Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Ysiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA NNE

★★★★★★★★★★★★★


Mlango wa geti la nyumba aliyoishi binti huyu ukafunguliwa, na hapo wakatoka watu watatu kuja nje bila shaka kuangalia nini kilikuwa kimetokea. Ilikuwa ni Zawadi mweupe na yule mwanamke mweusi, pamoja na yule kijana niliyemwona asubuhi hiyo hapo kwao akiwa anacheza mpira. Huyo kijana akaja upesi mpaka alipokuwa amesimama Mariam, akianza kumwangalia na kumshika hapa na pale kumkagua kama aliumia, na akiuliza nini kilikuwa kimetokea. Mariam akamkumbatia kwa nguvu sana huku akilia mno, na watu walioona tukio lile, hasa yule mwanaume aliyekuwa amesimama pale dukani kabla ya ajali, wakawa wanamwelezea huyo kijana mambo yote yaliyojiri. 

Zawadi mweupe na mwenzake wakafika hapo pia wakionekana kuwa na hofu mno, huku watu wakiwaambia isingekuwa ya mimi kumsukuma binti huyo basi mabaya mengi yangekuwa yamempata. Ni muda huo huo tu ndiyo Ankia akafika hapo nje pia na yule mmama aliyekuwa naye ndani, pamoja na muuzaji wa dukani, naye akanisogelea na kunishika mkononi, akiniuliza ikiwa nilikuwa sawa. Nilitambua kwamba wengi walitaka kunisikia nikiongea kwa sababu walinitazama mno, lakini sikusema lolote maana bado mapigo ya moyo yalidunda kwa nguvu mno na nilihisi miguu ikitetemeka kiasi kutokana na nguvu kunitoka.

"Ma' mkubwa, mpeleke Mamu ndani..."

Huyo kijana aliyekumbatiwa na Mariam akamwambia hivyo Zawadi mweupe, na mwanamke huyo akamchukua binti kweli na kuanza kwenda naye huku akimbembeleza. Yule mwenzake mweusi akanisogelea huku akinitazama kwa hisia sana.

"Asante sana baba'angu. Mungu akubariki, yaani sijui bila wewe ingekuwaje jamani..." akaniambia hivyo.

"Kaka... nashukuru sana kwa kumsaidia mdogo wangu. Sina uwezo wa kukulipa, lakini naomba ujue Mungu atakubariki mara mia zaidi. Yaani... ninakushukuru sana," huyo kijana akaniambia hivyo.

Ahaa! Kumbe alikuwa kaka yake Mariam pia? Basi bila shaka huyu alimfata Miryam kiukubwa kwa ndugu hawa, nami nikamwambia, "Haina shida kaka. Hakuna malipo yoyote yanayoweza kulinganishwa na uhai wa mdogo wako, kwa hiyo usijali. Nafurahi tu yuko salama."

Hatimaye watu wakawa wamenisikia nikiongea.

"Ubarikiwe sana baba," yule mwanamke akaniambia.

"Amina," nikamwitikia.

"JC, unatoka damu..." Ankia akasema hivyo huku akiushika mkono wangu.

Kweli nilihisi maumivu ya kukwaruza kwenye mkono, lakini sasa nilipojiangalia, nikaona damu zikiwa zinavuja kutokea kwenye kiwiko. 

"Eh! Pole baba jamani... twende tuka.... Tesha si kuna dawa ndani?" huyo mwanamke akasema.

"Ndiyo, ipo. Twende bro tukapasafishe..." huyo kijana, Tesha, akaniambia hivyo.

"Hamna shida mama... nitamnawisha tu huku kwetu na kupatibu. JC, twende ndani," Ankia akaniambia hivyo.

"Ankia, tunaomba tumpe tu huo msaada angalau, maana amemsaidia sana Mariam. Tafadhali," huyo mama akasema.

Tesha akanisogelea na kunishika begani kwa njia ya msisitizo kuwa niende pamoja nao, nami nikaamua kwenda pamoja na Tesha na mama yule mpaka ndani kwao. Ankia akatufata, huku watu wengine wakitutazama mpaka tulipoishia ndani. Sikuwa nimefikiri ningeiona siku hii ikibadilika ghafla namna hiyo, na bado nilikuwa nikijiuliza maswali mengi kuhusiana na huyo Mariam. Tesha akaniongoza kufikia bombani, naye Ankia akanisaidia kuinawisha mikono yangu sehemu ilipochafuka na kuumia. Mavazi yangu yalijaa vumbi chafu sana, yakiwa na uhitaji wa kufuliwa upesi kabla uchafu haujakomalia hapo. Tukaenda varandani pale baada ya kumaliza, na yule mwanamke mweusi alikuwa ameshaleta boksi lenye pakti nyingi za pamba, bendeji, na dawa. Akanisaidia kunipaka dawa kali sana kwenye michubuko yangu na kisha kufuta-futa kwa pamba, kisha Ankia akanifunga bendeji mkononi usawa wa kiwiko na kuniwekea plasta kwenye michubuko. Nikashauri afanye mambo yote hayo kwa njia nyepesi kuruhusu vidonda vipumue. 

Baada ya hapo, nikawashukuru kwa msaada wao na kuwaambia ningekwenda kuyatoa mavazi machafu na kujisafisha sasa, nao wakakubali hilo na kunipa karibu ya mara nyingine tena kufika hapo kwao. Tesha alionekana kuwa kijana imara, mjanja, na mwenye kujiamini. Huo ulikuwa ni mtazamo wangu wa kwanza tu kumwelekea kwa kuwa singeweza kujua utu wake kihalisi, kwa hiyo tukaagana vizuri tu huku akiniambia angekuja kunicheki baadaye kuona kama hali yangu iliboreka. Nikatambua kwamba alipendezwa nami upesi sana, kwa hiyo nikaondoka pamoja na Ankia kurudi ndani kwetu.

Ankia alionekana kujali sana kilichonipata. Aliniuliza ilikuwaje-kuwaje mpaka kilichotokea kutokea, nami nikaeleza tu kwa ufupi namna mambo yalivyokuwa. Nikamwambia ningeenda tu kuoga na kisha kupumzika, nami nikafanya hivyo bila kusumbuka tena kuwaza kuhusu ile ishu yangu ya awali pamoja na mwanamke huyu. Nilianza kujali zaidi kuhusu hali ya yule mwanadada niliyemsaidia asigongwe na gari. Alikuwa na matatizo gani? Ni mimi tu ndiye niliyeona kwamba alikuwa na shida ama labda watu wote pia? Kujiingiza sana kwenye maisha ya watu wasionihusu haikuwa njia yangu ya maisha, lakini baada ya kilichotokea muda mfupi nyuma, nilitaka sana kujua. Yaani nilitaka kumwelewa Mariam. 


★★


Masaa kama matatu yakapita baada ya mimi kuwa nimeoga tena na kubadili mavazi. Yale yaliyochafuka yalifuliwa na Ankia, ambaye alikuwa amesisitiza nimpe ayafue. Huduma nyingine tena. Kwa hiyo nilikaa tu chumbani kwa kujilaza kitandani mpaka giza lilipoingia, na bado maumivu ya vidonda vya mikwaruzo mkononi niliyahisi, ingawa sikuyatilia sana maanani. Mbu kuanza kuongezeka kukafanya wazo la kwenda kutafuta hizo dawa za kuwaua lije akilini ilipofika saa mbili usiku, nami nikajinyanyua kutoka kitandani ili nikazifate. Kwa sababu fulani, Ankia hakuwa amekuja kuniangalia tokea alipozichukua nguo ili afue, na mimi nilichukulia tu kwamba alikuwa na kazi zake ama alitaka tu kuniacha nipumzike.

Nikavaa T-shirt langu la mikono mifupi, na oh... nilikuwa napendelea kuvaa maT-shirt sanasana, hivyo nilikuwa na nguo nyingi za aina hii. Kwa hiyo nikatoka hapo na kufungua mlango, na salamu ya kwanza niliyopokea ilikuwa ni harufu nzuri sana ya mboga iliyopikwa kwa viungo vilivyoifanya inukie; kwa makisio ikiwa ni nyama au samaki. Niliposimama nje chumba hicho, ningeweza kumwona Ankia akiwa upande wa jikoni, akikoroga-koroga na kisha kufunika sufuria lenye mapishi hayo. Wakati huu alikuwa amevalia T-shirt lile lile alilovaa wakati tunaenda kwa mwenyekiti, na kutokea kiunoni alijifunga khanga. Akawa ameniona, naye akaanza kuja upande wangu taratibu. Alikuwa na tembea fulani hivi ya kudunda iliyofanya kifua chake kitikisike kwa mbwembwe, nami nikasimama hapo hapo mlangoni nikimwangalia mpaka alipofika karibu na kuuegamia ukuta kwa bega lake. Kilemba kichwani kama kawaida.

"Umeamka?" akaniuliza hivyo.

"Sikusinzia, nilijilaza tu. Ulidhani nimesinzia?" nikamuuliza pia.

Akatikisa kichwa mara moja kukubali.

"Vinanukia kweli. Unaonekana unajua kupika," nikamwambia.

Akatabasamu kidogo na kusema, "Kawaida. Mwanamke anatakiwa kujua kupika."

"Hivi... samahani kuuliza..."

"Usiombe samahani, niulize tu."

"Si na chakula natakiwa kuwa nalipia kama vile maji na umeme?"

"Chakula tunashiriki wote JC. Ukitaka kula kivyako sawa, lakini mimi nikipika changu lazima na we' ule," akasema hivyo.

Kauli hiyo ikanifanya nitabasamu.

"Vipi mkono?" akaniuliza.

"Uko poa. Nataka nikachukue dawa za mbu."

"Leta nikufatie."

"Hapana, si hapa tu nje? Nafata."

"Hamna, leta bwanaa... usitoke nje tena, usije'anguka."

"Ahahah... ila wewe! Ukiunguza je?"

"Nimepunguza moto. Nipe hela nikufatie..."

"Hapana, nafata mwenyewe. Usijali," nikamwambia hivyo kwa uhakika.

Jinsi alivyotazama pembeni baada ya mimi kusema hivyo ilikuwa kwa njia ya kukwazika, naye akaniangalia tena machoni.

"Vipi, mbona hivyo?" nikamuuliza.

Akaangalia chini kiasi na kusema, "JC..."

"Nambie," nikaitika.

"Muda ule... mama Ashura alipokuwa amekuja... najua ulijisikia vibaya..." akasema hivyo kwa sauti ya chini.

Nikatazama pembeni tu. 

"Nisamehe JC... najua nilikukwaza..." akasema hivyo.

"Usiniombe samahani Ankia. Tena nafikiri ni jambo zuri huyo mama kuja hapa na kutukatisha," nikamwambia.

"Kwa nini?"

"Asingekuja, nisingetoka nje, Mariam angeumia. Nadhani ilikuwa ni Mungu tu aliongoza mambo hivyo kwa hiyo... usijali. Sijakwazika wala," nikamwambia kwa upole.

"Kweli?" akauliza.

"Ndiyo, tuko poa. Mpangaji na mwenye nyumba marafiki."

"Mhm... kumbe marafiki?"

"Eee... ama we' siyo rafiki?"

"Ni kweli. Sisi marafiki."

"Aina hiyo," nikamwambia hivyo bila kuacha kumtazama.

Akatabasamu kwa haya kiasi na kuangalia chini.

"Halafu hivi... huyo Mariam... ana tatizo la kiakili au?" nikamuuliza hivyo.

Akaniangalia na kusema, "Ndiyo, hata mimi nadhani hivyo. Kuna mambo mengi kwenye hiyo familia kwa hiyo... sijui sana."

"Umemjua tokea muda?"

"Eeeh... tuko hapa muda. Huyo msichana hakuwaga hivyo unajua? Alianza tu... kuchizika ghafla."

"Kuchizikaje?"

"Sijui sana, ila watu huwa wanasema alirogwa eti," akaniambia hivyo.

Nilibaki kimya tu nikimtazama kwa umakini.

"Mambo tu yalianza kumwendea vibaya wazazi wao walipofariki kwenye ajali kwa pamoja. Dada yake ameshajaribu kumtafutia matibabu lakini inasemekana hospitali huko wamemwambia huyo binti ni wa kupeleka wodi za vichaa... lakini yeye Miryam anasisitiza kwamba mdogo wake siyo kichaa. Hataki kumwacha huko. Ndiyo kama unavyomwona..." Ankia akaeleza.

"Sidhani sana kama neno 'kichaa' linamfaa huyo msichana. Asingeweza kucheza na watoto kama vile alivyokuwa anacheza nao leo ikiwa angekuwa haelewi mambo vizuri," nikamwambia.

"Ndiyo kama hivyo sasa, we' hebu fikiria amezaliwa normal tu halafu akageuka kuwa haelewi-elewi vitu. Watu wanaisomaje hiyo? Hata kwa Mwamposa wameenda lakini wapi... hamna lolote huko," Ankia akasema.

"Mh? Kumbe ni wakristo?"

"Ulifikiri ni waislamu?"

"Ndiyo."

"Hamna, siyo. Ila hata waislamu mbona wanaendaga kwa huyo jamaa? Wanasema kikubwa imani lakini kwa wengi wanachoenda kuambulia ni kukombwa tu hela... sadaka," Ankia akasema hivyo.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Si ndiyo imani yenyewe sasa?"

"Mh... sidhani sana..."

"Ankia, siku hizi imani bila pesa, imekufa," nikamwambia.

Akacheka na kuniambia, "Unabadili kauli za biblia ziendane na mambo ya siku hizi, eh?"

"Me ndiyo nahisi hivyo. Kwa hiyo... wazazi wao walikufa kwenye ajali ya gari au?" nikamuuliza hivyo.

"Eee, yaligongana siku wametoka safari ya wapi sijui. Mabasi. Ndiyo ikawa hivyo. Lakini unajua nini, kwa shida kama alizonazo huyo Mariam ni ku...."

"Hodii..."

Sauti yenye kusema neno hilo ikamkatisha Ankia kwa kile alichotaka kuniambia, nasi tukatazama upande wa sebuleni. Ilikuwa sauti ya kiume, na sote tulifahamu mmiliki wake.

Ankia akasema, "Karibu..." kisha akaniangalia na kuniambia, "Tesha huyo."

Nikatikisa kichwa kukubali hilo, naye akaelekea mlangoni ili amfungulie jamaa.

Bila shaka kuja kwake Tesha kulikuwa kwa kusudi la kutimiza ahadi yake aliyonipa ya kuja kuniona, nami nikasogea mpaka hapo sebuleni nikimtazama Ankia alipomfungulia mlango na kuanza kusemeshana naye kiutani. Walionekana kuwa na uhusiano mzuri wa kaka na dada pia, naye Tesha akaingia ndani humo na kuniona. Alivalia T-shirt pana la mikono mifupi, pamoja na suruali ya jeans. Na alinukia vizuri pia. Mwonekano wake ulitoa taarifa ya haraka kwamba alipenda kupendeza na kuonekana msafi, na hilo lilikuwa jambo nililopenda pia. 

"Ah, kaka vipi?" akanisalimu kirafiki.

"Fresh tu, karibu," nikaitikia salamu yake. 

Tukagonga tano kwa ngumi zetu, kisha akakaa kwenye sofa moja, vilevile na mimi pia la pembeni.

"Unakunywa soda gani we' mbwa?" Ankia akamuuliza hivyo Tesha.

Nikacheka kidogo kwa pumzi.

"Asa' soda ya nini, mi' mgeni hapa? Ushaniita mbwa, unajua ni nyama tu ndo' natumia," Tesha akamwambia hivyo.

"Na mifupa tu," Ankia akamwambia.

"Hahahah... aloo... hiyo ishu ya saa zile imekuwa mkosi kitaa hiki, kila kona nasikia unaongelewa mchina tu..." Tesha akaniambia hivyo, nasi kwa pamoja tukacheka.

"Kwa mazuri lazima mchina wetu aanze kusifika," Ankia akasema hivyo, akiwa amekaa kwenye mkono wa sofa karibu na mimi.

"Hahah... me nafanana vipi na mchina bwana?" nikasema hivyo kiutani.

"Ah, si washamba wa huku tu kaka? Me mwenyewe naitwaga mpaka msudani eti kisa ngozi tu hii..." Tesha akaniambia.

"Sasa ndiyo kila mtu hapa atataka mazoea. JC hakuna kwenda nje," Ankia akasema.

"Aa wee... nisiende nje? Natoka nikitaka, na hakuna mtu ananisogelea. Sipendi shobo zisizo na maana..." nikasema hivyo.

"Wewe uko kama mimi bro, nawapaga gongo hili wanaoshoboka sana bila maana, yaani mtindo mmoja," Tesha akasema hivyo.

"Basi unajichetuaa..." Ankia akamwambia hivyo.

"Fact hiyo. We' mwenyewe unajua sisi tukoje, tunawapenda watu wakitupenda...."

"Na tunawatenda tusiowapenda," nikamalizia maneno yake Tesha.

Akacheka kwa nguvu sana na kusema, "Aminia, aminia," huku akigongesha kiganja chake kwenye ngumi yangu niliyomkunjia aipige. Alionekana kuwa mjanja kweli na mwongeaji, hivyo nilijua kabisa angekuwa mwepesi kuzoeleka.

"Haya bwana, mapacha mmekutana. JC, leta nikafate basi," Ankia akasema hivyo, akimaanisha nimpe hela afate dawa za mbu.

Nikampatia elfu moja.

"Zote?" akaniuliza hivyo.

Nikatikisa kichwa kukubali, naye akaenda upande wa jikoni kwanza kuiangalia mboga bila shaka. Nilipomtazama Tesha, alinifanyia ishara kwa mdomo wake kunionyeshea mwanamke huyo alipokuwa ameondoka, nasi kwa pamoja tukacheka kidogo bila kutoa sauti.

"Vipi, mdogo wako anaendelea vizuri?" nikamuuliza.

"Eh, yuko poa, yuko poa. Kichwa kilikuwa kinamsumbua kidogo, ila ameshusha dawa akalala. Akiamka atakuwa fresh zaidi," akasema.

"Miryam amerudi?" sauti ya Ankia ikauliza hivyo kutokea jikoni.

"Bado. Ma' mkubwa kamwambia kuhusu hiyo ajali akasema atajitahidi kuwahi. Unaelewa anavyojua ku-panick," Tesha akaongea kwa sauti ya juu kiasi.

"Hata me ninge-panick, we! Ajali siyo mchezo," Ankia akasema hivyo.

"Kwa hiyo... hawa walio hapo kwenu ni, mama zako?" nikamuuliza Tesha.

"Yah, mama wakubwa. Huyo aliyekupaka dawa saa zile ni mdogo wake na aliyemzaa mshua wetu... na huyo white ni dada yake na mama yetu. Ila... sisi wazazi wetu walishafariki," Tesha akaeleza.

"Aaa... sawa. We' unapiga mishe gani huku?" nikabadili mada upesi.

"Ah, nipo tu bro. Ajira kama unavyojua, ngumu kinoma kupata. Nimepiga-piga mishe kule Arusha miaka ya nyuma ila nilipofika huku, haba! Miezi inapita, lakini nitapata tu pa kuegamia," akaeleza.

"Ungemwomba sister akuunganishe sehemu," Ankia akasema hivyo akiwa anarudi sebuleni sasa.

"Ameshajaribu, ila michongo ya siku hizi haisimami fresh. Anataka nitulie mpaka apate panaponifaa," Tesha akasema.

"Na anavyowadekezaga sasa!" Ankia akasema hivyo na kutupita mpaka kuufikia mlango.

"Hiyo lazima, kupendwa kunaanzia nyumbani, we' vipi?" Tesha akamwambia hivyo kiutani.

"Halafu kunaishia wapi?" Ankia akamuuliza hivyo huku akifungua mlango.

"Masai," Tesha akamjibu.

Nikacheka kidogo, naye Ankia akakisukuma kichwa cha Tesha kwa kidole chake na kisha kutoka nje huku jamaa akimsindikiza kwa macho.

"Wali nazi..." Tesha akaniambia hivyo huku akinionyeshea ishara ya nyusi kuelekea upande wa Ankia.

"Usipime," nikasema hivyo.

"Ushaharibu mitambo mtu wangu?"

"Hahah... hamna, sijafika huko..."

"Uko nalo alone hapa, kamata tu."

"Napendaga kufanya vitu kwa mikakati," nikamwambia.

"Hahahah... liko vizuri, usichelewe sasa," akaniambia hivyo.

"Vipi, ushaangukia nini?" 

"We! Natamanigi tu, kuguswa halitaki eti. Aidha linaogopa ngoma ama mashauzi tu. Ila kwa wewe nafikiri litalegea."

"Kwani me nina nini?"

"Ah, HB. Halafu na vile umepiga action kama stelingi wa kihindi leo, nani asikutake?"

Nikacheka kidogo na kutikisa kichwa kwa kufurahishwa na utani wake.

"Una maumivu makali bado?" akaniuliza.

"Hamna, ni huu mkono kidogo tu unakwangua ila niko poa," nikasema.

"Sawa. Kama vipi... twende hapo Masai tukazimue kidogo, ama nini?" 

"Hapo bar?"

"Ee. Ama bia hupigi?"

"Nakunywa."

"Yah, twende tu mtu wangu tupige mbili tatu, urudi ulale umechangamka," akasema hivyo.

"Na huyu?" nikamuuliza hivyo, nikimaanisha Ankia.

"Tunaenda naye. Anapenda bia huyo!"

"Kumbe?"

"Wee! Sema humtoi humu ndani kama huendi kumnunulia za maana, ila kwa wewe HB hata kwa moja tu atakubali kutoka," Tesha akaongea kiutani.

"Ahahah... acha kufanya hivyo bana..." nikamwambia.

Akacheka kwa nguvu, nasi tukagongesha tano kirafiki tena.

"Vipi, mnanisema au?" 

Ankia akawa ameuliza hivyo baada ya kurudi muda huo huo. Mkononi alishika kifuko kigumu chenye kuonyesha dawa ndefu za kuchoma za mbu, na sisi wote tukamwangalia. 

"Ee, sugar mommy wetu we' ndo' mada kuu hapa. Tulikuwa tunafanya revision kidogo," Tesha akamwambia hivyo.

Ankia akasonya kiutani na kufunga mlango, naye akaanza kuja upande niliokaa mimi huku akisema, "Eti sugar mommy. Kuna sugar mommy hapa?"

"Si ndiyo wewe?" nikamwambia hivyo.

"Kwa ushuga upi? Nina miaka 32 tu mie msinizeeshe namna hiyo," Ankia akasema hivyo na kukaa pembeni yangu.

"Kwani mashuga mommy huwa wanaanzia miaka mingapi?" Tesha akamuuliza.

"32," nikampa jibu, naye Tesha akacheka.

Ankia akanikata jicho la kuudhika eti, nami nikatabasamu tu.

"Twend'zetu Masai," Tesha akamwambia.

"Kufanyaje? Me napika sa'hivi," Ankia akasema.

"Acha kupika wewe, utapika baadaye. Twende tukanywe pombe!" Tesha akaongea kwa msisitizo.

Nikacheka kidogo.

"Akili yako yote iko hapo tu. Me siwezi kwenda, nenda mwenyewe," Ankia akasema hivyo.

"Unazingua. Basi baki mwenyewe, me naenda na JayZee..." Tesha akamwambia hivyo.

Nikacheka sana pamoja na Ankia, na mwanamke huyu akamwambia Tesha, "Siyo JayZee, ni JC."

"Aaaa dah, nimechapia," Tesha akakiri.

"Mwishowe atakuita Chelsea," Ankia akaniambia.

"Wewe baki kupika, si unataka kupika? Sisi twende JC," Tesha akaniambia.

"Mh? Huna lolote. Eti kweli unaenda?" Ankia akaniuliza.

Nikamtikisia kichwa mara moja kukubali.

"Sasa je! Kwa hiyo?" Tesha akamuuliza hivyo Ankia.

Mwanamke huyu akaibana midomo yake kama kuonyesha anatafakari, huku sisi tukimwangalia, naye akasema, "Basi, ngoja nika-change nguo... halafu twende."

"Hahaaa... umeona? Si nilikwambia?" Tesha akasema hivyo kwa shauku.

Nikasimama huku nikicheka pia, naye Ankia akasimama pia.

"Amekwambia nini?" Ankia akaniuliza.

"Hajaniambia kitu, nenda kavae. Na mimi ngoja nikabadili gwanda," nikasema hivyo na kuanza kuelekea upande wa chumba.

Hali ya urafiki niliyokuwa nimeanza kujenga pamoja na wawili hawa ilinichangamsha sana. Nikaingia chumbani na kubadili mavazi; nikivaa T-shirt zito kiasi mithili ya sweta laini, pamoja na suruali nyeusi ya jeans. Nikachana nywele vyema, nikajiweka sawa kabisa mwilini na kujipulizia manukato, kisha nikarejea pale sebuleni. Tesha akasifia mwonekano wangu na kutania kwamba ningeenda kuua macho ya wengi pale Masai, nami nikakaa sofani kumsubiri Ankia. Dakika si nyingi sana mwanamke huyo akawa ametoka, akiwa amevaa gauni fupi jeupe lenye urembo wa maua-maua na lenye kuvutika lililoyaonyesha mapaja yake kiasi. Nilimtazama kwa umakini maana mwonekano huo ulimwelekezea sana fikira. Nguo hiyo yenye kuubana mwili wake ilikuwa na mikono mirefu, iliyoficha hadi shingo lakini ikiacha uwazi wa duara kifuani kwake kuonyesha mstari ulioyatenganisha uzuri wa kifua chake. Usoni alipendeza pia kwa kujiremba kiasi, huku nywele zake za kusukwa mtindo wa rasta fupi akiwa ameziachia tu pande za masikio yake. 

Alikuwa akiniangalia kwa njia iliyoonyesha alitaka kuona ningesemaje kuhusu mwonekano wake, nami nikamwambia amependeza sana. Tesha kama kawaida akawa anamsifia kwa utani mwingi, naye Ankia akasema mboga ilikuwa imeshaiva na alikuwa amebakiza kupika ugali, kwa hiyo angepika muda ambao tungerudi. Haikuwa na neno. Tesha alionekana kutaka sana kwenda kutubariki kwa vinywaji, bila shaka aonekane na rafiki mpya, na kwa hilo mimi pia nilikuwa tayari ili hiyo Masai na yenyewe niijue. Tukatoka baada ya Ankia kuzichoma dawa kwenye vyumba vyetu na milango kufungwa, nasi tukaanza kutembea kuelekea huko Masai. 


★★


Nilimuuliza Tesha ikiwa dada yake alikuwa na kawaida ya kuingia nyumbani usiku, naye akasema mara kwa mara alirudi usiku mpaka kufikia saa nne kabisa ikiwa kazi zilimhitaji zaidi, lakini kama sivyo basi angerudi mapema tu, ama hata siku zingine kutokwenda huko kazini kwake kabisa. Bado nilitaka kujua mambo mengi kuhusu mdogo wake, Mariam, na hizi hatua za mwanzo za urafiki baina yangu na Tesha huenda zingesaidia niweze kujiingiza zaidi kwenye ishu ya kuielewa vizuri hali ya yule binti.

Tukawa tumeifikia Masai. Kwa saa mbili hii joto bado lilikuwa halijapanda sana ndani humo, lakini tulipoingia tu kweli macho ya wengi yakawa kwetu; hasa mimi. Na mimi kama kawaida nilikuwa nimeweka mwonekano makini usoni, nikitembea nyuma yake Tesha huku Ankia akiwa karibu nami. Tesha alisalimiana kwa ufupi pamoja na watu aliofahamiana nao mpaka tulipofikia meza ndefu iliyotengenezwa kwa mbao nene, ikiwa imezungukwa na viti virefu vya plastiki ngumu vya kukalia, nasi tukaketi hapo. Hatukuwa tumeingia ndani sana kwenye sehemu hii, kwa hiyo Tesha akawa ananiambia ni wapi kulikuwa na vyoo na kumbi maalumu ya maVIP, pamoja na vyumba vya kulala wageni. 

Mhudumu mwanamke akaja na kutuuliza vinywaji gani tungependa kutumia. Tesha akatuambia tuagize, naye Ankia akasema aletewe bia tamu ya Savannah, nami nikaomba niletewe Serengeti Lite ya moto. Tesha angekunywa Serengeti Lager, naye akamwambia mhudumu atuletee sisi wanaume tatu tatu na Ankia aletewe Savannah mbili maana ni katamu ila kakali. Inaonekana Tesha alifahamika sana hapa kwa hiyo mhudumu akaondoka tu bila kuchukua pesa, ikimaanisha malipo yangekuja baadaye, hivyo tukaendelea kusubiri huku tunapiga 'story.' Muziki uliochezwa ulisikika kwa sauti nzito kwenye spika za sehemu hiyo, na TV za 'flat screen' zilizokuwa zimetundikwa juu sehemu kadha wa kadha kwenye kumbi hiyo. Kukawa na watu wachache ambao walifahamiana na Tesha pamoja na Ankia waliokuja mezani hapo kutoa salamu, nao wakawa wanatambulishwa kwangu. Ni salamu na kucheka kidogo tu ndiyo yaliyokuwa maitikio niliyowapa, na
sikuelekeza fikira kwa mwanamke yeyote hapo ingawa wengi walinitazama kwa macho ya uvutio. Bia zikaletwa, nasi tukaanza kunywa taratibu. 

Nilikuwa najitahidi kusoma mazingira ya hapo ili nipazoee upesi. Nadhani labda ni shauri ya muda kutokwenda sana ndiyo sababu hapakuwa pamechangamka kivile, ama labda kwa sababu haikuwa wikiendi, kwa vyovyote tu ila palikuwa kawaida sana. Ndipo akaja mwanamke fulani mweusi kiasi mpaka kufikia mezani hapo. Alifahamiana na Tesha na Ankia, naye akasalimiana nao kwa kuwakumbatia na kuanza kuzungumza kwa shauku. Alikuwa mzuri. Mwili wake haukuwa mnene, urefu wa kadiri, na alionekana kuwa mwongeaji sana. Alisuka nywele ndefu laini na kuzibana nyuma ya kichwa chake, akiwa amevalia nguo ndefu kama kijora iliyochoresha umbo lake vizuri kwa jinsi alivyoivuta kwa mbele, na alikuwa na macho mazuri madogo. Aliitwa Joy. 

Akatambulishwa kwangu, nami nikampa salamu huku nikimwangalia kwa upendezi. Nadhani njia yangu ya kutazama mwanamke kila naposema nimemwangalia kwa upendezi sikuzote ilikuwa inatoa ujumbe fulani wenye kuamsha hisia nzuri kwake, na huyo Joy alinitazama kwa macho yaliyonipa ujumbe wa "tukutane chumbani." Nikacheka kidogo tu, naye Tesha akacheka pia kwa sababu alinielewa sana inaonekana, hivyo akaanza kumsukumia Joy upande wangu eti akae na mimi. Joy alikuwa amefika na marafiki zake hapo ambao walienda kukaa kwenye meza nyingine kabla hajaja upande wetu kutusalimia, kwa hiyo akawa akisema anahitaji kwenda huko. Lakini Tesha akamsisitizia akae na sisi, akiniambia nimshawishi pia, nami nikaushika mkono wa huyo Joy na kuuvutia kwangu taratibu. Aliniangalia huku akitabasamu, naye akaja polepole kama vile amepumbazika. Nadhani jambo hilo lilimfanya Ankia ajihisi vibaya kiasi, lakini akajikaza tu na kuendelea kuweka utulivu huku akinywa. 

Nikamwambia Joy akae kiti kilichokuwa pembeni yangu, naye akakubali na kuketi. Tesha akamwagizia bia mbili pia, nasi tukaendelea kunywa taratibu huku Tesha akiongea na Joy sanasana. Nilipomwangalia Ankia, alikuwa ametulia tu akicheza muziki taratibu kwa kupeleka kichwa huku na huko bila kuniangalia, nami nikalishika paja lake kwa chini. Akanitazama, na jinsi nilivyomtazama kwa macho yangu ya uchokozi kukamfanya ashindwe kujizuia kutabasamu kwa haya, na hapo nikawa nimefanikiwa kumtuliza.

"Oy, sister huyo..." Tesha akaniambia hivyo huku akitazama upande wa nje kabisa.

Nikageuka na kuliona lile gari la Miryam likipita kuuelekea upande tuliotokea kule nyumbani, kumaanisha dada mtu ndiyo alikuwa anarudi.

Nikamwangalia Tesha tena, naye akasema, "Yaani sasa hivi ndiyo amewahi."

Alihitaji kuongea kwa sauti ya juu ili nimsikie, nami nikatabasamu kidogo.

"Dada'ako hatakuchapa ukienda home unanuka pombe kweli?" Ankia akamuuliza.

"Acha zako wewe, nani achapwe?" Tesha akamuuliza.

"Tena zile mboko za kuzunguka!" Joy akasema hivyo, nasi wote tukacheka.

"Sister hamaindi kabisa, sisi ndo' mayai yake bana," Tesha akajisifia.

"Unavimbaga kweli kisa dada'ako anawapendaa. Siku akiolewa sijui nawe utaolewa naye?" Joy akamwambia hivyo.

Ankia akacheka na kusema, "Lilivyo hili, litaenda naye kabisa ili malezi likayapate na huko ukweni."

"Aaa mnanichoresha vibaya, au mnadhani sijui kama sitakaa na sister tu maisha yote?" Tesha akasema.

"Kumbe unalijua?" Joy akamwambia.

Tesha akanywa bia na kuvimbisha mashavu kwa njia ya masihara, nasi tukacheka kidogo.

"Ila dada yako Tesha hataki kuolewa kabisa, eti? Ama hapendi tu wanaume?" Ankia akamuuliza.

"Eeh Tesha, nasikiaga wanakujaga hadi kumtolea posa ila anawatimua," Joy akamwambia.

"Siyo hivyo. Mambo magumu tu sa'hivi, sister anatutunza kwanza. Kama kuolewa ataolewa tu baadaye. Jana kuna bwege mwingine alikuja, na yeye akabebeshwa virago alivyovileta. Hapana cheza na Mimi!" Tesha akasema.

"Wewe ndiyo ulimfukuza?" nikamuuliza.

"Hamna, sister..." Tesha akajibu.

"Huwa wanamwita Mimi," Ankia akanijulisha.

"Ooh..." nikasema hivyo kwa uelewa sasa. 

Na hiyo ingefanya mambo yawe rahisi hata kwangu pia, kumwita Mariam Mamu, na dada yake, Miryam, kumwita Mimi.

"Unatiaga michumvi wewe! Eti akamfukuza. Alivyo mstaarabu dada'ako najua alimwambia tu, 'pole... nimeshawahiwa,'" Joy akasema hivyo.

Tukacheka kidogo mimi na Ankia. 

"Halafu bro, waliniambia ulifika kwanza wewe... sijui ulipotea eti..." Tesha akaniambia.

"Ee bana, nilikuwa naitafuta nyumba ya Ankia kwa kutumia map. Sasa kidoti chekundu kikanileta kwenu, siunajua zimekaribiana sana..." nikamwambia.

"Eee, dah! Ma' mkubwa ndiyo aliniambia, nawe ukajikuta unachangamkiwa kuwa mchumba..." Tesha akasema.

Tukacheka sana kwa pamoja.

"Kweli? Walifikiri ni yeye?" Joy akauliza.

"Ee..." Tesha akajibu.

"Hahah... mbona hukuniambia?" Ankia akaniuliza.

"Nilisahau tu," nikamwambia hivyo.

"Asa' si unaona, matatizo tu. Yote hayo kumfosi sister aolewe. Yaani wanawake na ndoa bana!" Tesha akaniambia hivyo.

"Ndoa sifa kwa mwanamke, hujui hilo baba, basi umeachwa..." Joy akamwambia.

"We' ya kwako iko wapi?" Tesha akamuuliza.

"Si nakusubiri wewe?" Joy akamwambia.

"Sawa, utasubiri sana," Tesha akasema hivyo, naye Joy akacheka.

Tukaendelea kunywa na kupiga 'story,' mpaka inaingia saa nne hivi, tulipokuwa mwishoni kumalizia vileo vyetu, bia zingine zikaongezeka mezani hapo. Tesha hakuwa ameagiza zingine, hivyo akauliza zimetokea wapi. Mhudumu akamwambia kwamba kuna mtu alikuwa amenunua kwa ajili yangu mimi, kwa hiyo tayari zilikuwa zimeshalipiwa na sisi tungetakiwa kunywa tu. Bia kiujumla zilikuwa 20. Tesha akamwambia mhudumu asepe, akisema inaonekana kuna sugar mommy hapo ndiye aliyekuwa amezituma hizo ili kuanza kunichokonoa, na bila shaka masaa ya kukaa hapo yangeongezeka mpaka suala la Ankia kupika ugali nyumbani lingesahaulika kabisa. Tukaendelea kunywa taratibu tu, huku mzuka wa hapo Masai ukizidi kupanda kadiri dakika zilivyoendelea kutembea.


★★


Mpaka kufikia saa sita bado tulikuwa hapo, na hata kabla ya kumaliza bia tulizoongezewa, zikaletwa zingine 20. Inaonekana huyo mtu alikuwa amenipenda ama kunitaka, lakini bado hakujitambulisha kwangu, na mimi sikujisumbua kumtafuta. Kuna watu waliokuwa wanakuja kuomba bia, nasi tukawa tunawapa, na mzuka ukazidi kuongezeka. Watu walicheza, waliimba, na sisi tukaendelea kunywa na kupiga story za kufurahisha hadi saa nane kufika. Niliufurahia muda huu kwa kweli. Siku ya pili tu ugenini tayari nikajihisi kuwa mwenyeji. Nilikuwa nimekunywa bia saba zilizofanya macho yangu yawe mazito kiasi. Wenzangu walishusha pombe kumi na bado walikuwa wanaendelea, kwa hiyo mimi mtegeaji nikawa macho zaidi yao. Ankia angenilalia begani na kuongea mambo mengi sana, na mimi niliendelea kutulia tu. Joy alianza kupitisha kiganja chake kwenye paja langu, akilipapasa na kulifinya mara kwa mara. 

Nilipoona uzito wa pombe unamlemea Tesha, nikasimama na kwenda kumtoa kwenye kiti, nikimwambia tuelekee nyumbani kwa kuwa tayari bia zetu za mwanzo alizoagiza alikuwa ameshalipia. Nikamwambia na Ankia tuondoke, naye akatii na kusimama huku akiyumba. Joy alikuwa amelewa pia lakini siyo ile ya kumyumbisha, akionekana kuwa mzoefu zaidi wa pombe, naye akatufata pia tulipotoka sehemu hiyo kwa pamoja. Tesha hakuweza kutembea vizuri, akiyumba huku na huko na akiongea sana, nami nikamsindikiza mpaka getini kwao, nikiwaacha Ankia na Joy wanaenda kule ndani kwetu. Usiku wa saa nane huo. Tesha alikuwa anasema ana kama wiki hajanywa pombe ila furaha niliyompa leo kwa sababu ya kumwokoa mdogo wake ilimfanya ajiachie namna hii, nami nikawa namwangalia tu kwa kujali kiasi. Alionekana kuwa mtu mwenye huzuni iliyofichwa, na sikujua tu ni kwa nini niliwaza hivyo. 

Geti likawa limefunguliwa, na aliyefungua hakuwa mwingine ila bibie Miryam. Alikuwa na mwonekano wa mtu aliyetoka usingizini, lakini si ule mzito mno. Alitutazama kwa umakini. Nilihisi labda angekuwa mkali kwa Tesha kutokana na kurudi usiku akiwa amelewa, lakini haikuwa hivyo. Akaacha uwazi ili kuturuhusu kuingia, naye Tesha akatangulia huku nikiwa nimemshika mkono kuhakikisha hajigongi getini.

"Mimi... ulikuwa umeshalala? Ungekuja nawe tukapiga bia kidogo," Tesha akamsemesha hivyo.

"Kulewa ndiyo bia kidogo? Em' ingia ndani," Miryam akamwambia kwa sauti tulivu.

Tesha akiwa ananesanesa, macho mazito mno, akaniangalia na kusema, "Umemwona? Huyu ndiyo mkurugenzi hapa. Chochote anachosema tunafata. Nampenda mno... naweza nikaua kwa ajili yake."

Tesha aliyasema maneno hayo kilevi, lakini yalibeba uzito nilioelewa kuwa ulitoka ndani ya moyo wake. Nikamwangalia Miryam usoni, naye akamshika mdogo wake mkononi ili amwongoze kwenda ndani. Lakini Tesha akaweka mgomo kiasi na kuingiza kiganja chake mfukoni, kisha akaitoa simu yake na kuiwasha, halafu akanipatia.

"Andika namba bro... nakukubali sana," akaniambia hivyo na macho yake kama yanataka kudondoka.

"Atakupa hata kesho," Miryam akamwambia.

"Ee kaka, nitakugei kesho," mimi pia nikamwambia.

"Hamna... andika bana, kwani saa ngapi? Mwishowe kuku awike. Andika hapo..." Tesha akasisitiza.

Nilihisi hali yote ya hapo ilimletea picha mbaya sana dada yake, lakini nikaichukua tu simu yake na kuandika namba upesi. Nikamrudishia, naye akaninyooshea kidole chake kwa kurudia-rudia kuonyesha jinsi alivyonielewa, halafu akaanza kuelekea huko ndani. Miryam akanitazama usoni, kasura kake ka kuvimba kakiwa na mwonekano wa kitoto shauri ya kutoka kulala. Sikujua alikuwa amepanga kunirushia maneno gani wakati huu, lakini nilikuwa nimeshalewa pia kwa hiyo nisingeyajali sana. Hapa kilichokuwepo ilikuwa kuondoka tu maana mdogo wake nilimrudisha kwao salama.

"Angalia asiangukie meza huyo..."

Nikamwambia hivyo kwa sauti tulivu tu. Alinitazama machoni kwa njia fulani yenye kujali, na nilikuwa sijalitambua hilo hata kidogo mpaka aliponisogelea karibu zaidi na kisha kunikumbatia taratibu!


★★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★★

Previoua Next