Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Ysiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA SITA

★★★★★★★★★★★★★


Tukapanda daladala, nasi hao tukaianza safari fupi kuelekea Rangi Tatu. Tesha alikuwa amesimama mbele yangu, kukiwa na mwanamke mbele yake ambaye alibananiza mwili wake kwake. Kutokana na nywele za mwanamke huyo zilizobanwa kwa nyuma kusababisha ziutekenye uso wa jamaa, akawa anahamisha uso wake huku na huko, na kila mara mwanamke huyo alipojigeuza ama kugeuza shingo angefanya nywele zake zimtekenye jamaa usoni. 

Basi tukawa tunageukiana na kucheka kivyetu tu, nikielewa pia kwamba Tesha alipenda sana vitu vingi vilivyohusisha wanawake. Asili yetu yaani. Mpaka tumefika Rangi Tatu, mwanamke huyo mtu mzima kiasi na mwenye mwili mnono usio mrefu wala mfupi sana, alikuwa amesimama tu kwa ukaribu na Tesha, naye jamaa akaanza kumsemesha. 

Sikujua alimpiga swaga zipi lakini nilijua tu zilifanikiwa baada ya Tesha kumpa simu yake na mwanamke huyo kuipokea, kisha akaandika namba zake kabla ya sisi kushukia eneo hilo. Tukamwacha mwanamke huyo akikaa kwenye siti iliyoachwa wazi, ikionekana aliendelea na safari kuelekea Tandika. 

Tesha akawa ananiambia jinsi gani ilivyokuwa rahisi kwake kubeba namba za wanawake wengi na kisha kuja kuyajenga pamoja nao ili ajifurahishe, na alipendelea sana wanawake wenye umri mkubwa. Akaniambia kwa jinsi ambavyo nilikuwa nikitazamwa sana kutokana na sura yangu nzuri basi na mimi ningepaswa kuhakikisha naondoka na namba ya mwanamke mmoja maeneo hayo, lakini nikamwambia kiutani kuwa kitabu cha kutunza namba kwenye simu kilikuwa kimeshajaa baada ya yeye kunipa yake ile jana. 

Tulitembea eneo hilo kuelekea mpaka mitaa ya Zakhem, tukazunguka na kutazama sehemu nyingi zenye shuhuli na wanaharakati wengi. Palikuwa na uchangamfu unaoendana kiasi na eneo kama la Kariakoo ingawa si sana, naye Tesha akawa ameniambia anataka twende sehemu fulani iitwayo Kijichi ili akachukue pesa. 

Hakuniweka wazi wapi hasa, nami nikaridhia tu. Alionekana kuwa mtu aliyependa kuchukua maamuzi mengi mapya kufaana na hali inayokuwepo, yaani kama vile ambavyo alikuwa amepanga tuje tu kuzurura Mbagala Rangi Tatu halafu akapata wazo la kuchukua pesa sehemu nyingine ili mizunguko iongezeke zaidi. Na mimi nilipenda sana kuona maeneo mapya, kwa hiyo nikakubali na kumwacha aniongoze. 

Tukachukua usafiri wa bajaji kutokea Zakhem, nasi tukashuka na barabara ndefu mpaka maeneo ya Kijichi. Huku palikuwa na aina fulani ya utulivu zaidi, kusiwe na pilika kubwa kubwa sana kama kule tulikotoka, na baada ya kufika kituo cha Upendo, tukashuka. Tesha akalipa nauli na kuanza kunipeleka upande wa mbele zaidi, kisha tukaingia kwenye barabara ya kokoto za lami mpaka kufikia usawa wa jengo kubwa kiasi la bidhaa. 

Kwa haraka ningeweza kutambua kwamba sehemu hiyo ilihusika na shughuli za uuzaji wa bidhaa mbalimbali za jumla, ikiwa kama duka kubwa ama supermarket tu kutokana na muundo wake pamoja milango mipana ya vioo, na baada ya kuliona gari jeupe la Toyota pickup nililolifahamu vizuri sana, nikaelewa Tesha alikuwa amenipeleka wapi.

"Oy, hapa ndiyo kazini kwa sister," akaniambia hivyo.

"Naona. Hukuniambia kama tunakuja hapa lakini," nikamwambia.

"Si ndo' surprise sasa? Nyie watoto wa kishua si mnapenda hayo mambo?"

"Ah... nani kakwambia me wa kishua?"

"Unaonekana tu we ni wa kishua. Ama nimewrong namba?"

"Hahah... me mtoto wa mtaani tu kaka..."

"Acha kuzingua bana..." akasema hivyo huku tukielekea mlangoni.

"Ndiyo anafanyia kazi hapa?" nikamuuliza.

"Duka lake kabisa," akasema.

"Aaa... kumbe..."

"Yah..." akajibu.

Eneo la kuzunguka jengo hilo lilikuwa safi sana, na baada ya kuingia ndani humo, nikaona kukiwa na maboksi mengi yenye bidhaa za matumizi mbalimbali ya nyumbani, vyakula vilivyofunikwa, pamoja na vinywaji. Kulikuwa na friji kubwa kubwa zilizotunza vyakula baridi, barafu na vinywaji, na upande wa pembeni tu kutokea kwenye mlango huo wa kuingilia ilikuwa ni meza laini ya mbao iliyowekewa kompyuta. 

Kwenye kiti katikati ya meza hiyo aliketi mwanamke mweupe aliyevalia baibui jeusi pamoja na ushungi mweupe uliofunika kichwa na kuacha uso wake nje. Macho yake makubwa kiasi yalituelekea sisi, na Tesha akasogea mpaka hapo mezani huku mimi nikiwa nyuma yake.

"Mamacita... nakuona..." Tesha akamwambia hivyo huku akitabasamu.

Mwanamke huyo alikuwa Mamacita kwelikweli, naye akatoa tabasamu lililofanya mashavu yake yatokeze vishimo vilivyompendezesha zaidi, halafu akaniangalia usoni. Nikasimama usawa wa meza pia na kumtazama machoni.

"Mtoto umependeza kama kawaida yako. Uko poa?" Tesha akamsemesha hivyo.

Akasema, "Niko poa. Karibu."

