Licha ya mzee huyu kwa Roma kujitambulisha kama Mbeba mizigo , hakutaka kuamini kirahisi hivyo , alipiga simu mahali na kuomba taarifa ya Roma na ndani ya dakika chache alitumiwa na kuianza kuisoma huku akionekana ni mwenye kushangazwa na taarifa hio.
“Haiwezekani , kama hii ni kweli kwanini afanye kazi inayomshusha hadhi yake, hata kama hii ripoti ni sahihi siwezi kukubali Edna aolewe na mwanaume kama huyu ,Edna ni mtu mkubwa haendani na huyu mpuuzi isitoshe nikiruhusu ndoa hii nitakuwa kwenye wakati mbaya na City Master ”Aliongea mzee huyu huku akikaa chini kwenye sofa huku akiendelea kufikiria.
“Abuu alishindwa vipi kumdhibiti Edna nilimpa kazi ya kuhakikisha anamuweka kwenye himaya yake na kumuoa ili mipando yetu iende sawa , lakini kakwama katika hili , huenda nilikosea kumchagua kama mwanaume wa kuwa na mwanangu , Hebu ngoja nimpigie simu huenda hata hili swala halifahamu”Aliongea Baba yake Edna afahamikae kwa jina maarufu kama Mzee Adebe kifupi cha Adebayoo.
“Abu umeshindwae kumdhibiti Edna… amekuja leo kumtambulisha Mume wake , huo mpango uliokuwa unajigamba nao uliishia wapi, Vipi swala la City Master tunalikamilishaje?”
“Mzee naomba utulie uniambie vizuri nini kimetokea?”Aliongea Abuu kwa pupa .
“Muda mchache Edna alikuja nyumbani kwangu na mwanaume aliejitambulisha kwa jina la Roma anaefanya kazi kama mbeba mizigo kutoka Rangi tatu na Edna amesema ni Mume wake kihalali na hataki kusikia ndoa tena na wewe ,hivi unaniambia umezidiwa kete na mtu kama Roma wewe”Aliongea mzee huyu kwa hasira na upande wa pili wala haukutoa jibu Zaidi ya simu kukatwa.
“My wife , nimejitambulisha vizuri eh”Aliongea Roma huku akimwangalia Venus aliekuwa makini na usukuni , lakini baada ya kutembea hatua kadhaa , alikamata breki na kusimamisha gari na kisha alimuamuru Roma kutoka kwenye gari yake, na Roma hakuwa mbishi alitoka , na alishangaa kurushiwa kadi kwa kupitia dirishani.
“Hakikisha saa moja kamili upo nyumbani , mahali unapotakiwa kufika angalia kwenye hio kadi ole wako uchelewe ”Aliongea mwanadada huyu kwa hasira na kisha alitoa gari yake hio kwa spidi na kutokomea akimuacha Roma kwenye hali ya mshangao.
“Mwanamke ana kisirani huyu , au bado ana hasira na mimi ya kumtoa bikra yake”Alijiongelesha huku akiangalia saa kwenye kijisimu chake na kuona ni saa kumi na nusu , aliangalia kadi iliokuwa kwenye mikono yake na kuona mahali ambapo anatakiwa kwenda kwenye makazi yake mapya.
“Mwanamke anadhambi huyu yaani anataka nitembee kutoka hapa Moroco mpaka Kigamboni”Alijisachi mfukoni na kukumbuka kuwa hakuwa na kitu mfukoni kwani nguo alizokuwa amevaa ni mpya na za kwake zilizokuwa na malipo aliziacha kule hotelini.
“Huyu ndio mke wangu niliekubali mwenyewe kumuoa , anamuacha mume wake barabarani , kazi ninayo”Alijiongelesha huku akitembea kwa umbali mrefu mpaka pale magari yaliposimama kwenye mataa , wakati akiwa anakagua magari hayo mara aliona mwanamke mmoja mrembo akinunua maji akiwa ndani ya gari aina ya Aud , wakati huu magari yakiwa yamesimama.
