CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TANO
★★★★★★★★★★★★★★
Baada ya Namouih kuwa amemkubalia Efraim Donald, wawili hawa wakatoka ndani ya chumba hicho baada ya dakika hizo chache, wakiwa na lengo la kwenda kule nje kwa sababu Blandina alikuwa amekaribia kufika huku tena; akirejeshwa na Suleiman. Wakiwa ni wapenzi rasmi siku hiyo hiyo tu waliyokutana, Efraim Donald alimwambia Namouih kwamba alikuwa na mengi sana ya kumwonyesha kuhusu maisha yake yeye, na alitaka kujifunza mengi pia kuelekea maisha ya mwanamke huyu mrembo. Lakini kwanza, akamwambia jambo muhimu zaidi kwa wakati huu lingekuwa kumsaidia mzee Masoud, hivyo angekuwa naye bega kwa bega kwa kila jambo ambalo lingehitajika.
Walikuwa wameenda kuketi tena pale pale walipokuwa mwanzoni, Efraim Donald akiwa anamsemesha Namouih kuhusiana na mambo yaliyomfanya aweze angalau kutabasamu mpaka Blandina aliporejea hapo. Rafiki huyu akamshukuru Efraim Donald kwa ukarimu wake, akiuliza pia ikiwa gari ambalo Suleiman alitumia kumwendesha lilikuwa lake kabisa, lakini Efraim akasema alikodisha baada ya kufika huku kwa kuwa alikuja na ndege. Ilimpendeza sana Blandina kujua Efraim alikodisha gari aina ya V8, tena kutoka kwa wauzaji na siyo kwa mtu, ikionyesha pochi aliyokuwa nayo ilikuwa nzito hatari.
Baada ya sekunde kadhaa, Blandina akawa ameuona mkufu wa dhahabu aliokuwa amevaa rafiki yake shingoni, naye akaanza kumsifia sana akisema amependeza mno. Lakini akauliza alikuwa ameutoa wapi ndani ya muda huo mfupi, na ndiyo Efraim Donald akaingiza vidole vyake ndani ya kiganja cha Namouih na kusema kwamba walikuwa wapenzi sasa. Blandina akashangaa kiasi na kuuliza kiutani nini ambacho Namouih alikuwa amefanya ndani ya muda huo mfupi alioondoka kilichopeleka mambo baina ya wawili hao hatua nyingine, naye Namouih akacheka kidogo huku akimwangalia mpenzi wake mpya kwa hisia.
Efraim Donald akamwahidi Blandina zawadi nzuri sana kwa kuwa rafiki bora kwa Namouih, naye akachukua namba zake pia. Baada ya kuwa wazi kwa wote kwamba Efraim alijua kuhusu hali ya bwana Masoud, akawa amewaambia kwamba wangekwenda pamoja kesho hospitalini ili aweze kuongea na daktari kwa kina kuhusu mambo yaliyohitajika kwa ajili ya tiba yake, halafu pia kwamba angependa kujitambulisha kwa wazazi wa Namouih ikiwa ingemfaa. Ingawa Namouih bado alihitaji muda kumjua Efraim vizuri na kumzoea, alithamini utayari wake wa kutoa msaada mapema, na hivyo akakubaliana na hilo.
Kwa sababu alihitaji kurudi hospitalini, Namouih akasema yeye na Blandina wangeondoka sasa, hivyo angewasiliana na Efraim baadaye. Mwanaume huyo akamtia moyo mpenzi wake kwa mara nyingine tena, akisema yuko hapo kwa ajili yake kwa lolote lile atakalohitaji, na marafiki hao wa kike wakatazamana na kutabasamu. Efraim Donald akamwita Suleiman hapo na kumwambia awapeleke wanawake hawa walipotaka kwenda, na mwanaume huyo akatii na kutangulia kwenye gari huku Efraim, Namouih na Blandina wakifata nyuma yake taratibu. Efraim hata akatembea karibu na Namouih huku amekishika kiganja chake, akisema vitu vya utani vilivyofanya marafiki hao wawili wamfurahie sana.
Baada ya kuagana sasa na mchumba wake mtarajiwa, Namouih na Blandina wakapelekwa mpaka eneo lisilokuwa mbali sana na hospitali, kisha Suleiman akawaacha ili kurudi kule kwa Efraim Donald. Blandina alitaka kujua kila kitu kilichotokea alipoondoka muda ule mpaka kukuta tayari wawili hao wamekuwa wapenzi, naye Namouih akamwambia watafute sehemu ya kuketi ili wazungumze kwa ufupi. Wakaelekea kwenye eneo la wazi lenye mabenchi na uwanja wa kupumzikia kwa yeyote aliyetaka, kukiwa na watu kadhaa eneo hilo, nao wakaketi kwenye benchi moja lenye sehemu ya kuegamia na kuendeleza mazungumzo.
"Wacha! Akakuingiza na muchumba kukuvalisha necklace? Ikawaje?" Blandina akaendelea kuomba simulizi zaidi.
"Hakukuwa na mambo mengi... nikakubali tu ndiyo akanikumbatia," Namouih akasema.
"Hata kiss hamna?"
"Kiss ya nini?"
"Ish! Najua utakuwa ulikaza hilo lisura lako mpaka akaogopa kukupiga busu..."
"Na ndiyo lisura langu hili hili kalipenda sasa..."
"Ahahahah... dah, hii ni noma. Kiukweli Nam, ninajua kuna pressure kubwa sana kwako cause of this, lakini Donald anaonekana kuwa mtu mzuri sana. Jipe nafasi kwake... yaani, jiruhusu umpende pia. Eventually mambo yatakuwa mazuri especially kwa sababu ana pesa! Utakuwa na taabu gani mommy?"
"Ila wewe..."