"Eeeh? 'Korribu' yaani umeing'ata kama mzungu vile! Shauri ya kumwona pedeshee hapa, ama nini?" Tesha akamtania.

Mwanamke huyo akacheka kidogo kwa haya, huku mimi nikimwangalia tu kwa macho yenye upendezi na tabasamu hafifu.

"Oy, huyu ni Soraya... au Tausi. Mtoto mweupee na mwepesi zaidi ya tausi," Tesha akaniambia hivyo.

Soraya akasema, "Ila wewe, nishakukataza kuniita mtoto. Si nalingana na dada yako?"

"Aaa kwo' unataka niwe nakuita kikongwe?" Tesha akamuuliza.

"Eee, tena ndiyo inafaa..." Soraya akasema.

"Mm? Haya bana. Sister yupo?" Tesha akauliza.

"Yupo," Soraya akajibu.

"Ngoja nimcheki Mimi faster. Nakuja," Tesha akaniambia.

"Poa," nikamjibu.

Akaanza kuuelekea mlango wa chumba kingine ndani hapo ulioonekana kwenda ndani ya ofisi ya dada yake, naye akawa anamwonyesha Soraya ishara ya vidole kunielekea mimi; kama kusema amemwachia mimi ili tuongee. 

Nikatabasamu kidogo tu na kumwona akiingia ofisini humo, nami nikamtazama Soraya usoni. Alikuwa na mwonekano fulani hivi wa kiarabu kutokana tu na namna alivyojiweka, nami nikaanzisha maongezi.

"Mambo vipi?" nikamsemesha.

"Poa tu. Karibu sana," akanijibu.

"Asante. Sehemu nzuri sana hapa..."

"Ee... mwanzoni hapakuwaga pamejaa namna hii, sa'hivi angalau vitu vinaongezeka... biashara inakua," akaniambia.

"Mnauzaga bidhaa kutoka kampuni moja?"

"Hamna, tunachukua kutoka kampuni mbalimbali. Azam, Jambo, Mo... ndiyo tumevijaza hapa..."

"Ahaa... na kwa huku wateja wengi wanasogea eh?" 

"Sana. Hii mitaa tuko sisi tu hapa, kwa hiyo wa madukani na watu wengi binafsi huwa wanachukulia vitu kutokea humu... then wanaenda kuendeshea shughuli zao pia..." akasema hivyo.

Alikuwa na sauti nzuri, isiyo nyembamba sana, nami nikampa tu uhakikisho wa kwamba nimeelewa alichosema kwa kutikisa kichwa kidogo. 

Akashika mouse ya kompyuta kwa kiganja chake cheupe kilichorembwa kwa michoro ya yna na kucha ndefu vidoleni zilizopakwa rangi nyekundu, na kwa sauti ya chini kiasi akauliza, "Unaitwa nani?"

"JC," nikamjibu.

"JC?"

"Ndiyo. Herufi mbili tu," nikamfahamisha zaidi.

"Sawa," akajibu hivyo.

Niliona aina fulani ya uvutio kutokana na namna alivyonitazama, na alionekana kuwa mpole sana. 

Nikamuuliza, "Umeolewa?"

Akaniangalia na kutabasamu kiasi, naye akatikisa kichwa kukubali.

"Wanao hawajambo?" nikamuuliza.

"Wazima. Sijui wakwako?"

Alipouliza swali hili, nikatulia kidogo nikitazama chini, kisha nikamwambia, "Sina watoto."

"Kwa nini?"

"Muda bado."

"Kwani unataka kupata mtoto ukifikisha miaka mingapi?"

"Labda 40 hivi..."

Akacheka kidogo na kutikisa kichwa.

"Kweli, ama ni vibaya?" 

"Hamna siyo vibaya, ila wanao watakuita babu maana utazeeka bado wadogo..."

"Hamna... wanaume hatuwahi kuzeeka kihivyo..."

"Sawa. Ni jambo jema," akaniambia.

"Yeah..."

"Kwa hiyo bado haujaoa?" 

"Bado."

"Kwa nini usioe sasa?"

"Ndoa siyo jambo la mchezo dada. Ni kitu kizito. Muda ukifika nitaoa tu. Na hata nikisema niamue kuwa na mwanamke na kuishi naye kama mke wangu, naweza... lakini ile kufunga kabisa pingu za maisha linakuwa jambo la kuweka akiba ya mbeleni kwanza..." nikamwambia.

"Mh? Hayo mawazo vijana wengi wanayo, lakini sioni kama ni sahihi. Unakuwa unacheza na watoto wa watu tu..." akaniambia hivyo.

Nikacheka kidogo.

"Hahah... si ndiyo? Na wewe ndiyo unafanya hivyo?" akaniuliza.

"Hamna bwana. Ama naonekana kama muhuni sana?"

"A-ah sijasema hivyo. Ila vijana wengi ndiyo mnafanya hivyo siku hizi. Ni bora kuoa mwanamke ukatulia naye ndani tu," akasema.

"Hakuna kitu kama kutulia ndani tu siku hizi dada'angu. Ndoa nyingi ziko kwa ajili ya fashion... kujionyesha tu, lakini bado hakuna anayetulia na mwenziye mmoja bila kutoka nje. Nadanganya?"

"Hapana, ni kweli..."

"Eee... ni vyema ukipata mtu aliyetulia, kweli mtatulia. Ila muda ukipita tu mkaanza kuonana kama ng'ombe aaa imeisha hiyo..." 

Kauli hiyo ikamfanya acheke na kufunika mdomo wake kwa vidole viwili; shau yaani. 

"Umeona? Na hayo mambo siyo kwa sisi wanaume tu, mpaka wanawake. Ukishajua mwenzio anacheat na we' unatafuta wa kukutuliza... kinachofata ni kuachana kama siyo kuuana, watoto wanabaki kuteseka. Faida gani? Ila ni bora tu kufanya vile moyo wako umeridhia, yatakayokuja ndiyo yatakayokuja. Basi," nikamwambia hivyo huku nikitabasamu.

Akawa anatabasamu pia, naye akasema, "Yote hayo ni kweli. Kila mtu ana maamuzi yake."