Roma alisogelea gari hili na kisha alisubiria biashara ile iishe atekeleze jambo lake lililompeleka hapo.
“Hey mrembo ! mambo”Alisalimiana na mwanadada huyo na kujibiwa bila dharau na kuona yupo mahali sahihi.
“Sasa mrembo naomba unisaidie jambo , mke wangu kaniacha njiani na sina kitu mfukoni hata hea ya nauli , naomba unisaidie kiasi chochote nipate nauli ya kunifikisha Kigamboni”Aliongea Roma bila aibu na mwanadada huyo alimwangalia Roma kwa mavazi yake na kuona huenda kuna ukweli ndani yake kwani Suti na kiatu alichovaa kilionekana cha bei ya juu na ni watu wachache sana wana uwezo wa kumudu aina hio ya mavazi.
“Pole kaka hela hii , hapa nadhani inatosha”Aliongea mwanamke huyu na kumpatia noti ya elfu tano Roma na hapohapo gari zilianza kuondoka na hata Roma alishindwa kutoa shukrani yake , ila alifurahi alikuwa amepata hela ya nauli.
Muda wa saa kumi na mbili na Nusu Roma alikuwa mbele ya geti kubwa ambalo kwa ndani ya fensi hii lilionekana jumba kubwa la kifahari ndani ya mtaa huu uliokuwa ukifahamik kwa jina la Sunlight Villa Hub , ni mtaa ambao hakukuwa na nyumba ya kizembe , majumba yote yaliokuwa yanapatikana ndani ya eneo hili yalionekana kuwa ni ya kifahari sana na hili lililifanya eneo hili kuwa maarufu kama eneo la Matajiri ndani ya mji huu wa Kigamboni.
Roma aliminya kengere baada ya kuona yupo mahali sahihi na ndani ya dakika , alifungua bwana mmoja mweusi alievalia suti huku sikioni akiwa na visikilizishi.
“Wewe ni nani?”
“Mimi ni Roma na ni baba mwenye nyumba kwanzia siku ya leo a.k.a boss wako mpya ”Aliongea Roma huku akiwa ameweka tabasamu na kumfanya mlinzi huuyu ashangae na kuona chizi wa leo alikuwa wa aina yake.
“Sasa Bosi wangu mpya kutokana na kwamba wewe ni chizi msafi leo naomba uondoke kimya kimya kabla sijachukua maamuzi makubwa”.Aliongea bwana huyu huku akimwangalia Roma kwa kumtathimi, lakini wakati akiendelea kumwangalia Roma ,mara alihisi uwepo wa mtu nyuma yake na aligeuka .
“Madam Boss..!”Aliongea kwa hali ya mshangao baada ya kumuona Edna alievalia gauni lililompendeza lililomfikia magotini na kumfanya aonekane kama malaika kiasi cha mwanaume huyu mlinzi kumeza mate ya kimatamanio.
“Nani yupo mlangoni Derick??” Aliuliza Edna na kabla Derick hajajibu alijishangaa akivutwa nje kwa spidi ambayo hakuitarajia na Roma kuingia ndani.
“Bebi wife ni mimi mumeo nimefika ndani ya muda..hehe bebi usiniambie ulikuwa ukinisubiria??”Aliongea Roma huku akiwa ni mwenye kuweka tabasamu usoni , akinyoosha mikono kuashiria anataka kumkumbatia , ila Edna hakumjali Zaidi ya kumkwepa.
“Derick huyu ni mume wangu Anaitwa Roma , kwanzia leo ataishi hapa na mumpe heshima yake kama mume wangu”Aliongea Edna kwa lugha ya kiupole ila iliojaa usiriasi kuonyesha kile anachokisema.
“Sawa Madam bosi”Aliitika Derick kwa kubabaika kwani sekunde kadhaa alimdhania mwanaume aliekuwa mbele yake kama kichaa msafi
“Utawaambia na wenzio”Aliongea Edna kwa sauti yake nzuri na kumfanya Roma atabasamu kwa utambulisho huo na akajiona angalau licha ya mwanamke huyu alikuwa akimdharau ,lakini afadhali alikuwa akimpa heshima yake kama mume.
Derick aliekuwa amesimama alishangazwa sana na utambulisho huo , kilichomfanya bwana huyu kushangaa ni ile hali ya kutokuamini kwamba mtu kama Roma anaweza kuwa mume wa bosi wake , kwake Edna alikuwa mzuri na mrembo sana kumilikiwa na Roma hivyo matarajio yake ni kuona mtu mwenye hadhi ya juu Zaidi kuwa mwanaume wa bosi wake , lakini leo jambo hili lilimshangaza , lakini hakutaka kujiuliza maswali mengi , Zaidi ya kutii na alipanga kumuomba msamaha Roma pale atakapo pata nafasi ya kufanya hivyo kwa kitendo cha kumuita kichaa.
“Kuna wanaume wamezaliwa na bahati sana , yaani jamaa kama yule ndio anamsugua bosi daah! Kweli wanawake sio wakuwaelewa kabisa”Alijiongelesha Derick mpaka pale aliposhituliwa na mlinzi mwenzake.
Roma alikubali uzuri wa nyumba aliokuwa akiishi Edna , ilikuwa ni nyumba kubwa mno kiasi kwamba ilimfikirisha kwa wakati mmmoja kwa kazi ambayo Edna alikuwa akifanya hapa mjini.
Jumba hili lilikuwa la gorofa tatu kwenda juu , lililokuwa na mandhari ya kuvutia sana , baada ya Roma kukaribishwa ndani na Edna alipokelewa na mama mmoja mtu mzima.
“Karibu sana Mister Roma ”Roma alitikia kwa heshima huku akisubiri utambulisho kutoka kwa mke wake.
“Roma huyu ni Bi Wema ni kama mama kwangu , ndio alienilea tokea nikiwa mtoto baada ya mama kufariki, Bi Wema huyu ni Roma niliekuambia , ndio mume wangu”
“Karibu sana Roma kwenye familia , jisikie huru hapa ni kwako”Aliongea bibi huyu na Roma alitabasamu na kukubali utambulisho huo na Edna hakuwa na maongezi mengi na Roma Zaidi ya kumwachia maagizo yote Bi wema .
“Karibu sana Roma , unaonekana ni kijana wa kipekee sana mpaka Miss Edna akakuchagua kuwa mume wake , niseme tu mimi nimemuona Edna tokea akiwa mtoto na hajawahi kutambulisha mwanaume yoyote kwangu kuwa nae kimahusiano , Edna amekuwa ni mtoto mpweke sana ambae amekuwa peke yake mpaka pale aliporithishwa kampuni na marehemu mama yake, hivyo nakuomba usije ukaamuumiza”Roma alipewa nasaha hizo na bibi huyu na kuzingatia , baada ya hapo alionyeshwa chumba chake ambacho atakuwa analala.
Chumba chake kilikuwa kwenye Floor ya pili , kilikuwa ni chumba kikubwa cha kifahari kilichokuwa na kila kitu kwanzia Tv kubwa ya Inch 64 , pembeni kulikuwa na meza iliokuwa na komputa kubwa ya kamouni ya Apple , masofa na makorokoro mengine ya gharama , Roma alilirdhika na chumba hiki na kumshukuru Bi wema kwa maandalizi ya chumba chake.
Roma aliingia bafuni na kuoga na kisha alifungua kabati la nguo na kukuta nguo nyingi zinazomtosha zikiwa zimepangiliwa kwenye kabati , alijiuliza maswali nin muda gani nguo hizo ziliwekwa humo , ila majibu yake aliyapata kwani nguo zote zlionekana kuwa mpya.
Baada ya kupigilia tisheti iliomkaa vyma na kipensi chake , alijilaza kitandani mpaka pale alipopitiwa na usingizi , alikuja kushituka usiku wa saa mbili na ilikuwa ni muda wa chakula cha usiku , alishuka mpaka chini sehemu ya chakula na kuungana na Bi wema na Mke wake na kisha kukaa.
Jumba hilo lote lilikuwa likiishi wanafamilia wawili tu , jambo ambalo lilimshangaza sana Roma.
“Babe Edna usiniambie jumba lote hili mnaishi wawili tu”
“Ndio Mr Roma tupo sisi tu na Miss hana ndugu wengi zaidi ya baba yake”
“Kwa hio na baba yake kule anaishi peke yake?”.
“Miss na mimi tulikuwa tukiishi nae wote ila baada ya wao kugombana mara kwa mara ndio tukahamia hapa”
Roma alitikia huku akiendelea kula bila wasiwasi kama vile ni wa siku nyingi ndani ya nyumba hio , kwani wakati wenzake walipokuwa sahani ya kwanza yeye alikuwa ameongeza Zaidi ya mara tatu na kumfanya Bi wema kutabasamu , lakini upande wa Edna alimwangalia kwa kumshangaa huku akijisemea ndani kwa ndani kuwa Roma ni mwanaume ambaye hakuwa na aibu hata kidogo
“Bi wema unajua kupika sana , mpaka miezi sita ikiisha nitakuwa na kitambi”.
“Kweli eh , kula kabisa wala usione wasiwasi na kuna chakula kingine kimebaki jikoni”
“Asante leo ngoja nipumzike mpaka siku ya kesho”Aliongea Roma na baada ya kula hakukuwa na stori sana na Edna kwali bado alionekana kumchunia mno na hakutaka stori nyingi Zaidi ya mwanadada huyo kupandisha juu kabisa kwenda kwenye chumba chake cha kujisomea.
Siku iliofuata asubuhi Roma aliamka mapema na alionyeshwa chumba cha mazoezi na Bi wema na kuingia kuanza kufanya mazoezi , alivyomaliza chai ilikuwa tayari na Edna alievalia gauni lililompendeza kama malaika alionekana akishuka huku akiwa na mkoba wake , aliweka kwenye sofa na kisha aliungana nao kwa ajili ya chai.
“My wife umeamkaje?”
“Safi”
“Niko poa babe”aliongea Roma ila hakuzingatiwa sana , kwani Edna aliendelea kunywa chai iliokuwa Zaidi ya chakula cha mchana kwa wingi wa vyakula , kwa Roma hakuwa mnyonge, kwani alikula kama hatokula tena .
“Babe Edna nikitoka hapa narudi Mbagala kazini kwangu”
“Hapana kuanzia leo ile kazi yako achana nayo, tafuta kazi nyingine yenye hazi na ufanye hapa utakaa lakini kumbuka wewe ni mwanaume hela ya matumizi siwezi kukupatia”Aliongea Edna kwa msisitizo na kisha alimuaga Bi Wema kama anaelekea kazini kwake na kuondoka.
“Ni kweli Mr unapaswa kuacha hio kazi , zipo kazi nyingi ambazo zinaendana na wewe na unaweza kufanya”.
Roma alifikira kwa muda na kuona maneno yao yana mantiki na aliona ni bora akafanya hivyo , lakini aliona ugumu wa kupata kazi inayoendana na hazi yake.
Baada ya kuwaza kwa muda aliona ni muda muafaka kwanza wa kurudi Mbagala kwa ajili ya kuchukua vitu vyake, alimuaga Bi Wema na kabla hajaondoka ,bibi huyu alimwambia amfuate nyuma ya nyumba na ndani ya dakika chache walikuwa mbele ya magari yaliokuwa yamehifadhiwa , yalikuwa ni magari kumi ya kifahari ambayo yalikuwepo hapo ndani.
“Miss Edna alinipa maelekezo kama ukitaka kutoka unaweza kuchagua gari yoyote unayopenda na itakuwa yakwako, nadhani unajua kuendesha gari”
“Ndio Bi wema niko vizuri”Aliongea kwa kutabasamu akiangalia magari hayo , kwani moja ya Starehe pia aliokuwa akipenda Roma ni kuendesha magari .
Alilisogelea gari moja aina ya BMW X7 na kumwabia Bi Wema atatumia gari hio kwanzia siku hio.
Basi baada ya kupewa ufunguo wake , kwa mbwembwe zote alitoa gari nje ya geti na safari ya kuelekea Mbagala Rangi tatu ikiwa imeanza.
“Leo watanikoma, ,Juma na wenzake wanaongea sana”Alijiongelesha Roma huku akikanyaga pedeli na kuongeza mwendo , huku kila alipokuwa anapita na gari lake watu walikuwa wakilikodolea macho.
Ni muda wa saa nne za asubuhi ,Roma alisimamisha Gari katika soko La mbagala Rangi tatu na kisha alishuka , huku wengi waliokuwa wakimfahamu wakimwangalia kwamshangao kama hawakuwa wakimjua.
“Oy Roma kaka ni wewe?”
“Nni mimi kaka , vipi mishe za hapa?”
“freshi kaka umebadilika sana aisee”
“Hahaha.. kawaida Seif”Aliongea Roma baada ya kusalimia na Seif aliekuwa akiuza Zabibibu ndani eneo hili la Stendi ya Rangi Tatu.
“Oya mwanaaa…!!! Aaah Romaaa .. daah ni wewe kweli?”
“Ni mimi Yusuph , hujanifananisha , ni maisha tu haya hahaha.. unaweza ukalala masikini ukaamka tajiri ndio kilichonitokea”
Yusuph hakuwa ni mwenye kuamini hivyo kiharaka ,Roma alimtafuta Juma mpaka akampata katikati ya soko akiwa anashusha mihogo kwenye kirikuu.
“Juma!” Roma aliita na kumfanya Juma ashanagae.
“Roma!” Juma alianza kumkagua Roma kuanzia juu hadi chini na akawa sio mwenye kuamini kama aliekuwa mbele yake ni yule aliekuwa akimdharau kiasi cha kumuita fukara na kutotaka amsogelee dada yake.
“Yes bro nimerudi , kuchukua mazaga na kumalizia hela ya kodi unayonidai nahamia town man”Aliongea Roma na kumshangaza Zaidi Juma , ambae hakufurahi sana kumuona Roma kwenye hali kama hio kwani siku zote alikuwa akijilinganisha nae na kuona yeye ndio mwenye unafuu mkubwa wa kimaisha , lakini kwa muonekano mpya aliomuona nao Roma aliona bwana huyo sio level zake.
“Poa ngoja nije tuelekee maana nilikuwa pia na wazo hilo hilo la kukuambia utafute mahali pengine , ila kama umepata itakuwa poa sana”Aliongea Juma huku akionekana sio mwenye kufurahia mafanikio ya ghafla ya Roma na Roma alitikia kwa kichwa na kisha alimwambia amsubirie anakuja na Juma alimwambia poa.
Roma alienda na kuchukua Gari yake na kuja nayo mpaka eneo alilokuwepo Juma , mwanzoni Juma hakujua nani anaendesha gari hio, na akawa mmoja ya watu wanaoishangaa.
Roma alishusha kioo na kumuita Juma alizidi kushangaa Zaidi baada ya kugundua anaendesha gari hio ni Roma.
“Roma ni wewe mwanangu??”
“Ndio ni mimi Mama Nasra”
“Hio gari ni ya kwako?”
“Ndio Mama Nasra hii nimepewa kama zawadi na mke wangu”Aliongea Roma na kuwafanya waliosikia neno ‘mke’ washangae.
“Umeoa lini Roma mbona hatujui muda wote huo kama una mke?”
“Nimeoa jana Mama Nasra ilikuwa ghafla na nilishindwa kupata muda wa kuwaambia”Aliongea Roma na watu walishangaa huku wakizidi kujawa na maswali ni mke gani amekubali kuolewa na mtu kama Roma asiekuwa mbele na nyuma na mpaka kumdhawadia gari.
“Ama kweli usimdharau mtu .. maana nyota zetu hazifanani”Alisikika mzee mmoja aliekuwa akimenya machungwa akiongea wakati huo Roma akiwa anapitisha gari lake kwa mbwembwe kielekea Bias.
Ndani ya gari hakukuwa na stori nyingi kati ya Juma na Roma , japo Juma muda wote macho hayakuwa yakitulia , kwenye maisha yake hakuwahi kuwaza kama atakuja kupata hata lift kwenye gari kali kama hii.
“Hongera kaka kwa kupata mke mwenye hela , nadhani Najma atakusahau na kuendelea na maisha yake sasa”.Roma hakujibu kitu Zaidi ya kutabasamu na kutingisha kichwa , iliwachukua dakika tano kufika Bias.
Roma baada ya kusimamisha gari huku majirani wakiwa wanamshangaa kwani ni siku ya jana tu habari zake za kutorudi zilikuwa zimesambaa kuwa hakurudi jana yake baada ya kuja kuchuliwa na mwanadada alievalia suti , kuna waliohisi huenda alitekwa nyara , na kuna wengine waliokuwa wakidhania huenda Roma alikuwa mtu mkubwa tu na alikuuwa akijifanyissha kuwa mbeba mizigo , kwani kitendo cha kufuatwa na mwanadada ambae alikuwa mrembo , kiliwashangaza wengi na hakikua cha kawaida na cha bahati mbaya , kila mtu alilipa wazo lake sababu na kuwa na nguvu ndani ya kichwa chake.
Moja ya watu waliokuwa katika hali ya wasiwasi ni mwanadada Najma , alikuwa ni mwenye mawazo kweli kiasi kwamba hata kazini hakuweza kwenda kwa siku hio , kwani ndani ya kichwa chake alikuwa akimuwazia Roma tu , alikuwa na taarifa zote zilizokuwa zikimhusu Roma jana yake kufuatwa na Gari la kifahari aina ya V8 jambo ambalo alipojumlisha na mawazo ya kimbea ya watu aliona huenda kuna ukweli wake, Roma hakuwa mwenzao kama walivyodhani , lakini licha ya hivyo bado aliamini kwamba Roma alikuwa akimpenda yeye na pia yeye alikuwa akimpenda na hivyo hakukuwa na kitu ambacho kinaweza kuwatenganisha, hayo ndio mawazo aliokuwa nayo Najma karibia asubuhi yote kaka yake alipoelekea kazini.
Najma alifkiria matendo ya kikarimu ambayo Roma ashawahi kuyafanya juu yake , alikumbuka kipindi Roma alivyomsaidia kiasi kikubwa cha pesa Zaidi ya laki nane kwa ajili ya kwenda kulipia malipo ya nusu umiliki wa shule aliokuwa akifundishia huku Roma akimwambia kuwa hakupaswa kulipa kiasi hicho na achukuliea kama fedha zilizotoka kwa ndugu , alifikiria pia siku ambayo pia aligharimikia matibabu yake kiasi cha shilingi laki moja huku Roma akikataa malipo , kwake aliona matendo yote hayo yalikuwa ni ya kimapenzi, aliamini Roma alikuwa akimpenda yeye na kikwazo kikubwa ilikuwa ni kaka yake, lakini licha hivyo Najma aliamini kama siku zote ataendelea kumpenda Roma basi siku moja kaka yake atakata tamaa na kuwaruhusu wawili hao wapendane.
Najma aliendelea kukumbuka miezi sita nyuma siku ambayo Roma alifika ndani ya nyumba yao na kumkuta akifua nguo muda wa jioni na kumueleza shida yake kwamba alikuwa akitokea mikoani na alikuja mahali hapo kwa ajili ya kutafuta uwezekano wa kupata chumba , hio ndio siku ambayo Najma alijikuta akivutiwa mara moja na mwanaume huyo , hakujua ni nguvu gani iliokuwa ikimvuta kwa mwanaume huyo , lakini katika akili yake aliona kuwa mtu aliekuwa mbele yake hakuja hapo kwao kwa bahati mbaya na ni Allah ndie ambae amemleta hapo kwake , na mtu aliekuwa mbele yake alikuwa ndio mume wake aliekuwa akimuota kila siku , siku hio ilichuku takribani ya madakika kadhaa kwa Najma kuacha kumshangaa Roma na kumtathimiini mwanaume huyo huku akiwa si mwenye kuamini kwamba mume wake hatimae amefika na kuja kumchukua.
“Kipo chumba kaka .. karibu”Najma aliitikia mara moja huku akiwa ni mwenye kupagawa .. alimuonesha Roma chumba hiko huku jambo moja ambalo Roma alikosa kwa muda huo lilikuw ani godoro na Najma bila ya kujifikiria mara mbili alimwambia Roma atamsaidia Godoro na atalalaia bure mpaka pale atakapokuwa na uwezo wa kununua la kwake , upande wa Roma alitabasamu na kupendezwa na roho nzuri aliokuwa nayo Najma , kwani mwanamke aliekuwa mbele yake sio kuwa mzuri tu na mrembo lakini pia alionekana kuwa mwenye kujali watu pasipo ya muonekeano wao, kwanzia siku hio Roma alianza kuwa na ukaribu na mrembo Najma , na hata pale kaka yake aliporudi kutoka kazini na Najma kumpa habari ya ujio wa Roma ,Juma yeye hakuwa na shida kwani alimini ujio wa Roma ni ongezeko la pesa katika walipa kodi.
Kutokana na Roma siku za mwanzoni kushinda Nyumbani walijikuta wakiwa karibu sana na Najma na kuzoeana kwa haraka , kwa upande wa Najma kila siku alipokuwa akikaa na Roma na kupiga stori kitu kipya kilijijenga ndani ya moyo wake.
“Huyu ndie mwanaume niliekuwa nikimuota , ni mwenyewe na sijakosea bila shaka”
Ndio sentensi aliokuwa akiongea Najma kila siku wanapokutana na Roma na kupiga Stori , mwanadada huyu alijikuta akijaa Huba ndani ya moyo wake dhidi ya Roma, matendo yote ya Roma kwa Najma yalikuwa yakiongeza kipande cha upando ndani ya Moyo wake.
Hata pale Roma alipoanza kuzoeana na kaka yake na wakawa marafiki na kuanza kufanya wote kazi katika soko la Rangi Tatu,Najma bado alisubiri muda wa kurudi kwa Roma awafungulie amuone Roma wake moyo wake utulie ,Roma nae kila alipokuwa akirudi kwenye chumba chake alikuta chakula kitamu kikiwa kinamsubiri aliishia kutabasamu na kula chakula hiko na kisha kuacha kimemo cha Asante kwa Najma , na mrembo huyu kila siku alipokuja kuchukua vyombo na kukuta kikaratasi hiko cha Asante na kusifiwa kama mpishi mzuri kiliufanya moyo wake uzidi kuloea juu ya Roma , kila kitu kwake Najma ilikuwa ni Roma , akila chakula ilikuwa ni Roma , akioga ilikuwa ni Roma ,, ilikuwa ni Roma , Roma, Roma kila siku ,kitendo ambacho kilimfanya kaka yake Juma kugundua dada yake alikuwa amempenda Roma.
Gunduzi hio ya mapenzi ya dada yake juu ya Roma ndio yalioibua hali ya chuki baina ya wawili hao , upande wa Juma aliona dada yake alikuwa mzuri sana kuolewa na mwanaume Fukara kama Roma hivyo mapenzi hayo kwake hakutakata yatokee , kila siku alijitahidi kumshawishi Roma wachelewe kurudi na kuwahi kazini , ili wawili hao wasipata nafasi ya kuonana , lakini bado Juma alishindwa kuwazuia wawili hawa kutokuwasiliana , kwani baada ya siku kadhaa Roma alinunua simu na namba ya kwanza kumpigia katika simu yake ilikuwa namba ya mrembo Najma, walitakiana heri kwa kila waamkapo wakielekea kazini na walitakiana heri walakati wa kulala , walishirikishana mambo mengi, mapenzi baina yao yalionekana kuwa na nguvu sana, matendo ya Roma yalionyesha wazi alikuwa akimpenda Najma na matendo ya Najma yalioneysha anampenda Roma ,Licha ya wawili hawa kutokuongea kuwa wanapendana lakini matendo yao yalikuwa ndio kila kitu kwao.
Baada ya muda mrefu wa Juma kuwa na mawazo , leo hii anajikuta moyo wake ukitulia mara baada ya Roma kupata mke , lakini mwanzo wa swala hili linaibuka swala linguine katika moyo wake na swala hilo lilikuwa juu ya mafanikio ya Roma , hakuamini mtu aliekuwa akimdharau leo hii alikuwa na mafanikio makubwa kuliko yake , jambo hili kwake hakutaka litokee kabisa.
“Nitamwendea kwa mganga huyu , na siku sio nyingi anakuja kulilia hapa nimpe hiki chumba , kwanza hela sio zake akiachwa anakuwa masikini , nitahakikisha mke wake anamuacha huyu mpuuzi”
Juma aliingia ndani ya nyumba yao na kisha alitoa ufunguo na kurudi nje na kumpatia Roma , Roma baada ya kuingia ndani ya chumba chake , alishangaa kukuta upekuzi uliokuwa umefanyika ndani ya hiki chumba,Juma nayeye alishangaa , kwani ni asubuhi tu alifunga , lakini hali aliokuta humo ndani ilimshangaza , alifikiria ni nani anaweza kufanya jambo hilo kwani mlango ulikuwa umefungwa na Zaidi pia aliukuta umefungwa kama alivyofunga, na ufunguo alikuwa akijua yeye tu lakini hakutaka kujiuiza maswali sana , kwanza aliamini Roma hana kitu cha thamani hapo ndani kiasi cha kuwaza.
Roma yeye alishangazwa na upekuzi huo , lakini yeye hakujali Zaidi , alisogea mpaka lilipokuwa gororo lake na kulinyanyua juu na akaangalia chini na alijikuta akivuta pumzi ya ahueni.
“Inaonekana walichokuwa wakikitafuta hawajakipata”
Aliongea Roma na kisha alichuchumaa na kusogea mpaka sehemu ambayo ilikuwa na alama ya mchoro wa Zero , wakati huu Juma alikuwa yupo nje akimpa nafasi Roma ya kufanya mambo yake amkabidhi hela zake .
Baada ya Roma kusogelea alama ile ya Zero alivuta pumzi na kukunja ngumi na kwa spidi alipiga katikati ya lile eneo na pakabaduka na kuacha uwazi , Roma alitoa mchanga na kiisha alivuta mfuko wa Rambo na kuutoa nje na kisha akaufungua , ndani ya mfuko huu ulionekana kuwa na kiboksi flani kirefu mfano wa mstatiri , alikifungua kiboksi hiki na kuona vitu vyake vyote vipo, alitoa kiburnguti cha hela na kutoa hela iliosomeka kwa mfumo wa Dola , ilikuwa ni Dolla Mia ambayo kwa hela za kitanzania ilikuwa ni Zaidi ya laki mbili, baada ya kutoa baadhi ya vitu vyake hivyo aliviingiza kwenye begi lililokuwa pembeni yake kubwa kubwa la kusafiria na kisha alisimama na kuvuta pumzi huku akionekana kama mtu anaeonekana kuaga chumba hiko, baada ya hapo alitoka nje na kumkuta Juma , Alitoa ile noti ya Dola Mia na kumpatia Juma na kumfanya ashangae , kwani Juma pia hakuwa kilaza ashindwe kujua thamani ya dolla Mia.
“Nadhani hio italipa deni langu la Kodi , lakini pia kunasehemu nimeharibu huko ndani so inayobaki itakuwa fidia”
“Sawa kaka Asante”
“Romaa..!!!”Ilisikika sauti ilioingia kwenye ngoma za masikio yake na kuitambua.
“Najma .. nilidhania upo kazini”Aliongea Roma huku akimwangalia mwanadada aliekuwa mbele yake , aliekuwa amesahau hata kuvaa Hijab kwa siku hii ya leo na kwa mara ya kwanza Roma anamuona mwanamke huyu akiwa hana Hijab na kuuona uzuri kamili wa Najma.
“Najma mzuri aisee”
Comments