"Ni kweli. Umeacha kuwaamini wanaume kwa kipindi kirefu sana, lakini siyo wote wako hivyo kama utakavyodhani. Usiishi kwa kuhofia tu kwamba vitu kama vya wakati uliopita vitakupata tena, sasa hivi ndiyo wakati wa kuijenga future yako kwenye upande wa mapenzi Namouih. Matatizo huwa yapo tu, lakini hata wewe unajua ajali huwa hazifanyi watu waache kuendesha magari. Kwa njia hiyo hiyo, usiogope kutengeneza kitu kizuri na Donald. Hebu jipe nafasi kwake honey," Blandina akaongea kwa kujali.
Namouih akainamisha uso wake huku akitabasamu kwa mbali na kusema, "Sijui ningefanya nini kama nisingekuwa na wewe kwenye maisha yangu Blandina."
"Ahah... always my friend. Wewe ndiyo dada yangu ambaye sikubarikiwa kumpata kwa tumbo moja," Blandina akasema.
Namouih akaangalia mbele na kusema, "Nitajitahidi. Efraim anaonekana kweli kuwa na moyo mzuri, lakini hakuna mwanaume mzuri kwa asilimia zote. Siyo kwamba nataka ukamilifu ila... bado tu sikuwa tayari. Nataka tu haya yote yaende vyema bila kuweka drama nyingi. Ni muda mrefu umepita sijawa kwenye mahusiano kwa hiyo... sijui kama nitamtendea haki..."
"Utaweza tu. Tena wewe hauhitaji hata kufanya lolote yaani, yule atakuwa anakupa kila kitu kabisa."
"Ni rahisi kuwaza hivyo kwa sasa ila inabidi kungoja tu kuona. Kilicho kwenye akili yangu zaidi kwa wakati huu ni baba... hata Sasha na Nasma pia," Namouih akasema.
"Halafu kweli... kuhusu Sasha. Hali ya yule binti imekaaje Namouih?" Blandina akauliza.
Namouih akashusha pumzi na kuanza kueleza. "Familia yetu kama unavyojua ina mgawanyiko kidini. Sisi tumefuata dini ya baba, na ijapokuwa mama alibadili jina lake kabisa lakini hajawa mwislamu kwa asilimia zote..."
"Ndiyo..."
"Yeah sasa, kuna kipindi fulani ilitokea kama... ugomvi kati ya baba na mama, na ingawa nilikuwa mdogo wakati huo niliweza kuelewa kwamba ilihusiana na tofauti zao ilipokuja kwenye suala la kidini, hasa kwa kuwa mimi nilifata upande wa baba badala ya upande wa mama kama alivyotaka. Kuna vitu alivyopenda mama ambavyo alitaka mimi pia nifurahie, lakini kwa misingi ya dini yetu havikuwa halali. Hiyo ilifanya wazinguane sana Blandina. Mambo mengine mengi yaliyoongezeka sijui sana lakini ilifikia kipindi mpaka wakatengana kwa muda mrefu..."
Blandina akaguna kwa kushangaa.
"Baba alienda kukaa mwenyewe sehemu nyingine, me nikabaki na mama. Mama... mama kama unavyojua siyo mtu wa kukaa sehemu moja... akawa anatoka na kijana mwingine, vile vile na baba pia... akaanza kutoka na mwanamke mwingine. Kwa mama ilikuwa kama fun tu, ila baba... inaonekana baba alimpenda huyo mwanamke aliyetoka naye kimapenzi. Huyo mwanamke aliitwa Sasha..."
Blandina akamwangalia kwa njia iliyoonyesha kwamba alielewa kule Namouih alikokuwa anaelekea.
"Yeah. Huyo mwanamke alipata ujauzito wa baba. Alipojifungua mtoto alipatwa na maumivu makali sana yaliyosababisha kifo chake siku 10 baada ya kujifungua, kwa sababu kuna sehemu nyingi ndani ya mfumo wake wa uzazi zilizoharibika vibaya. Huyo mtoto aliyezaliwa aliachwa na mama yake akiwa na siku 10 tu, ndiyo maana baba akamwita Sasha..."
"Masikini..." Blandina akasema kwa huzuni kiasi.
Namouih akaendelea kusema, "Ingekuwa ngumu kwa baba kumlea mtoto mdogo namna hiyo peke yake, kwa hiyo akamtafuta mama na kumwomba wasameheane kwa yaliyopita, ili amsaidie kumlea mtoto pamoja. Mama hakukataa. Alimlea Sasha kama binti yake wa kumzaa. Na anampenda. Ila sema tu... kuna mambo yalikuja kutokea baadaye yanayofanya anakuwa anamtendea jinsi ulivyoona anamtendea..."
"Ni nini kilitokea?"
"Nasri. Unafahamu kwamba mdogo wangu alikufa kwa kutafunwa na mnyama..."
"Ndiyo... uliniambia..."
"Well, wakati huo mimi nilikuwa chuo. Hiyo siku Baba na wengine wote walienda kutembelea wapi sijui... sehemu fulani ya kujivinjari, baba alikuwa ndiyo amerudi kutoka migodini huko kwa hiyo akawapa treat... hhh... Sasha alikuwa na miaka 10 wakati huo. Nasri 6. Si unajua michezo ya watoto wanaweza wakawa wanakmbia mara huku mara kule, kwa hiyo hata kama wangeenda mbali haikuonekana kuwa hatari kwa sababu mama alijua mtoto yuko na dada yake kwa hiyo...."
Namouih akaishia hapo tu na kubaki anatikisa kichwa kwa huzuni.
"Kwa hiyo... unataka kusema hilo janga lilipotokea, Sasha alikuwa pamoja na mdogo wako, lakini yeye akaokoka kifo. Kwa hiyo mama'ako anamlaumu Sasha kwa kilichompata Nasri, si ndiyo?" Blandina akasema kwa utambuzi.
"Alikuwa na miaka 10 tu Blandina. Na yeye alikuwa mtoto. Lile halikuwa jambo alilofikiria lingetokea yaani huwa sielewi ni kwa nini mama bado anamtendea vibaya kwa sababu hiyo... ni miaka mingi imepita... ah," Namouih akaongea kwa huzuni.