"Ndiyo hivyo. Mume wako anaweza kuamua kutembea na dada yako au rafiki yako na wewe usijue. Hata wewe ukiamua kuzaa na mimi na ukampeleka huyo mtoto alelewe na mume wako akidhani ni wake, unashindwa nini? Ndiyo system zililivyo siku hizi. Watu wanaishi kwa maamuzi wanayoona yanawafaa, kwa hiyo unaishi tu upendavyo ili life lisonge," nikamwambia hivyo.

Inaonekana aliingiza maneno hayo akilini mwake kwa utafakari wa kina sana, kwa sababu alinitazama machoni kwa mkazo mwepesi; yaani kama anajaribu kunisoma vile. Mimi kwa ubora wangu wa kuzungumza nilikuwa nimemwonyesha tu kwa maneno namna ninavyoona mambo, lakini nadhani nikawa nimeiingizia akili yake jambo fulani ambalo lilisisimua fikira zake.

Akaangalia chini na kutabasamu kwa njia ya shau, nami nikasema, "Kwa hiyo watoto na ndoa... vitakuja tu. Sa'hivi ni kutulia."

Akaniangalia na kuuliza, "Na kuula ujana?"

"Haswa!" nikamwambia hivyo kiutani.

Sote tukacheka kidogo, na hapo hapo mlango wa ofisi alikoingia Tesha ukafunguka. Jamaa akatokeza kidogo na kuniita kwa ishara ya kiganja, nami nikajiweka sawa na kuanza kwenda. Labda dada yake alitaka kuniona, ama Tesha ndiyo alitaka nimsalimie, yote ningeyajua hapo ndani.

Nikaingia ofisini humo. Palikuwa pazuri sana. Sehemu simple tu yenye usafi wa hali ya juu. Kulikuwa na masofa mawili mafupi upande wa mbele zaidi usawa wa dirisha lenye vioo vyeusi, picha kadhaa zilizotundikwa ukutani na hati za utambulisho wa masuala ya kikazi kama karatasi za TRA vile, na shehena fupi yenye madaftari na makablasha. 

Pembeni kutokea kwenye yale masofa ndiyo kulikuwa na meza ndefu kiasi ya mbao nzito iliyotengenezwa kwa ubunifu, iliyowekewa viti vyeusi vitatu kuizunguka; kimoja upande mmoja na viwili ule mwingine. Kwenye hicho kiti kimoja ndiyo alikaa mkurugenzi niliyetambulishwa kwake jana usiku, bibie Miryam. Na alionekana makini kweli. 

Kama kawaida, mwonekano wake ulivutia. Alivaa blauzi ya njano yenye mikono mirefu, bila shaka kwa chini akiwa amevaa sketi ndefu ingawa sikuiona vyema, na niliweza kuona ndala laini za kike zenye rangi ya njano miguuni. Uso wake ulipendeza sana, naye alikuwa ameweka viwiko vyake vyote mezani huku akiwa ameshika kalamu na kuizungusha-zunguza vidoleni, na mezani hapo pia kulikuwa na laptop aina ya HP. 

Tukasimama na Tesha usawa wa viti vile viwili, naye Miryam akawa ananitazama machoni kwa utulivu.

"Umemwona bosi?" Tesha akaniuliza hivyo.

"Nimemwona," nikasema hivyo bila kuacha kumtazama Miryam usoni.

Miryam akamwangalia mdogo wake.

"Si ulikuwa unafikiri nakudanganya? Huyu hapa sasa," Tesha akamwambia hivyo.

Miryam akaniangalia tena.

"Habari za kazi?" nikamuuliza.

"Nzuri. Uko poa?" akaniuliza na mimi.

Aisee! Hako kasauti! Yaani hata hakuilazimisha iwe tamu namna hiyo lakini iliposikika kwangu yaani niliipenda sana. Sijui alikuwa anafanyaje tu hapo kooni!

"Niko fresh kabisa," nikamjibu kiunyoofu.

"Da' Mimi nimemwambia niko nawe tunatembea, akafikiri namzingua. Ndo' nimekuita akuone. Unajua sister anakukubali kinoma toka umemwokoa Mariam..." Tesha akaniambia hivyo.

Nikamwangalia Miryam na kuona anatazama chini huku akitoa tabasamu hafifu la kuhukumu, ile njia fulani ya mtu mzima kuona kila kitu mdogo wake anachosema kuwa upuuzi au utoto tu, nami nikajikaza nisitabasamu na kumwambia Tesha kwa ishara ya mdomo 'ila wewe!'

Jamaa akacheka kidogo kwa pumzi, naye akamwambia dada yake, "Tumezunguka hapo Zakhem ndo' nikaona tupite na huku kukusalimu. Unapiga sana kazi dada."

Tayari nilikuwa nimeshasoma kile ambacho Tesha alikuwa amekuja kufanya hapa, na dada yake akanipa uthibitisho zaidi. Hakuzungumza wala. Akatoa tu shilingi elfu ishirini na kumpatia mdogo wake, naye Tesha akazipokea huku akitabasamu. Akaniangalia kwa yale macho ya kuonyesha kwamba alikuwa amepata ushindi, ikiwa wazi alikuja pamoja nami sehemu hii kumwomba dada yake hela.

"Asante Mimi. Sisi ngoja tusepe sasa. Bado namwonyesha shujaa wetu mitaa," Tesha akamwambia hivyo.

"Haya. Umemwachaje Mamu lakini?" Miryam akamuuliza hivyo.

"Yuko poa. Tukitoka mizunguko tunaingia skani tena kumcheki," Tesha akamwambia.

"Sawa. Matembezi mema," Miryam akatuambia hivyo.

"Poa," Tesha akamjibu.

Tukiwa tunaanza kuuelekea mlango, nikamwambia Miryam, "Kwa heri."

Macho yake yalinikazia tu mimi kwa umakini, naye hakutoa jibu isipokuwa kunitikisia kichwa kidogo kuonyesha ameikubali salamu yangu ya kuaga. Nikatoka ndani ya ofisi hiyo huku nikiwa natabasamu kiasi, shauri ya kukumbukia jinsi nilivyokutana na mwanamke huyo mara ya kwanza kabisa mpaka kufikia sasa. 

Tukawa tumeifikia meza aliyoketi Soraya hapo nje ya ofisi, ikiwa wazi zaidi sasa kwamba mwanamke huyo alifanya kazi kama msaidizi wa Miryam, na nilipendezwa na jinsi walivyojiweka kiumakini wa kikazi; wazungu wanasema "professionalism."

"Mtoto Soraya, sisi tunaenda sasa," Tesha akamwambia hivyo.

"Haya sawa, karibuni," Soraya akasema hivyo na kuniangalia.

"Haumuulizi pedeshee atarudi lini?" Tesha akamuuliza hivyo.

Nikatabasamu kidogo, naye Soraya akacheka kidogo pia.

"Kwetu lini sasa?" Tesha akamuuliza tena.

"Nitakuja tu," Soraya akamjibu.

"Lini?" Tesha akauliza kwa msisitizo.

"Nitakapoamua. Siyo lazima ujue kama wewe ulivyofika tu hapa," Soraya.

"Au siyo? Oya, chukua namba za mtoto. Mali safi hii, siyo ya kula kwa macho tu," Tesha akaniambia hivyo.

Nikacheka kwa pumzi tu.

"We! Nitakuchapa? Niheshimu, mi' dada'ako..." Soraya akamwambia hivyo huku akimnyooshea kidole.

"Acha kuzingua, JC ndo' habari ya jiji. Ama unaona aibu? Basi ngoja nitangulie, nimwache. Oy... changamka..." Tesha akasema hivyo.

Akanipiga begani kidogo na kunipita, akitoka nje kabisa na kuniacha hapo. 

"Huyu mtoto huyu!" Soraya akasema hivyo.

"Ahahah... ni mtundu. Ungependa tuwe tunawasiliana lakini?" nikamuuliza hivyo.

Akaniangalia na kutabasamu kiasi, naye akatikisa kichwa kukubali.

Nikatoa simu yangu na kuweka sehemu ya kuandikia namba, nami nikampatia. Hatukusemeshana lolote lile mpaka alipomaliza kuandika na kunirudishia, kisha nikaipigia namba yake kwa ufupi ili yakwangu ifike kwake. Simu yake iliyokuwa mezani ikaita, naye akaichukua na kuniangalia huku anatabasamu kwa mbali.

"Sora..."

Soraya na mimi tukaangalia upande wa mlango wa ofisi ya Miryam, na hapo tukamwona mwanamke huyo akiwa ametoka huku ameshika karatasi mkononi. Nadhani ndiyo alikuwa ametoka tu na kutaka kumwita msaidizi wake ili amwambie jambo fulani, lakini baada ya kuniona hapo maneno yake yakakatishwa.

Soraya akasimama na kuitika, "Abee..."

Miryam akaendelea tu kuniangalia, nami nikabana midomo kiasi na kumtikisia kichwa mara moja kama kuaga, kisha nikatoka ndani hapo. 

Sasa kilichoendelea hapo ndani ndiyo ambacho sikukijua, lakini ilikuwa rahisi kufikiri kwamba Miryam angedhani nilikuwa namtongoza msaidizi wake huyo. Angeniona kuwa bonge moja la muhuni, na hiyo ingeniharibia CV yangu nzuri kwake niliyoijenga kwa kumwokoa mdogo wake. 

Ila nisingeweza kujua saaana yaliyoendelea mpaka kuhukumu mambo kwa njia hiyo kwa sababu Miryam hakuonekana kuwa mwanamke mwenye kujali mno mambo ya wengine. Sema ni kale kahisia tu ka 'atanifikiriaje tena' hasa kutokana na historia yetu ya mara ya kwanza tulipokutana.

Nikamfikia Tesha, ambaye alikuwa akizungumza na simu, nasi tukaanza kutembea kuielekea barabara. Tukasimama sehemu ya kusubiria bajaji ili turudi kule Mbagala, nayo ikafika na kutubeba. Alipomaliza kuongea na mtu wake ndiyo story zikaanza. 

Aliuliza kama niliondoka na namba ya Soraya, nami nikakubali. Akasema nihakikishe natoka na yule mwanamke yaani kwa hali na mali zote, hata nikitaka anilipie chumba kwingine ili nisimuudhi Ankia kwa kupeleka mwanamke pale nyumbani basi angenilipia. Tesha alipenda sana hizi mambo! 

Mimi nikamweka wazi tu kwamba Soraya nilimwelewa, lakini haikuwa kwa njia hiyo ya kunisukuma nianzishe uhusiano naye wa kimapenzi, hasa kwa sababu wake za watu sikuzote ni sumu. Nikamwambia hayo mambo niliyafanya zamani sana kwa hiyo niliviona kuwa vitu vya kawaida mno, na sikuhitaji papara kushughulika navyo. 

Soraya angekuwa kama rafiki tu, na kuchukua namba yake ilikuwa njia ya kumridhisha tu jamaa lakini haikuwa imeniongezea uzito wowote wala haingepunguza lolote kwangu hata kama nisingeichukua. 

Kwa Tesha maoni kama hayo yalikuwa ya kizee maana yeye alikuwa amechacharika vibaya mno, lakini alinielewa vizuri zaidi kuona kwamba nisingeweza kusukumwa kufanya mambo nisiyotaka kufanya hata kama aliyetaka niyafanye alikuwa mtu wa karibu; labda tu iwe ili kuondoa kero, na hali za kuyafanya ziwe zinaruhusu.

★★

Hatukuchukua muda mrefu sana kuondoka Mbagala baada ya mimi kuwa nimenunua kofia ya kunikinga na jua, pamoja na Tesha kununua kacha nzuri za mkononi na kunipatia moja kama zawadi. Nilimuuliza Tesha ikiwa dada yake hufanya kazi mpaka usiku kwenye siku za wikiendi, naye akasema Jumamosi tu ndiyo Miryam huenda huko dukani kwake kwa siku za wikiendi, na huwa anawahi kurudi tu labda kama akitaka kupita sehemu zingine baada ya kumaliza shughuli zake. 

Tukarudi nyumbani ikiwa imeingia saa kumi na moja na nusu, naye Tesha akanipeleka mpaka pale kwao. Sikwenda hata mara moja kwa Ankia. Ndani pale, tuliwakuta mama zake wakubwa, pamoja na yule mwanamke aliyeitwa Shadya, bila shaka wakiwa wanaongea mambo fulani. 

Zawadi mweupe akanikaribisha vyema, na mwenzake akiwa anachambua mchele akawa amenikaribisha vyema zaidi kwa kutoka kwenye sofa alilokuwa amekaa ili mimi ndiyo nikae hapo, naye akakaa pamoja na Zawadi mweupe. Tesha akaketi sofa moja na Shadya, mwanamke huyo akiwa ananitazama sana usoni.

"Za huko mlikokuwa?" Zawadi mweupe akaniuliza.

"Nzuri tu mama," nikamjibu kiunyoofu.

"Mlienda mpaka wapi?" yule mwenzake mweusi akamuuliza Tesha.

"Hapo Zakhem, tukaenda mpaka kwa da' Mimi pia," Tesha akamwambia.

"Aaa... mmemkuta? Anasemaje?" Zawadi mweupe akaniuliza hivyo.

Nikatabasamu na kusema, "Yupo. Anaonekana makini na kazi."

"Eee... mchapakazi sana," Zawadi mweupe akasema.

"Siyo kama hili," Shadya akasema hivyo, akimaanisha Tesha.

Sote tukacheka kidogo, naye Tesha akamwambia Shadya, "Ih, hivi kumbe nawe upo hapa? Umefika saa ngapi?"

"Unachange mosheni eh?" Shadya akamuuliza hivyo kwa nyodo.

"Ah... umeniingiza kwenye mada isiyonihusu..." Tesha akamwambia.

"Baba, unaendeleaje? Mkono bado unauma?" yule mama mkubwa mweusi akaniuliza.

"Ah, si sana. Kufikia kesho utakuwa umepoa zaidi, nitaitoa na hii bendeji," nikamjibu.

"Hivi unaitwa nani?" Shadya akaniuliza.

"JC," nikamjibu, huku nikimwangalia kwa umakini.

"JC. We' ni mtu wa wapi?" akaniuliza tena.

"Mwanza," nikamjibu kifupi.

"Unafanya kazi gani?" akaniuliza tena.

Sikumjibu haraka, bali nikawa namwangalia tu machoni kwa mkazo.

"Ushaanza upelelezi wako Shadya..." Tesha akamwambia.

"We' naye, nimeongea na wewe?" Shadya akamuuliza kwa kukereka.

"Si umwache amjibu?" Zawadi mweupe akamwambia hivyo Tesha.

"Ah, ma' mkubwa kwani hujui mambo ya Shadya? JC akishamsemesha kidogo tu yatafika kwa mjumbe!" Tesha akasema.

"Unapenda kudakia maongezi ya wakubwa ili iweje? Nilikusemesha wewe?" Shadya akamuuliza.

"Basi jamani..." Zawadi mweupe akajaribu kuwatuliza.

"Sitaki umsemeshe sasa! Tuzoee sisi wengine, JC usimzoee..." Tesha akamwambia hivyo.

"Tesha..." mama mkubwa wake mweusi akamwambia hivyo kama kumzuia.

"Sijui linajionaje!" Shadya akasema hivyo.

"Najionaje nini? We' nakujua. Hata hiyo ishu ya juzi na da' Mimi najua ushaisambaza kwa watu maana una mdomo mrefu kweli! Utafikiri alikulazimisha umlete yule jamaa..." Tesha akamwambia.

"He! Yamekuwa hayo? We' yanakuhusu nini? Nilimleta akuoe wewe?" Shadya akamuuliza.

"Si alitimuliwa lakini?" Tesha akamwambia.

Zawadi mweupe akacheka kidogo.

"Ulikuwepo? Si ulikuwa huko unazurura tu? Una kiherehere wewe, na siyo ajabu unampandikizia dada yako ujinga mpaka anakataa kuolewa wakati umri unaenda. Umemgeuza awe kama mama yako, we' umekaa tu halafu unajiita mwanaume!" Shadya akamshushua.

"Eee! Usinitibue, n'takufukuza sasa hivi!" Tesha akamwambia kwa kuudhika.

"Unifukuze we' ndo' umenileta?" Shadya akamuuliza kwa shari.

Ilikuwa imegeuka kuwa ugomvi sasa. Kisa? Shadya kanisemesha. Nikatulia tu na kuangalia chini.

"Ila nyie, yaani hamwoni hata kuna mgeni hapa jamani?" mama mkubwa mkubwa akasema.

"Eti? Utafikiri mmeoana!" Zawadi mweupe akasema hivyo.

Nikacheka kidogo kwa pumzi.

"Ah, anazingua..." Tesha akasema.

"Nazingua nini? Yaani we' hauna adabu. Dawa yako inachemka," Shadya akasema.

"Ichemshe tu mpaka ikauke! Mwaka huu sikuachi. Uache umbeya, na uache kumtafutia dada wachumba. Hataki!" Tesha akamwambia hivyo.

"Haya Tesha, naomba ukae kimya! Inatosha," mama mkubwa mweusi akamwambia.

Tesha na Shadya wakaangaliana kwa chuki, na mama zake wakubwa wakanitazama na kutikisa vichwa vyao tu.

"Mariam anaendeleaje?" nikauliza hivyo ili kukatisha ukimya.

"Ah, salama. Yuko ndani, ngoja nimwite akusalimie. Mariam..." Zawadi mweupe akasema hivyo na kumwita binti.

Haikusikika sauti ya binti yule akiitika, naye Zawadi mweupe akamwita kwa mara nyingine tena bila kurudishiwa jibu.

"Ngoja nikamfate..." Tesha akasema hivyo.

Akanyanyuka na kuanza kuelekea upande wa vyumba, ikionekana alikwenda kwenye kile chumba cha Miryam alikonipeleka mwanamke huyo siku ya kwanza nimefika hapo. 

Mama mkubwa mweusi akanyanyuka pia pamoja na ungo wake wenye mchele na kwenda jikoni, kisha akarudi mikono mitupu na kukaa pamoja na mwenzake. Shadya alikuwa ananiangalia sana, yaani akinionyeshea wazi kabisa kwamba alitaka nimwone ananitazama ili nami nimpe umakini wangu, lakini nikawa nawaangalia tu mama wakubwa.

"Ankia alikuja hiyo mida ya mchana kumsalimia pia... ndiyo akatuambia mmeondoka na Tesha kwenda kutembea. Tesha amekupenda sana," mama mkubwa mweusi akaniambia.

"Aaa... ahah... ndiyo. Ananikubali sana. Hata mimi pia namkubali," nikasema.

"Unamaanisha, hata Mimi pia unamkubali?" Zawadi mweupe akaniuliza.

"Ah... hapana... nimemaanisha..."

"Amemaanisha YEYE pia anamkubali Tesha. Hajasema Mimi ya Miryam..." mama mkubwa mweusi akamwambia Zawadi mweupe kumsahihisha.

"Aaaa... hahahah... nimeelewa kushoto. Kama ujuavyo, majina na mazoea..." Zawadi mweupe akasema.

Sote tukacheka kidogo kwa pamoja.

"Basi hiyo jana jioni baada ya ile ajali, nilimshukuru sana Mungu kwa kukuleta hapa baba. Yaani umekuja ghafla tu lakini ni kama Mungu alikuleta ili umwokoe msichana wetu. Ulitufariji sana," Zawadi mweupe akasema hivyo kwa sauti tulivu.

Nikatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kwa uelewa. Nikatambua pia alikuwa mtu wa imani sana.

"Tulimwambia Miryam... yaani! Alikuwa amechanganyikiwa akidhani mdogo wake ameumia vibaya. Mliongea kuhusu hiyo ishu?" mama mkubwa mweusi akaniuliza.

"Ee... ndiyo, tuliongea. Ali... alinishukuru," nikampaka Miryam mafuta mazuri.

"Hata sisi tunakushukuru sana. Hawa watoto tunawapenda mno," Zawadi mweupe akasema hivyo.

"Nimesikia ulimrukia kama Tarzan eti..." Shadya akanisemesha pia.

Nikatabasamu kidogo, na ni hapo ndiyo nikamwona Tesha akiwa anakuja pamoja na mdogo wake hatimaye. 

Akiwa ameshikwa mkono kuongozwa na kaka yake, Mariam alionekana kuwa kama ametoka usingizini vile, uso wake ukiwa umevimba kiasi na macho kuwa lege. Alikuwa amevaa dera pana, huku nywele zake ndefu zikiwa zimevurugika kiasi, naye Tesha akamleta mpaka kwenye sofa nililoketi na kumkalisha karibu yangu, naye akakaa nasi pia. Yaani Mariam akawa katikati yetu mimi na Tesha, nami nikaingiza puani harufu nzuri ya manukato kama ya dada yao kutoka kwa binti huyu. 

Nikawa namwangalia tu huku nikitabasamu kirafiki, lakini nikitumia sekunde hizo chache kumtathmini zaidi.

"Mariam, umemwona kaka?" Zawadi mweupe akamsemesha.

Mariam akanitazama usoni kifupi sana, kisha akaangalia chini tena.

"Mwamkie," Tesha akamwambia hivyo huku akiwa amelishika bega lake kwa ukaribu.

Lakini binti huyo hakutamka neno lolote. Nikamwangalia vizuri zaidi na kuona jinsi kichwa chake na macho yake yalivyokuwa na aina fulani ya mtikisiko wa mbali sana, mtu mwingine angefikiria labda ni madoido, lakini nikatambua kwamba haikuwa hivyo. 

Kihalisi, kwa mwonekano wake wa miaka ya utineja, kuambiwa na kaka yake amwamkie mtu mzima ni jambo lililoonyesha kuwa alihitaji kukumbushwa kufanya vitu fulani rahisi sana hata kwa mtoto mwenye miaka 10 kukumbuka kufanya. 

Shadya akamsisitizia jambo hilo kwa kusema, "Mwamkie kaka. Si unamkumbuka? Alikusaidia jana usigongwe na pshh... gari."

Lakini hata kwa msisitizo huo, Mariam akaendelea tu kutazama chini. Nikaona nijaribu jambo fulani. Nikakichukua kiganja chake cha mkono wa kulia na kukinyanyua mpaka kufikia kwenye paji la uso wangu, nami nikakiweka hapo. Alinitazama usoni, na wengine wakawa wanatutazama pia.

Nikamwambia binti, "Marahabaaa... hujambo?"

Mariam akaachia tabasamu pana huku pumzi zake zikipanda na kushuka haraka kuonyesha furaha, uso wake ukipendeza sana alipotabasamu namna hiyo, naye akaangalia pembeni huku akiendelea kufanya hivyo. 

Nikakiachia kiganja chake huku mimi pia nikiwa natabasamu, na kwa kiasi fulani nikiwa nimeanza kuielewa hali ya huyu binti. Mama zake wakubwa walikuwa wanatutazama huku wakitabasamu, naye Tesha akaniangalia kwa umakini.

"Alikuwa amesinzia kabisa?" nikamuuliza hivyo jamaa.

"Ee... alikuwa amelala," akanijibu.

"Ungemwacha tu apumzike, si unajua usingizi ulivyo mtamu?" nikamwambia hivyo.

"Haina shida sana," mama mkubwa mweusi akasema.

"Eeh, akilala sana mchana usiku anaanza kusumbu..."

Nikiwa namwangalia Shadya alipokuwa anataka kusema jambo fulani kwa maneno hayo, ndiyo akawa ameyakatishia hapo kwa kilichoonekana kuwa kuzuiwa asiendelee kuzungumza. Labda kwa ishara ambayo mmoja wa wale mama wakubwa alimpa bila mimi kuiona.

Nikamgeukia Tesha na kuuliza, "Akilala sana mchana... ni vibaya?"

"Hamna... yaani... anaumwa-umwa, sawa? Anapata shida kulala usiku akitumia masaa mengi mno kulala mchana yaani... usingizi hapati. Hivyo," Tesha akaniambia.

Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa. 

Ilionekana kuwepo na mambo mengi sana kuelekea suala la msichana huyo kuwa namna hiyo lakini watu hawa hawakutaka kuzama zaidi ndani ya hizo mada; hasa kuziongelea na mgeni kama mimi. Na ilieleweka. 

Lakini, kutokana na mambo yote ambayo Ankia alikuwa amegusia kwangu kuhusu Mariam, na hilo jaribio dogo nililofanya hapo la kutoa salamu, nikawa nimeingiwa na wazo fulani kuhusu hali ya binti huyu; wazo ambalo bado sikuwa na uhakika wa asilimia zote kwamba lilikuwa sahihi. Kwa hiyo ningetakiwa kumwangalia vizuri hata zaidi ili niweze kumwelewa. Ni kwa sababu tu nilitaka kumwelewa, na labda kwa njia fulani... kumsaidia.

Basi baada ya hapo, Zawadi mweupe akawa ameuliza ikiwa tulikuwa tumeshakula ili aweze kuharakisha maandalizi ya kupika nasi tule pamoja, lakini Tesha akamwambia asiwe na hofu; tulikuwa vizuri tu, na tulipanga kutoka kwenda kutazama mechi. Tukaendelea kukaa-kaa hapo mpaka ilipofika saa moja kasoro robo saa, nasi ndiyo tukaaga kutoka. 

Mpaka kufikia muda ambao tulitoka ndani hapo, Mariam hakuwa amenena chochote kile zaidi ya kututazama mara moja moja sana, akiwa na zoea la kucheza na vidole vyake mwenyewe na kung'ata kucha kwa wingi, nami nikaondoka na Tesha huku akiba ya suala la binti huyo bado likiwa akilini.

★★

Mguu mmoja na rafiki yangu mpya mpaka kufikia Masai, nasi tukaingia kwenye kumbi hiyo na kukuta watu wakiwa ni wengi sana. Waliojaza nafasi za kukaa walikuwa ni mashabiki wa Simba, pamoja na mashabiki wachache wa Yanga waliokuja kuwazomea bila shaka, na wahudumu wa hapo walionekana kuwa bize kusambaza huduma. 

Nilikuwa nimemuuliza Tesha kuhusu Shadya, nikitaka kujua walikuwa na undugu wa karibu kiasi gani. Akawa ameniambia Shadya hapo kwao wanamwona kama shangazi kwa sababu alikuwa ni rafiki wa karibu zaidi na marehemu mama yao, na walisaidiana kwa mengi mno. Akasema amemjua tokea yupo darasa la tano, kwa hiyo wanamwona kama ndugu wa karibu zaidi. 

Akaeleza kwamba mwanamke huyo alikuwa na duka la nguo kule Mbagala, na alikuwa ameolewa pia. Watoto wake wawili kwa wakati huu walikuwa Tanga kimasomo, huku yeye akiishi na mume wake maeneo ya Kongowe kusiko mbali sana na mitaa hii ya Mzinga. Akawa amenionya eti niwe mwangalifu naye maana alipenda sana porojo, lakini akakazia kuwa alimpenda pia na alimwona kuwa wa muhimu mno kwa sababu ya ushikamanifu wake na familia yao. Hilo likawa limeniingia vizuri kichwani.

Kwa sababu hii ilikuwa ni Jumamosi yenye uwepo wa mechi ya timu pendwa kama Simba, nilikuwa nimetarajia idadi ya watu kuwa kubwa mapema tu, na kuingia kwetu hapo kukafanya macho yatuelekee kama kawa. Tesha akaniongoza kufikia sehemu aliyosimama DJ, DJ huyo akiwa amekingwa na kiukuta kifupi cha mbao zilizochorwa majina kwa mitindo ya kibunifu, naye Tesha akaanza kusalimiana na wanaume wawili waliokuwa wamesimama hapo. 

Mmoja alikuwa mfupi kwangu, lakini mwingine alikuwa mrefu hadi kunipita, mweusi, mwenye ndevu nyingi kutokea kwenye timba mpaka kufikia kidevu. Alisalimiana na Tesha kwa njia yenye uchangamfu mkubwa, na jamaa akanitambulisha kwake kwa kusema huyo ndiyo alikuwa Bobo. Yeah. Yule rafiki yake ambaye ni meneja wa hapo Masai, Bobo, ndiyo alikuwa huyo jamaa tolu. 

Alionekana kuwa mtu makini na mwenye nguvu sana, nasi tukasalimiana na kufanya maongezi mafupi ya kupatana, na akaonekana kunielewa sana. Tesha akamwambia tunatafuta sehemu ya kukaa ili tulicheki game vizuri, lakini hapo palionekana kujaa, hivyo Bobo akamwita mhudumu mmoja wa hapo na kumwelekeza atupeleke kule kwenye kumbi ya VIP. 

Kalikuwa keusi, kembamba, kamekomaa, nako kakatupeleka huko huku Bobo akisema angekuja kujiunga pamoja nasi. Tesha alikuwa amefikiria kuniingiza VIP mapema sana leo ila muda huo hata kama tungepata viti pale kwa watu wengi, basi tungekaa. 

Huyo mdada akatufungulia mlango wa chumba cha maVIP, nasi tukaingia. Hakikuwa kipana, bali kirefu. Kulikuwa na masofa mazuri pande zote za ukuta, meza za mbao nzito katikati, michoro ya urembo kwenye kuta, mlango wa chumba kingine mbele zaidi kilichoonekana kuwa choo, na TV kubwa ya flat screen iliyotundikwa juu kwenye ukuta wa usawa wa mlango tulioingilia. 

Tayari kwenye runinga hiyo ilikuwa imeshawekwa chaneli yenye kuonyesha mechi hiyo, wachezaji wakiwa ndiyo wanaanza kucheza, nasi tukakaa. Tesha akamwambia huyo dada atuletee bia za Serengeti Lite nne za moto kwanza, naye akachukua hela na kutuacha.

"Ah, mwana unaona vile watu wanatuangalia tukiingia hapa?" Tesha akaniuliza.

"Naona. Wanafikiri tuna pesa sana, au?"

"Wewe sanasana. Halafu wanafikiri mimi ndiyo nimekuleta huku ili kukudandia sasa..."

"Hahah... wakati wewe ndiyo pedeshee hapa..."

"Umeona? Hahahah... ila umepaonaje hapa? KaVIP kazuri eh? Kametulia, hakana mambo mengi, ama nini?" Tesha akaniuliza.

"Yeah. Pako poa. Ankia hakukosea lakini aliposema inafanana na sebule yake," nikasema hivyo.

Akacheka kidogo na kuniambia, "Fitina tu. Amekorogwa leo."

"Naona kama Chama hayupo..." nikamwambia hivyo kuelekea mechi.

"Ee, hajaingia. Shauri ya ile red aliyopigwa mechi iliyopita..."

"Aaa kweli... Moses Phiri ndo' anarekebisha mitambo leo... labda na Kibu..."

"Ah, Kibu hamna lolote. Mwana ana kasi, nguvu, lakini kufunga hawezagi..."

"Ahahah... uliona lile goli alilofunga Kariakoo Derby wakati mvua inanyesha? Ndiyo mpaka linatumiwa kwenye maPromo..."

"Ah, bahati sana. Yaani Kibu huwa anafunga kwa bahati sana. Umeshaona goli lake lingine toka amefunga hilo?"

Nikacheka kidogo tu, na hapo ndiyo mlango ukafunguliwa na mhudumu mwingine kuingia. 

Alikuwa mwanamke wa miaka ishirini na kitu hivi, mweusi wa maji ya kunde, mfupi kiasi, aliyevalia T-shirt jeupe la Simba na suruali ya jeans yenye kubana. Alibeba hips nene, kalio lake likitokeza vyema sana nyuma, ikiwa wazi ni moja ya vivutio maalumu vya wateja hapo. Alikuwa na macho makubwa, domo nene, nywele alizosuka mtindo wa rasta ndefu zenye rangi ya samawati, naye alishika kontena dogo lenye vinywaji kwa ndani. Akaviweka mezani, huku Tesha akianza kumchokoza kwa kumshika-shika pajani na kumpiga kalioni, nami nikawa natabasamu tu. 

Alipotufungulia bia, akataka kuondoka na kontena lake, lakini Tesha akaushika mkono wake na kumvuta, na mwanamke huyo akamwangukia na wote kulala sofani hapo. 

"Hee... wewe..." mwanamke huyo akalalamika.

"Unaenda wapi?" Tesha akamuuliza hivyo huku akitabasamu.

"Niachie, nina wateja bwana..." akamwambia.

"Kwani sisi fisi?" Tesha akamuuliza.

"Aa..."

Mwanamke huyo akajitoa kwa kutumia nguvu kiasi, naye Tesha akamwambia, "Nenda kwanza kwa huyo jamaa, anataka akwambie kitu."

Mwanamke akasimama vizuri na kusema, "Si niko hapa aniambie?"

"Msogelee, akwambie..." Tesha akamwambia hivyo kwa msisitizo.

"Ahah... ila jamaa wewe! Dada nenda, kaendelee na kazi..." nikamwambia hivyo mhudumu.

Akabeba kontena lake na kutoka.

"Asa' ndo' nini JC? Unazingua. Hujaona kishundu hicho?"  Tesha akasema kwa kuudhika.

Nikacheka kidogo na kusema, "Na Soraya je? Ye' kwani hana?"

"Aaaa kwa hiyo umemkubali Tausi kumbe! Mtafute sasa, la sivyo chukua na namba za huyu... ayaa! Baleke amekosa goli bro!"

Nikatazama TV pia na kuona rudio la mshambuliaji Baleke akikosa kufunga goli kwa shuti la karibu kwenye dimba la timu pinzani.

"Na huwa anakosa mengi..." nikasema hivyo.

"Ah, bwege tu. Turudi kwa mtoto Soraya..."

"Tesha tulia. Nimekwambia me siyo wa hivyo. Mwanamke mpaka niwe nimemkubali sana, ndiyo napita naye..."

"Unaangalia wale wazuri-wazuri eti? Hata me nawakubali, sema bei..."

"Dah! Angalia usife mapema kaka...."

"Ah, kufa kupo tu, kwanza...."

Maneno yake yakakatishwa baada ya mlango kufunguliwa tena, na hapo wakaingia wanaume watatu. 

Aliyekuwa mbele alionekana kuwa kama baunsa sijui, maana mwili wake ulikuwa mkubwa na alivaa kwa njia fulani kama jasusi eti, na miwani myeusi machoni. Niliona hilo kuwa kama ushamba maana tayari giza lilikuwa limeshaingia, sasa sijui alivaa miwani ya nini! Aliyefata alikuwa mbaba mwenye mwili mnene kiasi, mweupe, na mrefu pia, na nyuma zaidi ilikuwa ni Bobo. 

Sikujua sababu ilikuwa nini iliyomfanya Tesha akae vizuri zaidi kwenye sofa na si kwa mkao wa kujiachia, na wanaume hao wawili waliponipita, nikamtazama huyo mweupe kwa nyuma na kuona kitu fulani kikiwa kimetuna usawa wa kiuno. Nilipokiangalia kwa umakini zaidi, nikatambua ilikuwa ni bastola! 

Bobo akanipita pia na kwenda upande wa mbele zaidi ambao wanaume wale walienda kukaa, nami nikamtazama Tesha usoni. Uso wake ulionyesha hali ya utulivu zaidi, na kwa ishara ya mdomo akaniambia kitu fulani ambacho sikuelewa vizuri. Akarudia tena na kutazama upande wa TV upesi, nami nikawa nimeyaelewa maneno hayo kuwa, 'mwenye Masai.' 

Nikamtazama kiufupi mwanaume huyo na kukuta ananiangalia pia. Sijui ni nini tu ila kuna kitu kikawa kimeniambia kwamba hapa kuna jambo halikuwa sawa. Si sanasana kuhusu yale mambo aliyoniambia Tesha kumwelekea Joy aliyoyafanya kwa udhamini  wa huyu jamaa wake? 

Nikakumbuka kweli Tesha alinionya kutocheza sana na Joy hata kama mwanamke huyo alinitaka, kwa sababu huenda ningepatwa na matatizo ambayo yangeletwa na huyu jamaa yake. Sasa sijui ujio wake wa ghafla namna hii ndiyo uliokuwa umeyaleta matatizo hayo kwangu? 

Ikiwa labda aliambiwa niliondoka na manzi wake usiku wa jana, huenda mimi kufika tena Masai leo ndiyo kukafanya aitwe ili aje kuniona. Na alionekana kutokuwa mtu mwenye masihara kwelikweli mpaka Tesha kuamua kushusha miguu alipomwona. Vipi kama bastola hiyo ilinihusu mimi? Ningetokaje hapa?

 

★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next