Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

INVISIBLE

A Story by Elton Tonny

Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Unyanyasaji, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA SITA

★★★★★★★★★★★★


Yule jamaa aliyeketi nyuma akaangalia huku nilipokuwepo na kunyanyuka kidogo kuchungulia, mimi nikiwa namtazama akiangalia-angalia sehemu ile niliyojilaza, kisha akageuka mbele tena.

"Hamna kitu hapo wewe. Em' endesha gari bana... ungetudondosha ningekuua," akamwambia.

"Oya niko serious aisee... nimeona kichwa cha mtu hapo nyuma yako." 

"Nimekwambia hakuna mtu huku! Nimeangalia mwenyewe."

"A-aaa... sikia. Nilikuwa naangalia kioo hapa juu na nikaona kichwa kingine ambacho hakikuwa chako... huko nyuma. Sikutanii!"

"Ish... hivi we' vipi? Oya dogo, em' mwazimishe huyu miwani yako maana macho yake yameanza kuwa na matege! Yaani unang'ang'ania umeona mtu wakati hamna mtu, hivi unajua unatuchelewesha? Acha ubwege, endesha bana," akasema jamaa kwa ukali kidogo.

Nilihisi gari likianza kutembea tena na hiyo ikanifanya nitulie. Lakini nilijiuliza vitu viwili. Kwanza, dereva aliwezaje kuniona na pili, kwa nini mwenzake hakuweza kuniona. Nikakumbuka kuwa alisema alipotazama kioo cha juu, aliona kama kichwa cha mtu. Jambo hili likanifanya nigundue kwamba nisingeweza kuonekana kikawaida, lakini kama mtu angeweka kioo mbele yangu, basi ningeonekana. Kwa akili ya haraka, nikajitahidi kuifikia simu yangu mfukoni na kuitoa, kisha kuitolea sauti, iwe kwenye 'do not disturb mode' endapo mnyabi fulani angepiga bila kujua niko kwenye hali ipi.

Sasa mambo mengi yalikuwa yakiongezeka ndani ya akili yangu ambayo yalinichanganya. Sikujua huu uwezo wa kutoonekana chanzo chake kihalisi ilikuwa nini. Sikujua gari hili lilitupeleka wapi na kwa nini nilijiingiza kwenye hali hiyo iliyoanza kuwa ngumu sasa. Nikaanza kujiona nina kiherehere tu, bora ningebaki kule na kuendelea kumfukuzia mtoto mzuri badala ya kufata mambo yasiyonihusu.

★★

Niliendelea kujilaza pale nyuma kwa dakika kama ishirini hivi na hatimaye, gari ikasimama. Toka tulipoondoka pale shuleni, sikumsikia mvulana yule akisema neno hata moja. Wale jamaa wangeongea mara kwa mara, huku jamaa wa nyuma akimtania mara nyingi dereva yule kuhusiana na tukio la muda mfupi uliopita. 

"Wiyaa homuuu." 

Akasema jamaa wa nyuma kwa kejeli kisha kuanza kucheka kwa dharau. Nikajua alikuwa akimwambia William. Sauti ya geti likifunguliwa ilisikika, na gari likaanza tena kutembea. Lilisimama tena na kuzima, hapa nikajua tumefika tulipotakiwa kufika.

Baada ya kusikia milango ya gari ikibamizwa, nilinyanyua kichwa na kukuta wote wameshuka. Nilipotazama vizuri mbele, nikaona uwazi mkubwa wenye kiwanja chenye ukoka mfupi, na kwa mbele, swimming pool. Nikajinyanyua vizuri zaidi na kusogea mbele ya gari, na hapa nikaona vizuri hata zaidi sehemu ile. Ilikuwa na jengo kubwa lenye ghorofa mbili ndefu lenye rangi nyeupe, na lilikuwa pana sana. Upande wa kushoto ilikuwa sehemu ya kuegeshea magari na upande wa kulia bustani nzuri yenye miti na maua mengi yaliyotunzwa vizuri.

Nikawaona wanaume wale wakipanda ngazi pamoja na William za kuzungukia jengo kwa nje kuelekea juu, lakini sasa wakiwa watatu, na hilo likaniambia kuwa huyo mwingine huenda ndiye aliyetufungulia geti wakati tukiingia. Sikujua nyumba hiyo ilikuwa ya nani, lakini bila shaka walioishi pale walikuwa watu wenye pesa sana. 

Nilijua nilipaswa kwenda ndani mule ili kujua kilichoendelea hasa. Wazo lililokuwa akilini ni kwamba wale watu walikuwa majambazi na huenda walikuwa wameiteka familia ya matajiri ili kupata pesa. Na hawakuwa majambazi wa ovyo ovyo kwa kuwa walionekana wana umakini sana. Nilipotaka kushuka kutoka kwenye gari, nilijiona kwenye kioo kile cha mbele, na hilo likanikumbusha kuwa nilihitaji kuwa makini nisipite au kukaa sehemu zenye vioo ili nisije kuonwa.

Baada ya kushuka, nilianza kukimbia taratibu kwa njia ya kunyata na kuelekea mpaka mlango wa mbele. Nilipoukaribia, nikasimama kwa kuwa nilikuta mwanaume mwingine mwenye mwili mkubwa akiwa ameketi kwenye kiti huku anavuta sigara. Kwa vyovyote ingekuwa ngumu kuufungua mlango mbele yake, lakini hata hivyo... hangeniona. 

Nikafikiria haraka cha kufanya, kisha nikasogea karibu na usawa wa maua, nikitafuta jiwe. Uzuri nilipata jiwe dogo dogo, nikalirusha na kuponda miimo ya milango kwa juu. Alishtuka na kuanza kuangalia huku na kule, kisha akanyanyuka na kuanza kuelekea upande jiwe lilipotokea, akinipita hapo hapo bila kuniona. Nilisanuka upesi na kuwahi mlango, nikafungua kitasa na kuingia ndani kisha kuufunga taratibu. Nikatazama ndani pale na kiukweli palikuwa pazuri sana. Palipangiliwa kwa ujuzi na palinukia pia. Vitu vingi humo ndani vilikuwa vya gharama. 

Nikaanza kuzunguka-zunguka, nikiangalia kama naweza kuwaona wale watu. Vyumba vingi vya chini na jikoni na chooni hakukuwa na watu, hivyo nikaamua kupanda juu. Nilipofika mwisho wa ngazi niliona korido refu lililoundwa kwa njia ya kupinda, na vyumba kadhaa kwa kila upande. Nilijua haingekuwa busara kuanza kufungua kimoja baada ya kingine kwa kuwa sikutaka uwepo wangu pale utambulike. Ilikuwa ni wakati nanyata-nyata, pale niliposikia sauti za vilio kwa mbali zikitokea upande wa juu zaidi wa nyumba hiyo. Nilianza kutembea kwa haraka kidogo kuzielekea, nazo zikazidi kuongezeka.

Baada ya kupanda ngazi fupi zilizoonekana kuwa ndiyo za mwisho, nilitambua kuwa sauti ile iliyosikika ilikuwa ya mwanamke na mtoto. Nilipofika hapo nikakuta kuna chumba kimoja, juu zaidi, na mlango ulikuwa wazi. Nikaanza kutembea taratibu kuuelekea bila kuelewa yaliyokuwa yanaendelea.

"Please... tafadhali... mimi sijui lolote lile mnalosema..." mwanamke huyo alisikika huku akilia.

"Najua lazima atakuwa amekupa wewe. Unajua, jinsi unavyoendelea kujifanya hujui ndiyo unanipandisha hasira. Au unataka nimkate mikono mtoto wako mbele yako ndo' useme?!" sauti ya mwanaume ikasikika ikitoa kitisho hicho.

"Jamani... jamani... mwanangu amewakosea nini? Mimi sijui mnataka kitu gani, I swear... nimeshawaambia... eeh... msimuumize mtoto wangu jamani. Nitafanya mnachotaka lakini msimuumize mwanangu..." aliendelea kusema kwa kilio mwanamke huyo.

"Kama kweli hutaki tumuumize mwanao, sema iko wapi!"

"Mie sijui jamani... naapa kwa uzao wa mwanangu, sijui...." na kabla hajamaliza kusema maneno yote, nikasikia sauti ya kofi na kishindo, vitu vilivyoniambia kuwa alipigwa usoni na kuanguka.

Aliendelea kulia na sasa nikamsikia William pia akilia huku akiita 'mama' kwa huzuni. Nikakusanya ujasiri na kusogea mpaka hapo mlangoni; mbele yangu walikuwa wale wanaume watatu, mmoja kamshikilia William, mwingine kaegamia mbao iliyosimama akiwa kashika bastola, na mwingine akiwa amesimama mbele ya mwili uliokuwa umelala chini ukifunikwa na nywele usoni. Mwanaume aliyekuwa mbele ya mwili huo uliolala ndiye yule jamaa aliyekuwa ameketi nyuma ya gari na William.

Alichuchumaa na kuunyanyua uso wa mwanamke yule kisha kuzitoa nywele zilizokuwa usoni mwake. Nilipomtazama, kwa hakika niliingiwa na simanzi. Alikuwa mwanamke mrembo sana; mweupe, mwenye macho yaliyojaa machozi, na pua yake ilivuja damu. Nilitambua nguo yake laini aliyovaa juu ilikuwa imechanika-chanika mikononi na kifuani, na alikuwa amevaa suruali nyeusi ya skinny  iliyomsitiri vizuri.

Akiwa ameshikilia uso wa mwanamke huyo, mwanaume yule akamsemesha hivi kwa sauti ya utulivu, "Hutaki kusema, haina shida. Msubirie tu mbwa wako aje, pumbavu zenu nyie." 

Kisha akasukuma uso wake chini na kunyanyuka. Alifanya ishara kwa vidole iliyoniambia kuwa alimaanisha yeye na wenzake watoke humo ndani. Kwa haraka sana, nilijichomeka ndani humo na kusimama pembeni kiutulivu. Sijui kama alisikia kitu fulani vile, kwa kuwa alipofika usawa wangu, mwanaume huyo akasita kidogo na kuangalia upande niliokuwepo. Nikajituliza hivyo hivyo huku namwangalia machoni, naye akapotezea na kutoka ndani ya chumba hicho.

Yule mwanamke alianza kulia huku akiita kwa sauti, "William! William! Mwanangu jamani mnampeleka wapi... aahh... Williaaaam!" 

Kisha akaudondosha uso wake chini huku akilia kwa huzuni. Mlango ulifungwa kwa funguo ili kuhakikisha hatoki humo ndani. Nilimwonea huruma sana. Kufikia hapa nilikuwa nimetambua kuwa hawa watu walichotaka hakikuwa pesa, bali ni kitu kingine. Na lazima kilikuwa muhimu sana kiasi kwamba wangetumia wakati wao mwingi kumuumiza mwanamke huyu, hadi kutumia mtoto wake.

Nikaanza kutembea kumwelekea, na nilipokaribia alipokuwa, nikachuchumaa na kusema kwa sauti ya chini, "Aóratos."

Alinyanyua uso wake na kunitazama kwa kushtushwa na sauti yangu, kisha nikaweka kidole cha shahada kwenye mdomo wangu kumpa ishara ya kwamba asipige kelele. Niliona kwikwi zake kutokana na kulia zikigeuka na kuwa kuvuta pumzi haraka-haraka, na sura yake ilionyesha hofu. 

Nikatoa kidole changu juu ya mdomo na kumwambia kwa kunong'oneza, "Usijali... mimi siyo mtu mbaya. Nataka kukusaidia."

Bado alijawa na hofu usoni mwake na nilielewa haikuwa rahisi kwake kuniamini haraka sana kwa kuwa hakunijua. Nikakaa chini kabisa huku nimenyanyua mikono yangu juu kidogo na kumwambia, "Its okay." 

Yeye akaanza kujinyanyua huku akijisogeza nyuma. Ni hapa ndiyo nilitambua kwamba, alikuwa amefungwa na kamba ngumu sana mikononi, iliyopitilizia hadi kwenye miguu pia na kuifunga kwa pamoja.

"We' ni nani?" aliuliza huku midomo yake ikiwa inatetemeka. 

"Tristan... naitwa Tristan," nikamwambia huku bado nimeketi chini. Nikashusha mikono yangu na kuendelea kumtazama.

"Wewe ni mmoja wao, siyo? Mwanangu yuko wapi... mimi sijui lolote jamani... kama wamekutuma uje unipeleleze, me sijui... mwanangu jamani..." alianza kusema hivyo huku machozi yakimtiririka.

"Hapana..." nikajaribu kumtuliza, "... mimi siko nao. Me... me nimekuja kukusaidia dada'angu." 

Alinitazama kimaswali sana. 

Nikatoa wallet yangu mfukoni na kutoa kitambulisho changu kisha nikamwonyesha. "Mimi nafanya kazi kwenye hii kampuni.... niliwaona hawa jamaa walipomchukua mwanao kutoka shuleni ndiyo nikawafatilia mpaka hapa," nikamhakikishia.

Aliendelea kunitazama huku akipumua haraka-haraka. Nikarudisha wallet mfukoni kisha nikatoa kitambaa changu. Nikanyanyuka kidogo na kumsogelea. Alionekana kama anataka kunikwepa, hivyo nikamtuliza kwa kumwambia 'its okay,' kisha nikasogeza kitambaa changu hadi kwenye pua yake na kuanza kumfuta damu iliyokuwa inavuja. Alikuwa akinitazama sana mpaka nilipohakikisha damu haikuendelea kutoka. Nikarudi nyuma kidogo na kupiga goti moja chini huku nimeelekeza uso wangu kwake.

"Pole sana dada kwa mambo yote unayopitia. Lakini hawa watu wanataka nini?" nikamuuliza kwa upole sana.

Aliinamisha kichwa chake na kuanza kukitikisa, kisha akanitazama na kuanza kusema, "I don't know... yaani... hhh... sielewi. Wamekuja tu leo na kunivamia hapa ndani... hh.. wakanileta huku na hh... kunifunga... wakanipigahh..." 

Alianza kulia na kushindwa kutoa maneno yake vizuri. Machozi yalikuwa yanaanza kujaa kwenye macho yangu. Huyu hapa mbele yangu, mwanamke mrembo sana ambaye alistahili kuangaliwa kwa matamanio, alikuwa akiangaliwa kwa simanzi kutoka kwangu kwa sababu ya mateso yaliyomkabili. Nikasogea karibu zaidi na kumshika begani kwake, huku mkono wangu mmoja ukifuta machozi yaliyotiririkia mashavuni mwake.

Nikamwambia, "Its okay. Usijali... nitakusaidia. Kwanza nahitaji kukufungua hizi kamba kisha tuondoke hapa. Sawa?" 

Akatikisa kichwa chake kukubali. Kisha akaniuliza, "Uliingiaje hapa? Sikukuona sehemu yoyote ile."

"Itakuwa ngumu kukuelezea kwa sasa dada'angu. Wacha tuharakishe kuondoka hapa kwanza."

Nilianza kuhangaika na kamba zake zilizofungwa kwa njia tata sana. Nikaangalia mahali pale kama kulikuwa na kisu au kitu chochote chenye ncha kali ili nizikate.

"Lakini vipi kuhusu William?" aliniuliza.

"Tutamfata na yeye pia. Tutaondoka pamoja naye."

"Kivipi?"

"Yaani... sijui... nisemeje. Nina kama... nguvu fulani ambayo..." 

Kabla sijamaliza kumwelezea, sote tulishtushwa na sauti za vishindo vya miguu, vikiwa vinakielekea chumba hicho. Tulitazamana kwa kushtuka na bila kufikiria sana, nikafumba macho na kusema, "Aóratos," kisha kumwangalia tena mwanamke huyo. Bado nilikuwa mbele yake, lakini nikaanza kuona alivyochanganyikiwa akiangalia huku na kule kwa hofu kubwa. Hiyo ilionyesha wazi kuwa kwenye macho yake, nilipotea ghafla. 

Nilisimama na kutazama mlangoni, nao ukafunguliwa. Wakaingia wale wanaume watatu huku wakiwa pamoja na William. Baada ya kumwona mwanaye, mwanamke huyo alianza kulia na kumwita. William pia alikuwa akilia na kumwita mama yake kwa huzuni. Wote wakasimama wakimwangalia mwanamke huyu bila kutambua uwepo wangu hapo.

"Vipi mrembo? Natumaini haujatu-miss sana. Tumekuletea zawadi," akasema yule jamaa.

Hapo hapo, wakaingia wanaume wengine wawili wakiwa wamemshikilia kwa nguvu mwanaume mwingine katikati yao. Walimvuta na kumsukuma kumwelekea yule mwanamke. Huyo mwanamke alianza kulia zaidi na kujinyanyua, akijiburuza kumfata huku akitaja jina 'Malik.' Nikatambua huyu ndiye angekuwa ni mume wake kwa kuwa William alikuwa akilia huku akisema 'baba.'

Wakakumbatiana huku wakiwa chini hapo, bila kuweza kuzungushiana mikono kwa kuwa wote walikuwa wamefungwa. Nilipomtazama vizuri, mume wa dada huyo alikuwa mwanaume mtu mzima, kwenye miaka kuanzia 35 hadi 40 kwa kukadiria. Alikuwa mweusi mwenye nywele fupi na ndevu zilizochongwa vizuri kama za msanii Drake. Wanaume wale wakawatenganisha kidogo kisha yule jamaa, ambaye kwa sasa nilianza kuona kama ndiye alikuwa kiongozi wao, akainama na kuvuta nywele za yule mwanamke na kumbana mdomo kwa vidole vyake viwili kwa njia iliyomuumiza.

"Mbwa wako huyu tutamchinja usipotupa tunachotaka," alisema kwa ukali, lakini hakuwa akimwambia yule dada, bali mume wake.

"Tafadhali... please nakuomba... usimuumize mke wangu," akaomba kwa huzuni Malik.

"Mke wako tu? Hujamwona mtoto wako? Na yeye tunamchinja... sema iko wapi!" akasema yule jamaa.

Mwanaume yule alimwachia mdomo mke wake Malik huku bado kamvuta nywele kwa nyuma, na hapo mwanamke huyo akasema, "Malik... wanataka nini? Wape... kama ni pesa, wape," alisema huku analia.

Malik alianza kutikisa kichwa taratibu kama anakataa vile. Ndipo jamaa akamwachia yule mwanamke na kutoa bastola kisha kuikoki na kuielekezea kichwani pa William. Nilishtuka. Nikiwa bado nimetulia hapo nikiangalia tukio zima, hakuna aliyeniona. Yule mwanamke akaanza kulia na kumwomba sana mwanaume huyo asimuue mwanaye. William alikuwa akitetemeka. 

"Nahesabu mpaka tatu. Usiposema ilipo, naanza na mwanao," akatoa kitisho hicho bila utani.

"Malik tafadhali..." alisema mama yake William kwa huzuni. 

Malik alifumba macho yake huku machozi yakimtiririka pia.

"Moja..." 

"Malik please... wape wanachotaka... aah..."

"Mbili..."

"No, please no. Usifanye hivi kaka yangu... nitakupa unachotaka... tafadhali... William..." aliendelea kulia mama yake kwa uchungu.

Hapa sasa ilipita kiasi. Sikuweza kuvumilia tena kukaa tu hapo bila kufanya lolote kuisaidia familia hii. Nilijawa hasira sana nilipoutazama uso wa yule jamaa. Alinikera. Nikakusanya nguvu na kutaka kumfata nikiwa sionekani ili nimzuie asimdhuru mtoto yule, na wote pamoja. 

Ni pale tu niliponyanyua mguu wangu kidogo Malik aliposema, "Posta." 

Alisema hivyo akiwa amefumba macho bado. 

"Posta. Iko posta. Niliipeleka na kuiweka kwenye sanduku langu. Nitawapeleka kuifata... tafadhali... iachieni familia yangu," akawaambia.

Mwanamke yule alimwangalia Malik usoni asielewe alimaanisha nini. Mimi pia niliwaza Malik aliwafichia kitu gani Posta kilichowafanya waiumize familia yake namna hii, na kwa nini alikuwa mgumu sana kuwaambia. Jamaa yule alimtazama sana Malik na kisha akarudisha bastola yake kiunoni. Akawaambia wenzake wamnyanyue Malik ili waondoke pamoja naye. Ni hapa ndipo yule mwanamke akamfata Malik, akifanya kama kumng'ang'ania ili wasimchukue. Wakiwa wanaanza kuwatenganisha wakati amemkumbatia vile, akamnong'oneza haraka haraka, 'kuna MTU atakusaidia,' kisha wakatenganishwa.

Wanaume wale wote waliondoka pamoja na Malik na William, isipokuwa yule jamaa aliyejiona ndiye jambazi kuu kuliko wote. Alisimama kidogo akiwa ametazama mlango, kisha akageuka taratibu na kutazama pale chini, alipokuwa amekaa yule mwanamke. Mwanamke huyo alimwangalia kwa hofu pale jamaa alipoanza kumfata na kuchuchumaa karibu yake. Akashusha mkono wake chini, kama vile anaupeleka mapajani mwa huyo dada, halafu akaunyanyua ukiwa umeshikilia kile kitambaa nilichomfutia damu puani.
Hapo ndiyo nikatambua kuwa huenda kilidondoka chini wakati nanyanyuka juu wakati walipoingia. Alikiangalia sana na kumtazama yule mwanamke usoni.

"Kitambaa chako?" akamuuliza kwa utulivu wenye udadisi.

Yule mwanamke akatikisa kichwa taratibu kukubali, kisha jamaa akashusha macho yake na kupandisha akiuangalia mwili wake. Jamaa akanyanyuka kutoka hapo na kuondoka kuelekea chini. Huyo mwanamke alianza kuangalia huku na huku, bila shaka akinitafuta mimi bila kuniona.

"Aóratos," nikasema hivyo nyuma ya mgongo wake na kumfanya ashtuke huku akitoa macho ya hofu kuniangalia. Sasa aliweza kuniona.

"We... we... we ni nani? We ni... we ni jini, au...?" aliuliza kwa kutetemeka.

Nikasogea karibu yake na kumshika mabega yake yote, kisha nikamwambia, "Najua jambo hili si la kawaida. Lakini siwezi kuelezea hapa. Nahitaji kuwawahi hawa watu ili nimsaidie mume wako... nitarudi kwa ajili yenu pia." 

Nilimwambia hivyo kisha kumwachia na kuelekea nje ya chumba kile. Uzuri mlango haukuwa umefungwa hivyo nikatoka moja kwa moja. Ni mpaka nilipofika mwisho wa ngazi kule chini nilipotambua kwamba nilisahau kufanya mwili wangu upotee! 

Kwangu mimi, hata kama ningejipoteza mbele ya macho ya watu, bado niliuona mwili wangu, hivyo ingekuwa rahisi kujisahau. Ile nataka tu kusema lile neno, nikasikia sauti za miguu ikija upande wangu. Nikajibanza nyuma ya ngazi zile kwa chini, na kwa bahati nzuri, kulikuwa na kama mlango mdogo wa kuingilia kwenye chumba nilichodhani ni stoo au basement. Niliingia humo na kuurudishia taratibu, lakini siyo mpaka mwisho, na ile nageuka nyuma, nilishtuka sana kuona mwili wa mwanaume fulani ukiwa umelazwa pale chini; ukiwa na tobo la risasi juu kwenye paji la uso wake. 

Niling'ata meno yangu na kufumba macho nisiamini kuona mwili wa mtu ambaye bila shaka alikuwa hana uhai tena, ukiwa mbele yangu. 

Nilijikaza na kusema, "Aóratos," kisha kufumbua macho yangu. 

Nilijawa na simanzi kubwa. Nilipomtazama, mwanaume huyu alikuwa mgeni kabisa machoni pangu. Alikuwa amevaa sare za walinzi wa magetini, na hilo likaniambia kuwa huyu alikuwa mlinzi wa hapo bila shaka, ambaye aliuwawa na majambazi wale. Ni pale wakati bado namtafakari mlango ule uliposukumwa na kufunguka mpaka mwisho. Nikageuka na kukuta mwanaume yule aliyekuwa akivuta sigara pale nje wakati naingia ndani ya nyumba hii, akitazama-tazama humo ndani kama kuhakikisha mambo yako sawa. Nilijua bila shaka huyu ndiyo alihisi uwepo wangu muda ule nashuka kutoka juu ya zile ngazi mpaka nilipoingia ndani ya hiki chumba.

Baada ya 'kutokuona' jambo lolote humo, alirudishia mlango na kuondoka. Niligeuka kumwangalia mlinzi yule, aliyekuwa ameuliwa bila kosa lolote, kisha nikafungua mlango ule na kutoka. Nikaenda taratibu hadi kwenye mlango wa kutokea na kuufungua. Nilitazama nje pale na sikuona mtu yeyote. Nikatembea taratibu mpaka upande ule ambao gari tuliyokuja nayo iliegeshwa na kukuta yule jamaa, kiongozi wao nadhani, akiongea na simu yake karibu na Suzuki ile. Ghafla nikasikia vishindo vya miguu vikija kutokea nyuma yangu. 

Nikageuka na kukuta ni Malik na wale wanaume wawili wakiwa nyuma yake. Lakini wakati huu, hakuwa amefungwa kamba mikononi. Walinipita na kuelekea mpaka aliposimama yule jamaa, kisha Malik akampa funguo fulani hivi mkononi mwake. Baada ya jamaa kurudisha simu yake mfukoni, waliongozana kutoka pale na kuelekea upande wa kuegeshea magari wa ile nyumba. Kulikuwa na gari moja nyeusi aina ya V8 TX, iliyoonekana kuwa ya gharama. Kwa akili za haraka nikawa nimetambua kuwa, walimwambia akawafatie funguo za gari lake mwenyewe; au huenda la mke wake, ili waende nalo Posta. 

Wanaume wale watatu, pamoja na Malik, waliingia ndani ya gari lile na kuanza kuligeuza ili lielekee getini. Nilikimbia kuelekea geti na kusimama kando; hapo alikuwepo yule mwanaume mwingine aliyetoka kuangalia-angalia kile chumba chenye maiti ya mlinzi muda ule niko ndani. Aliwafungulia geti lile, nami nikarudi nyuma ya gari na kulidandia kwa nyuma; uzuri lilikuwa na ki-bumper kwa chini, hivyo niliweza kukanyaga pale na kushikilia kimkono cha mlango huo wa nyuma huku nimechuchumaa. Gari ikatoka pale na kuelekea barabarani.

★★

Muda mwingi wakati bado tuko mwendoni, nilimfikiria sana yule dada. Nilimfikiria mwanaye. Lakini pia, niliwaza ikiwa ningeweza kufanya mambo mengi zaidi ya kujibanza-banza tu. Nilijiona mwoga sana na nisiyekuwa na njia sahihi za kutoa msaada. 

Ila nilijipa moyo kuwa huko tunakoelekea, bila shaka ningefanya jambo fulani kubadili huu mchezo. Nilianza kuwatafakari wale wanaume. Kwanza, tulipokuja kwenye nyumba ile, walikuwa wawili. Wakati niko ndani ya gari baada ya wao kushuka, walikuwa watatu wakati wakipanda ngazi za upande wa nje kuelekea juu ya ile nyumba. Pale mlangoni alikuwepo mmoja, na wakati Malik analetwa kwa mara ya kwanza, alishikiliwa na wengine wawili. Hiyo ilimaanisha walikuwa sita. Lakini huenda hao walikuwa wachache tu niliopata kuwaona, labda hata kulikuwa na wengine zaidi.

Kwa vyovyote vile, ijapokuwa hali hii iliongezeka utata, bado kulikuwa na faida moja upande wangu; uwezo wa kutokuonekana. Nilifikiria kuwa nilipaswa kuutumia vizuri na kwa akili sana ili niweze kuwachengua hao majambazi. Nilijitahidi kukariri maeneo tuliyotoka na barabara tuliyotumia kupita kuelekea huko walikoelekea mpaka ilipotambulika kwa urahisi yalikuwa maeneo gani, ili iwe jambo jepesi kurudi bila kupotea njia. Nikajitahidi kujikaza sana hapo nilipokuwa nimeshikilia nyuma ya gari. 

Baada ya dakika kumi na kitu hivi, gari ilisimama na kuegeshwa. Nilishuka na kutazama jengo lililokuwa mbele yangu; jengo la Posta. Lilikuwa ghorofa refu kiasi, lenye vioo vingi kwa nje, na sasa wanaume wale wakashuka kutoka ndani ya gari pamoja na Malik. Walielekea ndani ya lile jengo, nami bila kusubiri, nikawafuata kwa nyuma. Waliingia kwa kuongozana huku Malik akiwa mbele yao, kwa utulivu sana ili mtu yeyote asihisi kulikuwa na nuksi. Nilitambua waliacha umbali fulani mfupi kutoka kwa Malik ili watu wasidhani wako pamoja naye. Malik alielekea kwa wahudumu wanaotoa funguo za masanduku ya posta, kisha nikaona akipewa funguo na kuanza kuelekea upande wenye vyumba vya masanduku. 

Haikuwa rahisi kwangu kutembea ndani mule nikiwa sionekani kwa maana watu walikuwa ni wengi, wakipita huku na huko kwa kupishana. Nisingeweza kupisha kila mtu bila kuniona maana wengine walikuwa wakinifata kabisa kwa kufikiri sehemu niliyopo ilikuwa wazi. Hivyo nikaamua kuzungukia pembeni mwa kuta za lile jengo, nikiwa makini nisikanyagane na mtu. Nilitambua fika kuwa nilipaswa kuunda mpango wa haraka ili kumsaidia Malik. Nikatazama sehemu ile kwa makini na kuona jambo ambalo lilinipatia wazo; askari wanne, wakiwa wamebeba bunduki. Sikuwahi kujenga urafiki na mapolisi kabla, hivyo niliingiwa na wasiwasi kidogo kwa sababu ya jambo nililotaka kufanya. Lakini niliazimia kulifanya, iwe isiwe.

Wanaume wale watatu walikuwa wamesimama mbele kule wakimsubiri Malik arudi bila shaka. Niliuweka mpango wangu mwendoni na hatua ya kwanza ilikuwa kusema "Aóratos." Kufikia wakati huu, nilikuwa nimejibanza sehemu yenye nguzo nene ya vigae, hivyo hakuna mtu aliyeniona nikirudi katika hali ya kuonekana. Nikatoka hapo na kuelekea upande waliokuwepo wale maaskari. Wawili walikuwa wametawanyika kidogo, kwa hiyo nikawafata wale waliokuwa karibu-karibu. 

"Habari zenu jamani," nikawasalimia.

"Safi tu," akajibu mmoja wao huku wote wakinitazama.

"Samahani, ila... kuna kitu cha muhimu nataka kuwaambia," niliwaambia huku nikiweka uso wa wasiwasi.

"Kuna shida gani?" akaniuliza.

"Wale wanaume pale... wale watatu... wana bastola. Nilikuwa naingia hapa wakati nilipowaona wanazikoki kisha kuzificha kwenye mikanda yao. Sijajua wana nia gani, ila nikahofia labda wanataka kufanya jambo baya," nikawaambia kwa uhakika.

Waliwatazama wale wanaume, kisha wakaniambia, "Sawa. Ondoka hapa sasa hivi. Na usimwambie mtu mwingine ili sisi tushughulike nao kwanza, umeelewa?"

Nikatikisa kichwa na kuanza kuondoka kuelekea mlangoni. Lakini nilikuwa nikijifanyisha tu kama naondoka; nikazungukia upande wa pili kutoka pale na kujibanza kwenye nguzo moja mule ndani. Niliwaona maaskari hao wakiwaita wenzao na kuanza kuongea nao kama wanafanya mpango kisiri. Nikatazama upande ule wa vyumba vya masanduku na kumwona Malik akirejea, mikononi mwake akiwa amebeba mfuko wa kaki wa mizigo midogo, uliokunjwa na kutuna kuonyesha ndani yake kulikuwa na kitu fulani. Askari wale walianza kwenda kuwaelekea wale wanaume, lakini kwa utulivu sana ili wasiwashtukie. Mimi pia nikawa najisogeza kupitia pande za ukuta kwa umakini.

Malik alikuwa akiwakaribia wale wanaume, pale maaskari waliponyanyua bunduki zao ghafla kuwaelekea huku wakiwazunguka. 

"Tulieni!" aliamrisha askari mmoja.

Yule jamaa akanyanyua mikono huku akisema, "Vipi jamani, kuna shida gani?" huku na wenzake wakinyanyua mikono juu pia.

Watu wengi walisimama kuwaangalia. Malik pia alisimama na kutazama tukio hilo. Moyoni nikawa namwambia Malik 'kimbia, ondoka hapo faster' lakini nilijua hangeweza kunisikia. Watu wengine walikuwa wakikimbia kuelekea mlango wa kutokea ili wasije kuumia ikiwa risasi zingefyatuliwa. Nilianza kujongea kuelekea huko mbele ili nimtoe Malik haraka.

"Tulieni hivyo hivyo," akasema askari mmoja na kuwasogelea wale jamaa. 

Alimwonesha mwenzake ishara kwa kichwa, kisha akasogea na wote wakaanza kuwapapasa wakitafuta bastola, huku wawili wengine wakiwaelekezea bunduki bado.

"Aisee... mnafanya nini eti?" 

"Kimya!" akaamrisha askari mmoja huku akitoa bastola kiunoni mwa jamaa na kumrushia mwenzake miguuni. 

Wale wanaume wawili pia walinyang'anywa bastola zao, kisha maaskari wale wawili wakaizungusha mikono yao kwa nyuma wakitaka kuifunga.

"Sikilizeni... aisee... mnakosea..." jamaa akawa anajaribu kujitetea.

Kufikia hapa, nilikuwa nimesogea karibu zaidi na usawa aliokuwa amesimama Malik. Niliwaza kwamba, ingekuwa vizuri kama ningeongea naye baada ya wale jamaa kuondolewa eneo hilo. Lakini kitu ambacho kingefata, ni kitu ambacho sikuwa nimetarajia kabisa! 

Askari mmoja, aliyekuwa akikagua vitu vyao vingine kama simu na wallet, alisema kitu chenye kushangaza sana.

"Bosco, hawa jamaa ni polisi!"

★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next