"Kama ujuavyo, uchungu wa mwana aujuaye...."
"Hata kama Blandina. Amemtendea vibaya sana tokea wakati huo, na mpaka kufikia kipindi hicho Sasha alikuwa hajui kama yeye siyo mtoto wake wa kumzaa lakini mama ndiyo akamwambia makusudi kabisa ili kumuumiza. Baba aliongea naye mara nyingi sana juu ya kumtendea Sasha bila heshima lakini hasikii. Sawa Nasri amekufa, kumtendea Sasha vibaya ndiyo kutamrudisha? Hizo kauli zake mbaya mbaya yaani Blandina nitahakikisha nazikomesha. Sikuwahi kuongea na mama juu ya hilo lakini niliona mengi, na yalinichukiza sana. Kwa hiyo ulivyoniambia amefanya vile leo nimeumia sana... yaani anamtendea mtoto bila ufikirio... eti anamwita muuaji...."
"Basi Namouih, basi..."
Blandina akaanza kumtuliza baada ya kuona kwamba Namouih alilemewa na hisia sana mpaka akawa karibu kulia tena.
"Inasikitisha sana. Lakini uko sahihi. Itakubidi uongee naye," Blandina akamwambia.
Namouih akajifuta machozi na kumwangalia.
"Hakuna mtu mwingine ambaye ataweza kuongea na mama yako vizuri kuhusu hili kama siyo wewe. Mwambie ajue anachokifanya siyo kizuri. Sasha anahitaji kuwa huru," Blandina akasema.
Namouih akatikisa kichwa kukubali ushauri huo, naye Blandina akavishika viganja vya rafiki yake na kuendelea kumtia moyo zaidi.
Dakika kadhaa kupita, wawili hao wakatoka sehemu hiyo na kurudi hospitalini hatimaye. Walikuta baadhi ya marafiki zake Masoud wakiwa wamefika kumpa pole, na wakati huu wadogo zake Namouih walikuwa wamesharudi nyumbani, akibaki Zakia pekee kumwangalia mumewe. Wakaendelea kukaa pamoja naye mpaka wakati ambao wengine waliondoka na kuwaacha Namouih, Blandina, pamoja na Zakia tu.
Namouih akaongea na baba yake. Akamwambia kwamba kesho alitaka kumtambulisha kwa mtu fulani muhimu sana, hivyo asishangae sana endapo angemleta mgeni huyo. Masoud alitaka kujua ni nani na kwa nini alikuwa dili kubwa sana, naye Namouih akasema angepaswa kutulia tu ili kesho ifike aweze kujionea. Zakia kama Zakia alikuwa ameshakisia kwamba inawezekana huyo mtu akawa ndiyo Donald, lakini alitaka kuhakikisha zaidi. Baada ya muda fulani mama huyo akawaambia wanadada kwamba yeye angebaki hapo usiku huo kuangalia mahitaji ya mume wake, hivyo wao wangeweza kwenda nyumbani tu.
Ilikuwa imeshafika usiku sasa, na ndiyo Namouih na Blandina wakamuaga mzee Masoud ili kwenda nyumbani. Wakati wakiwa wanaondoka, Zakia akawafuata na kuwasimamisha walipofika nje ya vyumba vya wodi, akisema anataka kuongea na binti yake mara moja. Blandina akamwambia Namouih anatangulia nje, hivyo akawaacha wawili hao sehemu hiyo. Namouih tayari alijua kile mama yake alichotaka kusema, kwa hiyo akatulia tu ili amsikilize.
"Huyo mgeni unayemleta kesho ni nani?" Zakia akauliza.
"Nimewaambia msubiri... mtamwona akija kesho," Namouih akasema.
"Si useme na we' naye... kwani ukiniambia atakufa?"
"Kwani nisipokwambia we' utakufa?"
"Namouih usiniletee nyodo. Haijalishi umekuwa mkubwa kiasi gani mimi bado ni mama yako, nikikuuliza swali nakuomba unipe jibu."
"Na wewe bado unaniona mimi kama mtoto wako? Basi naomba unipe jibu. Kwa nini bado unamtendea Sasha vibaya?"
"Nini?" Zakia akauliza kwa kutotambua swali hilo limetokea wapi ghafla.
"Bado hujaondoa kinyongo chako kisichokuwa na faida yoyote kwa huyo mtoto kwa nini?"
"Unaongelea nini... nani amekwambia... mbona me..."
"Mama nakujua vizuri. Na siyo kwamba nakuhukumu kwa sababu kila mtu ana mapungufu yake. Lakini unapoendelea kumtolea maneno makali Sasha, unamkandamiza sana. Mama huyu binti hastahili hayo, haikuwa makosa yake. Ninajua unaelewa nachomaanisha..." Namouih akasema kwa upole.
Zakia akabaki kumtazama tu kwa umakini.
Namouih akavishika viganja vyake Zakia na kusema, "Mama, wewe ni mtu mzuri, na unaweza kuwa mzazi bora zaidi kwetu. Ni suala la kukiondoa tu kinyongo chako kwa huyu mtoto, hakuna jambo lolote unalochukia juu yake ambalo ni makosa yake mama. Mliyopitia wewe na baba ni mengi, na wakati huu... sisi kama familia tunatakiwa kushikamana sana. Unaposema au kufanya vitu vinavyoumiza... unasababisha Sasha anaacha kukazia fikira mambo mazuri anayoweza kutimiza na badala yake anakuwa anajitenga... anajichukia. Mama tafadhali nakuomba. Usiwaze mengine. Sasha ni mtoto wako. Mtendee kama hivyo."
Zakia alikuwa ameachwa njia panda, akiwa hajategemea kabisa kwamba Namouih angeongelea jambo hilo muda huo, hivyo akabaki kimya tu kwa kutafakari maneno ya binti yake.
Namouih akaviachia viganja vya mama yake na kusema, "Ni huyo kaka uliyenitafutia ndiyo anakuja kesho. Usimwambie lolote baba mpaka mimi nimtambulishe kwake... sawa?"
Zakia alikuwa amekwishaishiwa pozi, lakini akafanikiwa kutikisa kichwa chake kwa njia ya kuonyesha ameelewa.
Namouih akageuka zake tu na kuanza kuelekea kule nje ambako alielewa Blandina alikuwa akimsubiri, huku akimwacha mama yake anafikiria vitu vingi sana. Hakuelewa ni kwa nini Namouih aliliongelea hilo wakati huu lakini alijua kile alichosema kilikuwa kweli kabisa, na ukweli huo ulimgusa sana moyoni. Akarudi tu kwa mume wake baada ya hapo.
★★
Namouih alikwenda nyumbani kwao pamoja na Blandina, nao wakapokelewa vyema na wadogo zake waliokuwa wametulia tu kutazama TV. Namouih akamsihi Blandina alale hapo kwa usiku huo, na rafiki yake huyo akakubali. Alikuwa anatania kuhusu namna ambavyo familia hii iliishi hapo kukiwa na wanawake tu kwa muda mrefu, yaani akionelea kwamba ni muhimu kuwepo mwanaume ili angalau kuwe na hali ya ulinzi, lakini Nasma akasema yeye ndiye aliyekuwa mlinzi wa wote hapo.
Baada ya kupata chakula pamoja na kuendelea kutulia ndani, Namouih akawa anaongea na Sasha kuhusu mambo yake binti, na kiukweli Sasha aliongea mambo mengi kwa uwazi mzuri sana kwa sababu alimzoea mno Namouih. Alizungumza kwa uchangamfu pia, na dada yake akamtia moyo aendelee kukomaa na masomo hasa kwa sababu mitihani ya kuhitimu kidato cha nne ilikuwa njiani. Vile vile na Nasma pia, ambaye alikuwa anakaribia kuanza mitihani ya darasa la tano, akatiwa moyo kusoma kwa bidii. Walikaa kupiga story na kuangalia vichekesho kwenye simu za Namouih na Blandina mpaka ulipofika wakati wa kwenda kujipumzisha, hasa baada ya Nasma kusinzia.
Mtoto wa kike akapelekwa chumbani kulala, akifuatwa na Sasha pia, kisha marafiki hawa wawili wakaendelea kukaa sebuleni kwa muda mrefu zaidi mpaka inafika saa saba usiku. Namouih akawa amemwambia Blandina kuhusu ile ishu ya mama yake, akisema alijitahidi kuongea kwa ufupi tu na kwa njia nzuri ili imguse moyoni, na kwa hilo Blandina akampongeza. Yalifuata maongezi kuhusu Efraim Donald, ambaye kwa muda wote ambao wawili hawa waliendelea kukaa sebuleni alikuwa anatumiana jumbe na Namouih zilizoonyesha upendo kwa mwanamke huyu. Alionekana kudata sana kwa Namouih mpaka Blandina akawa anasema kiutani kwamba wangemla hela mpaka zimwishie.
Basi, baada ya Namouih kutakiana usiku mwema na Efraim Donald kwenye simu, marafiki hao wakawa wameamua kwenda kulala, nao wakazima taa za sebuleni na kuingia chumbani. Wangelala kwenye chumba cha wazazi wa Namouih kilichokuwa na vitanda viwili, nao wakavua nguo walizokuwa nazo na kuvalia khanga kwa kuisitiri miili yao vizuri. Wakati Namouih alipokuwa amesogea dirishani ili kulifunika pazia vizuri, jambo fulani likavuta umakini wake kutokea nje ya dirisha hilo; kutokana na uwazi mdogo uliokuwa umeachwa na pazia. Akalisogeza pazia hilo kidogo sana na kuchungulia huko nje, na ndipo mapigo ya moyo wake yakaanza kukimbia kwa kasi kutokana na hofu fulani iliyomwingia.
Huko nje, kukiwa na sehemu zenye nyumba za hapa na pale za majirani na miti na vichaka kadhaa, aliweza kuona umbo la mtu aliyesimama gizani, tena kwa njia ile ile kabisa kama jinsi ambavyo alimwona mtu yule siku ya juzi wakati yuko mjini na Blandina mvua ilipoanza kunyesha. Lakini wakati huu mtu huyo aliweza kuonekana machoni, machoni tu, na ingawa ilikuwa kwa umbali fulani, Namouih angeweza kutambua kwamba macho yake yalikuwa yanamtazama yeye moja kwa moja, kana kwamba alikuwa ameona kwa uhakika kabisa sehemu hiyo ndogo sana ambayo Namouih alisogeza pazia.
Mwanamke huyu alishindwa kuelewa kilichokuwa kinaendelea, lakini jambo hilo lilianza kumwogopesha sana. Akiwa anataka kumhakikishia Blandina wakati huu kwamba alimwona mtu yule, akaamua kutoacha kumwangalia kabisa ili amwite rafiki yake hapo bila kumpoteza machoni mtu huyo kama ilivyokuwa juzi.
"Blandina... njoo... njoo haraka..."
Namouih akamwita kwa sauti ya chini sana, naye Blandina, aliyekuwa anajipaka mafuta ya kulainisha ngozi miguuni, akaona kwamba hapo kulikuwa na jambo fulani muhimu sana, hivyo akanyanyuka kutoka kitandani na kusogea alipokuwa mwenzake. Bado Namouih aliweza kumwona mtu yule asiyeeleweka alikuwa na shida gani, na baada ya Blandina kufika hapo akachungulia nje huko pia, wakati huu Namouih akipanua zaidi uwazi ule kwenye pazia ili kumruhusu mwenzake aone huko nje.
Blandina akamwangalia Namouih kiufupi, kisha akaangalia nje tena, halafu akamwangalia rafiki yake tena na kuuliza kwa sauti ya chini, "Nini?"
Namouih hakuwa ameacha kumtazama mtu huyo huko nje, naye akamwambia Blandina, "Angalia pale kwenye kona... ile nyumba ya ma' Gati."
Blandina akatazama huko tena kwa sekunde chache, kisha akasema, "Kwani kuna nini? Sioni chochote zaidi ya hiyo kona."
Namouih bado aliweza kumwona mtu yule pale, hivyo kauli ya Blandina ikamshangaza sana, na hofu yake ikazidi kupanda.
"Blandina acha masihara basi!" Namouih akasema hivyo huku akitazama macho ya mtu yule huko nje.
Blandina akamwangalia rafiki yake kwa kujali na kuuliza, "Tatizo nini Nam?"
Namouih akamwangalia rafiki yake kwa ufupi, na ile aliporudisha macho yake upande wa dirisha, mtu huyo aliyekuwa nje sasa akawa amesimama karibu kabisa na dirisha hilo, akimtazama Namouih kwa njia ya kikatili!
"Aaaah!"
Namouih akapiga kelele na kurudi nyuma kama vile amesukumwa mpaka akaanguka chini! Blandina alishtuka sana na kumfata hapo chini, akiuliza tatizo lilikuwa nini, lakini Namouih akaanza kurudi nyuma-nyuma mpaka alipoishia kwenye kabati la nguo za mama yake, huku akitazama dirishani kwa hofu. Blandina akamwacha chini hapo na kusogea dirishani tena, akaangalia nje kwa mara nyingine na kutoona jambo lolote lenye kutatiza, hivyo akalifunika pazia vizuri zaidi na kumfata rafiki yake hapo chini. Namouih alikuwa anapumua kwa presha, hivyo Blandina akakishika kichwa chake na kukikumbatia ili kumtuliza.
"Namouih... niambie umeona nini..."
Blandina akamwambia maneno hayo kwa sauti tulivu baada ya dakika chache kupita, na sasa Namouih alikuwa amefumba macho akijitahidi kurejesha utulivu.
"Nini kinaendelea Blandina?" Namouih akauliza baada ya sekunde chache.
Blandina akamwachia kichwani na kumwangalia usoni kwa ukaribu. "Nini? Niambie. Umeona nini?" akamuuliza.
"Yaani sielewi. Naota au? Hicho kilikuwa nini?" Namouih akaongea kwa kutatizika.
Blandina akaona ingekuwa vyema kumtoa hapo chini ili wakakae kitandani, naye akamsaidia Namouih kunyanyuka taratibu na kwenda kuketi hapo kitandani; Blandina akikaa karibu yake sana.
"Kulikuwa na kitu umeona hapo nje?" Blandina akauliza.
"Ndiyo. Nimeona... nimeona sijui ni mtu, sijui ni nini... oh Allah... this has to be a dream... nitaweza kulala kweli?" Namouih akasema kwa kughafilika.
"Nam niambie umeona nini... huyo mtu... wapi..."
"Unakumbuka juzi wakati... tuko nje mvua ikanyesha... nilikwambia utazame kule nilikoona mtu amesimama?"
"Ndiyo... nakumbuka. Ndiyo huyo uliyemwona sasa hivi tena?"
"Sijui kama ndiyo yeye au la, lakini alikuwa amesimama kwa njia ile ile kabisa. Nashangaa hujaweza kumwona. Nimekuangalia kidogo tu mara akawa ameshafika dirishani... eh Mungu wangu... nini hiki?" Namouih akazungumza kwa hisia.
"Mh... Namouih unaniogopesha..."
"Sikutanii Blandina..."
"Labda tusingechelewa kukaa mpaka sasa hivi... inawezekana wachawi wameanza yao..."
"Wananitaka nini mimi sasa? Niwaone mimi tu kwa nini? Utafikiri sina mambo ya kuwaza afu' hii mijitu inaanza kunisumbua akili... agh," Namouih akaongea kwa kuudhika na kusonya kwa hasira.
Blandina akawa anamtuliza kwa kuusugua mgongo wake taratibu, kisha akasema, "Vipi tukisali kwa pamoja?"
Namouih akatikisa kichwa kukubali, na marafiki hawa wakashikana viganja na kuanza kusali, lakini kila mmoja akisali kimoyomoyo kwa sababu ya dini kutofautiana. Baada ya hapo, Blandina akamwambia Namouih apande kitandani ili yeye aizime taa, kisha wangelala pamoja kitandani ili amsaidie rafiki yake kuituliza hofu yake. Akaenda na kuzima taa, kisha akapanda kitandani ambapo palikuwa pameshushiwa neti, halafu akaifunika miili yao kwa mashuka na kulala nyuma ya mwili wa Namouih akiwa kama amemkumbatia. Angalau jambo hili liliweza kumpa Namouih utulivu zaidi kutokana na hofu aliyoipata baada ya kuona jambo lile lisiloeleweka muda mfupi nyuma, na hatimaye usingizi ukawachukua warembo hawa kwa pamoja baada ya dakika chache.
★★★
Siku iliyofuata, ikiwa ni Jumapili ya mapumziko kwa wengi, Namouih na Blandina waliamka pamoja mida ya saa 2 na kuanza kujiandaa kwa kufanya mambo machache kwa ajili ya siku hii. Sasha alikuwa ameamka mapema sana na kufanya usafi wa nyumba pamoja na kuandaa chai, hivyo wakubwa wakafanya yao na kutulia kidogo kabla ya kuanza safari ya kuelekea hospitalini. Namouih alikuwa ameamka vizuri tu, na waliligusia suala lililotokea usiku wa kuamkia sasa kwa Sasha pia, aliyeshangaa na kusema pia kwamba lazima ilikuwa ni wachawi. Wakatania kuhusu jinsi ikiwa wangekuwa walokole namna ambavyo maombi yangepigwa mpaka asubuhi, wakiwaamsha majirani kwa sauti za juu kama namna ambavyo wanadini hao hufanya.
Basi, Blandina akiwa ndiyo msaidizi wa karibu wa Namouih, akawa amempa taarifa juu ya masuala fulani ya kikazi ambayo Namouih angehitaji kuyashughulikia upesi, kumaanisha kwamba hakuwa na muda mrefu wa kuendelea kukaa huku kwenye mkoa wao wa nyumbani; wangehitaji kurudi jijini kwao walikofanyia kazi ndani ya muda mfupi. Namouih akasema haikuwa na shida, na kwa sababu leo angetakiwa kushughulika na suala la Efraim Donald, akamwomba rafiki yake amsaidie kumpendezesha kiasi. Blandina alifurahi sana na kuanza kumpamba rafiki yake baada ya Namouih kumaliza kuoga.
Kuna kiwango fulani hivi cha msisimko uliomwingia Namouih kila mara ambapo Efraim Donald angemtumia ujumbe au Blandina kuanza kumwongelea vizuri, ikiwa wazi kwake sasa kwamba alikuwa ameanza kuufungua moyo wake kumwelekea pedeshee wake huyo, ingawa kwa asilimia ndogo sana. Akavaa gauni jeupe na refu lenye urembo wa maua, lililofunika sehemu kubwa ya mwili wake wote lakini kwa njia iliyoendana vizuri na umbo lake. Akaziachia nywele zake na Blandina kuzitengeneza kwa mtindo mzuri sana wa mikunjo-mikunjo (curls), huku akimwambia kwamba Zakia ndiye angeweza kumtengeneza vizuri hata zaidi kama angekuwa hapo. Namouih hakutaka kupendeza kupita kiasi, lakini hata kwa kiasi hicho kidogo ilionekana kama amepitiliza. Alikuwa mzuri mno.
Wote wakamaliza kujiandaa na kubeba yaliyohitajika kwa ajili ya kwenda nayo hospitalini, na ambaye angebaki hapo nyumbani ni Nasma kwa kuwa Sasha angeenda kubaki hospitalini na Zakia angerudi nyumbani kujiweka sawa kimwili. Walichukua usafiri kwa pamoja mpaka hospitalni, na Namouih akawa amewasiliana na Efraim Donald ambaye akasema hangekawia kufika huko, kwa hiyo Namouih awe tayari kwa ajili yake. Wanawake hao wakamkuta Zakia na mzee Masoud pamoja kwenye wodi, wakionekana kupata maongezi, naye Namouih akamuuliza mama yake kuhusu jambo lolote jipya lililosemwa na daktari. Hakukuwa na mengi yaliyohitajika kwa hapo zaidi ya uangalizi aliokuwa akipata mzee huyo, jambo la muhimu likiwa kumpa dawa na kutafuta njia ya kumfanyia upasuaji anaohitaji.
Haukupita muda mrefu sana Namouih akapigiwa simu na Efraim Donald, akimwambia kwamba tayari alikuwa hospitalini hapo, naye akaenda nje ili kumpokea. Alitoka nje ya jengo la hospitali lakini akiwa bado ndani ya uzio wa kulizunguka, naye akamwona Efraim akiwa amesimama usawa wa gari lake la V8 hapo. Alikuwa amevalia T-shirt nyeupe yenye mikono mirefu, suruali ya jeans na viatu vyeusi vilivyong'aa haswa. Mkononi alivaa saa yenye mwonekano wa dhahabu, naye alikuwa anamtazama Namouih baada ya kumwona mwanzoni mwa ngazi za kutokea kwenye jengo lile.
Namouih akataka kumfata hapo, lakini Efraim Donald akamwonyesha ishara kumwambia asimame tu; yeye ndiyo angemfata. Upepo ulipuliza nywele za Namouih na kufanya kiasi zimzibe usoni, naye akawa ametambua kwamba baadhi ya watu walimwangalia sana, lakini akawapuuzia na kuendelea kumsubiri mtu wake. Efraim Donald alipomfikia karibu, akamkumbatia moja kwa moja kabisa, naye Namouih akarudisha kumbatio lake na kuachia tabasamu la mbali, kisha wakaachiana na kuangaliana usoni.
"Najua siyo mahali pazuri sana kusema hivi but, you look stunning... umependeza sana," Efraim Donald akasema.
"Asante. Wewe pia," Namouih akamwambia.
"Mama na baba wote wako ndani eeh?" Efraim akauliza.
Namouih akatikisa kichwa kukubali.
"Okay, ni vizuri," Efraim akasema na kuangalia pembeni.
"Unaogopa?" Namouih akauliza kimasihara.
"What... ahah... hapana. Najiuliza tu kama wewe umeshakuwa na uhakika juu ya hili," Efraim akamwambia.
Namouih akabaki kumwangalia tu usoni.
Efraim Donald akamsogelea karibu zaidi na kusema, "Naomba ukumbuke jambo hili. Ninataka kufanya mambo yote kwa ajili yako kwa sababu nakupenda, na sitarajii uone labda muungano wetu kuwa kama malipo. Ninataka unipende pia. Kwa hiyo huu ni mwanzo tu, bado tuna mambo mengi ya kutimiza pamoja Nam-Nam."
Namouih akatabasamu kwa hisia sana na kutikisa kichwa chake kuonyesha amemwelewa.
"Okay. Twende," Namouih akasema.
Wawili hawa wakaongozana kuelekea ndani huku Efraim Donald akimwambia Namouih kuwa baada ya kumaliza kumtambulisha yeye kwa wazazi wake, angehitaji kuwa pamoja na Namouih wakati ambao angekwenda kuzungumza kwa undani na daktari aliyesimamia suala hilo la saratani ili apate mwanga zaidi wa mambo yaliyohitajika kufanywa. Namouih akakubali juu ya hilo, na wawili hawa wakawa wamefika sasa pale alipolazwa bwana Masoud. Zakia alimsalimu mwanaume huyu kwa shauku, akimkaribisha vizuri sana, naye Namouih akamtambulisha Sasha kwa Efraim pia. Kwa kuwa tayari jamaa alifahamiana na Blandina salamu yao ilijawa na tabasamu za furaha, na ndipo akasogea sasa kujitambulisha kwa mzee.
"Pole sana bwana Masoud kwa hali yako," Efraim Donald akamwambia.
"Asante," Masoud akaitikia.
"Mimi naitwa Efraim Donald..."
"Efraim... nafurahi kukujua. Ni wakati mbaya kukutana namna hii... ingekuwa vizuri hata kupeana mikono..." Masoud akaongea kivivu.
"Ahah... usijali mzee wangu. Utatoka hapa... na tutapeana mambo mengi zaidi ya mikono tu," Efraim akamwambia.
"Wewe ni mchungaji?" Masoud akauliza.
Wengine wakatabasamu kidogo, naye Efraim akamwangalia Namouih.
"Baba... Efraim ni... ni mchumba wangu," Namouih akasema.
"Mchumba?" Masoud akauliza.
"Ndiyo baba. Nimekuja kumtambulisha kwako...."
Masoud akaanza kukohoa kwa nguvu kiasi, na wanawake hapo wakajaribu kumtuliza.
"Pole... pole..." Sasha akawa anamwambia huku akiwa karibu yake.
"Samahani kijana wangu..." bwana Masoud akasema.
"Haina shida mzee wangu. Mchumba aliyeshuka tu ghafla na kufika hapa lazima ashangaze kidogo," Efraim akasema.
Masoud akacheka kidogo, na jambo hilo likafanya wengine watabasamu pia.
"Sawa Efraim. Namouih hajawahi kukuongelea kabisa maana ni... msiri mno... nafurahi kwamba amenitambulisha kwako," Masoud akasema.
"Mimi pia. Samahani sana kwa kuja ghafla... ila usijali, tutakuwa na mambo mengi sana ya kuzungumzia pamoja... wakati huo tukiwa tunaangalia na mechi za watani wa jadi," Efraim Donald akasema kiutani.
"Ahah... sawa. Una miaka mingapi kijana wangu?" Masoud akauliza.
"Thelathini na tisa," Efraim akajibu.
"Ahaa... sawa. Namouih..." mzee Masoud akaita.
"Bee... " Namouih akaitika.
"Umekua mama. Sasa hivi umeshapata na mchumba, utafunga ndoa, itakuwa jambo zuri sana. Natamani ningeishi muda mrefu vya kutosha kucheza na wajukuu wangu..."
"Masoud usiongee hivyo bwana... tena mbele ya mgeni siyo vizuri..." Zakia akamkatisha.
Namouih akawa ameingiwa na simanzi kiasi, hata Blandina alitambua hilo. Efraim Donald akasogea karibu yake na kuingiza kiganja chake kwenye kiganja cha Namouih, naye akampa ishara kwa kichwa iliyomwambia mwanamke huyu kwamba alimaanisha waondoke haraka kwenda kuongea na daktari. Akakubali, kisha akamwambia baba yake kwamba wanatoka mara moja kisha wangerudi muda si mrefu, naye bwana Masoud akakubali kwa njia iliyoonyesha uchovu wake mwingi.
Efraim Donald na Namouih wakaondoka hapo wakiwa pamoja na Zakia, na mwanaume huyu alikuwa akimtia moyo mama yake Namouih kwa kusema kwamba yeye na binti yake wangefanya kila kitu kusaidia hali ya mume wake, hivyo asiwe na msongo kabisa. Akamwambia kwamba wangehitaji kulishughulikia hili upesi sana ndiyo mambo mengine yafuate, hasa kwa kuwa hawakutumia muda mwingi kuweza kujuana vizuri, naye Zakia akamshukuru sana kwa hilo. Mama ya mrembo wetu akarudi kwa mumewe, akiwaacha wawili hao wanaelekea kumwona daktari. Walihitaji kusubiri kwa muda fulani kabla ya kuonana naye, ndipo wakaingia ofisini kwake ili kuweza kupata maelezo muhimu kuhusu mzee Masoud.
"Naitwa Efraim Donald," mwanaume akajitambulisha kwa daktari.
"Okay. Niite Doctor Sunil. Wewe ni mmoja wa familia hii?" daktari akauliza, akiwa ni mwanaume mtu mzima na mhindi pia.
"Ni mchumba wangu," Namouih akajibu.
Efraim Donald akakishika kiganja cha Namouih kwa kufurahi kusikia amesema hivyo ingawa hawakuwa wachumba rasmi.
"Ooh... okay sawa. Hali ya mgonjwa wenu bwana iko kama nilivyokwambia mwanzo... inaendelea, na itaendelea kuwa mbaya kwake kadiri siku zinavyosonga endapo kama hatapata matibabu sahihi..." daktari Sunil akasema.
"Doctor... nahitaji unielezee vizuri kila kitu kinachompata mzee wetu, na option zote best zilizopo ili kumpa msaada utakaofaa... specifics," Efraim Donald akamwambia daktari.
"Saratani aliyonayo imesababishwa na yeye kuvuta gesi ya radon. Hii hutoka kwenye chembe ndogo ndogo za kitu kinachoitwa uranium, ambacho huwa kipo ndani ya mawe-mawe yenye kutoa vumbi... na ikivutwa kwa muda mrefu ndiyo kama hivyo, huathiri au kuyaharibu kabisa mapafu. Tulipompiga X-ray na CT scan kweli tuliona ana cancer, na ili kujua aina ya matibabu yatakayomfaa tukafanya vipimo kwa njia ya PET-CT scan. Mzee Masoud ana saratani stage 3A ya mapafu, na imeathiri pafu lake lote la kulia. Najua kutokea mwanzo tumewaambia kwamba atahitaji upasuaji, lakini sasa hivi saratani yake imetanuka zaidi, na hiyo inamaanisha mtapaswa kufanya uchaguzi wa matibabu ambayo mtaona yanafaa kwa huyu mzee ili apatiwe..." daktari huyo akaeleza.
"Unamaanisha nini doctor?" Namouih akauliza.
"Matibabu ya kawaida huwa yanasaidia kuua seli za saratani kutokea pale zinapoanzia, yaani kwenye kiini chake. Upasuaji na huduma ya radiotherapy ndiyo matibabu ya kawaida. Lakini matibabu ya kutumia mifumo ya ndani zaidi huziua seli hizo popote zilipo ndani ya mapafu au hata zikiwa zimeshaanza kusambaa mwilini. Hizo ni kama chemotherapy, immunotherapy na zingine. Wakati mwingine radiotherapy na chemotherapy huunganishwa ili kuleta matokeo mazuri zaidi baada ya upasuaji kufanyika..."
"Mm-hmm..." Namouih akaguna kwa njia ya kumaanisha daktari aendelee.
"Stage ya kwanza mpaka 3A ya saratani ya mapafu zinaweza kutibiwa kwa upasuaji, lakini kuanzia stage 3b mpaka 4 huwa wanatumia muunganiko kwa radiotherapy na chemotherapy pia kwa sababu upasuaji pekee hauwezi kusaidia level hizo za saratani. Yeye ana 3A, lakini kutokana na muda ambao mzee huyu ameishi nayo, itabidi, kama akipata upasuaji, uunganishwe na huduma ya radiotherapy au chemotherapy..."
"Mwili wake una uimara wa kutosha ku-handle aina yoyote ya upasuaji... au hizo therapy?" akauliza Efraim Donald.
"Ndiyo, naweza kusema ana nguvu sana kwa sababu angetakiwa hata kuwa ameshafika stage 4 lakini mwili wake ulikuwa unapambana nayo sana... sema ni umri tu. Kwa hali yake, mkiamua kumpa upasuaji wa kawaida, basi inatakiwa kuwa moja kati ya njia hizi: lobectomy au pneumonectomy. Kwenye lobectomy, sehemu kubwa ndani ya pafu lake iliyoathiriwa na saratani itaondolewa, hasa kwa sababu ya kwake imo ndani ya pafu moja. Na kwenye pneumonectomy... pafu lote litaondolewa," daktari akasema.
"Pafu lote?!" Namouih akasema kwa mshangao.
"Ndiyo, naelewa unawaza ikiwa baba yako ataweza kuendelea kupumua akibaki na pafu moja lakini usijali... inawezekana kupumua vizuri hata ukiwa na pafu moja tu. Kwa hiyo... hivyo ndivyo hali ilivyo," daktari Sunil akawaambia.
"Asante doctor kwa kutuelezea hayo. Tunataka kutumia njia bora zaidi itakayomsaidia. Upasuaji kama ulivyosema... ninaona kutakuwa na risk. Sidhani kama kuna nyenzo nzuri sana kwenye hospitali hii au yoyote itakayohakikisha ushindi... kumradhi lakini," Efraim Donald akamwambia.
"Ndiyo uko sahihi. Kiukweli... itahitajika apelekwe kabisa nje ya nchi kwenye hospitali iliyo na wataalamu wengi zaidi... huku kuna limit," daktari akaongea.
"Ahh... doctor yaani ndiyo unatuambia hayo sasa hivi?" Namouih akashangaa.
"Haingefika huku ikiwa asingekaa kwa muda mrefu hospitalini. Ingawa dawa anazopata zinasaidia lakini siyo kwa kasi inayotakiwa kusaidia apate matokeo mazuri kama angefanyiwa upasuaji wa cancer yake huku huku. Samahani sana kwa hilo dada," daktari Sunil akamwambia.
Namouih akafumba macho na kutikisa kichwa kwa kusikitika.
"Doctor... ninaomba mfanye mipango yote itakayohitajika kumtoa hapa na kumpeleka kwenye hospitali ambayo atapata matibabu hayo haraka sana," Efraim Donald akasema.
Namouih akamtazama usoni.
"Unamaanisha... nje ya nchi?" daktari Sunil akauliza.
"Ndiyo. Wapi itakapokuwa sehemu nzuri zaidi kumpeleka?" Efraim akamuuliza.
"The best option naweza kusema London... Ulaya," daktari akajibu.
"Okay. Ninaomba taratibu zianze kufanywa haraka. Tutagharamia kila kitu huku, na kitakachohitajika huko," Efraim akasema.
Daktari akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa, kisha akaanza kumpanga Efraim Donald kuhusu mambo ambayo yangefanyika ili kukamilisha hilo suala.
Namouih bado alikuwa anamtazama sana Efraim, asiamini kama kweli mwanaume huyo angejitoa kugharamia kila kitu kilichohitajika kwa ajili ya matibabu ya baba yake mpaka nje ya nchi. Mwanzoni lilikuwa jambo la kawaida tu kwa sababu alidhani kwamba matibabu ya baba yake yangefanyikia hapa hapa nchini, lakini mpaka nje ya nchi ingekuwa jambo zito na la gharama sana. Alihisi furaha iliyoambatana na mshangao kwa kutotegemea kabisa kwamba mwanaume huyu aliyemjua kwa siku mbili tu alikuwa anafanya haya yote kumwonyesha anampenda kwa dhati, na kiukweli aliguswa sana moyoni na kitendo hiki cha Efraim.
Efraim Donald alipomwangalia Namouih usoni, akakuta anatazamwa kwa njia yenye kuonyesha hisia nyingi sana za shukrani karibu machozi yamtoke mwanamke huyo, na mwanaume huyu akatabasamu na kumwonyesha ishara kwa kufumba macho kwamba asijali, kila jambo lingekwenda vizuri kabisa. Namouih akatabasamu kwa hisia sana, akiviunganisha viganja vyake vyote kwenye viganja vya Efraim Donald, na baada ya hapo wakatoka kwa pamoja kwenda kushughulika na mambo mengi waliyoambiwa na daktari.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments