MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Ysiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TATU
★★★★★★★★★★★★★
Nikamwangalia Ankia machoni, nikiwa nimetulia tu. Tayari sasa alikuwa ameufunika mwili wake, lakini aliendelea kushikilia pale pa kufungia khanga kwa mikono yake yote kama vile amegandishwa kwa sababu ya kunitazama kwa umakini, ama labda butwaa. Ni wazi hakuwa amehisi uwepo wangu nyuma yake. Lakini hali ya utulivu tu aliyoweka, ilinipendeza sana. Hakuwa na makeke. Jinsi nilivyomwangalia machoni, ndivyo ambavyo na yeye pia aliniangalia. Ni kama alikuwa anasubiri niseme ama nifanye chochote kile, na ndiyo kitu ambacho nilipenda, kwamba alisubiri... kuona... nini... kingefata. Nikatabasamu tu, naye akatabasamu na kuweka vidole vyake kuziba mdomo kwa njia ya aibu. Jambo hili lilikuwa limesababisha mshkaji wangu kule kati aanze kunyanyuka kwa sababu alipenda sana sifa, kwa hiyo nikaamua kupiga hatua zaidi kuelekea pale 'extension' ilipokuwa na kuchukua chaja yangu, na nilipomtazama nikakuta amesimama vilevile huku akiniangalia kwa macho yenye subira.
"Niliacha chaja... nitachomeka simu chumbani," nikamwambia.
Akatikisa kichwa taratibu kama kusema sawa, huku midomo yake akiibana. Sura yake ilionyesha matarajio fulani hivi, yale matarajio ya mimi ndiyo nipige hatua ya kwanza kwenye wazo moja ambalo najua sisi wote tulikuwa nalo, lakini sikutaka kufanya matarajio hayo yaone mwanga.
Nikamwambia, "Usiku mwema, eti? Tutaonana asubuhi."
Akaangalia chini kiasi na kusema, "Sawa. Ulale salama."
"Haya," nikajibu hivyo na kumpita, nikielekea chumbani kwangu bila kumgeukia tena.
Nafikiri alijihisi vibaya, ama hata kama ikiwa hakujihisi vibaya, basi alijiuliza kwa nini sikufanya jambo lolote kuhusiana na tukio hilo dogo hapo sebuleni. Angefikiria labda sikupendezwa naye, lakini haikuwa hivyo. Ni kwamba tu sikuona ulazima wa kuchukua hatua yoyote ama kusema lolote kuhusu hilo, na ingepaswa kubaki kuwa namna hiyo maana mimi na yeye bado hatukujuana vizuri, na mambo ya papara hayakuwa kwenye mtindo wangu wa kushughulika na watu; hasa wanawake. Nikaingia zangu tu chumbani na kushusha neti, mbu wakiwa wengi utadhani wameajiriwa. Nikajilaza kitandani na kutumia muda mfupi kupita Facebook, WhatsApp na Twitch, kisha ndiyo nikaiweka simu chaji na kuanza kuhangaika kuutafuta usingizi huku nyimbo mbovu sana za mbu zikinikera mpaka kunako.
★★★
Nilikuja kuamka pakiwa pameshakucha sana, yaani ile kuamka ya hauwezi kusinzia tena. Mwili wangu ulikuwa na ukawaida wa kuniamsha mapema mno, nami ningeendelea kulala na kusinzia tena mpaka muda ambao ningechoka kuendelea kulala. Ila ilikuwa hivyo tu nyakati ambazo sikuwa na kazi za kufanya, kama wakati huu, na hata leo nilikuwa nimeamka mara kadhaa na kuendelea tu kulala mpaka sasa sasa. Nikajitoa kitandani na kuchukua simu yangu, nami nikakuta ni saa nne asubuhi. Kulikuwa na 'missed call' kadhaa kutoka kwa watu wangu wa karibu na jumbe kadhaa pia, nami nikawatafuta na kuongea pamoja na baadhi yao kwa ufupi, kisha nikanyanyuka na kwenda kabatini.
Nilipenda sana hii hali ya kuwa mwenyewe, yaani kama namna ambavyo mtu angechagua kwenda likizo na kutembelea sehemu za kifahari, lakini mimi nikaja sehemu hii yenye mazingira ya kawaida tu, kwenye uswahili zaidi, na nilikuwa na hamu ya kuona namna ambavyo watu kiujumla wangenitendea kadiri ambavyo muda ungepita nikiwa huku. Kitu ambacho nilihitaji kufanya kwa sasa ilikuwa ni kununua mswaki na dawa mpya za kusafishia meno, ili kinywa kikae safi. Nikavaa kaushi nikiwa na bukta kwa chini ili nitoke kwanza mpaka nje kwenda kukojoa, lakini nilipofungua mlango kidogo wa chumba hicho, nikaanza kusikia maongezi baina ya wanawake wawili. Sauti ya mmoja niliifahamu, ikiwa ni Ankia, lakini ya mwenzake sikuijua. Alikuwa rafiki labda, na mada waliyoizungumzia ilimhusu mwanamke yule niliyekutana naye jana mpaka akanipa lifti kwa msisitizo wangu wa kuumwa kimaigizo, yaani Miryam.
"Enhe..." nikasikia Ankia anaitikia.
"Basi, nasikia mchumba amefika, tena na wazazi wake sijui... Miryam hajamtolea nje! Eheee... shoga acha tu..." mwenzake akamwambia hivyo.
"Kamfukuza?" Ankia akauliza.
"Eeeh! Tena limeletwa hadi na gari, huwezi kuamini, lakini limbwende bado tu limekaza vyuma! Ahahaaa... haki ya mama. Miryam hataki kuolewa, yaani hataki. Sijui wamroge?"
"Atakuwa na sababu zake."
"Sababu zipi Anki? Umri unaenda, anazeeka, hajazaa bado, hayo yote alikuwa ananiambia Shadya leo yaani wameshamtafutia wachumba wa maana wanaoweza kummwagia mipesa ambayo sisi wenzake tunaililia ila haitufikii... shoga! Anaringa huyo! Anafikiri wataendeleaga tu kumpigia magoti eti!"
"Shadya ndiyo kakwambia ya jana?"
"Eeeh, kaniambia wamemletea mpaka na gari lakini kalikataa. Kisa? Eti bado anaitunza familia yake, inamhitaji. Kwani anashindwa kuwatunza hata akishaolewa, ama ni midenguo tu?"
"Asa' unafikiri watafanyaje, watamlazimisha? Kama hataki ndiyo hivyo... inabidi wamwache tu..." Ankia akamwambia.
Inaonekana walikuwa wanapiga umbea kuhusu ile ishu ya jana ya kuchumbiwa kwake Miryam, na ya huko kufika mpaka kwa Ankia namna hii ilimaanisha yangesambaa kwingi.
"Hana lolote mi' nakwambia, huyo mwanamke malaya tu. Usikute hapo alipo anatoka na limme la mtu huko, af' akirudi anajifanyaga mtakatifu kweli... eti familia yangu wananihitaji..." mwenziye akaendelea kusema.
"Huo wivu wako mama Chande unakufanya unamjaji vibaya dada wa watu. Mbona me naona yuko poa tu? Hayo ni maisha yake, acha ajiamulie anachotaka," Ankia akamwambia.
"Mm? Asa' me nimwonee wivu kisa nini? Hako kaweupe ama?"
"Siyo weupe tu, huyo dada mzuri sana ndiyo maana unaona wengi wanajibebisha hapo. Lakini hana shobo za huko, la sivyo angewaacha kweli watu wake wa ukoo na kuolewa na litajiri kama angekuwa hawajali..."
"Aaa wewe mtetee tu, ila tuulize sisi tunaomjua ndiyo utaambiwa. Siku akija kumchukua bwana wako ndiyo utasema mama Chande aliongea kweli..."
Ankia akacheka kidogo na kusema, "Unadhani hata kama ni wewe ukimchukua bwana wangu nitahangaika basi?"
"Wewe huyo? Ulivyo na wivu hivyo?"
"Akhaa, me siko hivyo. Mwanaume akiona abebe ndoo nyingine ya zege me nasubiri mbebaji mwingine aje anichukue, mbona wapo wengi tu?" Ankia akasema hivyo.
Kauli yake ikanifanya nitabasamu. Alionekana kupenda misemo sana, na alikuwa na akili iliyofunguka (open mind).
"Nyoo, utaongea hivyo na mtu mwingine asiyekujua, ila me hunidanganyi. We' ndo' wale wanaopiga hadi na magoti, michozi na mikamasi inakuvuja kisa umeachwa na mapenzi!" huyo mama Chande akamwambia hivyo.
Ankia akasikika akicheka.
Mama Chande akacheka kwa nguvu pia na kusema, "Au midadi imeshapanda kwa mchina wako?"
"Eh, wewe, punguza sauti... atakusikia..." Ankia akasikika akisema hivyo.
Mada ikawa imegeukia kwangu, nami nikaweka umakini zaidi.
"Usianze mambo yako. Kwanza umejuaje kuhusiana naye?" Ankia akamuuliza.
"Fatuma kamwona jana anaingia, akaniambia. Mbona umemficha ndani tu shosti, hutaki tumwone mchina nini?" mama Chande akasema.
"Siyo mchina. Ni mpangaji wangu... siyo mtu wangu. Punguza kelele," Ankia akamwambia.
"Mpangaji siku ya kwanza, ya pili ashakunyandua, na najua ndo' unachosubiri."
"Ila mama Chande..."
"Nini, kwani uwongo? Utasahau hadi kumtoza kodi akishaanza kuku(.....)," mama Chande akasema hivyo.
Nikacheka kidogo kwa pumzi huku nikitikisa kichwa. Huo ndiyo ulikuwa ule uswahili wenyewe, tena na hapo ni kwa kiasi chake tu, nami nilipenda sana.
"Acha sifa mama Chande, nitakufukuza sasa hivi..." Ankia akamwonya hivyo kwa sauti ya chini.
"Unafikiri natoka hapa bila kumwona mchina? Umeliwa! Hatoki mtu hapa hata usipopika," mama Chande akasema.
"Na ukimwona ndiyo itakuongezea nini labda?"
"Buzi... huwezi kujua..." mama Chande akamwambia.
"We' ni mshenzi..." Ankia akamwambia hivyo kwa sauti ya chini.
Mama Chande huyo akacheka kiumbea kiasi huku Ankia akimtuliza, nami nikaona nimpe alichokitaka.
Nikarudi sehemu ya kabati na kurekebisha uso kiasi, kisha nikavaa na T-shirt kusitiri mikono. Nywele zangu zingekuwa na mwonekano fulani wa nywele laini za kiarabu zilizovurugika kila mara nilipotoka kuamka, kwa hiyo sikuzichana kabisa ili nikitoka ionekene kweli ndiyo nilikuwa nimeamka muda huo huo. Nikaenda kuufungua mlango na kuanza kuielekea sebule. Niliweka uso makini, kama vile sijali lolote hapo, nami nilikuta Ankia akiwa amekaa kwenye sofa moja pamoja na huyo mwanamke. Mama Chande alikuwa mwanamke mwenye umri mkubwa kiasi cha kufikia miaka 40, mweusi wa maji ya kunde, mwenye mwili mwembamba kiasi, na ningeweza kusema urefu wake akisimama ungekaribiana na wangu kabisa. Alikuwa na sura iliyokomaa, akiwa ameweka kope za bandia machoni na lipstick nyekundu mdomoni, huku vazi lake likiwa ni jezi nyeusi ya Yanga iliyoficha kifua kikubwa kwenda mbele, pamoja na suruali nyeupe ya skinny iliyobana mapaja yake yaliyotokeza kiasi. Alikuwa na nywele fupi zilizopakwa dawa na kutiwa rangi ya njano mpauko, naye alifuga kucha ndefu mikononi zilizopakwa rangi nyekundu. Labda zilikuwa za bandia. Ankia yeye alikuwa amevaa dera, huku akijifunga kilemba kichwani kama nilivyomkuta jana tu, na kwa pamoja waliniangalia usoni nilipowakaribia zaidi.
"Za asubuhi?" nikawapa salamu kwa sauti tulivu ya kiume.
"Aa salama..." mama Chande akasema hivyo.
"Nzuri tu. Umeamkaje?" Ankia akaniuliza hivyo huku akitabasamu kiasi.
"Vizuri tu, na nyie?" nikawauliza.
"Ah, kama unavyotuona. Unalala kweli..." Ankia akaniambia huku akitabasamu.
"Ndiyo, ni uchovu. Wacha niingie uani," nikamwambia.
"Sawa," Ankia akajibu.
Nikawapita na kutoka ndani ya mlango wa kuingilia ndani hapo, na sikuwa hata nimetoka sehemu hiyo kabisa nami nikaanza kumsikia huyo mama Chande akisema mimi ni mweupe mno jamani! Nikakaza tu tabasamu na kwenda kukojoa, nami nilipotoka huko nikatazama upande wa ile nyumba niliyoingiamo jana. Sikuliona gari lile aliloendesha Miryam mnunaji, ikiwa wazi aliondoka bila shaka, lakini nikaweza kumwona kijana fulani akiwa anacheza mpira peke yake kwa kuupigisha mara nyingi kwenye mguu mmoja; tunaita danadana. Huyo alikuwa mgeni kabisa kwangu, hata jana sikumwona pale. Alikuwa na weupe pia, umri wake si mbali sana kufikia miaka 27 kimakadirio, akiwa na mwili mrefu kiasi na mwembamba pia. Alivalia jezi ya Simba na bukta nyeupe, na alinyoa mtindo wa kiduku bila kuwa na nywele nyingi sana juu ya kichwa. Nikawaza labda alikuwa ndugu yao mwingine akina Zawadi mweupe, nami nikarudi zangu tu ndani kwa Ankia.
Nikamkuta pamoja na shosti yake, lakini wakati huu Ankia akiwa amesimama usawa wa meza, na mezani hapo alikuwa ameweka chupa ya chai, kikombe, chombo cha kutunzia sukari na kijiko chake, pamoja na bakuli jeupe la udongo lililofunikwa kwa bakuli lingine la aina hiyo hiyo. Mwenzake alikuwa ametulia tu akionekana kuwa bize na simu, nami nikamtazama Ankia usoni na kuona anatabasamu kiasi.
"Karibu chai," akaniambia hivyo.
Ahe!
Nikarudisha tabasamu hafifu tu, kisha nikamwambia, "Asante. Nahitaji kusafisha mdomo kwanza, sijui hili duka la hapa nje wanauza miswaki?"
"Eee anauza," Ankia akaniambia.
"Aaa basi poa, ngoja nifate kwanza afu'..."
"Hamna, usijali, nipe tu hela nikufatie," Ankia akanikatisha.
Nikamwona kwa jicho la chini rafiki yake akitabasamu kwa kuikunja midomo kwa njia ya kichokozi, nami nikamuuliza Ankia, "Sikusumbui?"
"Hamna wala, haunisumbui," akanijibu.
"Haya, nakuja," nikamwambia hivyo na kisha kumpita kulekea chumbani.
Sijui ikiwa kila alichokifanya kunielekea ilikuwa huduma nilizohitaji kulipia baadaye labda, lakini huo mtindo wa kunifanya mimi nionekane kama mume wake vile haukuwa mbaya sana kwangu. Huenda aliwatendea wageni wake wote namna hiyo. Nikachukua buku tano na kurejea sebuleni tena, nikimpa anifatie dawa ya meno na mswaki imara, naye huyo akaenda zake. Nikaachwa sebuleni pamoja na mama Chande mwongeaji, aliyeonekana kupenda kusema sana watu pamoja na yule Shadya wa jana. Wakati huu alikuwa kimya tu, akiyapa macho yake ubize mwingi kutazama kilichoonyeshwa kwenye TV, huku mimi nikikaa sofa la pembeni nikipitia mambo fulani kwa simu yangu bila kujishughulisha naye. Sikumsemesha hata kidogo mpaka Ankia aliporudi, nami nikapokea vifaa vyangu vya usafi wa mdomo pamoja na chenji, shwaa chumbani. Kama vile ambavyo Ankia alikuwa ameniambia usiku uliotangulia, mimi pia sikuwa mtu wa kushoboka na mtu yeyote kabisa, labda mpaka awe amenielewa na kunionyesha hilo wazi, ndiyo na mimi ningezisoma naye ikiwa pigo na tabia zingekubaliana.
Nikatoka zangu tena na kwenda kuswaki kwenye lile sinki pale nje, kisha nikarejea ndani na kukaa sofani ili nishushe chai aliyoniandalia mwenye nyumba wangu. Yaani ilikuwa ni baada ya mimi kukaa tu ndiyo na yeye akanyanyuka na kuanza kuifungua chupa ya chai, kisha akaimimina kwenye kikombe nikiwa namtazama tu kwa utulivu. Mara kwa mara niliweza kuona bila kuangalia kwamba mama Chande alinitupia jicho sana, lakini umakini wangu wote ulikuwa kwa Ankia. Akanisogezea meza taratibu, kisha akarudi kukaa na shosti yake. Mwanaume nikajiongeza kwa kuweka sukari iliyonitosha, kisha nikafunua bakuli kukuta ni maandazi laini, ya moto. Nikawakaribisha, nao wakashukuru na kuendelea kukaa kwa utulivu kama Malaika eti. Nikaanza kukipa kinywa ladha tamu ya chai na maandazi. Chai ilikuwa ni tamu balaa, lakini maandazi, ah yaliniacha hoi. Yalikuwa yale maandazi ambayo ukiyaangalia nje yanakuwa yametuna kweli ila ukilishika na kuling'ata unaambulia kula ngozi tu maana ndani panakuwa hewa! Sijui huwa hata wanayapikaje wale wanaoyauza, yaani hamna nyama kwa ndani kabisa, na wanaume hatuyapendagi ya hivyo basi tu ukikuta mwanamke kashayaweka unayapiga kwa kujilazimisha. Wanawake hao wakawa wanaongeleshana tu kwa sauti za chini na kucheka-cheka mpaka nilipomaliza chai yangu tamu.
Ankia akatoa vyombo huku nikimshukuru, kisha akavipeleka jikoni na kurudi kuniletea maji ninawe. Nilishindwa hadi kujizuia kutabasamu bila kumwangalia, lakini nilijua na yeye alikuwa anatabasamu. Akasafisha meza na kupeleka maji hayo huko jikoni, kisha akarudi sofani na kukaa tena. Nikamuuliza ni muda gani ambao alitaka twende kwa mwenyekiti, naye akasema muda wowote tu ambao mimi ningekuwa tayari. Nikasema sawa, nimwache atumie muda huu na rafiki yake kisha mida ya saa saba hivi twende pamoja huko, ili aweze kunionyesha na njia za mitaa hiyo kwa ufupi. Kama kawaida yake akasema haikuwa na neno, nami huyo nikaelekea chumbani na kukiendea kitanda ili nipumzike kidogo.
★★
Saa kama moja hivi likapita nikiwa nimejilaza tu kitandani. Kulikuwa na joto ingawa niliacha milango ya madirisha wazi, nami nikawa nafikiria kwenda kuoga upesi kulipunguza fukuto baya mwilini. Nikiwa namalizia ku-chat na marafiki zangu kwenye simu mlango wa chumba ukagongwa. Nikasema tu 'karibu,' nao ukafunguka na mwanamke mwenye mji kuingia. Wakati huu nilikuwa nimelitoa T-shirt mwilini na kubaki na kaushi na bukta, nami nikakajiketisha. Ankia sasa alikuwa ameingia na mwonekano tofauti. Alivaa T-shirt nyeupe yenye mikono mifupi iliyoubana mwili wake wa juu na kufanya kifua chake kionekane kutuna sana kwa mbele, pamoja na sketi ya zambarau ya kitambaa laini iliyombana haswa na kulichora umbo lake la chini vizuri mno. Iliishia magotini, miguu yake yenye unene wa chupa ya bia ikionekana vizuri kwa usafi wake. Usoni alijitengeneza vizuri pia, na sasa hakuwa amevaa kilemba bali nywele zake ndefu za kusukwa aliziacha wazi ili sisi wote tuzione. Na harufu yake tamu ilikijaza vyema chumba hicho.
"JC... jiandae twende. Niko tayari," akaniambia huku akiwa ameushikilia mlango.
"Eh, saa sita na nusu... usingekuja labda hata ningesinzia. Asante," nikamwambia.
Akatabasamu kidogo.
"Ngoja n'kapige maji faster af' twende. Umedamshi kweli," nikamwambia.
"Ahahah... asante. Nitakusubiri, ukimaliza nishtue... niko chumbani," akasema.
"Poa."
Akataka kugeuka ili aondoke.
"Subiri kwanza, eti hivi...."
Akaniangalia tena baada ya mimi kuanza kusema hivyo.
"Hiyo feni hapo sebuleni inafanya kazi?" nikamuuliza.
"Aa hiyo... hamna. Ilikuwa nzima ikaharibika, nimeshaipeleka kwa mafundi lakini wamenila tu hela halafu haijatengemaa. Nikaikatia tu tamaa," akaniambia hivyo.
"Bado inaonekana nzuri, mafundi wengi unajua ukiwapelekea mashine hata zikiwa na tatizo dogo tu, wanatoa vitu fulani na kuviiba... halafu wanakuja wanakwambia tatizo ni kubwa sana ili wale tu hela yako..."
"Eti eeh?"
"Ndo' hivyo. Sema... nitakuja niiangalie. Ninaweza nikafanya maajabu ikakaa fresh."
Akatabasamu kidogo na kusema, "Utakuwa umenisaidia sana."
"Haya poa. Ngoja nifanye kuoga chap," nikasema hivyo huku nikisimama.
"Poa," akajibu hivyo na kuilamba midomo yake kisha kuibana.
Alipogeuka ili aondoke, nilishusha macho yangu kutazama umbile lake la nyuma, nami nikatabasamu tu kwa jinsi ambavyo lilionekana kuwa zito na lenye mikunjo mingi sana. Ni vitu ambavyo wanaume huwa tunapenda sana, hatushangai bodaboda ikiingia mtaroni shauri ya mwendeshaji kushindwa kujizuia kuvitazama!
Nikavua nguo upesi na kwenda kuoga, na nilikuwa na uhitaji wa kununua sabuni yakwangu peke yangu kwa ajili ya matumizi. Nikaingia chumbani na kujiweka vizuri kimwili, kisha nikatupia T-shirt laini nyeusi yenye mikono mirefu pamoja na jeans la samawati iliyokoza, zilinikaa vyema sana kwenye mwili wangu wenye uimara. Nikatengeneza nywele vyema na kuvaa saa yangu niliyokuwa nimeitunza tu kwenye begi. Kwa hiyo nilipokaa fresh nikajinukishia manukato yangu na kumfata Ankia, kumwambia tujage. Mwanamke akatoka, akionekana kuwa na furaha kiasi, nami nikamwambia anitangulie maana yeye ndiye aliyekuwa ameibeba dira ya Mzinga. Akatabasamu na kutangulia, nasi tukatoka mpaka nje zaidi baada ya kuifunga milango kwa funguo.
Tukaanza kutembea kuzipita nyumba kadha wa kadha, taratibu, na aisee, kila mtu alitutazama. Nadhani Ankia alikuwa tu na ile akili ya kuzaliwa kufatisha namna ambavyo mimi niliitikia mazingira kwa kutowatazama watu na kujali nyendo zetu tu, lakini angewasemesha kifupi wale waliomfahamu walipompa salamu na kuendelea kutembea pamoja nami. Nilikuwa wa namna makini sana. Shobo pembeni. Tukakata mtaa na kuingia mwingine kuelekea Mzinga, ambako kulikuwa na shughuli nyingi zaidi na masoko, na kama kawaida macho mengi yalikuwa kwa "mchina" mgeni na mwanamke wake. Tukafika mpaka pale ambapo nilishushwa na daladala ile usiku wakati nakuja kwenye lami, nasi tukakunja kona kidogo tu na mbele zaidi tukaifikia ofisi ya "Kata ya Mzinga." Ankia akanipeleka mpaka kuifikia, tukiwa tumepita kijiwe kikubwa cha wadau waliopenda kunywa kahawa na tangawizi kali, nasi tukaenda kuonana na mwenyekiti.
Watu wa humo walitutendea kwa njia fulani ya unyenyekevu, na baada ya Ankia kueleweshana na mwenyekiti kuhusu suala letu la upangishaji, nikapewa makaratasi ya kutia sahihi pamoja na Ankia na kopi za kutunza. Nilihitajika kupigwa picha ndogo za 'passport' ili zibandikwe pia kwenye karatasi, kisha jamaa akaweka mihuri yake, nasi tukasepa. Tukatoka zetu tena ili turudi pamoja nyumbani. Ndiyo, nyumbani. Angalau Ankia alikuwa ameanza kunipa malezi yaliyonifanya nijisikie kuwa nyumbani, na bado sikuwa nimemwonyesha shobo nyingi sana mwanamke huyu hata kama hali ya kuzoeana ilianza kuwepo baina yetu. Ndivyo nilivyokuwa. Tulipoanza kurudi tukapita sehemu waliyotengeneza chips, mishikaki, nyama za kuku, na ndizi za kukaangwa. Nikamwambia Ankia twende hapo ili nichukue msosi turudi nao maskani, naye akakubali. Tukaenda na kuomba huduma, watupatie chips-yai mbili, kuku za kukaangwa vipande vitatu-vitatu, pamoja na mishikaki mitano-mitano. Tukapatiwa misosi yetu, nasi tukapiga mwendo tena mpaka kule tulipoishi. Zamu hii tulitumia njia nyingine ili Ankia anizoeshe maeneo zaidi, na baada ya kufika pale dukani nikamwambia achukue soda mbili pamoja na sabuni nzuri za kuogea, nami nikatangulia nikiwa na funguo ya mlango wa kule ndani.
Yale makaratasi ya mwenyekiti alikuwa nayo Ankia, yakiwa salama ndani ya bahasha, naye akawa amefika ndani pia pamoja na chupa mbili za Pepsi baridi na kuziweka mezani. Tayari na mimi nilikuwa nimeweka mifuko ya vyakula mezani, hivyo Ankia akanipatia sabuni mbili alizonunua nami nikampa moja, kisha nikaenda chumbani ili nibadili nguo na kuvaa nyepesi. Nadhani muda mfupi niliotumia kubadili mavazi ulimtosha sana Ankia kufungua vyakula na kuviandaa kwenye sahani safi, kwa hiyo niliporudi sebuleni nikakuta vikiwa wazi tayari kukamuliwa. Nikakaa sofani na kujiandaa kula, naye akaniletea maji na kuninawisha. Akanawa pia, na alipoanza kusogeza meza upande wangu, simu yangu ikaita, nami nikapokea na kuzungumza na ndugu yangu mmoja aliyekuwa amenipigia. Ankia akafungua soda zetu na kisha kukaa kwenye lile sofa dogo, lakini nikamwonyesha mshangao kwa sura yangu na kumpa ishara kuwa aje kukaa kwenye sofa nililoketi mimi. Anakaa mbali kufanya nini sasa? Akatabasamu kidogo kwa shau, kisha akaja na kukaa karibu yangu.
Tukaanza kula pamoja, huku wa kwenye simu akigoma kabisa kutaka kuniacha. Ikabidi nimwambie simu inazimika hivyo ningemtafuta baadaye, nami nikakata na kuhamishia umakini wangu kwa Ankia. Alikuwa akijitahidi kula kistaarabu eti mbele yangu, lakini nikamwambia ajiachie zaidi maana mimi nilipenda kula kwa fujo hasa chakula kikiwa kitamu sana, na kama niko na mtu niliyemzoea. Muda si muda tukawa tunakula huku tukifurahia maongezi yenye utani mwingi, nami nilimchekesha sana kwa kumsimulia hadithi za baadhi ya mambo mengi niliyojua. Alikuwa na kicheko fulani hivi cha chini-chini chenye kuvutia, nami nilielewa kwamba mbele yangu alikuwa anajitahidi kukibana kile kicheko cha kimbea kama angekuwa anapiga porojo na mwanamke mwenzake. Tukawa tumemaliza kula baada ya dakika kadhaa, naye akanishukuru kwa kumnunulia chips na kuku, kisha akatoa vyombo na kuvipeleka jikoni. Akarudi na kukaa kwenye sofa pembeni yangu tena bila mimi kumwambia afanye hivyo.
Akachukua rimoti na kuiwasha TV, akianza kubadili chaneli huku mimi nikiwa nimekaa kwa kuegamia mgongo zaidi, nikiwa nimeshiba kweli, kwa hiyo yeye akaonekana mrefu kunipita maana alikaa kitako. T-shirt alilovaa lilikuwa limeinuka juu kidogo kuniruhusu nione nyama laini ya kiuno chake, nami nikamtazama usoni. Ulionekana kwa upande kutokea nilipokuwa nimekaa maana uso wangu ulikuwa nyuma yake zaidi, na akiwa bado bize kubadili chaneli, nikaona nimchokoze kwa kukigusa kiuno chake kwa kiganja changu. Akashtuka kidogo na kunigeukia, nami nikamtazama machoni kwa njia ya kichokozi zaidi huku nikiendelea kutembeza vidole viwili kwenye kiuno chake. Akanipa tabasamu fulani hivi la nyodo, kama hataki lakini kwa furaha eti, kisha akaigeukia TV tena bila kunizuia nisiendelee kumfanya hivyo. Nikaona nimchokoze zaidi kwa kuingiza vidole vyangu ndani ya T-shirt lake kupitia mgongoni mpaka kufikia ubavu wake mmoja, kisha nikamtekenya kidogo.
Akashtuka na kusogeza nyonga mbele huku akisema, "Iih, wewee..."
Aliniangalia kwa macho yaliyoonyesha hisia zinataka kumkolea, nami nikacheka kidogo kwa pumzi, kisha akarudisha mkono wake nyuma na kuutoa wangu mgongoni kwake kama kuonyesha anataka niache.
"Kwa nini mwanamke mzuri kama wewe unaishi peke yako?" nikamuuliza hivyo kwa sauti tulivu.
"Si nimependa tu?" akajibu bila kunitazama.
"Tokea lini umependa tu?"
"Tokea zamani."
"Mbona nasikia haukuwa unaishi peke yako?" nikamuuliza.
"Umesikia kwa nani?" akaniuliza hivyo na kuniangalia.
"Nina mitandao yangu..."
"Mitandao ipi wakati umefika jana tu?"
"Mengi yametokea jana kabla sijafika hapa, utajuaje?"
"Mhm..." akafanya hivyo na kuangalia TV tena.
Nikaingiza tena kiganja changu mgongoni kwake na kuanza kuukuna taratibu, kitu ambacho kilifanya niguse mikanda ya sidiria yake kwa nyuma, nami nikamuuliza, "Mume wako je?"
"Sina mume," akajibu bila kunitazama.
"Alienda wapi?"
"Sijui."
"Kwa nini aliondoka?"
"Si tuliachana?"
"Kwa nini mliachana?"
"Tulichokana."
"Kisa nyimbo za Ali Choki au?"
Akacheka kidogo.
"We' ni mzuri Ankia," nikamsifia kwa sauti zembe, makusudi.
"Uzuri wangu uko wapi?"
"Upo hapo hapo kwako."
"Mhm... huko Sinza ulikotokea hujaona wanawake wazuri?"
"Sijaona..."
"Unanipulizia moshi tu. Huko ndo' kuna pisi sana..."
"Hazikufikii..."
"Kwenda zako! Unanipaka tope tu, me kibonge wa Mbagala nitafanana na hao wanaojiona keki hapa jijini?" akasema hivyo na kukitoa tena kiganja changu mgongoni kwake.
"Me sivitaki hivyo vikeki bwana..." nikamwambia hivyo.
"Umeshapiga vingi eh?"
"Aa wapi, hata sijawahi kabisa..."
"Mh... nhaa..." akacheka kidogo.
"Ni kweli, si unaniona me bado mtoto?"
"Kwa hiyo kama we' bado mtoto?"
"Nahitaji malezi bora. Nani mwingine atanipa hayo sasa?"
"Si wa huko kwenu?"
"Me nataka ya huku..."
"Nenda Rangi Tatu utayapata..."
"Nimeshayapata mbona?"
"Wapi, Rangi Tatu?"
Nikaingiza tena kiganja changu mgongoni kwake na kusema, "Hamna, ni kwenye rangi yako."
"Rangi yangu imefanyaje?"
"Ni nzuri..."
"Mhm..."
"Una katabia fulani hivi nakapenda sana..."
"Kapi hako?"
"Unapozilamba na kuzibana hizo lips... na hayo macho lege..."
Akatabasamu kidogo na kuangalia pembeni, nami nikaushika ubavu wake ndani ya T-shirt lake. Akataka kuutoa mkono wangu, lakini nikauvuta mwili wake na kumfanya aegamie sofa kwa mgongo wake, na mpaka kufikia hapo nilikuwa nimeshasimamisha hisia zangu kwa hasira kali mno. Akaweka kiganja chake kifuani kwangu huku akigoma kunitazama machoni, kwa kuwa sasa nyuso zetu zilikaribiana sana.
"Mm... JC..."
"Nini?"
Akaishia kushusha pumzi tu.
"Mbona unakuwa hivyo?" nikamuuliza hivyo kibabe.
"Unanipenda... au unanitamani tu?" akaniuliza hivyo.
Khh! Mbona kaanza kuingiza Bongo movie tena?
Nikamwambia, "Tunaanzaga kutamani. Kupenda ni baadaye."
Akawa anapumua kilegevu eti, huku mimi nikiwa bado nimemshika kiunoni na mkono mwingine ukilishika paja lake lililo ndani ya sketi aliyovaa, naye akasema, "Me siwezi..."
"Usiweze nini?"
"Kufanya unachotaka..."
"Kwa nini usiweze?" nikamuuliza.
"Wanaume waongo sana..." akaniambia kwa deko.
"Wamekudanganya wengi?"
Hakujibu na kuibana tu midomo yake.
"Lakini me si mtoto? Hapa unafanya tu kunitunza mama," nikambembeleza.
Akaniangalia machoni, nami nikawa bado nampa tabasamu la kichokozi. Nikamvutia zaidi kwangu kwa mkono ulioshika kiuno chake, naye akataka kujirudisha nyuma lakini nikamshika shingoni kwake na kuivuta mpaka karibu zaidi na uso wangu, kisha nikaanza kuibusu.
"...hhh... JC..."
"Nini?"
"Ana'eza akaja mmtu...."
"Nani aje bwana? Em' tulia..."
Nikazinyamazisha kelele zake na kuanza kumbusu kinywani. Hakuwa mtaalamu sana wa kupiga busu lakini midomo yake mikubwa ilivutika vizuri sana kwangu. Na angalau hakunuka mdomo la sivyo ningesitisha zoezi hilo hapo hapo! Akawa anaguna kwa pumzi nzito huku akiniangalia kama vile anateswa, maana niliendelea kumpandishia hamu kwa kufanya mengi na kuzidi kuipandisha tu. Akakibana kichwa changu kwake zaidi ili niendelee tu kumtafuna, nami nikaona tuyatoe mambo yetu sebuleni na kuyapeleka chumbani. Alionyesha uzito, labda hisia alizokuwa nazo zilifanya awe mzito mno, kwa hiyo nikawa namvuta kukielekea chumba huku amenishikilia na kutembea kwa kuyumba utadhani hakujiweza. Kiukweli nilikuwa nimesisimka sana na nilitaka kufanya jambo la maana pamoja na huyu mwanamke, lakini ile tu tumeufikia mlango wa chumba changu hizo fikira zikavurugwa.
"Ankiaa!"
Tukaivunja busu yetu na kuangalia upande wa nje, ambako ndiko sauti hiyo ilitokea. Ankia akaniangalia kwa njia ya kubabaika, akionekana kutaka kuniachia hasa baada ya kuutoa mkono wake kwangu, lakini mimi nikambana zaidi. Huyo aliyemwita kutokea huko nje alisikika akiwa anakuja upande wa ndani zaidi, ikiwa ni mwanamke ambaye sikumfahamu.
"Ankia mama, toka nje malaika akuone..." mwanamke huyo akasema hivyo.
Malaika gani huyo amekuja kuniharibia 'mood' tena? Nikamwonyeshea Ankia ishara ya kutoitika, nikimzuia asijibu mwito huo, lakini akajitoa kwangu kwa nguvu kiasi huku akinionyesha ishara kwa kiganja kuwa niingie chumbani.
"We' vipi? Kwani lazima umpokee?" nikamuuliza hivyo kwa sauti ya chini.
"Ni mama Ashura, mwanakikundi mwenzangu mambo ya vikoba na madeni, nilimwambia aje leo tuongee... ingia chumbani..." akasema hivyo.
Alirudi sebuleni upesi na kuzitoa nguo zake pamoja na bukta yangu baada ya kuparekebisha vizuri, kisha akakimbilia chumbani kwake kwa njia ya kunyata. Hii kitu iliniudhi sana, basi tu. Nikasikia mja akiwa amefikia mlango, naye akamwita tena Ankia huku akiugonga. Ankia akaitika, nami nikiwa bado pale pale mlangoni kwenye chumba changu nikamwona akitoka huku akiwa ameshavaa dera lingine zuri na akijifunga kilemba kichwani.
"We' naye, unakaa ndani kama umekufa vile?" mwanamke yule huko nje akasikika akisema hivyo.
Ankia akanionyesha kwa ishara ya kiganja kuwa niingie chumbani, akinisisitizia kwa uso uliojaa hisia, nami nikasikia mlango unafunguliwa. Ikanibidi tu niingie chumbani humo na kufunga mlango, huku nikiwasikia walivyoanza kuongea mambo yao ya vikoba na ujorojoro mwingi wa wanawake. Bonge moja la kata stimu maana hata mtambo wangu haukutaka kushuka chini bado, nami nikajilaza tu kitandani huku sauti za maongezi yao zikiendelea kunipa kero kwa sababu ya kukatishiwa starehe yangu. Angalau nilikuwa nimeshaanza kupiga hatua nzuri na mwanamke huyo lakini nayo ikawa imevurugwa. Hakuna hisia nzuri sana ya kupiga hatua za jambo hilo kama ile unayoipata unapolifanya kwa mara ya kwanza na mtu fulani; haiwi kama kwenye mara ya pili, na ya tatu, na ya nne. Kwa hiyo huyo mama wa vikoba kuniharibia ishu yangu ya mara ya kwanza na Ankia kuliniboa sana, maana hata kama tungekuja kuwa kivyetu tena, ingeonekana kuwa ni mara ya pili, yaani mzuka hauwi kama vile unavyokuwa kwenye mara ya kwanza!
Ila nikaona 'fresh' tu, labda nijizamishe kwenye jambo lingine ndani hapo mpaka huyo mwanamke akiondoka. Nikavuta simu yangu, kuingia intaneti, bando limeisha. Agh! Sikuwa hata na mia Tigopesa ama la sivyo ningenunua hapo hapo, hivyo ikanibidi tu ninyanyuke ili niende kuchukua vocha pale kwenye duka la nje kwenye nyumba hiyo. Bado nilikuwa na boksa na T-shirt tu, kwa hiyo nikavaa suruali nyeusi na kuchana nywele vyema, kisha nikatoka kulifata duka. Kama kawaida, niliweka uso makini na kumkuta Ankia akiwa pamoja na mwanamama huyo mweupe kiasi pia, akiwa amevaa nguo ya kitenge kama gauni. Nikamwamkia na kisha kuwapita tu, bila kumtazama Ankia hata kidogo. Ikiwa jioni ndiyo imeingia sasa, jua halikuwa kali sana na watu kadha wa kadha walionekana kupita ama kufanya mambo yao kwenye nyumba za majirani pale nje, nami nikafika dukani hapo na kusimama. Kulikuwa na mwanaume aliyesimama bila shaka kupata huduma, lakini alionekana kupata huduma ya maongezi zaidi kutoka kwa mwanamke yule niliyemwona jana usiku dukani humo, lakini wakaacha kuzungumza nilipofika.
Nikaona hiyo ndiyo nafasi ya kuomba vocha ya buku nikaperuzike, lakini hapo hapo akawa amekuja mtoto mdogo kwa kasi sana na kuomba apewe unga wa sembe, nusu. Mwanamke wa dukani alimpuuzia na kuniuliza ninataka nini, lakini nikamwambia amhudumie mtoto kwanza. Mwanamke huyo alikuwa ameweka sura makini zaidi baada ya mimi kufika hapo, na hata yule mwanaume akabaki kimya tu, na wala sikujisumbua kuwaweka akiba akilini. Nikaangalia pembeni kiufupi wakati mwanamke huyo alipokuwa anampimia dogo unga wake, nami nikaona watoto wengi kiasi, wasichana sanasana, wakiwa wanacheza mchezo wa 'rede' pamoja. Binti mmoja akavuta umakini wangu, lakini ndiyo hapa nikasikia...
"Sh'kamoo..."
Nikamtazama mtoto huyo aliyekuwa ameniamkia hivyo hapo dukani, nami nikasema, "Marahaba. Hujambo?"
"Sijambo," kakajibu, kakiwa ni kasichana.
Kalionekana kuganda kunitazama sana usoni, nami nikarudisha macho yangu kwa yule binti mwingine. Kwa watoto waliocheza pale, ni yeye pekee ndiye ambaye hakuwa "mtoto." Ilikuwa ni yule binti niliyemkuta jana kwa akina Zawadi mweupe, Mariam bila shaka, naye alicheza 'rede' pamoja na wasichana wengine kana kwamba alikuwa mtoto. Nikamwangalia kwa umakini zaidi. Alisimama usawa wa barabara pamoja na wenzake huku yeye akiwa mrushaji wa mpira ili kumponda aliye katikati, lakini jinsi alivyoitikia mambo mengi ilikuwa kwa njia... tofauti. Angerusha mpira na kuanza kurukaruka kwa shangwe hata kama hajamponda mtu, huku akipiga-piga makofi na kucheka kwa furaha sana. Uso wake ulipendeza mno alipotabasamu, sura nzuri mno kama ya dada yake mkali ikanifanya niendelee kumwangalia tu, nikijiuliza pia ni kwa nini binti mkubwa angecheza mchezo wa watoto pamoja na watoto. Dogo akawa amepatiwa unga wake, na sasa zamu ikawa yangu kuomba huduma.
"Naomba tigo ya elfu moja," nikamwambia muuzaji.
Akaanza kuchangamka kuitoa vocha, nami nikiwa navuta pesa kutoka mfukoni nikawa nimeangalia tena upande wa Mariam. Kutokea mbele zaidi kwenye barabara hiyo ya changarawe iliyoelekea pande mbili tofauti lilikuja gari jeupe aina ya Toyota Corola, taratibu tu, na wakubwa waliokuwa wameketi kwenye vibaraza vya nyumba zao wakawaambia watoto wasogee pembeni kwanza ili isije kutokea ajali. Watoto kweli wakasogea pande za pembeni, na Mariam akavutwa mkono na wenzake wawili kuja upande wa duka niliposimama mimi. Ilionekana ni kama vile hakuelewa mambo vizuri sijui, lakini ghafla gari lile likaongeza kasi na kuanza kuelekea upande huu ambao Mariam na wenzake walikuja!
Nilishtuka. Mwanaume aliyekuwa hapo dukani akasema 'nyie' kwa njia ya tahadhari, na wale wasichana wadogo wawili wakakimbia kuliepuka gari hilo lililokuwa likija kwa mwendokasi ulioongezeka. Mariam alibaki kusimama hapo huku akiliangalia kwa hofu, nami sijui niliingiwa tu na nini lakini nikaruka na kumfikia karibu zaidi binti huyo, kisha nikampamia na kuanguka naye ardhini kwa kuviringika huku gari lile likiwa limetukosa kidogo tu! Nilianguka na Mariam mpaka katikati ya barabara ile, na hilo gari likafunga breki ya ghafla kubakiza nafasi ndogo tu kuligonga lile duka. Yule mwanaume alikuwa amekimbilia upande mwingine, na nilisikia kelele za yule mwanamke wa dukani, aliyeogopa bila shaka.
Sasa nilikuwa chini, nikilala kwa juu kuufunika mwili wa binti huyu, nami nikalitazama hilo gari. Halikupitisha upenyo wa kuona kupitia kioo cha mlangoni, hivyo nisingeweza kumwona aliyekuwa ndani. Tairi la mbele likageuza kuielekea barabara, nalo likatoka hapo na kuingia barabarani; likinyoosha mbele kwa kasi mpaka kutokomea upande ule wa baa ya Masai. Watu walianza kuongezeka sehemu hiyo, kelele zikizidi, vumbi likitawala angani, nami nikamtazama Mariam chini yangu. Alikuwa analia kwa kwikwi, huku viganja vyake vikitetemeka karibu na uso wake, nami nikanyanyuka na kuanza kumsaidia anyanyuke pia. Aliogopa sana mpaka akawa hataki nimguse. Watu walipotusogelea, kila mtu alikuwa na lake la kuongea, na wanawake kadhaa wakamsaidia Mariam kusimama na kuanza kulipangusa dera lake huku wakimwambia asilie maana Mungu alisaidia ajali ile isitokee.
Nilitazama upande ule ambao lile gari lilielekea, kisha nikamwangalia huyo binti. Kama ni mimi peke yangu ndiye niliyeona kila kitu kilichotokea, basi ningekuwa mtu pekee wa kusema kwamba hiyo haikuwa ajali. Lilikuwa ni jambo lililopangwa kutokea, na mlengwa wa mpango huo usiojulikana ulitokea wapi alikuwa ni Mariam. Nilijiuliza sana ni sababu ipi ambayo ingefanya binti huyo alengwe shabaha namna hiyo, na ni nani ambaye alitaka kumgeuza awe marehemu. Alikuwa amebeba nini kikubwa msichana huyu kilichofanya mtu yeyote atake kumuua? Kwa nini Mariam?
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments