri mpaka muoane huko, maana haitakuwa nzuri kwa mzee Masoud..."

"Ndiyo, najua. Ni kwamba tu... nahisi ni kama ni.. a.. yaani... hhhh... Blandina maisha yangu yatageuka kuwa maigizo makubwa sana. Natamani sana kama ingekuwa rahisi kwangu kufanya hivi, sijui tu hata nitaigizaje kwa huyu mtu kwamba...."

"Namouih, usi-stress hivyo. Nakujua jinsi ulivyo shupavu, we' ni jasiri utaweza tu, hii ishu mbona ni Tuesday? Just relax, kila kitu kitakuwa sawa darling," Blandina akamtia moyo.

Namouih akashusha pumzi na kuangalia chini tu.

"Bila shaka mama yako amefurahi sana," Blandina akasema.

"Usiniambie," Namouih akaongea huku ameendelea kutazama chini.

"Baba yako je? Utamwambia kwamba...."

"No. Hapana. Hatakiwi kujua kuhusu hilo kwa sasa. Nitapaswa tu nifekishe mambo mengi vizuri. Sipaswi kumshtukiza sana, na sitakiwi kumwacha kwenye mataa. Nataka tu kuhakikisha kwamba anabaki sehemu nzuri kimtazamo baada ya haya yote... Nasma na Sasha pia," Namouih akamwambia.

"Okay. Halafu... kuna kitu nataka kuuliza Nam," Blandina akasema.

"Ndiyo..."

"Hivi... mama yako huwa ana tatizo gani na Sasha?"

Namouih akamtazama na kumgeukia vizuri zaidi. "Kwa nini unauliza hivyo?"

"Yaani kuna nyakati ambazo nimeshawahi kuona anamfokea, ah... ile tu unachukulia kawaida kwamba ni mama na mtoto, huwa ipo. Ila Nam kuna maneno ambayo Zakia anaweza kumsemesha Sasha ni mazito sana mpaka huwa nashangaa..."

"Maneno kama yapi?" Namouih akauliza kwa umakini.

"Kipindi kile kwenye birthday ya Nasma, alitaka kwenda naye wapi sijui nje ya nyumba mida kama ya saa mbili, nilimsikia mama'ako akisema, 'unaenda naye wapi? em' mwache usije ukaniulia mtoto mimi.' Hiyo niliona ni kama alikuwa amemkasirikia labda, lakini na leo tena alikuwa anamwambia aharakishe kabla hajasababisha mtu mwingine kufa..."

Namouih akafumba macho na kuinamisha kichwa.

"Nam, Sasha mara nyingi namwonaga huwa ni kama anakosa amani hasa mama yako akiwepo, na huwa anaonekana mstaarabu tu lakini nimekuja kugundua kuwa hiyo ni huzuni. Kuna kitu chochote ambacho kimewahi kumpata huyu mtoto?" Blandina akauliza kwa kujali.

Namouih akamtazama rafiki yake kwa sekunde chache, kisha akasema, "Ni story ndefu Blandina. Ila nitahitaji kuongea kwanza na mama, nawe nitakuja kukusimulia. Shukran kwa kuniambia."

"Huwezi hata kuniambia kwa kifupi?"

"Mambo ni mengi. Ngoja tu kwanza nishughulike na haya yaliyopo sasa, nitakuja kukuelezea," Namouih akamwambia.

Blandina akaridhia kwa hilo na kumpa pole kwa sababu ya changamoto hizi za kihisia, naye akamwambia labda akikutana na huyo Donald huenda angemsaidia kuziondoa kweli. Wakarejea ndani tena baada ya hapo kujiunga na wengine.

★★

Muda mfupi baadaye, Namouih akapigiwa simu na Efraim Donald, akimwambia kwamba tayari alikuwa amefika mjini kwao, na yeye Namouih aende sehemu fulani kukutana naye hatimaye. Kwa kutaka kuwa mwangalifu, Namouih akamwambia kwamba angekwenda na dada yake, akimaanisha Blandina, naye Efraim Donald hakuwa na kipingamizi. Mwanaume huyo akamwambia Namouih ikiwa angependa basi eti atume gari mpaka alipo ili limchukue na kumpeleka, lakini mwanadada wetu akakataa na kusema angekwenda kwa usafiri yeye mwenyewe. Alikuwa mgumu balaa! Mwanaume huyo akasema tu kwamba sehemu ambayo angekutana naye ilikuwa ya hadharani, kwenye mgahawa wa kisasa nje ya hoteli kubwa, hivyo angemsubiri tu hapo yeye na dada yake.

Baada ya kumaliza maongezi hayo, Namouih akamjulisha Blandina kuhusu kila kitu, na rafiki yake huyo akafurahi sana kujua aliunganishwa kwenye "collabo" hii. Akamwambia ni vizuri kwamba alikuja na gari, hivyo angempeleka Namouih nyumbani kujiandaa kisha ndiyo waende. Lakini Namouih akapinga hilo, akisema hakukuwa na haja ya kuoga wala kujiandaa; angeenda kuonana naye hivyo hivyo. Blandina alimshangaa sana kwa sababu alielewa kwamba alikuwa akifanya hayo kwa makusudi tu, na hakuwa na jinsi ila kumwacha afanye atakavyo. Akamwambia mwanaume akimkimbia kwa sababu ya kuogopa harufu ya jasho basi ndiyo atajua alikuwa amebugi sana.

Wawili hawa wakawaaga wengine kwa kusema wanatoka kidogo, naye Namouih akamwahidi baba yake kurudi baadaye tena kukaa pamoja naye, kisha wakaondoka hospitalini hapo.

★★

Ndani ya dakika ishirini tayari Blandina akawa amemfikisha Namouih alipotakiwa kwenda. Hawakushuka kwanza, bali Namouih akampigia jamaa simu na kumwambia wameshafika eneo hilo, naye akasema angekuja kumpokea. Alikuwa ameweka loud speaker ili na Blandina asikie, na rafiki yake huyu akamwambia Namouih kweli jamaa anaonekana yuko "sharp." Namouih alikuwa amekwishamwonyesha Blandina picha ya Efraim Donald, na shosti yake alimsifia kweli jamaa akisema yaani ingekuwa ni yeye ndiyo amepata hiyo bahati asingekuwa anadengua kama Namouih alivyokuwa akifanya.

Sekunde chache zikapita, na Namouih akamwona Efraim Donald kwa mbele, akiwa amesimama pembezoni mwa barabara ya lami nje ya eneo lililoizunguka hoteli ile ya kifahari kiasi. Alikuwa amevalia T-shirt yenye mtindo wa pundamilia lakini rangi zikiwa nyeupe na blue-bahari, suruali nyeusi ya jeans na viatu vyeusi vilivyong'aa sana. Blandina akamwona pia, naye akatabasamu na kuanza kumbonyeza-bonyeza Namouih mkononi kwa shauku, lakini Namouih akawa anamwangalia tu mwanaume huyo kwa umakini.

Efraim Donald alionekana kuangaza huku na kule, kisha akanyanyua simu yake na kuiweka sikioni, na ndani ya gari walipokuwa wanadada hawa simu ya Namouih ikaanza kuita. Akapokea, na jamaa akauliza mrembo alikuwa upande gani. Namouih yeye akasema ameshamwona, hivyo asimame hapo hapo alipo na yeye angemfata. Simu zikakatwa. Blandina akamwambia wawahi kwenda sasa maana alikuwa na hamu sana ya kuisikia tu hata sauti ya pedeshee huyo mubashara, naye Namouih akatikisa kichwa na kutoka ndani ya gari pamoja naye. Wakaanza kuelekea mpaka sehemu ile aliyosimama pedeshee sasa, na baada ya Efraim Donald kuwaona, akaachia tabasamu la mbali na kubaki amemwangalia tu Namouih.

Blandina akamsukuma Namouih kidogo kichokozi walipokuwa wamemkaribia jamaa na kumfanya mwanadada huyo ajikaze kucheka, na sasa wakawa wamemfikia kamanda.

"Mambo," Efraim Donald akawasalimu.

"Saaafii," Blandina akajibu huku akitabasamu.

"Naitwa Efraim, ukipenda niite Donald," akajitambulisha kwa Blandina.

"Sawa, Donald, mimi ni Blandina. Pacha mweusi wa Nam-Nam," Blandina akajitambulisha pia.

"Ahahah... sawa. Mmependeza sana warembo..."

"Asante," Blandina akasema.

Efraim Donald akamwangalia Namouih. Mwanamke huyu alikuwa anamtazama kwa njia ya kawaida tu.

"Uko poa?" Efraim Donald akamuuliza.

Namouih akatikisa kichwa kukubali bila hata kutabasamu. Blandina akaikaza midomo yake kucheka na kuangalia pembeni.

Efraim Donald akachekea kwa chini na kisha akauliza, "Mbona umenuna?"

Blandina akashindwa kujizuia kucheka kidogo sasa, lakini akajikaza zaidi.

"Sijanuna," Namouih akamwambia.

"Tabasamu sasa kidogo nione ma-dimple hayo," Efraim Donald akasema.

Namouih akatabasamu kidogo na kumwangalia Blandina, ambaye alikuwa ameibana midomo yake kuficha kicheko.

"Vipi sasa, unanionaje? Bado sionekani kama Prince Charming?" Efraim Donald akauliza.

"Ahah... unakaribia lakini siyo sana," Namouih akamwambia.

"Ahahahah... halafu alisema eti hawezi utani," Efraim Donald akamwambia Blandina.

"We,' anaongea huyu! Hujamkuta akiwa kwenye mahakama yaani hakuna anayemshinda maneno," Blandina akasema.

Namouih akatabasamu zaidi sasa, na ni kweli tabasamu lake lilifanya ma-dimple yake yakaonekana zaidi. Efraim Donald akafurahia sana urembo wa mwanamke huyo, nao wakatazamana machoni kwa sekunde chache. Kisha...

"Karibuni bwana. Nimefurahi sana kukutana nanyi. Tunaweza kuelekea pale kukaa kama itawafaa..." Efraim Donald akasema.

"Ndiyo, bila shaka," akajibu Namouih.

Pedeshee akaanza kuwaongoza kuielekea hoteli ile. Ilikuwa na ghorofa 6, na kwa nje kulikuwa na sehemu pana kiasi ya maegesho ya magari na upande mwingine kama mgahawa mpana kwa ajili ya vyakula na vinywaji. Namouih na Blandina walikuwa wakitembea huku wameshikana viganja vyao, Efraim Donald akiwa pembeni yao, naye akawa anawaambia kuhusu safari yake kutokea mkoani alikokuwa mpaka kufika huku mjini kwao Namouih, akisema haikuwa mara ya kwanza kuja huku, isipokuwa tu kufika kabisa maeneo ya huku walikokuwa hawa warembo.

Wakaifikia meza moja na kuketi kwenye viti vilivyoizunguka. Zilikuwa meza za duara, zilizotengenezwa kwa vitu vyenye ufanani wa mkeka lakini mzito na mgumu sana, na hata viti vilikuwa vya namna hiyo hiyo. Namouih akawa amekaa pembeni yake Blandina, huku Efraim Donald akikaa upande ambao aliwatazama wanawake hawa kwa pamoja.

"Vinywaji?" Efraim Donald akasema.

"Napendelea Serengeti Li...."

Namouih akamkanyaga Blandina alipokuwa akisema hivyo, naye akamwangalia usoni kimaswali.

"Okay, Serengeti Lite. And you?" Efraim akageuza swali kwa Namouih.

"Mimi niko sawa," Namouih akajibu.

"Eti ni kweli yuko sawa?" Efraim Donald akamuuliza Blandina.

"Hapana, yaani hajala kutokea asubuhi, sijui yukoje!" Blandina akasema.

"Lakini Bla...." Namouih akaishia tu hapo na kuweka kiganja karibu na mdomo wake.

Efraim Donald akatabasamu, kisha akasema angekwenda kumwagizia Blandina kinywaji na kumfatia Namouih chakula. Kabla hata Namouih hajapinga, tayari jamaa akawa amenyanyuka na kuondoka hapo.

"Eh-eh! Bibi tunafatiwa vyakula, oh nimekosea, unafatiwa chakula. Haki ya Mungu kupendwa ndiyo huku," Blandina akasema na kuanza kucheka.

"Halafu una kisebengo wewe, yaani bora tu hata ningekuacha!" Namouih akamwambia.

"Ahahahah... halafu nipitwe na hizi raha? Sahau! Kwa mashemeji ndiyo sehemu ya kuwa bibi we," Blandina akamwambia.

"Siyo kirahisi dear. Mtu hata sijui katokea wapi, anataka nini kwenye maisha yake, halafu niwaze ndoa naye haraka hivyo?"

"Umeanza tena!"

"Siendi kichwa kichwa. Je kama ameenda kuweka madawa kwenye hicho chakula anachokileta?"

"Basi ujue utakufa huku unatabasamu!"

Namouih akampiga kofi laini begani, naye Blandina akawa anacheka. Baada ya dakika chache, Efraim Donald akarejea na kuketi hapo pamoja nao, naye akawaambia kwamba msosi ulikuwa njiani kufika. Mhudumu mmoja akaleta chupa tatu za Serengeti na glasi na kuziweka mbele ya Blandina, naye akafurahi sana. Efraim Donald akamwambia Namouih amwambie mhudumu kinywaji cha kumletea pia, naye akasema aletewe maji tu. Mhudumu akaondoka, naye Efraim Donald akawa anamtazama tu Namouih usoni.

"Namouih ni jina zuri sana," Efraim Donald akavunja ukimya.

"Asante," Namouih akamwambia.

"Kwa hiyo kwa pamoja nyie ni wanasheria... mnaosaidizana?" Efraim Donald akauliza.

"Yeye ndiye attorney, me ni paralegal wake. Ni kama boss na assistant, ila kwa ukaribu sana," Blandina akamwambia.

"Aaa... okay. Nadhani itakuwa jambo zuri nikija kukuona unavyoshughulika na kesi..."

"Kwa nini?" Namouih akauliza.

"Ili nione ulivyo na maneno mengi," Efraim akamwambia, naye Namouih akatabasamu.

Chakula kikaletwa hapo. Ilikuwa ni nyama choma ya mbuzi iliyowekewa na roast, soseji chache na chips kavu nyingi na vionjo muhimu kama pilipili na tomato; zote zikiwekwa mbele ya wanawake hawa, bila kusahau maji ya Namouih. Blandina akamtazama mwenziye huku akitabasamu, na Namouih akamwangalia pia.

"Mnajua yaani na me sijagusa chakula safari yote kwa hiyo, karibuni tupate hii kitu pamoja," Efraim Donald akasema.

"Umekuja kwa usafiri gani kutoka huko?" Namouih akauliza.

"Nimepaa kwa ndege ndogo," Efraim Donald akajibu.

"Wow, kweli?" Blandina akauliza.

"Ndiyo. Kwa kawaida huwa zinawahi, ila niliyochukua leo sijui kwa nini ilinichelewesha kufika kwako," Efraim akamwambia Namouih.

Blandina akachekea kwa chini, naye Namouih akaendelea kumwangalia tu jamaa.

Efraim Donald akawakaribisha kwa mara nyingine tena, nao kwa pamoja wakaanza kupata chakula. Yalifata maongezi kuhusu sehemu ambayo Efraim Donald aliishi zamani mpaka anakua mkubwa, akisema familia yake iliishi maisha ya hali ya chini sana. Akawasimulia jinsi ambavyo alifanya kazi nyingi kwa bidii kwa muda mrefu sana bila kupata mafanikio, lakini mwisho wa siku Mungu akamwonyesha rehema na mambo yakamwendea vyema. Biashara alizokuwa ameanzisha ziliendelea kukua, naye akazidi kufanisika kadiri miaka ilivyosonga, hivyo kwa wakati huu alihitaji kuwa na mtu wa kufurahia naye maisha, ampe kila kitu atakacho, yaani amtendee kama malkia wake.

Blandina alipendezwa haraka sana na Efraim Donald, na hata Namouih alipendezwa na ufasaha katika njia ya kuzungumza ya mwanaume huyu. Efraim Donald akaanza pia kuwauliza kuhusu maisha yao wakiwa kama marafiki; jinsi walivyokutana na mambo waliyojionea. Blandina hasa ndiye aliyezungumza kwa niaba yake na Namouih, na mara kwa mara Efraim alishindwa kujizuia kumtazama sana Namouih, akionyesha wazi kwamba umakini wake ulikuwa kwa mwanamke huyu zaidi.

Wakiwa katikati ya mlo wao, Blandina akapigiwa simu, na baada ya kuongea na aliyempigia, akamwambia Namouih kwamba aliyempatia gari alihitaji alirudishe kwa kuwa alitaka kwenda sehemu, hivyo hii ingemaanisha angepaswa kuwaacha tu wawili hawa peke yao. Efraim Donald akamuuliza ikiwa huko alikohitaji kulirudisha gari ilikuwa mbali, naye Blandina akakubali. Akamwambia asubiri kwanza. Akatoa simu yake na kupiga namba fulani, kisha akasema tu "njoo" na kukata. Namouih na Blandina hawakuelewa alichokusudia kufanya mpaka mwanaume fulani mwenye mwili mkubwa alipofika hapo na kuwasalimu wanawake hawa, kisha akamkazia uangalifu Efraim.

Efraim Donald akawaeleza kwamba huyo alikuwa ni dereva wake, na bodyguard pia, aliyeitwa Suleiman, kisha akamwambia jamaa achukue gari, aende kule Blandina atakapokwenda, halafu atarudi naye. Yaani, atalifuata gari la Blandina mpaka kule atakapoliacha, halafu Blandina ataingia kwenye hili la Suleiman ili amrudishe huku na hivyo waendelee kuwa pamoja. Blandina akasema haikuwa na haja hasa kwa kuwa alihisi ingekuwa vyema kuwaacha wawili hawa peke yao, lakini Efraim Donald akasisitiza kwamba arudishwe tu, kwa sababu alifurahia uwepo wake pia. Jambo hili lilimfurahisha sana Namouih, ila hakuna aliyejua hilo.

Basi Blandina akaondoka na Suleiman baada ya hayo, akiwa ameichukua chupa moja ya Serengeti Lite kwa kuwa nyingine mbili alikuwa amezimaliza, akisema angepita nyumbani kuiweka huko kabisa ili baadaye aweze kuitumia. Efraim Donald alikuwa amemtania kwamba akirudi angekuta kreti linamsubiri, na kwa haraka ikawa wazi kwamba walizoeana upesi. Wakawa wamebaki wapendanao hapo, isipoeleweka vizuri ikiwa ni wapendanao tayari kwa sababu hata urafiki haukuwa umekita mizizi.

"Naona Blandina anakupenda sana," Efraim Donald akamsemesha.

"Ndiyo, ni mbali tulikotoka," Namouih akamwambia.

"Hakukuwahi kutokea zile za 'umenichukulia bwana wangu'?"

"Ahahahah... hapana. Mimi kwenye ku-date sikuwa active sana."

"Ila yeye?"

"Ni kipaumbele."

"Ahahahah... anaonekana anajua kujiachia. Inanifanya nikisie kwamba na wewe una hiyo side, na ninataka sana kuiona..."

"Ahah... hapana. Mimi sina fujo sana kaka'angu..."

"Niite Efraim..."

Namouih akatabasamu na kuangalia chini.

"Yaani unajua kiukweli bado ni ngumu kuamini kwamba uko nami now... niliisubiri siku hii kwa muda mrefu sana," Efraim akasema.

"Why?"

"Kwa sababu hakuna mtu mwingine aliyeiteka akili yangu namna ambavyo wewe ulifanikiwa kufanya..."

"Hiyo yote kwa sababu tu uliniona kwa conference... na penyewe hata sikumbuki ni conference gani hiyo..."

"No, siyo kwa sababu tu nilikuona. Ni kwa sababu moyo wangu ulikupenda sekunde hiyo hiyo niliyokuona. Yaani sikuacha kukutazama. Ilikuwa ni kama nimeona kitu fulani kigeni kabisa machoni pangu. Nilitaka kukujua. Nilitaka kukufata hata tu kukuuliza 'hey, hivi mbona kama nakufahamu? Tulishawahi kucheza makopo pamoja?'"

Namouih akatabasamu kidogo.

"Yeah... yaani nilitamani nikufate niseme chochote tu mradi niongee nawe, lakini nikakukosa kwa sababu ya kushughulika na mambo mengi. Sasa hivi ni kama siku hiyo imejirudia tena. Nahisi kupaa yaani," akasema Efraim Donald.

"Ahah... ni vizuri kujua wewe ni mwanaume unayeweza kuji-express. Nimependa hilo kuhusu wewe," Namouih akamwambia, lakini maneno hayo yalikuwa ya kumfurahisha tu jamaa siyo kwamba yeye alifurahia kuyasema.

"Najua bila shaka hivi siyo jinsi ulivyotazamia kuanzisha urafiki wa kimapenzi na mtu fulani, siyo?" Efraim akauliza.

"Kwa nini unauliza hivyo?" Namouih akauliza pia.

"Ni kwa sababu ya hali unazopitia..."

Namouih akabaki kumtazama tu.

"Baba anaendeleaje?" Efraim akauliza kwa kujali.

Namouih hakuwa ametegemea swali hilo, hivyo kwa sekunde chache akabaki kimya, kisha akauliza, "Umejuaje kuhusu..."

"Usijali my dear, usijali. Ninakuelewa vizuri sana. Magreth aliponipa namba yako aliniambia kwamba baba yako anaumwa sana, na ndiyo maana ulikuwa huku kwa kipindi hiki. Nilianza kujiuliza ikiwa ingekuwa busara kukufata kwa wakati huu, lakini nilishindwa kujizuia. Nataka tu kuwa karibu nawe angalau... kama kukupa faraja, na kwa jambo lolote litakalohitaji msaada, basi nipo hapa kwa ajili yako. Okay?" Efraim akaongea kwa kujali sana.

Namouih akabaki tu kumwangalia usoni, na mwanaume huyu akakishika kiganja chake kilichokuwa mezani kama kumpa faraja, kisha akasema ikiwa angependa kuzungumzia hali ya baba yake, basi yuko tayari kumsikiliza. Namouih akaanza kumwelezea tu kwa kifupi kuhusu tatizo la baba yake, akisema kwamba mwanzoni walifikiri alikuwa na ugonjwa wa kawaida tu ambao wangeweza kuupatia suluhisho la kawaida, lakini sasa walitambua kwamba alihitaji upasuaji wenye utaalamu na gharama ya juu kwa kuwa mzee wake alikuwa na saratani kwenye pafu lake. Akasema kwa hizi wiki kadhaa za nyuma yeye na familia yake wamekuwa wakijitahidi kumpatia msaada wa kitiba, lakini alikuwa akiendelea kudhoofika taratibu hasa kwa kuwa alikaa nayo kwa muda mrefu sana bila kujua.

"Kwa hiyo madaktari wakasema uwezekano wa yeye kupona upo kabisa?" Efraim Donald akamuuliza.

"Ndiyo, lakini ndiyo itahitaji mambo mengi ambayo kiukweli sijui ikiwa yatamsaidia au kumwongezea maumivu tu. Yaani mpaka naogopa," Namouih akaeleza kwa huzuni.

"Usiogope. Sikia. Ninataka sana kukusaidia Namouih... ninaomba tu uniruhusu nifanye hivyo..."

"Sitaki matatizo yangu kuwa mzigo kwako Efraim..."

"No, usiseme hivyo. Ninatamani, ninatamani sana kukuondolea jambo lolote lile linalokutatiza. Yaani Namouih sitaki na sitaki kukuona unaumia. Nitafanya kila kitu kwa ajili yako kukuonyesha jinsi gani ninavyokupenda Namouih..."

"Ahah... yaani... ki... kihivyo tu? Hata kama tuseme nyumba yetu ingeungua kwa...."

"Ningekununulia mbili zaidi," Efraim akamkatisha na kusema hivyo.

"Kwa nini? Kwa nini umenipenda mimi?" Namouih akamuuliza.

"Naweza kusema ni moyo tu. Moyo hauna hiyana," Efraim Donald akamwambia.

Namouih akatabasamu kidogo na kuangalia chini. "Sijui nisemeje... yaani... sikutegemea..."

"Njoo," Efraim akasema huku akisimama.

Namouih akamwangalia tu bila kuelewa alichomaanisha.

"Njoo nami, twende," Efraim Donald akamwambia.

Namouih akasimama na kuanza kumfata.

Walielekea mpaka ndani ya hoteli ile, nao wakafika mpaka kwenye chumba kimoja ghorofa ya tatu, naye Efraim Donald akaufungua mlango wake. Akamwambia aingie na asiwe na wasiwasi, naye Namouih akapita na kuingia ndani. Efraim Donald akaelekea mpaka kitanda kilipokuwa, na tayari Namouih alikuwa ameona kisanduku kidogo sana cha rangj ya samawati hapo. Efraim Donald akakichukua, kisha akamsogelea Namouih na kukifungua mbele yake. Namouih akabaki kuutazama tu mkufu mzuri sana aliouona hapo, kwa haraka akitambua ulikuwa wa gharama kubwa mno. Akamtazama tu Efraim usoni, kwa njia ya kawaida na si shauku.

"Ninataka ukiwa nami, kila kitu utakachotaka, na hata kama hujakiomba, ukipate kutoka kwangu. Nitaka kugeuza huzuni zako kuwa furaha Namouih, na lolote litakalokupa furaha niliongeze maradufu zaidi. Ninaomba tu uniruhusu niwe sehemu ya maisha yako," Efraim Donald akasema kwa hisia.

Namouih akatulia kidogo, kisha akauangalia mkufu huo tena. Efraim Donald akautoa kwenye kisanduku chake na kisha kuzungukia nyuma ya mwanamke huyu, naye akaupitisha shingoni mwake na kumvalisha akiwa kwa nyuma. Kulikuwa na kioo sehemu ya mwanzo ya kuta za chumba hiki, hivyo Efraim akamsogeza vizuri hapo na kumtazamisha jinsi alivyopendeza shingoni kwake. Kupitia kioo hicho, Namouih angeweza kumwona Efraim, jinsi alivyotabasamu kwa matarajio mengi, naye Namouih akatikisa tu kichwa chake, kuonyesha kwamba alikuwa amekubali kile Efraim Donald alichomwomba.

Mwanaume huyu alifurahi sana, naye akaugeuza mwili wa Namouih taratibu ili watazamane. Sura ya Namouih kiukweli bado ilionyesha kutokuwa na uhakika, lakini kuona jinsi ambavyo Efraim alifurahia sana kukamfanya tu atabasamu pia. Efraim Donald akaanza kuusogelea uso wake Namouih zaidi, akionyesha ni kama anataka kumbusu, naye Namouih akatulia tu bila kuonyesha itikio lolote lile. Efraim alipoukaribia mdomo wa Namouih, akatulia kidogo, kisha akaahirisha kumbusu na kuamua kumkumbatia tu. Hili wala halikumshangaza Namouih, bali kwa utulivu wake akaendelea kubaki ndani ya kumbatio la jamaa.

"Mimi na wewe, bado tuna safari ndefu. Sitachoka kusubiri mpaka moyo wako unikubali kwa asilimia zote. Always remember that. Nakupenda."

Maneno hayo yaliyosemwa kwa njia nzuri sana na Efraim Donald yalimtuliza sana Namouih, kwa kuwa ni kama alikuwa akisema yuko tayari kusubiri mpaka hisia za Namouih kumwelekea zikite mizizi zaidi, yaani ampende kama vile yeye anavyompenda. Kuamini mwanaume tena lilikuwa jambo fulani gumu kwake hasa kwa sababu aliwahi kupitia usaliti uliomuumiza sana, lakini kwa wakati huu angetakiwa kujitahidi kuonyesha yuko tayari kupenda pia, hasa kwa kuwa mwanaume huyu alionekana kuwa mtu mzuri sana.

Taratibu nwanamke huyu akaipitisha mikono yake mgongoni kwa Efraim Donald, akirudisha kumbatio lake pia, naye akafumba macho yake kwa hisia akiwaza mambo ambayo yangefuata baada ya kukubali ombi la mwanaume huyo.

★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next